‘Shemeji, sasa mimi ndio ninaondoka..
‘Hata hivyo
shemeji..mimi, nitajitahidi nipitie kwenu, ili mmoja wa ndugu zako waje, kwa
hali kama hiyo huwezi kubakia peke yako..
‘Mimi ..najua
nakwenda kinyume na maagizo dada yangu mpendwa, lakini huko alipo atanielewa,
anisamehe sana,..
‘Najua kabisa nilimpenda
sana dada yangu na niliahidi kuwa nitafuata yale yote aliyoniagiza lakini sasa nifanyeje
mimi..ndugu zangu wamanisusa kwa kujitolea hivi, na wamesema litakalonipata ni
juu yangu mwenyewe, wameniambia niondoke, na jana tu wamepiga simu kuwa
nahitajika nyumbani haraka, sijui kuna nini…. ,
‘Hebu shemeji
niambie mimi nitafanya nini na mimi ndiye niliyekuwa msiri wa dada yangu, …ndio
maana nimejitolea kuwa nawe japokuwa naumia, Napata shida, sina amani,na sijui
itakuwaje kesho au kesho kutwa …nielewe tu shemeji, sina budi niondoke….’ hapo
aliguna na kumezameza hayo maneno ya mwisho...nilijua kabisa alitaka kusema nini…
‘Nilitaka
kumwambia, ..huondoki unasubiria nini..lakini kauli ilikataa kusema kwani kuna
kitu kingine kilikuwa kinaanza kujijenga akilini….
‘Lakini nitafanyeje
mimi jamani..…mimi mwenyewe sasa ninaanza kuogopa, uvumilivu wangu umefikia
kikomo..…ninaogopa chochote chaweza kunipata, nakumbuka yaliyowahi kutokea huko
nyuma, nahisi kuna dalili kama hizo, kwahiyo unisamehe tu..unisamehe sana
shemeji, kwaheri…’akasema huyo mdada, kwangu mimi nilimuona kama binti,
Ilikuwa kama salamu
ya kuagana kwa mtu uliyemzoea, ..ilikuwa kama kitu fulani nilichokizoea sasa
kinaondoka, ..ilikuwa kama mtu ambaye nilikuwa tayari kusema niwezavyo, lakini
bado anakuvumilia, anakupatia huduma zote bila kujali, ni kama mzazi wako....sijui
nisemeje, kwani huyu binti alishatokea kuwa mtu wangu muhimu…sasa ndio huyu
anaondoka.
Mara nikahisi kichwani sauti nyingi zikiwa
zinanikemea,..hizo sauti zilitokea kwa pamoja, kila mmoja akisema lake, niliweza
kubahatisha kuzigundua badhi ya sauti, zilikuwa sauti za mke wangu, za docta,
za mke wa docta, za wazazi wangu..nyinginae za wanandugu…na kila mmoja alikuwa akisema
lake..na walikuwa wakisema kwa pamoja…, lakini cha muhimu zaidi ilikuwa
kunisihi… nisimuache huyo binti aondoke..
‘Ukimuacha akivuka kizingiti cha mlango, basi
umemkosa, hutampata tena…’ilikuwa sauti …ambayo sikufahamu kaongea nani, na
hapo ndio huyo binti ilishafika hatua ya tatu, ili sasa akanyage au kuvuka
kizingiti cha mlango, ..sikusubiria….
*****************
Kwa haraka
nilikurupuka kama mtu aliyeamrisha kwenye mbio za mashindano ya mbio fupi..na
tahamaki nikawa mgongoni mwa huyo binti, nilichofanya nikimshika begani, nahisi
mkono wangu ulimgusa kwa nguvu,….kwasababu,sijui vipi huyu binti alinifikiria,
maana alishtuka, mpaka akadondosha lile begi alilokuwa kalishika.
Na zaidi,
akanigeukia, ....kwa haraka akapandisha mkono kuzuia mdomo wake uliokuwa
umepanuka tayari kwa kupiga yowe la kuomba msaada…na mimi kwa haraka nikawahi
kuongea…
‘Binti tafadhali, ninakuomba nisamehe….’
Nikasema na nilimuona akiniangalia kama kaona shetani au kitu gani cha kutisha,
macho yamemtoka pima kwa woga…sasa akawa anajirudisha kichwa nyuma.
‘Nipo chini ya
miguu yako,….nielewe binti..’nikasema nikijribu kumsihi.
Kwa jinsi nilivyomuona nilijua kwa vyovyote
atapiga yowe, na ikitokea hivyo sijui jamaii itanielewaje, na sijui kwanini
kawa hivyo..mimi kwa sauti ya kusihi, nikasema;
‘Binti, ninakuomba
kabla hujaonaoka, kwanza… unisamehe…nisamehe sana ,kwa hayo niliyokutendea….’nikasema
nikijua nikisema hivyo hiyo hali aliyokuwa nayo itamuondoka…
Yule binti sasa
akawa anahema, unajua kule kuhema kwa mtu anayeogopa kitu, …ndivyo ilivyokuwa kwake,
na sijui kwanini alipatwa na hiyo hali, sijui alikuwa akinionaje mimi…. mara ghafla
akayumba yumba….mara huyo akaporomoka chini, sikuweza hata kumzuia, akadondokea
begi lake na ku-lala sakafuni. Na huko nje nikasikia gari likisimama….
‘Oh ni nani
huyo..kama ni mtu baki nimeumbuka, lakini atakuwa ni …ni….DOCTA..’ nilikisia
hivyo…
Kitendo hicho
kilitokea kwa muda mfupi sana, nikabakia sasa mimi kuduwaa, nilishikwa an
bumbuwazi ya ghafla….., nikijiuliza imekuwaje mlango ukagongwa.
Na muda huo ndio
binti keshalala sakafuni…mlalo wa kuonyesha kapoteza fahamu….
**************
Macho yangu yalikuwa yamekodoka, yakiangalia
pale alipolala huyo binti sakafuni ni mbele kidogo na pale nilipokuwa
nimesimama mimi, maana alipodondokea begi aliweza kusogea kidogo akawa mbali na mimi.
Mimi pale nilipo..niliogopa
hata kumsogelea, …na muda huo, mlango ndio ukafunguliwa…ujue nilihisi tu kuwa
docta, hata sauti ya kusema hodi, haikuwa sawa sawa na docta, lakini mimi
akilini nilihis kuwa ni yeye,… ni docta, na niliombea awe ndio yeye, kwani angelikuwa
mtu mwingine, ingelikuwa ni balaa…,
Na kweli alikuwa ni
docta…
Docta akajitokeza,
na macho yake yakawa pale alipolala huyo binti..
‘Umefanya nini
jirani…’akasema sasa akimwangalia huyo binti kwa macho ya tahadhari pale
alipolala..
‘Sijamfanya kitu
docta,..naomba msaada wako,..msaidie huyo binti apone, sijamfanya kitu kabisa
docta…naapa mbele ya mungu…sijamgusa kabisa…’nikawa nasema , ujue muda huo
nilikuwa kama natetemeka.
Docta kwa haraka
akachukua leso yake akaiviringa mkononi, na kwa tahadhari akamsogelea huyoo
binti, alifanya alichofanya, na aliporidhika, akamweka huyo binti sawa, na
kuanza kumkandamiza kifuani mara tatu…mara huyo binti akakohoa.
‘Nilipumua ile ya
kuchoka,..nikajitahidi kujisogeza pale walipo, docta na huyo binti, lakini
docta aliniashiria nisisogee, akawa anamfanyia hudum a ya kwanza, na
alipojirizisha akanigeukia,..
‘Haya niambie
kulitokea nini..?’ akaniuliza, na mimi nikawa namwangalia yule binti pale
alipolala, siongei kitu, na docta akawa anaangalia saa yake kuonyesha ana
haraka kutaka kuondoka.
‘Docta samahani sana
usiondoke,..nakuomba uhakikishe huyu binti yupo salama..sitaki tena
itokee..sitaki tena nimkose,….’nikasema nakushindwa kumalizia.
‘Yupo
salama..nahisi alipatwa na mshutuko..anahitaji muda wa kupumzika, kama hali
itabadilika basi itabidi apelekwe hospitalini….’akasema docta.
Aliposema hivyo, mimi kwa haraka nikataka
kwenda pale alipolala huyo ….docta akanizuia na kusema;
‘Kwa hivi sasa
jitahidi kuwa mbali na yeye, hatujui kwanini ikatokea hivyo, ni kwanini
anakuogopa kiasi hicho, kama ulivyosema ni sahihi… kama ni hivyo, hiyo ni hali
ya kawaida tu itakwisha…jitahidi kumuondoa wasiwasi…’akasema docta, akawa sasa
ana-angalia begi la huyo mdada.
‘Kwani
vipi..alikuwa anaondoka…?’ akauliza na mimi sasa sikumjali alivyoniambia
..nikasogea pale alipolala huyo binti,binti na kumuinamia, alikuwa katulia
kimia, na ile hali ilinifanya nikumbuke mke wangu siku nilipokwenda kumuona
baada ya kuambiwa kafariki,….alikuwa katulia hivyo, hawezi kusema tena…
Haraka nikapiga
magoti,na kumuinamia huyo binti, na machozi yakaanza kunitoka, na muda huo docta
akawa kasogea na kusimama nyuma yangu, alikuwa kama haniamini, na mimi
nikageuza kichwa kumuangalia docta nikasema;
‘Docta nisaidie
nifanye nini..kwani hata sijui kimenitokea nini… mimi mwenyewe najiona kama sio
mimi tena…’nikasema
‘Kwahiyo kuna kitu
ulitaka kumfanya huyo binti…?’ akaniuliza
‘Hapana sio hivyo
docta, sijakusudia kufanya lolote, mimi nilitaka kumsihi tu asiondoke,..ila
mimi mwenyewe najihiis sipo kawaida,…mwili wangu umebakia buwa tupu, sina
nguvu....nikuambie ukweli mke wangu alikuwa ndio mwili wangu na
keshaondoka,…sasa huyo tena..hapana, nisaidie docta…’nikasema.
‘Nikuulize kitu
ndugu yangu, jirani yangu, rafiki yangu…, je unampenda huyu binti..?’
aliniuliza swali ambalo sikulitegemea, na ilinifanya nipepese macho,
nikashindwa nisema nini, nikawa natikisa kichwa tu,….na hapo akili yangu
ikaanza kufikiria nyuma…
Kwanini
nisimpende..au….
Binti huyo ni binti
aliyejitolea sana kipindi nikiwa na shida, hakuna ambaye angeliweza
kunivumilia, ilifikia muda, nilizidiwa, akawa anasafisha na maji, kama
kunikanda,..na nikizindukana namtukana , namfukuza..bado akaendelea
kunivumilia..
Binti huyu
alihakikisha hali chakula, mpaka ahakikishe mimi nimekula, na kama nikikataa,
atafanya kila njia ili nile angalau kidogo, nilikuwa nakasirika akinibembeleza
mpaka naamua kula kwa hasira…
Binti huyu
alihakikisha napata dawa kwa wakati, na mengine mengi….binti huyo alikuwa
kipenzi cha mke wangu, akisikia mke wangu ana tatizo, alikuwa wa kwanza kuja
kumsaidia…lakini pamoja na hayo, niliwahi kutaka kumdhalilisha…bado aliendelea
kujitolea kwa ajili yangu.
‘Oh…nimefanya nini mimi
docta, hata sijui nimefanya nini…jamani,lakini sikumgusa kabisa, ..’ nikageuka
kumuangalia huyo binti,
‘Ewe binti mtiifu
kwangu….ina maana na wewe unataka kunitoka,kama alivyonitoka dada yako, hapana,
..hapana, usiondoke na wewe,nitabakia na nani kwenye hii dunia, nisamehe kwa
hayo niliyokutenda, najua hii hali inakutokea kwasababu ya ujianga wangu,
kwasababu ya ukipofu wangu…mimi…najua yote ni sababu ya kukufokea, kukukutendea
vibaya, lakini bado umeendelea kunijali….
Docta alishika
begani, kama kunituliza akasema;
‘Tulia usijali, huyu
bint kwasasa yupo salama, ila kwasasa nahisi anakuogopa, …ngoja tusaidiane
tumlaze hapo kwenye sofa, na ingelikuwa vyema ukamuacha peke yake kwanza…
muache apumzike kwanza…’akasema docta.
‘Hapana docta,
siwezi kumuacha, ataondoka huyu, ataniacha peke yangu, ninasema ukweli, ..nampenda
sana, nampenda sana docta…, japokuwa hawezi kuziba nafasi ya mke wangu, lakini
nimekubali..nimekubali, …nimeitikia wito wa mke wangu, nipo
tayari,….docta,….nisaidie docta…’nikasema sasa nikiwa nimesimama na kumng’ang’ania
docta.
Docta
akatabasamu…akasema;
‘Pamoja na
hayo,…ujue una kazi kubwa sana, kazi ya kumshawishi kuwa wewe sasa sio yule
…unanielewa hapo…..’akasema docta akigonga gonga mgongoni baada ya kuhakikisha
huyo binti kalala vyemaa kwenye sofa.
‘Kwa taarifa yako
tu, …nimesikia juu juu, kutoka kwa wife wangu, kuwa huko kijijini watu wengi
wanamtaka huyu binti…, sasa kazi kwako , chelewa
chelewa utamkuta binti sio wako,…. mimi ninaondoka….’akasema na mimi
nikageuka kumuangalia yule binti pale tulipomlaza kwenye sofa, alikuwa akihema
kwa mbali…vitita viwili vikipanda na kushuka!
‘Mhh,watu wengi wanamtaka….oh…’nikawa najisema
moyoni, sasa hali fulani ya kukosa, hali fulani..ya kutaka …hali fulani kama
wivu vikateka nafasi yangu….
Niligeuka
kumuangalia docta alikuwa keshaondoka,, nikageuka kumuangalia tena huyo binti,
sasa kwa macho ya kipekee, yule binti niliyekuwa nikimchukia,…yule binti ambaye
nikimuona hali ya chuki inanipanda, yule binti ambaye nikimuona namuona kama
ndiye sababu ya kunikosanisha na mke wangu, sasa sio huyo..ni ajabu kabisa…,
kuwa mwanadamu anaweza kubadilika kama kinyonga…
Sasa moyoni ninajuata,kumbe binti wa watu hakuwa
na hata chembe moja ya ubaya niliokuwa nikimdhania mimi..
‘Oh, sasa huyu binti
nitamlipa nini….hata kama nitamfanyia nini, sidhani kama naweza kulipa fadhila
zake,…na sasa ndio huyo, kijijini anatafutwa kama alimasi…’nikajisemea nafsini
mwangu.
Nilikuwa peke yangu
na huyo binti nikiyawaza hayo, muda huo alishaondoka, keshaniachia kazi ya
kufanya, ..kazi ambayo sasa naiona itakuwa nzito ajabu, nilijiona sasa nipo
kama mvulana mdogo mwenye aibu, anayetaka kumposa binti mwenye hadhi, …yupo
mbele ya huyo binti, anashindwa hata aseme nini…
Kwanza cha muhimu nikaona nitii agizo la
docta, kuwa nikae mbali na huyu binti, lakini sikutaka kucheza mbali, nia yangu
ikawa kutoka nje, na kukaa karibu na mlango, asije akatoka na kuondoka.
Nikachukua begi la
huyo binti kuhakikisha nimeliweka mbali, na wakati nafanya hivyo, mara
nikasikia huyu binti akimumunya maneno,…ni kama kutaka msaada..nikayakumbuka
hayo maneno, aliyatoa mdomoni ni kama ya siku ile nilipotaka kumdhalilisha…na
baadaye akatulia, halafu tena akawa anasema kwa sauti ya usingizini..
‘Dada mimi simtaki
huyu mtu,…, simtaki…ataniua…’halafu akabakia kimia…
‘Oh….hanitaki mimi
au hamtaki nani, na huyo dada yake ni nani, ni mke wangu au…?’ nikasema sasa
nikiwa nimenyong’onyea, nikawa kama mtu ambaye sasa anakikosa kitu muhimu sana
maishani mwake..nikageuka kumuangalia tena pale alipolala…, alikuwa kalala…uso
mwororo, binti mwelekevu..mrembo…oh, ama kweli mtoto huyu aliumbika…eti sasa
namuona hivyo…
Nikatoka nje… na
wakati ndio nataka kufunga mlango, mara nikasikia sauti
‘Ananibaka
ananibaka, njoo nisaidie….niokoe niokoe…simtaki simtaki,….’baadae kukawa kimia,
nikageuka kutaka kurudi, lakini nafsi ikanikataza, nikataka kuondoka, lakini
nafsi haitaki…..
NB: Naishia hapa
naona salio, na muda, tukijaliwa tutamalizia sehemu hiyo ya mwisho, ya mvulana
mwenye aibu akitaka kumtongoza binti mwenye hadhi yake..
WAZO LA LEO: Upendo wa kweli hujengeka kutoka moyoni, haijalishi mtu
yupoje, haijalishi hali ya mtu, au maumbile yake…wangapi wangapi wameoana,
lakini sura au maumbile hayaendani…tunawaona eti wana sura mbaya
Kiukweli…. Tabia
njema, kauli na jinsi gani unavyojali watu, huna dharau, uvaaji wako,..maadili
mema ya dini , yatakuwa mapambo mema ya kumvuta mwenza wako. Tujitahidi sana kujivika
mavazi hayo.
Ewe mola tuongoze
kwenye njia sahihi, na utujalia tuwe waja wako wema, Aamin.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment