Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeWednesday, October 5, 2016

UKITAKA KUMUUA MBWA....1‘Siwezi kuamini kama nipo nje…, na kuwa nipo hai,…..hadi hivi sasa nawaangalia watu kwa uwoga, siwezi kuamini kama ingelifikia hapo..hapana, jamani …ogopeni sana mke wa mtu,….’jamaa yangu alianza kunisimulia tukio lake ambalo lilimkuta, nilisikia tu watu wakiongea lakini sikuwa na uhakika.

Jamaa huyu ni mpole sana, mcha mungu,na ni nadra sana kumuonaa kwenye makundi mabaya, sasa nikasikia hayo yaliyotokea, sikuamini, ikabidi nifike kwake kumuona, akiwa ndio katoka jela,…kwa dhamana, baada ya kukaa huko karibu  miezi mitatu sasa.

‘Kwani ilikuwaje…?’ nikamuuliza

‘Unajua zamani watu wakisema, ….ni shetani tu kanipitia, kila wakifanya jambo nilikuwa nawazarau sana na kusema hayo wamejitakia, lakini sasa limenikuta mimi…na ..hakuna anayeweza kuniamini tena…’ akatulia

‘Maneno mengi mabaya yameshapandikizwa juu yangu,..eti nilikuwa  simba mwenda kimia,..nimejivika ngozi ya kondoo wakati mimi ni chui, najifanya mcha mungu kumbe ni shetani aliyevaa miwani ya jua, n kila neno baya limetupiwa kwangu….yaani siwezi hata kuamini..natamani hata dunia ipasuke nizame chini..’akasema akishika kichwa

‘Hapana usifanye hivyo….’nikasema

‘Sasa nina thamani gani tena..mke niliyempenda keshafungasha virago, kaenda kwao,..na zaidi kaondoka na watoto….hapa nilipo hata kazi sina tena, muajiri wangu alishanifukuza kazi …sasa ni mawazo, mawazo na mimi, afya ndio hii, maana jela sio mchezo, pasikie tu..’akasema

‘Unajua mimi,…najiuliza ni kwanini, ni kwanini ikanitokea hivyo… ni kwanini watu hawanielewi, ina maana hili tu, ina maana wao hawafanyi makosa, hawajawahi..yaani hili tu,…ndio limenichafulia jina langu..hapana, …walimwengu wana hila, wanakuchukia tuu….labda ni kwa vile nilikuwa napendwa na watu kuwa ni mtu mwema,..labda…mmh,, sasa imetokea hili ndio wameamua kunichafua…’akatulia

‘Mhh,kwani ilikuwaje..?’ nikauliza

‘Kweli nimeamini huo usemi kuwa, ukitaka kumuua mbwa kwanza umuite majina mabaya…nilishaanza kupakaziwa hayo, kuwa mimi….hata siamini….walikuja hata kumpandikizia mke wangu kuwa kweli nina tabia hiyo chafu….sasa,..yaani walishataka kuniua, aliyekuja kunikoa ..ni..ni….’akatulia

‘Kwani ilikuwaje….?’ nikamuuliza

‘Unajua ni huyo mdada, mimi namuitaga madamu,…. alianza kunizoea sana..mimi nilichukulia poa tu, si jirani yangu, mwenza kibiashara tu ..kumbe nyumba ya pazia kuna jambo linasukwa, sikujua kabisa, na mpaka sasa sijui ni nani alikuwa nyuma ya hili…., wakati mwingine nahisi ni kama walipanga ili itokee hivyo, ili wanaiharibie jina na ndoa yangu…’akasema

‘Ehee, kwahiyo … kwahiyo unataka kusema kuwa ulisingiziwa, ..maana nilivyosikia sio mara ya kwanza mlikuwa mkitoka naye,…ndio mkawekewa mtego, mkanaswa..ndivyo nilivyosikia..’nikasema

‘Ni kweli nilikuwa natoka naye..lakini sivyo kama walivyosema walimwengu….mimi nilikuwa namsaidia madamu tu, kwenye mambo yake ya kibiashara, …..’akasema

‘Walisema hilo la kuwa mlikuwa na mambo ya kibiashara mlilitumia kama kisingizio tu..’nikasema

‘Walimwengu hao….sio kweli,..si kweli kabisa ..naambieje ili mnielewe…’akasema akionyesha huzuni machoni

‘Sasa ukweli ni upi , hebu tuambie…?’ nikamuuliza

‘Huyu madamu…..siku moja, alikuja kuniomba, nimsaidie mahesabu yake ya biashara, na alipoona kuwa mimi ni jua mambo hayo ya mahesabu, ndio akaniomba kuwa niwe naye kwenye biashara zake, ana wateja wake, wakati mwingine wanakutana kwenye mahoteli, au hata kusafiri, Zanzibar..nchi za jirani, kwahiyo alihitajia mtu wa kumsaidia,… ambaye san asana anajua mahesabu……kwa vile mimi najua mambo ya mahesabu, basi nikamkubalia, ..si unajua mambo ya biashara yalivyo..’akasema

‘Ok..sasa hebu kwanza nikuulize hayo mume wake anajua, kuwa mkewe yeye ni mfanyabiashara wa kihivyo, au yeye na mume wake wapoje…?’ nikamuuliza

‘Hayo ya familia yao wanajuana wenyewe, ila alinigusia kuwa yeye na mume wake kuna kutofautiana kidogo, lakini hakupenda sana kuongelea mambo yake ya ndani,…ila aliniambia kuna muda mume wakealitaka mkewe aachane na hiyo biashara,  lakini madamu alimwambia mume wake, yeye hawezi kuacha biashara zake kwani walioana akiwa na biashara zake kama hizo,..

‘Madamu alisema  kinachomsumbua mumewe ni wivu, akazidi kusema mbona yeye hamfuatilii mumewe kwenye mambo yake ya kikazi kwani mumewe kuna muda anasafiri na anaweza kukaa huko mwezi, na wanakwenda na katibu wake muhutasi, na huyo katibu wake ni mwanamke, yeye anasema hawezi kumzuia maana anajua ni mambo ya kikazi na cha muhimu ni kila mtu ajichunge ajue umuhimu wa ndoa yake....’akasema

‘Lakini sasa sio ndio hivyo wamethibitisha,..kuwa kweli hamkuwa na mambo ya kibisahara tu, siku hizi kuna utaalamu, kila kitu  kimeonyeshwa wazi kwenye kanda za video..’nikasema

‘Ndio maana nasema baada ya hilo, wanadamu hawatanielewa tena…walimwengu wanachukulia mambo juu, juu tu…, hili ni kama lilipangwa ili linikute, na dhamira yao itimie, wanimalize...’akasema

‘Alipanga nani sasa, mume wa mke, …au mkewe, na kwanini wafanye hivyo, ..?’ nikamuuliza

‘Hapo sijui ….sana sana ninaweza kusema labda walitaka kuniharibia jina langu tu na ndoa yangu,..yawezekana ikawa ni mume ili kunikomoa na kumkomoa pia mkewe…’akasema

‘Lakini..kwanini …ndio mpaka yatokee mauaji, na mbona mume mtu nasikia hakuwepo , alisafiri kikazi, je anahusikanaje na hilo…..?’ nikauliza, na jamaa akatikisa kichwa, kuonyesha masikitiko makubwa

‘Yaani inaniuma sana….na inavyoonekana, ni kuwa mimi ndiye muuaji..lakini sijafanya hivyo,…na mpaka sasa wameshindwa kulithibitisha hilo,kwanini mimi nifanye hivyo…inaniuma sana, nilishazoeana saana na madamu,…siamini..kwanini.…’akasema kwa uchungu

‘Ok..hebu elezea ilikuwaje?’ nikamuuliza

‘ Ni hivi, huyo madamu alipokuja kwangu kuniomba nimsaidia hayo, nilikubali,…lakini kwanza nilimtahadharisha kuwa yeye ni mke wa mtu, kwanini mumewe asihusishwe, tukaongea pamoja, akasema kila mtu ana mambo yake, na biashara yake haihusiani sana na mumewe..labda ikibidi..lakini mume wake ana kazi yake ambayo haimpi nafasi hiyo…’akasema

‘Basi nikakubali, nikawa kweli natoka na huyo mke mtu, nikawa kama mwenza wake kibiashara, ni kweli alikuwa mfanyabiashara mnzuri tu, na alikuwa akipata tenda..yaani anakutana na wafanyabiashara wanaohitaji mizigo mbali mbali, ambayo yeye anaiagiza kutoka nchi za ughaibuni…

‘Ni kweli kwa njia hiyo…., anapata wateja wazuri tu, hata mimi sikuwa nimeamini hivyo,…basi kwa shughuli hiyo na mimi nikawa naambulia kipato humo humo..,kuna  kipindi hata mume wake anakuwepo…hasa tukiongelea nyumbani….’akatulia

‘Lakini kiukweli nilihisi.. kuna hisia fulani kwa mume kwake, hasa  akiniona mimi, zilijionyesha wazi wazi machoni,….nilimuona kama ananiangalia kwa jicho baya, na hata nikifika kwao kwa ajili ya kukutana na mkewe, akiwa kaniita au kuna mkutanio fulani, nikimkuta yeye na kumuulizia mkewe, anakuwa kama hapendi, …hanijibu vyema…’akatulia

‘Basi nikamuelezea mke wake kuwa mume wake anaonekana hapendi, akiniona nikiongozana na yeye ….mkewe akasema ndivyo mume wake alivyo niachane naye hayo ni mambo yake ya nyumbani…basi mimi nikaamini hivyo…’akatulia

‘Ok..kabla hujaenda mbali, je wewe na mkeo wako ilikuwaje je yeye alikuwa hana wasiwasi na wewe, kuwa unakwenda na mke wa mtu kibiashara nk…?’ nikamuuliza

‘Mke wangu alikuwa ananiamini tu, anajua ni katika shughuli zangu za kibiasahara ,…, siwezi kusema hakuwa na wivu, alikuwa nao..kuna kipindi nikipigiwa simu, akiona ni huyo madam, anakasirika, analalamika, kuwa madamu kazidi, ...lakini nilimuelewesha, akawa ananielewa, japo kwa shingo upande,..na mimi nilijua ni swala la muda tu…na mke wangu hakuwa na chuki kama niliyoiona kwa huyo mume mtu…’akasema

‘Ok, sasa ikawaje..?’ nikamuuliza

‘Kuna tenda moja, ilikuwa madamu anakutana na wazungu kutoka Afrika kusini,..hawa walikuwa ni wateja wapia, na mwanzoni tulikutana hoteli kubwa, baadaye hao wazungu wakasema wanahitaji kuona jinsi jamii yetu ilivyo, maana biashara hizo zilihusu jamii san asana…, kwahiyo wakaomba twende kwenye hoteli ndogo ndogo…basi tukafanya hivyo,na tulipofika huko, wakawa wanakunywa pombe,..mimi hwaga sinywi pombe ..kabisa,..kabisa…’akasema akionyesha kiapo

‘Ehe..lakini nasikia wakati mumefumaniwa wote wawili mlikuwa mumelewa, au sio…sasa ilikuwaje..?’ nikamuuliza

‘Subiri nikuambie ukweli, mimi sinywi pombe hata mke wangu analifahamu hilo..siku hiyo, wao ndio walikuwa wakinywa, na madamu, …..madamu yeye huwa anakunywa, lakini sio kihivyo…siku hiyo sijui ilikuwaje,…alikunywa sana,..na hao wazungu wakawa wanapiga picha za video huku na kule, wakisema ni katika mambo ya kujitangaza kibisahara,…mimi sikuipenda ile hali, lakini ningefanya nini

‘Basi , …ikatokea muda mimi nikaenda maliwatoni…’akatulia kama anatafakari jambo….

‘Nikiwa huko nikapigiwa simu na mtu nisiyemjua,..ilikuwa namba ngeni, na nilihisi kama kaigiza sauti, yaweza ikawa …sina uhakika, lakini ni kama mtu anagiza sauti ya kibabe hivi,  akasema;

‘Ndugu yangu jinasue..huyo ni mke wa mtu,….usije ukaja kujilaumu…’ kabla sijamuuliza akakata simu…

Basi nikatoka pale maliwatoni, …wakati natoka nikawa na mawazo sana kuhusiana na hiyo simu, ni kama nafsi mbili, moja inaniambia niondoke, na nisirudi pale mezani na nyingine inaniambia nirudi tu, hakuna tatizo…

Wakati nawaza, nikawa natembea na nikajikuta nimeshafika pale mezani, lakini akili , au nafsi ikaniambia niamuage madam, kuwa mimi naondoka,….

Nikapanga hivyo kweli, na nilipofika mezani kiuungwana, nakamalizia kinywaji changu- ilikuwa soda, sprite,..nilipoimaliza tu , nakumbuka kabisa, hapo nikaanza kuhisi vingine…hapo ninahisi .., waliniwekea kilevi…sijui ni nani, maana huyo madamu alikuwa kalewa hajitambui,..na hao wazungu ..sio watu wakufanya hivyo..kabisa, siwezi kuwasingizia..’akatulia

‘Sasa ni nani alifanya hivyo.?’ Nikamuuliza.

NB: Hili ni tukio la ina yake,  ni kisa kigeni kabisa, nimeona nikiweka hewani kabla hakijapoa


WAZO LA LEO: Tuweni makini sana, na wake au waume za watu, hasa tunapojikuta kwenye maungano au ukaribu wa aina mambo mbali mbali, yawezekana ikawa ni ya kikazi au ya kibiashara, kama ni lazima, ya kusafiri au kufanya mambo ya kuwa wawili kati ya wanandoa tofauti.. .tuhakikishe kuwa tunachukua tahadhari, tukijiuliza hivi mimi ningefanyiwa hivyo ningekubaliana nalo, na ni vyema kukawa na makubaliano manzuri kati ya wanandoa. Ni kweli mtu hachungwi, na kila mtu anajua jinsi gani ya kujilinda, lakini dunia ina mengi… na tukumbuke hisia za watu kwa wenza wao wa ndoa zipo ndani, wivu hauwezi kukwepeka, ndiyo asili  ya mwanadamu ilivyo.
Ni mimi: emu-three

No comments :