Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeThursday, October 27, 2016

TOBA YA KWELI-15


‘Sasa kabla sisi hatujaondoka, maana tunasafiri mimi na mke wangu leo…, basi mimi ninataka kutimiza ile ahadi yangu kwako…, ile ahadi niliyokuambia kuwa ukiweza kumfanya mke wangu akarudi, basi kwanza kwa moyo mmoja, nitakuwa nimeweza kukusamehe kiukweli-kweli kutoka moyoni…nilishakusamehe…lakini bado nafsi yangu ilikuwa inaendelea kusononeka….

‘Sasa ….nipo na furaha,..sina kinyongo na wewe hapa duniani na kesho ahera…’akasema.

‘Nashukuru kwa hilo…’nikasema.

‘Lakini hata hivyo ..nitakuwa na uwezo sasa wa kukuambia kile nilichoagizwa, ambacho kilitegemea haya yote,….baada ya hayo uliyoyafanya… natumai hili lililobakia ndio itakuwa kazi yako ya mwisho…kwa hili sasa utakuwa umepata msamaha wa huyo aliyetuagiza…., labda kama una mengine, ambayo ulikuwa bado hujayatekeleza…’akasema docta.

‘Mhh…sijui, nimejitahidi  kadri ya uwezo wangu,..mimi sijui nimeshatubu, nimemuomba mungu msamaha, nimawaomba wote niliowakumbuka …ambo aniliwakosea, na yote hayo nimeyafanya kwa moyo mkunjufu…sasa sijui kama wao wamenisameeh kweli kama walivyonitamkia,….mmh, sasa docta  wewe niambie tu…hicho ulichoagizwa…’nikasema.

‘Hili agizo, kama nilivyokugusia awali, linatoka kwa mke wako mwenyewe….’akasema

‘Mhh, sawa, alisema nini,..au kakugiza nini tena…maana wewe na mke wangu, kweli mlishibana, …lakini usijali mimi nimekuelewa wewe niambie tu…’nikasema

Docta kwanza akasimama, na kujinyosha, akatembea hatua kadhaa hadi kwenye dirisha akaangalia nje,..halafu baadaye akanigeukia, akasema
‘Kwanza nikuulize yule binti anayekusaidia hapo nyumbani bado yupo…?’ akaniuliza, na mawazo yangu yakaenda mbali, najua wengi, hawaniamini, wanasema labda huyo binti kawa hawara yangu, lakini kiukweli,…sina hisia hizo kabisa , huyo binti yupo hapo nyumbani kama hayupo,

‘Kwanini unamuulizia, ninajau wengi mna hisia mbaya dhidi yangu,…nikuambie ukweli, mimi.. sina hisia zozote kwa huyo binti, na bahati mbaya nimetokea kumchukia sana, na nimekuwa nikimkemea kumsema mabaya, kila anachofanya lakini amekuwa akinivumilia tu…nilitaka aondoke, lakini haondoki….sijui kwanini….

‘Mimi sina wazo hilo, nimekuuliza tu, maana ni lazima uwe na mtu wa kukusaidia,…ni kawaida, nilitaka niwe na uhakika huo, na kama hakuna mtu nikutafutie…’akasema docta

‘Wa nini…sihitaji mtu, ningefurahi kama ningebakia mwenyewe, huyo binti bado yupo, nilishamwambia aondoke, lakini anasema eti alishauriwa na mke wangu awepo kunisaidia, ..kiukweli mimi simtaki…’nikasema

‘Kwanini humtaki, kwanini unamchukia kihivyo, nakumbuka siku moja ulianiambia kuwa yeye ndiye aliyekuchonganisha wewe na mkeo, ya kuwa yeye ndiye anayemuambia mkeo siri zako, na kumfanya mkeo akufikiria vibaya, lakini..sio kweli, kutokana na maelezo ya mke wako..huyo binti hajawahi kumwambia lolote kukuhusu wewe, hata alipojitahidi kumuuliza…’akasema docta.
‘Kwani atakubali..achana naye….’nikasema.

‘Huo ndio ukweli…’docta akasema, na kuongozea.

‘Au una jingine kubwa la kukufanya umchukia huyo binti…?’ akaniuliza docta, na kabla sijamjibu akasema;

‘Huyo binti wa watu hana kosa…hebu fikiria, yeye yupo nawe usiku na mchana…anakusaidia sana, hakujali kuwa uliwahi kutaka kumdhalilisha, hajaogopa kukaa karibu na wewe…na sijui unamlipa shilingi ngapi..lakini hajali hicho kiasi kidogo unachomlipa…’akasema

‘Kasema namlipa kiasi kidogo, unaona jinsi alivyo…naona anatoa siri za ndani kwaa watu sasa, yaani leo nikifika anaondoka,…’nikasema kwa hasira.

‘Jirani …hajaniambia hivyo, ila kama upo na hali mbaya useme, nikusaidie kumlipia, maana huyo ni mfanyakazi, na moja ya sharti la mfanyakazi, ni kuwa alipwe kabla jasho lake halijakauka….’akasema

‘Nikuulize docta, huyo mwanamke, ..mmh, huyo binti, amekuja kwako kulalamika kuwa sijamlipa mashara wake,…?’ nikamuuliza.

‘Hapana,..sijawahi kukutana naye tokea mkeo afariki, nilijua labda keshaondoka kwenda kwao, lakini nikasikia kwa watu kuwa bado yupo….sasa nilitaka uhakika tu…na najua hali yako, …kama naweza kusaidia hilo niambie tu…’akasema

‘Huyo binti bado yupo lakini ataondoka, kama sio leo basi, kesho, mhh…mimi simtaki…’ nikasema, ni kweli moyoni nilishatokea kumchukia huyo binti sijui kwanini, ..pamoja na moyo wangu kuwa kwenye imani, na ya kuwa sitakiwi kumchukia mtu, lakini kwa huyu binti, kila nikimuona nahisi hasira tu…sijui kwanini..ninamchukia sana huyu, nahisi nifanya jambo baya, kama kumpiga,..kumsema ovyo… wakati mwingine natamani kusema  yeye ndiye kachangia mke wangu…lakini nihisia tu!

‘Huyu binti wa watu, hana tabia mbaya, kama unavyomfikiria, na kama una hisi zozote mbaya dhidi yake…, unahitajika kumuomba msamaha, vinginevyo utakuwa hujakamilisha zoezi lako la toba….’akasema

‘Na hilo lipo kwenye hayo maagizo,na je ulitaka kuniambia na hilo..mimi sijamdhania huyo binti kihivyo, ila simpendi tu, na naona akiendelea kuwepo hapo, watu wataendelea kunifikiria vibaya,..kwa hivi sasa mimi sipendi kueleweka vibaya na watu…nata niwe huru, kimwili na kiroho…’nikasema

‘Haya kama humtaki huyo binti akusaidie, basi  mimi nipo tayari kukutafutia mtu mwingine ambaye atakusaidia kwenye kipindi hiki kigumu, na nitakusaidia kumlipa, unasemaje kwa hilo…?’ akasem na mimi nikasema;

‘Hapana, haina haja …’ Na niliposema hivyo, docta akatulia kama anawaza jambo, na mimi nikasema;.

‘Mhh..unaonaje ukiniambia hilo agizo, au hicho ulichataka kuniambia, au ndio hilo la kumuomba huyo binti msamaha, kama ni hilo, nilishalifanya, ila nimeona akiendelea kuwepo hapo nyumbani, nitazidi kumchukia, kumsema sema, na…sipendi tu awepo…’nikasema nilipoona kama anapoteza muda.


***********

‘Jirani, kwanza mimi natimiza kile alichoniagiza mke wako…sifanyi haya kwa matamanio yangu, maana mambo mengine ni mambo binafsi, na mtu akishafiwa inachukua muda sana kusahau, hasa akifiwa na mwenza wake…’akasema

‘Mhh..’nikaguna hivyo tu

‘Lakini mkeo alitusisitizia sana kuhusu hilo…aliyaona maisha yako ya mbeleni kabla hajafariki, na aliwekeza kwa hilo, akapanga mambo mapema, uone jinsi gani alivyokuwa anakupenda…’akasema na mimi nikakaa kimia

‘Mkeo alituagiza kuwa, akishafariki,… ukapita muda wa mambolezo, ukapita muda muafaka, na ukayatimiza yale yote uliyokuwa ukifuatilia, likiwemo hilo, la wewe kufanya jambo litakaloweza kunirizisha mimi,..na moyo wangu ukawa mweupe dhidi yako, basi alisema kwa kauli yake kuwa wewe uoe haraka iwezekanavyo..’akasema

‘Eti nini..acheni hayo jamani, hata nyie..…huo sasa ni uhuni, mimi nioe, hahaha….hapana,..hilo siwezi ku-ku-kubalia, hata siku moja, sitaki kusikia swala la kuoa, niliyempenda keshaondoka, na mimi nilishakufa kihisia, sitaki sitaki tena mahusiano na wanawake……’nikasema.

‘Kwanini, unasema hivyo, una wasiwasi gani,…?’ akaniuliza docta

‘Sio swala la wasiwasi,… wewe unasema hivyo kwa vile hayajakukuta, na hata hivyo, mimi mwenyewe nafahamu matatizo yangu, sitaki tena haya yaliyopita yaje kunitokea tena, sitaki, namuomba mungu anisaidia nibakia hivi mpka siku ya kuitoa roho yangu …mmh’ nikatulia kama vile nimetamka neno gumu sana.

‘Hebu jirani, nipe sababu za msingi mimi ninakusikiliza,…maana hujanishawishi ni kwani ni hutaki kuoa… unakumbuka nimekuambia nikirudi nitahakikisha nafuatilia afya yako, nataka nikupime nione tatizo lipo wapi, ….’akasema.

‘Ili iweje….tatizo gani, ..mimi siumwi..sina tatizo, na yaliyopita, haya maana tena kwangu, sitaki hata kuyasikia, maana nafsi yangu ilijawa na ubinafsi wa kutaka kutafuta mtoto, kumbe namuumiza mwenzangu, na kwa hilo nastahiki kuadhibiwa, …na moja ya adhabu yangu nikubakia hivi…peke yangu bila kuoa…halafu nyie mnasema nini, eti nini…?’ Nikawa kama nauliza.

‘Unakumbuka mkeo alikuhangaikia sana, na nia yake ilikuwa nyie mpate mtoto kweli si kweli....unakumbuka mke wako alikuhangaikia sana, nia uweze kuishi maisha ya furaha, hata kama yeye hayupo hapa duniani, kwahiyo wewe,  sasa unataka juhudi zake zipotee bure, ndio maana yako….’akasema.

‘Docta, ninataka unielewe, mimi sasa siyo yule mtu wa zamani aliyekuwa na tama hizo, mimi sina hisia zozote tena, nioe ili iweje, kifupi mimi…sitaki kuoa,..hilo liondoe akilini mwako, ..hata angelikuwa nani, nimeshasema ninataka kuishi hivo hivi mpaka siku ya kumfuata mke wangu huko alipo,…’nikasema.

‘Sikiliza,…sio mimi ninayetaka wewe uoe…hili ni agizo la marehemu mke wako, kama kweli unampenda, na kama kweli bado unaendelea kumpenda basi ulitimize hilo, na kama ulikuwa unampenda kinafiki, basi endelea kukaa hivyo unavyotaka wewe…, mimi siwezi kukulazimisha kwa hilo…, lakini nina uhakika hutaishi kwa amani, utakuwa ukitokewa na mkeo mara kwa mara..’akasema.

‘Hilo docta, siwezi, acha nieleweke hivyo, ni bora tukosane tu…ni bora na hata yeye kama alilitaka hilo, basi anielewe hivyo,… kwasababu hizo ni hisia zangu,….kifupi mimi sitaki , sitaki kabisa kuoa tena…kama agizo lilikuwa  ni hilo basi ngoja mimi niondoke…’nikasema na kusimama kutaka kuondoka.

‘Unajua, mimi nimeshafahamu ni kwanini hutaki kuoa….najua unajiuliza baada ya haya yote ni nani atakayekukubali wewe umuoe, kwa hali ilivyotokea ni kama ulijiweka uchi kwa jamii, naelewa sana hilo..lakini mkeo alishaliona hilo na alishajipanga kwa hilo…, na kila kitu alikiweka wazi,…’akasema

‘Hawezi kuingilia hisia zangu…na ni kitu gani alikiweka wazi kuhusu mimi, kama ni hilo la kuoa, hilo siwezi kukubaliana naye, sawa, hapo mimi na yeye hatutaelewana, na najua huko alipo atanielewa,…kwahiyo jamani, kama ni hilo, naona tuachane, kwaherini….’nikasema sasa nikiwa nimedhamiria kuondoka.

‘Jirani, mimi ni metimiza wajibu wangu,…kwanza kukuambia agizo hilo, lakini hilo agizo halijakamilika, kama nilivyokuambia,…mkeo alipanga kila kitu juu yako, kwa nia ya kukusaidia,..sasa subiri kwanza nimalizie agizo lake, halafu wewe mwenyewe utakuja kuamua …kwenye maamuzi ni sisi hatutaweza kukuingilia…’akasema docta.
‘Agizo gani jingine…maana hilo peke yake sijakubaliana nalo, …kama kuna jingine la namna hiyo, basi nyie acheni tu, maana naona nyie mnafikiria kirahisi rahisi tu, mtu afiwe na mkewe, halafu haraka akimbilie kuoa, ..hivi mnalionaje hili, mnanionaje mimi…’akageuka kumuangalia docta na baadaye akageuka kumuangalia mke wa docta

Mke wa docta muda wote alikaa kimia, akisikiliza, na alipoona anaangaliwa, akajua kuwa na yeye anahitajika kutoa mawazo yake, akakohoa na kusema;

‘Samahani niwaingilie kidogo, maana hilo hata mimi linanihusu, hata mimi niliwahi kupewa hayo maagizo,…wakati marehemu mkeo ananiambia mimi kuhusu hilo,mimi nilichukulia kimzaha tu, sikulitlia maanani, lakini  sasa nimeliona lina umuhimu wake…’akasema

‘Shemeji mimi ni mwanamke, na hayo aliyokuambia mume wangu, kama ningekuwa sijaisikia kauli ya marehemu mke wako, ningelipinga….kabisa, ningepinga swala la wewe kuoa kwasasa…maana ningelichukuliaa kuwa ulisubiria mkeo afariki ndio ukimbilie kuoa…lakini mimi niliambiwa na kukokotezewa, nikasisitiziwa…kwahiyo hata mimi nilazima nitimize wajibu wangu huo kukuambia…hayo ni usia kutoka kwa mkeo…’akatulia na mimi nikabakia kushangaa, halafu nikasema;

‘Kwahiyo shemeji unamuunga mume wako mkono..hujielewi kuwa na wewe ipo siku unaweza ukaondoka, na mumeo akakimbilia kuoa kwa haraka kweli inapendeza …’nikasema

‘Naelewa sana shemeji,…..na hujui kwanini mkeo alisema hayo, hujui ni kwanini mkeo alikuhangaikia hivyo…alijua angekuambia muda ule akiwa hai usingelikubali hilo…, alikuwa tayari umuolee mke mwenza…lakini …’hapo akatulia.

‘Mwambie…’akasema mume wako alipoona mkewe kabakia kimia

‘Lakini alisubiria umalize maombi yako ya toba…na alishaona dalili za toba yako kuwa ni za kweli,..aliniambia wewe sasa ulishaiva, yamebakia mambo machache tu , ..na sasa hata akiondoka, utakuwa umeshafanikiwa kuwa mume mwema….hata sio kwake, lakini kwa huyo utakaye muoa… na hilo la wewe kuoa, alilitaka ulifanye kwa haraka, usichelewe, ili upate matunda yake, sijui kwanini alisema hivyo…’akasema mke wa docta.

‘Jamani kama ni hilo, niacheni tu..kama agizo lenyewe ndio hilo, ..mimi sipo tayari kabisa leo a hata kesh…mimi kwasasa niseme hivi…, nawatakia safari njema, ..’nikasema nikianza kuondoka.

‘Lakini hatujamaliza, mkeo hakutuagizo hilo tu…’akasema docta na mimi nikasita kuondoka, nikatulia.

‘Na mimi siweki kuondoka bila kukuambia yote aliyotuagizia mkeo…maana hayo maagizo hayataki kuchelewesha, kama ni kuchelewesha iwe juu yako….na lolote likitokea tusije kuja kulaumiwa na mbele ya mungu tuwe salama, ….’akasema docta, na mimi nikasimama pale pale…moyo ukianiambia ondoka haraka lakini miguu ikawa mizito.

Niliyoyasikia baadae, sikutaka hata kusubiria,...niliondoka humo ndani hata bila kuaga, nikiwa nimejaa hasira..…..

NB: Alisikia nini….


WAZO LA LEO: Tupende kuwa na subira na baadae kushukuru pale tunapopewa nasaha au ushauri, hata kama anayekupatia huo ushauri kwako unamuona hana maana, labda kihali .kielimu, kiumri, ..hata kitabia, lakini yeye akaamua kukupatia nasaha, au ushauri. Usikilize kwanza, na ufanye busara kumshukuru huyo mtu. maana ushauri mwingine waweza kupitia kwa mtu, lakini umetoka kwa muumba wako. 

Ni mimi: emu-three

3 comments :

Anonymous said...

Mkuu mbona wachelewesha mambo

Anonymous said...

Naona wewe sasa kazi imekushinda...

Anonymous said...

Vipi sehemu ya mwisho..ulisema ni sehemu ya mwisho au?