Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeFriday, October 21, 2016

TOBA YA KWELI-14Docta alikuwa amekaa kwenye sofa akiwa na mkewe, nyuso zao zilitawaliwa na furaha,..hata mimi moyoni nijisikia furaha,…kwanza docta akambusu mkewe shavuni halafu akasimama na kunujia, akanikumbatia kwa nguvu,..huku akinishukuru sana, halafu akasema;

‘Mkuu, hata sijui nisemeje..ngoja nirudi ….’akasema

‘Una safari,…..au ndio hiyo ya…..’nikasema na yeye akanikatisha na kusema;

‘Kabla sijaondoka,..hatujaondoka ….’akamgeukia mkewe.

‘Mimi ninajua nina deni kubwa kwako…hili sio mimi,…’akatikisa kichwa na akakunja uso kama anawaza kitu, halafu akaniangalia na kusema;

‘Haya ni maagizo niliyopewa na niliambiwa nifanye kama ifuatavyo…, na ndivyo hivyo nilivyokuambia na-, na eeh,…., kwa jinsi nilivyoagizwa, mimi, imebakia hilo agizo moja,..baada ya hilo, hayo mengine sijui, kama kuna watu ulikuwa hujawafikia, ukawaomba msamaha, hilo ni juu yako, ..ni hili ni agizo , mimi natimiza wajibu wangu tu..…’akasema

‘Mhh, docta, sijakuelewa, ni agizo ..kutoka kwa nani…?’ nikamuuliza nikiwa na mashaka, maana nakumbuka mtu wangu wa imani aliniambia maneno kama hayo, kuwa nifanye mambo kadhaa ili nifanikiwe kwenye matatizo yangu, sasa isije ikawa ndio huyo huyo....

‘Hahaha, eti kutoka kwa nani…unajua mkuu.., hebu kaa kwanza,....utulie…’akasema akiniashiria nikae maana nilikuwa bado nimesimama, nikiwa na hamsa fulani, nilitaka kuyafahamu hayo maagizo ambayo yalisubiriwa mpaka nitimize hilo la kwenda kumshawishi mkewe arudi nyumbani, 

Mimi nikasogea kwenye sofa, nikakaa..na kutulia,... kukawa na ukimia fulani halafu docta akasema;

‘Tuna muda kidogo……’akasema docta akiangalia saa yake, halafu akamgeukia mkewe, halafu mimi,... na mimi nikasema;

‘Mhh…unajua  docta mimi nimekuwa nikisoma shajara ya mke wangu, na mengi aliyokuwa ameyaandika, nikijaribu kuyafuatilia, nafanikiwa, au kupata jambo fulani, sasa uliponiagiza niende kumfuata mkeo, nilijaribu kutafuta kwenye shajara hiyo kama kuna agizo kama hilo,mhh sijaona,..

'Sasa, kuna kitu nilikuwa nakisoma kabla sijafika hapa, aliandika hivi,…. ‘….nimemuacha mume wangu nikiwa na huzuni, …sikuweza kutimiza kile alichokitaka, hili kwangu naliona kama deni,..sijui ni nani wa kunisaidia kulilipa,… lakini ninaomba ,..’

‘Mmh, hapo nakumbuka  aliandika… ‘ namuomba mungu, kama inawezekana hicho anachokitaka ...kipitie kwa wapendwa wangu…..` hicho anachokitaka …’ nahisi ninachokitaka mimi au sio, mhh, ninachokitaka mimi, hapo nimeelewa, najuata kwa hilo, maana hilo lime..oh, nisamehe sana mke wangu, sijui huko ananisikia, sijui, mungu wangu ndiye unayelijua hilo, hata sijui…?’nikawa naelezea huku nikijaribu kukumbuka ilivyokuwa imeandikwa…

Docta akawa anatikisa kichwa kama kukubaliana na mimi..hata sikuelewa anakubaliana na mimi kuhusu nini hasa, hiyo kauli yangu au hayo niliyoyanukuu kutoka kwa shajara ya mke wangu….mimi nikaendelea kusema;

‘Na, …na, najiuliza sana, hivi, mmh,  hao wapendwa wake ni akina nani hasa, na wewe, ni nani,...hata sijui….’nikamalizia hivyo na docta akatabasamu na akaendelea kutikisa kichwa halafu akasema;

‘Umeoanaee, mkeo alishayaona maisha yako ya kabla , kutokana na ibada ya mkeo ya muda mrefu,yeye alijawa na hisia za mbeleni, wengine wanaita ...maono…au sio,..kutokana na kumuomba mungu kwake…alishaweza kuonyeshwa mambo ya mbeleni…, na ndio maana siku ile alipozidiwa, ilibidi aniambie tu, kwa mdomo, maana hiyo diary yake hakuwa nayo siku hiyo.

‘Alisemaje…?’ nikauliza nikiwa na hamasa kuyasikia hayo aliyoongea mke wangu, japokuwa nilikuwa na hamasa zaidi ya kujua hicho alichoniitia docta, 

Docta alitulia, akabadili sura ya kuwa na huzuni na ndipo akaanz kuelekezea siku hiyo, ilivyokuwa;

                 *******
‘Docta najua mimi sitapona, …naiona saa yangu ya mwisho….nateseka sana docta, maumivu ninayoyahisi sasa..hata baada ya dawa ya maumivu lakini..ooh’ akawa anagugumia kwa maumivu…’akasema docta akiijaribu kuigiza sauti ya mke wangu.

‘Docta , ..namuomba mungu anaichukue roho yangu haraka…, ila kwa sasa nakuomba jambo moja, najua mengi nimekuwa nikiyaandika kwenye `diary ’ imekuwa hulka yangu hivyo,…nina imani mume wangu atakuja kuiona hiyo shajara,  na kuyasoma yote,….kama hatayaona naomba uje umuelekeze atafute hiyo diary, ipo kwenye kabati langu ataiona tu….’docta akatulia.

Akaendelea kusema docta, ….`muda huo mkeo anaongea kwa shida, …na ukumbuke muda ule hakuwa na hiyo shajara yake, yupo chumba cha wagonjwa mahututi, yupo mimi na yeye tu... mkeo anapenda sana kuandika mambo yake kwenye `diary’…hata mimi ilikuwa hivyo zamani, lakini nikaja kuacha,…’akasema docta, halafu akatulia kama anawaza jambo, na mimi nikasema;

‘Docta mimi naomba uniambie hayo maagizo,….’nikasema nikikwepa kutoa machozi maana niliona kama ananikumbushia mambo yenye kunizidishia huzuni.

‘Nitakuambia ….maana ni muhimu,..ila nilitaka kuanzia hapo, …’akasema docta na kutulia,..hii hali ya kuongea na kutulia ilikuwa ikinitesa, nilitaka aongee kwa haraka haraka, lakini…

‘Sasa, unajua docta …mmh, sijui kwanini,…. kwahiyo unataka kusema yeye, ndiye alikuambia ufanye hivyo kabla hajafariki....sijaona lakini..kwenye shajara...hajaandika hivyo...'nikasema.

'Hajaandika kuhusu nini...?' akaniuliza

' Kuwa unitume mimi nikaonane na mke wako, halafu,…sasa, hebu unifafanulie hapo, maana mimi sijakuelewa..?’ nikamuuliza

‘Naweza kusema  hivyo `ndii-ooh’…' akasema na kutabasamu

'Japokuwa hakuwa na maelezo hayo ya moja kwa moja, lakini hata mimi nilikuja kuliona hilo kuwa kwa kupitia wewe, hili swala langu lingelifanikiwa, maana kisa cha tatizo ni nani, ni wewe au sio…?’ akaniuliza na kuniangalia na mimi nikaguna tu.

'Mhh...'

‘Na…wewe ulishaamua kujitakasa,…na hilo ni moja ya mambo ulitakiwa uyafanye…au sio…uende kwa mke wangu ukutane naye…umuombe msamaha au sio, umuelekezee ukweli wote, au sio…. na najua mungu ameshaanza kukisikia kilio chako, maombi yako..,siumeona eeh,  nashukuru sana maana sasa nipo na mke wangu….’akasema akum-mpambaja mkewe.

‘Hata mimi nimefurahi sana kwa kweli….sikutarajia kuwa shemeji engelifika…nilimuomba sana mungu afike….usiku sikulala, nilikesha nikiomba…’nikasema nikiwaangalia kwa macho ya wivu

‘Unajua kiukweli, wewe sasa umefanikiwa, kiukweli wewe sasa hivi moyo wako umeshasafishika,…sasa kila utakachoomba mungu atakutimizia kwa mapenzi yake lakini,…lakini kuna jambo, …’akatulia akiangalia saa, nilijua anaogopa kuwa atachelewa na mimi nikaliona hilo, kwahiyo nikasema;

‘Shemeji…’nikasema nikimgeukia mke wa docta

‘Namu shemeji….’akaniitikia,

‘Mhh…hata sijui…..lakini nakumbuka wakati tunaondoka mzee wako alituagiza nini, mimi na wewe mguu kwa mguu, tumchukua huyu jamaa,…. sasa siku ya ngapi leo, mzee atakuwa kwenye hali gani jamani, au kuna taarifa gani kutoka huko, maana ubinafsi umetutawala zaidi…?’ nikasema na kuuliza.

‘Shemeji nakumbuka sana hilo,..ndio maana tukakuita uje kwa haraka, maana sisi hapa tupo safarini,…na kifupi tu, baba hajambo,…na hahaha..unajua haya mambo unaweza ukacheka, lakini hucheki kwa raha,..unajua baba kabadilika kabisa,sio yule baba ninayemfahamu mimi,..eti,  keshatoka hospitalini na kuanza ile kazi uliyokuwa ukiifanya wewe…’akasema

‘Kazi gani hiyo niliyokuwa nikiifanya mimi,… acha mzaha, mimi kazi zangu za nguvu, na mzee wako, hastahiki kuzifanya hizo kazi, au…, ni kazi gani….?’ Nikauuliza

‘Kazi ya toba……’akasema na mimi nikatabasamu, na kusema;

‘Oh, hahaha, TOBA, mhh, nahisi hiyo itakuwa `toba ya kweli ‘…..nimefurahi sana kusikia hivyo, kumbe sipo peke yangu….’nikasema.

Docta akaingilia kati na kusema;

‘Sasa kabla sisi hatujaondoka,..nataka kutimiza ile ahadi yangu kwako…, na najua hutaniangusha kwa hilo…kwani, …eeh, kama nilivyoambiwa,… hiyo ndio itakuwa kazi yako ya mwisho, baada ya hapo….mmh, mungu mwenyewe anajua, nikirudi tu, nitakuhitajia hospitali, tufanye check up….’akasema docta.

‘Sawa, mimi hilo sina shaka nalo, siumwi, sasa hivi najihisi mzima, yale matatizo, ile hali, lakini bado,…nina tatizo, mmh, lakini yote namuachia mungu,…’nikasema

‘Ni kweli….najua unataka kusema nini…’akasema docta

‘Haya..kama mnasema mzee hajambo, basi mimi nipo tayari kukaa kusikiliza kuwasikiliza kama sitawachelewesha mnaondoka na usafiri wenu au kwa njia ya basi….’nikauliza

‘Usafiri wetu , ndio maana sina shaka….’akasema

‘Maana …mimi  si nipo, mkirudi tutaongea au…?’  nikasema japokuwa moyoni nilitaka niambiwe haraka hicho alichotaka kuniambia.

‘Hilo haliwezi kusubiria kwa sasa, inabidi nikuambia ili nikirudi nikute matokeo,…kiukweli hilo  lina haraka ...na ni muhimu sana kwako,sikutakiwa nicheleweshe hivi, lakini pia ilitakiwa lifanyike , eeh….baada ya hili zoezi kukamilika, niliambiwa hivyo..na nashukuru kuwa kila kitu kinakwenda sawa…., sasa iliyobakia ni sehemu ya mwisho tu, ambayo, usipoitekeleza, basi….’akatulia

‘Mhh, kwanini…..sijaelewa, ni nani alisema hivyo, …?’ nikauliza

‘Ni huyo aliyeniagiza nikuambie, ..na haya yeye, alisema hivyo, `…usipolitekeleza hilo…, basi’ hakunimalizia,….sasa sijui hiyo ` basi…’ ilikuwa na maana gani…’akasema docta

‘Mhh, ina maana hayo aliyasema mke wangu au kuna mtu mwingine zaidi yake...?’ nikauliza.

Docta akatikisa kichwa, huku akitabasamu, halafu akabadili taswira ya sura yake, nakuonekana anazama kwenye huzuni, kumbukumbu ilimtawala zaidi.  Kwa kipindi hiki kifupi niliona jinsi gani docta alivyoasirika, baada ya mke wangu kufariki, haikuweza kufichika machoni mwake.

‘Kama nilivyosema, mke wako alishakuwa mtu mwingine,..japokuwa hakuweza kuyazuia mauti, maana umauti hauzuiliki, muda ukifika umefika,..na nahisi ndio maana alipotamka kuwa anaomba kifo kimjie haraka, mungu hakumchelewesha…’akasema docta

‘Sawa…naona huko upaache, niambie docta,..hilo unalotaka kuniambia…’nikasema

‘Hayo,…ya kwenda huko, kufanya hili na lile, niliyokuagiza mimi, ndio aliyasema mkeo…., marehemu mkeo…,’  akigeuka kumwangalia mke wake, akapitisha mkono wake nyuma mgongoni kwa mkewe, na mkewe akajiegemeza begani kwake hadi raha…nikawaonea wivu.

‘Sasa sikiliza maagizo haya kwa makini ….’akasema docta akiangalia saa yake.

NB: Mhh..mbona maneno yanazidi kuwa mengi…nashindwa kumalizia hapa, basi tuishie hapa kwa leo, sehemu iliyobakia sio ndefu saana, …ngoja niwape muda wa kupumua,na kujiandaa na ijumaa. Ijumaa kareemu

WAZO LA LEO:  Kumbukumbu ni muhimu sana katika misha yetu, kumbukumbu ni historia yenye kudumu, na inakuja kusaidia, au kuwasaidia wengine baadaye. Kuna wengi hawalijali hili, lakini lina umuhimu wake.  Na tujenge tabia ya kuweka kumbukumbu zenye manufaa, zenye heri, maana kumbukumbu hizo zinageuka kuwa nyenzo, au rasilimali, kwahiyo zikiwa ni za wema, malipo kwako, wewe uliyetengeneza kumbukumbu hizo, au yaraka hizo,.. ni makubwa, unapata Baraka na thawabu, zikiwa kinyume chake, ni madhara pia.

Wapo wengi wetu , wamekuwa wakiandika tu, tunaona ni kawaida tu..uzushi, fitina , mambo machafu yenye kuathiri kizazi..nk..tunaona ni kawaida tu... Lakini hala hala mti na macho, maandishi ni kumbukumbu na ushahidi wa kudumu, ipo siku utasimamishwa na hayo uliyoyaandika yatatolewa kama ushahidi,…sijui utajiteteaje…


Tumuombe mola atupe hekima ya kuyapima yale tunayoyaaandika, ili yaje kuwa neema na msaada baadaye, na atuepushe na kuandika mambo mabaya yenye kuharibu jamiii…..Aamin
Ni mimi: emu-three

No comments :