Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeThursday, October 20, 2016

TOBA YA KWELI-13


‘Pole sana shemeji, nafahamu kuwa upo kwenye wakati mgumu sana, nakumbuka sana dada aliniomba sana,…..’ilikuwa sauti ya kike, na kwangu mimi sikupenda kabisa kusikia sauti ya kike hapo nyumbani kwangu, nilitamani sauti ya kike iwe ni ya mke wangu. Najua mke wangu hayupo, ..ndio maana sikutaka sauti..kama hiyo niisikie tena, inanikumbusha mbali…

‘Lakini ile sauti ilinifanya nishtuke na kukaa vyema, kwani nilikuwa kama nimepitiwa na usingizi, na niliyekuwa nikimuota kwa muda huo mfupi, alikuwa ni mke wangu,  kanijia na kuanza kuniliwaza, na akawa ananielekeza jambo…kabla sijaelekezwa ndio nikashutuka,  sasa suti iliyokuwa ikitoka kwa mke wangu kwenye ndoto, ni sawa na huyu mdada .Kiukweli sauti za wawili hawa zinafanana.

‘Mhh…samahani lakini nilishakuambia uondoke, urudi kwenu, maana sasa hivi sitaki ….sitaki….samahani unielewe, sio kwamba nakufukuza, lakini una..sauti…oh…’nikasita.

‘Kuondoka nitaondoka shemeji…., japokuwa itakuwa kinyume na matakwa ya dada, ..dada aliniambia nikusaidie, …mpaka hatua ya mwisho, sasa nikiondoka sasa hivi itakwua ni vibaya hujaweza kupona, hujaweza...ndio maana sipendi kuondoka…’akasema kwa sauti ya upole.

‘Sihitaji msaada wako, unanielewa, maana badala ya msaada unazidi kuniumiza, unazidi kunikumbusha, si-si-, wewe ondoka tu, mimi nitakuwa sawa..…’nikasema.

‘Dada aliniambia …..’akataka kusema jambo na mimi sikutaka kabisa kumuambia, haraka nikasimama na kuelekea chumbani.

Kule chumbani nilikaa nikiwaza nifanye nini, kwni docta ameshaniweka mahali pa gumu sana, na ahadi ni deni… na mara akili ikaniambia kwanini nisichukue hatua tu, kama ni kufa nitakufa tu…kwnini nisifunge safari tu, niende huko alikonituma docta, litakalo tokea na liwe…yaani ilikuja hali hiyo na bila kupoteza muda, nikaingiwa na nguvu za ajabu. Nikatoka nje na kumkuta huyo mdada akijiandaa kuondoka.

‘Samahani usiondoke, mimi nina safari, na nyumba haiwezi kubakia peke yake….samahani lakini, kwa kauli zangu za awali, naomba unielewe tu…, nimechanganyikiwa…’nikasema.

‘Wala usijali shemeji…lakini nilishapanga kwenda kusalimia nyumbani unajua ni muda mrefu sijafika huko.., ila kwa vile una safari ya muhimu naweza kusubiria tu, ukirudi na mimi nitaondoka…’akasema.

‘Sawa….nitashukuru kwa hilo…, mimi nitaondoka kesho alifajiri, na sina haja ya kukuamusha,…’nikasema na kurudi chumbani kwangu. Kiukweli sijui kwanini, kama huyu binti asingelikuwa mvumilivu angelishaondoka mapema, maana nilimuonyesha chuki za wazi, …kila alifanyalo kwangu nililiona ni baya, japokuwa alikuwa akifanya kwa usahihi….alijitolea sana kwa ajili yangu, lakini sijui kwanini….

**********

Ni kwei nilifunga safari hadi nyumbani kwa wakwe wa docta, nia kukutana na mkewe, mke wa docta! Na…., nilifika mchana tu… , sikuwapigia simu kuwa ninatarajia kufika huko…,kwahiyo ilikuwa safari ya kuwashutukizia tu,….Nilipofika hapo nyumbani nilikuta kupo kimia, nikapiga hodi…

Aliyefungua alikuwa binti mmoja, nikajitambulisha kwake, na yeye akasema watu wote wapo hospitalini, baba mwenye nyumba anaumwa sana, ….hata yeye alikuwa akijiandaa kwenda huko huko..

‘Oh, anaumwa nini..ok, basi tutaongozana..’nikasema,

Basi  nikamsubiria, akijiandaa, baadaye tukaondoka naye hadi huko hospitalini, na wa kwanza kukutana naye alikuwa mke wa docta, alikuwa nje akiwa anahangaika na simu yake kama anatafuta namba,…aliponiona kwanza alishutuka, halafu akaniangalia kwa macho yenye mshangao…., tofauti na nilivyotegemea cha kwanza tu akasema;

‘Umefuata nini hapa….?’ Akauliza na kabla sijajibu akauliza swali la pili;

‘Ni nani kakuletea taarifa kuwa unahitajika hapa…?’ akaniuliza akiwa bado ananiangalia moja kwa moja usoni. Mwanamke huyu ana ujasiri fulani , anaweza kukuangalia machoni moja kwa moja bila kupepesa macho!

‘Ninahitajika, na nani…?’ nikamuuliza na yeye akaniangalia na ilionyesha wazi kuna  mshangao fulani usoni mwake, akasema;

‘Sasa umefuata nini hapa……?’ akaniuliza, sasa akimuangalia yule binti niliyekuja naye, halafu akagauka kuniangalia mimi;

‘Nina mazungumzo muhimu sana , mimi na wewe….’nikasema

‘Kuhusu nini….?’ Akasema sasa akionyesha sauti ya kijasiri,nikajua sasa hapo ipo kazi, hekima inahitajika,….

‘Kiukweli, kuja kwangu hapa ni sababu ya mume wako…..’nikasema.

‘Anaumwa….?’ Akaniuliza akiniangalia kwa mashaka

‘Ndio,…anaumwa…. na wewe ndiye dakitari wake…’nikasema, na kumfanya acheke, halafu akasema;

‘Kwanza kabla ya yote, unatakiwa kuonana na baba yangu, hapa tu tulikuwa tunatafauta namna ya kukupata kwa simu….mimi nilishafuta simu yako kwenye simu yangu, …hata baba..sasa ghafla baba anakuhitajia….’akasema

‘Mhh..kwanini, ananihitajia mimi, anataka kunifanya nini….hapana, mimi nimekuja kwako, sio kwa baba yako, ..kwani yupoje, anaumwa sana,..au….?’nikawa nauliza maswali mengi huku nikibabaika.

‘Mimi sijui , twende haraka ukaonane naye, ..umefanya vizuri sana kuja…., sijui..ina maana hakuna mtu aliyekupigia simu kuwa unahitajika..?’ akaniuliza akitangulia kuelekea huko alipolazwa baba yake..nilisita kumfuata lakini baadae taratibu nikaanza kumfuata nyuma, kama mbwa anayemuendea chatu!

‘Hakuna mimi nimekuja na yangu, nimekuja kukufuata wewe….’nikasema na wakati huo tulishafika chumba alichokuwa kalazwa huyo mzee, tukaingia…nikawa nimesimama pale mlangoni, naogopa kuingia.
Mle ndani ….. niliwakuta watoto wa huyo mzee, na mkewe wakiwa wamemzunguka huyu mzee,…aliyekuwa kalala kitandani,…alikuwa kawekewa maji ya dripu, na alikuwa kama yupo usingizini.

‘Oh, umempata wapi huyu mtu…?’ ilikuwa sauti ya mke wa huyo mzee, na kabla hajajibiwa yule mzee akafungua macho, na tukawa tunatizamana, na yule mzee, cha ajbu kabisa akatabasamu halafu kusema;

‘Nilijua utakuja tu…nimekuota kuwa unakuja,..oh, kama ninahitajika kuamini nguvu za mungu, basi mimi sasa natakiwa niwe na imani hiyo…na sijui ..kama nitaendelea kuishi basi mimi nitabadilika kabisa…nataka uniambie jambo moja…je…. wewe umewezaje kufanikiwa kiasi hicho…?’ akaniuliza na kila mtu akawa kanikodolea macho mimi.

‘Kufanikiwa,..sijakuelewa mzee… kwani vipi…..?’nikasema na kuuliza

‘Nimeambiwa ili niweze kufanikiwa, nikuulize wewe…..wewe unajua kila kitu, wewe umeweza, na upo njiani kufanikiwa,..ila..bado ..una mitihani michache tu, sasa sijui ulifanya nini, niambie kabla milango ya koho koho.. ….toba, haijafungwa…’akasema huku akikohoa.

Kwakweli sikumuelewa, nilikaa kimia kwa muda, lakini sijui kilinijia kitu gani, nikaanza kumuelezea mzee yale niliyokuwa nikiyafanya, nilimuelezea kwa kifupi tu…, na yeye alikaa kimia akiniskiliza kwa makini…, hadi nilipomaliza, na nilipomuangalia machoni, nilishangaa kuona michirizi miwili ya machozi, …..

‘Ndio hivyo mzee….’nikasema

‘Basi kwanza naanzia kwako..nisamehe sana..nisamehe sana, ….najua nimekukosea, najua nimewakosea wengi, nami naanzia kwako, uniambie hapa hapa, kuwa je umeshanisamehe…’akasema huku akijaribu kujiinua lakini hakuweza.

‘Mzee mbona mimi ndiye nimekukosea, niliyo-yafanya kwa binti yako, ni makosa makubwa sana, nilikuwa natafuta njia ya kuja kuonana na wewe, lakini nilikuogopa , nilijua kuja kwangu kwako,…..ni kujitakia umauti…’nikasema

‘Ooh…sasa ndio hilo tatizo,na matokea yake ndio haya. ..na najua nipo kwenye mtihani, ila naanza, ..namuomba mungu anisaidie…nitajitahidi kufanya kama ulivyofanya wewe,…binti yangu yupo wapi…?’ akauliza akigeuza uso huku na huku..alikwua akimtafuta binti gani sijui!

‘Nipo huku baba….’ilikuwa sauti ya mke wa docta.

‘Sasa…sasa hivi ondoka na huyu mtu, mguu kwa mguu hadi kwa mume wako, kampigie magoti, mwambie namuhitaji hapa haraka, ili tuyamalize haya mambo, nakuhitaji wewe na huyu mtu muende huko pamoja,..kama kweli unanipenda mimi kama  baba yako…utekeleze haya ninayokuambia….haraka iwezekanavyo…’akasema.

‘Baba…aah, lakini baba siwezi kuondoka, kwa hali kama hiyo uliyo nayo…’akasema huyo binti kwa sauti ya unyonge.

‘Ukiendelea kubakia hapa ndio nitazidi kuwa na hali mbaya, dawa yangu ni hiyo,…ukamuite docta, na ….mke wangu nitakupatia majina ya watu fulani uende ukawaambie waje hapa, haraka…kama kweli mnataka mimi nipone… nimesema haraka….kabla sijaanza kukoroma kukata roho ….’akasema huyo mzee.

Na kweli ikawa ndio nafasi yangu ya kuweza kumpata mke wa docta, ili niongee naye na kumuelezea dhamira yangu ya safari, na niliona hapo mzee karahisisha kila kitu, kwahiyo ikabidi tuondoke hapo hospitalini na njiani sikujua niende huko nyumbani kwa huyu mke wa docta ili apate muda wa kujiandaa, au nitafute hoteli,  maana huyo mdada alikuwa kanuna kweli…, hataki kuongea..

Mara…. mdada akasema;

‘Huyu baba ana nini…eti anataka mimi niende kumpigia magoti huyo mshenzi..mimi niende kwa huyo mtu…hata siku moja..baada ya yote haya yaliyotokea,…kwanini mzee kasahau haraka hivi…mmh…, sio mimi, …siwezi…’akawa anasema tukiwa njiani..

Mimi nilianza kazi ya kum-bembeleza, na kujaribu kumueleze kila kitu…  mpaka nikaona sasa kalainika, ….na baadaye akasema;

‘Mimi nitakwenda huko, kwasababu ya baba tu….. ila siwezi kuongozana na wewe, hapa tu najisikia vibaya sana kuwa na wewe karibu, nasikia kutapika., ..wewe tangulia huko mjini, sitaki uendelee kuwa hapa…, mimi ninaweza kuja huko baadaye, kwani bado ninahitajia muda wa kulitafakari hili…’ akasema.

Na kweli mimi nikatangulia kuondoka kurudi mjini…, na niliporudi huku mjini sikuonana na docta moja kwa moja siku hiyo…, kwani yeye alikuwa kazini…na hata ningeonana naye ningesema nini..nikabakia nyumbani kwangu nikiendelea na toba zangu,…nilishabadilika kabisa, nilishakuwa mtu wa imani…

Siku ya pili yake,….. mara nikapokea simu ya huyo docta, kuwa ananihitajia haraka nyumbani kwake…..

‘Oh docta samahani sana…., unajua jana nilichoka sana na...na, sikuweza kuja kuonana na wewe kukupa taarifa ya mke wako, unajua nilimkuta baba yake anaumwa,na..na…’nikasema nikianza kujitetea na yeye akanikatiza na kusema.


‘Wewe njoo haraka nyumbani kwangu …’akasema na kukata simu. Nilijiuliza kuna nini, na ilionekana wazi docta ana jambo, sauti yake iliashiria hivyo...jirani ni muhimu sana , nikakumbuka maelezo ya mwalimu wangu wa imani.


 Basi sikuwa na namna, japokuwa nilikuwa bado sijajipanga jinsi gani ya kujitetea kuwa ni kwanini nimeshindwa kuja na mkewe.., Kwa haraka nikatoka nyumbani kwangu na kuingie kwenye geti la nyumba ya docta.., nilipofika nikagonga mlango, ….

‘Fungua upo wazi….’sauti ikasema kutoka ndani, nikafungua mlango, ile jicho la kwanza, nilichoona mle ndani,.. nilishikwa na butwa, nikasimama na kuanza kupikicha macho yangu,….sikuamini….


WAZO LA LEO: Ujirani una haki zake, na ukweli ulivyo, ujirani ni muhimu sana, ndio maana watu wa imani wametukokotezea sana KUUTHAMINI UJIRANI..,  kuwatendea majirani zetu ihsani, wema, na kuwa makini na matendo yetu ili yasiwakwaze majirani zetu.

 Wengi wetu hili tunalipuuzia sana, tunatenda mambo mengi ya kuwauzi majirani zetu, tunapiga miziki kwa sauti kubwa bila kujali jirani yako anaathirika vipi na starehe zetu,…tunakesha na ngoma, hatujali kuwa kuna wagonjwa, wasiopenda kelele, wanateseka kwa ajili ya shughuli zetu, basi tuwaambie kabla ili wajiandae..au, tuwaombe radhi, lakini ni nani anafanya hivyo jamani hatuna huruma na wagonjwa,…

Haya kwa ujumla ni madhambi na anayefanya hili, atakuwa na kesi ya kujibu mbele ya mungu. Na tueambiwa `hana imani na hataingia peponi yule anayembughudhi jirani yake...mnalijua hili?


Tumuombe mungu atusamehe kwa makosa haya maana wengi wetu tunafanya haya bila kujua…kuwa ni makosa makubwa, na tunakuomba mwenyezimungu utuongoze tuishi vyema na majirani zetu..ili amani na upendo vidumu maishani mwetu. Aaamin
Ni mimi: emu-three

1 comment :

Anonymous said...

Duuh, huo sasa ni mtihani,...JIRANI, mm wengi wanafanya hivyo!