Nilipofika
nyumbani, sikupoteza muda nikaiendea ile shajara aliyoacha marehemu mke wangu,
nikawa naisoma, hatua kwa hatua….na kila hatua ilikuwa ni kama najizidishia mchungu,…
Ikafikia hatua
siwezi kujizuia tena… machozi yakawa yakinilenga
lenga…nilishindwa hata nifanye nini..kumbe mke wangu aliteseka sana kwa ajili
yangu.., aliyaelezea hayo machungu aliyokuwa akiyapata, .alitoa mfano kwa
kusema,’...ilikuwa kama jipu…na mtu
analigusa gusa kwa kitu chenye ncha kali..na yalikuwa hayaishi….
Alisema alikuwa
hapati usingizi,…maumivu usiku na mchana, akawa anagugumia kwa machungu, na
akawa anajitahidi asinionyeshe kuwa anapata hayo maumivu mbele yangu…, akawa
usiku halali akimuomba mola wake……ni mateso, kwa mateso, lakini ikafikia mahali
akashindwa….
Anasema siku
aliposhindwa, alikuwa amepoteza fahamu mara tatu, na kila akizindukana anajipa
moyo…lakini ikafika mahali akasema hapana…..siwezi tena, na ilitokea siku hiyo
alipohisi kuwa huenda huyo mtoto atakuwa sio sura ya mumewe, ya kuwa huenda
mtoto huyo atafanana na docta, yeye alijua kuwa ..mimba hiyo ni ya docta..
‘Nilipoona sura za
watoto wa wengine zipo sawa na docta, nikajua na mimi itakuwa hivyo-hivyo.., na
mume wangu badala ya furaha atazidi kunichukia zaidi..hapana…siwezi kumuumiza
mume wangu zaidi…, ni bora niitoe tu hii mimba…..’akaandika hivyo.
‘Nimeitoa hii
mimba, maana sina jinsi, nampenda sana mume wangu, nilitaka nimpatie zawadi
japo mtoto wa nje, kama alivyotaka yeye …..lakini nilipenda huyo mtoto aje
kufana na mimi ili asije kujua, …ukweli….lakini nahisi, haitakuwa hivyo, nahisi
kiumbe cha watu kitazaliwa, na kije kupata taabu, nikiwa sipo duniani..hapana,
mungu nisamehe….’akaandika hivyo.
‘Siku hii …sitaweza
kuisahau, maana…natenda madhambi, dhambi juu ya dhambi, lakini ni
kwanini..mungu wangu ni kwanini…naomba baada ya hili ichukue roho yangu haraka…,..ili
nisiendelee kuteseka, ili nisiendelee kumuona mume wangu akipata shida, shida
ya kutafuta mtoto….’aliandika.
‘Ninajua…juhudi
zake zote hizo, ..za toba nk..si kwa jingine, ni ili tu apate mtoto,..je
asipopata huyo mtoto….itakuwaje….itakuwaje..itakuwaje….’aliyarudia hayo maneno
nahisi mpaka peni iligoma, maana hayo maneno mengine yakawa hayaonekani
vyema…..
Niliendelea kuisoma
hiyo shajara, mpaka macho yakaingiza kiza….
Ilifikia muda nikaishiwa nguvu kabisa,
nikajilaza pale sakafuni,…..unajua akili ilikuwa haitaki kukubali, kuwa mke
wangu hayupo tena, kuwa mke wangu alikuwa tayari kufa kwa ajili yangu,…ilikuwa
nasoma shsjara hiyo ni kama yupo mbele yangu ananisimulia hayo yote.
Na kuna sehemu aliyandika,…akimsifia na
kumshukuru docta…hapo alinifanya nihisi kuwa huenda docta ana mambo mengi zaidi
kanificha, na huenda alikuwa ni mpenzi wake wa siri, na kila nikifikia hapo, kumfikiria
docta kuwa ni msaliti wangu, najikuta napandwa na jaziba..lakini nikikumbua
mateso ya mke wangu, jaziba hizo hunywea…
Sikumbuki nilikaa
pale kwa muda gani, ila ninachokumbuka ni kushtuka nikiwa nimeshikwa kwenye
unyayo, nikashtuka na kukaa vyema, huku nikihema sana, na mbele yangu alikuwa
kachuchumaa yule mdada anayenisaidia akiwa kashikilia sinia la vyakula,
‘Una nini tena
shemeji, mbona upo hivi…?’ akaniuliza
‘Wewe weka hilo
sinia hapo chini, na ondoka, sina hamu ya kuongea na mtu…sina hamu ya mtu tena
mbele yangu..ukitaka ondoka kabisa…..’nikasema na yule binti alifanya hivyo na
kuondoka..huyu binti alijaribu sana kuwa karibu name, alijaribu sana
kuniliwaza, lakini alikuwa akijua ni wakati gani nipo tayari kuongea na wakatii
gani sitaki kuongea, ….mungu alimjalia busara na hekima hiyo.
Usiku nikaendelea kumuota mke wangu,…tunaongea
naye…, mara ananielekeza hiki na kile,…na baadaye akawa ananikumbushia jambo
fulani…., lakini nilipozindukana, nakawa nimesahau ni jambo gani alinielekeza
nifanya…,..ilinipa shida kuwaza ni jambo gani alinielekeza mke wangu, na
ilionekana ni muhimu sana kwake…., na sijui kwanini nilisahau.
Basi wakati
nasubiria muda, ili ikibidi niende kwa docta kwa mazungumzo yetu nikapitiwa na
usingizi,…na hapo ndio mke wangu akanitokea tena kwenye njozi, na safari hii
alikuwa hana raha..
‘Kwanini huna
raha…?’ nikamuuliza
‘Kwasababu wewe
hutaki niwe na raha…’akasema
‘Nifanye nini ili
uwe na raha..?’ nikamuliza
‘Hujatekeleza yale yote
uliyoyaahidi,.. wapo jirani zako…umewatendea mabaya, lakini hutaki kuwaomba
msamaha…’akasema
‘Ni nani hao..?’
nikamuuliza
‘Ni wale unaowaona
ni maadui zako, lakini wamekutendea wema ambao huwezi kuulipa…nenda kabla
hujachelewa, timiza dhamira yako ili ufanikiwe unachokitaka, na ili ukipate
hicho pia fuata maagizo yangu…’akasema
‘Maagizo gani hayo
niyafuate..ni hayo ya kuomba msamaha, au kuna mengine zaidi..…?’ nikauliza na
mara nikazindukana kwenye huo usingizi wa mchana-jioni, kumbe ilikuwa simu
inaita. Alikuwa docta akisema tayari kesharudi, kama ninaweza kwenda kuonana
naye . Sikusubiria, haraka nikakimbilia nyumbani kwake.
***********
‘Docta…samahanini
sana..leo nimekuja maalumu,…naomba unisamehe sana…’nikaanza moja kwa moja na
kwa kusema hayo huku nikijishusha kupiga magoti, na docta akabakia kushangaa!
‘Nikusamehe! …kwani
vipi tena….nakumbuka tulishamalizana…au kuna jingine…?’akasema
‘Hapana, ….hatujamalizana…sizani
kama umenisamehe…’nikasema huku nikitembea kwa magoti kuelekea pale alipokuwa…,
nikamuona anatoa macho ya kushangaa,
hakunigusa akaniacha vile vile na kugeuka kuangalia dirishani,halafu
akasema;
‘Unajua
sijakuelewa….’akasema
‘Nisamahe sana kwa
hayo niliyokufanyia…najua hutaelewa,,..lakini mimi nimeshakuwa mtu mwingine,
nisamehe sana, nipo chini ya miguu yako…bila msamaha wako bado nitakuwa
sijatimiza dhamira yangu…’nilisema huku nikitembea kwa magoti,..na docta akageuka
kuniangalia, akanitizama kwa muda, baadaye akanishika begani na kusema;
‘Siamini….unajua
kiukweli moyoni nilikuwa nateseka,… sijui umejuaje, ni kweli nilikuwa najaribu
kukusamehe, lakini nilikuwa najiuliza, je wewe umgundua kosa lako…oh,..utamsameheje
mtu ambaye hajui kama katenda kosa,..oh, kwa hilo nisamehe na mimi..’akasema na
yeye sasa akinipiga magoti.
‘Wewe hujanikosea
kitu docta hustahiki kunipigia magoti mimi,…’nikasema na sote tukashikana na
kusimama, tulikumbatiaa kwa muda,..na yeye akanielekeza kwenye kiti nikaa,
akasema
‘Ni kweli, nilijiuliza
sana, hivi kweli mimi nilichofanya nilikukosea, ni kwanini baada ya yote hayo
bado ulikuwa hujanishukuru ...ninajua ni wajibu wetu sisi madakitari, sisi kama madakitari kazi yetu ni kutimiza
kile mola alichotujalia, na …hatuhitaji shukurani..lakini mimi nilifanya hayo
zaidi ya dakitari kwa mke wako na kwa nia safi kabisa…huwezi kulielewa hilo
mpaka uiweke nfsi yako mahali pangu!
‘Docta nimekuelewa,
nakuomba tena na tena unisamehe, na ninashukuru sana kwa wema wako
huo….’nikasema
‘Anyaway…nashukuruu sana, kwa hio,na mimi
..sasa moyo wangu umetulia…’akasema docta.
‘Nashukuru sana na
nipo tayari kufanya lolote lile docta, niambie ni gharama gani nikulipe,
japokuwa sitaweza kutimiza, fadhila ulizonifanyia, lakini angalau
nitakupunguzia machungu na hasara, na naahidi mola akinijalia, nitakutafutia na
kukulipa, ….ili tu moyo wako uridhike…’nikasema.
‘Mimi sasa sina
kinyongo na wewe, na sina gharama zozote kwako, nilichofanya ni kwa mapenzi ya
ujirani mwema, na mkeo alikuwa rafiki yangu, hilo siwezi kukuficha, lakini sio
urafiki wa kimapenzi, unielewe hapo, urafiki wangu wa kimapenzi uliisha pale
wewe na yeye mlipofunga ndoa…’akasema
‘Nimekuelewa
docta…’nikasema
‘Sasa mhh..pamoja
na hayo, kuna kitu nakuomba,…ni mambo
mawili tu, ninajua wewe ndiye wa kunisaidia, hakuna mwingine anayeweza hilo…’akasema
‘Sawa kabisa docta
mimi, nipo kwa ajili yako, nitafanya chochote, ilimradi,..eeh, yaani wewe
niambie tu, ilimradi unisamehe…’nikasema
‘Sawa kabisa,..…,
la kwanza ukilitimiza hilo…ndio, nitakuja kukuambia la pili..naomba sana
unisaidia kwa moyo wako wote, maana sina namna nyingine,..’akasema docta.
‘Mimi nipo tayari
docta,..nimeshaahidi…, niambie ni mambo gani hayo…?’ nikasema kwa kujiamini.
‘Kwanza ninataka wewe…uende,…ukamshawishi
mke wangu arudi nyumbani,… turudiane mimi na yeye…, unajua baada ya yote haya,
niliachana naye, yeye kwa hasira aliamua kurudi kwao, akasema mimi na yeye basi,
na alipofika huko akaongea na baba yake , baba yake akanipigia simu na
kunihoji, nilijielezea, lakini mzee akaona mimi nina makosa, na alisema
niachane na binti yake kwa amani, na nisije kukanyaga nyumbani kwake tena....’akasema
kwa sauti yenye huzuni.
‘ Docta, unasema
nini,….sikukusikia vyema, ....unajua pamoja na hayo yaliyotokea mimi..mi- mbona
sina mazoea sana na mke wako, … yaani ilitokea tu siku zile, mke wako ni mkali
sana, sijui hata siku ile ilikuwaje, …nilichukulia hasira zake na kumshawishi,
samahani sana….’nikatulia
‘Hayo sawa
nimeyakubali,..yasahafanyika, sasa ombo langu ni hilo….’akasema
‘Docta….mkeo, ooh,
mbona kama sijakusikia vyema , unajua baada ya lile tukio, mkeo …alijisikia
vibaya sana na akawa hataki hata kunitizama usoni,..alilia sana siku ile…na
alisema hataki kuniona tena…., hujui kilichotokea baadaye siku ile, hapana…’nikasema.
‘Ninajua na nina
uhakika, wewe ukikutana naye ukamwambia ukweli atakuamini, akijua kuwa kweli
mimi sina makosa….. , mimi na mke wako ilikuwa ni kazi ya udakitari tu …muhimu
umwambia ukweli, nina imani atakubali kurejea, mimi siwezi kukutana na baba
mkwe, najua alivyo, ila wewe hili ni jukumu lako, ni wewe, ulisababisha haya
yote…’akasema docta
‘Mimiii…., hapana
docta, we-we- we-we…kwanza nitaanzaje, hapana docta..hilo siliwezi, ..kabisa
kabisa, siku ile angeliniua,..unajua baada ya ….ilibidi nikimbie, wewe hujui
tu,…oh, hapana docta, mengine sawa lakini sio kwenda kuonana na hiyo familia,
halafu baba yake wewe si unamfahamu vyema,…, alivyo mkali, anaweza kuniua,….nimekuahidi
kuwa nitafanya lolote lile ilimradi unisamehe, lakini kwa hili hapana…’nikasema
nikitikisa kichwa kukataa..
‘Ahadi ni deni, na
ukumbuke dhamira yako….huna budi kufanya hilo, vinginevyo nami, …sijui kama
nitaweza kukusamehe, sijui kama nitaweza kuku…ambia hilo jambo la pili,…ukifanikiwa
hilo ombi langu,ukafanikiwa mke wangu akarudi hapa,… basi na mimi nitakuja
kukuambia hilo la kwako, na utakuwa umetimiza dhamira yako, nina uhaika huo..,
kama uliweza kumuhadaa mke wangu,…mkafanya mlichofanya, kwanini sasa uogope
hili, eeh, wewe si kidume…’akasema docta.
‘Kwahiyo docta
unataka kusema nini, unataka mimi…nifanyeje…siwezi docta,…nitamuanzaje kwanza,…kwanza
nitafikaje kwenye hiyo familia….unanitakia mema kweli wewe….mmh, wewe mwenyewe
unaogopa, ndio unanisakizia mimi….hapana, tutafute mtu mwingine, sio mimi,
kwanini mimi…ili nikauliwe au?’ ..nikasema na mara simu yake ikaita, akaipokea …
, alipomaliza kuongea na hiyo simu akasema;
‘Siwezi kuongea na
wewe jambo jingine kwasasa, hapa kichwa kimechoka, unasikia wananiita huko
kazini, kuna dharura tena, kuna mgonjwa mahututi kaletwa, hapa nyumbani kuna
mambo kibao ya kufanya, hapa sasa ndio naona umuhimu wa mke angelikuwa hapa
nyumbani, ..ooh, yaani sasa hivi naiona nyumba kama hema tu, haina raha, kisa
ni nini…’akasema akiniangalia machoni
‘Nisamehe sana
docta hilo mimi sitaliweza kulifanya…. , kabisa kabisa, hapana, unataka
nikauwawe…wewe mwenyewe unawafahamu hao watu, mmh hapana….’nikasema nikitikisa
kichwa na kutoa ishara kwa mikono.
‘Mimi ninachokuaomba,
wewe, eeh,… katimize hilo, maana ni muhimu sana kwangu, na kwako…hapa kichwa
kinaniuma, ninawaza sana, nifanyeje mke wangu arudi, hakujua hili, na
alishahadaika na- na, na… wewe, mmh, kichwa kinauma kweli, ‘akasema akishika
kichwa
‘Pole sana docta
lakini….’nikataka kusema lakini akaniwahi kwa kusema;
‘Ha…hahaha, docta
hajigangi au sio…, najua unataka kusema nini, ..lakini najua dawa yangu,.. dawa
yangu ni mke wangu….ukinisaidia hilo, mengine yatafuata, namuomba mungu tu, anipe
uzima, ili niweze kukuambia hilo la pili na hilo kwako ni muhimu sana kama
ilivyo kwangu kumrejesha mke wangu hapa nyumbani….nisaidie , name nikusaidie…’akasema.
‘Mhh….lakini haiwezekani
docta, nitawezaje kukutana na mkeo..nimeshakuambia
mimi siwezi, siwezi siwezi…. alisema hataki kuniona kabisa kwenye macho yake,
hataki hataki…sasa wataka mimi nikafanyeje…’nikasema nikiwa sijui nifanyeje…
‘Fanya ufanyalo…..mimi
sijui…’docta akasema na sasa akawa anajiandaa kuondoka, na mimi ikabidi
niondoke.
Nilifika nyumbani kwangu,
nikiliwazia hilo,…kwakweli, kwa hilo nilishindwa kabisa, najua kwenda huko ni
sawa na kujipeleka kwenye mdomo wa mamba, nakumbuka siku ile…alisema nisije
kukanyaga kwake, na akasema atamwambia baba yake kuwa mimi ndiye nilijenga
fitina,..baba yake alikuja kuambiwa, na mzee huyo akasema wazi wazi, kuwa, siku
nikukutana naye atajua ni nini cha kunifanya.
‘Mzee, ni, ni shetani tu alinihadaa, alitufanya tuamini hivyo..lakini hata binti yako, anajua kuwa mume wake ana mahusiano na mke wangu,
na ilikuwa….’nikasema na mzee huyo akanikatiza kwenye simu na kusema;
‘Nasikia wewe
unajifanya una hasira sana,….sasa mimi zangu hazina kikomo na nikiahidi kitu ni
lazima nikitimize, nataa tukutane mimi na wewe, tuone ni nani zaidi, wewe si
kidume sio, basi mimi ni zaidi yako,….unasikia, umemuharibia mke wangu ndoa yake,
..wewe na huyo mshenzi wako anayejiita docta, mtanitamabua,..’akakata simu.
‘Hivyo ndivyo
ilivyokuwa rafiki yangu, sio kwamba nilikataa kwenda kwasababu ya aibu, hapana,
nilijua kabisa huko, kuna hatari ,
wanaomfahamu huyo mzee wanaweza kukusimulia visa vyake, yaani siku ile
niliishiwa nguvu kabisa, nikajua sasa nimeshindwa
‘Sasa nifanyeje,…’nikawa
najiuliza, na mara mlango wangu ukagongwa….
NB: Nikuache hapa
kwanza nisimalizie yote…kwa leo ili utafakari kidogo, hebu jiulize haya maswali
kwanza, je ilikuwaje, na je docta anataka kumwambia nini huyu jamaa kama jambo
la pili, na je huyu jamaa ataweza kwenda
huko anapotaka kwenda, na hata akienda labda…. kweli atafanikiwa, na je kama
hatafanikiwa itakuwaje…?
WAZO LA LEO: Kukoseana kupo, kama binadamu hatuwezi kuwa sawa, kuna
kusigishana kwa hapa na pale. Maudhi...kutofautiana, , na hata kufikia
kuwekeana visasi kwa sababu mbali mbali..lakini tujiulize, kwa kufanya hivyo
tunapata faida gani….kama unaona kuna faida…sijui…., sawa, lakini jiulize tena
je mungu analirizia hilo, au ni mambo ya kidunia tu…hii ni dunia tu dugu yangu…,
wapo walifanya hivyo, wababe , wana pesa, watawala nk…lakini sasa wapo wapi..na
huenda wanapambana na adhabu kubwa na wanajuta, wanatamani warudi duniani ,
lakini haiwezekani tena…tukumbuke jambo
moja muhimu:
Kusameheana kuna thamani kubwa sana kuliko
kinyume chake!
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment