Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeSaturday, October 15, 2016

TOBA YA KWELI-11

  


Sehemu iliyopita mnakumbuka nilianza kuisoma ile shajara ya mke wangu, na humo niligundua mambo mengi, mojawapo nililogundua ni kuhusu mahusiano yake na docta,…japokuwa nilishaanza kubadilika, hasira zile mbaya mbaya zilishapungua, lakini kwa jinsi shajara ile ilivyokuwa ikimtaka docta,..nikashindwa kuvumilia, na hapo nikaamua kwenda kukabiliana na huyo docta, je kulitokea nini…
Tuendelee na kisa chetu, nikiwa naongea na docta

                        **************
‘Docta kwanini mlinifanyia hivyo..?’ nikamuuliza nikiwa nimesimama nikimuangalia kwa hasira…

‘Kwani kuna nini tena, si tullishamalizana mimi na wewe…tumeshasameheana au sio….’akasema

‘Mke wangu alikuwa na tatizo kubwa, mkawa mumeligundua wewe na yeye kwanini hukuniambia..?’ nikamuuliza

‘Oh,..oh, ni nani kakuambia..najua umegundua shajara yake nini…..mmh, najua sana….lakini ni vyema kuwa umeligundua hilo mwenyewe, kiukweli ni kuwa ni yeye mwenyewe alitaka iwe hivyo,….mimi ningefanya nini..nilimshauri sana akuhusishe na wewe, lakini alikataa kata kata…’akasema

‘Kwa vile wewe ulikuwa ni hawara wake au sio….’nikasema

‘Sikiliza nikuambie ukweli…..’akasema akiniashiria nikae kwenye sofa, sikupinga nikasogea kwenye sofa na kumsubiria aniambie ukweli.

Na ndipo akanihadithia jinsi waivyohangaika yeye na mke wangu kutafuta tiba, na hatimaye ndio mke wangu akaja na wazo la kubeba mimba ili azae tu, huku akijua kwa kufanya hivyo kungeliweza kumuharakishia maisha yake….

‘Ni hatari, kwani mimba ingelimu-maliza mapema,..lakini hakukubali ushauri wangu, …’akasema

‘Kinachoniuma ni kwanini ….hukuniambia huo ukweli..hayo hayo yamepita,…sasa ili tuelewane,…niambie ukweli,…ulifanyaje kwasababu ulisema kizazi chake kilikuwa kimeharibika…?’ nikamuuliza

‘Mke wako ni rafiki yangu mkubwa toka hata kabla hujamuoa wewe, ilitakiwa mimi ndiye nimuoe, lakini ndio ukashinda wewe, …yote  hayo ni mapenzi ya mungu,...na nimekuwa msiri wake mkubwa…na alipolipanga hilo mimi sikuwa na kipingamizi, lakini tatizo lilikuwa ni jinsi gani ya kuibeba hiyo mimba , bila ya kukutenda, na bila ya kuisaliti ndoa yake.’akasema

‘Ndio mkapanga kuzini wewe na mke wangu au sio…sema ukweli tu?’ nikamuuliza nikikunja uso kwa hasira

‘Mke wako alikuwa muadilifu sana, pamoja na yote hayo uliyomtendea wewe,…wewe hujui tu, yeye hakutaka kabisa kukusaliti…lakini alihitajia mtoto kama ulivyomtaka wewe…, alitaka kabla hajafa akupatie wewe mtoto…hilo lilimtesa sana, na ndio siku moja akaja na hilo wazo…’akatulia

‘La wewe nay eye mzini au sio, wewe si kidume mbegu….’nikasema

‘Subiri nikuambie ukweli… hata yeye hakulipenda hilo…lakini alifanya hivyo kwa vile anakupenda wewe..alikuwa tayari…, afe kwa ajili yako….’akasema

‘Basi, …mimi nikamshauri sana,..akasema nifanye lile nitakalo liweza ili tu yeye apate mtoto, na kwa vile alishaona ..nimewafanyia wengine, akaona kwanini nisimfanyie na yeye…mimi ni dakitari wa mambo hayo, nikaanza harakati za kukiweka sawa hicho kizazi chake, upasuaji …nk…,..ni hatari, lakini…kwa uwezo wamungu, kizazi chake kilikuja kukaa sawa….achilia mbali huo ugonjwa wake!..’akatulia kidogo.

‘Kwahiyo ndio ilikuwa kazi yako..ujanja ujanja tu..mbona hakupona sasa, mbona hakumpata huyo mtoto…?’ nikamuuliza nikiwa bado nimekunja uso kwa hasira

‘Wewe hujui mitihani ninayokumbana nayo kwenye hii fani yangu,..wewe hujui watu wanavyohangaika pale wanapokosa mtoto, hasa mwanamke…sipendi,lakini wakati mwingine huruma hunijia, na ….ndio..mengine ni siri yangu…., hayo ninakutana nayo ni siri yangu,…lakini kwa mke wako yeye ilikuwa tofauti…’akasema

‘Kuzini ni kuzini tu, hakuna utofauti…’nikasema huku nikitikisa kichwa kuonyesha hisia zangu.

‘Mimi nimekuwa nikifanya uchunguzi, ..kuona jinsi gani ninaweza kumwekea mwanamke mbegu kwenye kizazi kilichoharibika….kwa njia ya kupandikiza mbegu…ili aweze kuzaa..unakumbuka kuna kipindi nilikuambia unipatie mbegu zako za uzazi ili tukazifanyie uchunguzi,ili tuone kama kuna tatizo…?’ akaniuliza

‘Lakini ile …..’nikatulia nikikumbuka, ni kweli nilifanya hivyo, kipindi hicho tunahangaika angalau nipate mtoto, lakini nilijua ni kazi bure. Na nilikuja kukata tama nikijua huyu docta hawezi kitu.

‘Ndio…ilikuwa ni namna niliyoitaka nione kama ninaweza kufanikisha uchunguzi wangu, sikukuambia nilichokuwa nataka kukifanya…niliziweka hizo mbegu kwenye kizazi cha mkeo…na hata siku ile anakuja kwangu kutaka tutende tendo ili apate uzazi, kwa vile kwako imeshidikana..nilikuwa nimeshazipandikiza hizo mbegu kwenye uzazi wake..nilikuwa nasubiria matokeo sikutaka kumwambia…

‘Kwahiyo kumbe ni kweli,..mlizini..’nikasema nikimkazia macho.

‘Nisikilize kwanza…..’akasema
‘Docta, docta, docta…ni nini ulifanya…., kama sio kuzini na mke wangu….’nikasema na hutaamini…siku hiyo ilikuwa tofauti, pamoja na hasira …lakini haikuwa kama ile hasira yangu ya awali..nilishabadilika, lakini docta alikuwa akiniangalia kwa mashaka akijua nimekuja kwa shari.

‘Kiukweli siwezi kukuambia undani wake nilivyofanya….ila siku ile alikuja kwa vile nilishamwambia kizazi chake kipo sawa kinaweza kubeba mimba, ila mume wake, yaani wewe…inaweza mimba isishike, kwahiyo ndio akaja kwangu, … hakulipenda hilo….’akatulia

‘Mke wako alikuonea sana wewe huruma…na, angelifanya nini na wewe ulikuwa unataka mtoto…,siku ile mimi  nikamuhadaa tu ili ahisi nimefanya hivyo,na sikutaka kumwambia kuwa tayari nimeshapandikiza mbegi kwenye kizazi chake.. ,nika….na akajua labda..na hilo nililifanya ..huwezi amini…lakini sikufanya na yeye tenddo…’akawa hamalizii maneno yake.

‘Niambie ukweli docta, wewe ulizini na mke wangu, huo ndio ukweli, tunalijua hilo, yeye  alikuwa mpenzi wako wa siri, kwanini hukubali ukweli ukatubu kama …yaishe tu, …?’ nikamuuliza na kusema

‘Sikuzini na mke wako, niamini hilo….’akasema

‘Kama hukuzini na yeye, kwanini aliamua kuitoa hiyo mimba…?’ nikamuuliza

‘Mimi nilikuwa kwenye  uchunguzi wangu…bado naendelea hatua kwa hatua…, na sikutaka hata yeye alifahamu hilo kwanza,…na kwa vile alishafikia hatua hiyo, nikamvunga kinamna,....sikufanya naye tendo hilo abadani,…’akasema

‘Mimi sikuelewi, kwa vipi, hahaha, nyie watu …’nikasema nikitikisa kichwa nikawa kama nacheka kwa dharau.

‘Niamini,…… mke wako nilikuwa namuheshimu sana, baada ya wewe kuoana na yeye, tuliapa kuwa urafiki wetu uwe kama wa kaka na dada....ila kwa siku ile hata yeye alijua nimefanya hivyo, lakini kiukweli sikufanya tendo hilo,..najua ni kitu gani nilifanya, hiyo ni siri yangu…., ila ninaomba uniamini hivyo…,ukweli ndio huo sikuwahi kuzini na mkeo….’akasema

‘Hivi unafahamu ni nini maana ya kuzini…..?’ nikamuuliza

‘Naelewa sana…’akasema

‘Sasa ilikuwaje hahaha…utafikiri nacheka,…. najua unaniogopa tu…, kiukweli siwezi kukufanya lolote kwa hivi sasa, sina nguvu hiyo tena…, ila mimi ninachotaka ni ukweli tu, je ulizini naye sema ukweli, moyo wangu utulie..basi ukiniambia ukweli ….basi nitafanya nini tena,…je ulizini na mke wangu..?’ nikauliza nikitaka kuujua ukweli.

‘Mkeo alikupenda sana..na yote yaliyotokea ni kwa ajili yako…alikuwa akikuhurumia sana, ..ndio maana , japokuwa alijua kuwa unatembea na wanawake wengine nje…, lakini hakutaka kukuambia,..alijua yote hayo….kiubinadamu aliumia tu ndani kwa ndani…aliniambia yote hayo, kuhusu wanawake zako, ukafiki hata kutembea na ndugu zake,..na kila mara alikuwa akikuombea upate mtoto hata wa nje,..lakini haikutokea…kwasababu una madhaifu kwenye …..’ hapo hakumalizia akatulia .

‘Unataka kusema nini, kuwa mimi siwezi kuzaa,…. ndivyo ulimdanganya mke wangu hivyo….docta usiniharibie sifa yangu, mimi ni mwanaume,…sitaki kulisikia hilo, nimeambiwa na-na yule …..ok, ok, …oh, nimejisahau, nisamehe…..haya sema ukweli sasa ikawaje..?’ nikamuuliza docta

‘Kwa vile saratani hiyo ilishakwenda mbali..haikuweza kusaidia kitu, japokuwa mbegu zile ziliweza kukaa vyema kwenye sehemu ya uzazi, lakini, nilijua ni hatari, ila nilimuomba mungu sana, oh..ilikuwa na mateso sana kwa mkeo…alipata shida sana, maumivu makali..

‘Oh…inanipa shida sana kuliongelea hili….ilifikia hatua mimi nikamshauri mkeo ni bora tu aitoe hiyo mimba..lakini yeye hakusikia, …akazidi kuvumilia..mkeo aliteseka sana, fikiria  miezi mingapi ya mateso,..na hata siku alipoamua kuitoa hiyo mimba, mimi sikuwepo,….’akasema.

‘Ungeniambia mapema, ningeliweza kulizuia hilo…..’nikasema nikitikisa kichwa.

‘Sizani…nakuja, kama anavyokujua mke wako….ngoja niendelee….mke alikuja kuniambia tu kuwa kashindwa, aliniambia akilia kwa uchungu kuwa hatimaye kashindwa kukupatia kile ulichokitaka na sasa atakufa ukiwa huna amani, alilia sana, basi mimi moyoni nikashukuru sana…na niliipomchunguza, nikajua sasa basi,  …sizani kama ataweza kuendelea kuishi zaidi ya miezi kadhaa.., maana hali ya kizazi likuwa mbaya sana..nikajitahidi kadri ya uwezo wangu, …na kuna dawa hizo ambazo nilitakiwa kila mara niwe ninampatia, kwa muda  maalumu,…’akatulia akiangalia saa yake…na simu yake ikawa inaita, akaangalia, akaikata,…

‘Hizo dawa ni aghali sana..unakumbuka siku ile nilipofika kwako..nikakuambia nataka kumpa mkeo dawa…ukanipiga na kuniumiza…, ilikuwa namletea mkeo  hizo dawa…sawa nashukuru maana nilishaahidi kuubeba huo mzigo..’akasema

‘Mhh…lakini mimi sikujua hayo…’nikajitetea

‘Kwa ufupi ndio hivyo, jirani yangu…kinachokuponza wewe ni hasira,na tamaa.. kama wote tungeichukulia hivyo, nahisi dunia isingelikalika …sijui kama leo hii..hata kwa hayo uliyonitendea..mmh, nahisi  leo tusingeliweza kuongea hivi, ingelikuwa ni uhasama, ndio maana nilikuambia tatizo letu wanadamu ni `uoni’..jinsi gani ukomo wa uoni wetu ulipofikia, sikuwa na maana ya kukudharau…kwa neno hilo uoni, wengi hatuwezi kujijua..’akatulia

‘Sawa…..’nikasema

‘Kwani kuna watu wanaamini vitu vya ajabu, kuwa ni miungu nk…na huwezi kuwaambia kitu, ..uoni wao umefikia hapo..tukubali hilo kuwa uwezo wa kufikiria una ukomo kwa kila mtu hasa inapofikia kwenye imani….umenielewa hapo….?’ Akasema

‘Mhhh….’nikaguna tu.

‘Na kwa ujumla… , hatupo sawa , hata ukiona maumbile yetu…,na hivyo hivyo,  hata kwenye kuwaza… hatupo sawa kabisa….kila mtu awaza lake, kwa jinsi aonavyo yeye na nafsi yake…, muhimu kwa sasa ni kuvumiliana…na tuzidi kuwaombea wenzetu waliotangulia mbele za haki, hasa mke wako…huwezi kujua jinsi gani alivyoteseka kwa ajili yako,inaniumiza sana, sana,…mimi kama docta nilijua ni nini hatima yeke, lakini ilibid inifanye yale…niliyoona huenda yatakusaidia….ili mkeo awe na amani….na bado nilikuwa namuomba mungu alete heri zake,…kuna muda nikiliwazia hilo ninalia sana…’akatulia

‘Oh..lakini mimi sikujua hilo….’nikasema

‘Najua,…. ndio maana nikakuambia `uoni’…haupo sawa, wewe uoni wako uliishia hapo, …’akasema akiangalia simu yake, kuliingia ujumbe wa maneno.

‘Sasa ni hivi, cha muhimu timiza yale yote aliyokuwa akiyataka marehemu mke wako..,na yale yote aliyokuagizia wewe uyafanye naomba uyatekeleze kwa kadri uwezavyo…, maana hayo ndiyo yatamfanya mkeo huko alipo astarehe,….’akasema

‘Sawa, lakini yapi hayo mbona sikumbuki,..si-si kumbuki mke wangu  kuniagiza kitu, au una maana gani kusema hivyo.….’nikasema.
‘Kwa leo..sina muda… nawahi hospitalini.., kuna ujumbe umeingia kwenye simu yangu kuna mgonjwa mahututi..nikirudi uje tuongee zaidi,..kuna mengi ambayo nahisi unataka kuyafahamu na  kuna maagizo yako nitakuambia nikirudi….’akasema na kuanza kujiandaa kuondoka, na mimi ikabidi niage niondoke..hata hivyo pale nilikuwa navumilia tu, moyo ulikuwa unaniuma sana nikajikuta ninalia…

‘Hata nikilia itasaidia nini..keshaondoka, oh…inaniuma sana….’

Nikarejea nyumbani kwangu nikiwaza ni kitu gani hicho ambacho mke wangu alimuagiza docta, na mimi hakuwahi kuniambia, maswali yakazidi kunijaa kichwani na kichwa kikawa kinauma sana…, nilipofika nyumbani nikaichukua ile shajara na kuendelea kuisoma, kuanzia pale nilipoachia ….

NB: Tuishie hapa kwa leo, sehemu ijayo ndiyo itafichua ukweli wote na siri kubwa ya toba…toba ya ukweli ilivyokuja kufanya kazi….na mengi ambayo yatakuwa ni heri kwetu kutokana na hiki kisa….na huenda ikawa ndio mwisho wa kisa hiki.

WAZO LA LEO: Kuna mengi tunayapanga hapa duniani, na mambo mengi ya heri yanakuwa na lugha `nikijaliwa..’ yanakuwa hayamaliziki kama mambo ya kidunia tu ambayo hayana heri kwetu….


 Basi tukiwa na marafiki, tukiwa ni wanandoa, tunafahamiana sana, na bahati mwenzako akikutangulia mbele ya haki, jaribu kukumbuka mema yake, jaribu kuyatekeleza yale ambayo alijitahidi kuyafanya na bahati mbaya hakuweza kuyamaliza, ili kuendeleza hayo mema, na  huku ukimuomba mola kuwa haya nayafanya kwa ajili ya…rafiki yangu huyo, mwenza wangu huyo nk, mzazi wangu huyu nk,..na mola ni mwingi wa rehema, anaweza kuyapokea kama malipo yake kwani yeye ndiye anayetufahamu zaidi.

Ni mimi: emu-three

No comments :