Niliachana na
dakitari yule hasimu wangu, nikatoka ofisini kwake na kuelekea chumba
alicholazwa mke wangu, moyoni nikiwa tayari nimeshajaa mawimbi ya hasira, na
mimi nikishaingiwa na hasira nakuwa kama mtu aliyechanganyikiwa..yale maneno ya
dakitari yaliniumiza sana moyo wangu..
‘Ni kosa la nani….?’
‘Ufahamu!…ufahamu
wako ni mdogo sana….
Huyu mtu
ananidharau mimi..kwa vile yeye ni dakitari ananiona mimi sina ….haiwezekani
…ni lazima nitamuonyesha kuwa mimi nina akili zaidi yake..ngoja nimalizane na
mke wangu, nikitoka huko nitamrudia, ..yaani haiwezekani..’akilini mwangu
nilikuwa nachemka,..hadi nikafika mlango wa kuingilia, bila hata
kujijua…nikajikuta nimeshaingia kwenye hicho chumba alicholazwa mke wangu.
‘Paaah….’moyo
ulishtuka!
Na pale nilipoingia
chumba alicholazwa mke wangu, nilipatwa na mshituko, …wasiwasi na mashaka
vikaugubika ubongo wangu, na kwa ile hali ya hospitalini, na kile chumba
kilivyo, ghafla hata lile wimbi la hasira likaondoka, na huruma ya kibinadamu
ikaanza kuniingia!.
Nilitupa jicho
mbele yangu pale kilipotakiwa kuwepo kitanda,…..nikabakia nimeduwaa,…mmh,
..haiwezekani…macho yaliona lakini ubongo haukutaka kukubali nafsi ilisema
vingine..haiwezekani...
Pale kwenye kitanda
kumezungushiwa uzio, mapazia, na ile ilikuwa na ishara nyingine, ..
‘Haiwezekani..’nikasema
huku mwili ukianza kuishiwa nguvu.
Sikuweza kusogea,…wasiwasi
ukanisonga….woga, mashaka….na hata majuto…
Tuendelee na kisa chetu
*******
Kwanza nilisimama
nikawa nimeduwaa tu..na mara nikaona mtikisiko fulani kwenye lile pazia,..nikakodoa
macho kuhakikisha…na mara nikaona mtikisiko ule ukizidi,..na mara, akatokea
nesi akiwa kashika beseni likiwa na vifaa …mara akatokea dakitari.
Nikapumua kwa
nguvu, lakini bado …maana lile pazia lilikuwa halijaondolewa, yawezekana,
walikuwa wakimuweka sawa…mmh, niliogopa hata kulitamka hilo neno..
‘Hapana
haiwezekani..’nikajikuta nimesema kwa sauti.
Mara Yule dakitari akaniona,…na haikupita muda
wote wawili wakaanza kulisogeza lile pazia lilokuwa limezunguka kitanda, ..na
kitanda sasa kikawa kinaonekana na mtu kalala pale kitandani,akili ikawa
inajiuliza je huyo mtu ni mzima au….
‘Oh…nani kakuambia
uingie..’Ilikuwa sauti ya dakitari iliyonishtua, toka kwenye dimbwi la mawazo
na mashaka.
‘Ni- ni..dakitari
mkuu…kaniambia naweza kuja kuonana na mke wangu, …’nikasema
‘Haiwezekani….lakini
sawa hata hivyo nimemalizana naye, anasubiria …upasuaji tu…’akasema
‘Upasuaji! Upasuaji
wanini,..? Kwani mke wangu anaumwa nini…?’ nikauliza na Yule dakitari hakusema
kitu,…akanipita na kuanza kuondoka bila kunijibu kitu, kitu ambacho kinifanya
nizidi kuwa na mashaka, na nesi akatabasamu naye akiwa anataka kunipita ,
akasema;
‘Usiwe na wasiwasi
utaambiwa baada ya vipimo…’akasema na wote wakaondoka na nikabakia mimi na mke
wangu, na wakati huo mke wangu alikuwa kama vile kalala hatikisiki ndivyo
nilivyomuona nilipogeuka kumuangalia.
Nilianza kutembea
hadi pale kitandani, kiukweli mke wangu kwa siku hizo mbili alikuwa kabadilika
kabisa, alikuwa kama sio yeye, mwili umemuisha, usoni kakunjamana kama mzee wa
siku nyingi.
‘Unajisikiaje…?’
nikaanza kusema na ni kama vile mke wangu hakujua kuwa nimefika, maana
nilipotoa sauti yangu ndio akageuza kichwa kuniangalia, kwani muda wote ule
alikuwa kalala kafumba macho huku akiangalia juu.
‘Aheri umekuja,
maana nilijua safari yangu itafika, na tusiweze kuonana tena…nilikuwa namuomba
mungu sana, ili utokee, ili uje tuyamalize….na kama usingelitokea, sijui
ningekuja kusema nini mbele muumba wangu…’akasema.
‘Safari ya wapi,
utapona tu mke wangu..’nikasema.
‘Ningelifurahi kama
ingelikuwa hivyo,..lakini mungu mwenyewe kapanga iwe hivyo, ishara zote
zinajionyesha, na nimeomba iwe hivyo, kuliko kuendelea kuteseka, kifupi… sina
budi kuitikia…’akasema.
‘Kwani mke wangu
tatizo ni nini..maana nashangaa mimi mumeo sijui ni nini kinachoendelea, naona
hata aibu kuwauliza madakitari,..kwanini umenificha kiasi hicho,kwani unaumwa mke
wangu…?’ nikamuuliza.
‘Najua…, unisamehe
kwa hilo, na nimefanya hivyo kwa vile nakupenda, sikutaka kukutwika mzigo
mwingine kichwani mwako …’akasema.
‘Lakini ugonjwa
haufichwi..ikizingatiwa mimi ni mume wako, ni nani wa karibu kama mume au mke
wako….’nikasema
‘Ninajua..na ..sasa
kila kitu kitakuwa wazi, utajua kila kitu pindi…’akasema akijaribu kuinua mkono
kuniashiria nisogee nikae karibu naye. Kiukweli mkono ulionekana mdogo, na
hauna nguvu, nilianza kujilaumu, maana kumbe nilikuwa naishi na mtu anateseka,
anaumwa lakini mimi sijui, mimi na maisha ya kutafuta pesa tu.
‘Nisamehe sana mke
wangu,….’nikajiukuta nimesema
‘Nashakuru sana
kama hayo maneo yanatoka moyoni, na sijui huo msamaha unaoutaka wewe ni kuhusu kitu
gani hasa…’akasema.
‘Kwa vile unaumwa
na mimi hata sijui…ni ajabu kabisa…inaonekana kama vile tulikuwa hatuishi
pamoja,…, nimekua sikujali, sikuulizi, ..mimi nilijua ndivyo ulivyo, kuna siku
niliwahi kukuta …unalia, nikakuuliza ukasema ni maombi yako kwa mungu….nikajua
ni kweli ni hizo ibada zako za kila siku…’nikasema.
‘Hayo sasa yamepita
mume wangu na nina imani toba yangu, maombi yangu yamekubaliwa, ila imebakia
kitu kimoja, ...’akasema.
‘Na hicho ndicho
nilichokuwa nikikiombea, …sasa mume wangu nilichokuitia hapa ni yale mazungumzo
yetu,…nakumbuka nia yetu ilikuwa kutubia madhambi yetu,..ulianza wewe, na
ikafikia hatua yangu, na mimi kwasasa ninataka kusikia kauli yako, je umefikia
wapi, upo tayari kunisemehe…?’ akauliza.
‘Mke wangu muhimu
ni wewe upone hayo mengine hayana maana kwangu, na mengine yote tuyaache
tushughulikie afya yako…’nikasema.
‘Yana maana sana
kwangu…nataka kusikia kauli yako kutoka moyoni,kabla hatujachelewa …’akasema
‘Mke wangu, hayo ya nini..na kwanza hebu
niambie kwanza unaumwa nini maana hata madakitari nawauliza wanasema wewe
utaniambia, au …sasa wamesema wanasubiria vipimo…kuna tatiz o gani, ni nini
kinachoendelea…?’ nikauliza
‘Nataka kwanza
kusikia kauli yako kuwa je umenisamehe, na ninataka itoke moyoni, isiwe kwa
ajili ya shinikizo la kwa vile ninaumwa…’akasema.
‘Kwa hali kama hii
uliyo nayo, nina haja gani ya kutokukusamehe..mimi ninachotaka ni wewe upone,..utibiwe
upone ili tuweze kurejea maisha yetu, na najua hili litapita afya yako
itaimarika, na kwa vile…sijajua kuwa wanakusafisha tumbo au vipi, sizani kama
itazuia wewe kupata mtoto, kwani si lile tatizo la kizazi au sio…?’nikasema kwa
kuuliza.
‘Kwahiyo wewe
mawazo yako yote ni huko, mtoto, au sio, ninajua, lakini kwanza fuata masharti
ya toba yako, ili uje kufanikiwa, je umeshajifunza, au bado una hasira na mimi…?’
akaniuliza.
‘Mke wangu kwanza
upone, ndilo muhimu, na haya matibabu yasaidie ili kila kitu, kiende sawa….na
wewe mwenyewe unaelewa kuwa hata wewe linakugusa sana, au sio…’nikasema
‘Kwahiyo kama
sitakuzalia mtoto wewe itakuuma sana…, kwako muhimu ni mtoto au sio…?’
akaniuliza.
‘Sijasema hivyo,unielewe
mke wangu, ..lakini hata wewe hilo la mtoto si muhimu kwako pia…, eti mke
wangu?… najua hata wewe kuumwa hivi inatokana na mawazo ya kukaa muda mrefu bila
ya kupata mtoto, hali hiyo imekuwa ikikutesa sana, ndio maana hata mimi
nimekuwa nikihangaika sana kwa ajili yako..’nikasema
‘Muda unakwenda
mume wangu niambie hicho nilichokuulizia, .. je umenisamehe…?’ akauliza.
Nilihema kwa nguvu, na sio tu kwa vile
namuonea huruma, sio kwa vile tu ..lakini moyoni nilianza kuingiwa na upendo wa
ajabu, nikakumbuka maisha yetu ya nyuma ..nikakumbuka jinsi nilivyompata
…kiushandani kweli kweli na hatimaye tukajikuta tumekubaliana..kumbe hata yeye
alikuwa akinipenda….
Kumbu kumbu hizi
zilikuja kwa haraka kichwani, na sijui kwanini..
‘Rafiki yangu nikuambie
ukweli, mimi ni jasiri sana, na huwezi kuliona chozi langu kirahisi ..lakini
kwa hali niliyomuona mke wangu, na kumbukumbu hizo za nyuma ziliponijia akilini
machozi yalinilenga lenga, sijui kwanini!
‘Nimekusamehe mke
wangu, sina kinyongo na wewe, iliyobakia ni wewe upone tu..ninajua kosa ni
langu..mimi nimekuwa mkosaji sana, …lakini ndio hivyo nilishaanza safari ya
kubadilika,…kutubu,….’nikasema
‘Mungu akusaidie
mume wngu utimize lengo lako…’akasema
‘Ni kweli mke
wngu..mimi nina imani nikiweza kutimiza yote hayo…mungu akanisamehe madhambi
yangu,na watu niliowakosea,…. wakanisamehe, basi shida zote tulizo nazo…zitaondoka
na wewe utaweza kupona kabisa…na nina imani…uta…’nikasema nakukatisha kauli.
‘Nitakupatia mtoto…natamani
ingelikuwa hivyo…’akamalizia yeye.
‘Itakuwa hivyo mke
wangu..unafikiri…wewe utaona tu..’nikasema
‘Mume wangu , …mimi
nina tatizo kubwa sana…najua kilicho kipaumbele kwako ni nini, lakini mungu
anajua zaidi….’akaanza kusema
‘Tatizo litaisha
mke wangu…., mimi naamini sana alichoniambia Yule mtu wa mungu, na Yule mcha
mungu akisema neno lake kawaida hadanganyi, ana karama, ana kipaji cha kuona
mbali, alivyonielezea na hata kufikia kuubadili moyo wangu, mimi nimemuamini
sana, tutafanikiwa tu…’nikasema
‘Ni kweli, mungu
akipenda na kwa jinsi aonavyo kwake kuwa ni sahihi, lakini kwanza unisikilize
kwa makini kuna kitu ninataka nikuambia mume wangu…’akasema
‘Mke wangu docta
kasema nisikuongeleshe kwa muda mrefu,kwani hali uliyo nayo haitakiwi uongee
sana, ….wewe subiria ukatibiwe, na mimi nipo pamoja na wewe, tutakuja kuonge
tu, kwani mimi naenda wapi..’nikasema
‘Ninajua wewe haja
yako kubwa ni kupata mtoto..na yote hayo uliyoyafanya nia na lengo lako ni
mwenyezi mungu akujalia upate mtoto..sawa ni heri kwako..na nikuambie kitu..,
mtoto utakuja kumpata, kwani mwenyezi mungu hamnyimi mja wake anachokiomba,
..na nina..oh…kwanza mimi ninashukuru kwa kauli yako kuwa umenisamehe, najua
hiyo kauli yako kweli inatoka moyoni…’akatulia
‘Kabisa mke wangu,
nakupenda sana mke wangu …nimekusamehe leo na kesho kiama….’nikasema na ukweli
huo sasa ulitoka moyoni, na ukumbuke hadi hapo nilikuwa bado sijafahamu ni nini
hasa kinachomsumbua mke wangu,..nilijua labda ni kutokana na kizazi baada ya
kuharibika mimba.
‘Ninajua baada ya
haya utasahau…na utanisahau, yote ndivyo maisha yalivyo, na ningelipenda iwe
hivyo, ifike muda usahau yote haya, usihuzunike sana, endelea na maisha kama
kawaida, kwani yote ni mapenzi yake muumba, ufanye hivyo tafadhali…’akasema.
‘Mke wangu
kwanini..’nikasema lakini yeye akaendelea kuongea
‘Mume wangu, nilikupenda
sana, nabado ninakupenda…japokuwa tuliambiwa mpende umpendaye lakini ipo siku
itafika mtaachana naye…na ukweli ni ukweli, kwani sisi ni nani, ni wanadamu tu,
‘akasema
‘Sasa mume wangu unielewe,
maana hata mimi sikutarajia kuwa yote haya yangelitokea..lakini ya mungu mengi,
huenda ilitakiwa itokee hivi ile iwe ni sababu…’akasema.
‘Usijali mke wangu
hayo yamepita tugange yajayo..kwanza ni wewe upone..’nikasema na yeye
akaendelea kuongea;
‘Mume wangu,
…nasikia ulimpiga docta, kwanini..’akawa kama anauliza lakini hakunipa muda wa
kutoa jibu.
‘Mimi..najua hasira
zako zipo karibu sana, lakini mume wangu, yeye…docta hana kosa kabisa, wengi
wanamuonea tu, najua utasema hivyo kwa vile..au nina mtetea,..lakini ukweli ni
kuwa yeye sio mkosaji…, ni sisi tunaokwenda kwake kumuomba iwe hivyo, na
inafikia na yeye kiubinadamu anaingia kwenye majaribuni ….na kwa hilo, kama ni
kosa basi hilo ni kosa langu mimi mwenyewe…’akatulia.
‘Achana
naye..sitaki kumuongelea huyo mtu…’nikasema.
‘Ni lazima
tumuongelee, ili niweze kukuondoa kwenye giza la hasira dhidi yake, na ili ujue
kuwa nilifanya hayo kwasababu gani..huwezi kuamini, ila kiukweli nilifanya hayo
kwa vile ninakupenda wewe mume wangu, hutaweza kuelewa kwasasa…, na huyo docta
amekuwa msaada mkubwa kwangu…’akasema na alipoendelea kumtaja huyo docta moyo
wangu ukaanza kwenda mbio….niliona kama anataka kuzifufua hasira zangu.
‘Kwanini tusiachane
naye tu mke wangu…’nikasema;
‘Ulikuwa unataka
mtoto…na umekuwa ukihangaika, ukiumia, nakumbuka hata siku moja wakati
tunataniana, uliwahi kusema ..hivi jamani kwanini nisipate hata mtoto wa
kusingiziwa,..iliniuma sana…sio kwamba nilichukulia hilo kama kigezo,..hapana
hilo nililifanya kwasababu nyingine kabisa….’akatulia
‘Kwakweli mke wangu…nakuomba
usiliongelee hili…maana unanifanya nirudi nilipotoka, hasira dhidi yake ni
kubwa sana…sijui…hata..wewe yaache tu’nikasema
‘Uliniambia kuwa ,
kati ya mmojawapo uliyemkosea ni yeye,..ulimtaja kwa jirani..nilijua tu ni yeye….
lakini nashangaa hukuonana naye, ukaonana na mke wake tu….sasa najiuliza kwani uliyemkosea
ni mkewe au ni yeye…?’ akauliza.
‘Sijui…hata sijui…..’nikasema
‘Mkewe mlikubaliana
au sio..eti kwa vile mlikuwa mkinishuku mimi…au sio, kuwa nina mahusiano na
docta au sio…hivyo ndivyo mlivyokuwa mnafikiria tokea awali, au sio.., lakini
awali ilikuwa sio kweli, hilo lililokuja kutokea lilitokea tu , na ni siku
moja,..kiukweli hata sijui ilikuwaje, ipo siku utajua….’akatulia.
‘Ndio hivyo…ukipona
tutaongea tu mke wangu, sasa…, yaishe, sasa..tulia kuongea….’nikasema lakini
alikuwa kama kaseti iliyorekodiwa hakuwa akinisikiliza akawa anaongea tu.
‘Ukweli ni kuwa
huyo mtu alikuwa akihangaika sana na mimi kupambana na tatizo nililokuwa nalo,…nilipimwa
kwingine , nikaja kumwambia yeye,akaanza harakati za kunisaidia..hata hivyo
mimi nilimuomba sana iwe siri kati yangu mimi na yeye…..’akatulia nilitaka
kumuuliza swali lakini akaendelea kuongea.
‘Kwa vile yeye
ndiye alikuwa dakitari wangu , tukajikuta tumejenga ukaribu,…lakini sio ukaribu
wa kimapenzi, hilo halikuwepo kabisa…na alijitahdii kadri ya uwezo wake
kutimiza wajibu wake kama dakitari…amejitolea hata kugharamia kwa pesa zake,
sijui utaweza kumlipa nini…mungu peke yake ndiye anajua hilo..’akasema
‘Kiasi gani
anakudai…?’ nikauliza, lakini hakunijibu akaendelea kuongea
‘Na kwa hilo,…juhudi
zake , gharama, kujitoa mhanga kwake,..uvumilivu wake, mimi ninakuomba mume
wangu ukitoka hapa uende kwake ukamuombe yeye msamaha, kama kweli nia yako ipo
safi ya kusamehe wale wote waliokukosea na uliowakosea, huyo umemkosea , kama
mimi umenisamehe, na huyo anahitajia msamaha zaidi yangu, wewe unastahiki hata
kumpigia magoti…..’akasema
‘Mke wangu…achana
na huyo mtu…siwezi hata siku moja….’nikataka kumkatisha lakini hakunipa nafasi.
‘Wewe ulidirikia
kwenda kwa mkewe mkaongea, na yeye , mkewe akakukubalia kuwa hata yeye
kaligundua hilo, kuwa mimi na docta tuna mahusiano…ujanja wenu ukapitia hivyo,…mkajenga
usuhuba,..kweli si kweli, yote nimeyajua , niliongea na mke wake…’akasema
‘Na…kwahiyo mkafanya
kama kulipiza kisasi lakini pia ukihangaikia kutafuta mtoto, lakini je mlimpata
huyo mtoto..je wewe una tatiz gani, jiulize sana hilo?..mungu alitaka
kukuelelesha ili ujue kuwa mambo mengine yanapatikana kwa uwezo wake, na sio
kwa utashi wetu…’akasema.
‘Kwahiyo unataka
kusema nini..lakini hata hivyo mke wangu hayo yameshapita sawa, ..sasa nimejua
kosa langu tuyaache hayo, na ni kwanini unazidi kunipandisha munkari…’nikasema
‘Mume wangu, ujue
ni kitu gani unachokifanya…na ni lazima nikuambie hilo kama hujaelewa,..mimi hilo
nimeliona kwa matendo yangu mwenyewe, mimi nilianza kutubia mapema kabla yako,
ila ilibakia kwako tu…’akatulia
‘Hali iliyokukuta
wewe, kwangu ilikuwa ni zaidi….mmh, najua umenisamehe….na sijui kama mungu
atanisamehe kwa hili, namuomba sana anisamehe… lakini muhimu ni wewe kwanza
unisamahe….kama hutaweza kunisamehe wewe kutoka moyoni mwako, basi….sina budi
kwenda kupata adhabu kali …inaniuma sana,…lakini maji yameshamwagika
hayazoleki..’akasema kwa uchungu.
‘Oh…’nikaguna hivyo
‘Ni kweli mume
wangu tatizo la kutokuzaa lilinisumbua sana mimi huwezi mimi nimehangaika hadio
kwa waganga wa kienyeji…lakini hayo niliyafanya kwa siri..meng nimeyafanya,na
kwanini nilihangaika hivyo, hata bila ya kukuambia,…..huenda mimi na wewe
tungeliweza kuvumilia, lakin jamaii iliyotuzunguka, ilikuwa ni tatizo….
‘Jamii hasa ndugu
zako, ….ilinifanya nishindwe kuwa na amani, kila siku naulizwa,..mwishowe
nikaanza kuitwa mgumba…je ni kweli mimi ni mgumba..’akawa kama anauliza.
‘Hilo ndilo swali
nilijiuliza na hatimaye shetani akaniingia , nia ni kutaka kuhakikisha,
kuwahakikishia watu kuwa mimi sio mgumba, ila kulikuwa na tatizo jingine..najua
hata wewe ulishafikia hatua ya kunifikiria hivyo, na wewe ukaanza kufanya hayo
uliyoyafanya,..japokuwa mkuki ni kwa nguruwe…’
‘Sitaki kulalamika
sana juu ya hilo....ila nataka unielewe…kwavile mimi nimeshaionja adhabu yangu
hapa duniani,..ninajua kabisa hii ni adhabu,sijui huko mbele itakuwaje…’akatulia
nikaona kama anakunja uso..kuashiria anahisi
maumivu makali.
‘Upo sawa kweli
wewe..kwanini hutulii mke wangu, inatosha…’nikasema na yeye kwa shida
akaendelea kuongea.
‘Mume wangu
nakupenda sana,..hata kama nilifanya kinyume cha ndoa yetu,…na kinyume cha
uhalisia wa kupenda , maana tendo nililolifanya ni kama vile humpendi mwenzako,
au sio..hapana , ..nakupenda sana mume wangu, na hilo nililifanya ili
usihangaike, ili uweze kuwa na kile unachokitamani,..ambacho ni mtoto…na na mtu
wa kunisaidia akawa ni do-do-ctaah’naona hapo sauti ikaanza kufifia.
‘Mke wangu wewe pumzika
sasa inatosha, inatosha sitaki kusikia tena hayo.. tu…’nikasema
‘Nita-nitapu-pumzika,
hilo halina jinsi,…na nikipu-pu-mzika, najua ndio moja kwa moja…’akasema
‘Kwanini unasema
hivyo mke wangu, docta kasema unakwenda kufanyiwa upasuaji na baada ya hapo
utakuwa huna tatizo tena..utapona tu mke wangu, sasa tulia usiongee.., na
…’akanikatisha.
‘Ni hivi mume
wangu, docta hana makosa, siku alipokuwa akinichunguza, yeye aligundua,
hakuniambia akanielekeza kwa docta bingwa wa mambo hayo..na huyo docta
akagundua kweli kuwa nina tatizo,..na nilimuuliza tatizo hilo ni la muda gani,
nitaweza kuhimili kwa muda gani, akasema hata mwaka, lakini itakuwaje..’hapo
akatulia
‘Unasema…?’
nikajikuta nimeuliza
‘Basi , kwa vile
nakupenda mume wangu, nikajiuliza nina maana gani hapa duniani,..unataka mtoto
na mimi sijui nitawezaje kukupatia mtoto...na kiukweli , siku aliponiambia kuwa
sina muda hapa duniani…nikaanza kuyaacha yake masharti yote niliyoambiwa…ili tu
unipatie huo ujauzito..lakini haikuwahi kutokea….nikawa sina raha…’akatulia
‘Nikajiuliza itakuwakuwaje
maana mimi sina muda hapa duniani, nifanye nini ili ubakie kuwa na raha..ili
angalau upate mtoto, hahaha,… sio nacheka ila nikakumbuka kauli yako
ulivyopenda kusema..nipate mtoto..tu, hata kama wakufikia..basi nikaona kumbe
ninaweza kuutumia huo mwaka kwa ajili yako..ili niweze kukupatia kile
unachokitaka, kabla muda haujafika,..hata kama… lakini ..’akatulia.
‘Mke wangu achana
na hayo maneno,ukifanyiwa upasuaji, utapona tu…,hilo nina uhakika nalo baada ya huo upasuaji kila
kitu kitakuwa sawa..’nikasema.
‘Ni kosa kubwa mume
wangu nilifanya, kwanza nikakiuka masharti , pili nikavunja miiko ya ndoa,
tatu..aah..na kiukweli docta alinishauri sana, lakini mwishowe
..mmh..mwishowe..mhhh, nikajitolea mhanga, sasa kipo wapi…’ akasema
‘Sasa kipo
wapi..tuacheni jamani…unajua mimba hiyo ilikuwa kama sindani nimeimeza
tumbaoni, kila mtu ananichoma…nikawa nahisi maumivu makali sana..ikafikia muda siwezi…siwezi..maumivu,
yalikuwa …ni makali sana, nikaona pamoja na mengine niliyowahi kukuelezea awali
kuwa…unaku-ku-mbuka, nika-nika-shindwaah kukupatia..na-na- sijui tena, …’mara
akaanza kuhangaika, kama anapata shida fulani,…’nikageuka huku na kule, kuona
kama naweza kusaidia au kumuita docta.
Chumbani mle
kulikuwa hakuna mtu mwingine, …nilikuwa mimi na mke wangu tu, na nilipoona mke
wangu anazidi kuhangaika ikabidi nipige ukulele.
‘Docta, njoo
haraka..’nikasema lakini hakukutokea mtu, nikaendea kengele ya dharura
nikaibonyeza na haikupita muda docta akaja, na kuniambia nitoke nje. Nilikataa
lakini wakanilazimisha kwa kunitoa kwa nguvu.
Nilifika nje nikiwa
sasa natetemeka, mwili hauna nguvu, miguu haina nguvu kabisa, na hii hali
ilinianza siku za karibuni, sikuwa na tatizo hili kabla, …sijui kwanini..
Na kwa muda ule
akili yangu ilishindwa kufanya kazi, nikaenda kwenye kiti pale nje na kukaa,nikasimama,
nikakaa nikasimama na kukaa ! Mtu aliyeniona alijua labda nimepewa adhabu ya
kukaa na kusimama, …
Yaani sijui
ilitokeaje, yalikuja maumivu makali kichwani, …na mara maumivu makali yakatokea
moyoni, kilichofuata hapo ni giza kutanda usoni, nikajikuta naelea gizani, na
sikujua kilichoendelea…
Nilipoamuka
nilijikuta nipo kitandani…hospitalini..
NB: Naishia hapa
kwa leo
WAZO LA LEO: Kipindi mtu anaumwa, au akiwa na shida kubwa kubwa, ndicho
kipindi mtu huyo anastahiki kupendwa, kusaidiwa kuhurumiwa na kila mtu mtu
anayemuhusu, hata kama ulikuwa ni adui wake, inabidi uadui huo, au chuki hizo
kuziondoa. Imani ya kweli ya dini, inaonekana kipindi hicho, kwani tumeambiwa
hivi;-
‘’Hatoamini mmoja wenu
(kikweli kweli) mpaka atakapompendelea ndugu yake kile anachojipendelea nafsi
yake…’ ni nani asiyependa siha njema,…afya, maisha bora …nk
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment