Siku ya pili,
Nikiwa nimelala
kwenye hifadhi ya jamaa yangu, kiusalama,
Niliamuka asubuhi
sana nikijiandaa kuondoka, kiukweli akili sasa ilikuwa imetulia na nilianza
kujilaumu kwa hayo niliyoyafanya, sio kawaida yangu kujilaumu kwa mabaya…
lakini sasa nafsi ilianza kunisuta,.
Kwanza nikawasha
simu yangu….nilipoona miito mingi ya simu, na ujumbe za maneno zikinitafuta,
lakini hakuna ujumbe uliosema lolote zaidi ya kuulizwa upo wapi…nikaizima simu …na
wakati nafanya hivyo mlango ukafunguliwa, akaingia mwenyeji wangu,
Tuendelee na kisa
chetu…
*********
Mwenyeji wangu
alipoingia, nilimtupia jicho kwa haraka, nikamuona ni mwingi wa
wasiwasi,..ninamfahamu sana maana tumeishi naye kwa muda mrefu, na mimi nina
hulka ya kumtambua mtu alivyo nikimuangalia usoni mwake.
‘Kuna tatizo…?’
mimi nikaanza kumuuliza hata kabla hajasema lolote. Na yeye kwanza akasogea
hadi kwenye dirisha akafunua pazia na kutizama nje, halafu akageuka kuniangalia
akasema;
‘Ni vyema ukawahi kuondoka, maana hali sio
shwari,…sio kwamba nakufukuza lakini unielewe tu ndugu yangu, siunajua,…. mimi naweza kuonekana
nimeshirikiana na wewe…na mimi nimeamua ..na jamii inafahmu hivyo, sitaki tena
kujihusisha na jambo lolote baya…’akasema
‘Ni kweli, usijali.,
nimekuelewa, nashukuru sana kwa kunihifadhi na matibabu
uliyonifanyia,…nisameheni sana kwa usumbufu huo’nikasema
‘Mhh, rafiki yangu
kweli umebadilika, …kufikia kunitamkia maneno hayo,…kweli hujafa hujaumbika,
kwako neno samahani sidhani kama lilikuwepo kwenye msamiati wako,…’akasema
Ni kweli mimi
nilikuwa nduli, amri ndio kauli yangu, kiburi,…sikupenda kuishi kilege lege,
ukikosea ni adhabu papo kwa papo…na ole wako uje useme samahani nimefanya hiki
nimekosea, nimeharibu, hatukufanikiwa...kitakachofuata hapo ni kipigo..sijui
kwanini niliishi hivyo…niliweka masilahi mbele, na sikupenda mtu aniingize
kwenye hasara kwenye biashara zangu.
‘Unajua,… awali
uliponiambia unataka kufanya toba, sikuamini, kwa jinsi nikujuavyo….lakini sasa
naanza kukuamini kidogo…’akasema na mimi nikawa nimesimama, sikusema kitu.
‘Lakini kiukweli…toba
ya kweli sio rahisi kihivyo…ni shida tu ndio zinatusukuma, au sio…’akasema kama
anauliza
‘Mhh….’mimi
nikaguna tu, nilitaka kumwambia mbona yeye kaweza, lakini sikusema neno,
nikaguna hivyo tu.
‘Unajua kama kweli
tungelifahamu msingi wa kuletwa kwetu hapa duniani, sizani kama kuna mtu
angelihangaika sana na hii dunia zaidi tungelihangaika na ibada, na kufanya
yale tu tuliyoamrishwa tufanye, nikimaanisha matendo mema..’akasema
‘Hebu chukulia
mfano mtu akiamuka asubuhi ni nini cha kwanza anachofikiria kwenye kichwa chake… cha kwanza atakimbilia kuangalia saa, au
kuangalia nje, kuwa ni saa ngapi, …wasiwasi nimechelewa kazini, nitapatia wapi
pesa, nitakula nini…mungu hapo hayupo, hata ile kushukuru kuwa umeweza
kuamuka,kupumua, ambavyo vyote hivyo ni neema ya mungu hatkumbuki…’akasema
‘Mhh…’nikaguna.
‘Nikuulize ndugu
yangu, ulipoamuka leo asubuhi ni nini cha kwanza kuwaza…?’ nikamuuliza
‘Nilikumbuka yaliyotokea
nikaona niwahi kuondoka…’nikasema
‘Umeonaaeeh….mungu
hukumkumbuka kwanza, kwa rehema zake ukaweza kuamuka, kwa rehema zake ukaendelea
kupumua,…kwa rehema…’akasema na mimi nikamkatiza kwa kusema.
‘Ndugu yangu
samahani , muda…’nikasema.
‘Ni kweli,muda…ila ninataka
kukuweka wazi kabla hujaondoka,…kukujenga kiimani, maana imani ya kweli ni
pamoja na kujitambua wewe ni nani, …ni nani kakuleta hapa duniani…ukimjua huyo
ukamtii, ukamshukuru ukamuomba, ukamtegemea yeye, mbona haina shida…’akasema
‘Ni
kweli….’nikasema
‘Ni kweli..lakini imani
hiyo tunayo…, na tungelikuwa na imani hiyo kwa kila mtu mbona tungelikuwa
peponi, twaishi kwa amani tu…tatizo wengi wetu au karibu kila mtu anahisi kuwa
huenda tumeletwa hapa duniani kushindana katika kutafuta mali, ndio imani yetu
kweli si kweli, kama ni hivyo…tunajidanganya,….’akasema na kusogea kuangalia
dirishani , kulishapambazuka vyema.
‘Unataka kusema
nini, kuwa tukae tu,….tukumtegemea mungu au…?’ nikamuuliza
‘Ni sawa,..kuhangaikia
dunia ni muhimu, tunahitajika kutafuta mali, lakini hata hivyo basi,…tuitafute
mali hiyo kwa njia iliyo halali… ni nani
anaweza kujithibitishia kuwa mali aliyo nayo ni halali tupu..?’akaniuliza na
mimi nikasema..
‘Sijui…..’nikasema
‘Mimi kwa kweli
nakutakia mafanikio mema, uweze kulifikia hilo daraja la ucha mungu,maana hayo
unayoyafanya ni …kuutafuta ucha mungu wa kweli, na ucha mungu wa kweli huanzia
huko,kwenye toba ya kweli….’ Akasema
‘Aamin..’nikasema
nikataka kuanza kuondoka.
‘Lakini
sikiliza…najua una haraka sana,…mimi ninakufahamu sana wewe rafiki yangu, wewe
uliishi maisha mabaya sana kama ilivyokuwa mimi…, lakini nikupe angalizo moja,….
kwa mungu, yeye ni mkwasi, humsamehe
yoyote Yule hata kama alikuwa mbaya kiasi gani, muhimu uwe amedhamiria kiukweli
kutubia..’akasema
Mimi nilishakuwa
tayari kuondoka ….
‘Ndio nimekuelewa…’nikasema
nikiinua mguu kuondoka.
‘Nilikuuliza awali
je upo tayari kufanya hivyo, ukasema ndio…, nilijua tu sio kweli, ulikubali tu
kwa vile ulikuwa na shida…mungu akakujaribu kidogo tu, naona ilivyotokea,..sasa
wazia hilo tena kabla hujaendelea na hicho unachotaka kukifanya..’akasema ,
nikatikisa kichwa tu, nilitaka kumwambia nachelewa, lakini niliona sio busara.
‘Ndio
nimekuelewa…’nikasema
‘Umenielewa sio?….au
unanijibu kwa vile una haraka, nakuambia hili nikiwa na maana yangu…huko
unapokwenda sasa hivi unakwenda kukutana ni mitihani mikubwa, unakwenda
kupambana na wenye dola, kupambana na nafsi yako, sasa sijui…mimi niseme tu
nakutakia kila la heri…’akasema
‘Wewe hujui shida
gani ninazozipata..sina raha ndugu yangu,…naumwa, mali naiangalia hivi hivi…ina
maana gani,sina hata mtoto wa kuniliwaza, ina maana gani,sasa hata Yule
niliyekuwa nikimtegemea ndio huyo,kanisaliti….hapana ni lazima ..ni lazima
nifanye jambo…wewe huniamini tu…’nikasema
‘Unajua ….mimi
nahisi bado haupo tayari…maana ili ufanikiwe kwa hilo,kwanza pamoja na kutaka
kusamehewa, na wewe ukubali kusamehe….kumbuka uliyowafanyia wenzako ,yaliwauma
hivyo hivyo, ulivyoumia wewe natoba ya kweli kwanza kabisa huanzia moyoni mwako,
hapo umeongea unalalamika, bado hujaiva…’akaniambia
‘Sasa nifanyeje,…nimejitahidi
sana, hebu fikiria na wewe…., hata ingelikuwa ni wewe, mke wako anakufanyia
hivyo, ..hapana unajua, inauma sana …natamani kuumiza, natamani kulipiza kisasi…tatizo
ni kuwa nilimuamini sana mke wangu…, sikutegemea hata siku moja kuwa
atanifanyia hivyo alivyonifanyia ..ni kwanini..’nikasema
‘Na je ni kwanini
na wewe ulimfanyia hivyo ulivyomfanyia…., wewe hujuoni tu, uliyowafanyia
wenzako yanaweza kuwa ni mabaya zaidi ya hayo uliyofanyiwa wewe, lakini sio
rahisi kwa nafsi zetu kujiona, wamnyoshea mwenzako kidole, ni kimoja tu je wewe
vidole vingapi vimekunyoshea wewe, chunguza kwanza hilo…’akaniambia
‘Lakini yeye ni mke
wangu, na..na yeye hatakiwi kujilinganisha na mimi, yeye ni mtunza dhamana ya
mume wake,..kama alifanya hivyo kwa kujilinganisha na mimi,sizani kama anafaa
kuwa mke wangu…’nikasema
‘Hahaha unaona eeh,
kwetu sisi dunia ni hivyo, umimi tu…mke kwako ni tofauti na wewe…kumbuka huyo
ni mwenza wako, utakavyo kutoka kwake nay eye halikadhalika anataka hivyo hivyo
kutoka kwako,…tusigeuze dunia hii ni uwanja wa fujo, mwenye nguvu
mpishe…mhh..kama bado una hisia hizo, mimi naona bado kabisa hujaiva, hebu sasa
nikuulize ukitoka hapa unakwenda kufanya nini huko..?’ akaniuliza
‘Nitajua huko mbele
kwa mbele…lakini muhimu nijue kinachoendelea, na dhamira yangu ipo pale
pale,….kutubia, kuomba msamaha, lakini lazima niupate ukweli, kuhusu mke wangu,
bado nina maswali mengi kichwani hayajapata majibu….lakini nina uhakika nitayapata
tu, kama bado yupo hai…’nikasema
‘Haya…lakini
usisahau sharti hilo… kuwasamehe waliokukosea….ulinicheka sana kipindi kile..,
lakini nione mimi, sasa hivi nipo huru,….nahisi nipo dunia nyingine, ya
utulivu...’akasema
‘Hongera…’nikasema
‘Sasa kama na wewe
unataka ufanikiwe,…ujue mtihani wake ni mkubwa, sio rahisi kihivyo,…lakini
rafiki yangu nisikukatishe tamaa, maana ugumu unakujaje , kwa vile bado
hatujajitambua sisi ni nani na tumekuja hapa duniani kufanya nini…hilo
nalirudia tena na tena kwako…’akasema huyu jamaa , na mimi nikamwangalia jamaa
yangu huyo nikiwazia mbali….
Jamaa huyu alikuwa
na mimi kwenye kuhangaika, kwenye kutafuta maisha,…tulikuwa washirika kipindi
Fulani kabla hajabadilika, nilimshangaa siku moja akaniambia yeye, kaamua
kubadilika, hataki tena mali ya dhuluma, …’
‘Kwani mlikuwa
mnafanya mambo gani zaidi wewe na yeye…?’ nikamuuliza na yeye akaendelea
kuongea kama vile hakunisikia.
‘Rafiki yangu
aliposema kaamua kubadilika …hataki biashara tuliyokuwa tunafanya tena,..nilimcheka
sana kipindi hicho, lakini hakurudi nyuma,…aliamua na kweli akabadilika,…na
katika mabadiliko hayo alifikia kipindi akawa hohehahe…nilimuonea huruma sana, nikakata
urafiki naye kabisa,lakini sasa huwezi amini, ana furaha, ana familia yake…..kesharizika
na maisha yake!
Sasa uone kinyume chake, mimi sasa namtegemea
yeye kiushauri,…yeye alinishauri kuwa, ni bora niende kwa kiongozi mmoja wa
kidini, anayejulikana sana kwa kuombea watu, kuwashauri nk….na mara nyingi kiongozi
huyo wa kidini akikuambia jambo ukilifuatilia, unafanikiwa,...
Jamaa yangu huyo aliponiona nimezama kwenye
mawazo akasema;
‘Ndugu, una uhakika
upo sawa sasa…,upo tayarii kukabiliana na kazi iliyobakia,ujue hiyo kazi
iliyobakia ndio kubwa zaidi…kukubali kusamehe,..na kuwa tayari kwa lolote lile
hata ikibidi kufungwa , je utaweza…?’ akaniuliza
‘Eti nini, kufungwa…wewe…’nikamkazia
macho jamaa na jamaa akatikisa kichwa sasa yeye akigeuka kuondoka.
‘Mimi ninakumbuka
vyema, Yule kiongozi wa dini aliniambia
kwamba, nikifanya toba, nikamaliza mambo yangu yatanyooka, sasa wewe unaniambia
nini, kwanza hujamambia umesikia nini..?’ nikamuuliza jamaa yangu huyo hakusema
neno, akawa anatembea kutoka nje….
‘Sikiliza mimi
siwezi kwenda jela,..siwezi kabisa, kama nitafungwa ujue ninakwenda kufia huko,
mimi ni mgonjwa…ninaumwa,..unasikia naumwa, usinione nimenenepa hivi….ok, kama
hutaki kunieleza zaidi ngoja niende huko huko nitajua mbele kwa mbele,lakini
siwezi kujipeleka jela, ……’nikasema na mimi nikaanza kuondoka...
WAZO LA LEO: Hatuwezi tukawa wachamungu wa kweli mpaka tumfahamu
mwenyezimungu, na kumkubali ndani ya nafsi zetu. Tuwe na imani thabiti kuwa
mwenyezimungu yupo na yeye ndiye katuleta hapa duniani, tumuabudu, tufanye
aliyotuamrisha (mema) na tuyaache aliyotukataza (mabaya)
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment