Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Sunday, July 24, 2016

TOBA YA KWELI-6



Unajua unapofanya kosa hata kama upo peke yako utakuwa unajihami, hujiamini…ndivyo ilivyotokea kwangu, japokuwa nilijua nipo ndani kwangu, nimefunga mlango, lakini bado nilihisi kama kuna mtu kaniona kwa yale niliyoyafanya…nilijua nimefanya kosa, nilijua nimeua….na zaidi ni kuwa niliyemuua ni mke wangu mwenyewe…mke niliyempenda sana.
Kiukweli nilimpenda mke wangu sana, niliweza kufanya mabaya kwa wengine huko nje lakini nikirudi kwa mke wngu nilikuwa najitahidi kuonekana tofauti…nazikunjua kunyazi zote za usoni…na zaidi nilikuwa na wivu sana kwa mke wangu, lakini sikujijua upande wa pili wa shilingi.….
‘Ninajua kila kitu…’ilikuwa sauti iliyonifanya nigwaye…sauti iliyozidisha hasira na chuki moyoni, ….sauti iliyonifanya harufu ya damu isikike kwenye hisia zangu, sauti iliyoniondoa kwenye ubinadamu….
‘Ninajua kila kitu….’anajua nini..nikajiuliza
Kwanza niligeuza kichwa kwa tahadhari, lakini nilipojua kuwa huyo aliyekuwa nyuma yangu ni adui lakini nina uhakika hana silaha, nilipoligundua hilo nikageuka mzima mzima, na kwa haraka nikajitutumua, nikijiweka tayarii kwa mapigo ya kumaliza.
‘Ninajua kila kitu…na …kila kitu kipo tayari,kama lolote likinitokea mimi,au familia yangu polisi watajua kuwa ni wewe…’akasema na kauli hiyo ilinifanya nianze kusinyaa,,..ni kama puto lililokuwa na upepo, ghaflalikatoboka, na kuanza kusinyaa.
Pamoja niliwahi kuwa askari lakini sikupenda sana kukabiliana na polisi, kwangu mimi hao watu niliona kama vizingiti vya kuyafikia malengo yangu, na kwenye shughuli zangu nilijaribu sana kuwa mbali nao…ikibidi , imebidi lakini mara nyingi nilikuwa nikimtumia wakili wangu apambane na hao watu….sasa huyu jamaa ananitamkia hilo..
‘Umeingiaje humu ndani…?’ ilikuwa kauli yangu ya kwanza, huku nikijitahidi kurejesha hali yangu lakini sikuweza, kilichoanza hapo ikawa ni kwikwi, nilijiwa na kwikwi ya ghafla….naye alipoiona hiyo hali akasema.
‘Chukua maji kunywa na utulie, maana hasira hazitakusaidia lolote…kiukweli ilivyo sivyo ilivyo kihalisia….kuna makosa yamefanyika,…na hata mkeo halijui hilo…’akasema.
‘Usi…usi…usi…..’kwiikwi ikawa imenibana sana,na jamaa,akazidi kunishauri ninywe maji,….yeye mwenyewe akayafuata maji na kunipatia,…nikanywa, huku nikitetemeka, hasira,….nilijua bila kufanya jambo sitaweza kutulia…ile ile gilasi, nikaivurumisha ikaenda kupiga ukutani..mlio uliotokea hapo ulikuwa kama bomu.
Jamaa akashtuka na kubakia mdomo wazi…akajua sasa kaingia kwenye choo cha kike na ndani kamkuta mama mkwe!
Nikaanza kupiga kila kilichokuwa mbele yangu,viti,..vunja vunja, ilichukua robo saa,kila kitu kilikuwa chini…vitu nikavunja vunja,…vilivyopona nikatupia chini.. damu zikawa zinanitoka utafikiri nilikuwa napigana na mtu mwenye silaha….na baadaye nikawa nimechoka, nikapiga magoti na kuanza kulia…
Nililia kwa nguvu, mpaka hamu ikaisha, halafu nikatulia,…
Jamaa alikuwa kasimama,anatetemeka,….haamini anachokiona,,….na hata alipoona nimetulia bado hakujiamini,nilimuona kama anataka kukimbia, lakini hakuweza, alikuwa na mkoba wake kasimama tu na alipoona nimetulia, akahema na kabla hajasema neno mimi nikasema..
‘Nataka uniambie ukweli,je ni kweli, hivyo mke wangu alivyoniambia….?’ Nikasema.
‘Mimi sijui kakuambia nini, ila kiukweli kuna makosa yaliyofanyika, na sijui ni nani alifanya hivyo na kwa nia gani,…na sijui mkeo kakuambia nini na kwa kiasi gani, maana hata yeye haufahamu ukweli wote….ndio maana nikaja kwa haraka….’akasema,
‘Nakuuliza tena, ni kweli ….alivyosema mke wangu kuwa ….yeye ndiye aliyeitoa hiyo
mimba…..?’ nikauliza.
‘Hiyo ni kweli, kwa jinsi alivyonielezea, na hakutaka ukweli ujulikane…’akasema.
‘Ni wewe uliyemsaidia kuitoa hiyo mimba…kama sikosei…?’ nikauliza.
‘Hapana, mimi nilimsaidia pale alipoona ana tatizo, …sijui na hakuwahi kuniambia kabla kuwa ana mimba..’akasema.
‘Je ni kweli kuwa mtoto huyo sio….alikuwa sio wangu…?’ nikamuuliza.
‘Hilo sijui… sina uhakika nalo sana…lakini kuna kitu nilikuja kugundua,…ndio maana nilitaka nionane na wewe kwanza…nahisi hapo kuna makosa yalifanyika, sijui ni nani alifanya hivyo, na hata mkeo hakunielewa vyema, na kuna uvumi mbaya dhidi yangu, sio kweli….’akasema akijiuma uma.
‘Uvumi mbaya!! Mhh, kwanini wakuseme wewe, wewe si unajijua bwana kuwa wewe kidume mbegu, mtaalamu wa mapenzi , au sio.. niambie ukweli kabla sijauchana uso wako vipande viwili, nita-ta-kura-ru-a….’nikawa nashindwa hata kuongea.
‘Ngoja nikuambie kitu wewe ni mwanaume kama mimi….japokuwa ni kweli sihitajiki kujiingiza huko, lakini…sijafanya makosa kama wanavyosema watu, hayo yaliyotokea ni ..hata wewe usingeliweza…nimejitahidi sana,…naomba unielewe hayo ya ndani zaidi siwezi kukuelezea, ….’akajitetea.
‘Hujafanya makosa wewe eeh, hivi kuzini na mke wa mtu hujafanya makosa..hahaha? kweli wewe ni kidume, …kidume mbegu sio..eti kwa vile,..unapendeza una umbile zuri…unajua mapenzi sana, au sio..mtaalamu wa mapenzi hahaha, sasa nikuambie kitu mimi leo, nitaviharivu hivyo vyote…ila nataka uniambie ukweli kwanza…’nikatulia nikijizuia nisianze uharibifu wangu.
‘Ndugu nielewe, kwanza tusipoteze muda, kuna ..matibabu yanahitajika kwa mkeo ndio maana nimepitia hapa, na mengine nikuambie ukweli ni katika hali ya kuharibiana tu kibiashara..mimi sija….hata nimesikia na wewe na mke wangu, lakini sikuami..najua ni fitina tu.’akasema na mimi nikamnyoshea ishara ya ngumi, kuashiria sasa naweza kufanya lolote.
‘Je ni kweli….kuwa unautumia udakitari wako kama mtego wa kutimiza tama zako za kimwili,…kuwa wakija akina mama na matatizo yao wewe unawarubuni kimapenzi ili wapate watoto’nikamuuliza huku nikimsogelea.
‘Sio kweli….sijawahi kufanya hivyo, mimi natumia udakitari wangu ipasavyo, mengine ni ….maswala binafsi, sijawahi kumlazimisha yoyote yule au kutumia ujanja wowote ule , wengi wao wameniomba tu… , wamenitaka wao wenyewe kwa ridhaa yao,…na..na..wengine nawakatalia,…’akatulia.
‘Unasema nini….?’ Nikamuuliza huku nikijaribu sana kujizuia…, sijui siku hizi nimepatwa na nini, maana kwa muda huo huyo jamaa angeshaliharibika sura….
Nikajitutumua…
‘Niambie ukweli….sema haraka….’nikatoa sauti ya nguvu iliyomfanya ashutule na kusema;
‘Mimi kama dakitari …siwezi kukuambia zaidi mambo ya ndani, maana hiyo ni siri yangu kati yangu na wateja wangu,…ila ninakuhakikishia kuwa mengine sio kweli….’nilikuwa nimeshamkaribia.
‘Unasema nini…?’ nikamuuliza sasa tukiwa tunaangaliana uso kwa uso…niliona kwa jinsi alivyokuwa kachanganyikiwa kwa uwoga.
‘Wananisingizia tu….’akasema.
Hapo nilishindwa kujizuia, kwa haraka nikarusha ngumi iliyomuingia barabara jamaa huyu dakitari usoni, akarushwa na kudondoka chini kama gunia. Moja ya sifa zangu ni kuwa ngumi yangu ilikuwa na nguvu sana, ikikupata ni lazima uende chini.
Nikamuuendea pale chini, nikitaka kuanza kumsindilia mingumi,…na mara nikasikia sauti ya kugugumia…ilikuwa sauti ya mtu kama anahema huku akigugumia, …
Mwanzoni nilijua sauti hiyo inatokea nje, lakini niliposikiliza kwa makini nikajua inatokea ndani , chumbani alipokuwa kalala mke wangu, hapo nikasita , ina maana …mke wangu bado yupo hai…hata kama yupo hai huenda ndio anaishia…nikawaza hivyo!
Docta alikuwa kalala sakafuni akiwa hoi, hakutarajia kipigo hicho, na yeye aliweza kuiskia hiyoa sauti na kwa sauti yenye uwoga na maumivu akasema;
‘Hu-huyo ni mkeo a-a-si- sio… mke-o anahitajia huduma yangu tafadhali.., kuna dawa natakiwa nimpatie, ndio maana nimekuja hapa kwa haraka…’akasema.
‘Najua umekuwa ukitumia mbinu hizo ili mfanye uchafu wenu….’nikasema.
‘Sio kweli..mkeo anaumwa…’akasema
‘Anaumwa eeh! Hahaha, kweli anaumwa, hebu niambie…anaumwa nini,…uzinzi, au…’nikasema .
‘Sio hivyo mkeo anaumwa sana….’akasema
‘Unanijua mimi lakini,…yaani sijui leo nimekuwaje, mpaka sasa unapumua,…ok, ok…haya inuka, nenda kamtibie huyo Malaya mwenzako..nenda..na, mkimalizana huko...'nikasema huku moyoni nikimuwazia mke wangu
'Kama anaumwa haya, kama kafa haya...ila ukitoka huko, ama zako ama zangu ….huenda mkafungia hiyo ndoa kuzimuni..hilo nawaahidi…’nikasema na Dakitari akiwa anatoka damu puani, akasimama.
‘Unafanya makosa sana, sio kweli kama unavyofikiria wewe….’akasema huyo dakitari
‘Nini…..unataka kunitibua tena…’nikasema nikimuendea, na yeye kwa haraka akaelekea chumbani.
Yaani nilianza kujilaumu kwanini nimekuwa mrahisi kihivyo, nikageuka nikitaka kuwaendea huko ndani, lakini sijui ni kitu gani…nikajaribu sana kujizuia, …baadaye nikaona nikiendelea kukaa hapo nitaua, nikageuka na kuanza kutembea kulekea mlangoni, kutoka nje.
Kiukweli nilipotoka pale sikuwa na jingine zaidi ya kutokomea kokote nilihisi kama nikirudi hapo sizani kama kuna mtu atapona, nikawa natembea kwa mwendo wa haraka, na ole wake mtu angepita mbele yangu,… mbio mbio,…nikawa natembea tu, kumbe akili yangu ilikuwa ikinisukuma niende mahali fulani, ..
********
Nikajikuta nipo mbele ya nyumbani moja, nikagonga mlango, na aliyenifungulia alikuwa mwanamke,..mwanamke yule aliponiona akapiga ukulele akijaribu kushika mdomo kujizuia asiendelee kupiga ukelele….sikujua ni kwanini, na haraka akakimbilia ndani, ..baadaye akajitokeza mwanaume.
‘Vipi, kuna nini kimetokea…?’ akaniuliza huyo mwanaume akiniangalia kwa mashaka. Jamaa huyo amekuwa rafiki yangu wa muda, na ndiye mtu anayenisaidia sana kiushauri, na ndiye aliyenishauri nikamuone mtu wa dini ili niweze kupata ushauri nasaha wa kiroho, japokuwa na yeye mambo hayo anayajua kidogo.
Aliponiona nipo kwenye hiyo hali, akangalia huku na kule…nahisi alijua nafukuzwa na polisi au…
‘Sijui kumetokea nini, ninaomba unisaidia ndugu yangu…’nikasema na yeye akafungua mlango, na kunipisha niingie ndani, nilihisi mwili ukinilegea, mwili uliisha nguvu kabisa, na kitu kama giza kikatanda usoni mwangu na kudondoka sakafuni, nikazama kwenye giza…
**********
Sijui ilichukua muda gani, kwani nilipozindukana nilijikuta nimelala kwenye mkeka, na pembeni yangu kuna beseni la maji,….niliona yale maji yana rangi, kama nyekundu hivi, yalikuwa kama yana rangi ya damu.
Kwa haraka nikajaribu kujiinua, na nikahisi mkono ukinizuia, niendelee kulala.
‘Endelea kupumzika utajitonesha…’sauti ikasema
‘Oh kumetokea nini…?’ nikauliza
‘Umeumia sana,…ni kama uligongwa na gari, au…hata hatujui, kwani ilikuwaje, sisi tulitaka kumuita dakitari, lakini tukaona kwanza tukufanyie huduma ya kwanza, hebu niambie kama unakumbuka vyema, kulitokea nini…?’ ilikuwa sauti ya huyo jamaa yangu na pembeni yangu kulikuw na mtu mwingine.
‘Hata sijui..mimi nahisi nimeua mtu…’nikasema.
‘Umeua mtu kwa vipi…ulikuwa unapigana, au ?’akaniuliza huyo jamaa mwingine.
‘Nimepiga…hatujapigana…hata sijui kwanini…hata sitaki kukumbuka….’nikasema
‘Sasa unajuaje kuwa umeua, mimi sijakuelewa…’akaniuliza huyo jamaa mwingine.
‘Tuyaache hayo, nasubiria matokea, lakini kwasasa sijutii, na ikiwezekana naweza kuua tena…’nikasema.
‘Ni hivi ninajua una hasira sana…na ulichokifanya huko ulipotoka sizani kama ni sahihi,siku ile ulikuja kwangu nikajaribu kukusaidia kiushauri, …’akasema.
‘Nimeshindwa mkuu wangu wa imani , nisemehe sana,….siwezi..’nikasema
‘Nilijua tu…nilijua hatua ya kwanza kwako utaiona ni rahisi, kuomba kusamehewa ni rahisi kwa namna moja au nyingine, maana unataka utendewe, kila mtu anajipenda atendewa yale yatakayomridhisha nafsi yake au sio…lakini hata hivyo mimi nakufahamu sana, nilishakuona wewe ni mtu uliyetawaliwa na jazba,…kiburi cha pesa..na hiyo ni hatari..’akasema.
‘Pesa hazina maana tena kwangu….’nikasema nikisita maana sio kweli, mimi na pesa ilikuwa kama pete na kidole, ukiniambia kuna kazi ya pesa umenifanya kinywa kibakie wazi kwa tabasamu…
‘Nilikuambia nini, kwanza anza tabia ya kuchunga hasira zako, pili tubia makosa yako mpaka moyo wako ulainike. Halafu waendee uliowakosea uwaombe msamaha, utubu yale uliyowafanya mbele yao, usiwafiche, je uliweza kufanya hivyo?’ akaniuliza
‘Ndio..lakini…’nikataka kujitetea.
‘Hiyo ilikuwa hivyo, ili uone wenzako walivyo mbele yako,…ni rahisi au sio, unaomba, unaipiga magoti..wengi watakuonea huruma, …. lakini hatua hii ya tatu, ndio hiyo imekushinda..
Hiyo ni hatua ambayo na wewe,unatakiwa… uwasamehe wale waliokukosea, nilikuambia wazi kwa jinsi nilivyooteshwa, …mimi ssiwezi kukuhakikishia, lakini mara nyingi njozi zangu huwa ni kweli,…na kama ungelifanya hivyo, ungelifanikiwa, matatizo yote uliyokuwa nayo yangelimalizika, sasa umeharibu, …..’akasema .
‘Nimeharibu…kwanini, kwahiyo…si..si wezi kufanikiwa tena..?’ nikauliza na kabla sijapata jibu simu yangu ikawa inaiita.
Niliangalia na kukuta namba nisiyoifahamu, nikataka kuizima, lakini nikashikwa na shauku kuichunguza vyema, niliona kuna miito mingi ambayo haikipokelewa, na kabla sijaizima Yule jamaa yangu mwenyeji aliyenisaidia akasema;
‘Samahani sana, simu yako iliita sana na mimi nikaamua kuipokea,…’akasema
‘Sitaki kuongea na mtu kwa hivi sasa, …’nikasema huku nikiizima kabisa hiyo simu.
‘Sasa sisi tunakushauri urejee nyumbani kwako, usije kutuletea matatizo mengine..’akasema huyo jamaa aliyenisaidia na Yule mshauri wangu wa kidini akasema;
‘Ni kweli, unatakiwa upambane na matatizo yako wewe mwenyewe, na kamwe usiyakimbie matatizo yako, kumbuka hilo..na kwa vile ulishaanza ni muhimu sana kwako kukamilisha kazi uliyokwisha kuianza kama kweli una nia njema, ni ngumu na huenda ukaingia matatani, lakini …baada ya dhiki huwa inakuja faraja kama nia yako ilikuwa kama ulivyoniambia…’akasema huyo mtu wa dini..
‘Nia ilikuwa hivyo, lakini..hapana, na leo kama nikirudi huko sizani kama kutakuwa na usalama,sizani kama nitaweza kujizuia, ni lazima nitaua tena, sitaki kabisa kurudi huko…’nikasema.
‘Kuua tena…! Hapana, wewe sio Mungu,…nakusihi, ichunge nafsi yako isikutawale, kama utaiachia nafsi yako ikutawale, hutafanikiwa,…
‘Sasa ni hivi nimeongea na huyu jamaa rafiki yako , yeye anaweza kukuhifadhi hapa kwake kwa hii leo. Iwe hii leo tu, lakini kesho ni bora urudi kwako ukapambane na mambo yako…’akasema huyo jamaa baada ya kunielewa.
Basi siku hiyo nikalala hapo hadi asubuhi, mtu tajiri mwenye nyumba zake, mali, leo naishi kwa ufadhili..!
Hatimaye kukapambazuka, na mambo yakaanza…
NB: Je mambo gani hayo yalianza
WAZO LA LEO: Kuyakimbia matatizo yako mwenyewe sio suluhisho la matatizo hayo. Wapo watu wanazikimbia hadi familia zao eti kwa vile maisha ni magumu, kuna wengine wanakimbia eneo walilokuwa wakiishi au kufanyia kazi kwa vile wamefanya makosa, je hilo ndilo suluhisho la tatizo, je ukifanya hivyo ndio tatizo limekwisha…

No comments :