Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeFriday, July 15, 2016

TOBA YA KWELI-5


  'Je kweli una uhakika,..utaweza kunisamehe mume wangu....?’ akaniuliza tena mke wangu na hapo nikatulia nikiwaza, ni kwanini mke wangu aniulize hilo swali mara mbili, ana nini, kuna nini alifanya, hapo nikamtupia jicho,nilimuona bado machoni kuna machozi, nikasema;

‘Mke wangu mbona huniamini…?’nikasema kwa kumuuliza

‘Kwasababu nakufahamu sana mume wangu…’akasema

‘Hata mimi nakufahamu sana mke wangu, wewe ni mcha mungu, na ukitenda kosa itakuwa ni bahati mbaya sana….’nikasema na hapo mke wangu akainamisha kichwa chini kama anamtiii bwana wake, akawa kafanya vile kwa muda kidogo…

Nilianza kuhisi mashaka, lakini nikajipa matumaini , nikijua kua mke wangu hawezi kufanya madhambi yoyote, kwa jinsi nimjuavyo, haiwezekani, nikataka kusema neno lakini kabla sijasema yeye akaanza kuongea…

Tuendelee na kisa chetu

*********************

'Mume wangu unakumbuka ile mimba iliyoharibika miaka kumi iliyopita,...?’ mke wangu akaanza kuniuliza hivyo, na mimi nikatikisa kichwa kukubali, huku nikivuta kumbukumbu za tukio hilo,

 Kiukweli ni tukio ambalo liliniumiza sana, siku hiyo nililia…utafikiri mtoto alishazaliwa na kukua, halafu akafa….nililia mpaka mke wangu akanionea huruma sana….sikuamini,…siku hiyo ilikuwa moja ya siku ambayo sitaisahau maishani.

‘Mume wangu usilie, haya yote ni mapenzi ya mungu….’aliniambia mke wangu.

‘Lakini kwanini, …mungu wangu kwanini, tunahitaji mtoto, tumekaa sana, kila mtu amekuwa akituuliza nyie vipi mbona hamzai..sasa bahati imekuja, ..halafu ndio hii imeondoka, inaniuma sana mke wangu..’nilisema.

‘Tumuombe mungu,…atatujalia tena, tutapata mwingine…’akasema mke wangu.
Kiukweli ilipita muda nikiwa sina raha, na siku zikapita, nikitrajia itashika mimba nyingine, lakini haikuwa hivyo …na mke wangu akawa anaumwa umwa sana,….akaanza kukonda, nikampeleka hospitali, akapimwa, na docta alikuja kuniambia mke wangu anahitajika kusafishwa kizazi.

‘Kwanini kusafishwa kizazi kwani kuna nini, je kizazi kipo salama, ataweza kuzaa tena….?’ Nilimuuliza docta

‘Ni kawaida tu, mimba iliyoharibika imeacha uchafu, ….ni jambo la kawaida…usijali kizazi kipo salama…’alisema docta. Na tendo hilo lilipita, na siku zikaenda, lakini haikutokea mke wangu kushika mimba, na mimi nikaanza kuumwa, kupimwa nina kisukari,…sijakaa sawa, shinikizo la damu, mara matatizo ya moyo..ndio katika kuhangaika, nikaja na agizo hili la kutubu;

                                                *********
Mke wangu akasema;

‘Ni miaka mingi sana, lakini mimi kila siku nahisi ni juzi, maumivu yale bado yananiandama hadi hii leo….kila muda unaopita tukio hilo linakuwa kama lilitokea jana, ….linanitesa sana…’akasema mke wangu

‘Oh, mke wangu….Lakini hayo yalishapita mke wangu sio kosa lako au sio..?,  hayo ni mapenzi ya mungu, mungu hakupenda tupate mtoto kwa muda huo,…ndio maana nahangaika,..’nikasema na mke wangu akatikisa kichwa kwa kusikitika.

‘Unajua mke wangu nilipogundua kuwa wewe huna tatizo, kizazi kipo, nilijipa matumaini kuwa ipo siku…ipo siku tutapata mtoto tu,…unaona… ,..ndio maana unaniona, nahangaika, yote haya nia yangu ni sisi tupate mtoto..eeh, labda tungesema tatizo ni mimi, lakini hapana docta kasema matatizo yangu hayanizuii mimi kupata mtoto na hiki kisukari na presha vitakwisha tu….’nikasema

'Ni kweli mume wangu, hata mimi nasema hivyo hivyo kuwa hayo yaliyotokea ni mapenzi ya mungu, lakini mbona ndani ya nafsi yangu haitaki kuikubali hiyo hali kuwa kweli hayo yalikuwa ni mapenzi ya mungu…’akasema mke wangu kama ananiuliza

‘Kwasababu wewe kama ilivyo mimi tunahitajika kupata mtoto au sio,…lakini muda unapita hatupati, kikawaida nafsi itajiuliza…lakini docta mwenyewe alisema hatuna matatizo, sasa tatizo ni nini, unaonaeeh, ndio maana hata aliponiambia huyo mkuu wa dini kuwa nikitubu dhambi zangu, itakuwa ni dawa, nikakubaliana naye, unaona mke wangu...’ nikasema

‘Ni kweli..lakini kwa vipi…?’ akasema mke wangu kama ananiuliza huku akijikuna kichwa kwa nguvu kama kinawasha.

‘Kwa vipi! Aah mke wangu,, ….ni hivyo hivyo kama nilivyoambiwa kuwa kwanza tutubu madhambi yetu, tuwasamehe waliotukosea, halafu tumuombe mungu, huku tukihangaikia na dawa, tutafanikiwa tu,…yule mkuu wa imani aliniambia matatizo mengine yanatokana na madhambi yetu, aah, madhambi yangu maana wewe mke wangu huna kosa, huna kosa kabisa…’nikasema

‘Hapo hapo….ndio maana na mimi nikaliwazia hilo, nikaona haya yaliyonitokea mimi, ili nafsi yangu itulie, yanibidi na mimi nitubu, bila ya toba ya kweli, sizani kama roho yangu itatulia, najua huenda uhai si kitu kwangu, lakini siwezi kwenda hivi hivi huku nikiwa nimebeba mzigo huu...'akasema mke wangu huku akilia.

‘Lakini mke wangu kwani vipi…?’ nikamuuliza swali kama lile aliloniuliza yeye, na taratibu mke wangu akainua kichwa na kuniangalia, machoni alionyesha huruma sana, nikata kusimama na kwenda kumpa pambaja, lakini mwili ukawa mnzito, sijui kwanini.

Mke wangu kwa muda ule alikuwa kakaa kwenye kiti cha kawaida na mimi nilikuwa nimekaa kwenye sofa, kwani yeye nilimkatiza kwenye shughuli zake, na alikaa tu kwa vile mimi nimemuita, sasa alipotamka hayo, akainuka kwenye kiti, na mara akaja pale nilipokaa kwenye sofa, na kunipigia magoti, huku akisema anaomba msamaha kwa kosa alilolifanya…
Kwanza nilibaki nimeduwaa, sikuelewa anamaanisha nini. Baadaye nikainama nikitaka kumuinua huku nikisema;

‘Mke wangu haina haja ya kunipigia magoti…mimi nimeshakusamehe..haina haja, unanipigia magoti wakati mimi ni mchafu…sistahili kufanyiwa hivyo, mke wangu inuka,….niamini mimi…’nikasema na hapo mke wangu akiwa bado kapiga magoti, akasema;

‘Mume wangu,…sina budi nikuambie kila kitu, najua sina muda zaidi..lakini ni haki yako kujua….’ Akasema na mimi akilini nikawa najiuliza ‘kujua nini, anataka nijue nini…labda, ni kuhusu ..hapana, mke wangu hawezi kunificha kitu, hana tatizo..’ hayo mawazo yalipita kichwani haraka sana,

‘Mume wangu tatizo linaloniumiza mimi ni kuhusu ile mimba iliyoharibika…’akasema na kutulia na kabla sijasema kitu akaendelea kusema;

‘Kuharibika kwa ile mimba imekuwa ndio sababu ya haya yote, na huenda….ni adhabu mungu kanipatia,…’akasema na mimi nikamwangalia mke wangu, kuna kitu kilipiga moyo paah, lakini nikakitupilia mbali, nikasema;

‘Hapana mke wangu sio kweli…hiyo sio adhabu, kama ni adhabu ni mimi ninayestahiki, sio wewe, huna kosa mke wangu, amini usiamini tatizo ni mimi…’nikasema.

‘Mume wangu unajua ile mimba haikutoka yenyewe…’akasema mke wangu na akaniangalia mara moja halafu akainamisha kichwa chini.

‘Haikutoka yenyewe, unataka kusema nini..?’ nikauliza, ni kama sikusikia vyema, na akili haikutaka kufikiria vingine nikasema;

‘Najua haikuharibika yenyewe, …yawezekana ni kutokana na mihangaiko, ulikuwa unafanya kazi sana, huku unaumwa kila siku, nilikuambia utulie..ukawa hunisikii ulibadilika ukawa mgeni kabisa kwangu..nilijua tu ni mabadiliko kutokana na uja uzito…! 
Lakini huo sio muda wa kulaumiana kwa hilo, hayo yameshapita au sio mke wangu..’nikasema.

Mke wangu akatikisa kichwa kama kulikataa hilo, akasema;

‘Mume wangu, ilimradi nimeamua kulifanya hili, kuwa nikuambie kila kitu, nitafanya hivyo kwa vyovyote iwavyo na iwe…nitakuambia ukweli wote,….hicho kilichotokea sivyo kama unavyofikiria wewe…’akasema mke wangu

‘Kufikiria vipi….?’ Nikamuuliza

‘Kuwa hiyo mimba iliharibika yenyewe,…sio kweli, ile mimba ni mimi niliamua kuitoa baada ya kushindwa kuvumilia ….’akasema.

‘Nini….mke wangu, unajua unachokisema…! Mke wangu najua mimba ile ilikutesa sana,..ulikuwa kila siku unaumwa, …sasa labda mimi nahisi, wewe unahisi labda katika kuteseka huko kuumwa labda ndio ..kulisababisha iliharibika kihivyo,..hapana,.hiyo mimba iliharibika kwa vile haikupangwa iwepo, niamini mke wangu….’nikamwambia.

‘Mume wangu…hiki ninachokuambia sasa hivi ndio sahihi, ya kuwa ni mimi niliitoa hiyo mimba kwa makusudi,…’akasema na mimi nikashtuka, nikataka kusema neno lakini mke wangu hakunipatia nafasi akasema

‘Mimi niliamua kufanya hivyo kwasababu niliogopa,…’akatulia

‘Mume wangu,..nilifanya makosa makubwa sana…najuta sana,…niliogopa kkubakia na hiyo mimba, halafu nikijifungua ugundue hilo kosa, moyo ulikuwa ukanisuta, nisingeliweza, na hata wewe usingeliweza, ninakufahamu sana mume wangu , ….’akasema na mimi hapo nikashikwa na kigugumizi.

‘Sikuelewi mke wangu…’nikasema sasa nikihisi mwili ukinisisimuka…nahisi kuna jambo linakuja, nikatuliza kichwa, akili haitaki kuamini…hapana, hapana ..haiwezekani…!

‘Damu yake ni kali sana mume wangu , kiushahidi, nilijionea na ..hata watoto wake wote unawaona walivyo, wanafanana na yeye kabisa,…’akasema

Hapo nikarudisha kichwa nyuma, ni kama nimezabwa kofi la kushitukiziwa, nikataka akili itulia, lakini nilihisi kitu kikianza kuchemka, sikuweza kusema neno, nikabakia kimia na mke wangu akaendelea kusema.

‘Huyu mtu..aliamua kutumia utaalamu wake vibaya, lakini sio kosa lake, ni mimi..mwishowe niliamua na mimi,..nijaribu…sasa tatizo ni kuwa kila mtoto aliyemzaa alikuwa kifanana na yeye…’akasema

‘Mke wangu unajua nini unachokisema, upo sawa kweli wewe..?’ nikamuuliza

‘Ni kweli…nilijua hata mimi huyo mtoto kama ningeliweza kuvumilia nikamzaa atakuwa akifanana na yeye...'akasema na mimi hapo nikatikisa kichwa, sikutaka kusikia hayo, sikutarajia hayo,

Unajua nilianza kubadilika,…moyo wa kiimani, moyo wa subira ambao alishanijenga Yule mtu wa imani, ulianza kuyeyuka…nikaanza kuhisi mwili ukinichemka, ilikuwa kama mtu kanisindilia kisu kifuani, nilihisi maumivu, mdomo ukanikauka,..macho yakanitoka…

 Kuna jambo jingine ambalo sikukuelezea kuhusu mimi, ..mimi nina wivu sana, na nikihisi wivu mwili mnzima unanisisimuka na damu hunichemka, na ole wako uwe unahusika …., naweza kukufanya kitu kibaya sana…ogopa nikibadilika, ogopa shetani mbaya akiniingia akilini, huwezi kuamini kuwa ni mimi….

'Unasema nini..?' nikamuuliza mke wangu na sauti hiyo ilimshtua mke wangu, akainua kichwa kuniangalia, macho yake yalijaa huruma, na machozi tele, huruma ilinijaa, japokuwa kuna kitu kilishaanza kuuharibu ubongo wangu, nafsi yangu ya siri, ilishaingiliwa…, tofauti na nilivyodhania awali…

Nilijaribu, na kujaribu kuirejesha ile hali, lakini…ooh, …hata hivyo kwa vile nilishasema nitamsamehe, nikajikausha na kujifanya ninatabasamu, tabasamu la kuigiza.

'Tatizo ni rafiki yako, rafiki yako sijui ana nini..nilijitahidi sana kujizuia, lakini siku hiyo nilishindwa, akanishawishi, akisema tufanye majaribio …..’hapo akatulia

‘Mhh, mke wangu sijakuelewa, ni nani huyo rafiki yangu…?’ nikamuuliza nikijaribu kujituliza.

‘Ukumbuke mume wangu ulisema utanisamehe…’nikasema

‘Ni..na..nataka unieleze ukweli wote…’hapo nikasema nikijaribu kuizuia hasira. Na mke wangu akashutuka kwa jinsi alivyoniona nilivyobadilika usoni. Akasema;

‘Rafiki yako,..yeye anapendwa sana na wakina mama, sijui kwanini, na mimi sikufanya kwa jili hiyo, ila nilitaka kuhakikisha, je nisamehe tu mume wangu....na shetani alinipanda, kwa vile ...nikaona nijaribu nione,..mtoto akizaliwa si wetu itakuwa siri yangu, kwanza tumekaa muda hatupati mtoto,...’akasema

‘Mhh..mke wangu unauhakika na unachokisema….?’ Nikamuuliza sasa nikiwa sina utani, nilishajua mambo sasa yameharibika, sijui kama nitaweza kuvumilia.

‘Ninatubu haya mbele yako mume wangu nisamehe sana, ..nilipanga iwe siri yangu, nilipanga nife nayo, lakini kwa vile umeniahidi kuwa utanisamehe ndio maana nimeamua kukuambia, ili hata nikiondoka niondoke kwa amani….’akasema

‘Uondoke kwenda wapi…?’ nikauliza sasa kwa sauti ambayo ukiisikia , kwa wale wanaonijua , wanajua sasa kitakachofuata ni damu kumwagika.

‘Mume wangu,..uliniahidi ukumbuke..’akasema mke wangu.

‘Nataka kusikia kila kitu…siamini , siamini…wewe…wewe, kwanini hukuniambia, kwanini….hapana,…hapanaaah’nikasema kwa ukali.

‘Mimi nitakwambia na …nipo tayari kwa lolote utakalonifanyia, maana najua nilikosea,…’akasema mke wangu sasa akiwa kaka chini kabisa, nahisi nguvu zilimuishia.

‘Ile mimba niliamua niitoe, …japokuwa tulihitajia mtoto…’akasema.

‘Ina maana ile mimba ilikuwa sio ya kwangu…?’ nikauliza kwa ukali.

‘Mume wangu ilikuwa ni bahati mbaya sana na wala sijui ilikuwaje,..sijawahi kunywa, lakini siku hiyo nilikuwa kama nimelewa, sijui ni nani alinilewesha, nilijikuta nikifanya kila alichoniambia…’akasema

Hapo nikasimama…nikashika kichwa, nikaruka ruka…halafu nikamkazia macho mke wangu na kusema;

‘Acha uwongo, toka lini ukanywa pombe wewe…ina maana ulijifanya hivyo ili kutimiza matakwa yako na hawara yako, na ninani huyo rafiki yangu, maana sijui kama ananifahamu vyema, sijui..atakimbilia wapi, sijui…sijui, ni nani huyo ni nani huyo….’nikawa sasa nimebadilika, sio mimi tena, ogopa nikiwa kwenye hiyo hali…

‘Ni kweli mume wangu haya ninayokueleza ndivyo ilivyokuwa,…nitakueleza kila kitu na wewe unifanye upendavyo, maana nastahiki kaudhibiwa, nilikukosea sana mume wangu…najua ulishaamua kufanya toba, na nilijua upo tayari kusamehe, kama ulivyosamehewa….’akasema na mimi nikamwangalia huku mwili ukinitetemeka.

‘Kusamehe…unasema nini…mke wangu mwenyewe..hapana, ..ni nani huyo rafiki yangu..’nikageuka kuangalia mlangoni kama vile huyo jamaa atatokea.

‘Mume wangu,…sijui kwanini nilifanya hivyo, …siku nilipogundua tu nina mimba nikajua sio ya kwako,….’akasema na mimi nikataka kusema neno lakini nikashindwa, sauti ilikuwa haitoki,…

‘Nikajitahidi sana kujizuia na kuamini kuwa, sio kweli, sina mimba, lakini baadaye ndio  ….nikaja kukuambia kuwa nina mimba, na wewe ukafurahia sana,….furaha yako iliniuma sana, maana nilijua sio mimba yako, nikajitahidi sana kujikausha lakini kiukweli sikueweza…’akasema.

‘Siku baada ya siku nikawa naumia,..mawazo, kujuta ilikuwa kama kisu kilichokuwa kikinichoma tumboni…sikujua lini maaumivu hayo yangeliisha, nikawa naumia, Napata maumivu makali kila siku ya mungu inayopita…ndio maana muda wote uliniona nikiumwa…’akatulia.

‘Ikafika muda sikuweza tena kuvumilia…’akasema

‘Na zaidi kuna mwanamke mmoja alitembea naye, akajifungua mtoto,…oh, nilipokwenda kumuona, huwezi amini, alifanana kila kitu na ..na ..huyo rafiki yako…’akatulia
Mwanamke mwingine naye ilikuwa hivyo hivyo, na watatu ilipotokea hivyo nikajua, …hii haitaweza kuwa siri tena….’akatulia.

‘Waume wa hao wanawake walipogundua …na …walichokifanya kwa wake zao….kilifanya nizidi kuogopa…’akatulia.

‘Nakupenda sana mume wangu….ni hivyo tu, sasa mume wangu…, uamuzi ni wako…kuniua, sawa..hata hivyo nimeshjifia sitamani kuishi….mateso ninayopata natamani ….oh, mume wangu nisamehe…’akasema

‘Sikuelewi….’nikasema sasa nikimsogelea,..nilishabadilika, nilishakuwa sio mimi tena.

‘Unataka niseme nini zaidi mume wangu…siwezi, naumia,….niache nipumzike, hapa mwili hauna nguvu tena…lakini mume wangu ulisamehewa,..na wewe jifunze kusamehe…’akasema mke wangu hapo akanichefua, nikamsogelea na mikono ikakamata shingo yake.

‘Nitakuua….yaani wewe ndio umenifanyia hivyo…’nikasema huku mikono imeshikilia shingoni, niliona ulimi ukimtoka, lakini akili haikuwa yangu tena..haikupita muda mke wangu akalegea, na kulembemka sakafuni, kimiaa, sikujua kama nimemkaba sana, nilipogundua hilo nikashutuka, akili ikaanza kunirejea, nikagundua kuwa nimefanya kosa, nikainama;

‘Mke wangu..mke wangu…usife ..hatujamalizana, usife…usife…’nikaanza kulia, nilipoona mke wangu kweli hainuki, nikapeleka sikio puani kwa mkewe wangu kusikilizia, kimiaah, mwili wangu ukaisha nguvu, magoti yakaanza kugongana.

Mara nikasikia mlango unagongwa…hapo nikajua sasa nimeumbuka,sasa naenda jela, akilini nikawa najuta, nikaijutia hasira , huku naangalia mlangoni nikijiuliza ni nani huyo aliyegonga mlango….bila kufikiria zaidi, nikambeba mke wangu begani nikaingia naye chumbani nikamlaza kitandani, haraka nikatoka chumbani, huku nikihakikisha kuwa nimefunga mlango wa chumbani.

Nilipotupa macho mlango huo wa kutoka nje, nikaukuta upo wazi, mwili ukaanza kusisimukwa, huku nikijiuliza jinsi gani mlango ulivyofunguliwa maana huo mlango ukijifunga, ukiwa umefungwa mpaka mtu wa ndani akufungulie, labda uwe na ufunguo.
Nikaduwaa…ina maana kuna mtu kaingia..ni nani, na kasikia nini….

Sauti ya kuhema ikasikika nyuma yangu, nikahisi vinywele vya mili vikinisisimuka, na hali hiyo kwangu inaashiria hatari…kwa hali kama mimi inakuwa ni kama vile nipo  vitani, kila kitu karibu yako ni adui, nikawa nageuza kichwa taratibu kwa tahadhari kuangalia wapi sauti hiyo ilipotokea…

‘Najua kila kitu…’ilikuwa sauti iliyonifanya moyo wangu ulipuke,….nikahisi mwili ukinisisimuka, nikatetemeka, …unajua kutetemeka,

Sio kuetetemekakwa uwoga, ni kutetemeka kwa hasira, mikono inataka kukamata mwili,…misuli imekakamaa.. wanaonijua waulize, nikifikia hapo kinachoweza kuituliza hiyo hali,sijui ….ni kitendo cha kuumiza, kuua, nilifukuzwa jeshini kwa hali hiyo…!
Naishia hapa kwa leo ….

NB: WAZO LA LEO: Tabia nyingine ukiziendekeza mwilini, zinaweza kuwa ni ugonjwa,…hasira, uwoga,…visirani, kuteta, umbeya..nk, haya hujijenga taratibu, na mwisho wake inakuwa ni donda ndugu. Tabia nyingine pia huweza hata kuathiri maumbile, …ukawa tofauti na jinsia yako, hii ni kasumba, ambayo mtu hujijengea mwenyewe..ndugu zanguni tujihadhari na tabia hizi, na tujaribu kuwakwepesha watoto wetu na tabia hizi.

Ewe mwenyezimungu tujalie sisi na vizazi vyetu kujizuia na kukwepe tabia zenye kuja kuleta madhara katika maisha yetu,…tupe afya njema tabia njema na riziki za halali..amini. 
Ni mimi: emu-three

No comments :