Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeWednesday, July 13, 2016

TOBA YA KWELI-4


‘Ina maana kweli uliwahi kuua…?

‘Je na hilo ulitubu, ulitubu kwa nani sasa….?

Ni maswali niliyomuuliza , na hapa anaendelea kusimulia…..

                                  ************

‘Unataka nifungwe….hapana, hilo la kuua, nilimuachia mungu,maana kitendo hicho kilifanywa na wenzangu, mimi nilishirikishwa tu, maana na mimi muda huo nilikuwa natafuta, natafuta mali, natafuta utajiri. Nilijua mali na utajiri ni kila kitu, lakini nikuambie ukweli, hivyo ndio kila mtu anavitaka, lakini mali ya haramu, haina usalama moyoni, asikudanganye mtu…’akatulia kidogo halafu akasema

‘Kwahiyo kweli uliua kwa ajili ya kupata mali..?’ nikamuuliza tena.

‘Hilo swala..hapana, tuliache tu, siwezi kulihadithia lote….lakini sikuliacha hivi hivi, nilikwenda kwa wanafamilia tuliowakosea, na mimi nikawaelezea ilivyokuwa…unajua tena kwenye udhia tumbukiza rupia..na mengine tukamuchia mungu..lakini, nisamehe kwa hilo, siwezi kuliezea zaidi kwako…’akasema

‘Mhh..hapo sizani kama ulitubu kisawasawa, kama ndivyo ulivyoelekezwa na huyo kiongozi wako wa imani…, uliambiwa useme kila kitu kwa wahusika,je uliwambia kila kitu, wakakusamehe….?’nikamuuliza na akakunja uso kama hataki kuliongelea hilo, na nilipoona hivyo nikasema

‘Sawa nimekuelewa…’nikasema

‘Hilo…siwezi…maana hata haya nimekuambia tu kwa vile wewe ni rafiki yangu lakini ninaumia sana….unajua kuumia..ninateseka, sijui kama kuna mtu atanielewa….’jamaa yangu akasema huku akitikisa kichwa na alipotaka kutamka jambo jingine nikamuwahi na kusema;

‘Hilo tuliache tu…nimekuelewa rafiki yangu…, turejee kwa mkeo, maana hapa ndio naona kuna ngoma ya kucheza, mlimalizanaje na mkeo, je alikusamehe…?’ nikamuuliza

 ‘Rafiki yangu, kuna kitu nikuambie, wake zetu, mungu kawajalia sana…ni wepesi sana kusahau na kusamehe..kama wasingekuwa na uthibiti huo…sijui kama wangeliweza kuzaa tena….nitalihakikisha hili kwenye hiki kisa..utajionea mwenyewe…’akasema

 Kiukweli kutokana na yale niliyomwambia mke wangu, siku hiyo nilijua kabisa…mke wangu hataweza kunisamehe..maana ilifiki mahali akagoma kunisikiliza mpaka nikaona basi tena, kama hataki nifanyeje, lakini haraka nikakumbuka jambo…

‘Mke wangu nimekuambia, yote hayo ya kutembea na ….mdogo wako, binti wa kazi, na…yule yatima…na …na…’nikasita na mke wangu akageuka na kuniangalia kwa jicho baya, na kusema;

‘Sizani kama mungu atakusamehe kwa hayo, yaani hata siamini…haya umenielezea hayo kwa nia ya kuniomba mimi msamaha, je hao uliowatendea,tuachie mbali mdogo wangu maana kama ulivyosema wewe na yeye mlikubaliana, mkiwa na malengo yenu…je mimi…mliyenidhulumu,…je mimi ..oh,… ulikubaliana na mimi kuhusu hilo…hapana..

‘Haya tuche mimi, maana…oh…je huyo binti yatima, uliyeudhulumu utu wake, ukamdhalilisha kabla ya ndoa, ulikwenda kumuomba msamaha, akakukubalia ….usiniambie ulikwenda ukamhonga tena, ndio akasema amekusamehe, najua naweza lakini kumbuka muda ule wakati unamdhalilisha, alisononeka kiasi gani, sizani kama unaweza kuilipia ile hali…’akasema

‘Mke wangu usinione hivi, ..nilumia sana, baada ya lile tendo, nililia sana…huwezi amini, lakini yalishafanyika, sasa nifanyeje..ndio maana natubu,…nimemtaka mwenyezi mungu msamaha, na hao nimekutana nao, ..huwezi amini mke wangu…’nikatulia

‘Nilienda mguu kwa mguu kwa kila mmoja wao, nimeongea nao, nimewaomba msamaha..ni kweli, ….ilibidi nifanye chochote cha kuwaliwaza, huyo binti yatima keshaolewa, lakini nilifanya chochote cha ..kumliwaza…nashkuru sana kuwa alinielewa, akanisamehe…’nikasema

‘Ama kwa mdogo wako naye ana mume wake kwa sasa, mwanzoni hakutaka hata kuongea naye, kwani alisema nilimuhadaa..ni kweli nilimuahidi kuwa nitamuoa kama akishika mimba, lakini.anyway, tuyaache hayo nisamehe tu mke wangu,..’nikasema

‘Mke wangu unajua kwa vile wote niliowatendea hiyo dhambi sasa wana waume zao, haikuwa kazi ngumu kwao kunisamehe..tatizo ilikuwa huyo mke wa jirani, bado kidogo..anasema we tu yaache tu haeleweki…’nikamwambia mke wangu.

‘Mke wa jirani yupi huyo…?’ akaniuliza

‘Mke wangu hayo ya kwao naona tuyaache, lakini ninachotaka kukuambia ni kuwa lengo langu lilikuwa ni mtoto, kuachia hayo mambo mengine ya kimaisha, je mke wangu wewe hutaki tupate mtoto, niambie ukweli..hutaki mtoto?’ nikamuuliza

‘Swali langu , je una uhakika gani kuwa ukifanya hayo yote utapata mtoto…..?’ akaniuliza

‘Una maana wewe humuamini mungu…?’ nikamuuliza

‘Sijasema simuamini mungu..lakini …’akasita na mimi sikutaka kumchelewesha nikamwmbia;

‘Mke wangu, usihofu kabisa, niliongea na kiongozi wetu wa dini, si unamfahamu alivyo, akikuambia jambo, ufanye…eeh,  ukifanya kama alivyokuelekeza mara nyingi wengi wamefanikiwa…yeye ana makarama yake…’ nikamwambia na mke wangu akatikisa kichwa kama kukataa, na mimi nikasema;

‘Mke wangu wewe ni mcha mungu, nikuulize ukiwa na tatizo ukataka kurejea kwa mola wako akusaidie kwanza unafanya nini…?’ nikamuuliza. 

‘Najua ..hilo, kuwa kwanza unatakiwa utangulize toba, uombe msamaha kwa yale uliyoyakosa…utubu madhambi yako…na pia na wewe uwasamehe waliokukosea, ili moyo wako uwe safi, ndio tena uanza kuomba..lakini, swali langu ni je uliowakosea una uhakika gani kuwa kweli wamekusamehe..na je umeangalia ukweli wa hicho unachokitaka, kuwa kweli kinawezekana…?’ akaniuliza

‘Mke wangu mbona leo waonyesha kuwa na mashaka na imani yako ya dini, wewe mara nyingi mambo yako unayafanya kwa kumtegemea mungu..vipi leo unalitilia mashaka hili..?’ nikamuuliza na mke wangu akainamisha kichwa chini kama anawaza jambo, nikahisi kuna tatizo, ..na nahisi hajaweza kunisamehe kiukweli moyoni mwake.

Kiukweli mke wangu alikuwa mcha mungu sana, kwani hata yeye hayo matatizo yetu yalikuwa yakimuumiza sana, aliweza kuamuka usiku na kumuomba mungu, akikesha kwa kuswali.. alikuwa akifunga,..na kushiriki kwenye ibada mbali mbali, kusaidia mayatima, …

Nilijua pamoja na matatizo mengine lakini lakini hilo la mtoto lilikuwa kipaumbele kwake pia, hebu fikiria tuna miaka kumi sasa tupo naye na hatujajaliwa kupata mtoto, mali tulikuwa nayo lakini hatukuwa na raha nayo, ....unajua,..kama nilivyosema mali ninayo lakini siwezi kuitumia, nina kisukari, nina presha,....ugonjwa wa moyo, hayo kwa uchache...nitaitumiaje hiyo mali, naiangalia tu...'akasema rafiki yangu.

‘Pole sana…’nikasema

 Kwakweli Mke wangu baada ya kuwaza sana, baada ya kutulia sana, akanielewa, na kusema ni sawa;

‘Mume wangu, tumetoka mbali, pamoja na …ubaya ulionifanyia, lakini..nitafanyaje, wewe ni mume wangu, na tunahitajika kuwa pamoja kwa kila jambo, japokuwa wewe uliamua kufanya mambo mengine kivyako,..na matokea yake ndio haya, ni kweli madhambi huzaa matatizo, na mola anatujaribu ili tuweze kutubia na kumrejea yeye…’akasema mke wangu na mimi hapo nikapumua

‘Kwahiyo umenisamehe mke wangu..?’ nikamuuliza

Hutaamini mke wangu alisema kuwa kanisamehe ...

‘Mimi ninaweza kukusamehe mume wangu, na ninaweza ili tuyasahau yaliyopita na tuwe pamoja, tusaidiane…maana toba ni muhimu sana, na nimefurahi kuwa lile jambo ambalo mimi nimekuwa nikilifanya kwa muda mrefu, …la kuwa karibu na mungu, kumuomba msamaha..sasa wewe ndio umelianza..ni kweli mimi najua kabisa toba ya kweli ya kutoka moyoni hukubaliwa na mola wako…lakini iwe sio kwa ajili ya….’akatulia

‘Ni mkuu wa imani kanishauri na mimi yakaniingia, ..ndio mwanzo huo…niamini mke wangu…’nikasema

‘Sawa mume wangu, sasa mimi sijui,…. maana nionavyo wewe lengo lako ni kupata, hutubu kwasababu umekosa,au sio…hapo nina mashaka,..je usipopata, utasemaje, utarejea kwenye dimwbi la maasi…?’ akaniuliza

‘Hapana mke wangu, lengo langu ni kuwa msafi,..nataka maisha yetu yabadilike, lakini wewe unalionaje hili, tumehangaioka wewe, kizazi chaki hakina matatizo na mimi tatizo ni hiki kisukari na presha,ndio vimelete huu udhaifu, vikiisha mambo yatakuwa safi..lakini haya yanatakiwa tuwe pamoja au sio..’nikasema

‘Mhh…’mke wangu akakubali kwa kutikisa kichwa.

‘Mke wangu wewe hulioni hili,..tukiwa hivi peke yetu huoni kuna walakini, ilitakiwa wawepo watoto karibu yetu, hilo ni moja ya ombi langu kwa mungu…kama huna tatizo na mimi, tatizo linaweza kuondoka..na shida sana au sio…ni haya madhambi tu, ninauhakika toba hii ikikamilika, kila kitu kitakuwa sawa…’nikasema

‘Mungu humuombi makosa yako kwa ajili ya kupata ….muombe makosa yako ili akusamehe, kupata sio dhima yako, hayo yapo kwenye mamlaka ya muumba,.yeye anaweza kukupa hata kama una madhambi, yeye anaweza kukupa kwa wasaa wake, kwa jinsi aonavyo ni sahihi, kutubu dhambi ni kitu muhimu …haya, lakini hayo tuyaache, maana sijui mumeongea nini na huyo mkuu wako wa imani..

‘Mimi nimekuelewa, na ..japokuwa nimeumia sana, lakini..sioni kwanini nisikusamehe,..’nikasimama nikitaka kumkumbatia mke wangu, lakini akaninyoshea mkono wa kunizuia akisema;

‘Ila kabla ya msamaha wangu, kabla ya kutoa kauli yangu ya kukusamehe, ..moyoni nimeshaamua hivyo, lakini kabla sijakutamkia ..maana na mimi ni binadamu kama wewe, na mimi nina makosa yangu, na mimi nahitajika kutubia kwako pia kama wewe ulivyofanya kwangu au sio...’akasema mke wangu.

`Kweli eeh mke wangu mbona itakuwa jambo jema’ nilimuambia mke wangu nikiwa na furaha tele moyoni, najua mke wangu ni mcha mungu haswa…, hana makosa makubwa kama yangu,..kwahiyo sikutarajia kubwa zaidi ya makosa madogo madogo.

Mke wangu aliposema hivyo, kwanza akainamisha kichwa chini, alikaa hivyo kwa muda, baadaye akainua kichwa, nilishangaa kuona mchozi yamejaa machoni mwake,…alikuwa akilia, kwanza nikashikwa na mshangao, lakini baadaye nikajua ni namna ya kwake ya kutubia. Mke wangu mara nyingi nilimfuma usiku akiwa katika ibada zake akilia..akimlilia mola wake…ndivyo alivyo..

Alipotulia, akaniangalia machoni na kusema;

'Mume wangu hili ninalotaka kukuambia niliapa kuwa sitakuambia, kwa vile ninakufahamu ulivyo… niliona iwe ni siri yangu ya moyoni mpaka kufa kwangu…, lakini kwa vile wewe umeanza, na kiukweli nimeona dhamira ya kweli ya kutoka moyoni mwako, ...sioni kwanini nisikuambie,sioni ni kwanini niendelee kuteseka maisha yangu yote..'akasema mke wangu.

‘Ninamuomba mola anisamehe …na namuomba mola siri hii isiwe siri tena, na nikiitamka iwe na heri …isije ikawa ni sababu, na kama…hutanisamehe..sijui..maana nilipata, sasa navunja kiapo hicho…kwa vile tu..nimeona una dhamira ya kweli…’akasema mke wangu

Kiukweli sikuwa na shaka yoyote dhidi ya mke wangu, nilimuamini, na usingeliweza kuniambia jambo lolote baya kumuhusu mke wangu nikakukubalia, mke wangu ni mcha mungu, mnyenyekevu…kila mtu mtaani anamsifia, sembuse mimi… hapo sikusita kusema;

'Niambie mke wangu, usiwe na shaka, mimi nitakusamehe, na tena nitafurahi sana, tukiwa hivi, mmoja akikosea , akimkosea mwenzake anamwambia, tunasameheana, mimi naona ni jambo jema sana,..na huenda mola akatusaidia tukaondokana na mashaka haya… na akatujalia tukapata familia,…mimi hilo la watoto ..mmmh, mke wangu, wewe niambie, sema yote na mimi nitakusemehe….'nikamwambia...

Mke wangu akaniuliza swali kwa mashaka,

'Je kweli mume wangu una uhakika,.kweli wewe nikujuavyo …kweli utaweza kunisamehe wewe....?' akaniuliza na mimi nikasita kidogo, na kumuangalia machoni mke wangu, nikijiuliza ni kitu gani hicho mke wangu anataka kuniambia ambacho anahisi sitaweza kumsamehe…sikusita kumwambia ,nikasema;

‘Mke wangu ina maana huaniamini…Usiwe na shaka mke wangu wewe niambie tu, hahaha, mke wangu, leo naona huaniamini, kama wewe umeweza kunisamehe kwa makosa hayo niliyokufanyia, kwanini mimi nishindwe kufanya hivyo….’nikasema.

Kabla mke wangu hajaanza kuniambia, nikuambie kidogo kunihusu mimi, mimi nina tabia ya ajabu sana, mimi pamoja na kuwa mpole sana kwa mke wangu, lakini nina tabia moja, ..hasira..huwa sijui ni kwanini, na nikikasirika naweza kufanya jambo ambalo huwezi amini..na kushuka kwa hasira yangu ni mpaka nikulipizie, nifanye jambo la kisasi..sijui ni hulka gani niliyojijengea.

Ndio maana mke wangu aliniuliza mara mbili,…

'Je kweli una uhakika,..utaweza kunisamehe mume wangu....?’ akaniuliza tena

NB: Tuishie hapa kwa leo…nilipanga tukimalize hiki kisa leo, lakini kuna maswala nataka kuyaweka sawa kwenye hitimisho la kisa hiki..ili tupate mafunzo sote…, sehemu ijayo inaweza kuwa hitimisho la kisa hiki,  ili tuendelee na kisa chetu cha `Yote mapenzi ya mungu…’
WAZO LA LEO: Ahadi ni deni…, wengi wetu ni wepesi sana kutamka maneno bila hata kufikiria au kuona athari zake mbeleni. Tunaweza kufanya hivyo tukiangalia masilahi zaidi, au tukitarajia kupata,…au kuwa na manufaa Fulani,  hata kama yale tunayoyatamka hatuna uhakika nayo. Tunajiapiza, tunakubali au hata kukataa wakati tunajua kauli hizo sio sahihi, ni kauli za kimasilahi zaidi..utasikia ndio nimekubali..naapa ni kweli, au sio mimi wakati kweli ni wewe uliyefanya…

Nawausia wenzangu na kujiusia mwenyewe kuwa tuache hizi kauli hasa zenye mfumo wa ahadi, tuwe makini nazo maana ukiahidi ujue hilo ni deni. Ewe mola wetu tunajua wewe ni mwingi wa kusamehe, tusamehe kwa yale tuliowahi kuahidi na tukashindwa kutekeleza, tusamehe kwa makosa ya ulimi, makosa ya kauli zetu ….aaminiNi mimi: emu-three

No comments :