Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Wednesday, May 11, 2016

YOTE NI MAPENZI YA MUNGU-5


Jamaa aliposikia nasema ;

‘Afande vipi…’ akajua kweli mimi sitanii, kwani nilimuona akiangalia muelekeo wa mlangoni, na kwa ile hali ni kama anataka kukimbia, na mimi nikasogea na kukaa mbele, kama kumkabili hivi, nikamwambia;

‘Rudi ukae tuongee,….’nikasema

‘Siwezi, mimi naondoka….’akasema na kabla hajamaliza mlango ukagongwa,…alistuka utafikiri alisikia mlio wa risasi, akageuka taratibu kuangalia tena mlangoni, na mara akaingia jamaa mmoja, kwa umbile huwezi kukosea ….sura na umbile ulionyesha kuwa huyo ni mtu wa usalama.

Jamaa kwanza akajikuna kichwani, halafu akageuka kuangalia dirishani akawa anasubiria, sijui sasa atachukua hatua gani,ataondoka au atasubiria….

                                  ***********

Huyu aliyeingia alikuwa mpelelezi wa polisi akiwa kavalia kiraia, na tukasalimiana naye, wakati huo jamaa alikuwa bado kasimama akishindwa kuamua kukaa au kuondoka, Yule mpelelezi akajitambulisha na kutoa kitambulisho chake, akamuonyeshea   jamaa…

Na jamaa akageuka kuniangalia akasema

‘Haya yote  , yana maana gani..?’ akaniuliza akimwangalia kwanza huyo mpelelezi  na halafu akageuka kuniangalia mimi, akawa anaashiria kwa mikono kumuonyesha huyo mpelelezi.

‘Mimi sijui…muulize yeye mwenyewe,…’nikasema

‘Mimi nimefika hapa kukufuata wewe, nilifika nyumbani kwako nikaambiwa haupo, nikaelekezwa kuwa huenda upo hapa….’akasema huyo mpelelezi akimwangalia huyo jamaa

‘Kuna nini kwani, nimefanya nini, …na ni nani  huyo kakuambia nipo hapa?’ akauliza maswali mengi kwa mfululuzo, kuonyesha jinsi gani hakulitazamia hilo.

‘Ni maswala machache  ya kujirizisha, …nilikuwa nataka kuulizia maswala yanayohusiana na kifo cha kaka yako…’jamaa kusikia hivyo, akashtuka kidogo…na akamgeukia huyo mpelelezi, na kusema;

‘Kuhusiana na kifo cha kaka yangu!?’ Akauliza kwa mshangao

‘Ndio….’akasema mpelelezi

‘Sielewi, maana kaka kafariki muda, iweje leo  ….kwani kuna nini kimetokea mpaka muanze kufuatilia, au mumegundua nini…?’ akauliza jamaa na sauti yake ilikuwa kama inatetemeka.

‘Usiogope,  ni maswali ya kawaida tu, ya kujirizisha kabla hatujafunga jalada lake…, hata kamamtu kafariki  zamani, inawezekana kukatokea kitu cha kutufanya tuchunguze, hata hivyo, jalada la kaka yako lilikuwa halijafungwa, ….’akasema

‘Ndio nauliza kuna nini cha zaidi, maana mnataka kutukumbusha ya zamani, na haya mkiongea na mjane, mtazidi kumtonesha…na kwa hali yake ilivyokuwa, naomba chonde, tusiyaongelee hapa, kama kuna jambo mumegundua….’akasema

‘Hapana…ni mambo ya kawaida tu,,…ni kweli kaka yako alifariki kwenye ajali ya gari, hilo halina shaka,..lakini kuna mambo bado tunahitajia kuyaweka sawa ili kumbukumbu zetu ziweze kuwa kamilifu…na sizani kama hata shemeji akiyasikia yatamuathiri kitu…yanaweza kumsaidia kutuliza moyo wake….kwahiyo usijali kwa hilo’akasema huyo mpelelezi.

‘Ok, ulitaka kujua nini, maana huyu naye ana maswali yake hata simuelewi, nashindwa hata….sasa sijui nianze na nani….?’ Akaniuliza na mimi nikabakia kimia tu

‘Uanze na nani kwa vipi…kwani….?’ akauliza huyo mpelelezi akiniangalia halafu akamuangalia huyo jamaa

‘Huyu si mwenzenu, hamjuani, au…?’ akawa kama anauliza na kuniangalia mimi kwa dharau fulani, na mimi nikawa kimia tu, sikusema kitu…

‘Ok, sawa…sio lazima tujuane, huenda anatokea kitengo kingine…’akasema huyo mpelelezi

‘Mhhh….naona sasa….’akasema jamaa

‘Kwani kakuuliza nini cha kukufanya uwe na mashaka na yeye..?’ akauliza

‘Unajua yeye nimemkuta hapa akiwa na shemeji yangu, na katika kuongea akaanza kuniuliza maswali, ambayo yamenifanya nimtilie mashaka, …’akasema na huyo mpelelezi akaniangalia  tena kama anataka kusema neno, lakini akaghairi, na mimi kwa muda huo nipo kimia tu!

‘Maswali ya namna gani, ….?’ Akamuuliza  huyo jamaa,

‘Aaah… muulize yeye mwenyewe,  eti haamini kuwa kaka anadaiwa benki , eti anahisi deni hilo ni la uwongo, sasa mimi sijui kwa vipi….. ‘akasema.
‘Ila wewe unaamini kuwa deni hilo lilikuwa ni kaka yako…?’ akaulizwa

‘Baada ya kujirizisha,….nilifuatilia nikaja kuona vielelezo, nikaamini, ….’akasema

‘Ok, ok, mimi sioni kwanini uwe na mashaka na yeye , wakati anachokifanya ni kusaidia jamii,….mimi nimemuelewa, sasa unaogopa kumuambia ukweli, wewe ukweli si unaujua, kwanini unaogopa kuusema…..?’ akaulizwa

‘Hapana sijaogopa…, lakini hili swala tulishaliongelea na wenzenu, kipindi cha mwanzo, …..baadaye wakatuelewa, baada ya kuona ushahidi wote kutoka benki, sasa huyu anakuja na jambo lile lile,…ndio maana simuelewi, na ananitia mashaka….’akasema

‘Unajua hayo maswala ya benki yana watu wake…mimi sihusiki huko, kwahiyo siwezi kuliingilia hilo, mimi nimekuja na mambo yangu,…kuhusu kifo cha kaka yako ambacho kimetokea kwasababu ya ajali, sasa nilitaka kukuuliza baadhi ya maswali, ambayo yaliachwa bila kupata majawabu…’akasema

‘Maswali gani hayo,…mbona mnataka kuturudisha nyuma,….tulishaanza kusahau machungu…’akasema kwa sauti ya huzuni.

‘Ni maswala ya kawaida…kwa jinsi ajali ilivyotokea na eneo lenyewe na  gari ….lakini kabla hatujaenda huko, je mumemalizana na huyu mtu wa jamii…?’ akaulizwa

‘Bado….naona bado,  mimi nilitaka kuelewa kabla hatujafika huko, huyu mtu kwanini asiende kuwauliza watu wa benki, kama ni mtu wenu lakini… , na kama sio mtu wenu, huoni kuwa anaweza kuwa ni tapeli…’akasita alipoona namwangalia, halafu akasema

‘Natumia neno hilo…tapeli, kwa maana yake sio kama namkashifu, unielewe, maana…, amekuja hapa kutaka kumghilibu shemeji, na sasa amesababisha hata mtoto kupatwa na matatizo na kwa kifupi sijamuelewa…’akasema. Mpelelezi akaniangalia akitaka kama anataka kuniuliza kitu  lakini nikaona anasita akamgeukia jamaa na kumwambia.

‘Sawa…..unaonaje akiwa anakuuliza hayo maswala,…si maswala ya deni  linahusiana na marehemu, au sio, hata mimi nitafurahi kuyasikia, ili tuone huo unaosema utapeli, umenielewa?’ akasema na jamaa akaonekana kunywea, na mpelelezi akasema

‘Hayo maswali, naona hata mimi yatanisaidia sana katika kufunga jalada la kaka yako, na huenda yakanisaidia kuhitimisha kile nilichokiona, na haki ikaweza kutendeka, kwa manufaa ya familia …sasa nikuulize wewe, kwani  kuna uzito gani, wewe si unatakiwa kusema ukweli unaoufahamu, au?’ akamuuliza.

‘Sijashindwa kuyajibu hayo maswali unielewe…ila sio kwa kila mtu…na mimi unielewe hapo…dunia sasa haiaminiki, kuna watu wajanja wajanja….ok,…sawa kama wewe umemuamini, haina shida,….’akasema
‘Kwahiyo upo tayari kuyajibu maswali yake…?’ akaulizwa

‘Hamna shida…, ndio nilikuwa nataka aniulize hayo maswali, lakini yaonekana hayo maswali mpaka yatoke mbinguni sijui…maana kila nikimwambia aniulize, ana….chelewesha, kwa visingizio mbali mbali, …mpaka namtilia mashaka, …na aheri wewe umetokea, ili umbane,kama ni tapeli awajibike…’akasema na mpelelezi akageuka mara moja kuniangalia, halafu akasema;

‘Basi mimi nipo tayari kusikiliza hayo mazungumzo yenu.., yeye aendelee kukuuliza ,mimi nitasikiliza na kama kuna maswali yatanigusa mimi kwa upande wangu, usiogope nikiingllia, na kukuuliza, au ….?’ Akauliza

‘Sawa,….haya uliza, …lakini wasi wasi wangu huyu ni nani….?’ Akakubali halafu tukashangaa anauliza tena.

‘Wewe usijali,…mimi nimeshamfahamu, kazi zake zinatusaidia hata sisi, wala sio tapeli….huyu ni mwanajamii…anaweza kukusaidia hata wewe…’akasema

‘Ok….kumbe mna kitengo cha namna hiyo siku hizi, haya….. lakini sioni kama kuna umhimu wa kuulizwa tena maswala hayo ya benki tulishamalizana na wenzenu, na benki… halafu,..ni kwanini mimi, unajua imefikia hatua ,mpaka najiuliza kwanini mniandama mimi hivi…ni kama vile mnanishuku, au hamuniamini au kuna nini kinaendelea, mimi hata sijui, matokea yake mnafanya hata mtoto anapata mateso  ‘ Akasema

‘Mtoto yupi…?’ akauliza askari huyo na kabla hajajibiwa akaendelea kusema ‘…..huyo mtoto  anapata mateso gani….na, yeye anahusikanaje na maswala hayo….?’ Akauliza mpelelezi na jamaa akasema

‘Najua huwezi kuamini, mpaka yakukute, hata mimi sikuwa nimeamini mambo haya….Kuna mambo ya mizimu ya baba yake,…..aah, eeh, lakini haina haja kukuambia, tutapoteza muda, na  huenda usielewe, kutokana na kazi zenu,….ila swala ni kwanini mnifuatilie mimi , mnanishuku nini mimi….?’ Akasema na kuuliza

‘Kwasababu tumeambiwa wewe ndiye uliyeachiwa majukumu yote ya hii familia, kweli si kweli…na tukajua wewe unajua kila kitu, au….?’ Yule mpelelezi akasema na kumuuliza halafu akageuka kuniangalia,  mimi, na mimi nikatikisa kichwa kukubaliana naye

‘Haya …niulizeni hayo maswali, mimi sina wasi wasi kwa hilo,  ….kwasababu sio mara ya kwanza, kuna wenzenu walikuwa na mashaka kama hayo, wakaniuliza maswali mengi tu, mpaka wakaridhika wakaondoka, sasa nyie sijui mnataka nini zaidi, na sijui kwanini hamshirikiani , wangewaambia huo ukweli,…..lakini sawa …. Haijalishi kitu, labda kila watu wana maswala yao,…haya uliza maswali yako….’akasema akinigeukia mimi.

 ‘Sasa ni hivi, ….nataka nikuulize maswali fulani fulani,..na ni muendelezo wa  yale maswali ya awali, kuhusu deni lilopo benk, nataka unijibu vyema hayo maswali ya msingi….maana wewe ni mkuu wa hii familia, sasa kama kweli unaijali hii familia, nataka uonyeshe kwa vitendo, …..’nikasema na yeye akakaa kwenye sofa na kukunja nne, akaweka mikono mdomoni kama anayeomba, akawa anaipuliza puliza…

Kitendo kile kitufanya tumuangalia kwanza yeye, na mpelelezi akanitupia jicho kama anataka kujua jamaa anafanya nini, mimi nikasema;

‘Na  usiwe na mashaka na mimi kuwa huenda ni mtu tapeli kama ulivyosema, ….kazi yangu ni ya kuisaidia jamii, ….na nia kubwa ni kubaini ukweli wa hilo deni  ambalo limefikia kuifanya familia iliyokuwa ikiishi humu mjane na watoto wake,.... isiwe na amani, na imefikia sasa inataka kufukuzwa kwenye nyumba yao waliyoachiwa na marehemu…’nikasema , na jamaa  akawa anaendelea kufanya kile kitendo kwa muda halafu akasema;

‘Lakini ukweli wa hilo deni  lililopo benki utaupatia huko benki, wao wana vidhibiti vyote… eti afande, mimi nitakuwa na msaada gani zaidi ya watu wa benki…?’akasema na akamgeukia  huyo mpelelezi, na kabla huyo mpelelezi hajasema neno, mimi nikadakia na kusema;

‘Mbona hujiamini….wewe subiria uone kama hayo maswali yanaihusu benki au wewe….’nikasema

‘Mimi najiamini bwana, wewe vipi, haya uliza….wewe niulize hayo maswali yako….’akasema  na mara shemeji akatokea, akiwa kabeba begi la safari na mtoto Yule mdogo kambeba mgongoni, ….na alipomuona huyo mtu  akasita kidogo, ni kama anamfahamu au anamfananisha, mimi kwa haraka nikasema;

‘Dada usiwe na shaka huyu mtu wa usalama, …kama nilivyosema awali, swala lako linafuatiliwa kwa karibu…, ujue kuwa serikali ipo na wananchi wake kuhakikisha kuwa haki inapatikana, usiogope kudai haki yako, hata kuwe na vistisho gani, haki ina nguvu, na dhuluma kamwe haiwezi kuishinda haki…..mbona upo hivyo…?’nikasema na kumuuliza na kabla huyo mama hajajibu, huyo  jamaa akadakia na kusema;

‘Lakini hayo ya mtoto kupandisha homa, kuumwa,….na…..nilishakuambia yapo juu ya uwezo wangu, unielewe hapo, msinibebeshe mzigo usio kuwa wa kwangu, mimi nimetumika tu, na tuseme kosa langu ni kwa vile nilikwenda huko nikaubaini ukweli……’akasema na shemeji  alikuwa kama anataka kusema kitu, nikaona kama anasita, nikamuuliza;

‘Dada kuna tatizo…mbona waonekana kutaka kuondoka, unakwenda wapi?’ nikauliza

‘Tatizo!….haya yote ni  matatizo kwangu, hapa nilipo moyo hautulii, nahisi kama lolote baya laweza kutokea kwa mwanangu…Jamani mimi nimeona  bora niondoke kabisa kwenye hii nyumba,…nimeamua niondoke niende kwetu, humu ndani hakuna usalama, hatulali kwa amani, na mtoto ndio hivyo,kuuumwa magonjwa ya ajabu…..’akasema

‘Kwanin shemeji,ndio hivyo tunataka kulimaliza hili, usikate tamaa, kwanini ukate tamaa haraka hivyo, eti shemeji…?’nikamuuliza na mpelelezi akauliza.

‘Huyo mtoto  anakuwaje, anaumwa nini, hebu nipeni maelezo yake kwanza maana sasa naanza kuvutika na hili tuki…?’ akauliza

‘Mimi hata nashindwa kuelezea, huyu mtoto amekuja kushikwa na ugonjwa wa ajabu hali ikibadilika anaumwa mpaka anapoteza fahamu,tumeenda hospitali hana tatizo, …fikiria mtoto anachemka homa mpaka anapoteza fahamu lakini vipimo vinasema hana tatizo, sasa tatizo ni nini….’akatulia

‘Na kwanini hali yake ibadilike kila nikitaka kufuatilia haki zao, haki ya nyumba, haki…..na …..mimi sijui,ndio maana sitaki tena kuyafuatilia hayo, na tatizo ni humu ndani nikienda kuishi kwingine watoto wangu wanakuwa hawana tatizo, sasa naona tatizo ni hii nyumba, ngoja niondoke, wachukue tu….’akasema huyo mama kwa uchungu.

‘Lakini shemeji si ulishaambiwa ni kwanini hayo yanatokea, tatizo ni wewe unakiuka …..’ akasema huyo jamaa,na huyo mama akamkatisha na kusema

‘Ndio maana nimeamua niondoke,  siwezi  kuchezea maisha ya  watoto wangu tena,  eti kwasababu ya mali, kama ni jasho langu, kama ni jasho la watoto wangu, mungu mwenyewe atalipa, na yte namuachia mungu, kwa mapenzi yake najua ipo siku….’akasema kwa huzuni, na shemeji yake akasema;

‘Lakini shemu ukisema hivyo unamlaumu nani, je kweli deni halipo, sasa ulitakaje, ni nani atalilipa hilo deni, tutalilipaje, kama hili halitafanyika, ….na sio sisi, ni benki wanataka haki yao,na deni hilo linamtesa mumeo…hebu niambie ulitaka tufanyeje…?’ akamuuliza

‘Unataka nikujibu…?’ akauliza

‘Sio unijibu, utoe ushauri wako, unavyoona…’akasema jamaa

‘Je mtoto wangu hataumwa…..maana niliyoyataka kufanya ndio hayo yamefikia hapa , natakiwa nifunge mdomo, …sasa unaniuliza swali, nikuulize je nikitoa huo ushauri sitakuwa nimevunja hiyo miiko…?’ akauliza na jamaa akabakia kama kapigwa kibao. Na mimi nikaingilia na kusema;

‘Dada nakuomba usiondoke, …rudisha hiyo mizigo ndani, na kamlaze mtoto, …haya mambo tunayamaliza leo hii , wewe niamini kabisa, na huyo mtoto hawezi kupatwa na hayo marue rue tena…huyu mtaalamu yupo hapa.’nikasema  na kumuonyeshea huyu jamaa.

‘Hapana,… nyie msisumbuke tena, mimi nipo tayari niache kila kitu, wafanye watakavyo, kama ni nyumba wanataka waache wachukue…nawaombeni mnielewe, hamjui kiasi gani ninavyoteseka…’akasema  huyo mama, sasa akionyesha wazi anataka kuondoka.Jamaa akawa kama anakubaliana na mawazo ya shemeji yake lakini hakutamka neno na mimi nikasema

‘Sawa  dada, kama wataka kwenda utakwenda, lakini mimi nakuomba kidogo tu dada, ..kuna mswali tunahitajika kumuuliza  shemeji yako,  tunahitajia na wewe uwepo…’nikasema

‘Maswali gani, ya kuhusu mali ya marehemu au deni,..hapana hayo ndio yanahatarisha afya ya wanangu…nab ado mnataka kuyarudia, hivi jiulizeni kama ingelikuwa ndio nyie, mtoto anaumwa hivyo, mngefanya nini….hebu niambieni, au kwa vile yapo kwa mwingine…hivi,…hapana,mimi ni mama nina uchungu na wanangu,….siwezi , …mimi nimeamua kumuachia mungu , najua mume wangu kafa, yote mapenzi ya mungu,…..’akasema na machozi yakimtoka.

‘Mwacheni aende,mimi nitafuatilia kila kitu…’jamaa akasema na mimi nikasema

‘Dada niamini mimi,..nakuhakikishia hilo, leo hii tutalimaliza, kuna maswali ya msingi, tukipata majibu yake basi tutakuambia ni nini cha kufanya, kwa taarifa yako, hatua mbali mbali zimeshaanza kuchukuliwa, na haki itapatikana, niamini  mimi….’nikasema na jamaa akanitupia jicho, akitaka kusema neno, lakini akasita akatulia, na mimi nikasema;

‘Dada ujue kuwa haya maswala sio kati yako na ….hao watu, sasa ni maswala kati ya serikali inayotaka  kulinda raia zake,ndio maana huyu mtu wa usalama yupo hapa…sasa hiyo mizimu ije …ipambane na serikali…..’nikasema na huyo mpelelezi akaitikisa kichwa kukubali.

‘Lakini hamjaelewa,…tatizo ni deni…kwanini hamtafuti njia ya kulilipa, kama mnaijali hii familia, tatizo sio shemeji au mimi, tatizo ni hilo deni, mnaelewa hapo, sasa mengine yote hayatasaidia kitu , hata kama serikali ikiingilia, vinginevyo labda iseme itasaidia kulilipa hilo deni…’akasema jamaa.

‘Deni ndio tatizo, lakini je denii hilo ni halali,…je ni kweli kuwa deni hilo alichukua kaka yako, hayo ndio maswali tunataka kuyauliza kwa namna yake,…vinginevyo, nahisi kuna namna…’nikasema

‘Kuna namna…hahaha…’ huyo jamaa akijifanya anashangaa, na kutikisa kichwa na mimi sikumjali nikamwambia huyo dada;

‘Huyu mpelelezi anayechunguza kuhusu kifo cha mumeo, lakini hakuja kukuuliza wewe chochote, ilitakiwa kuonana na wewe awali, lakini kipindi hicho kutokana na hali yako hakuweza kuonana na wewe…na kama angebahatika kuongea na wewe …nahisi mengi yangelijulikana mapema…’nikasema na jamaa akanitupia jicho.

‘Sasa hakijaharibika kitu…ukweli wote sasa utabainika, …na haki itatendeka, na wewe mwenyewe moyo wako utakuja kutulia, kwani utakuwa umetimiza wajibu wako, ….kupigania kile alichokiacha, na ka kufanya hivyo, haya yote yanayotekea hapa yatakwisha, ….maana mengine ni mitihani tu…’nikasema

Mdada huyo akawa anatikisa kichwa kama kukatakaa….na shemeji akaonyesha ishara ya kama anasema unaona…haina haja..tunapoteza muda tu..kitu kama hicho, ..lakini mimi nikampuuza na kusema;

‘Ila kwa sasa mpelelezi huyu anataka kuongea na shemeji yako, na kwa vile kamkuta hapa,…itakuwa vyema kwetu maana  atahakikisha kila kitu kinakwenda sawa, nikimaliza maswali yangu kwake, ataendelea na mpelelezi , …na nina uhakika, tutamaliza kazi…’nikasema nikimgeukia  huyo mpelelezi

‘Sawa kabisa, …shemeji usiwe na wasiwasi…..hilo ni jukumu letu…usiwe na shaka, ….’akasema huyo mpelelezi, na jamaa yetu kwanza akamuangalia shemeji yake….kwa jicho la aina yake,…, halafu akamgeukia huyo mpelelezi, …baadaye akaniangalia mimi…na kusema;

‘Haya mimi nipo tayari kwa maswali yako uliza…’akasema, na shemeji yake akataka kuongea kitu lakini nikaona amesita kutamka neno, akabakia kimia akiwa bado kasimama na begi lake, na huku kamshikilia mkono Yule mtoto mkubwa na Yule mwingine yupo mgongoni.

NB: Ni nini kitatokea....mdada kasalimu amri, akiangalia watoto wake, mjamaa, anapambana akiangalia mali( nyumba) iuzwe ili deni lilipwe, je...ni nini kitatokea.

WAZO LA LEO: Tusiogope kutafuta haki zetu, japokuwa wakati mwingine tunajikuta kwenye mitihani, mitihani hiyo tuichukulie kama ngazi za kuifikia hiyo haki. Tukumbuke kuwa haki wakati wote ipo juu ya dhuluma.
Ni mimi: emu-three

1 comment :

Anonymous said...

Hi, i feel that i noticed you visited my website so i came
to go back the choose?.I'm attempting to find things
to improve my web site!I guess its adequate to use a few of your
ideas!!