Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeMonday, May 9, 2016

YOTE NI MAPENZI YA MUNGU-4Nilimwangalia Yule mama pale alipokaa na mtoto wake, nikajua mambo yameshaharibika, tayari mtoto anachemka homa! Hata bila kumuuliza Yule mama, nikaiona hiyo dalili, mtoto macho yalionyesha, yanaonekana kama yanasinzia, kalegea….nilipoiona ile hali hapo hapo nikakumbuka  maneno ya huyo jamaa, akisema, …usije kukiuka hiyo miiko,…mwisho ni mara tatu, basi….sasa jiulize ni  hii ni mara ya ngapi

Nilipokumbuka hayo maneno nikamwangalia jamaa, jamaa alikuwa kama hana habari, anashughulika na simu yake, nahisi alikuwa anachat..au anaandika ujumbe wa maneno..

‘Shemeji hawa watu hawajui tunavyoteseka na huyo mtoto, na hiyo hali ikijirudia hatuna la kufanya, mimi nanawa mikono yangu,  mimi ni baba yake lakini kutokana na mtaalamu, sitaweza kufanya lolote tena…unakumbuka ulivyoambiwa,….

Hii kama ikitokea tena itakuwa ni mara ya nne, ina maana kwa mujibu wao huyo mtoto kuumwa, ilishazidi  kile kiwango, kwahiyo kupona kwake ni mashaka, kwa mujibu wao,…na huyo jamaa hawezi kufanya lolote tena…..nilipoiona hiyo hali, akili ikaanza kuchemka, nifanyeje sasa…, je kama ni kweli  itakuwaje…..

‘Ooh, sio kweli , hawa ni wajanja tu…’ mimi nikajipa moyo kwa kusema hivyo kimoyo moyo…., huku nikimtupia macho Yule mama, ….yule mama alikuwa kamshikilia mtoto wake kama kashikilia nini, kampakata mithili ya kumkumbatia, ….huku machozi yakimtoka, nahisi moyoni anaumia sana, lakini hanacha kufanya….

‘Huu sasa ni mtihani, …’Nikajikuta nikisema kwa sauti bila kujua,  na jamaa akanitupia jicho,….uso ulionyesha dharau fulani.

Bila kupoteza muda nikaona  sasa na mimi natakiwa nicheze karata yangu ya mwisho, kwa sauti ya haraka nikasema;

‘Umesema huniogopi, kwa maana huogopi maswali yangu, au sio….na ina maana kuwa  unajiamini kuwa wewe huna makosa….,si ndio hivyo…sasa nataka tupambane  mimi na wewe ili nihakiki hilo kama kweli huna makosa, ….nataka tupambane mwanaume kwa mwanaume, ….’nikasema

‘Uliza hayo maswali yako bwana …’akasema akiwa haniangalii usoni akaonyeshea kwa mkono huku kainamia simu yake.

‘Tatizo wewe ni mnafiki na muoga,…’nikasema, na maneno hayo yalimfanya ainua kichwa na kuniangalia, uso ukambadilika, akasema;

‘Eti nini…mimi ni nani, …?’ akauliza sasa akiniangalia kwa hasira, na mimi nikatulia tu nikimkagua, kweli maneno hayo yalifanya kazi yake, aliacha kile alichokuwa anakifanya na kuendelea kuniangalia, akiwa kakunja uso.

‘Mimi sipendi ugomvi….umesema unataka kuniuliza maswali, nimekubali, sasa hiyo ni lugha gani, , hii inaonyesha wewe huna nia nzuri,…unanitaka ugomvi, na inaonyesha wewe ndiye  mwoga…na mnafiki, sio mimi...’akasema na mimi nikaendelea kukaa kimia,

‘Kwanini unasema mimi ni mwoga na….kwa vipi…wakati….nimesema uulize hayo maswali,….uliza sasa?’ akasema akiwa kashusha hasira yake….huyu mtu ni mjanja sana, ….anajua kuigiza, anajua kucheza na utashi wa watu kwani kazoea kupambana na watu wenye tabia tofauti kwenye biashara yake, mtu kama huyo hutarajii kumkasirisha kwa haraka hivyo.

‘Wewe kama unajiamini kwanini unapambana kwa kupitia mtoto,…’nikasema hapo  kashtuka kidogo, akamwangalia Yule mtoto, halafu akajirekebisha na kunigeukia akasema

‘Mimi sikuelewi, napitia kwa mtoto kwa vipi…?’ akaniuliza akigeuka kidogo kumwangalia mtoto, au shemeji, halafu akageuka kuniangalia mimi lakini kwa jicho la pembeni.

‘Hivi wewe kweli una uchungu na hii familia, hivi kweli wewe una ubinadamu, …unajiita baba…..’nikasema na yeye akaniangalia na kusema;

‘Hebu ongea kwa kujiamini…niambie mimi nimefanya kosa gani,…?’ akauliza akinikodolea macho

‘Nikuulize wewe hivi, kama angelifanyiwa mtoto wako hivyo, kweli ungelifurahi, kumbuka ….ubaya umtendao mwenzako ipo siku utakurejea wewe mwenyewe…kumbuka haya maneno yangu…’nikasema akawa sasa katulia, akiniangalia mimi, na mara akageuka kumwangalia Yule mtoto na mama yake kwa macho yenye kujiuliza!

‘Una maana gani wewe, kwani shemeji kuna nini kimetokea….?’ Akauliza na shemeji yake akawa kimia, kamuinamia mtoto wake tu huku machozi yanamtoka, alivyomshika mtoto wake utamuonea huruma!

‘Unajifanya hujui….nikuulize kwanini wewe unamtumia mtoto katika kushinikiza mambo yako,…kama kweli unajiamini na huna kosa, kama kweli una ubinadamu,… kwanini umtumie mtoto ambaye hana kosa, huyo mtoto anajua nini,…hajui kabisa kinachoendelea..’nikasema nikimkimuangalia moja kwamoja usoni, nia yangu ni kumchanganya kichwa, akasirike. Mtu akikasirika huropoka ovyo…

Ilikuwa kama nimemmwagia maji, akataka kusema kitu, lakini kikawa hakitoki, akatikisa kichwa, halafu akasema;

‘Unajua mimi nilikuheshimu sana, nilikuona ni mtu wa maana, sasa sijui nikuite nani, nimejaribu kukulezea kwa busara, lakini wewe hutaki kunielewa, na sasa unataka na….hivi wewe unanijua mimi…tatizo wewe hunijui,….’akasema akitikisa kichwa.

‘Nakufahamu sana, wewe ni dalali, na mbinu zako za udalali zinajulikana, ukitaka kitu ni lazima ukipate, si ndio hivyo, kwa njia yoyote ile, na ndio maana umeamua kutumia mbinu hii chafu, ili ushinikize upate kile ulichokusudia,…wewe na huyo mtaalamu mumeamua kumtumia huyo mtoto…unabisha..?’nikasema.

‘Hayo ndio maswali yako….?’ Akaniuliza na mimi nikabakia kimia nikitaka kujua atachuku hatua gani, alikuwa bado amekaa, sasa uso ukiwa umetahayari. Mbinu ya kumshinda mnafiki ni kumwambia ukweli, mbinu hiyo ikafanya kazi, japokuwa hadi muda huo, nilikuwa  bado sijakuwa na uhakika na kauli yangu hiyo!

‘Wewe sasa huna la kuniambia,…huna lolote lengo lako ni kunipakazia ubaya kwa shemeji…shemeji huyu ni mwongo, mchonganishi….usimsikilize….halafu,  naona hata hayo maswali yako hayana maana, na kwa kauli yako hiyo tunaweza kufikishana kubaya…nikuambie ukweli..ohoooh’akasema, na mimi nikamwambia;

‘Sasa nikuambie kitu…nina uhakika kuna sababu ya huko kuumwa mtoto na haya yanayoendelea , ili kumtisha  mama yake asihangaike kupata haki yake na familia yake,…na hii mbinu ya kishetani, imefanywa kwa kumtumia huyo mtaalamu na wewe….nitakuja kukuthibitishia hilo…, sasa sikiliza kwa makini,  kama hali ya mtoto ikiwa hivyo, mimi nakuhakikishia utakwenda kuozea jela…’nikasema

Hapo akaniangalia kwa macho ya mashaka, akasema;

‘Ina maana kweli umedhamiria na hiyo kauli yako, ina maana sasa unanitisha,….kwanza unasema nini, ina maana unafikiri mimi ndiye namfanya  huyo mtoto hivyo…wewe….sikiliza…’akatikisa kichwa na kugeuka kumuangalia shemeji yake, halafu akanigeukia na kusema

‘Kwanza  wewe unasema hivyo kama nani,….hahaha, eti nitaozea jela…unanitisha mimi, hahaha, tatizo lako hunielewi…hivi wewe ni nani, unajua nilikuwa nakuheshimu, sasa….unataka nini kwangu?’ akaniuliza sasa akasimama, na mimi nikawa nimetulia tu, akavuta hatua, kama ananijia, halafu akasita, akageuka kumwangalia shemeji yake.

‘Shemeji huyu ni nani kwako…..?’ akauliza na shemeji yake akawa kamkumbatia mtoto wake,kama vile hataki amtoke huku machozi yakiendelea kumtoka, kama maji...mimi nikaona napoteza muda, nikasema;

‘Wewe si mwanaume, na huogopi maswali yangu, kama mwanaume kweli kwanini unatumia kiumbe hicho kisicho na hatia, unamtesa mtoto wa watu bure…nimakuambia hivi angekuwa mtoto wako kafanyiwa hivyo ungejisikiaje,….au unafiria mungu haoni,…’nikasema na kabla hajasema neno nikasema;

‘Sasa mimi nakuambia hivi kama wewe unajiamini, basi pambana na mimi, sio kwa kupitia huyo mtoto, nifanyie mimi hayo unayomfanyia huyo mtoto, …mimi sasa nimeamua kufanya hayo usiyoyataka, hamisha hayo …kwangu unasikia,….’nikasema

‘Mimi sikuelewi, unaongea nini….’akasema akionyesha mikono ya kukata tamaa

‘Wewe kama huna hatia,…..basi mwachieni huyo mtoto, upambane na mimi, acheni kumtesa huyo mtoto, unaona hapo…homa hiyo imeshaanza kupanda…na unalijua hilo…umeshawasiliana na jamaa yako afanye hivyo, …unafikiri mimi iyajui hayo….’nikasema na yeye akaguka kidogo kumwangalia huyo mtoto halafu akageuka kuniangalia mimi. Akasema

‘Sasa mimi naona….unanitaka makubwa, unasema mimi ndio namtesa huyo mtoto, ina maana mimi ni mchawi au sio,…au mimi ni mzimu, maana hayo yanatokea kwasababu ya mizimu, wewe, ….wewe, kwa kauli hiyo mimi sizani kama tutaelewana….shemeji , kama huyu ni ndugu yako, ….muonye kwa mara ya mwisho, nitakachokifanya hapa,msije kunielewa vibaya…unanifahamu vyema shemeji mimi ni mvumilivu sana lakini ikivuka mpaka,…ohoooo!’ Akasema sasa akinionyeshea kidole.

‘Sikiliza,….nijibu maswali yangu nitakayokuuliza,….sitaki uwoga hapa… na nia yangu ni kuhakikisha kuwa kweli wewe huna makosa, wenye makosa labda ….labda, tuseme ni benki, au labda tusema kuna mtu mwingine yupo nyuma ya hili, ….sasa kama sio wewe, nataka tulijue hilo kwa kupita kinywa chako,…na tumgundue huyo mtu mwingine ni nani, kwa masilahi ya hii familia, hawa watoto wanahitaji haki yao, kwanini wateseke, kwanini tusiwe na mioyo ya huruma,…’nikasema

‘Sawa….mimi nimekustahi, sitaki kugombana na wewe, maana kutokana na kazi yangu ninapambana na watu wengi kama wewe…hasira zangu zipo mbali saana….sasa nakuambia  uliza maswali yako…uondoke zako….’akasema na kurudi kukaa.

‘Siwezi kukuuliza maswali wakati mtoto yupo katika hiyo hali….wewe  si mjuzi, umefundishwa na huyo mtaalamu wako, fanya uwezavyo huyu mtoto asipandwe na hiyo homa ili mimi na wewe tuweze kuyaongea haya na unijibu maswali yangu kwa amani…’nikasema na yeye akashika magoti, kama anataka kusimama, na mimi nikaendelea kusema

‘Kama huyo mtoto anachemka homa hapo, nitakuulizaje hayo maswali, kama huyo mtoto anaendelea kuchemka homa, mimi sina namna, ni lazima nichukue hatua nyingine, na si zaidi, nitawaita polisi,nina ushahidi kuwa kuna namna inafanyika ili kuwatisha watu wasitatufe haki yao, na namna hiyo inafanywa kwa kupitia huyu mtoto, huo ni unyama, huo ni ushetani, polisi wakija hapa nitawaonyesha huo ushahidi na wewe utakwenda kuozea jela na huyo mtaalamu wako…..’nikasema kwa hasira.

‘Mimi nilishasema, sina namna ya kufanya kama hali ya mtoto ikijirudia, kama homa ikimpanda tena, dawa tuliyopewa haiwezi kufanya kazi,…. hiyo ni  kutokana na mtaalamu alivyosema,…mimi kwa hivi sasa siwezi kufanya chochote ni miiko niliyopewa… unielewe hivyo, sio mimi, ni mtaalamu kasema hivyo,….’kabla hajamaliza mara shemeji yake akadondoka sakafuni….

Oh,….mtihani!

‘Shemeji vipi….’akauliza alipoona ile hali,na mimi nikaona mambo yamekuwa sasa manzito, ikabidi kwanza niende kumchukua Yule mtoto maana anaweza na yeye kudondoka, …mtoto alikuwa anatetemeka,…nilipomshika nikaona joto lipo juu,…nikambeba hadi kwenye sofa nikamlaza,…nikageuka kumuangalia mama yake, alikuwa kalala sakafuni,…kapoteza fahamu!

 Shemeji mtu kuiona ile hali, akasimama na kumuendea shemeji yake, akainama kumuangalia, akasema;

‘Sasa unaona, haya yote umeyataka wewe…unaona wewe mtu…sijui umetoka wapi wewe hunielewi, sasa umeharibu, …hali ya shemeji ikirudia tena,….oh, sijui itakuwaje….’akasema bila kuniangalia mimi, na mimi nikasema

‘Nimeyataka mimi au wewe, ngoja polisi wafike hapa , utasema yote …..’nikasema

‘Shemeji, shemeji…..’akawa anamtikisa tikisa shemeji yake, halafu akageuka kumwangalia mtoto, pale nilipomlaza kwenye sofa, akasema;

‘Kwanza kwani  vipi ina mtoto kapandwa tena na homa, sasa…niliyowaambia, mtajionea wenyewe, mimi sipo.. wewe umemshawishi shemeji akafanya mambo kinyume na miiko aliyopewa, mimi hapo sijui tena la kufanya….maana hii ni zaidi ya mara tatu, na miiko imenikataza kufanya lolote, shemeji, shemeji, hebu amuka, …’akasema akiwa anamtikisa tikisa shemeji yake kumshitua aamuke!

Oh, nikaona mambo sasa makubwa, shemeji shinikizo la damu limeshapanda…kwanza nikamuacha mtoto, nikaenda pale alipolala huyo shemeji mtu, na kuanza kumfanyia huduma ya kwanza . Wakati nafanya hayo, nikamgeukia jamaa na kusema;

‘Sasa hivi nawaita polisi, ..waje waione hii hali jinsi gani mnavyofanya hawa watu kwa tamaa zenu…sasa kabla hilo halijafanyika …, nataka huyo mtoto hali yake ijirudie ili huyu mama akiinuka hapa amkute mtoto wake yupo salama, vinginevyo, ….’simu yangu ikaita, kwa haraka nikaichukua na kuangalia ni nani mpigaji, …walikuwa vijana wangu, nikaanza kuongea nao .

‘Vi-vipi mumeshafika kituo cha polisi, …..sasa waambie waje hapa haraka,  mtu wao yupo hapa, …’nikasema na kusikiliza

‘Ok…wewe ….uje na huo ushahidi, ..fanya haraka…’nikasema na jamaa kusikia, hivyo akamwendea mtoto, pale kwenye sofa,  akachukua ule unga kwenye karatasi,  akafanya alichofanya, akampaka mtoto, halafu,…mtoto akapiga chafya. Mimi nikaendelea kumfanyia huyo mama huduma ya kwanza mpaka akazindukana.

Jamaa alipoona shemeji yake kazindukana akasema;

‘Mbona mtoto yupo safi….ila sijui kama itachukua muda, sijui, kama itafanya kazi….maana hii ni mara ya ngapi sijui, …shemeji mimi nilishawaambia…kwani kitu gani mnafanya, kwanini mnamtesa huyu mtoto…’akasema  huku akiangalia saa yake na nilimuona kama anataka kuondoka, nikamkabili na kusema;

‘Unataka kwenda wapi…subiria maswali yangu….?’ Nikamuuliza, na yeye akasema

‘Mimi nilishakuambia nina mambo yangu, nilikupa muda wa kutosha kuuliza hayo maswali yako hukutaka kuniuliza kwa haraka, ….halafu sasa nashangaa kwanini umewaita polisi ili iweje,…mimi naondoka zangu, sitaki maswala ya kukutana na polisi hapa,  nina kazi zangu za kufanya za haraka…’akasema sasa akianza kuondoka.

‘Sikiliza, …huwezi kuondoka mpaka ujibu maswali yangu, na polisi wanajua upo hapo, na amri yao ni kuwa uisondoke hapa mpaka wafike,…ukiondoka hapa umekiuka amri ya serikali, sasa utatafutwa kama mhalifu..’nikasema ,  nikamuona akibadilika usoni, uwoga…., akasema

‘Kwanini mimi nimefanya kosa gani, …?’ akaniuliza

‘Polisi watakuja hapa…wao watakuambia kwanini wanataka kukuona….ila ninachosema ni kuwa kama watakuta mtoto yupo kwenye hali mbaya, itakuwa ni moja ya ushahidi wao, na …wewe ndiye utakuwa umesababisha hayo yote, wewe na huyo mtaalamu…mtahitajika kuisaidia polisi…, kwanini mnamtesa huyu mtoto…’nikasema.

‘Ngoja…kwanza,….wewe unasema nini…...’akasema na kumuendea huyo mtoto pale kwenye sofa na kwa muda ule mtoto alikuwa kalala, sasa akawa anamkagua huyo mtoto mwilini kuona kama ana joto….akasema;

‘Lakini mbona hakuna joto…huyu mama yake vipi…huyo mtoto kalala tu, hana tatizo…lakini sijui zaidi ya hapo,….’akasema akimuangalia shemeji yake

‘Sawa sasa ni hivi sisi tutaendelea na maswali, na wakati tunafanya hivyo,…sitaki itokee mtoto kupandisha homa tena, na sitaki hiyo hali ijirejee tena iwe mwanzo na mwisho, ….’nikasema;

‘Mimi siwezi kuendelea kukaa hapa,…nimeshakuambia,  ni lazima niondoke…maana mimi, nina wateja wangu wananisubiria, kama mnaona nina kosa, waambie polisi wanifuate nyumbani kwangu….’akasema na mara simu yangu ikalia, nikaipokea na kusema;

‘Hali ya mtoto ipo shwari…mnaweza kuwaambia hivyo, waambie bado namuuliza huyu mtu wao maswali, na kama nitaona ana hatia basi nitawaarifu…nini anakuja,ok….’nikasema na jamaa akaniangalia akiwa kasimama, ….halafu akasema ;

‘Hivi wewe unahisi kuwa mimi nahusika na haya yote, kuwa mimi naweza ku….ku…mtesa mwanangu….hivi wewe una akili kweli….shemeji usimsikilize huyu mtu…huyu mtu ni-ni-ni….’akashindwa kumalizia na mimi nikasema;

‘Ni nani, ….malizia, usiwe na kigugumizi, toka lini dalali akawa na kigugumizi…vinginevyo naona maji yameshakufika shingoni, utapeli wenu utawatokea shingoni…’ nikasema

‘Mimi siwezi kufanya kitu kama hicho, kwanini niifanyie familia yangu…niajiibia mwenyewe..hujui hawa ni familia yangu, hebu muulize shemeji,mimi na kaka tulikuwaje,….kaka hayupo, mimi hapa nasimama kwa niaba ya kaka….hayupo mimi nipo,…tatizo lako wewe unaingilia mambo bila kutaka kujua zaidi…hayakuhusu haya’akasema

‘Sasa nataka tulihakikishe hilo,….kama kweli unaijali hii familia,… kama kweli unasimama kwa niaba ya marehemu kaka yako  au…kwa niaba ya utapeli, kwa nia ya kupata mali ya marehemu kwa udanganyifu, na kumtumia mtoto kama silaha ya kushiinikiza hayo…’nikasema

‘Hahaha..wewe mtu bwana,…una mawazo duni,…unasema hivyo unafikiri nitapaniki…hunipati kwa hilo, nikuambie kitu,  walinikabili polisi, wapelelezi wakashindwa, ….wewe sijui ni nani, utaweza nini wewe, sasa sikiliza kwa vile sitaki kuelekeweka vibaya mbele ya shemeji , wewe yaulize hayo maswali yako ya kipuuzi, nayaaita ya kipuuzi maana ni ya kubuni, ….uchonganishi tu, wivu….’akasema halafu akamgeukia shemeji yake akasema

‘Shemeji mtoto kalala huyo,kwa hivi sasa hana tatizo, zaidi ….mimi sijui, anajua mtaalamu, nenda kamlaze huyo mtoto ndani….’akasema na shemeji yake ambaye kwa muda huo alikuwa kakaa karibu na mtoto wake, akasema;

‘Jamani,…mimi sitaki tena haya mambo….mimi sitaki tena haya maisha, mimi sitaki tena kumtesa mtoto wangu, kama  ni hii nyumba chukueni, waache wachukue, …niachieni mtoto wangu salama…, sitaki jamani, basi …basi,…sitaki…’akasema huyo mama akimbeba mtoto wake….’

‘Dada niamini mimi haya yote yanakwisha,…. leo hii hii utaujua ukweli….’nikasema.

‘Hapana mimi sina haja tena …..waache wachukue wanachokitaka, na mimi nitamuachia mungu,kama kapanga iwe hivyo, yote haya ni kwa mapenzi yake, waache wachukue kila kitu watakacho, waniachie wanangu,, …wachukue kila kitu watuachie amani yetu, mimi na watoto wangu, mimi sitaki tena, ..sitaki sitaki, nimechoka jamani….’akasema na shemeji mtu akawa kashika kidevu.
‘Dada wewe kamlaze mtoto, haya nayamaliza sasa hivi, haki ya mtu haipote, nakama hali ya mtoto ikibadilika haraka polisi watafika sasa hivi,…. Usiwe na wasiwasi, haya maswala sasa yamefika kwa wenyewe…’nikasema na mara simu yangu ikaita,ilikuwa namba ya mpelelezi mmoja wa polisi….nikaipokea ,

‘Afande vipi?’ nikauliza na kusikiliza ….jamaa akawa ananitazama kwa macho yalijaa wasiwasi nikamuona akigeuza shingo kutizama uelekeo wa mlango….

NB: Kuna nini kinaendelea….

WAZO LA LEO: Tutafute mali kwa njia za halali, tuutafute utajiri kwa njia za haki…, lakini sio kwa kutumia jasho la mtu mwingine. Jasho la mtu ni ushahidi , na malipo ya kudhulimiwa jasho la mtu ni kwa Yule mdhulumaji kuishi maisha ya mashaka na mwisho wake dhalimu huyo ataishia kudhalilika kwa mabalaa mbali mbali.Ni mimi: emu-three

3 comments :

Anonymous said...

imenigusa sana

Anonymous said...

Bonge la simulizi tupo pamoja miram

Anonymous said...

I admire sana simulizi zako but unaweka late sana jitahidi bhana but keep it up bro