Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeTuesday, May 31, 2016

YOTE NI KWA MAPENZI YA MUNGU-10


Siku kabla ya hukumu! Dalili za mwanzo…

Siku ya pili nilifika kituoni kama nilivyoagizwa, na nikaambiwa nisubirie kwanza, kwani Dalali anahitajia wakili wake awepo akiongea, ikabidi tusubirie kwanza , lakini baadaye mimi nikaruhusiwa kuingia ndani, kwani wakili wake alichelewa kufika. Niliingia  kwenye chumba maalumu cha maongezi, na humo sikumkuta mtu baadaye kidogo, Dalali akaja akiwa kaongozana na askari;.

Dalali aliponiona  akaanza kucheka ile cheka yake ya dharau,  akasema;

‘Ehee wewe tapeli, niambie, umakuja eeh, …wewe mpuuzi kwelikweli…, yote haya umeyasababisha wewe, yaani mimi nalazwa humu kituoni kama mhalafu,..naumwa na mbu, kwasababu yako, ….wewe mtu wewe, …tatizo  wewe hunifahamu…yaani hili utalilipa, hutaamini…’akasema

‘Kwani ni mimi ndiye nimekuweka ndani, …wewe si uliona pale, si mimi ndio nilitakiwa kuweka ndani, na wewe ulikuwa unashabikiwa iwe hivyo…hukujua kuwa haki ina nguvu sana kuliko dhuluma, umeonaeeh,  mungu alivyo, hutoa kila kitu kwa haki…na kwa ajuavyo yeye, pole sana ndugu yangu, na mimi sikukuombea kabisa uyapate haya…je hali yako vipi…?’ nikamuuliza


‘Hali yangu vipi….wewe lala humu ndio utaniuliza swali hilo….’akasema akijikuna, suti ilikuwa imejikunja kunja.

‘Najua sana hali ya hapo, nimeshalala humo mara nyingi tu, lakini kuwekwa kwangu humo ilikuwa tofauti na wewe…nilikuwa natete wanyonge, ….’nikasema

‘Sawa bwana….endelea kutetea tu,…’akasema akiendelea kunyosha nyosha suti yake, na kuweka tai yake vyema.

‘Yaonekana unajipenda sana…’nikasema na akatabsamu na kusogeza kichwa karibu yangu,kama anataka kuniambia jambo la siri au la muhimu akasema

‘Sasa siliza . ile familia ilikuwa ikinitegemea mimi,  nibangaize ndio ipate kula,...unanisikia sana…’akatulia kidogo.

‘Sasa mkuu, kuanzia sasa nakuachia wewe utajua jinsi gani hao watu wataishi, wewe si umejifanya kidume bwana,  wewe ni kaka mtu, au sio..na unajifanya una huruma zaidi yangu, haya sasa kazi kwako….’akasema kwa sauti ya juu, halafu kama vile kajitambua akashusha sauti,, kama  vile hataki watu wengine wasikie wakati tulikuwa wawili tu na Yule askari alikuwa katoka alikuwa kwa nje mlangoni.

‘Je kama ulikuwa unaionea huruma hiyo familia mbona unaacha wanafukuzwa kwenye sehemu yao ya kuishi , wangeenda kuishi wapi, au una nyumba nyingine ya kuwapatia maana nyie madalali bwana…mnatajirika tu kwa majasho yaw engine… mhh, mpaka nyumba ndogo mnawajengea nyumba, wewe kiboko,…’nikasema  kama utani na yeye akacheka, akitikisa kichwa

‘Wewe mjanja sana wewe, sikuamini, hebu nikuulize  wewe anakulipa nani kwa kazi hii,…ya upeku peku …. hahaha, eti nyumba ndogo, acha hiyo kabisa…najua unaelekea wapi….hahaha hunipati ng’ooo’akasema akikaa kwenye kiti na kujiegemeza, akawa ananyosha tai yake vyema, halafu, akageuka huku na kule kama anawatfuta watu wengine.
‘Hawa watu wapo wapi…?’ akauliza huku akiinua mkono kama anaangalia saa, na mkono haukuwa na saa, na mimi kwa kupoteza muda nikazidi kumtania.

‘Kwahiyo sasa umekubali ukweli …upo tayari kutubu, au sio….?’ Kwanza akatabasamu, halafu akanikazia macho na kusema;

‘Kutubu nini, kuhusu nini, nitubu kosa gani, …unafikiri kwa vile wamenishikilia hapa, nina kosa au, au ndio huo upeku upeku wako…’akatulia kama anasubiria jibu kutoka kwangu, na mimi nikawa nimetulia tu, halafu kwa sauti ya chini, akaniuliza

‘Hebu niambie mimi nina kosa gani , maana haya yote umeyaanzisha wewei..?’ akauliza akinikazia macho.

‘Hivi hukusikia kuwa mtaalamu kaongea kila kitu…? ‘ nikamuuliza , akacheka kweli kweli, halafu akatikisa kichwa, akasema

‘Wewe mjanja sana…wewe eeh, ni kiboko…hahahahaha.’akasema na kuendelea kucheka.

‘Kwani hujaambiwa,…yeye  bwana kajitakasa na kusema ukweli wote….’nikasema

‘Ukweli upi  bwana, usifanya mimi mtoto mdogo….nilishakuambia kama unahisi kuna makosa yamefanyika,  …leta ushahidi … upo wapi huo ushahidi wako, nikuambia ukweli, likiisha hili mimi ninakushitakia rasmi,….hilo ujiandae nalo..’akasema na kunikunjia uso kuonyesha hatanii.

‘Ushahidi  si ndio huo…shahidi mmojawapo ni Mtalaamu, kaelezea yote kabla hajatoroka, au hujaambiwa , labda ndio maana umeamua kumuita wakili wako…mimi ningekushauri kitu kama rafiki yangu, shemeji yangu..useme ukweli tu, maana mwisho wa siku utabakia wewe mwenyewe…’nikasema kama utani

‘Wewe unajifanya mjanja sana,nimeshakuelewa mbinu zako, nitabakia mimi mwenyewe kwa kosa gani,,….hebu niambie mimi nina kosa gani, mbona hutaki kulisema hilo….?’ Akauliza sasa akiwa makini.

‘Unaweza ukashitakiwa kama mshirika  mwenza , kama hutakuwa mkosaji,  kama atapatikana mtu mwingine aliyetenda hayo,  wewe utakuwa mshirika wake, ndio maana nakushauri useme ukweli, yaishe, ili haki itendeke, mjane na mayatima wake wapate haki yao…hilo deni sio haki , huo ndio ukweli,sasa kama deni sio halali, ni nani aliyafanya hayo, unaona ilivyo….’ akanikatiza na kusema

‘Hebu niambie kwa hilo , maana hapo tu yaonyesha huna uhakika, mkosaji hajafahamika, au sio….sasa  mimi nitashitakiwa hapa kama nani, kama mshukuwa, haya, kama ni hivyo ushahidi upo wapi,..kwanza tafuteni mkosaji ndio muanza kumkamata, kama mtampata, mtaniambia,’ akasema

‘Huyo mkosaji alikwenda kwa mtaalamu, akamwambia yote, na alitaka mtaalamu afanye mambo yake ili kumlinda,….’nikasema nikimuangalia atakuwaje usoni, lakini hakuonyesha dallili ya kushituka, ila alitanabasamu kwa dharau tu.

‘Ndio maana nakuambia mwenzako,….mtaalamu,  yeye kasema  yote,  kuwa kazi yake ndio biashara yake, mteja akija akimuomba amfanyie jambo,kama linawezekana anamfanyia….na ndio akakubali kuwa alikuja mteja akitaka afanyiwe hayo yaliyofanyika, ili …..’akanikatiza

‘Acha kutunga  hadithi…..wewe ni mtunzi mnzuri wa hadithi, lakini ukumbuke kuwa hii sio hadithi, hapa unacheza na uhai wa mtu,….unaijua jela ilivyo..hakuna mtu anayeweza kufanya ujinga kama huo…’akasema kwa hasira sasa.

‘Sasa sikiliza nikuambie ukweli alivyoongea mtaalamu….kuwa kwake wanakuja wateja wengi wakitaka kufanyiwa ma- jambo, ili hkulindwa…., yeye ni mtaalamu wa kulinda watu wenye matatizo mbalimbali, kama wana madeni wasidaiwe, kama wana maadui, maadui washindwe kumfanyia kitu, kama wana matatizo ya mizimu mashetani…na mambo mengine,

‘Akaulizwa siku kadhaa nyuma alikuja mtu kwa shida hizi na zile…akataka kufanyiwa hivi na vile…tuambie …akasema hawezi kukumbuka, akaambiwa afanye utaalamu wake amkumbuke, la sivyo atalazimishwa akumbuke…akapinga kidogo, akakumbushwa kiaina,….’akamkatiza
‘Kiaina kivipi…?’ akaulizwa

‘Wanajua wenyewe polisi….’nikasema

‘Uwongo…’akasema

‘Alipokumbushwa akasema ndio anamkumbuka mtu kama huyo, alikuja kwake, lakini kutokana na miiko yake, ilikuwa ni ngumu lakini kwa vile alihitajia pesa, na pesa alizoahidiwa ni nyingi akakubali….akaubali kufanya dawa za kinga na dawa za kulinda watu wasifuatilie…..’nikatulia

‘Wewe mjanja…eehe…’akakaa mkao wa kunisikiliza
‘Basi akafanya mambo yake,..akatengeneza mzimu,.shetani sijui…kwahiyo akaliweka sehemu ambayo litawagusa watu hisia zao ili wasifuatilie,…’nikatulia nikimuangalia niliona japokuwa alijitahidi lakini ilimgusa, akasema

‘Ni hadithi nzuri sana…..’akasema

‘Na mwisho wa siku akaambiwa amtaje huyo mtu kwa jina maana polis wana uhakika kuwa anamfahamu huyo mtu, …. ni nani…, akaanza kusema,eeh…. yeye kutokana na kazi zake huwa anamlinda mteja wake, harushusiwi  kumtaja, lakini si unawajua polisi walivyo, mwisho wa siku alimtaja.. ‘nikasema

‘Hahaha, jamani….., ni huyo huyo mtaalamu ninayemfahamu mimi,…haya alimtaja nani ,…alimtaja mtu gani , niambie….?’ Akauliza

‘Kwanini hujiulizi ni kwanini polisi baada ya kuongea na huyo mtaalamu wakaja kukukamata wewe…’nikamwambia na yeye akatikisa kichwa kama kukataa

‘Hilo sijui,….. wao wamesema wananishikilia ili kuisaidia polisi , nahisi  kama…mshirika wa huyo mtaalamu, kwa vile anawahadaa watu…eti serikali imetoa amri wataalamu wanaohadaa watu wakamatwe, na huyo mtaalamu wanahisi anaweza akawa …..wanamshuku tu kwa vile hawamfahamu vyema, ….. ndivyo nijuavyo mimi, na mimi mpaka sasa hawajaniambia kosa langu ni nini,…etu natakiwa kuisaidia polisi, sasa nimewashtukia, ….’akasema

‘Mtaalamu anawahadaa watu kwa jambo gani,….nimakuambia awali, alihojiwa akasema alimjia mtu, huyo mtu alimjia kwa jambo gani..hujiulizi, hapo, walimtega kuwa anahusiana na mambo ya kukatwa watu viungo, si unajua polisi walivyo wajanja, kuona kapelekwa huko akasema hapana yeye hahusiki na hayo, yeye akafanya kadha na kadha,…akabanwa kinamna akaropoka yote,,…wewe nakupa kama angalizo, mtaalamu keshakutaja baba…’nikasema

‘Kanitaja mimi….kwa vipi!..... Nikuambie kitu, mimi nimeshajiandaa kwa vyovyote vile, nina uhakika sina kosa,na kwa uwongo wakoo huo….hunipati  ng’ooooo’akasema

‘Sasa kama unajiamini ni kwanini umeamua kumuita wakili….?’ Nikamuuliza, na kabla hajanijibu mara akaingia mtu, alikuwa ni wakili wake, na Dalali akatabasamu, na kutikisa kichwa kama kukubali …
                                                ************
Wakili, akaingia na briefcase yake mkononi,....na majigambo yake, ni wale wale aina ya Dalali, majigambo kwa kila hali, mavazi, kutembea, mdomoni,…..Na alipoingia tu…akaniangalia kwa makini halafu akamgeukia mteja wake, akauliza

‘Huyu ni nani….?’ Akauliza

‘Peku peku…’akasema na wakili akasogeza kitu kukaa karibu na Dalali, huku akiendelea kuniangalia kwa makini halafu akatikisa kichwa kama kukubali jambo.

‘Haya niambie…nilitaka tuongee kwanza, kabla hujaanza lolote lakini foleni bwana, sasa tuanzie wapi..na tutaongeaje na huyu mtu hapa…?’ akauliza

‘Kwanza hakuna muda wa kuongea, …mimi nimekuita kwanza unisikilize,….utanisikiliza wakati naongea na hawa watu,  kuna mambo nataka wewe uyaweke wazi kisheria, mbele ya hawa watu akiwemo shemeji, ….shemeji naye anatakiwa kuwepo…’ akasema;

‘Mambo gani…?’ akauliza wakili , huku akiniangalia, halafu akageuka kumuangalia mteja wake,na mara mpelelezi akaingia akiwa na mtu mwingine ambaye alionekana ni mtu wa kuchukua hayo maongezi kwenye mitambo yao, kwa ni alikuwa kabeba laptop yenye kamera juu yake…mambo ya kisasa hayo!

Wakili akamgeukia mpelelezi , naona walishaonana huko nje kwani hawakusalimiana akasema

‘Hebu niambie mteja wangu kashikiliwa hapa kwa kosa gani…?’ akauliza

‘Mteja wako! Ok, hajakuambia eeh,,…yupo hapa kuisaidia polisi, kuna maswali tunahitajia kumhoji, lakini akang’ang’ania  hawezi kuhijiwa mpaka uwepo, kiujumla sisi tuliona ni maswali ya kawaida tu, sasa huenda anahisi vinginevyo….’akasema mpelelezi na wakili akamgeukia mtu wake, na Dalali akasema;

‘Usiwe na wasi wasi, wakili wangu, ..ninachotaka ni wewe usikilize tu, kama utaona ninakosea unaweza kunionyesha ishara mimi nitajua tu, kuna huyu mtu kanishuku , na shuku hii naona imekwenda mbali hadi polisi wameingilia kati, lakini kiufupi haina mshiko….sasa wewe sikiliza tu,….’akasema akitikisa kichwa kujinadi.

‘Kwahiyo…..’akataka kusema wakili wake, lakini Dalali akamuashiria kwa mkono kuwa anyamaze, na Dalali akanigeukia mimi na kusema;

‘Hasa wewe…ndio nina usongo na wewe….najua wewe ndiye chanzo cha haya yote, sasa nataka kuuondoa huo uwongo wako wote, ili jamii….hasa wanafamilia wasiwe na shaka juu yangu,…’akasema

‘Kuna swala nimekuambia muda mchache uliopita, …nikakuomba kama rafiki unasemaje kwa hilo…?’ nikaanzia hapo

‘Kwanza nikuambie ukweli, mimi sina kosa, siwezi kukubali kosa ambalo sijalifanya, kama mtaalamu aliongea hayo  mbele ya polisi, hayo ni yake yeye…., na kwanza sio kweli, hayo uliyoniambia, umeyasema ili kunifanya niongee, …
‘Lakini  wewe unataka mimi niongee nini, nidanganye kuwa nimefanya,…..hapana siwezi kufanya hivyo,leo nitaongea ukweli tu…’akageuka kumuangalia mpelelezi.

‘Mimi namfahamu sana mtaalamu hawezi kusema mambo kama hayo, eti amekiri kosa,  sizani, sijui….na hata kama kasema alilosema huyu ndugu…, labda, sijui…labda walimtesa, akasema waliyotaka wao….na kama mumeona  ana kosa basi makosa hayo ni yake yeye mwenyewe…mimi yananihusu nini…’akasema .

‘Yeye kama mtaalamu, kazi yake inatokana na wateja wake….na nikakuambia alishamtaja huyo mteja wake, ambaye alifika kwake kutaka kinga yake….’nikasema  hivyo, nilimuona akikunja uso, labda hakutarajia nitaliongea hilo,kwani alijua nilimuambia yale awali kama utani, sasa anaona naliongelea hapo mbele ya mpelelezi, … akasema.

‘Kwanza…mimi ndiye nimekuita ,.. nataka mnipatie muda wa kuelezea ’akasema
‘Sawa….nimekuja, na nijuavyo mwito wako ni kuhusu maswali niliyokuuliza kule nyumbani kwa marehemu au sio..au kuna jingine?’ nikauliza

‘Mhh…..ndio, .lakini mtu mmoja hajafika,….siwezi kuyaongea niliyokuitia mpaka shemeji yangu awepo, ninataka hili jambo limalizike kabisa,….sitaki tena kusumbuliwa, hamjui jinsi gani ninavyopata taabu kwa jukumu nililopewa, naacha kushughulikia familia yangu…na sasa mpaka nalazwa rumande kwa kosa ambalo sio sahihi…...’akasema na mara mlango ukafunguliwa akaingia yule mama mjane, akasalimia kwanza kwa kumshika mkono mpelelezi, ambaye alikuwa karibu yake, halafu akaja kwangu.

Alipofika kwa shemeji yake akasita kuutoa mkono, akawa anamwangalia shemeji yake machoni, ilichukua muda, akimwangalia hivyo halafu baadaye, akatikisa kichwa, halafu akainua mkono na kusalimiana na shemeji yake, kitendo kile naona kiliacha  maswali mengi , nahisi hasa kwa Dalali, je shemeji yake kafanya vile kwa kumuonea huruma au kuna jambo…hata hivyo kwa mtu kama Dalali mwenye uzoefu wa kazi zake, hakutaka kuonyesha dalili yoyote machoni mwa watu, akasema

‘Shemu usijali , mimi sina hatia, haya yatakwisha , leo hii hii, wataumbuka hawa watu….’akasema hivyo .

‘Haya Dalali, tunataka tulione hilo….’akasema mpelelezi

‘Na mtaliona kweli….’akasema
‘Sawa  mjue hiki ni kikao tu cha kuulizana,…sio kikao cha kushitakiana, baada ya hapa, sheria itachukua mkondoo wake, ….’akasema mpelelezi.

‘Sawa  mimi nipo tayari….’akasema  Dalalii kwa kujiamini kabisa

‘Haya wanandugu, Dalali…ulisema unawahitajia, hawa watu , haya hawa hapa wamefika, na ulisema ulihitajia uhojiwe kuhusu hilo deni ili uondokane na sintofahamu iliyojengeka juu yako,kuwa wewe umelitambua hilo deni kuwa ni kaka yako, na kwa kulitambau hivyo, wengi wamekudhania vibaya….! ‘akasema mpelelezi

‘Ndio…’akasema hivyo

‘Hayo ni kwa kauli yako,  na ulianiambia kuwa wewe huna shaka na hilo deni kwani  wewe una uhakika kuwa kweli hilo deni ni la kaka yako, na ushahidi unao…, ‘akazidi kusema mpelelezi.

‘Ni sawa, kama kuna mtu ana ushahidi kinyume na huo, wa kutoka benki ninataka tuuone,…kwa nyongeza hapo….’akasema

‘Na ulianiambia huyu mwenzetu hapa amekuwa akikuhoji kama vile unahusikana na hilo deni, au sio…anakushuku vibaya kitu ambacho hukukipendezewa, kwahiyo unahitajia awepo ili uondoe hiyo dhana uliyoiita dhana potofu, au sio?’ akasema mpelelezi na kuuliza hivyo

‘Ndio…nataka yeye atoe ushahidi, vinginevyo, mimi sitakubali, nitamchukulia hatua stahiki…sheria zipo, na ikishindikana kwa sheria…ok…..lakini tuyaache hayo…, ‘akasita kuendelea na sikutaka kusema neno hapo, nikabakia kimia, akaendelea kusema;

‘Kiukweli inaniuma sana,..nimewaza sana, nikaona ni kwanini, …..kwahiyo  mimi ninachotaka,  hili jambo la kunishuku sijui nini…aah,  mimi ninataka limalizike hii leo! Na kwa ujumla  mimi naona tulimalize hili jambo kwa amani, kuliko kupelekana mahakamani,.na zaidi ya hayo ninataka shemeji  yangu awe na amani ….’akasema

Alipotamka hivyo akamuangalia shemeji yake, alishangaa kumuona shemeji yake akimuangalia kwa macho ya mashaka, na walipoangalia na huyo mjane, yule mama  alitikisa kichwa kama anasikitika na usoni akionyesha  huzuni, akashika shavu, dalali usoni akaonekana akibadilika kama kinyosha, uso wa kushangaa, halafu uso …akatabasamu. Sijui pale alikuwa akiwaza nini, huenda ni jinsi alivyomuona shemeji yake, anashindwa kumuelewa kuwa labda shemeji yake anamuonea huruma au kuna jingine, akaona sasa aulize;

‘Shemeji kuna tatizo huko nyumbani, umesema watoto hawajambo, lakini mbona naona kama kuna tatizo…?’ akauliza

‘Tatizo!...’akasema shemeji yake kwa mshangao

‘Najua hali za nyumbani, hawa watu wamenishikilia hapa sijui mna nini cha kula huko nyumbani, inanipa shida sana kuwawazia..sasa muulize huyu kaka yako nimeshamwambia…nyie mnanitegemea mimi nibnhaize ndio mpate kula, …..inaniuma sana ’akasema kwa sauti ya huruma, huku akininyoshhea kidole.

‘Kula…ndio unaona ni muhimu kwetu,…kula  shemeji sio tatizo, mungu hamnyimi mja wake riziki, ila hili, nakuonea huruma unavyoteseka huku rumande….na labda huna kosa,.’akasema shemeji mtu

‘Shemu mimi sina kosa kabisa…hawanielewi tu…’akasema

‘Ndio maana nasema tuyaache tu haya mambo, tumuachie mungu  yeye ndiye anafahamu ukweli….maana yote haya ya nini, ni sababu gani, sababu ya mali,…mali watu wanaona ni muhimu kuliko ubinadamu, nikuambie kitu shemeji,….mimi nimeshanyosha mikono  yangu juu, na kumuachia yeye mwenye uwezo, kama kweli mungu anasikia duwa za waja wake waliodhulumiwa, basi ….sina la kusema zaidi…’akasema huyo mama mjane akinyosha mikono juu.

‘Shemu ndio maana nimekuita hapa,  ni muhimu nilithibitishe hili ili moyo wako uridhike…usiwe na shaka, hawa watu wabaya sana,…wataumbuka  wao wenyewe, utaona shemeji nitakavyowaumbua, na wewe mwenyewe , utahakikisha kuwa mimi sina kosa …, na mimi sijui, kwani deni hilo limetokea benki,kwanini hawaendi kuwauliza benki,…kwahiyo kwa hivi sasa nakuomba shemeji yangu uniamini…..unanifahamu vyema, nimeishi kwenye mikono yako …waache nipambane nao...’akasema na mimi nikasema;

‘Utuelewe Dalali, shemeji yako anataka kauli yenye kumtia faraja,..kauli itakayoondoa huo uwongo wa kusema mume wake ana deni, kwake yeye huo ni uwongo, je una kauli gani ya kumsaidia kwa hilo….labda ungelisema kuwa  wewe umegundua kuwa kweli kaka yako hakuwa ni deni, na hilo deni huenda, …’akanikatisha na kusema

‘Hivi wewe unasema nini..niukatae ukweli,hivi hapo namsaidia kaka yangu au ninazidi kumuingiza motoni, sikuelewi…’akasema
‘Sasa kwa kauli yako hiyo inazidi kumuuza shemeji yako, maana yeye ndiye anamfahamu kuliko hata wewe, hakubaliani na hilo,….labda wewe unajua zaidi, kama unajua zaidi, basi  utubu,…’nikasema

‘Nitubu….kwanini nitubu, nitubu nini…?’ akaniuliza kwa hasira

‘Kuwa ulifanya makosa, na unaungana na sisi kuwa deni hilo halipo, sio la kaka yako , basi tushirikiane kulitafuta hilo deni ni la nani na kwanini limeingizwa kwenye akaunti ya kaka yako,…hapo shemeji yako  atajisikia vizuri….’nikasema na jamaa akaniangalia kwa hasira akasema

‘Unajua mimi sikuelewi,….hilo deni ni la kaka, haina haja ya kumdanganya shemeji, ili iweje, ni kwanini yeye asiukubali huo ukweli , wakati kila kitu kipo wazi, …hivyo tutamuumiza kaka na kumpendelea shemeji si ndivyo tunavyotaka, kwa vile yeye hayupo hai kujitetea au sio….’akasema

‘Ndio, kwa vile yeye hayupo hai kusema kweli kuwa hilo deni sio lake, na walioanya hivyo, wamekusudia hivyo, kuwa yeye ni marehemu hakuna wa kumtetea, na ndiocho inachomuumiza shemeji yako…’nikasema
‘Shemeji haumii kwa hilo… umemsikia mwenyewe akisema, .nyie hamjali ubinadamu mnachohangaikia hapa ni mali tu, ugeuze maneno ili deni libakie, haya likibakia ni nani atalilipa, huoni roho ya marehemu itakuwa kwenye mateso, je nini kitakuja kutokea kwenye hiyo familia tena, hujiulizi hilo…sasa nakuambia hivi kama nia yako ni kupata mali, …hupati kitu hapa,’ akasema

‘Mimi na wewe na yoyote yule anapotenda kosa jambo jema ni kutubu, kuomba msamaha, ukikiri kosa tutakuelewa, huo ndio uungwana, na baada ya hapo tutaona tufanyeje, hiyo inaleta neema, lakini tukijifanya wajanja wa kuhadaa, , …sijui kama hiyo mikono iliyoinuliwa juu itarudi chini bure, sijui..’nikasema na yeye akabenua mdomo kwa dharau

‘Wewe  mjanja sana  …na usitake tuharibu hiki kikao, ..unakazania mimi nitubu, mimi nitubu  nini,…..nimeshakuambia mimi sina kosa..na hili ninataka ulithibitisha hii leo, kama mimi  kweli nina kosa toa  huo ushahidi  wako ulio nao ,na ikidhirika hivyo mimi nipo tayari kuadhibiwa,….sina shaka na hilo, hata kaka aliniamini hivyo, nyie tu ndio mumelata fitina zenu, muulizeni shemeji…’akasema akigeuka kumuangalai shemeji yake.
‘Na..na, mimi nawaambia ukweli kwa hili, …maana mimi nimejitolea kwa hiyo familia, na pili nataka kuisafisha roho ya kaka itulie mahali pema,..nyie mnaleta vikwazo, ….mungu atawalipa kwa hilo, mungu ananiona, mungu atanisaidia nitashinda tu….’akasema na shemeji yake akasema;

‘Aaamini….kama huna kosa shemeji yangu, mungu atakusaidia,…na huyo anayemsingizia mume wangu , kwa mapenzi ya mungu atabainika  tu, sisi tuna nini,…ni mjane tu, watoto wangu ni yatima tu, watafanya nini, mungu pekee ndiye anajua hatima yake,  …..nyumba , haya na kila kitu wanachotaka waache wachukue watuachie roho zetu, ….’akatulia kidogo

‘Umeona eeh shemeji…mimi nipo pamoja na nyie msitie shaka….’akasema

‘Sawa sasa mimi nimeambiwa wewe umeniita,  sikutaka kuja hapa,…mimi na watoto wangu tulitaka twende kwetu, tusubirie lakini ….nimeambiwa nisubirie na kwa hili, nisingetaka watu wapate shida na huenda hawana hatia, tumuachieni mungu tu, kama tutaishi kwenye miti, sawa,…ndivyo tulivyokadiriwa, lakini siwezi kusimama mbele ya mahakama tena kusema kitu…..hapana, nieleweni jamani, ’sauti  ilimtoka huyo mama mjane ikiwa ni ya huzuni, niligeuka kumuangalia Dalali kama imemgusa, lakini nilimuona akishika kidevu kama anawaza jambo.

‘Ni sawa shemeji, hawa hawajui..angalia mtoto anavyoteseka, …mimi ninakuahidi shemeji utalala kwenye miti, nitahakikisha unapata nyumba yako, hata kama haitakuwa sawa na hiyo….haya tulishayamalzia, lakini sababu ya huyu…..’akaninyoshea kidole!

‘Basi inatosha msinyosheane vidole niambieni mlichoniitia, kama ni hivyo, basi mimi sina zaidi naomba nindoke….ila nasema hivi,..mume wangu hawezi …..sijui lakini ya mungu mengi, labda yeye mwenyewe atokeze asema ukweli,..sijui kwa vipi…lakini nimjuavyo mimi, sio kweli……sio kweli jamani, msimsingizie uwongo marehemu…’akasema na ilikuwa kama anataka kulia.

Dalali, akataka kusema neno, lakini sauti ikawa kama imempotea,  akageuza kichwaa kuangalia mbele, ni kama vile aliona kitu,…akawa anatizama mbele tu huku macho yakizidi ukubwa, ni kama alikuwa anatizama kitu na sote tukageukia huko anapotizama, lakini hakukuwa na kitu,…..aliyatoa macho yaliyojaa uwoga, huku akisema maneno haya;

‘Haiwezekani…., bro…haiwezekani…sio yeye, hapana, msinitishe, wanga wakubwa nyie, sikubali, sio yeye….’ halafu akainamisha kichwa chini, sijui alikuwa akiwaza nini, kwa hapo hatukujua ni nini alikiona, na hatukujua  maneno hayo  ya shemeji  yake yalimgusa  vipi, na kwa hali ile tukatulia tukimsubiria atuambie jambo, akawa kimia, kainama hivyo hivyo tu…
Je nini kilitokea….!

NB: Nawaomba muwe na subira, kuna mlolongo wa maswali na majibu,….Tukio hilo ndivyo lilivyokuwa hadi ukweli ukajulikana, bila hata kumuhusisha hakimu wa duniani,…tuwe na subira tuone somo na hekima cha tukio hili, soma katikati ya mistari utanielewa, tupo pamoja

WAZO LA LEO: Mwenyezimungu kwa kutupenda sisi waja wake,tunapokosea anatupatia muda wa kujirudi, na kutupatia nafasi  ya namna kwa namna iwe kwa maono yaliyodhahiri, au ya ishara , ili tu tuweze kutubu, wengine wanazidishiwa hata mali, lakini wengine hupata mitihani kama  maradhi nk.., ili tu tumkumbuke mola wetu, tutubu makosa yetu

Lakini kwa kibure chetu, na kujisahau tunatakabari, na kujiona ni wajanja, tumesoma, tuna mali, tuna nguvu, tuna cheo, warembo nk…na tunajiona tuna muda, wa kufanya lolote…tunajiona ni sisi ndio tumependwa zaidi, …walioondoka walikosea…nani kakudanganya!.
Ni mimi: emu-three

2 comments :

Anonymous said...

MKUU UPO?

Anonymous said...

If umekwama twaambie tukukwamue...we need your story very much.