Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Monday, May 2, 2016

YOTE MAPENZI YA MUNGU-3



  Ni wakati  ule mjane, ambaye namuita shemeji anataka kunipatia vielelezo vinavyohusikana na mkopo uliosababisha nyumba hiyo kupigwa mnada, …ndio wakati ule mtoto alipoanza kuumwa, hali ilimbadilikia ghafla, mtoto akaanza kutetemeka, kumchunguza joto lipo juu ….

Cha ajabu kabisa mtoto mwanzoni alikuwa mzima, hana dalili yoyote ya kuumwa, sasa anachemka homa, anahema kwa shida na ghafla mtoto akalegea, …akawa kama kapoteza fahamu…na muda wote huo tunahaha, mama anakwenda huku anarudi kashika kichwa, huku akisema ;

‘Mungu wangu…nimefanya nini,….. mungu wangu…..nisaidie…..’

‘Kwani tokea asubuhi alikuwaje…?’ nikauliza

‘Alikuwa mzima,..ndio hayo niliyokuwa nikikuambia, unaona sasa…sitaki haya mambo tena, sitaki jamani mtoto wangu jamani…..’akasema huku anapiga miguu chini..

‘Lakini hii ni homa…tena homa kali, sijawahi kuona hivi,.. tunatakiwa tumpeke haraka hospitalini….’nikasema

‘Wewe hujui tu…..nilikuambia, inakuwaga hivyo,…jamani sasa nitafanya nini…na shemeji ndio hayupo, yeye ndiye anajua la kufanya ikitokea hivi, …..ngoja kuna dawa huwa anampakaga, lakini sijui anafanyaje….kuna jinsi anamuombea mimi sijui…halafu…’akasema huku akitaka kwenda huko ndani, mara anarudi, alikuwa kachanganyikiwa kabisa.

‘Hiyo dawa iko wapi sasa….?’ nikamuuliza

Kwa hali ya huyo mtoto sikuona umuhimu wa kuendelea kukaaa hapo, mimi nilataka tumpeleke hospitalini, ….maana sasa lawama natupiwa mimi,….

Nikaona nipambane sasa kama mzazi, kwanza nikamfanyia huduma ya kwanza, kujaribu kumzindua, nikawa nakanda kanda yule mtoto na maji,…na kwa muda huo  mtoto alikuwa kalegea kabisa, ni kama vile kapoteza fahamu, hahemi kabisa, joto lilikuwa juu, sasa nashika miguuni ….nilishituka miguu imeanza kuwa ya baridi, ubaridi usio wa kawaida… mtoto kimia, hapo na mimi nikaanza kuogopa.

Kwa mashaka nikajaribu kuangalia mapigo ya moyo, ….hakuna kitu, mapiga ya moyo hayasikiki…mhh….sasa nimesababisha makubwa, moyoni nikasema  sasa ukiona mtu anafungwa ndio hapo, maana huyo mama kweli alinikanya, sikusikia,….nikasema;

‘Unajua shemu, ….huyu tumpeleke hospitalini…’nikasema

‘Nilikuambia,…nilikuambia..ndio haya yametokea sasa, unaona….jamani nitampoteza mtoto sasa…’...mimi sasa nikaanza kumuomba mungu, kwa duwa zote nizijuazo,  mtoto yupo kimia, ni kitendo cha muda mfupi, lakini jasho lilinitoka….

Hali ya mtoto ikawa haionyeshi dalilii yoyote, ya matumaini,  ….lakilini akilini wazo jemanililoliona ni kumpele lakini kwa vipi, ….

Na kabla sijasema lolote zaidi ndio mara  mlango ukagongwa, …

                                                                    *********

Mgongaji aligonga tu…kuashiria kuwa kuna mgeni,  lakini mlango ulikuwa wazi, huyo mgongaji akaingia, alikuwa jamaa mmoja kavalia suti safi yaonyesha ni bosi fulani au sijui…na, mkononi kashika briefcase, ni kama ofisa katokea safari  kutoka Ulaya, ….mimi kwanza sikujua ni nani,  ila huyo mama ndiye aliyeanza kusema;

‘Oh ahsante mungu, Shemeji karibu, ….aheri umekuja, mtoto kazidiwa tena….’huyo mama akasema akionyesha matumaini, mimi nilikuwa nimeganda,nikiwa sasa napoteza matumaini kwa mtoto…. lakini akilini nilitaka mtoto apelekwe hospitalini, nikijipapasa mfukoni sina kitu!. Patamu hapo…

Yule jamaa kwanza aliniangalia, halafu akasogea hadi pale nilipokaa na huyo mtoto, akamshika huyo mtoto shavuni kupima joto….alivyokuwa akifanya utafikiri docta, akatikisa kichwa kama kukubali kitu,…akamshika miguuni, akamuachia kwa haraka, …akaguna tu `oooh,…’

‘Imepita muda gani…?’ akauliza

‘Hata robo saa haijapita…’akasema shemeji yake.

Akashikanisha viganja vya mikono baada ya kuvipuliza, halafu akaviwekea viganja vyake kichwani kwa huyo mtoto,  akawa awewesa maneno, sikuweza kuyasikia vyema, mdomo ulikuwa ukicheza cheza tu, alifanya hivyo kwa muda, mtoto kimia, akamwangalia mama yake, akatikisa kichwa, akasema;

‘Mumefanya nini tena shemeji…mnataka kuua mtoto nyie…..Nipe ile dawa ya unga…..’akamwambia shemeji yake. Mimi simu ikawa inaiita lakini sikutaka hata kuipokea, ….

‘Pokea simu yako….’akaniambia, na mimi nikaitoa simu yangu kutoka mfukoni,  na kuiminya kupokea, ilikuwa ni maelezo ya vijana wangu kwa kazi niliyowapa kufuatilia maswala ya huyo mama, nikawa nasikiliza kwa muda, …nilichosikia kilinifanya nianze kuwa mashaka, nikamuangalia huyo jamaa akiwa anachezesha chezesha viganja vyake vya mkono, akivisugua sugua huku  na badaye kuvipuliza, akawa anafanya hivyo kwa muda

Mimi nikawa naendelea kusikiliza maelezo ya vijana wangu mmoja baada ya mwingine, halafu nikasema;

‘Nyie endeleeni…tutaongea baadaye,…nipo site…’nikasema na kukata  simu,

Nilitaka kuurudidhs ile simu mfukoni , lakini nikakumbuka kitu, … sasa akili ilishaanza kufanya kazi, nikajua sasa nipo kwenye mapambano, sitakiwi kupoteza kitu,  nikaiminya simu sehemu ya kurekodia matukio, bila jamaa kufahamu, nikaiweka ile simu kwenye meza.

‘Hizi simu kwa sasa nazona hazina maana, nimechanganyikiwa kuhusu huyu mtoto….’nikasema huku nikiiweka ile simu pale mezani.

‘Hiyo simu ya bei mbaya, unaweka hapo unaweza ukasaishau, na watu leo wanaingia humu ndani na kutoka…’akasema huyo jamaa akiitizama pale nilipoiweka.

‘Ni za kawaida tu…sitaweza kuisahau…nikisahau wewe si utanikumbusha au..’nikasema kama nauliza

Mara shemeji akaja na karatasi imekunjwa, kuonyesha kuwa kuna dawa ndani yake au kitu kimefungwa humo, akampa huyo shemeji yake, shemeji yake akaifunua na kutoa kitu kama unga unga hivi, kwenye vidole na kuweka puani mwa huyo mtoto, na mara huyo mtoto akapiga chafya, mara tatu…..

‘Tayari, keshaondoka huyo….’akasema

Baadaye akawa anasema maneno fulani huwezi kuyasikia vyema,…., akampaka Yule mtoto usoni ile dawa, halafu taratibu bila wasi wasi akasogea hadi kwenye sofa,  akakaa, na kukunja nne, yaani utafikiri docta anayejua anachokifanya,  inaonekana huyu jamaa ana majigambo fulani hivi.

Mimi nilikuwa bado nimempakata huyo mtoto, na Yule mtoto sasa akaanza kujitikisa na baadaye akawa anajiinua kutaka kusimama, lakini akawa bado hana nguvu, nikamsaidia kuinuka, akasimama…hapo nikapumua, eehuuuuh, …..

Mtoto akasimama akitaka kuinua mguu,  akawa anayumbayumba, nikajiinua kidogo na kumshikilia, bado nilikuwa sina imani, moyoni nataka tumpeleke huyo mtoto hospitalini. Nikasema;

‘Jamani huyu mtoto tumpeleke hospitalini…hii hali sio ya kukaa nyumbani’nikasema

‘Haina haja,…’akasema huyo jamaa, sasa nikainua uso na kumuangalia vyema huyo jamaa usoni, nahisi niliwahi kumuona mahali,…sikumbuki wapi, hata hivyo,kwa muda ule akili yangu ilikuwa bado kwa mtoto..

‘Huyu mtoto kwa hali hiyo inabidi tumpeleke kwa docta bingwa wa watoto, msiseme tu haina haja, mlishawahi kumpeleka huko  kwa docta bingwa wa watoto, kama tatizo kama hili huwa linajirudiarudia ujue kuna kitu anatakiwa kuchunguzwa….?.’nikauliza.

‘Hayo sio maradhi ya kupelekwa hospitalini, hata hivyo,…ni kweli mtu akiumwa, hasa mtoto inatakiwa kufanya hivyo, na sisi mwanzoni tulifanya hivyo, kwa vile tulikuwa hatujui na haikusaidia,…..’akasema

‘Kwahiyo….’nikasema na yeye akapiganisha viganja kama anajifuta  kitu  akasema

‘Kwahiyo….?, kwahiyo nini, haina haja kumpeleka hospitali,…, kwa hivi sasa yupo safi kabisa….’akasema huyo jamaa akiangalia dirishani, hana wasiwasi, ….

Na kweli  Yule mtoto sasa akawa kachangamka, akamwendea mama yake, na mama yake akamwinua na kumpakata miguuni mwake…., mama alimuangalia mtoto wake kwa macho yenye huzuni, …na mara machozi yakaanza kumtoka huyo mama, pale nilipo nilihisi hasira, sijui ni hasira za nini…nikageuka kumuangalia  huyo jamaa. Alikuwa sasa kashika simu, anachat, au …huku akisema haya maneno;

‘Hawa watu bwana….wanataka kuja kesho, duuh, sasa ninani , hapa ni mwenye kisu kikali, …..hawa watu wana haraka….ngoja tuone.’akainua uso na kumwangalia shemeji yake, akamuona shemeji yake machozi yakimtoka,  alipoona hivyo akasimama na kumsogelea shemeji yake, huku akisema;

‘Shemeji lakini si nilikuambia, … usivunje miiko, unaona sasa, unamtesa huyo mtoto bure,…kuna kitu ulitaka kukifanya, kweli si kweli…., ulitaka kufanya nini, au umefanya nini,?’ akamuuliza shemeji yake lakini shemeji akawa anatoa machozi tu.

‘Shemeji, wewe unajua kabisa,…. baba yake hataki mambo hayo, …si unakumbuka maagizo tuliyopewa…sasa haya ni matokeo yake, kwahiyo ukilia, haisaidii kitu kama hutatimiza hayo uliyoambiwa,….kutokutii hayo maagizo…itakuwa hivi, na sasa ni kubaya zaidi.’akasema jamaa

‘Samahan kidogo, umesema baba yake hataki, baba yake yupi hataki mambo hayo, baba yake si….., marehemu au ?’ nikauliza na kabla sijajibiwa nikauliza swali jingine…

‘Na hataki mambo gani?’ sasa nikawa nimemkazia macho huyo jamaa na huyo jamaa akaniangalia na kusema;

‘Shemeji anajua,…’akasema akionyesha dalili za kunishangaa, alinitizama kwa muda halafu akageuka kumuangalia shemeji yake.

‘Na mimi nataka kujua pia, maana hii sio hali ya kawaida…mtoto anakuwa hivyo, halafu ….hapana, niambieni tatizo ni nini…’nikasema kama mtu mwenye mamlaka

‘Kwanza wewe ni nani unayetaka kujua mambo ya nyumba hii?’ akaniuliza akigeuka kuniangalia, ilikuwa sauti ya msisitizo kama mwenye nyumba.

‘Mimi kama uncle wa huyo mtoto,….nataka kujua kwanini imekuwa hivi, mtoto alikuwa mzima ghafla akaanza kuumwa, na wewe umekuja, umemshika kichwani akapona,….na hutaki tumpele hospitalini,  kuna nini kinaendelea kwenye nyumba hii,… , hebu dada niambie..’sasa nikajifanya ni kaka wa huyo mama, ili niweze kufanya mambo yangu.

‘Ndio hivyo, kama ulivyoona, inaniuma kwa kweli,lakini nitafanya nini, ni hivyo kama ulivyoona akianza kuumwa hapo ni …aah, inakatisha tamaa, sasa sijui, kama ni hiyo mizimu sijui, kwanini iwafuate watoto wangu…, hawa watoto masikini ya mungu wana makosa gani, …wangenifuata mimi basi, si mimi mkosaji, basi iniandame mimi, sasa..sasa…kwanini wananitesea watoto wangu….’akasema huyo mama kwa uchungu.

‘Anayewatesa watoto ni wewe usiyetaka kuelewa shemeji, mimi nilishakuambia hilo, hiyo ni mizimu, huyo ni baba yake, hataki maswala hayo unayoyataka kuyafanya wewe….., nilikuambia kabisa achana nayo, naona kama ulitaka kufanya kitu, unataka kufanya nini wakati kesho hawa watu wanakuja kumalizia tatizo,…hivi nikuulize wewe unaona nyumba hii ina maana sana kwako,…’akasema akionyeshea kidole kuzungusha akielekezea juu.

‘Shemeji, hawa watoto wakipata shida watakuja kukulaumu wewe kwa kuangalia mali zaidi,..muhimu ni afya yao, muhimu ni uhai wao,…hivi huyo mtoto akifa, hatuombei mabaya, lakini kwa jinsi tulivyoambiwa, ukichelewa tu,….ukiendelea kufanya hivyo mara tatu, ikamtokea mara zaidi ya tatu, mtoto utamkosa, sasa utakuwa na furaha gani, hata ukiipata hii nyumba na mtoto keshakufa….hutakuwa na raha yoyote…’akasema huyo jamaa.

‘Samahani  kidogo hapo…, ni nani atamuua huyo mtoto ndio hiyo mizimu, au….mimi nijuavyo mtu akifa anakufa kwa mapenzi ya mungu au sio,…’nikasema na huyo jamaa akanitupia jicho la dharau, halafu akasema;

‘Lakini ….eeh,  wewe mwenyewe  si-umeshuhudia hapa, huyo mtoto alikuwa na hali gani, , ….jinsi mtoto alivyobadilika, si uliona, sasa nikuambie kitu, sisi hayo, tulihangaika nayo, mpaka basi, hebu jiulize, ….je sasa nisingelitoka kwa muda muafaka ingekuwaje, hebu niambie  unafikiri kingetokea nini hapo, walisema ikitokea hivyo, mtoto akaachwa saa moja,…basi…tunakwenda kuzika’akatikisa kicha kusikitika

‘Kweli…..?’ nikasema

‘Ndio, akiwa katika hiyo hali, damu imesimama,…akaachwa zaidi ya saa moja akiwa kapoteza fahamu, ndio basi tena, ….na hii ya kupoteza fahamu ni dalili mbaya, mwanzoni alikuwa hapotezi fahamu , ni joto tu kuwa kali, sasa hii,…ya kupoteza fahamu kutokana huyo mtaalamu alivyosema hiyo ni dalili mbaya shemeji …achana na hiyo tamaa, nyumba, nyumba ….nyumba kitu gani mbele ya uhai wa mtoto ,….’akasema akimuonyeshea kidole shemeji yake.

‘Lakini sijafanya kitu shemeji….huyu ….huyu , she-, eeh, kaka yangu, alikuwa akiniulizie jinsi gani tulivyofuatilia, nikataka kumuonyesha jinsi tulivyohangaika, sasa…..’shemeji akamkatiza kwa kusema.

‘Shemeji hao jamaa hawadanganyiki,..unajidanganya mwenyewe…’akasema , halafu akanigeukia na kusema.

‘Jamaa gani hawadanganyiki..?’ nikauliza

‘Mizimu….’akasema na kabla sijamuuliza swali jingine akasema;

‘Unajua ndugu, Sisi  tumemuhangaikia sana  na huyu mtoto na ndio tukaambiwa ni baba yake hataki maswala ya kesi, …na baya ni kuwa kaondoka duniani akiwa kaacha deni, hilo deni linamtesa, kwahiyo anataka hilo deni lilipwe kwa gharama yoyote ile,….ili yeye aweze kupumzika huko alipo, kauli ya marehemu ni muhimu sana, maana hatujui huko anapata shida gani….., sasa huyu shemeji yangu sijui haelewi…’akasema

‘Ohooo kwahiyo kumbe, nilikuwa sijaelewa, ….kwahiyo kumbe mtoto alipoanza kuumwa ndio mkaenda kwa mganga,au sio? Si ndio hivyo au? Na huko  mkaambiwa kuwa tatizo lake sio la hospitalini, ni maswala ya kimila, au sio…?’ nikauliza na kujifanya nipo pamoja na yeye

‘Haswa,…..lakini hatukuanzia kwa mganga, hapana…..wewe, usininakili vibaya,…sisi sio watu wa namna hiyo…kwanza tulihangaika na mambo ya hospitalini, kila akipimwa hana tatizo, mtoto anazidi kuteseka, homa haishuki….mtoto anaweweseka, wengine wakasema ni degedege, wengine UTI, naimonia na nini sijui ..lakini kwenye vipimo hakuna kitu kama hicho….wakatibia aah wapi, …..’akaonyesha kwa kidole mdomo akitamka hiyo `aa wapi…’

‘Ni kama ulivyoona leo, ….je nikuulize wewe , ulipokuja hapa ulikuta huyu mtoto anaumwa….?’ Akaniuliza

‘Hapana alikuwa mzima kabisa…sikumuona na dalili yoyote ya kuumwa…..’nikasema

‘Sasa umeona, kuna mambo yakifanyika mambo amabyo yanakwenda kinyume na matakwa, maagizo tuliyopewa, miiko….mtoto huyo huanza kuumwa,…’akawa anachezesha mkono kama anaongea jambo, lakini sasa akawa  hatamki neno baadaye akasema;

‘Ujue  na sisi awali tulikuwa hatujui hilo….tunahangaika huku na kule, hospitalini ,dawa hizi na zile…wakati  tunafuatilia, maswala ya mkopo, maswala ya deni, kumbe hayo ndio tatizo,hatujui masikini,, twauliza huyu mtoto ana nini, mbona hivi, mtoto anaumwa haponi….homa inageuka sasa kama anapandisha mashetani, mtoto mdogo apandishe mashetani, wapi na wapi, ….tuliona ajabu sana….hospitalini akipimwa, hana ugonjwa,…’akatulia

‘Mara kwa bahati akatokea mzee mmoja, akasema nyie huyu mtoto mpelekeni kwa mtaalamu,…kwa mtaalamu!, ….’akasema akitamka neno hilo la mwisho kwa mshangao.

‘Ndio….tukabakia kuulizana ni nani huyo mtaalamu…. Unajua tena sisi wa siku hizi  mambo ya waganga wapi na wapi….lakini sasa tufanyeje, na mimi ndiye baba yao, nikamwambia shemeji hilo…shemeji naye ndio mambo hayo hayajui kabisa, …nikaona na yeye anasita sita, Mimi nikaona hakuna jinsi, mimi ni baba yake…nikaanza kazi ya kuulizia,maana hao watu wapo wengi, na wengine hawaaminiki…nikampata anayestahiki….’akaonyesha mkono wa kishujaa akiwa kakunja ngumi.

‘Na kwa bahati nzuri kipindi hicho hapa nyumbani kulikuwa na ndugu yake shemeji, yeye alikuwepo hapa kumsaidia dada yake…yeye ni mkubwa kwa shemeji, ana akili za utu uzima akajitolea kwenda na mimi, ….tukaondoka naye…kama angelikuwepo mungemuuliza vyema yeye, ….maana mimi nikisema mtaona labda aah...lakini ujue mimi ni baba yake  mdogo, mimi ni mzazi wa mtoto pia, nina uchungu zaidi….’akatulia

‘Ni sawa nakuelewa, ikawaje….’nikasema

‘Sasa tulipofika huko…ubosi ukanitoka, si unajua tena mambo ya huko, yalivyo, kuna msharti sharti, ukifika utajionea mwenyewe, … ikanibidi …nikakalishwa chini, kuna vitu vya ajabu ajabu unatapakwa mimi hapo ni mzazi wa mtoto…. utafanya nini tena hapo, huko ndio tukaambiwa tatizo ni hilo….’akatulia

‘Mliambiwa tatizo ni nini….?” Nikauliza na yeye akatikisa kichwa na akawa kama anacheka

‘Kama nilivyokuambia awali, kuwa marehemu kaacha deni,…na marehemu anataka deni  hilo lilipwe, na kingine yeye hataki mambo ya kesi kesi,hapendi kesi na kweli toka kaka akiwa hai huwa hapendi maswala ya kesi kesi….lakini cha muhimu ni kuwa…hilo deni lilipwe kwanza, sasa kama kutakuwa na jingine la kutuhusu sisi wa duniani, haya, lakini kwanza deni..’akatulia

‘Ni nani anasema hivyo…?’ nikauliza

‘Wakati huo anayeongea ni huyo mtaalamu, lakini akiwa kapandisha na sauti tunayosikia kwa muda huo ni sauti ya marehemu kaka, ….’ooh, waungwana, nawaambia nimeondoka duniani nikaacha deni, hilo deni linamtesa huku nilipo…fanyeni kila mbinu lilipwe haraka….’  Akawa anaigiza sauti nyingine.

‘Mimi pale sikujivunga, maana nitadanganya, nitapatia wapi hizo pesa zote…nikasema hatuna  hizopesa tufanyeje, …deni hilo ni kubwa sana, …sauti ikasema ‘hata kama ni nyumba  iliyokuwa yangu, na iuzwe ili deni lilipwe haraka,….vinginevyo,…’hapo akasita halafu akasema

‘Sauti ikasema , ikatoa onyo kuwa hilo deni lisipolipwa haraka, … mmoja baada ya mmoja ataondoka….’akatulia akimuangalia shemeji yake.

‘Hiyo ilikuwa lini,…?’ nikauliza huku naangalia saa maana nilitakiwa kukutana na watu wangu, kuna jambo walitakiwa waniambie.

‘Lini kwa vipi….?’ Akaniuliza na yeye akiangalia saa yake

‘Yaani  ni muda gani tangia hilo tatizo la mtoto lianze?’ nikauliza

‘Mhh, eti shemeji, nisaidie hapo…hivi, mtoto alianza hayo matatizo lini,maana sikumbuki, mambo yamekuwa mengi, mara yeye ….unajua hata kuumwa kwa shemeji, kumbe mambo ni hayohayo, hatukujua, yalianzia kwake…..shemeji hali yake ilikuwa mbaya sana,..sasa kidogo unamuona hivyo , tena sio kidogo, unaona anatembea sema ….yupo imara kiimani, …..muulize mwenyewe ilikuwaje…’akasema

‘Ok,…sasa mimi nauliza kuhusu huyu mtoto kuanza kuumwa ilianza lini,…..?’ nikauliza huku naangalia simu pale mezani niliona kama imezima..lakini mara nikaona ishara kuwa bado inafanya kazi.

‘Tuseme eeeh…mimi nafikiri, hata mwaka haujaisha, ni karibuni tu, yalipoibuka haya maswala ya kesi kesi au sio shemeji.. ….’akasema akimuangalia shemeji yake.

‘Yalipoibuka hayo maswala ya benki au sio,shemeji yako alipojua kuwa kuna deni na nyumba inatakiwa kupigwa mnada au sio.. na hasa alipoanza kufuatilia, au sio…na alipokwenda polisi wakachunguza wakagundua kuna jambo nyuma ya pazia, kuhusu hilo deni,….sasa hapo mizimu ikaibuka,  wameona dili inataka kufichuliwa, au sio…?’ nikauliza

‘Unataka kusema nini hapo, sijakuelewa….?’ Akauliza akiniangalia usoni, niliona hali ya mashaka i machoni mwake.

‘Unasema huko kwa mganga ulikwenda na  ndugu yake shemeji, ni nani huyo.?’ nikauliza kama vile nawafahamu hao ndugu zake shemeji yake wakati hakuna hata mmoja ninayemfahamu lengo nikimuweka huyu  jamaa sawa asinishutukie mapema.

‘Kuna ndugu yake mmoja, …nimekuambia ni mkubwa wake shemeji,…shemeji, hebu mwambie ni nani,…maana sasa naona nimechoka kuongea, tatizo unauliza maswali kama polisi, hao polisi wenyewe walinisumbua wee mwishowe wakasalimu amri….’akatulia

‘Polisi waliniuliza maswali.., utafikiri mimini mhalifu, hawajui kuwa mimi ni mzazi wa hawa watoto, nina uchungu zaidi ya wanavyofikiria wao, na. unauliza kuhusu huyo ndugu yake shemeji, …huyo ndugu yake shemeji tulikwenda naye…akaona hivyo vitu vya huyo mtaalamu,…na tulipofuatilia wanavyotaka wao hali ikawa nzuri, muulize mwenyewe shemeji , mtoto akawa na afya yake nzuri tu, sasa nahisi kaanza tena, keshasahau…’akasema

‘Ninachojiuliza ni kwanini hayo yatokee kipindi hicho,  kipindi hiki yaani… kwanini hayakutokea huko nyuma, kwasababu  ….mume wa dada alifariki muda, au sio..sikubahatika kufika hapa…, lakini ni muda sasa, kwanini hayo matatizo yakudai kuwa ana deni, hayakutokea kipindi  cha nyuma baada ya mume wa dada kuondoka, yaje kutokea wakati shemu anatafuta ukweli…si kumepita muda, eti…hapo ndio  nauliza?’ nikauliza

‘Sasa hayo mimi sijui….kamuulize huyo shetani anayemtokea huyo mtoto, ukiniuliza mimi…nitakuambia nini, … nitajuaje hayo ni kwanini, marehemu huko anajua ni kwanini,huenda katika kuhojiwa ndio ilikuwa imefikia muda muafaka wa hilo swali, …’akasema

‘Kwahiyo huyo anayemtokea huyo mtoto ni shetani..?’ nikauliza

‘Sasa utamuitaje,….eeh, hebu niambie wewe,….’akasema akiniangalia, halafu akasema;

‘Na ujue , haya mambo ni ya ajabu sana, unajua  marehemu anaweza kujitokeza kwa njia yoyote ile ili kuleta ujumbe wake…unaweza ukamuota kwenye ndoto, hiyo ni ahueni…na  hawezi kujitokeza mwenyewe,  si unajua hilo, maana akijitokea mwenyewe…ooh,  si tutakimba, kwahiyo yeye kaamua kujitokeza kwa kupita kwa mtoto wake...’akasema

‘Huyo Shetani sio,….?’ Nikauliza

‘Eeeh bwana, ….hunielewi…na sauti tuliyoisikia ni ile ile ya kaka, mimi naijua vyema …’akasema.

‘Lakini si umesema ni shetani, au nimekosea, kinachomtokea mtoto ni kama mashetani, ulisema hivyo,..na nijuavyo mimi, shetani huwa hashauri  mambo mema au sio, anaweza kushauri mambo mkayaona mema kumbe yana mtego, yana ajenda ya siri..?’ nikamuuliza na kuelezea hivyo.

‘Inategemea na aina ya shetani kuna….kuna, hayo madudu yanakuwa mazuri, yanakuja kwa nia njema,…mizimu, hapo tunazungumizia tuseme mizimu, naona nikitumia neno shetani, unakuwa huelewi,….ni mizimu,kuna yenye nia njema na mbaya na pia wengine wanaweza kufanya yote mawili, wao si wana uwezo huo, ..’akasema

‘Nikuulize kitu kwanza ili tuwekane sawa, naona unabadili maelezo yako ya awali kuhusu shetani, ni wapi wamesema hivyo,maana kwa vyovyote utakavyowaita ni hao hao, mizimi, vibwengo, hao wote ni mashetani,…mimi nijuavyo kwenye vitabu vya dini shetani ni muasi,shetani aliasi , alikataa amri ya mungu ndio akaamua kutupoteza na sisi wanadamu, au sio….sasa iweje tukubali maagizo yake, na yeye alivyo ana mbinu nyingi, anaweza kutumia mbinu kadha wa kadhaa…?’ nikamuuliza na maelezo juu.

‘Sasa huko unapokwenda, aah,…. mimi sio mtaalamu nako, sina ufahamu huo ….mimi nafuatilia aliyosema huyo mtaalamu…yeye anajua yote,….yeye hiyo ni fani yake, na kuhusu kasoma sana, dini anajua, alituchambulia maandiko  wenyewe tukaduwaa, kwahiyo sio kwamba hajui dini, anaijua vyema na hata wewe ukienda ukamsikiliza utajua kuwa kweli anafahamu yote, …au nikupeleke kwake, ukamsikie mwenyewe, kama hutaamini…….’akasema

‘Huyo mtaalamu unamuamini vipi…maana mtu na biashara zake bwana, ni lazima atajua jinsi gani ya kumteka mteja wake akili, si anataka kuvutia wateja wako…., sasa wewe ulimuaminije, unamfahamu vipi,…najua wewe ni dalali, unajua hayo au sio?’ nikamuuliza na nilipotaja neno udalali, nikaona anashtuka! Nilishamkumbuka huyu jamaa pamoja na kazi nyingine pia anafanya kazi ya udalali.

‘Hayo maswali gani sasa,….sisi tulichotaka ni mtoto kupona…unaona ndugu, hayo ya udalali yanakujaje hapa…sisi tulihangaikia mtoto, na katika kuulizia tukaambiwa kuhusu huyo mtaalamu, ndio tukaenda kwake,…ndio hapo na mimi nikamfahamu, ina maana mimi nilifanya vibaya , kwa vile mimi ni dalali, au una lako jingine, na kwanini unachunguza chunguza, ili iweje,…hebu niambie unataka nini…unanishuku….?’akasema sasa akionyesha kubadilika.

‘Hapana, …sina nia mbaya na wewe …najua wewe ni mzazi wa huyu mtoto na ulitakiwa kuhangaika sana, nashukuru kwa hilo, maana hata kwa jinsi ulivyoweza kumtibia huyu mtoto hapa, ooh, nimekuaminia…sasa mimi nataka unielewe,….hili tukio kwakweli limenigusa sana, ndio maana nataka kujua hatua kwa hatua, ili nisije kuhangaika na mimi, wakati wewe ulishafanya jitihada….’nikasema kumweka sawa.

‘Ndugu ..unajua nyie watu mnaojifanya wazungu , au nisema wa kileo, nikiwemo mimi, ….mnasahau mambo ya kimila, wazee wetu hawakuwahi kwenda shule kipindi hicho, walikuwa wanajitibiaje…?’ akawa kama ananiuliza hakusubiria nijibu akasema

‘Wazee wetu, walikuwa wanajuaje matatizo yao, ni kwa njia hizo, tunazozipuuza ….kulikuwa hakuna hospitali, hospitali ni kwa wazee wetu ilikuwa kwa hao wataalamu, waganga wa kienyeji,…na wao dawa zao zaidi ni miti shamba, na kufuata masharti fulani fulani….na zaidi walikuwa wakifuata mizimu na mambo yao yalikwenda vyema , hebu angalia hivi sasa  na usasa wetu…., mambo ni magumu,maisha ni magumu….sababu ni haya  maswala ya kupuuza mambo ya mila..’akasema sasa akiongea kwa utaratibu.

‘Kwahiyo wewe kwa hivi sasa unafuata mambo ya mila, unaabudu mizimu, na naona umekuwa mtaalamu na wewe au sio?’ nikamuuliza

‘Sijasema mimi nafuata mambo hayo, wala siabudu mizimu, lakini mambo yakizidi inabidi …na katika kufuatilia haya ndio nikajifunza kuwa kumbe haya mambo  yapo, maana huyu sio wa kwanza kwenye familai yetu kuna ndugu wanapandisha hayo mapepo, ….tulihangaika sana, tulipofuatilia tukaambiwa tulikiuka miiko,…mila fulani fulani… tukafanya walivyotaka hao mizimu…’akatulia

‘Kwa huyo huyo mtaalamu…?’ nikamuuliza

‘Hapana alikuwa mwingine…huko kijijinu kwetu…’akasema na kabla sijamuuliza swali jingine akaendelea kuongea

‘Na mizimu ni mababu na mababu zetu uelewe hilo….ndiyo haya yanamsumbua mtoto, lakini hilo la deni lipo wazi, ni kweli kuna deni, kaliacha kaka, na deni hata kidini latakiwa kulipwa hata kabla marehemu hajazikwa, sasa sisi hatukuljua hilo deni ndio maana hata mimi niliposikia hivyo nikaamua kufuatilia..’akasema

‘Wewe ulipojaribu kufuatilia kulitokea nini kwa watoto wako…au ….maana si hivyo, ulikiuka miiko,au sio… kwa muda huo…ni kitambo etu.., sawa si sawa, kwanini kusitokee kitu kama hicho muda huo, hapo ndio najiuliza, unaweza kunijibu hilo…?’ nikauliza na yeye akatikisa kichwa kama kusikitika.

‘Unajua wewe hunielewi….na nimekumbia maswali mengine yapo juu ya uwezo wangu, ni kwanini, hayakutokea muda huo eeh, sijui nini…, mimi siwezi kujua….mimi sina ujuzi huo, labda turudi kwa huyo mtaalamu tukamuulize…’akasema

‘Ok,ok…naona muda unakwenda, …kwahiyo wewe unajua jinsi gani  ya kumfanya huyu mtoto apone… hiyo hali ikitokea, kama ulivyofanya hapa kwa mtoto, kwanini hukumfundisha shemeji ili ikitokea na yeye afanye hivyo..?’ nikamuuliza

‘Ndio mimi najua na ni mimi tu naweza kufanya hivyo, yeye hawezi, maana …kuna miiko hapo, sasa siwezi kukuambia zaidi hayo ukitaka utaambiwa na huyo mtaalamu , nafuata alichoniambia, ….’akasema

‘Miiko…kwenye kutibia,….sasa ukifa je…?’ nikauliza

‘Huyu mtaalamu alinielekeza, kuwa hali hiyo ikitokea, na….haitokei mpaka mtu akifanya yale yasiyotakiwa, akikiuka miiko,..na nikuambie ukweli, pindi hilo deni likilipwa, hakutatokea tena kitu kama hicho, tatizo hapa ni hilo deni, ndivyo alivyosema huyo mtaalamu…kwahiyo mimi silali, nahangaika huku na kule kuhakikisha hilo deni limelipwa…na hakuna njia nyingine maana hiyo pesa ni nyingi sana…’akasema

‘Kwahiyo hilo deni, una uhakika aliliacha marehemu au sio?’ nikamuuliza

‘Ndio, hajakuambia dada yako…si umesema huyo ni dada yako, hajakuambia…hata yeye hakulijua, lakini tulifuatilia tukawa na uhakika huo..’ akasema

‘Mimi kiukweli bado  nina mashaka na hilo deni,..’nikasema

‘Una mashaka …!?’ akanikazia macho, mimi nikatulia kwanza sikusema kitu, na ndio akaendelea kuongea

‘Una mashaka gani, ni sawa hata sisi tulikuwa na mashaka hayo, siwezi kushangaa, lakini ili kuyaondoa hayo mashaka, nenda kafuatilie benki, sisi…mimi mwenyewe nilihangaika kufuatilia hilo, nikachemsha, maana hatujua ,  na hata shemeji naye akajaribu akachemsha,…’akatulia kidogo

‘Tatizo kaka alichukua mkopo huo bila kumwambia mtu, na matokea yake ndio haya, na mbaya zaidi ukifuatilia unamuumiza mtoto, unaona jinsi ilivyokaa vibaya…muhimu hapo kwasasa ni kulilipa hilo deni…’akasema

‘Kwahiyo kwa msimamo wako, kwa hekima zako, wewe umeona ni vyema  tuache, nyumba ipigwe mnada, ili lilipwe hilo deni….huoni kuwa tutakuwa hatujawatendea haki hawa wanafamilia, mama na watoto wake?’ nikauliza

‘Hii ilikuwa nyumba ya marehemu na yeye ana mamlaka ya kufanya apendavyo,…si ilikuwa nyumba yake, na  maswala ya watoto wana riziki yao, haikupangwa iwe yao, mungu atawajalia watapata ya kwao, hata mimi sio kuwa napenda iwe hivyo, hiyo ni amri ya benki, kama kuna namna nyingine tusaidie wewe, au niambie sisi tutapatia wapi hiyo pesa…?’ akasema

‘Mimi sijakataa ..maana kama imefikia hapo ina maana ulijitahidi kutafuta njia nyingine ukashindwa,…na kama mkopo ulichukuliwa ina maana kulikuwa na namna,  mtu alijua ataurudisha kivipi,, au sio…na kwa vile hamkuwa na taarifa ya huo mkopo, mtakuwa vile vile hamjui jinsi gani ya kuurejesha  au sio…l?’

‘Ndio…’akasema akitikisa kichwa kukubali

‘Ndio hapo mimi ninakuwa na mashaka na huo mkopo, yawezekana huyo kaka yako hakuchukua huo mkopo…kama aliuchukua mkewe angejua, wewe ungejua, na kungekuwa na mradi…kitu cha kuzalisha, je miradi ya marehemu ipo wapi…?’’nikauliza.

‘Hakuna mradi kama mradi alioacha,…nijuavyo mimi, miradi yake ilikuwa ya kuchukua mizigo anauza, mzigo ukiisha anakwenda kuchukua mwingine ni hivyo tu…na akiba akawa anaweka benki…na ni pesa ndogo tu tuliyoikuta benki, ina maana alipoondoka alitoa pesa karibu yote, kwenda kuchukua mzigo, akijua akirudi, atapata fadia kubwa….’akasema

‘Hapo sasa ndio naona kweli yeye hajachukua huo mkopo…kuna namna, kuna mtu kachukua huo mkopo kwa ujanja, …..’nikasema

‘Kwanini unasema hivyo, ….hahaha, eti hakuchukua huo mkopo …’akacheka kwa dharau,

‘Wewe unasema alichukua pesa iliyokuwa benki karibu yote kuchukulia mzigo, huo mkopo mkubwa hivyo ulikuwa ni wa nini…?’ nikamuuliza hapo akasita kidogo.

‘Huenda alichukua kwa shughuli nyingine, hatujui….’akasema  ‘ unasema labda kuna mtu mwingine alichukua, hebu niambie, huyo mtu mwingine angelichukuaje,…unakuwa kama hujasoma bwana, mkopo uchukuliwe benki na mtu mwingine uwekwe kwa mtu mwingine, kwa vipi…wewe kweli sikuelewi,…nakutilia mashaka na elimu yako….au huwaamini  watu wa benki au….’akasema

‘Nitakuja kukuonyesha kuwa kweli mimi nimesoma wewe subiria tu, ila kwanza nataka uelewe kuwa hata huko benk kunaendeshwa na watu, na watu wote sio sawa, na kuna ushahidi huo, nitakuja kukuonyesha hilo, ila kwasasa nakuambia hivi,…nina mashaka kabisa hilo deni halikuchukuliwa na kaka yako….’nikasema

‘Hilo sasa ni jipya, …hahaha…wewe mtu wa ajabu kweli, nyie ndio mnaopenda kuzusha mambo…, hata wapelelezi wa polisi hawakuwahi kusema hivyo,….’akasema

‘Wao walisema nini…?’ nikamuuliza

‘Wao walihisi kuwa mimi nilikuwa najua hilo deni , maana deni lilishathibitishwa kuwa lipo…ya kuwa kaka  kweli kachukua, wao wakahisi kuwa huenda  mimi nafanya mbinu labda, ili hilo deni lifutwe….sasa wewe unasema kaka hakuchukua, hizo hati alizosaini, kila kitu kipo wazi, mimi nimeona sahihi yake….’akasema

‘Sahihi inaweza kuchezewa na wajanja….’nikasema

‘Kwa vipi, sahihi, dole gumba je…mimi sikuelewi ukisema hivyo, …sasa hebu niambie alichukua nani, hebu niambia wewe, kama benk wameleta vithibitisho, hebu na wewe leta vya kwako, ili tuone kama kweli sio deni halali…tusaidie kwa hilo, tutashukuru sana, na ujue hapa tunapambana na muda, kesho, mnada..kesho ni mnada, hata shemeji anajua…na jingine tunamtesa mtoto…’akasema

‘Huo mnada hautafanyika…’nikasema

‘Eti nini, hautafanyika, nani kakuambia, wakati kila kitu kipo tayari, unajua mimi sijakuelewa wewe mtu, ni nani na unataka nini, una ushahidi gani kuwa hilo deni sio la kaka, kwa vipi, wewe unanipotezea muda wangu hapa bure, huo ushahidi upo wapi….?’ Akauliza kwa mshituko

‘Kwanza tunachotaka kujue ni ukweli wa hilo deni, hilo deni lina mashaka,…na ukweli huo tunataka kujua kuanzia kwako, kwasababu wewe ndiye uliyepewa dhamana,…., kwahiyo ili kusaidia hilo, ili tujue huo ukweli, tunataka wewe ujibu maswali yetu ya msingi, na baada ya hapo nitakuonyesha hivyo vidhiti unavyotaka wewe, na hivyo tutavipeleka mahakamani…’nikasema

‘Sasa wewe….unataka kuleta matatizo mengine kabisa…’akasema akimuangalia shemeji yake, na ilionyesha keshaingiwa na wasiwasi, mimi nikamtizama anavyobadilika,…hawa watu wanaoishi kwa ujanja ujanja kuna namba ya kuwapatia,….ukweli tu…na hapo nikawa na uhakika na shuku yangu.

‘Nataka unijibu maswali yangu ya msingi…..upo tayari muheshimiwa..?’ nikamuuliza

‘Wewe uliza hayo maswali yako, na… nataka unionyeshe hivyo vidhiti, tusipotezeane muda hapa lakini, unaona hali ya huyo mtoto , mimi sitaki tena hiyo hali  imrudie, ujue hiyo hali ikimrudia tena mimi sina uwezo wa kufanya lolote, ndivyo mtaalamu alivyosema, hata angekuwa nani, hawezi kumsaidia tena..tutampoteza mtoto kwa uzembe wenu, mimi sipo ….’ Akageuka kumuangalia shemeji yake

‘Shemeji unaona hawa watu, wanataka tumpoteze mtoto,..upo tayari kwa hilo,yale mambo ya kesi ambayo tulishaambiwa hayatakiwi mpaka deni lilipwe, hawa wanataka kuyarudisha tena, jamani, hivi…mali, nyumba, ina tahamani gani mbele ya mtoto, haya, shemeji mwambie, usije kunilaumu mimi,  ..’ akasema akimuangalia  shemeji yake, na shemeji yake alikuwa kainama chini tu. Mimi nilikaa kimia nikimuangalia tu.

‘Shemeji hawa watu hawajui tunavyoteseka na huyo mtoto, na hiyo hali ikijirudia titafanya nini, mimi nanawa mikono yangu,  mimi ni baba yake lakini kutokana na mtaalamu, sitaweza kufanya lolote tena…unakumbuka ulivyoambiwa,….?’ Akamuuliza shemeji yake na shemeji yake akahema kwa nguvu, lakini hakusema neno.

‘Ingelikuwa nimekwenda mwenye ungesema labda, lakini  ndugu yako mwenyewe ambaye alisikia maneno kutoka kwa huyo mtaalamu, alikuambia hilo na kukusitizia,…usije kukiuka hiyo miiko,…mwisho ni mara tatu, basi….sasa jiulize ni  hii ni mara ya ngapi….’akasema na simu yake ikatoa mlio wa ujumbe wa maneno, akaitizama

‘Sasa ….., unaona  eeh,….’akawa anasoma huo ujumbe, na akatikisa kichwa kama anakubali kitu.

‘Shemu, unaona sasa mtoto joto likipanda anafikia kupoteza fahamu, jamani hebu tusaidiane kwa hilo….tafadhali ndugu zanguni, mimi inaniuma sana, mimi sasa ndiye baba yake, ni lazima niwe kama kaka,….mnielewe jamani,  shemeji hebu mwambie huyu ndugu yako ohoo, hayeni...’akasema akimwangalia shemeji yake

‘Sasa kwani tatizo lipo wapi hapa,  kwanini unaogopa hayo maswalii yangu,  mbona unakuja juu kama unajihami, una wasiwasi gani, mimi kwa kuulizana hayo maswali tutakuwa tumekiuka hiyo miiko…ina maana hiyo miiko inasema tusiulizane maswali, tusitake kujua ukweli, kama ni hivyo basi kuna kitu…au unaniogopa, …?’nikasema

‘Nakuogoa….hahaha, nikuogope nini wewe…., kwanini nikuogope…kwani wewe nani, utanifanya nini mimi eeh, …eti nakuogopa, uliza…..’akatulia kwanza

‘Hivi,….unafikiri mimi ….hiyo kauli yako sijaipenda, sasa, nasema, uliza hayo maswali yako yote na mimi nitayajibu moja baada ya jingine, uliza….hivi unanionaje mimi, ’akakaa vyema. Na mara nikamuona shemeji akimshika Yule mtoto shavuni, na akaonekana anakunja uso, kuashiria kuna tatizo…..

NB: Nisiwachoshe kwa leo tutaendelea sehemu ijayo,ni mwendo wa maswali na maswali yalikuja kubaini ukweli,lakini mtoto je……tuwemo kwenye sehemu ijayo.


WAZO LA LEO: Mbinu za mnafiki ni fupii tu….ni kumwambia ukweli!
Ni mimi: emu-three

2 comments :

Anonymous said...

Kiss niko hot kinasisimua

Anonymous said...

Miram usichoke Baba tupe kiss kinafundisha Sana Kuna watu wanatamaa Sana.Mungu msaidie mjane Wako maana WW ndo mume