Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Friday, April 22, 2016

YOTE MAPENZI YA MUNGU (duwa ya mwenye kudhulumiwa)


                                                      
                                      YOTE NI MAPENZI YA MUNGU
                                              (Duwa ya menye kudhulumiwa)
‘Mama sasa sisi tutakwenda kuishi wapi, nyumba yetu ndio hiyo inauzwa,…kwanini lakini wanatufanyia hivyo…?’ ilikuwa ni sauti ya  mtoto yatima

‘Nimeshawaambia, haya yote ni mapenzi ya mungu,  iliyobakia tumuachie mungu mwenyewe, yeye ndiye atajua tutaishi wapi…’akasema mama mjane kwa huzuni, …wakiwa wamekaa wakisubiria  nyumba ije kupigwa mnada, kisa ni kutokana na deni , deni lilikopwa benki

Je watu hawa watakwenda kuishi wapi, mama mjane na  watoto wake…, je hili deni lilitokea wapi, maswali haya yalinifanya niingilie kujua undani zaidi wa kadhia hii na ndipo nikagundua makubwa ualiyokuwa nyuma ya pazia. Ama kweli yale yote  yanatotokea juu ya uwezo wetu , yote ni mapenzi ya mungu…

Tukio hili na kauli hizo hapo juu ziliniandama sana kichwani na ndio nikaamua nikiwekehiki kisa ili tuweze kupata fundisho sote, Inshallah…
                                                       *********

‘Mnada ,mnada ….kesho ndio kesho,  kwa idhini tuliyopewa na mahakama, kesho tuna mnada mkubwa wa hadhara, wa kuuza nyumba kubwa ya kisasa, ili kulipia deni la benki… fika ujionee mwenyewe…., fika ununue nyumba ya kisasa yenye kila kitu, ikiwa na uwanja mpana, na sehemu kubwa ya kuegesha magari…’ aliendelea kutoa wasifa wa nyumba hiyo, huku kila mmoja wetu akijiuliza ni nyumba gani hiyo.

Nikasikia jamaa mmoja akisema;

‘Hiyo itakuwa ni ile nyumba ya Yule jamaa aliyekuwa ulaya, …’akasema na niliposikia hivyo kuwa ni nyumba ya huyo jamaa aliyekuwa huko Ulaya nikaikumbuka hiyo nyumba, kwani niliwahi kupita maeneo hayo siku za nyuma, wakati huo ndio ilikuwa inamaliziwa ujenzi, na kila mtu aliyeiona aliisifia na ukiuliza ni ya nani watu waliishia kusema ni ya jamaa kutoka ulaya, lakini ilikuwa muda kidogo …

Tashwishwi ikaniingia kutaka kujua zaidi na nilijaribu kuangalia huku na kule kama kuna mtu anayeweza kunipatia majibu hayo, lakini sikumuona kwa muda ule, hamasa ikaniingia zaidi kila nikisikia jamaa wa anayepiga hiyo mbiu kwenye gari akizidii kuipa sifa hiyo nyumba…hapo tena sikutaka kumuuliza maswali mtu, nikaona niende nikajionee mwenyewe.

Nilifika eneo hilo,  ilikuwa eneo pembeni kidogo na maeneo yaliyojaa nyumba, ilijitenga kinamna, kutokana na mwiinuko, nikapanda ule mwinuko na kupitia kwenye barabara  inayoelekea kwenye hiyo nyumba.

Sikuwa na wasiwasi, kwasababu hiyo nyumba  ilikuwa inapigwa mnada nilijua sitapata kizuizi cha kuweza kuiona, na kweli nilipofika, niliwakuta watu wakiikagua , lakini wengi walikuwa nje ya geti, nikahisi huenda hawaruhusiwi kuingia ndani ya geti, lakini sio hivyo, wao walishaingia na sasa walikuwa wakihakiki kwa macho tu, na mimi nikaona niingie ndani nijionee jinsi ilivyo….

Nikakupumbuka kwa kipindi kile ndio ilikuwa kwenye ujenzi wa mwisho mwisho, na sikuwahi kuingia ndani kuona jinsi ilivyokuwa, japokuwa nilitamani sana niingie, kutazama ilivyo, kwani ilikuwa na muundo wa kipekee …sasa ndio imezungushiwa geti kubwa la kisasa lenye nyaya za usalama, nahisi zina umeme.  Geti lilikuwa wazi, nikaingia ndani.

Mashallah, …kiukweli ilikuwa ni nyumba kubwa, na mjengo wake kwa mbele tu, ulikuwa ni  wa kipekee, wanasema ramani hiyo jamaa alikuja nayo mwenyewe kutoka ulaya,…na mafundi wake walikuwa wa kimataifa, na ilijengwa kwa gharama kubwa sana …na kile aliyeulizwa alisema ni muundo wa ulaya

‘Huu ni muundo wa huko Ulaya, toka chini msingi ni wa mawe matupu..inakuwa kama imewekezwa juu yam awe…!’akasema jamaa mmoha alipoona naangaza macho kuangalia yale mawe yalivyopangwa, ni mawe makubwa,magumu…

Watu walikuwa wakiingia na kutoka, na kila mmoja aliongea lake, lakini mimi kichwani nilijiuliza maswali mengi, yakihitajia majibu, hata hivyo sikupenda kuwauliza kwanza, nikaona niwahi kuingia ndani ya nyumba yenyewe kwanza

Nikawa nahesabuu hatua, huku nikijiuliza  ni kwanini ilifikia hatua hiyo, …watu kukopa pesa na kujenga nyumba ya gharama hivi, baadaye wanashindwa kulipa deni, na hatimaye ndio hiyo inapigwa mnada….na je wao wenyewe watakuwa wapi, yawezekana  labda wana nyumba nyingine wanaishi…au wapo huko ulaya!

Nikawa   natembea taratibu kama vile mnunuzi kwenye zile njia za bustani  sasa nikiwa naelekea kwenye mlango mkuu wa nyumba yenyewe….maua mazuri ya kila namna yalikuwa yamestawi, na kuzidisha nakshi ya hiyoo nyumba, na moyoni nikatamani , kama ningelikuwa na pesa, ….hahaha…itakuwa mwendo wa bilioni, ikawa ni ndoto za Alinacha

Kiukweli kunapendeza, utafikiri upo wapi vile,….., sasa nikawa naangaza huku na kule, kabla sijafikia mlango wenyewe, eneo la kuingilia ndani …nikageuka kulia , nikaona eneo kubwa limependwa miti na migomba, na ..ndege walipita huku na kule, ..nakataka kugeuka kushoto, mara nikasikia sauti, mwanzoni nilijua ni watu waliokuja kuitizama hiyo nyumba lakini haikuwa hivyo…

Hiyo sauti ni masikitiko,…na kama kilio, kwikwi ya kilio,…nikasita kutembea , nilipoona kumetanda ukimia, nikainua hatua moja , mbili  , tatu, sasa nilishafika kwenye maru maru za kupanda ngazi, nikaanza kupanda, ngazi ya kwanza, ya pili ya tatu, mara macho yangu yakanasa kitu,…na moyoo wangu ukalipuka kwa mashaka.

Nikasimama, …kwanza sikuamini, maana nilijua humo kwenye hiyo nyumba hakuna mtu tena,…mpaka inafikia kunadaiwa ina maana wenyewe watakuwa sehemu nyingine lakini ….mhh kumbe bado kuna watu, ni akina nani hawa? nikajiuliza

 Pale kwenye mlango mkubwa wa kuingilia kulikuwa na mama mmoja akiwa kakaa mkao wahuruma, ule mkao wa mtu kukaa chini, miguu imejikunja na kichwa kinakuja kulala kwenye magoti…na pembeni yake kulikuwa na watoto wawili,….

Mama Yule alikuwa analia, ….! Nina uhakika alikuwa analia….

Kwanini analia, nikawa najiuliza sasa….na cha ajabu watoto wake walionekana kama wanambembeleza, itakuwa ni watoto wake!

Nikawa nimepigwa na butwaa,

 Mtoto mkubwa alikuwa upande wa kushoto kwake, akiwa naye kakaa chini na mkono wa mmoja wa huyo mtoto upo kichwani kwa mama yake, na mtoto mwingine yeye alionekana sio mkubwa sana, alikuwa naye kakaa akiwa kajiegemeza ubavuni kwa  huyo mama, na alikuwa kainama kuficha uso, huenda na yeye alikuwa analia

Hali ikanibadilikia…nikahisi mwili ukinisisimuka…

Ile hali ilinitia simanzi, japo sikuwa nafahamu kisa cha wao kuwa vile ni kama vile kuna msiba …

Kwa muda wote huo  walikuwa kama hawajaniona, au hata kama walioniona hawakuwa na hamasa namimi….,huenda walishachoka na watu waliokuwa wakiingia na kutoka, maana watu walikuwa wakija na kuondoka,  kwahiyo kwa hivi sasa walikuwa hawana habari na hao watu tena, swali likajijenga kichwani hawa ni akina nani , nijuavyo waliokuwa wakiishi humo hawapo!

Haya maswali ya huenda , huenda sikuyapenda yajirudie kichwani mwangu, nikaona niwasogelee wale  watu ili nijue wao ni akina nani, na kwanini wapo kwenye majonzi kiasi kile…., na nilipowakaribia ndio nikasikia kauli hiyo, …kauli iliyonifanya niache ile kazi ya kuikagua hiyo nyumba na kuwaelekea wao …

‘Mama sasa sisi tutakwenda kuishi wapi, nyumba yetu ndio hiyo inauzwa,baba mdogo haji, toka majuzi, na mama …kwanini wanatufanyia hivyo…?’ ilikuwa sauti ya Yule mtoto mkubwa

‘Nimeshawaambia yote tumuachie mungu, yeye ndiye atajua tutaishi wapi…’akasema mama huyo kwa sauti ya huzuni

‘Tutamuachiaje mungu mama….kama ni hivyo kila mtu angemuomba mungu apate kila akitakacho, na akasubiria akipate, lakini kila mtu anahangaika kwanza…sasa tukikaa hapa tu, watakuja kutufukuza…hata hivyo, mama mimi sitaondoka hapa, nitabakia hapa hapa, hii ni nyumba yetu, baba alitujengea kwa pesa zake, kama ni kutuua watuue tu…’akasema huyo mtoto

‘Hata mimi siondoki hapa mama, ….’akasema Yule mdogo

Na alioongea huyo mdogo ndio huyo mama akainua uso, na alipoinua uso ndio akaniona, nilikuwa sasa nimefika pale walipokaa, akanitizama, nilichokiona usoni kwa Yule mama ni machozi,….mhh, moyo wangu ukasononeka…nikajitahidi kusema;

‘Habari zenu….’nikasalimia na wote walibakia kimia, nahisi walishachoka na hizo salamu

‘Samahanii jamani nilikuwa nauliza nyie ndio wenye hii nyumba…?’ nikauliza sasa nikiwa mkabala na wao, na Yule mama akainua uso , halafu akageuka kumuangalia mtoto wake mdogo!

‘Nzuri,….. samahani tunaomba usizidi kutuongezea machungu zaidi….’akasema

‘Hapana mimi sio lengo langu hilo…’nikasema

‘Wewe unasema wenye nyumba wakatii unasikia kuwa nyumba hii  inapigwa mnada…sisi hapa hatuna chetu tena…wenye nyumba sasa ni hao wenye uwezo wao, waje wanunue …kama ni wewe haya kagua uondoke zako, mtuachie na majonzi yetu,….’akasema huyo mama

‘Mimi sijui kabisa kinachoendelea, nimesikia huyo mtu wa mnada akinadi kuwa nyumba hii inauzwa, na inatokana kuwa mwenye nyumba alikopa pesa benki akashindwa kurejesha…’nikasema

‘Kama umesikia hivyo yatosha….’akasema huyo mama na mtoto wake akamkatisha na kusema kwa sauti kama ya ukali..

‘Mwenye nyumba hajakopa pesa yoyote, waongo hao…mwenye alikuwa ni baba yangu sasa ni marehemu angekopaje hizo pesa….’alisema huyo kijana mkubwa na hapo nikashikwa na mshituko, …mwenye ni marehemu ina maana hawa ni yatima……!

‘Oh, ina maana mwenye hii nyumba sasa ni marehemu ndiye alikuwa baba yenu…? Nikauliza na hapo hakuna aliyenijibu, na mama huyo baadaye akasema

‘Ndio hivyo, ….’akasema hivyo tu kwa sauti ya huzuni.

‘Oh poleni sana, mimi sikujua siku nyingi zijapita maeneo ya huku, nashangaa hata huo msiba sikuwahi kuusikia…’niliishiwa cha kuongea maana kiukweli sikuwahi kusikia kuwa mwenye hiyo nyumba sasa ni marehemu,….sikumbuki kabisa kusikia hata mtu mmoja akisema hivyo…watu walikuwa na hamasa tu ya kuiona, na kuitamani, huenda wengine ni madalali, wanataka kukimbia kuwatafuta wanunuzi wapate
cha juu…

‘Ina maana huyu…hata siamini, Yule jamaa sasa ni marehemu…’nikabakia nimeduwaa.

‘Mbona ni muda mrefu sana mume wangu alishatangulia mbele ya haki, na wengi walishasahau, ile mwenye kovu usizani kapoa, mimi nimekuwa nikiombeleza miaka yote hiyo…na haya yanayotokea sasa yananizidisha machungu, na kuzidi kunikumbusha marehemu mume wangu,….’akatulia na akavuta pumzi ya kutaka kulia.

‘Pole sana…’nikasema

‘Najua ndio basi tena,sitamuona tena… sasa sina jinsi inabidi nikubali hali, inabidi nikateseke kama wanavyotaka wao, wanafikia kusema si ulikuwa unaringa..jamani, lini nilifanya hivyo, ‘akatulia

‘Hiyo ni kawaida ya vinywa vya watu…’nikasema

‘Lakini nina uhakika  kama angelikuwepo hai haya yote yasingelitokea…’akasema huyo mama kwa uchungu,na hapo akaanza kulia.

Akilini nilikumbuka yale maneno ya mazito ya mtu wa imani akisema; ‘mpende umpendaye ipo siku mtaachana naye, kipende ukipendacho ipo siku utakiacha…itakayobakia kwako ni amali yako njema…na wakati nawazia hayo Yule mama alikuwa bado analia, nikamsogelea na kuanza kumliwaza kwa kusema;

‘Yote ni mapenzi ya mungu, poleni sana na mola aiweke mahali pema peponi, ….shemeji cha muhimu sasa sio kulia zaidi, kwa kuonyesha mapenzi yako kwake, wewe uzidi  kumuombea  marehemu maghafira na najua , nimjuavyo mimi, mume wako alikuwa mtu mwema sana,…sasa hivi atakuwa sehemu njema…’nikasema

Ni kweli huyo jamaa alikuwa mtu mkarimu sana, pamoja na kutokea hukoo alipokuwa ulaya hakuonyesha ile hali ya kuringa, hakuweza kukupita njiani na gari lake kama anakufahamu ni lazima atasimama akuchukue, na hata kukufikisha nyumbani kwako, lakini sasa ndio hivyo hatunaye tena…Yote mapenzi ya mungu.

‘Ni kweli yote ni mapenzi ya mungu, lakini haya yanayotokea sasa, yanatuzidishia machungu, maana kila alichokiacha sasa kinachukuliwa, hebu fikiria hata haya makazi yetu ya hapa duniani, sehemu ya kusitiri aibu yetu nayo ndio haiyo nayo inatakiwa kuchukuliwa, sisi tutakwenda kuishi wapi….’akasema huyu mama akiangalia juu, kuiangalia hiyo nyumba!

‘Oh…’nikaguna hivyo na huyo mama akaendelea kuongea kwa sauti yanye huzuni

‘Hawa watu sijui mwishowe wanataka nini kwetu, walianza kutunyang’anywa kimoja baada ya kingine…mashamba yake aliyoyanunua mume wangu akiwa hai yamegawanywa…’akatulia kidogo

‘Yamegawanywa kwa nani…?’ nikauliza

‘Kwa wanandugu kila mmoja akija na visingizio vyake, mara hili shamba lilikuwa la familia, na mmoja akifa shamba linatakiwa kurudi kwa familia,..mara hili eneo walinunua kwa umoja wa familia eti walichangiana ndugu wakanunua kwa pamoja  kwahiyo sasa linakuwa mikononi mwa familia, nikajiuliza ina maana sisi sasa sio miongoni mwa familia, jamani hata hawa mayatima hawana haki, waniache mimi mjane lakini hawa ni haki yao….’akatulia akiwageukia watoto wake mmoja mmoja!

‘Ina maana wewe wakati mume wako ananunua hayo mashamba hukushirikishwa…?’ nikamuuliza

‘Hayo mashamba eti…wanawake hahaha,….. usijifanye hujui…kiukweli yeye aliniambia ananunua hiki na kile na wakati mwingine tunakwenda naye, lakini yeye kwa upendo aliokuwa nao kwa ndugu zake, kila kitu aliwaweka mbele walikuwa kama sehemu ya maendeleo  na familia yao, yeye hakupenda ubinafsi, na ndugu zake walikuwa muhimu sana…’ akasema

‘Ikiwemo na wewe pia au sio..?’ nikauliza

‘Mimi si ndio yeye, alichofanya yeye kipindi hicho ni kama nimefanya mimi, sikuwa na wasiwasi wowote…’akasema

‘Sasa kwahiyo wewe unauhakika kuwa mume wako ndiye alinunua hayo mashamba, na kama alifanya hivyo  si kuna hati na kitu kama hicho, mume wako hakukuonyesha, au ilikuwaje hati hizo zikawa mikononi mwa ndugu?’ nikamuuliza

‘Kipindi hicho sikuwa natilia maanani, sikujua haya yatakuja kutokea, sikujua kuwa hawa ndugu watakuja kunibadilikia,….mimi sikuwa na wazo hilo kuwa nichukue hati, au….niliwaona hawo shemeji zangu kama alivyo mume wangu…’akasema kwa uchungu.

‘Sasa kwanini walikuja kubadilika….?’ Nikamuuliza

‘Hayo mimi sijui…na kiukweli tabia hiyo hawakuwa nayo kabisa….walianza kubadilika pale walipooa…nakumbuka hata alipokuwepo mume wangu, ndugu zake hawa waliishi kwa ushirikiano na kaka yao, lakini baadaye walianza mabadiliko fulani,….walipooa, hata hivyo kwa muda huo walimuogopa kaka yao….walikuwa wakimuheshimu sana kaka yao...’akasema

‘Kwahiyo unataka kusema labda tabia hiyo ya ubinafsi ilichangiwa na wake zao..?[ nikamuuliza kwa umbeya ili kutaka kujua hisia zake

‘Mimi siwezi kuwasingizia wake zao maana msimamo ni mtu mwenyewe, kama mume unatakiwa uwe na msimamo wako ujue nini majukumu ya familia, usiyumbushwe, lakini nii hisia zangu ziwezi kusema zaidi kuhusu hilo..’akatulia

‘Sasa hao wake wenza kwa shemeji zako, hawakuwa na ushirikiano mwema kama walivyokuwa shemeji zako, maana mlitakiwa muwe pamoja au sio, kwani haya yanaweza kuwakuta hata wao au sio..?’ nikamuuliza

‘Wewe hujui sisi wanawake, tuyaache hayo….’akasema na kutaka kuacha kuongea lakini ghafala akasema

‘Klichonishangaza hata kushindwa kuamini ni pale tu mume wangu alipokwisha kulazwa kaburini, …hao hao nilioishi nao kwa upendo akiwemo kaka yao, walinibadilikia, ule upendo wa shemeji zangu haukuwepo tena…yaani hata siwezi kuamini, hata wengine wananisingizia mabaya, hata siamini, niwezeje kumuaa mume wangu…yaani inaniuma sana...’akatulia pale mtoto wake mkubwa alipomshika akimuashiria asiendelee kuongea zaidi.

‘Mama akiongea hayo anazidi kulia..ni bora mama usiyaongee, yameshapita, mungu atawalipa, kama ni haki yao waendelee kuwa nayo, lakini kama ni haki yetu ipo siku mungu atatulipia…’akasema mtoto mkubwa, alikuwa na kama umri wa miaka kumi na mbili hivi…

‘Ndio hata mwalimu wa dini alituambia dhuluma haidumu,ukidhulumiwa ukimuomba mungu dua zinapokelewa moja kwa moja , tunamuomba mungu atatusaidia mama,…’akasema yulemdogo, huyu anaweza kuwa ana miaka nane au tisa.

‘Mhhh…mimi bado hapo sijaelewa,…hati za mashamba na mali ya mume wako walikuja kuchukua wao, au ilikuwaje,,,?’ akauliza

‘Nikuambie kitu, hawa shemeji zangu, wote walianzia maisha yao humu, walikuwa wakiishi humu, lakini baadaye mume wangu akawasaidia kila mtu akawa na nyumba yake, na ndio wakaoa mmoja mmoja, kwahiyo humu ndani walipafahamu sana, kila kitu walijua kipo wapi,….nina uhakika wao walikuja kuchukua kipindi mimi sijiwezi, kwani nilizitafuta hati sehemu zilipokuwa sikuziona na nilipowauliza nikaambiwa hayanihusu, ….’akasema

‘Je kwa hali hiyo, mashamba kuchukuliwa, ….wewe ulikaa kimia tu, hukutaka kudai haki zako….maana hiyoo ni haki yako wewe na watoto….?’ Nikamuuliza

‘Nikuambie ukweli hayo yote yalifanyika kipindi sijiwezi , ni miaka mingi sikuwa mnzima nilikuwa nusu mfu…itakuwa ni muda huo wao wakaja wakachukua hizo hati, na mashamba wakagawana wakidai ni mali ya familia,…’akatulia

‘Na hilo nisingeligundua hadi pale  nilipoanza kupata nafuu,….ni siku moja nilianza kufuatilia, maana hali ilishaanza kuwa ngumu, angalau ikiwezekana tuuze kipande cha shamba, ndio nikashangaa kukuta maeneo hayo mengine yamejengwa nyumba za watu , nauliza naambiwa wameuziwa…’akasema

‘Mhh…basi yaonekana uliumwa sana, ilikuwaje kwani, ni mshituko au…?’ nikamuuliza

‘Kifo cha mume wangu kilinichukua sana, nilipatwa na mshtuko, nikawa nimeishiwa nguvu mwili mnzima, wanaita kiharusi,… nikawa mtu wa kitandani, siwezi hata kuinua mkono,…nilibakia hivyo miaka nenda rudi kila kitu kitandani…’akatulia

‘Mume wangu akiwa hai, nilikuwa na kazi yangu, kutokana na mshutuko huo, kuumwa huko, hata kazi niliyokuwa nayo nikafukuzwa,…na pesa yote iliyobakia ya mume wangu ilitumika kunitibia,..kiukweli mimi nilijua ni maiti tu….’akatulia

‘Kilichokuwa kikinizuia ni hawa watoto…hebu fikiria sasa hivi nipo hai wanafanya hivi, je kama ningelikuwa nimekufa ingelikuwaje, yaani hapo ndio namshukuru mungu kuwa nipo hai, japokuwa siwezi kupambana nao, lakini …’akasema na kuinua mikono juu

‘Kwahiyo kwa miaka mingi nilikuwa kitandani sijijui…ikafikia watu wananiona kama mnzigo, walioweza kuja kunisaidia ni ndugu zangu wa kuzaliwa nao, na wao ikafika muda na wao wamechoka, maana na wao wana familia zao,…kuuguza mtu kama mimi ilikuwa  ni kazi kweli,…siwezi kuwalaumu..’akatulia

‘Na hao shemeji zako je…?’ nikamuuliza

‘Mhh, namshukuru sana huyu shemeji aliyekuwa amechaguliwa kama msimamizi, kiukweli….sijui kwanini hili likatokea,….lakini alijitahidi kuwa mwema kwangu.alinisaidia sana.’akatulia

‘Kwahiyo unataka kusema kuna mtu , yaani kati ya shemeji zako yeye alichagiliwa kama msimamizi…au sio? Yeye  akapewa mamlaka yote, ikiwemo hati za mali au sio…..?’ akaulizwa

‘Ndio …..kutokana na hali yangu ilibidi ikafanyike hivyo, na mimi hilo, japokuwa sikuwepo, japokuwa sikujua ni lini hayo yalifanyika, lakini ilibidi…unaniona naongea hivi, sikuwa hivi, nilikuwa mfano wa maiti…kwahiyo walikubaliana wakiwemo ndugu zangu kuwa awepo mtu wa kuchukua hatua, na huyo shemeji yangu ndio akachaguliwa akayachukua majukumu yote, ya  mali, ya watoto, matibabu….akajitahidi alivyoweza…na ubinadamu tena, sijui ….’akatulia akitikisa kichwa.

‘Mhh….naona hapa bado kuna maswali mengi, lakini ngoja kwanza nikuulize , sasa hii nyumba kwanini inapigwa mnada, na unasema,… mtoto kasema baba yake hakuwahi kukopa hizo pesa ilikuwaje, ina maana ni deni lilikuja baada ya mume wako kuondoka, au  ilikuwaje?’ Nikamuuliza

‘Katika kitu ambacho mume wangu alikuwa hataki, ni kukopa, hasa mikopo yenye riba, mume wangu alikuwa mcha mungu sana, na aliwahi kuniasa kipindi nilipotaka kujiunga na vikoba, kuwa riba ni sumu ya mali halali, riba inatafuta baraka yote kwahiyo niachane na maswala ya kukopa kwa riba,…ni kusema kuwa mume wangu hakuwahi kukopa benki hilo nina uhakika, wakisema eti lilikuwa deni la mume wangu ni uwongo…’akasema

‘Sasa ilikuwaje mkopo huu ukatokea maana ni mkopo mkubwa sana, …?’ nikamuuliza na hapo mjane huyu akajaribu kujinyosha na kusema;

‘Ndio maana nikasema haya yote ni mbinu za kuhakikisha kila kitu tunanyang’anywa…mkopo huu sikukopa mimi, na wala sijui ulivyokwenda hadi ikafikia pesa nyingi kiasi hicho, hata mimi nashangaa, utakopaje, huku hujui jinsi ya kulipa, hiyo si mbinu jamani…’akasema

‘Atakuwa ni baba mdogo…’akasema mtoto wake na mama yake akamuashiria anyamaze..

‘Kama mtoto anavyosema, yawezekana kuwa shemeji au msimamizi wenu ndio alikopa, na wewe wakati anafanya hivyo, ulikuwa bado hujawa na ufahamu, au ulivyoambiwa hilo deni lilitokea wapi..?’ nikamuuliza

‘Lakini nikuulize unaniuliza haya maswali yote ili iweje….sisi yote haya tumeshamuachia mungu, na nimekuambia hayo niliyoweza kukuambia,…yatosha,…’akasema na kujikuanyata.

‘Samahani sana shemeji usione nakusumbua, nina nia njema, huwezi jua msaada wangu kwako, mimi…’kabla sijamalizia akasema

‘Mimi sitaki tena kuja kuonekana mbaya, mungu yupo, nasema haya kwani kuna kipindi tulikuja kukorofishana na huyu shemeji yangu, akaongea maneno mengi mabaya sana,…kuwa yeye kajitokea, bila yeye ningekuwa wapi, kawa name muda wote, akawa hahangaiki na familia yake ananihangaikia mimi tu, sasa nimepona naanza kuleta kiburi….unaona, sasa mimi nashindwa kidai chochote…ndio maana imefikia muda nimeona nimuachie mungu….inatosha’ Akasema  sasa akiwa hataki kuongea tena.

NB: MAMBO ndio hayo, msinione nilikuwa kimia , nina mengi nimeyapata kwa jamii….matatizo, visa vingi, lakini ndio hivyo nitafanyaje,bado sijapata sehemu ya kujishikiza, lakini kwa uwezo wa muumba, ipo siku,

WAZO LA LEO:

USITENDE WEMA, ukiwa na malengo na kujinufaisha, wema hulipwa na mwenyewe muumba, kama utataka unufaike na huo wema, basi huo sio wema, hiyo ni biashara yenye kuhitajia malipo na malipo yake ukiyapata huo wema haupo tena! Kumbuka wema hauuzwi, unajiuza wenyewe kutoka kwa muumba!

Ni mimi: emu-three

2 comments :

Samira said...

Sawa ndugu wa mm tupo pamoja

Anonymous said...

Je tukio hili halijawahi kutokea maeneo ya kwenu, kwa jamaa zenu...watu kuwadhulumu yatima, wakala haki zao. Twashukuru sana kwa visa vyako