Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeFriday, April 8, 2016

YOTE MAISHA Jana wakati naenda shamba, nilipita sehemu  yanaposimama mabasi ya daladala, japo sio kituo rasmi, pembeni ya hiyo barabara alikuwepo kasimama dada mmoja, kwa muonekano alikuwa kavalia kiofisi, akiwa kamshikilia mkono mtoto nahisi mtoto huyo ana miaka saba au nane japo anaonekana mnene kidogo, nahisi atakuwa ni mtoto wake.

Mimi nilitaka nipande basi ili niwahi shamba, unajua tena siku hizi najipa mazoezi ya kulima, nikawa nimemkaribia huyo mdada, na kwa muda ule akawa kila mara anaangalia saa yake huku akitikisa kichwa, baadae akashindwa kuvumilia akasema:

 'Hawa watu vipi, mbona hili gari la shule mbona limechelewa hivi sio kawaida yake...mmh, watanifanya nachelewa kazini, na hizi foleni aah, ..' akawa analalamika lakini hakuna aliyemjibu. hata mimi sikuwa na cha kumjibu.

 Pembeni ya huyo mdada, kulikuwa na mama mmoja, yeye alikuwa kavalia khanga, kinyumbani zaidi na yeye alikuwa na mtoto wa umri sawa na yule wa kwanza, japokuwa mtoto wake hakuwa mnene kama huyo mwingine lakini ukiwatizama watakuwa na umri mmoja.

Tofauti ya watoto wawili hao ni kwenye sare zao za shule. sare za yule wa mwanzo ni za mistari mistari, na huyu wa sasa ni shati jeupe, ila yule wa mwanzo kaongezea na tai juu yake, maendeleo hayo, kufanya tofauti kidogo.Yote maisha.

 Lakini macho yangu hayakuvutika zaidi na hao wanawake wawili na watoto  wao. Macho yangu
 yalivutika zaidi na mdada mwingine, aliyekuwa akifanya biashara ya mihogo.

 Kwa muda ule huyu mdada anayekaanga mihogo alikuwa amemaliza kukaanga, na sasa anawauzia wateja na mmoja wa mteja wake ambaye kwa muda huo alikuwa akinunua ni yule mtoto wa mama aliyevaa kinyumbani, na  mama yake alikuwa akimtizama.

 Yule mtoto mwingine aliyevaa sare za shule na tai,  yeye alikuwa kashikilia kikasha maalumu cha kubebea vyakula, kuashiria kuwa keshaandaliwa kutoka nyumbani, vyakula maalumu, kwahiyo hakuwa na haja ya kununua mihogo ya njiani. Yote maisha.

 Sasa huyu mdada niliyekuwa nimevutika naye , huyu anayekaanga mihogo, pembeni yake kulikuwa na mtotom ni mtoto wake maana kila mara nilisikia mtoto huyu akimuita mama, nataka hiki mama nataka muhogo....mtoto yule alikuwa kavalia nguo kuukuu, kinyumbani, na kwa umri wake alistahiki na yeye kwenda shule, lakini alivyovaa, alionekana sio muendaji shule.

Kichwani nikawa na maswali mengi, lakini sikuwa na jinsi ya kuyapata majibu, nikawa nimetulia tu nikisubiria usafri nami japo kuwa nilikuwa na yangu kichwani lakini ile hali ilinifanya niwaze na kuwazua.

Mtoto huyu wa muuuza mihogo, sasa  alikuwa  kasimama,akiwatizama watoto  wale wawili waliovalia sare , jinsi alivyoonekana akiwatizama wenzake ilionyesha wazi anawaza jambo na hisia zilionekana hata usoni.

 Akili yangu haikutulia, nikaona niwe mdadisi nikasogea pale kununua muhogo, na wakati nanunua nikamuuliza yule mtoto.
'Mbona unawaza sana, unataka muhogo nikununulie,...?' nikamuuliza

'Kashiba huyo, katoka kula sasa hivi...'akasema mama yake

'Mhh,,...na kwanini huendi shule?' nikamuuliza swali mtoto nikijua mama yake ndiye atajibu

 Na ni kweli dada mkaanga mihogo akadakia kwa sauti, bila hata kuremba akasema:

 ' Aende shule bila sare ya shule....'akasema

'Kwanini , kwani sare zake zimekwenda wapi...?' nikauliza

'Huko shuleni, walimfukuza eti sare zake zimechakaa, tungefanyaje na haya maisha...ndio hapa nahangaika kuuza mihogo nipate pesa..' akasema sasa kwa sauti ya huzuni

 Nikageuka kumuangalia yule mtoto ambaye kwa muda huo alikuwa akiwatizama wenzake waliovalia sare wakipita na hawa wawili waliopo hapa kituoni , na kwa akili yangu na mawazao yangu ya haraka nahisi mtoto yule ndani ya nafasi yake atakuwa anaumia akiwaona wenzake wakienda shule,...

Na hata huenda, kwa akili za kitoto asiwazie zaidi masomo, lakini akikumbuka kuwa shuleni atakutana na wenzake kucheza..... na kusoma pia, ni lazima moyon anasononeka, lakini utafanyaje, yote maisha

 Mara gari la shule likafika, yule mtoto mwenye sare na tai, akamuaga mama yake kwa kiingereza, na busu juu, taratibu akatembea kuelekea kwenye basi lile liliondikwa jina la shule hiyo anayosoma,na kundoka, huku akimpungia mama yake mkono na mama yake akifanya hivyo. Na yule mama aliyevalia kiofisi akaondoka kuvuka barabara upande wa pili. Kumbe kule kuna gari lake! akaingia kwenye gari lake na kuondoka, alitupita pale pale...

 Sasa shauku yangu ikaenda kwa huyu mama aliyevalia kinyumbani, akiwa na mtoto wake, yeye alionekana anasubiria daladala, nikamuona kama kazama kwenye mawazo, na machoni ni kama anataka kulia,  nikataka kumchokoza nikasema

'Mhh...kwanini hili basi la shule, lisingeliwachukua na watoto hawa na wao wakawahi shuleni....'nikasema na huyo mama hakujibu akawa kimia tu...

Nilipoona huyo mama kabakia kimia nikamtizama mtoto wake, nikashangaa kumuona kashikilia shavu, kile kitendo hakikunifurahisha, nikasogea na kumuondoa yule mtoto ule mkono shavuni, na mama yake akasema

'Anakumbuka kipindi cha nyuma baba yake akiwa hai alikuwa akipanda gari kama hilo...sasa ndio hivyo, hatuna jinsi nimemuhamisha shule ya  kulipia sasa anasoma shule za serikali maana siku hizi ni bure, sina uwezo wa kumlipia ada tena...'niliposikia hivyo nikageuza uso upande, huzuni ilinitanda, kumbe huyu ni yatima.....

Tutakuja kusema nini mbele ya mola, kwa watoto hawa yatima, ambao kila mara wakiona tendo fulani wanawakumbuka wazazi wao, ...hata hivyo mimi ningefanya nini, nikatulia kwa muda, nikizama kwenye mawazo ya udadisi


 Baadaye ikaja daladala, cha ajabu kondakta akateremka na kuzuia mlangoni na kusema kuwa ndani ya gari lake kumejaa wanafunzi, hapandishi tena mwanafunzi.Hakuna aliyemsemesha wakapanda watu wazima na hilo likaondoka, mimi nikawa nimetulia tu maana gari la kuelekea huko ninapokwedna lilikuwa halijafika

 Ikabidi huyu mama na mtoto wake waendelee kusubiria, mimi japokuwa nilikuwa naenda shamba, lakini ile  hali iliniumiza sana moyoni , kwanini kusiwe na taratibu za usafiri kwa wanafunzi, hili jambo kweli lina uzito kihivyo...hawa wenye magari binafsi wangejitolea basi kila mmoja achukue wanafunzi hata wawili....au ndio kuogopa, ...usumbufu, mimi sijui..Ukiwa huna unayawazia hayo!

  Baadaye sana ilikuja daladala na mtoto yule akapata nafasi ya kuingia kwenye gari, sijui huko shuleni atafika saa ngapi. na mama yake akaonekana akiondoka pale kituoni kiuonyonge, nahisi atakuwa akilia moyoni, kama mume wake angelikuwa hai, huenda ingelikuwa ni tofauti....Yote maisha.

 Mawazo yangu yakamrejea huyu mdada mwenye mtoto aliyefukuzwa shule kwasababu sare zimechakaa, na sasa anakaanga mihogo ili ajitahidi apate pesa za kumnunulia mwanae sare, maana sasa elimu ni bure, muhimu ni sare na nauli ya dala dala.... nikajiuliza jinsi gani sasa mtoto huyo ataweza kufidia masomo aliyopteza,, jinsi gani huyo mtoto anavyosononeka akiwaona wenzake wakienda shule....mmh yote maisha

 Zaidi najiuliza, huyu ni mzazi wa kike, je baba wa huyu mtoto yupo wapi, hapo sikuweza kuvumilia, mdadisi wa diaru uangu nikaona nipate ukweli wa hili,

 Sijui kwanini, nikajikuta nimesogea tena kwa yule mama muuza mihogo, nikanunua kipande kingine nikisema

'Hii mihogo yako mitamu sana, natamani nikaipande shambani kwangu...'nikasema

'Aheri ya wewe umeamua kulima, maana kazi nazo zina wenyewe....'akasema akinikagua

'Ndio hivyo...yote maisha..'nikasema

'Na hata ukisoma kama hujaandikiwa kupata kazi ya kuajiriwa ni kazi bure...'akazidi kusema na mimi hapo nikawa sina la kusema maana alinigusa moyoni lakini sikutaka kusema neno kuhusu mimi nikajikuta nikuuliza swali hili:

 'Hivi sasa mtoto hatasoma mpaka apate sare, sasa baba wa mtoto huyu anasemaje kuhusu sare za mtoto..?' na yule mama akacheka kidogo, halafu akasema;

 'Aseme nini, kazi hana, walipunguzwa kazi, na hao Wahindi, na  sasa hivi kawa kama kachanganyikiwa...aah, we acha tu...' akasema

'Kwanini achanganyikiwe...?' nikamuuliza

'Ilikuwa ghafla sana,mume wangu alikuwa mchapakazi mnzuri, aliichukulia kazi hiyo kama yake,na ilipotokea kuambiwa hivyo, kuwa sasa hakuna kazi , hakuamini, walishtukiziwa, na mafao waliyolipwa ni mwezi mmoja tu...pesa aliyoipata itasaidia nini..na bahati mbaya, siku kaenda kuchukua hiyo pesa ili aanzishe angalau genge la nyanya, akaibiwa, basi akachanganyikiwa.

'Oh mungu wangu...'nikajikuta nikisema na yule mtoto akasema

'Ipo siku nitakuwa raisi,..nitawafunga wezi wote na baba yangu atapata kazi nzuri ...'akasema na watu waliopo hapo wakacheka/

Mara daladala ikaja na mimi nikapanda basi kuelekea shambani, huku nikijiuliza maswali mengi.

 Hivi kweli itatokea wanadamu tupendane, tuhurumiane, tusaidiane...sijui.

 Nikakumbuka maneno ya mtu wa imani akisema,

 'Hamtaweza kuwa wachamungu wa kweli mpaka muwe na imani , imani kuwa mungu yupo, na hamtaweza kuwa imani ya kweli mpaka mpendane, muhutumiane, msaidiane na mtu awe tayari kumpa mwenzako kile unachokipenda, ...'

Moyoni nikasema kweli, wachamungu hapa duniani hawapo, kwa hali hii..

Lakini ndio hivyo yote maisha

Ijumaa njema

.. mimi: emu-three

1 comment :

Yasinta Ngonyani said...

EEhh Mungu wangu...nimesoma hii habari nzima huku nikibubujika na machozi. Kwanza huyu mdada wa kwanza kwa nini hakumpeleka mtoto Wake shule kwa usafiri Wake? na pia kwa nini hakuweza tu hata kumchukua yule mtoto mwingine basi na kumfikisha shuleni kwake? Ama kweli binadamu hatuna huruma....IJUMAA NJEMA nawe pia ...Kapulya