Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeFriday, April 1, 2016

SIKIO LA KUFA HALISIKII DAWA- 22 (MWISHO)
  Mdada alipoinua macho na kutuangalia, haikupita muda akaanza kutoa machozi, na ilichukua muda kidogo kabla hajatulia vyema, na muda huo alikuwa ameshasogea kwenye kile kiti alichoambiwa akae, akawa kakitizama kwa muda bila kukaa,…hakuna aliyemsemesha sote tulibakia kimia

Kwa haraka nikajua ndiye mdada, mrembo malikia wa kijiji….
 Nikajaribu kumchunguza vyema huyu mdada, pamoja na matatizo yote hayo, lakini bado alikuwa na uzuri wake wa asili, na mwili wake umejengeka vyema, nikisema hivyo mtaelewa vyema, kiujumla ana umbile lenye mvuto, nahisi ndio maana hawa watu walimuhitajia sana kwenye uigazaji….

Alikaa kwenye kiti, na sasa akawa katulia, lakini muda wote alikuwa kainamisha kichwa chini, hakuinua uso wake kumwangalia yoyote,na mara kichanga kikaanza kulia, ikabidi Yule mdada mwingine aliyekuwa kambeba huyo mtoto, kusimama na kutembea pale alipokaa huyo mdada, mama wa hicho kichanga, na kumkabidhi

‘Naona anataka hoteli yake….’akasema na mdada akamchukua, na haikupita muda kichanga kile kikanyamaza , kilikuwa na shughuli ya kupata hoteli yake.

‘Jamani naona tuendelee kwani kwa mujibu wa ratiba ya docta, mzazi huyu atachukuliwa ili akapate matibabu yake na taratibu nyingine za dawa, lakini tukaona kuwa kuna umuhimu aje mumuone , ili kama ana lolote au nyie mna lolote liongelewe, na kumalizana, kwani baada ya hapa,hatutaruhusu mtu yoyote kuonana naye, …kiusalama zaidi..’akasema huyo mpelelezi

‘Wanandugu kutananeni na Mdada, au mrembo, au malkia wa kijiji….’akasema na mdada akawa kinama vile vile….

‘Japokuwa mwenyewe kasema hayo majina hayataki tena, lakini wapi utapita huko kijijini umtaje usisikie sifa zake…japokuwa pia sasa zimeharibiwa, lakini ndivyo ilivyo, wenye sifa zao hupitia kwenye changamoto hizo…’akatulia

‘Mdada…, hawa waliopo hapa ni marafiki zako, kila mmoja amekuwa akijaribu kukusaidia kwa namna yake…’akasema halafu akamgeukia docta na kusema

‘Yule pale unamfahamu sana, ni docta wako mshauri na nasaha, na yule pale ni jamaa yenu wanhuko kijijini…wote hao unawafahamu vyema, huna haja ya kuigopa, ila kwa hawa wawili labda ndio watakuwa wageni kwako, lakini ….sio wageni….’akatulia akituangalia….’hapo akasita kidogo, halafu akasema

‘Ni wageni usoni kwako, lakini ni wenyeji wako , kwani walishakufahamu kutokana na taarifa uliyowatumia..’aliposema hivyo, mdada akainua uso kutuangalia kwanza alitutupia jicha la haraka, akainama lakini baadaye akainua uso na kutuangalia vyema.

‘Labda nia yako uliwatumia hiyo barua pepe, ukitaka iwe siri, labda hukutaka ifahamike kwetu…, lakini kutokana na haya yaliyotokea imekuwa sio siri tena,…kuwa imetoka kwanani, au sio,… labda kama wewe mwenyewe utasema wasiandike chochote tunaweza kuwazuia, hili tutakuachia wewe na wao, mtakavyoaminiana na kukubalianai….eti nyie waandishi, sizani kama mumeshaiweka hiyo habari yake hewani….’akasema akituangalia sisi.

‘Bado….’tukasema

‘Hawa ni watendaji wa diary yangu, natumai unawafahamu sana kimtandao…wewe uliwatumia barua pepe, ukitaka waweke hewani, ili watu, au ….wasome’aliposema hivyo mdada akainua uso tena kutuangalia, na baadaye akiinamisha kichwa chini.

‘Utashangaa kwanini wamekuja kukuona,….wao baada ya kupata ujumbe wako, au taarifa uliyowatumia, kwa haraka walifika hospitalini wakitarajia kuwa watakukuta na kukuokoa…’akasema na mdada akainua uso tena kutuangalia

‘Kuniokoa…lini walikuja…?’ akauliza

‘Najua utashangaa hivyo, hata sisi tumeshangaa vilevile,   kwa vipi waje kukuokoa, ….wakayi tukio hilo lilitokea muda… ni wiki ya tatu sasa zimepita, inakimbilia mwezi, hawa ndio wanaonekana kulikoni…’akatulia
‘Labda ni kwasababu ya mtandao, …ndivyo ilitakiwa au inatakiwa ionekane hivyo, bado tunachunguza….ila kiukweli taarifa yako ilichelewa kuwafikia kwa wakati muafaka,..na wao walijua kuwa ni tukio la siku hiyo kumbe muda ulishapita…’akatulia

‘Sasa wao walikuwa na haja sana ya kuonana na wewe, kuongea na wewe, kukuuliza maswali kujua unaendeleaje…hatukupenda watu wakusumbue tena na tena, lakini kwa ajili ya hili,..tukaona ni bora tulimalize hivyo, kwani kutokana na wao, pia wataweza kusaidia watu wasiendelee kukufuatilia, maana wakiiweka hewani taarifa yako kila mmoja atakuwa na hamasa ya kukuona, na kujua ni nini kinachoendelea…’akatulia

‘Labda niwaachie wao wakuulize maswali, kabla hujasema lolote , …’akatulia akituangalia

‘Pole sana mdada kwa mitihani iliyokupata, …kiukweli tuliposoma kisa cha maisha yako, sote tulijiukuta tukitoa machozi, hatujui tukikiweka hewani wengine itakuwaje, na hatutaweza kukiweka hewani mpaka wewe mwenyewe utupe idhini yako, japokuwa ulisema tukiweke hewani ili huyo mlengwa aweze kujua…’nikatulia nilipoona anataka kusema neno, lakini alikaa kimia

‘Tulitaka tukuwahi kwanza…kukuokoa, ikiwezekana.’akasema mwenzangu, na mimi nikaendelea kutoa maneno yangu

‘Maisha yana changamoto zake, na milango ya kutokea kwenye hizo changamoto inatofautiana, mingine ni migumu sana kufunguka, na hata ikifunguka inaweza ikawa na changamoto nyingine milango mingine zaidi ya kufungua….ili ufike kuzuri zaidi, lakini hatutakiwi kukata tamaa, kwani mwisho wa yote ni ushindi.’nikazidi kumwambia.

Na mwenzangu akaendelea kusema;

‘Tunajua umepitia machungu mengi, na hata kufikia kukata tamaa, kutaka kujiua….hebu tujiulize ni nani hatakufa, kila mtu atakufa, kwa siku yake maalumu, kama ni hivyo ni kwanini ulazimishe kufanya hivyo,…’akasema na mimi nikasema

‘Nii kweli kama kila mtu atakufa basi kila mtu inambidi kuisubiria hiyo siku yako huku tukiomba iwe njema, tuombe mwisho mwema, na sio mwisho mbaya utakao kuwa ushahidi wa kuingia motonu,…hivyo basi kila mmoha wetu anahitajika kuwa na maandalizi ya matendo mema, na kama ukiteleza, ukafahamu jirudi, tubia, na tena mema….’nikasema

‘Ni kweli,…mkuu, ..mdada niongezee hapo, kuwa,  sisi sote ni wasafiri, hapa duniani ni kituoa tu cha kupumzikia, …, tukumbuke kuwa safari hiyo haina kurudi, je una masurufu gani…..hilo nimuhimuu sana tukajiuliza….tunakuambia haya ili moyo wako ujae imani, imani ya kumuogopa mungu…’akasema mwenzangu.

‘Swali letu ni kwa hivi sasa maana mengi tumeshayafahamu,  je  ni kwanini ulifikia hatua ya kujiua, baada ya ushauri nasaha, na hata wewe mwenyewe kuonekana kukubali …..je ni kwasababu ya shinikizo au ni kutokana na hizo nakama za maisha….?’ Akauli mwenzangu alipoona nataka kuzidi kuongea.

Mdada  alitulia hakujibu kwa haraka ni kama vile alikuwa akifikiria cha kuongea,…, alikaa kimia kwa muda, na mimi nikasema

‘Mdada ujue kuongea, ni sehemu ya kujisaidia …na ukiongea unapunguza mzigo uliopo moyoni mwako, sisi hapa tupo pamoja na wewe, ….na hilo la kuambiwa sikio la kufa, ni namna ya kukukatisha tamaa,….sisi tunaamini, kila tatizo lina ufumbuzi wake, na sisi hata kuja hapa ni kutaka kushirikiana nawe kutafuta dawa hadi  sikio hilo lipone na kama ni kufa iwe na kwa uwezo wake mungu, kapanga iwe hivyo….’nikasema na nilipotamka hivyo `sikio la kufa’ akainua uso na kuniangalia, akasema

‘Dawa gani ya sikio la kufa..kama ni la kufa, ni la kufa tu…jamii ilinitenga, wazazi na kila niliyewahi kukutana naye alinisakama kwa hili au lile, kisa eti mimi nimekuwa mhuni, ‘Mimi nimetwika sifa ya uMalaya…..nilijiuliza sana kwanini mimi…ni umalaya gani nilioufanya ambao haujawahi kufanyika…sijui, labda mimi nilitembea uchi barabarani nikijiuza…na mimi sikufikia huku…yote yaliyotokea ni kwa mitihani tu….sikudhamiria, ndio sikuwasikia wazazi wangu awali, nilikuwa nikikaidi, lakini ni kutokana na upendo wangu kwa aliyekuwa mchumba wangu, yeye ndiye sababu…..’akatulia na kuanza kulia, baadaye akatulia

‘Mchumba wangu nitamlaumu sana kwa haya yote, aliniaminisha akanifanya nimuamini….mungu amsamehe……japokuwa marehemu hatakiwii kusemwa kwa mabaya, lakini yote haya yasingelitokea kama isingelikuwa ni yeye…’akasema na sisi tukadakia

‘Ina maana mchumba wako ameshafariki…?’ tukauliza

‘Ndio ni marehemu kwa hivi sasa….ndio hiyo ninayosema toka lini sikio la kufa likasikia dawa, mimi najua yeye kaondoka na sisi tupo nyuma yake,…tutakwenda wengi kwa hilo…., najua na mimi nipo njiani, lakini hata huyu kiumbe wa watu, ana hatia gani ….’akatulia akijizuia kulia

‘Usijali mdada, kutokana na vipimo vyako, asilimia kubwa ya hiyo sumu imeshaondolewa…na kwa taarifa tu mtoto hana tatizo, yeye dawa zimefanya kazi haraka na inainyosha hata kuwa na tatizo hilo tena, ila inahitajia ufuatiliaji, na vipimo, vya mara kwa mara…, ‘akasema docta

Mdada akatikisa kichwa kutokukubaliana na yeye na docta akaendendelea kusema;

‘Mdada hilo nakuthibitishia, nimekaa na wataalamu wenzangu, wamesema kuwa kwa hali uliyo nayo…, kama utaendeela hivyo hivyo, ukafuata matibabu, na masharti,…dawa za kurutubisha kinga,  utapona kabisa….’akasema mshauri nasaha.

‘Hahaha…ugonjwa wa upungufu wa kinga upone hiyo dawa iligunduliwa lini, au mnanifanya mimi ni mjinga,…mnanipa matumaini ya kuishi au sio…, sawa, nitaishi kwa matumaini, kwa vile siku zangu hazijafika, lakini msinidanganye kuwa nitapona…’akasema akitikisa kichwa kukataa

‘Tunaosema hivyo ni sisi wataalamu, ujue ugonjwa huo uliona nao, ni wa kutengenezwa, sio sawa na ugonjwa huo wa kawaida, hawa watu ni wabaya sana, hata ma vyakula haya tunayokula ya makopo, tuwe makini nayo sana…’akasema docta

‘Na hata hivyo mdada  ukumbuke hata huo ugonjwa wa kawaida wa kupunguza kinga za mwili siku hizi una dawa za kupunguza makali yake na watu wengi wamefikia hatua ya kupona…’akaambiwa.

‘Kupona!!! Hayo nimeyasikia sana hapo kwenu…hata siamini tena…,eti jamani mliwahi kusikia mtu kapona akipatwa huu ugonjwa…?’ akatuuliza na sisi tulibakia kimia, akasema

‘Najua…huwezi kupona,ni kunipa moyo na matumaini tu….’hapo akawa analia halafu akatulia na alipokuwa akilia sote tulikaa kimia, na yeye mwenyewe akasema

‘NI kwanini ninalia,… kinachoniliza ni …ni huyu mtoto, kila nikimuangalia, nawazia mbali, najiona mimi kama muuaji, nilitaka kukiangamiza kiumbe hiki kisicho na hatia, sijui nitakuja kumueleza nini akiwa mkubwa, kama nitafikia huko…kama kweli tutafika huko’akasema kwa huzuni akimuangalia Yule mtoto.

Docta ushauri akasema;

‘Hayo yasikutie shaka, kila kitu na wakati wake, na huyo mtoto, atakua na akisoma vyema, akasikia huko ulipotokea atakusifia sana, kuwa wewe ulikuwa mama mjasiri sana…muhimu kwasasa ujue huyo ndiye jembe lako, mtunze, mpende, na wala usionyeshe hayo machungu mbele yake maana ukilia lia utamjengea huzuni moyoni mwake…’akaambiwa
Kukapita kitambo, tukiogopa kumuuliza maswali mdada tulitaka atulie kwanza na mwenzangu akaukatiza ukimia kwa kusema
‘Samahani mdada kwa kukuuliza hili swali tena,…Je ulitaka kujiua kwa shinikizo au kwa hisia zako kuwa hutaweza kuishi tena?’ jamaa yangu akauliza hilo swali tena. Na mdada akatulia kama anawaza halafu akasema

‘Hata sijui niwaelezeje…ilifikia hatua nikahisi hivyo, …ndio ni kweli hawa watu walitutisha sana, na nilijua hata nisipojiua wao watakuja kuniua tena kwa mateso makali,..na zaidi wangeliwaendea wazazi wangu wakawatesa, hadi kufa…’akasema

‘Una uhakika na hilo, kuwa huwa kweli wanakwenda kwa wazazi na kuwatesa?’ akaulizwa

‘Nyie mnahitajia ushahidi wa moja kwa moja…ndio maana hawa watu wanawashinda, kuna wazee wanauwawa kwa kusingiziwa uchawi, je ni kweli ni wachawi..?’ akamgeukia ofisa upelelezi

‘Mliwahi kulichunguza hilo vyema, ni wazee wa watu hawana hatia, maisha magumu mpaka macho yanabadilika, eti kubadilka kwa macho, kubadilika kwa sura kutokana na shida, inaonekana kweli ni wachawi…’akasema

‘Ina maana ni wao wanasababisha hayo…?’ akaulizwa

‘Wanapotaka kuua, kutesa, wanatafuta mbinu za kila namna , ili kuwe na sababu, ili uchunguzi uamini hivyo, , ..lakini kumbe ni mbinu za hawa watu…wazee wanachomwa moto, wanakufa kifo kibaya, cha mateso kweli mnachungaza hivyo vifo kwa undani…?’ akawa kama anauliza
‘Hamuwezi ….mtajifanya kuchunguza na wananchi kwa vile wameshahadaiwa kiakili na hawa mawakala wao…mkiwauliza hawatakosa sababu….’akatulia
‘Na hata hivyo….hii aibu ya haya yote,…..najua kijijini huko najulikana kwa jina baya sana,…nakumbuka babu aliniambia, ukitaka kumuua mbwa kwanza umuite kwa majina mabaya, ndivyo ilitokea kwangu,..kwahiyo pamoja na haya yote,mmh, nilichanganyikiwa, niliona ni heri kufanya hivyo…’akatulia kidogo kama anawaza jambo, halafu akasema;
‘Naikumbuka sana siku ile, nilitaka kweli kutimiza dhamira yangu..

‘Kiukweli …nilishadhamiria kutimiza hilo, sikuwa na kurudi nyuma…baada ya kuitoa ile bahasha yenye dawa, …. ndio nikasikia mtu anakuja…kwa haraka nilitoa kidonge kimoja nikakiweka kwenye ukucha, kuna jinsi tulifundishwa…’akanyosha kidole kidogo juu na kukiweka mdomoni.

‘Kile kidonge ukikiweka hapa kwenye ukucha, ikifika muda unakitumbukiza mdomoni,…kinatotaka tu maana kikikutana na umaji maji  kinayeyukia…hata sijui walivyoniokoa,

‘Ila kuna kitu natilia shaka, …huyu nesi, ni kama  aliniona, akajifanya hanioni, na alipohakikisha nimeweka kidole mdomoni, ndio akanifuata na kunishikilia mkono, akaita saidia…saidia…lakini sina uhakika na hilo…’akasema

‘Huna uhakika kwa vipi..?’ akaulizwa

‘Kama alikuwa ana nia ya kuniokoa, asingelifanya vile , hakutumia nguvu kunivuta mkono…nashindwa kuongelea hili, …lakini, mhh, hata sijui, ngoja niache tu…’akasema.

‘Usiwe na shaka, hilo tunalifuatilia…’akasema ofisa upelelezi

‘Unajua Ile dawa, ni kidonge kidogo sana, ukikifikisha mdomoni, kinayeyuka, na kuteleza, kwahiyo kitatoka kwenye ukicha na kuingia mdomoni,…i…sasa pale, nahisi wakati nainua mkono…nahisi ni kwa vile…, mkono ulikuwa na maji maji ya jasho…kwahiyo nahisi kilidondoka kabla hakijafika mdomoni…nahisi hivyo, …’akasema

‘Kwanini unahisi hivyo…?’ nikauliza

‘Kwahiyo ilikiona kikidondoka chini..?’ mwenzangu akauliza

‘Sikukiona kikidondoka, muda huo nilishafumba macho…, ila kwa vile kidole kilipofika mdomoni, sikuhisi hiyo dawa, ulikuwa ukicha tu.. na nikahisi hakijayeyuka, …ila nina uhakika wakati nainua mkono ili niweze kulifanya hilo tendo, nilikiona kikiwemo kidoleni….sasa kilikwenda wapi, kama kweli hakikudondoka chini…’akasema

‘Na bafuni kulikuwa na maji , kama kilidondoka kitakuwa kiliyeyuka na kupotelea kwenye maji, tulichunguza hivyo, lakini hatukuona dalili hiyo…’akasema ofisa upelelezi.

‘Kwanini sasa mlichunguza…kwani mlikuwa na uhakika kuwa hakukimeza…?’ tukamuuliza ofisa
‘Ni kawaida ya uchunguzi wetu kuchunguza kila kitu…na wakati wengine wanamchunguza watu wa huduma za kwanza na madakitari waliendelea kumchunguza mdada kuhakikisha tunawahi kumuokoa, …lakinii hakukuwa na dalili za dawa yoyote….’akasema mpelelezi

‘Na tulivyoona hivyo, tukaingiwa na hamasa ya kuchunguza eneo lote, ….’akasema

‘Mdada aliwaambiaje  kuwa alishakunywa hiyo sumu au la, hakuweza kutoa ushirikiano…?’ akaulizwa

‘Kwa muda huo alikuwa kama kachanganyikiwa, hakutaka kusema chochote, alikuwa kimia tu…’akasema docta

‘Kwa hali kama ile, tulichelea kumfanyia upasuaji,…tukasubiria hadi siku ya pili yake,  na siku zote zote hizo alikuwa kimia, haongei…. lakini wenzangu walipompima na kuona hana shinikizo, hana tatizo lolote wakasema wanaendelea na huduma za upasuaji…ikafanyika hivyo, na upasuaji ulifanikiwa….’akasema docta

‘Kwa kifupi ni kuwa mdada hakufanikiwa kukimeza hicho kidonge…?’ nikauliza

‘Hakufanikiwa….hilo tuna ihakika nalo kabisa, kama angelikimeza asingelichukua muda angelikata roho…vile vidonge vimechunguzwa, ni hatari ….na dalili zake za mwanzo, muathirika au muhanga anatoka na mapofu, lakini hayakai muda, yanakauka kwa haraka sana..ukifika huwezi kugundua kitu, tulipofika kumuokoa, hakukuwahi kutokea kitu kama hicho….na ni muda mfupi sana!

‘Au nesi alichelewa kuwaita…’akasema mwenzangu

‘Hapana…tuna uhakika hakukimeza…nawaambia ile ni simu kali, inakimbilia haraka kwenye damu na kukata mawasiliano ya mapigo ya moyo’akasema docta

‘Kwanini mdada uliamua kukimeza hicho kidonge huko bafuni..na usisubirie ukiwa kitandani?’ akaulizwa

‘Nilishahisi kuna kitu kinaendelea, nikahisi huenda wameshanishtukia, kuna sauti iliniambia nifanye haraka kwani wanataka kunizuia, nikumbuke wazee wangu watateswa. Huyu mtu alikuwa ni nani..’akawa kama anauliza

‘Kuna mtu, au sauti au hisia zako…?’ akaulizwa

‘Hata mimi sijui.. ndio maana nasema huenda hata humo hospitalini wapo hao watu, sizani kama ni sauti za majinamizi, au hisia zangu tu….ndio maana nikaona bora nijikate mwenyewe kihivyo, niende  nikajipumzikie kama huko kuna kupimzika…’akasema

‘Una maana gani kusema kuwa huenda hapo hospitalini wapo hao watu?’ akaulizwa

‘Kila usiku kuna mtu alikuwa akinijia na kunitishia,…’akasema

‘Huyo mtu mwanaume au mwanamke, ni docta au ni nani,..?’ akaulizwa
‘Kiukweli siwezi kusema ni nani…maana inavyotokea inakuwa kama naota, mtu ananiambia jambo, kwa sauti nzito, lakini cha ajabu …nikiamuka simuoni huyo mtu, ….’akasema

‘Unasikia sauti kabisa..?’ akaulizwa

‘Nasikia sauti kabisa nikiwa usingizini, sizani kama ni ndoto…na jingine…’akatulia kama anasita kuongea

‘Na jingine lipi…?’ akaulizwa

‘Jamani hebu jiulizeni hata nyie, ni kwanini hiyo barua pepe haikufika kwa hawa watu kwa wakati muafaka, mna uhakika kweli, kuwa ni tatizo la mtandao….lakini mimi sijui, labda ni hisia zangu tu…’akasema

‘Hilo usijali tumelifanyia kazi, hebu tuambie, kuna Jambo jingine lolote linakufanya uhisi kuna watu humo hospitalini, au…, wewe sema tu usijali…?’ akaulizwa na mpepelezi, na mdada alionyesha kama kusita kuongea

‘Na kwanini nilielekezwa niende kwenye hiyo hospitalini…na wakati kule hospitalini walisema nipelekwe muhimbili. ….’akasema akimuangalia mpelelezi halafu kwa haraka akamtizama docta mara moja na kugeza kichwa kumuangalia mpelelezi.

‘Yawezekana waliokuelekeza huko wanakifahamu kituo hicho kuwa taasisi inayohudumia wagonjwa wa namna hiyo kwa haraka…’akasema mpelelezi

‘Mhh…mimi nimejiuliza sana hilo swali, sijui nyie wenzangu, labda ni sawa ni hivyo, waliona hivyo…au ndio imetokea tu, labda ni hisia zangu tu, ila inanipa maswali mengi yasiyokuwa na majibu…!’akasema na dakitari mshauri akatikisa kichwa kama kuonyesha kuwa mgonjwa hajakuwa sawa.

‘Hebu nikuulize ni nani alikuwa mara kwa mara akikuhudumia pale hospitali, ambaye mara kwa mara alikuwa nawe …?’ akaulizwa
‘Kuacha docta..au?’ akauliza na hakusubiria kujibiwa akaendelea kuongea
‘Mtu ambaye alikuwa yupo name nami mara kwa mara ni nesi,…huyo alikuwa anaonekana kila mara mle ndani…na ikitokea tatizo huyo nesi huwa anamuita Yule dakitari msaidizi…’akasema

‘Je hiyo sauti unayosema inatokea ya kukutisha kuwa ujiue,…. ni sauti ya kike au ni ya kiume?’ akaulizwa

‘Mhh, ni vigumu kusema, maana ni sauti nzito, ya kiume, lakini wakati mwingine nahisi kama ni sauti ya kike ila anailazimisha iwe nzito kama ya kiume, …si unajua …lakini huyo hata kama ni mwanamke, basi atakuwa na sauti nzito ya kiume ume hivi…’akasema

‘Mhh, kwanini unasema hivyo..?’ akaulizwa
‘Kwanini iwe kama ya kulazimisha,…unajua mwanaume akiwa na sautii yake nzito, hahitajii kulazimisha iwe nzito zaidi,…sasa huyo anakuwa kama anailazimisha zaidi isikike kama ya kutisha…’akasema na docta mshauri akataka kusema neno, halafu akaacha akamuangalia ofisa upelelezi

‘Unajua kuna kitu kitu nimekikumbuka,….’akasema

‘Kitu gani….?’ Akaulizwa

‘Unakumbuka tulivyoongea siku ile….haiwezekani ikawa hivyo…?’ akauliza na mwenzake akatikisa kichwa kaka kukubali.

‘Basi ngoja nihakikishe kitu….’akasema na kuchukua simu, akapiga namba , na kuanza kuongea kwenye simu.

 ‘Huyo nesi anayehudumia wagonjwa mahututi yupo?’ akauliza na kusikiliza

‘Kaenda wapi, dharura gani imempata, ok mimi nilikuwa sijui maana leo nimepitia huku kituo cha polisi moja kwa moja…, ok sawa….?’akakata simu akamgeukia ofisa upelelezi, na kusema.

‘Unajua huyo nesi ana sauti nzito, na siku moja aliwahi kunitisha kwa kuongea sauti nzito kama ya kiume nikiwa nimeinama bila kumtizama, nikajua kweli ni mwanaume anaongea....na mdada alipoongea hivyo…nikashtuka kidogo, ..hata hivyo nesi huyo ana dharura kaomba ruhusa ya siku kadhaa….’akasema docta

‘Usijali docta, hilo limeshafanyiwa kazi, vijana wangu wanafuatilia, hatutakiwi kuharakisha haya mambo…na kwa safari hii, wote wanahusika watakamatwa,..wengine ambao watashirikiana nasi tutawashikilia tu kwa usalama wao…, docta, tupo pamoha, wewe utapata taarifa badaye…’akasema ofisa upelelezi, na docta akawa sasa kama hana amani fulani hivi.

Sisi pale tukawa tunaangaliana, ni nani aulize swali kwani mambo yalikuwa yakiongezeka, na mlengwa wetu ni mdada, hatukutaka kuingilia kazi zingine….na ofisa Upelelezi akasema;
‘Kwa ujumla tatizo hili ni kubwa sana, kinyume na Inavyofikiriwa…inahitajia muda mrefu sana wa kulimaliza, ngoja tuone hii awamu, awamu ya kazi, wengi wataibuliwa…’akatulia akiangalia saa yake

‘Ni sawa tunakuunga mkono kwa hilo, lakini ni kama hao watendaji wenye dhamana watakuwa kwa ajili ya wananchi, wawe karibu na wananchi na kazi iwe kazi kweli,…maana pia hawa watu wabaya wana mbinu nyingi ni wajanja sana,…sasa hivi wameshajigeuza na hutaamini , kwa ujanja wao wameshajipenyeza kwenye `system’ lakini nina imani kuwa watagundulikana tu, …’akasema docta

‘Unavyoongea hivyo ni kama vile mnawafahamu…’akasema mwenzagu

‘Kwa tabia zao…mali walizonazo…wewe fikiria wamewekeza hadi nje, wana dhamana za benki huko nje…walipata wapi hizo pesa, tukianza kurudi kinyume nyume tukachunguza nyendo zao…watajulikana tu hebu jiulize kwanini viwanda vingi vya serikali vilikufa ni nani walikuwa wakurugenzi, na sasa wana nini,….yaonekana kabisa ilikuwa ni mbinu ya kujinufaisha…’akasema docta akimuangalia ofisa na ofisa akaitikisa kichwa kama kukubali

‘Sasa kwanini hawakamatwa, ni kwasababu kila jambo na wakati wake…, kulikuwa na uhuru wa kuwekeza, ukaja wa kulipa kodi, ukaja wa miundo mbinu sasa ni kuwajibika….ni hatua hizo za utekelezaji….nyie mtaona tu, waaminini viongozi wenu’ akasema ofisa mpelelezi

‘Mimi nina wasiwasi..,maana kila awamu, sio kwamba hawa watu wamelala,wao wanajua ni nini na nani atakuwepo ….wameshajipanga, na watu wao wameshatayarishwa…sasa sijui mtawabana kwa mbinu na ushahidi gani…’akasema docta

‘Ushahidi sio lazima…ila matukio kama haya ndio yatatusaidia, tunajua hawa watu ni matajiri,wana pesa, wana mawakili wao, na ukumbuke na tunajua kuwa kuna watu wao pia wanawabeba, wamewekeza kwa hilo, na watu waliosoma sana , huwezi kuwatilia mashaka,…na ndio maana kesi  zinakuwa ngumu sana na hata kutukatisha tamaa….lakini wakuu wamejipanga kwa hilo, maana hawa wakuu wa sasa wametoka wapi, wanawafahamu, walikuwa wakiumia sana, na sasa wamepata nafasi ya kuwabana, ni swala la muda tu…’akasema

‘Haya sisi tutawasikiliza nyie, hasa watu wa usalama, muwafichue, na muhakikisha mnawawajibisha mkifanya hivyo kila mtu ataogopa, na nchi haitakuwa shamba la bibii tena, lakini bado, bado…’akasema docta akisita kuendelea

‘Ni kweli….ila tutambue hii kazi sio ya viongozi peke yao, ….kila mtu asiogope kufichua haya maovu, maana wavumao baharini ni papa,…lakini samaki wengine wapo…..swali ni nani ni nani, kama alivyosema mdada ,  hawa watu ni waigizaji wakubwa, wanakwenda na nyakati, hivi sasa wameshavua ngozi zao , ni watakatifu kweli, wachapakazi wa kikweli ukiwaona, na wanajifanya kutetea watu, hutaweza hata kumtambua yupi ni yupi, ….’akatulia kidogo

‘Mimi naona huu muda serikali ingewashirikisha wananchi, wananchi wanawafahamu sana hawa watu,…kama kutakuwa na namba fulani za kura za siri…mnaweza kupata msaada mkubwa…majambasi wanaishi na watu, achilia mbali hao mafisadi ambao sasa wana maeneo yao tofauti wamejenga mahekalu yao, lakini wanajulikana,……..’akasema jamaa yangu

‘Sheria ina namna yake, kushuku ni kitu kingine, na kuwa mkosaji ni kitu kingine, sisi kama wapelelezi tunafanya kazi yetu na tunajua ni nini tunachokifanya, …ni kweli kuna changamoto zake maana haya hayakuanza leo, ushahidi, ukiupata unakutwa umeshachakachuliwa, na siwezi kukataa, hata huku kwetu hao watu wapo, lakini hatua kwa hatua tutalimaliza…’akatulia akiangalia saa yake

‘Kila mtu analishaona kumbe, …..ujanja kuwahi, kumbe…na mimi nikizubaa nitakosa, kila mtu akawa anachukua chake mapema,wakawekeza watoto wao kwenye elimu, shule za kimataifa..ili waje kushika madaraka…. Kwahiyo huu ni mtandao mpana, na ndio maana hivi sasa huwezi kuwabaini tena wamaeshajibadili kabisa,….ngozi ya kondoo, hili ni tatizo sugu….’akasema

‘Lilikuwa kama kama sikio la kufa,…’akasema docta akimuangalia mdada na wakati huo ,mdada alikuwa kama hayupo, alionekana kuwaza mbali

‘Lakini niwaambie kitu,…`system’, mfumo ni tatizo kubwa ….’akatulia, hata hivyo tusikate tamaa, ni tatizo lakini linaondokeka, na hili ni rahisi sana,  kwa mwananchi wa kawaida kuliondoa kama watakuwa na umoja, huyu mtu wa kawaida akiamuka, akajitambua, akajua haki yake ni ipi, mabadiliko yatakuja tu….na viongozi wa kweli  watatokea huko…kwa mwananchi wa kawaida anayejua shida,….’akatulia pale mlango ulipogongwa.

Mara akaja mtu akasema

‘Mdada anahitajika kwenye taratibu zako za dawa..’

Na mdada akabakia amekaa, akageuka kutuangalia, na kusema

‘Ahsanteni sana wanandugu, najua mumetoka huko mbali kuja kuniona, kuja kunisaidia, lengo lenu lilikuwa jema, …japokuwa,….’akasita kuendelea

‘Hatukufanikiwa kufika kwa wakati….’akasema mwenzangu

‘Lakini sio kusudio langu kuwa mfike kwa wakati, kuja kuniokoa, nilitaka huo ujumbea ufike kwa mlangwa….hata hivyo, imanipa faraja kuwa bado wapo watu wenye huruma, nawashukuruni sana kwa hilo. Na kwa ajili hiyo, nimeridhia …. muiweke hewani,  ili watu wajifunze kutoka kwangu…nataka jamii ielewe mambo yaliyojificha nyuma ya pazia….’akageuka kumuangalia ofisa upelelezi.

‘Huko uraiani hali ni mbaya,…na hii ni kutokana na maisha magumu, wenzetu mjini wana huduma zote muhimu, kijijini zippo wapi, hata umeme ni shida, barabara mbovu, maji tunategemea chemu chemu au kwenye mabwawa machafu tunapokezana na mifugo …..mnajua wenyewe hali ilivyo, …

‘Kwahiyo, watu, hasa vijana  wakisikia watu wanatoka, wana maisha mazuri, magari, nyumba nzuri, …wanakuwa na hamasa ni kwa vipi, ni sababu ya kazi za ofisini, au ni sababu ya sanaa, muziki, urembo, au ..basi wanavutika kuiga,…’akatulia kama anawaza jambo

‘Ni kama vile unavyoangalia kwenye sinema ukavutika na ‘stelingi’, zile sifa zake, ushupavu wake, au utajiri wake au muonekano wake, basi kila mtu atapenda kujiigiza kama yeye, japokuwa ni kuigiza tu,…ni hivyo,…’akabenua mdomo idogo

‘Na maishe yetu huko kijijini, ndio hivyo,  watoto, vijana ni ya kuiga iga tu, kila mmoja anatamani kuja huku mjini, na hili la kuiga iga, sio huko kijijini, tu…nadhani hata huku mjini, ndio hivyo hivyo, au nadanganya, huku wanataka wawe kama wazungu, au sio…..si-unaona watu walivyo, wanaiga hata kuvaa uchi, hatuwezi kuiga kutengeneza magari…kwasababu hakuna vifaa, mhhh, ….’ Akajitahidi kutabasamu

‘Ni kutokana na maisha…wenzetu wamewahi,….na wanataka kuendelea kutunyonya, sasa wafanye nini, wanabuni mbinu, wakagundua kumbe… wanaweza kuwekza jambo kwenye hali hiyo,…wajanja kweli kweli wakabuni hayo madawam ili kutumbaza akili,…’akatugeukia

‘Kama mungu atanijalia nikapona na mwanangu, na mimi nitajitahidi…, nije tuungane kuielimisha jamii kuhusu haya yaliyonikuta…mungu akipenda

‘Lakini jamani kwa hivi sasa sitaki kabisa mtu kunifuatilia,…niachane, haya ninayopambana nayo yanatosha, kwasababu hapa nilipo bado nipo kwenye mapambano, ya kufa au kupona,..na sijui kama nitapona…ni kunipa matumaini tu….na huyu mwanagu….’akamwangalia mtoto wake

‘Utapona tu mdada,….haya yote utayasahau….’akasema docta

‘Mungu ndiye anajua zaidi, …mimi na mtoto wangu, tupo kwenye ukingo wa kaburi, kwahiyo, tumuombe yeye, akijalia, kama nitaishi, ….nitawatafuta,…’ akasema huku akimwangalia mtoto wake, na docta ushauri akamkatiza akisema….

‘Jipe moyo mdada,…sote tupo kwenye ukingo wa kaburi, hakuna anayejua ya kesho, mungu pekee ndiye ajuaye hayo, lakini kwa mwanadamu, hatutakiwi kukata tamaa,..muhimu ni kujipa matumaini, kuwa nitaishi, nitaiona kesho na kesho kutwa na hata miaka ijayo, kama vile utaishi milele, usikate tamaa, na pia kumuomba mungu ni wajibu tumuabudu mungu kama vile safari imewadia, yote ndiyo maisha ….’akasema akionyesha mikono juu

‘Kwa hivi sasa mdada, Inatosha, umesikia ulivyo ambiwa, hivi sasa unahitajika kwenda kwenye dawa, ….’akasema docta na yule mwanadada mwingine akasogea na kumchukua mtoto, wakatangulia kuondoka, na baadaye Yule ofisa upelelezi akatugeukia na kusema

‘Na nyie mpo huru kuondoka..’ akasema na hatukuwa na zaidi, tuliwashukuru na kuondoka.


                                                       MWISHO


WAZO LA LEO: Maisha ya mwanadamu ni kupambana na mazingira, kuhangaika, kitafuta, kama vile tutaishi miele, lakini kwa njia zilizohalali, na wakati huo huo, tunahitajika kumcha mola wetu, kumuabudu yeye na kumshukuru kwa neema alizotupa kama vile hatutaiona kesho. Yote ndiyo maisha  yetu. Tusitende yasiyo haki na kujaa kiburi.  

Ni mimi: emu-three

3 comments :

Samira said...

Ndugu wa mm kid a kimetupa fundisho sana na changamoto nyingi alopitia huyu dada namuomba awe strong mungu yupo

Anonymous said...

Tupo pamoja

emu three said...

Tupo pamoja kwa saana