Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeFriday, April 29, 2016

MAPENZI YA MUNGU(Duwa ya mwenye kudhulumiwa)-2REJEA: Kisa hiki ni cha mjane na watoto wake, waliotakiwa kudhulumiwa mali zao, ikiwemo nyumba, ikafikia nyumba kupigwa mnada ili kulipia deni la nyumba…mama na watoto hawajui waende wapi, hawajui deni hili limetoka wapi, ndugu wa kiumeni  wanawapiga vita…kisa ni nini….mama akiulizwa anasema yeye kamuachia mungu, maana yote hayo ni mapenzi ya mungu…Je iwe hivyo tu…
Tuendelee na kisa hiki tuone ukweli nyuma ya pazia…
                                                          *********
‘Lakini nikuulize unaniuliza haya maswali yote ili iweje….sisi yote hayo tumeshamuachia mungu, na nimekuambia hayo niliyoweza kukuambia,…yatosha,…’akasema na kujikuanyata.

Kauli hii yake hiyo ilinifanya hata mimi nijiulize, je ninavyomuuliza haya maswali nitawezaje kumsaidia huyu mama mjane na watoto wake,  akili yangu ilifanya kazi kwa haraka nikamkumbuka rafiki yangu aliyebobea kwenye sheria na mara nyingi hujitolea kuwasaidia watu kama hawa, nina uhakika akilisikia tatizo la huyu mama, huruma itamuingia anaweza akamsaidia, ndipo nikamuambia huyo mjane;

‘Shemu unajua matukio huja, humtokea mtu kama mitihani, na mara nyingi tunayaona kama matukio tu,…na pengine mtu kujiona yeye labda kaonewa na mungu, lakini matukio mengine yanasababu, hayatokei hivi hivi tu, ….kuna dhuluma zimetengezwa, ….mimi katika hayo maelezo machache uliyoniambia, nimehisi kuna tatizo,…hapo kuna jambo halipo sawa, …’nikasema

‘Ndio kuna tatizo lakini, sioni sababu tena ya kuhangaika, mimi nimeshaamua…., tuyaache kama yalivyo…wewe nenda kamtafute mnunuzi unayemuona,….. kama sio wewe unayetaka kununua, nyumba ndio hii hapa inapigwa mnada, nyumba mume wangu aliyoihangaikia kwa ajili ya watoto wake, sasa hayupo,…mimi nimeshindwa, nitafanya nini masikini  wa mungu….’akasema kwa uchungu.

‘Shemu sio kwamba nataka kukukosanisha wewe na shemeji zako,…hapana, ila nahisi kuna tatizo, linaloweza kusababishwa huenda na wao,…hata hivyo bado siwezi kulihakiki  hilo tatizo mpaka nisikie maelezo yako yote…’nikasema

‘Ili iweje…?’ akauliza akiniangalia kwa jicho moja

‘Shemu wakati mwingine watakiwa kuipigania haki yako, na katika kuipigania haki yako, unatakiwa umuweke mungu mbele kuwa akusaidie, usiogope, usiwe mnyonge, pambana vinginevyo, watu wenye mioyo ya dhuluma, watachukua kila kilicho chako na kamwe hawatosheki……’nikatulia nilipomuona anataka kusema neno lakini hakufunua mdomo.

‘Unajua shemu, mungu  humsaidia zaidi Yule anayejihangaisha, na huwezi jua mimi naweza kuwa mmoja wa msaada wako kwa kupitia…. , jiulize kwanini nimeweza kufika hadi hapa, wakati sina uwezo wa kuinunua hiyo nyumba, mimi sio mnunuzi, sina uwezo huo, lakini nikavutika kuja hapa na kuonana na wewe…kiukweli mungu mwenyewe anajua ni kwanini, ….’nikatulia nilipomuona yanamuingia.

‘Mhhhhh’akaguna hivyo tu.

‘Sasa shemu mimi naona tufanye kila kinachostahiki, ….tuchukue hatua , tujitahidi kuitafuta haki, ili mali ya hawa watoto, mali yenu mliyoihangaikia wewe na mwenzako akiwa hai  isiende mikononi mwa watu wasiostahiki, na mengine tutamuachia mungu, lakini kwanza tufanye jitiihada…nina imani kwa mapenzi yake mungu tutafanikiwa…’ nikasema na yeye akatikisa kichwa kama vile kukataa…moyoni nikajiuliza ni kwanini  huyu mama anakataa kudai haki yake ni lazima kuna jambo!.

‘Labda mimi kwanza nijitambulishe kwako,….’nikasema na yeye akanikatisha kwa kusema

‘Haina haja, wewe kama sio mnunuzi, mimi naona uondoke tu, kwani  oh, sijui nisemeje, ….ila nikuambie kitu, kama unachotaka kusema ni kwenda mahakamani, ….hapana , mimi sitaki tena kwenda huko mahakamani,….nikafanye nini tena huko, nimechoka..’akasema akitikisa kichwa

‘Ina maana kumbe uliwahi kwenda mahakamani…!...?’ nikamuuliza na yeye kwanza akabakia kimia, baadaye akasema;

‘Ilibidi nifanye hivyo…..’akasema na kutulia, baadaye kabla sijasema neno akasema

‘Ni baada ya kupewa barua ya notisi kuwa nyumba hii inatakiwa kupigwa mnada,…nilishtuka sana siku hiyo, na siku hiyo shemeji hakuwepo, ikabidi nianze kufuatilia ni deni gani hilo,…na nilikuwa bado sina nguvu, lakini ….ikabidi nikajitetee, maana sasa tungeenda wapi, ..hawa watoto watakwenda kuishi kwa nani,  hata hivyo, sikufanikiwa…’akasema

‘Shemeji  mimi nina mtandao wangu wa jamii, na moja ya kazi yake ni  kutetea wanyonge, tunajaribu kutetea haki za wanyonge kwa njia ya kuandika visa na matukio yaliyowafika watu,mbali mbali kwa ridhaa yao, na kwa njia hiyo taarifa zinafika kwa wengi,…’

‘Na kwenye wengi pana mengi, miongoni mwao  kuna mungu kawajalia hekima , busara, kawajalia utashi, kawajalia duwa zenye kujibiwa, na zaidi kuna ambao hujitolea kwa ajili ya watu….. nimekuwa nikiwatetea akina mama, watoto..wazee, wanyonge, waliodhulumiwa, …na imeleta mafanikio,..japokuwa ni kazi ya kujitolea tu!’nikatulia pale aliponitupia jicho kama la kujiuliza.

‘Ina maana unayafanya hayo bure…?’ akaniuliza

‘Ni nani atakulipa,….ujue hapo unatetea wanyonge watu wasio na kitu, unataka nini tena kwao…sisi anatulipa mungu….’nikasema

‘Lakini mimi sihitajii huo msaada wenu….na sitaki mambo haya yajulikane, ….sitaki kabisa, naombeni tafadhali…’akasema akionyesha wasi wasi mkubwa.

‘Usiogope,….kwani kwa jinsi sisi tunavyoandika  hizo habari,  inakuwa haipo wazi kihivyo, kuwa watu watakufahamu waje kukusumbua, hapana…tunachofanya ni hivi baada ya kuupata ukweli ulivyo, tunakahakikisha  ukweli wake, hatutaki kuzua, unaona, ….kwa njia zetu tunajua jinsi gani ya kuupata huo ukweli…,

‘Tukishaupata ukweli, tunatafuta watu wanaoweza kulifuatilia hilo jambo…na wakati kazi inaendelea ndipo sisi tunashika kalamu,…unajua kalamu ina nguvu sana kwa wenye kuelewa, kalamu ni silaha, silaha yenye kuua au kusaidia, silaha yenye kujenga au kubomoa,…’nikatulia kuona kama ameelewa

‘Hapo ndipo  tunaanza kuliandika hilo tukio, kutokana na ushahidi tulioupata, ukweli  na uhalisia wake, na kuliweka  hilo tukio hewani  , kuna watu wenye mioyo yao safi wanalifuatilia hilo jambo  kwa kujitolea…najua dunia ya sasa kila kitu ni biashara, lakini wema …..sio biashara.  Na tunachotaka sio kumsaidia muhanga tu…, tunapoliweka hilo tukio hewani,  tunakuwa tumesaidia jamii kubwa…., na haki inapatikana…’nikasema

‘Mimi nimekuelewa, lakini kwa hili langu, usijisumbue bure, hujui ni kitu gani kipo hapa, huwajui hawa watu walionizunguka,….kifupi mimi sitaki kuendelea ku-kukuelezea zaidi maana naogopa…’ akawa anasita kuniambia jambo.

‘Kwanini uogope shemu, kwani hii sio haki yako, nyumba ,mashamba si mali yenu, kwanini uogope…?’ nikamuuliza

‘Mimi naomba uniache,…sitaki tena kuongea zadi, japokuwa nyumba, mashamba, ni mali halali ya watoto wangu, mali aliyoichuma baba yao kwa shida, akajinyima….we acha tu, ni haki yao, lakini utafanyeje…., kwa hivi sasa Mungu pekee, ndiye anayeweza kutoa haki, sitaki tena, kama ni mali wachukue tu, waniache mimi na wanangu, sisi tumemuachia mungu kwa mapenzi yake najua haki itapatikana….’akasema akiinua mikono juu, halafu akainama na kukaa mkao ule wa huruma.

Nikaona ni muingie kwa njia nyingine, nikauliza…

‘Hebu  kwanza, nikuulize,  huo mkopo  ulijaribu kufuatilia ukajua  ulitolewa kwa ajili gani, kufanyia biashara, kujengea au kufanyia kazi gani, …?’ nikamuuliza, alikaa kimia kwanza bila kunijibu nikajua labda hataki kuongea tena, na ghafla akasema

‘Mhh, huo mkopo …walisema ulichukuliwa kwa mambo mbali mbali, ikiwemo biashara, kusaidia familia, na utarejeshwa kwa kupitia biashara,  na dhamana yake ikawa ndio hii nyumba, na …hapo sielewi zaidi na pia walisema ni , kwa ajili ya matibabu yangu, haya ya matibabu alianiambia shemeji  ni hivyo tu…’akasema

‘Shemeji…. ukiwa na maana huyu aliyechaguliwa kuwa msimamizi wenu…?’ nikamuuliza kuwa na uhakika zaidi

‘Ndio, yeye ndiye angeliweza kufanya hilo…., huyo  aliyechaguliwa kama msimamizi wa mali ya marehemu mume wangu…’akasema kabla hajatulia  nikauliza swali la haraka haraka

‘Ulisema yeye  alichaguliwa kuwa msimamizi wa mali ya marehemu mume wako wakati wewe hujitambui au sio na baadaye ulipoanza kujitambua mkawa mnashirikiana naye au sio?’ nikamuuliza

‘Ndio kama nilivyosema awali, kipindi hicho, nilikuwa sijiwezi,  sikuwa na utambuzi mnzuri, nilikuwa kama maiti tu,….wanasema nilikuwa kama nimechanganyikiwa siongei, nipo nipo tu, …nimelala mwili haufanyi kazi, … ‘nimeparalize’.. kwahiyo asingeliweza kushirikiana nami, yeye alifanya kile alichoweza yeye kufanya…’akatulia kama kakumbuka jambo, lakini akasita kusema

‘Sasa kuhusu huo mkopo, ujuavyo wewe, au ulivyoanza kufuatilia, ulitolewa lini, na ulikuwa umechukuliwaje,  maana nauona utakuwa mkubwa sana …’nikasema.

‘Hilo ndilo lilinifanya ning’ake, kwanini wamesinginizie mume wangu kuwa yeye ndiye aliyeanza kuchukua  huo mkopo benki kabla hajafariki, hilo sikubaliani nalo kabisa na denim bona kubwa sana….’akasema

‘Hayo uliyajulia wapi, kuwa mume wako ndiye alianza kuchukua huo mkopo….`alianza ..’ au sivyo?’ nikamuuliza

‘Siku nilipoamua kufuatilia, niliambiwa deni hilo ni la siku nyingi, limeanzia kipindi mume wangu akiwa hai…’akasema

‘’Alianza, yeye ndio alianza….ok,  sasa ni nani alikuambia hivyo..?’ nikamuuliza

‘Ni watu wa benk….’akasema

‘Hapo sasa tunakwenda sawa, watu wa benki ndio waliokuambia au sio….’nikasema

‘Ndio hivyo….’akasema kama vile anajua nimemalizana naye, nikamuuliza

‘Nirudi nyuma kidogo, …ulifanya yote hayo , kufuatilia, ni baada ya kwenda mahakamani kufuatilia ili kuweka pingamizi  si ndio hivyo?’ nikauliza

‘Ndio hivyo …..nilipopokea hiyo barua ya kuwa nyumba itapigwa mnada deni lisipolipwa, …nilichanganyikiwa kabisa, sikujua ni deni gani, na kipindi hicho shemeji alikuwa hayupo kasafiri sehemu ya mbali na hatarajii kurudi karibuni, nikaonana na mtu ninayemfahamu, yeye ndio akanisaidia, tukafungua pingamizi,…’akatulia.

‘Ok, ikawaje…?’ nikauliza

‘Pingamizi ina maana ili lipite natakiwa niende mahakamani….mambo yao haya siyaelewi, mambo ya mahakama ningeyajulia wapi…..ndio tukafika mahakamani kabla ya kesi, kuna kusikilizwa kwanza,  nikaambiwa nipeleke vielelezo vya kusaidia hilo….nikauliza vielelezo gani…?,  wakaniambia vya kuthibitisha madai yangu…sasa hapo…uone, mimi ningevipata wapi hivyo vielelezo…’akatulia

‘Ndio nikarudi kwa huyo rafiki yangu akanishauri niende benki, na ndio nikakutana na hiyo kauli, kuwa hilo ni deni ni la siku nyingi….halikuwahi kulipwa kutokana na makubaliano,…kuna mkataba wa mkopaji na benki  ulitaka deni hilo lilipwe kwa kiasai fulani kila baada ya muda fulani, lakini haikuwahi kulipwa….,

‘Nikaomba tu nipewe hiyo statement,ili niweze kuipeleka  mahakamani …hiyo wakanipatia haraka, lakini nilipopeleka nikaambiwa hiyo haitoshi, natakiwa nakala ya mkataba, hati za malipo na vitu kama vitatu hivi,……ilikuwa kazi kuvipata kwa watu benki, maana ilibidi nirudi tena mahakamani wanipe barua, ndio nikarudi tena benk wakanipatia…..’akasema

‘Kwahiyo hilo deni la siku nyingi au sio, kama ni la siku nyingi ni kwa muda gani, tangia mumeo akiwa hai au sio, ina maana ni deni  alilochukua mume wako bila yaw ewe kujua, au….’akanikatisha,

‘Mume wangu hajachukua mkopo…nimeshakuambia unielewe, mume wangu hakuwahi kuchukua mkopo, huo ni uwongo….’akasema kwa hasira,

‘Lakini huwezi jua, yawezekana mume wako alichukua mkopo huo kwasababu ya kupanua biashara, hakutaka kukuambia hilo, sizani kama benki wanaweza kutoa kitu cha uwongo…, hebu nikuulize wewe una uhakika gani kuwa mume wako hakuwahi kuchukua huo mkopo, ?’ nikamuuliza

‘Nina uhakika, kwa hilo na kamwe sitokubaliana nalo kabisa, ….hebu jiulize yeye kila siku alikuwa akinikanya nisije nikachukua mkopo wenye riba, kwanini yeye anikanye hivyo halafu yeye achukue mkipo huo wa benki ambao una riba kubwa tu…’akasema

‘Hebu nikuulize , huko benki walipokupatia hizo hati, hivyo vielelezo, si vyote vinaonyesha  sehemu mume wako alipoweka sahihi yake…hata kwenye mikataba ya deni hilo,kuna sahihi yake au sio,  je  nyaraka zote hizo uliwahi kuziangalia kwa makini, hukuona sahihi ya mume wako,…?’ nikamuuliza

‘Ndio….walinionyesha vyoye hivyo,….’akasema

‘Na sahihi ya mume wako unaitambua vyema,….?’ Nikamuuliza

‘Ndio …naitambua vyema…’akasema

‘Na kwenye mikataba hiyo, uliona sahihi kuwa ni yake au sio….?’ Nikauliza

‘Ndio ni sahihi yake…ndio hapo nikachanganyikiwa, lakini haiwezekani, sio yeye, siamini kabisa….na kingine kwenye hilo deni jipya eti na mimi nilihusika nikaweka sahihi yangu…sikumbuki kufanya hivyo, ila….’akasita kidogo

‘Deni jipya, kwahiyo kuna madeni mawili, au zaidi ya hilo….?’nikamuuliza

‘Lipo zaidi ya moja, kuna hilo la zamani, wanalosema ni la mume wangu, ndilo kubwa, kuna jingine kipindi baada ya kufariki na kuna jingine jipya kabisa….’akasema

‘Na kwa hayo mawili mapya , ya baada ya mume wako kufariki wewe unahusika,….?’ Nikamuuliza

‘Ndio…nahusika, wamenionyesha sahihi yangu…na kweli ni sahihi yangu..’akasema

‘Kwahiyo wewe hukumbuki kuwa uliweka hizo sahihi..?’ nikamuuliza

‘Mara nyingi,  shemeji alikuwa akija kwangu japokuwa sijiwezi kujiinua, baada ya kuanza kujitambua na ananiambia anataka kufanya hili na lile, mimi naitikia tu kwa kichwa…maana japokuwa nilikuwa sijiwezi kihivyo, kichwa kilikuwa kinaweza kutikisika, kuona, kusikia…..’akatulia kidogo

‘Na kwa vile nilimuamini, na yeye ndiye aliyechaguliwa  kuwa msimamizi wa kila kitu sikuwa na shaka naye, na nilikuja kujua hiloo kuwa yeye ndiye msimamizi nilipojitambua, walifika shemeji na baadhi ya ndugu zangu wakaniambia , nikiwa kitandani, nikawaitikia tu kwa kichwa.

‘Na ndio nakumbuka pia, kuna kipindi alikuwa akija huku analalamika kuwa hali ngumu, lakini akasema nisiwe na wasiwasi atajitahidi kuweka mambo sawa….ni hivyo ninavyokumbuka mimi….’akatulia

‘Lakini hakuwahi kukuambia anataka kuchukua mkopo benki….?’ Nikamuuliza

‘Kwa hilo, hakuwahi, sikumbuki kitu kama hicho, sizani, labda kama aliniambia kipindi sijitambui…yawezekana, aliniambia kipindi hicho, na huenda  nikaitikia, lakini kusema kweli, sikumbuki, na kwa vile alishapewa hayo mamlaka ya kufanya aonavyo ni sahihi, labda alioona kuchukua mkopo ni sahihi…’akasema

‘Kwa vile hukumbuki, yawezekana pia alikuambia uweke sahihi ya mkopo, ukaweka, na umesahau kuwa ulifanya hivyo  au sio?’ nikamuuliza

‘Hapana, hilo haliwezekani kabisa….nimejaribu kukumbuka, ..haijatokea, …wasinifanye mimi mjinga, na kwanini kama ni hivyo, anifanye niweke sahihi kitu kama hicho, wakati anajua sijitambui…hebu kumbuka kipindi hicho mimi ni mtu wa kulala….alinifanyaje mpaka nikaweka sahihi….mhhh, sijui ilikuwaje..’akasema

‘Je unahisi shemeji yako anaweza kufanya hivyo, yaani kufanya ujanja ujanja kwa nia mbaya…?’ nikamuuliza

‘Kiukweli, shemeji huyo ni mtu mwema tu, sina sababu ya kumuhisi vibaya, lakini sasa kwa haya nitafanyaje,… yeye ni mmoja wa watu wanaoaminika sana, kutokana na shughuli zake, na  kwa jinsi alivyojitolea kunisaidia, nashindwa  kumshuku vibaya…na ndio hapo naingiwa na sintofahamu, na….na…sitaki kwenda mbele zaidi…’hapo akatulia pale kijana wake alimuashiria kuwa sio kweli.

‘Kwani wewe unamjua vipi…’akasema huyo mama

‘Mama, baba mdogo angekuwa mtu mwema, asingelifanya haya…tatizo la mama anapenda kumtetea sana baba mdogo kwa vile tu kajitolea kwake, …mama anaogopa kwasababu ya mdogo wangu …., mimi mwenyewe niliwahi kumsikia baba mdogo akiongea na  ….’akasema mtoto  na mama yake akamnyamazisha

‘Mwanangu, wewe hujui dunia ilivyo, haya yote nayafanya kwa ajili yenu,…hujui ni nini kinachoendelea shukuru nyota yako ni kali, ungekuwa kama mdogo wako, nyamaza na usiseme kitu …’akasema akimuangalia mwanae kwa jicho la ukali.


‘Lakini muache aseme huenda ikasaidia…kwani mdogo wake ana nini….?’nikasema na kuuliza

‘Sitaki wanangu kujiingiza kwenye haya mambo, kuna mabaya yapo nyuma ya pazia, inabidi niwalinde kwa kila hali, hizi mali, nyumba,mashamba haya maana kwao zaidi  ya afya na usalama wao,…’akasema halafu akamgeukia mtoto wake na kusema kwa upole.

‘Sikiliza mwanangu nielewe, usijaribu kuniingilia au kuongea chochote bila ruhusa yangu, unasikia, wewe hujui lolote kuhusu dunia na watu wake…’huyo mama akasema na mtoto akainamisha kichwa kwa heshima.

‘Sasa kama huyo shemeji yako alikuwa mwema kihivyo , kwanini achukue mkopo , na kuweka dhamana ya nyumba  yenu bila ya wewe kujua, maana sasa ulishapata nafuu, akachukua mkopo mwingine, na kumbe kuna jinsi ya kulipwa, lakini hakuwahi kukuambia, mpaka uliposikia kuwa nyumba inatakiwa kupigwa mnada…?’ nikamuuliza

‘Hakuwahi kuniambia hayo ya mkopo….., ila kuna siku alikuja akaniambia mambo hayaendi vizuri, anataka kufanya jambo, anakwenda benki, lakini hakusema anakwenda kufanya nini…halafu akasema kumbe kaka alifanya hivyo, kwanini hakuniambia…nikamuuliza kuna nini, kaka yako alifanya nini…lakini hakusema kitu akasema tu, usijali, …nitamaliza nao…, nitahakikisha mpo salama, halafu akaondoka…’akasema.

‘Hebu niambie kidogo kuhusu shughuli za mume wako zilikuwaje kabla ya kifo chake….hakuna kipindi kilikuwa kigumu kwenu, huenda kipindi hicho aliamua kufanya jambo kwa nia ya kujikwamua na angelirejesha hilo deni kabla riba haijawa kubwa….?’ nikamuuliza

‘Hapana kwa mume wangu kuchukua huo mkopo sitakubaliana nalo mpaka kesho….ndio  mume wangu alifariki kipindi hana kazi, pesa zote alizokuwa nazo tulishatumia, na kidogo alichobakiwa nacho alikiwekeza kwenye mipango ya kujiajiri…pesa akaziwekeza kwenye biashara, lakini alikuwa na msimamo wake, kufanya kutokana na kile alicho nacho…kidogo kidogo akawa anainukia kibiashara….’akatulia

‘Akaanza biashara za kutoka , kwenda mikoani,..na biashara hizo hakuzianza zamani kabla ya kifo chake, kwenda mikoani ilikuwa ni mara ya pili, ….ndio ilikuwa ni mara ya tatu ndio akakutana na umauti…kwahiyo huo mkopo haukutokana na mume wangu ni lazima ulikuwa baada ya yeye kuondoka..au kuna namna…asingeliweza kunificha’hapo akatulia

‘Kabla sijakuuliza jinsi gani mume wako alivyofariki, hebu kwanza niambie kuhusu mahakamani, ulipofuatilia na kuwaonyesha  hivyo vidhibiti,  ilikuwaje…?’ nikamuuliza na yeye akabakia kimia kidogo kama anawaza jambo.

‘Unasema ulikwenda  mahakamani, ukaambiwa upeleke vielelezo, ukawapelekea,sasa.ni nini mahakama iliamua…?’ nikamuuliza

‘Haya ya Mahakamani achana nayo kabisa nimeshasalimu amri, ….’akasema

‘Ni muhimu niyafahamu, tafadhali….’nikasema

‘Wao walipoona hivyo vielelezo vyote, walisema hilo deni lipo kisheria, sio kwamba nasingiziwa,  wakaniuliza kama ulivyoniuliza wewe kuhusu sahihi ya mume wangu, kama ndio yenyewe, kama naifahamu….nikakubali, basi wakasema hilo deni ni sahihi….’akatulia

‘Na wakili wao akadai hilo deni jipya, mimi niliweka sahihi, lakini kutokana na hali yangu, bado nilikuwa na tatizo la kusahau, kwahiyo eti  niliweka sahihi na nimesahau kuwa nilifanya hivyo, …mimi hapo naona kuna kitu ….’akatulia

‘Kwahiyo unahisi kuna kitu ….kitu gani labda…?’ nikamuuliza

‘We acha tu, siwezi kuamini hayo yote, ilitokeaje, kwanini ..najiuliza tu bila majibu,…lakini nashindwa nifanyeje, maana kwa yote hayo aliyekuwa ni karibu kumshuku ni shemeji , na yeye …aah, ni mtu wa watu kanisaidia sana, sitaki mabaya naye tena, siwezi …’akasema

‘Je shemeji aliporudi na kwa hali kama hiyo hukuongea naye kuwa unafuatilia kuhusu hilo deni la zamani linalomuhusu mume wako, na ya kuwa wewe unahisi kuna kitu zaidi ya hilo deni kinachohitajika kufuatiliwa ili ukweli ujulikane,…kama ana nia njema angekusaidia,…je alisema nini…?’ nikamuuliza

‘Nilimuamba, akasema….yeye alishafuatilia akachoka, ….kwani hata yeye hakujua kuwa kuna deni kama hilo, …hata yeye hakuwahi kusikia kutoka kwa kaka yake na yeye ndiye alikuwa mtu wake wa karibu na hamfichi kitu….anasema alifuatilia akitutetea kuwa huyo mdaiwa keshafariki na…waliobakia ni mjane na mtoto….sasa iweje deni hilo lirithiwe…akahangaika kutafuta njia za kisheria kutusaidia  lakini ikashindikana kutokana na mkataba …’akasema

‘Kutokana na mkataba, unasemaje….?’ Nikauliza

‘Mkataba ulianza kuvunjwa kwa kutokulipa kama ilivyokubaliwa, haikuwahi kulipwa hata kidogo,kuashiria kuwa mkopaji alifanya makusudi…..na mambo mengi  ya kisheria, sitaki hata kuyakumbuka…..’akasema

‘Ikawaje sasa….?’ Nikauliza

‘Alisema…. ngoja aniache na mimi nijaribu bahati yangu, huenda nikasaidiwa, kwa huruma wakiniona mimi mjane na watoto…kwahiyo hakutaka kwenda na mimi, ila kila nikirudi alikuwa akiniuliza imekuwaje,mwishoni akaniambia, unaona hata mimi niliambiwa hivyo hivyo…’akasema

‘Kwahiyo ikawaje?’ nikamuuliza

‘Niliamua kwenda polisi kufungua jarida la upelelezi, wajaribu kunisaidia kuwa labda  kuna namna imefanyika kutubambikia deni, huenda kuna watu wametumia  nyumba yetu kama dhamana bila ya mimi kufahamu….’akasema

‘Ulienda polisi, kumshitaki nani sasa…?’ nikamuuliza

‘Rafiki yangu mume wake ni polisi, alishauriwa na mume wake nifanye hivyo, kuwa kunaweza kufanyika upelelezi ukweli ukabainika, ninachotakiwa nikwenda polisi kutoa hiyo taarifa, mimi nikafanya hivyo….upelelezi ulipoendelea, siku moja akaja kukamatwa  shemji kuwa huenda anahusika kwa namna moja au nyingine…’akasema

‘Ikawaje…?’ nikamuuliza

‘Ndugu zake ndio wakaingilia kati wakanijia juu,…’akatulia kama anaogopa jambo

‘Yaani shemeji zako wengine….?’ Nikauliza akaitikia kwa kichwa halafu akasema;

‘Mimi katika kujibishana, japokuwa hata mimi sikupenda hiyp hali ya kukamatwa shemeji, nikawaambia ni kwanini yeye aliamua kuchukua mkopo kwa dhamana ya nyumba bila ya kuniambia…na, baada ya mimi kuwa na nafuu, kwanini hakunifahamisha mapema kuhusu hilo deni ina maana alikuwa akinificha kwa masilahi fulani….’akatulia kidogo

‘Kiukweli kauli hii lilimfanya shemeji  akasirikie sana…kuwa baada ya hayo yote hizo ndizo fadhila zangu, na ya kuwa yeye hataacha kuwasaidia watoto kwa vile ni watoto wao..ila mimi naonekana nina roho mbaya, sina shukurani….na hata dada zao walifikia kuniambia mimi ni mwanga, mchawi, eti huenda..nilichangia kaka ya o kufa..ikawa ni vita sasa, kwanini wananiambia mimi ni mchawi, eti nimloge mume wangu ili iweje….’akasema

‘Lakini hayo yote yalikuwa kwenye harakati za polisi kufuatilia na kutafuta ukweli  au sio, na swala hilo la kutafua ni nani alifanya hujuma….lilikuwa bado halijafika mahakamani au sio,…kuacha lile la mwanzo la kutafuta ukweli wa deni kama ni halali au la?’ nikamuuliza

‘Ndio….’akasema

‘Ehe …ikawaje sasa?’ nikamuulza

‘Baadaye ndugu walikuja wakaanza kuniomba kuwa niachane na mambo hayo ya polisi hilo swala turudi kuliongelea nyumbani, mimi nikawaambia hata tukiliongelea nyumbani hilo deni atalipa nani, ni lazima tutafute ukweli wa hilo deni, kwani huenda kuna mtu mwingine anatuchezea…, ‘akatulia

‘Sasa walipoona sikubaliani na hilo, kukaanza vitisho kutoka kwa wanandugu huku wakiniambia kuwa mimi sina fadhila, sina shukurani…hawakujua kuwa mimi nipo hivyo, basi kama ni hivyo na wao watafanya hicho ninachokitaka….na watahakikisha,najuta, nitakiona cha mtema kuni…’akasema

‘Ni nani alikuwa akiongea hayo…?’

‘Ni hao ndugu zake shemeji na wake zao, na mawifi…’akasema

‘Na kweli haikupita muda mara mtoto wangu huyu mdogo akaanza kuumwa, kweli kweli..kila ikifika muda wa kwenda mahakamani anazidiwa, maana mimi niliamua hayo mambo yafikishwe mahakamani, kutokana na uchunguzi wa polisi, sikukubali mume wangu asingiziwe hilo deni, nataka haki ipatikane,…wao wakasema tutaona…’akatulia

‘Na muda huo mshitakiwa ni shemeji yako, kutokana na uchunguzi wa polisi…?’ nikasema kwa kuuliza

‘Ndio…’akasema na kabla sijamuuliza swali jingine akasema

‘Kiukweli hata mimi sikutaka ifikie hapo…maana sasa namshitaki shemeji , mtu aliyenisaidia sana, lakini sisi tutakwenda wapi, maana ilikuwa nifanye hivyo, ili pingamizi liendelee kuwepo, au nyumba ipigwe mnada, na polisi walisema kuna uwezekano shemeji yangu huyo anahusika kwa namna moja au nyingine na mahakama ndiyo itaitafuta haki, na huko kunaweza kuliondoa hilo swala la kupiga nyumba hii mnada,…’akasema na kutulia kidogo

‘Cha ajabu wao wanasema nyumba ina umuhimu gani, zaidi ya ubinadamu, nasahau fadhila,…yote eti yalifanyika kwa ajili yangu na watoto..na kama ni denii lipo kwanini nisiche tu nyumba ipigwe mnada ili lilipwe na pesa itakayobakia tujenge nyumba nyingine ,eti kwa kufanya hivyo, kwenda mahakamani namshitaki marehemu aliyekopa hilo deni,…..’akasema

‘Unasema mtoto akaanza kuumwa, … hilo la kuumwa kwa mtoto wako linahusikanaje na hiyo kesi,  unahisije kuwa mtoto wako anaumwa kutokana na hilo tatizo, kwani wewe unaamini mambo hayo ya kishirikina,…kuwa huenda wao walifanya ushirikina kwa huyo mtoto wako..?’ nikmuuliza

‘Unajua nikiongea haya utadhani mimi naamini haya mambo ya kishirikiana,…mimi siamini hayo kabisa, mimi namuamini sana mungu , nimelelewa hivyo na ….moyoni mwangu, siamini sana mambo ya kulogwa, japokuwa yapo, siwezi kukataa…. lakini hujui ni nini kimetokea, naishi maisha yasiyo salama, vitisho, na mambo ya ajabu ajabu yanatokea kila siku, usiku hatulali, mapaka…sijui vitu gani vinacheza kwenye bati juu..ni shida kweli, …., na sana wakaamua kuwalenga watoto wangu, hawa wana makosa gani….’akasema kwa uchungu

‘Kwa vipi?’ nikamuuliza

‘Huyu mtoto mdogo, hakuwa na tatizo hilo kabisa, sasa kila nikitaka kufuatilia hilo jambo..hiyo kesi, mtoto anashikwa na homa kali mpaka anakuwa kama ana dege dege, anapoteza  fahamu…., hapo wamenigusa pabaya, siwezi kuvumilia….na utashangaa siku hiyo ikipita anapona…’akasema

‘Siku gani ikipita…?’ nikamuuliza

‘Yaani siku ikiwa ni ya kwenda kulipeleka hilo shitaka   mahakamani, au nikitaka niifuatilie jambo kuhusu mali ya mume wangu, mtoto huyo anaanza kuchemka homa….ni homa kweli, anachemka mpaka anakuwa kama anawehuka, ooh, ilipotokea zaidi ya mara tatu, nikaona sasa basi, kama ni mali wanataka basi wachukue tu…mimi sina la kufanya,nawapenda sana watoto wangu,…. yote sasa nimemuachia mungu..’akasema

‘Ulihakikishaje…sio kwamba nakupinga kwa hilo, lakini jinsi gani ulihakikisha kuwa mtoto anaumwa kwa sababu hiyo…?’ nikamuuliza

‘Mtoto anaumwa jamani…akianza kuchemka homa namkimbiza hospitalini, akipimwa hana malaria hana tatizo, …anaishia kupewa panadol…..nikirudi na kusema niachane na huko kufuatilia mtoto ni mzima kabisa, utasemaje hapo, …..sasa ulitaka nihakikisheje..’akasema

Ilipita muda kidogo nikiliwazia hili, je mama kama mama atawezaje kupata haki zake kwa hali kama hii, kama alivyosema kila akitaka kufanya jambo, mtoto wake anaumwa,na keshahaikisha hilo…kwa mapenzi ya mama kwa mtoto wake itakuwa vigumu sana, hapo itakuwa vigumu, sasa …nitamsaidiaje, nikaona ni lazima nifanye jambo, nikasema

‘Shemeji wewe si unamuamini mungu?’ nikamuuliza


‘Swali gani hilo, kama nisingelikuwa namuamini mungu kwa hali kama hii ungelinikuta nimeenda kwa waganga kupambana na hayo, lakini mimi namuamini  sana mungu na kwa haya sijawahi hata kwenda kwa waganga,  au hata kufikiria hivyo, zaidi ya kumuomba mungu..’akasema

‘Sasa kama unamuamini mungu huoni kuwa huo ni mtihani tu, unajaribiwa tu , ili tu usitete haki zako, mimi nakushaurii sasa  tuifufue hii kesi …mimi kuna watu nitawasiliana nao wataweza kwenda mahakamani, ….wataweka pingamizi …..tusipoteze muda, unaonaje kwa hili…..’nikasema

‘Hapana…’akasema

‘Kwanini…hii ni haki yako, au sio…’nikasema

‘Ni haki yangu ndio, lakini sitaki …..kwanza nitaanzia wapi wakati nimeshakubaliana na hawa wana ndugu tukasema basi yaishe, kama ni nyumba watauza , italipiwa deni na kiasi kilichobakia tutajengea kibanda nyumba nyingine ya kawaida inatosha hata kama ni kibanda cha vyumba viwili inatosha…’akasema

‘Wewe niamini mimi, hapa kuna ujanja umechezwa, kuna mtu anakuzunguka, ili aifisidi haki ya wanao,…nikubalie tuipiganie haki ya watoto, kwani ukiacha hivi hata mume wako huko alipo atakulaumu, ina maana juhudi zote alizofanya zinapotea bure na wewe upo hai….mimi kuna watu wangu watapigania hili hadi haki yako itapatikana, niamini,….’nikasema na yeye akabakia kimia, halafu akatikisa kichwa akasema lakini sitaki mimi nijulikane kuwa nimeifufua hiyo kesi, sitaki nihusike, mfanye mjuavyo wenyewe, mnaweza kufanya hivyo…?’ akauliza

‘Ngoja niwasiliane na watu wangu, nitakuambia….’nikasema nikapiga simu kwa watu wangu nikawaelezea kwa kifupi ni nini kinatakiwa kifanyike, …kazi ikaanza mara moja!

Hutaamini, wakati anaanza kunionyeshea baadhi ya nyaraka alizokuwa nazo…, mara Yule mtoto mdogo akaanza kutetemeka, joto likaanza kupanda, mama akaanza kuhaka, na kusema

‘Unaona ndiyo haya siyataki, hawa wanajua kila ninachotaka kukifanya, unaona …’ akawa anamshika mshika mtoto wake ambaye kwa muda huo alikuwa na joto kali , nikaanza kazi ya kumsaidia, kumsiponji, na kumpa dawa ya kutuliza..lakini wapi….mtoto akawa hajiwezi mpaka anapoteza fahamu

‘Tumpeleke hospitalini..’nikasema

‘Tunajisumbua , dawa ni kuachana na hayo madai,…’akasema mama mtu

Nilimuchunguza  Yule mtoto, kweli joto lilikuwa juu kweli, wakati mwanzoni alikuwa hana dalili ya kuumwa,  na kwa hali kama hiyo nilionelea tumpeleke hospitalini lakini mama mtu akasema huko tunapoteza muda, cha muhimu ni tuachane na hilo tulilotaa kulifanya

‘Shemeji  usiamini mambo hayo, wewe usiogope shemeji hivi ni viini macho tu, muombe mungu, tuendelee na hili hebu kwanza lete panadon….nikasema akaleta panadoni nikaisomea kwa imani yangu, nikachukua maji nikayasomea, nikamwambia ampe mtoto anywe….mara mlango ukagongwa, na aliyeingia alikuwa shemeji mtu….

NB:  HAYA MAMBO YAMEANZA, KAMA NI WEWE UNGELIFANYA NINI


WAZO LA LEO: Mwenyezi mungu anaweza kutupima kwa mitihani mingi, ….magonjwa, kukosa kazi,  misiba na kila jambo lenye kutia wasiwasi, na mashaka. Haya yakitokea, kamwe tusikimbilie kumshirikisha Mungu…tukafikia  kwenda kupiga ramli na mambo kama hayo, tukifanya hayo tutakuwa tumekufuru! Muhimu ni kuvuta subira, huku tukimuomba yeye, kutubu makosa yetu na hatimaye tutaishinda mitihani hiyo,…Tumuombe mungu atunusuru ni mitihani yenye kuzishinda nafsi zetu.

Ni mimi: emu-three

1 comment :

Anonymous said...

hongera mkuu