Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeFriday, March 25, 2016

SIKIO LA KUFA HALISIKII DAWA-21 (hitimisho 3)‘Mleteni…’

Hiyo  ilikuwa sauti ya ofisa  upelelezi, akiagiza kwenye simu, …je aliagiza nani aletwe?
Pale tulipokaa tulianza kujiuliza ni nani huyo aletwe, hata hivyo hatukuweza kufanya kitu zaidi ya kusubiria, tukabakia tumetulia lakini  ndani ya nafsi zetu, kwenye akili zetu tukiwa tunawaza, kumuwazia huyo anayekuja ni nani, nani kwanini lugha hiyo ya ‘mleteni’ itumike…..

Tulifahamu kama tulivyoambiwa mdada hatuwezi kumuona tena, sijui kwanini, sijui hali yake ipoje, sijui..labda ndio hayupo duniani..kwahiyo hawezi kuwa ni yeye anayetakiwa kuletwa…sasa ni nani….

Sote macho yetu yaliekea mlangoni, tukisubiria kwa hamu, na kila mmoja akiwazia lake, kwangu mimi nilijua anayeletwa ni Yule jamaa wa kijijini ili aje kuthibitisha yale aliyoongea huyo mpelelezi, maana kwa mujibu wao huyo jamaa ndiye amekuwa msaada wao mkubwa, na kwa vile alishajitolea kwa lolote lile amekuwa haogopi kuongea…,wamekuwa wakimtumia sana kuelezea hali ilivyo kwa kundi hilo haramu, japokuwa bado walikuwa hawana imani naye sana…

Kulitokea kuchelewa kidogo na ofisa upelelezi akaamua kufuatilia mwenyewe, akasimama na kutoka nje, sisi tukabaki mle ndani tukiwa watatu, mimi mwenzangu  na dakitari ushauri, na mimi hapo hapo nikawa na shauku ya kuongea na dakitari huyo, nikaona ni muda muafaka wa kumuuliza swali kwani hatujui huenda tukarejeshwa tena rumande

Mimi nikakumbuka kuwa docta huyu wakati anatuelekezea ilivyotokea, alikuwa hajamaliza maelezo yake aliyokuwa akituhadithia siku ile,

Siku ile mdada alipataka kunywa hiyo sumu, nikawa na hamasa kujua hilo, nikauliza

 ‘Docta najua hili halitakwenda kinyume na amri ya watu wa usalama kuwa usiongee lolote kuhusu huyo mdada, lakini shauku yetu ni kufahamu jinsi gani mlivyoweza kumuokoa asiweze kunywa ile sumu, ….ulisema mlibadili na kuweka dawa nyingine lakini nakumbuka ulisema kuwa hamkuwa na uhakika kuwa kule kwenye bahasha kulikuwa na dawa ngapi…

‘Ni kweli, lakini sisi tulibahatisha kuwa zitakuwa ndio hizo tu…ndio maana kwa haraka  tuliweka dawa zinazofanana na hizo, na zikiwa na sifa ya kuyeyuka, na kwa kuziangalia usingeliweza kuhisi ni dawa tofauti na zile, na ambazo hazitaweza kumuathiri mdada kwenye upasuaji wake ulitegemewa kufanyika…..’akasema docta

‘Tulipohakikisha kuwa kile kitu kimerejeshwa kama ilivyokuwa kwenye huo mkoba wake, tulifanya ishara ili nesi arudi na huyo mdada,…lakini wakati tunafanya hilo,  ghfla tukasikia nesi  akiita kuwa anahitajia msaada….’docta akatulia

‘Kulitokea nini…?’ tuliuliza maana hapo docta mshauri nasaha alitulia kuendelea kuongea

‘ Tuliposikia hivyo kwa haraka tukakimbilia huko bafuni, na tulipofika tulikuta nesi akipambana na mdada, nesi alikuwa kashikilia mkono wa mdada ambaye alikuwa kauweka mdomoni,  akiwa kuashiria kuwa alikuwa anatumbukiza kiti mdomoni,, tukajua ni yale yale….tuliyokuwa tukiwazia, kumbe kweli mdada alishakuwa na kidonge hicho kabla,….

‘Oh, sasa ikawaje….?’ Tukauliza pale tulipoona mshauri nasaha akisita kuendelea na kutuashiria mlangoni, na kweli mara mlango ukagongwa mara moja na kufunguliwa, na aliyeingia ni Yule askari  mpelelezi na jamaa mwingine na askari mpelelezi akasema;

‘Huyu ndiye Yule jamaa anayetoka kijiji kimoja na mdada, tunamshukuru sana kuwa amekuwa msaada mkubwa kwetu, na ameweza kufanikisha tukaweza hata kugundua hilo genge la wahalifu huko nachi ya jirani…’akasema

‘Kilichosaidia ni hiyo hali yao waliyotengenezewa bila hata kujuana, wamejengewa tabia ya kutokuaminiana, kila mtu anamchunga mwenzake, kila kaambiwa huyo mwenzake mchunge sana, na ukiona dalili za usalitu tuambie, lakini usije kumwambia, na kwa vile wao ni maaskari waliivishwa na viapo vyao, hufata wanavyoambiwa…

‘Wanaambiwa na nani, ni nani anayewapa maagizo hayo….?’ Tukauliza

‘Tunapewa maagizo kutoka huko kwa wakubwa, ….nchi za nje, na mara nyingi maagizo hayo yaafika kwa ishara maalumu ambazo tumefundishwa, inaweza ikawa kwenye mtandao, au kwenye simu, lakini kwa alama maalumu ambazo sisi tunakuja kuzitafsiri wenyewe…’akasema

‘Hizo ishara au elimu hiyo wote mnaifahamu..?’ tukamuuliza

‘Kwa viongozi ndio tunaifahamu , lakini sio wote wanaoifahamu…..ni elimu ambayo inajulikana kwa wacheche  sana, na mimi kama kiongozi wa mtandao, naifahamu, na ….ila kwenye kutafsiri, inategemea imemlenga nani,…kama ni mtu binafsi inatumiwa kwenye simu yake kama ni kwa ajili ya kundi inatumwa kwenye mtandao na mimi nitafsiri kwa kuindika kwa mkono….’akasema

‘Sasa kwa mfano amri hiyo inamuhitajia mtu kwenye matawi yenu ya sehemu nyingine mikoani,…mnafanyaje ili iwafikie ili waelewe…, maana umesema alama hizo ni nyeti na wanaozifahamu ni wachache, hususani viongozi, na wengine hawatakiwi kufahamu…?’ akaulizwa

‘Mikoani ni lazima kutakuwepo mtu anayezifahamu, na huyo ndiye atawaelewesha wengine kwa namna aliyoelekezwa, ni …..namna ya kuhakikisha taarifa haifiki kwa watu wasiohusika…’akasema

‘Kwahiyo makao yenu kwa huku kwetu yapo wapi…?’ akaulizwa

‘Hakuna kitu kama makao makuu, au sehemu maalumu ya kusema hapa ndio ofisi au makao, hii kwa ajili ya usalama, kwahiyo karibu kila siku ni kuhama kutafuta eneo maalumu,na mara nyingi inakuwa sehemu zile za starehe au sehemu ambazo huwezi kuhisi kunaweza kuwepo na kitu kama hicho…’akasema

Nchi ya jirani tuliweza kukaa vyema, maana hakuna ufuatiliaji sana wa mambo binafsi, starehe za kila namna zinaruhusiwa, kama makasini, majumba ya ulevi, ukahaba…makumbi ya starehe, humo ndipo ofisi zetu zinakuwepo, na wakati mwingine hata kwenye majumba ya Ibada…’akasema

‘Majumba ya ibada, inakuwaje….!!!?’ Tukaliza

Ili kufanikisha azma hiyo, wanachama waaminifu walipelekwa mashuleni kwa kila Nyanja, na wengi waliopelekwa huko ni wateule,wale wenye akili sana,…wakafunzwa fani hiyo kutegemeana na akili yake, kwahiyo kulikuwa na waelewaji wa dini, walifunzwa dini hiyo na kufuzu sana,…sasa hao walihakikisha wanakuwa viongozi kwenye nyumba za ibada,na wanatekeleza majukumu yao kwa njia za siri kabisa, huwezi kumfahamu….’akasema

‘Na viongozi hao wanakuwa na karama, watoa mijuiza, wanafanya mambo ambayo jamii inahitajia sana, ….utakuta majumba yao hayo yanajaa watu, wanakusanya pesa kwa waumini huku wanatengeneza mambo mengine ndani kwa ndani biashara za kisiri zinafanyka, ni nani atashuku hilo…’akasema

‘Hata kwenye siasa kuna watu wameivishwa kwa fani hizo, na wamesoma kweli, wameandaliwa kushika madaraka sehemu nyeti,…na kwa vile wana elimu, ni wataalamu ni rahisi kwao kuchaguliwa, na wanajitambulisha kwa wanachi kwa utendaji mwema kabisa, lakini akilini wana ajemda ya siri…..hawa wanakwenda na wakati, wanajua ni nini wafanye kwa wakati gani….’akasema

‘Una maana gani kusema hivyo, maana kama ni wanasiasa mara nyingi huwa wanachaguliwa na wananchi au kuteuliwa na kiongozi anayeshikilia madaraka kwenye eneo husika, sasa wao wanajuaje kuwa huyo mtu wao ni lazima atachaguliwa au wanatumia mbinu gani mpaka mtu wao achaguliwe?’ akaulizwa

‘Kama nilivyokuambia, hawa watu ni wasomi, sio usomi wa kubahatisha…wana akili za hali juu, na wapo kwenye kila fani, utaona wengi wamefikia kiwango cha uprofesa , udocta….sasa utasema nini hapo..na, sio usomi wa kubahatisha…kwahiyo uwezekana wa wao kuchaguliwa kuwa kiongozi, kushika nyazifa fulani ni mkubwa na kwa hivi sasa wapo wengi tu,  na pia ikibidi huwa wanatumia mbinu nyingine za ziada za propaganda, ili kufanikisha malengo yao ….

‘Hebu ni waulize kwenye kuchagua viongozi wa siasa, au hata kazini,  kuna namna yoyote ya kuwachunguza watu au hao viongozi wametokea wapi….chimbuko lao hasa kiundani, wamesomea wapi kwa vipi,,..walisomeshwa na nani,….hakuna kitu kama hicho, kuwa mtu anachekechwa kihivyo kujua historia kwa undani…kweli inafanyika hivyo…?’ akauliza na sisi tukaa kimia

‘Kiukweli haianyiki hivyo….’akasema

‘Kwahiyo watu hawa walilifahamu hilo, kuwa kiuhalisia watu huangaliwa jinsi gani wanavyotoka, wanavyoongea wanavyoshawishi, hasa kwa kutumia midomo yao, lugha ikipewa kipaumbele,….na fani huja baadaye….’akasema

‘Mimi bado sijaelewa hapo, maana viongozi wengine wanachaguliwa na mkuu au kiongozi mkuu husika, unataka kusema kiongozi huyu anayewachagua hawawafahamu hao watu aliowachagua vyema, ukumbuke kuna watu kama wa usalama wa nchi, unataka kusema wao hawana uwezo wa kuligundua hilo…?’ tukauliza

‘Nikuambie kitu makundi haya ni chimbuko la wazo na huyo jamaa aliyetaka kuiweka dunia mikononi mwake ,…wengi waliliona wazo hilo  kama wazo la mwendawazimu, lakini athari zake ndio hizo, yeye alianza kama muota ndoto, akalifanyia kazi, …sasa wanachama wake wamelipeleka mbali zaidi na wanamuenzi hadi kwa mbinu hizo za ishara zake….’akasema

‘Ishara gani hizo…?’ tukamuuliza

‘Zipo nyingi, ….muhimu ni kuwa kuna ishara wanatumia kama zile za komputa, herufi ndogo tu inaweza kuunda kitu…kuna ishara za tarakimu…kuna ishara za vitendo kwa kuonyesha,…kuna ishara za alama mbali mbali..vyote hivyo vilikuwa ni ndoto za huyo jamaa…..’akasema

‘Lakini huyo jamaa alipatikana, na sehemu kubwa ya kundi lake walikamatwa…’nikasema

‘Yeye ni mtu aliondoka,  lakini mfumo wake bado upo na utaendelea kuwepo,….namna ya utawala, namna ya kuwezesha watu wao kuendelea kumiliki, kutawala, ili mfumo huo uendelee kuwepo,,namna ya kuwatetea wenzetu, wanajijua wenyewe wenzetu ni akina nani…kwahiyo watafanya kila njia wao waendelee kuwepo madarakani na wengine ambao hawana masilahi na wao, wasiepewe nafasi,….huo mfumo bado upo…sio lazima mtu , lakini muhimu ni mfumo wao…’akasema

Ukumbuke mtu huyu alichokifikiria kikubwa ni elimu, elimu hii akaiangalia kwa namna ya ubinafsi, kuwa kumbe unaweza ukaiwekeza kihivyo, kuwatafuta wataalamu, lakini…wale wenye mleno wao, ubinafsi…, utawagundua tu wakiwa kwenye vyeo vyao, hata walipwe nini hawataosheki…na zaidi ya hayo, hakuna utu mioyoni mwao, muhimu kwao ni masilahi….’akasema

‘Kama mnakumbuka lile tukio la yule jamaa aliyetaka kuiweka dunia mikononi mwake, alianza kuwasomesha wataalamu, wataalamu hawa walipikwa kinamna, wakasomeshwa…..mnakumWataalamu hawa walipomaliza  kusomesha wakaiva, walitawanywa sehemu mbali mbali wakiwa wamepewa majukumu, na mtandao ukaenea, mfumo ukashika hatamu, umimi, umwenzetu ukawa upo kwenye damu…na zaidi propaganda….hata kama Yule mwanzilishi hayupo lakini mfumo wake bado upo unafanya kazi,  kila mmoja kwenye eneo lake aliwekeza na yeye, akapika watu wake kwa mfumo ule ule……’akasema

Ukimuona mtu yupo lakini hana elimu,…au utaalamu fulani ujue huyo ni chambo tu…’akasema na kucheka kidogo.

‘Kwa maana hiyo unataka kusema hakuna makao maalumu yao na wao hawana kiongozi wao mkubwa, mfumo ndio kiongozi wao, haiwezekana sasa kwa njia hiyo wao wanawezaje kujiongoza?’ tukauliza

 ‘Ni kweli, ….lazima kwa hali kama hiyo kuwepo na viongozi, viongozi hao wapo, na mara nyingi wao huchaguana kutokana na ujuzi, yule mwenye ujuzi mkubwa kwenye hiyo fani, na huku juu kabisa wapo wale waasisi, ambao ni mabaki ya Yule bwana aliyetaka kuiweka dunia mikononi mwake ….

Uongozi wao ni mfumo, upo tu,…kwahiyo  huwezi kumkamata mmoja ukasema huyu ndiye kiongozi, basi nimemaliza hilo kundi, unajidanganya, kwasabau wao wanakwenda na mfumo, ambao ni kama imani yao,  mfumo huo upo, na nguzo yao ni kipaji, Yule mwenye uelewi wa hali ya juu, anajikuta ndiye kiongozi,…na kazi yao kubwa ni kuhakikisha kuwa wao wanaendelea kumiliki njia zote za uchumi, wanakuwa wao ni watawala…maana wana kipaji cha kuongoza, kushawishi, na wanajua jinsi gani ya kubadili muelekeo,

Na kitu kikubwa kinachowasaidia ni propaganda, kuzua mambo na mambo hayo yakaja kuonekana ni sahihi kwenye jamii,kuhahikisha kuwa mfumo wao unatambulikana, kwa vile pia wanamiliki mamlaka ya maamuzi makubwa huko juu…kuna mambo jamii iliona hayafai, lakini kwa propaganda zao, leo yanaonekana ya kawaida…!.

‘Na mara nyingi wao wamekuwa maadui wakubwa wa dini,misimamo isiyotaka mabadiliko, wanaipinga sana, na kwanjia ya propoganda, njia ya kuharibu tamaduni za dini, tamaduni za asili wameweza kupandikiza mifumo yao kila mahali…

Kwa ujanja wao, wamekuwa wakiwekeza sehemu zile ambazo hazina ufuatiliaji wa sana na hata kama upo huwezi kuwashuku kabisa.

Wakiwa nchi ya jirani, ambapo kuna mitambo za kisasa, waliweza kuweka vyombo vyao vya kisasa ambavyo viliweza kuona sehemu mbali mbali na kunasa matukio wanayoyataka,  wakitumia zaidi hizi simu za mikononi na computa zenye hizo zana…

‘Sasa kwa ushahidi huo,  huyu hapa alikuwa mmoja wa wataalamu wa kuendesha mitambo hiyo, akiwa nchi ya jirani, jamii huyu ni mtaalamu sana wa komputa, uone walivyo wajanja, walimgundua na wakamshawishi wakamuendelea zaidi na kumuwekeza, akawana kampuni yake ya kuweka mikondo ya mawasiliano, mitandao, na kutengeneza CDs, na humo wakawekeza mambo yao….’akageuka kumuangalia huyo jamaa

‘Zimwi likujualo halikuli likakesha,…jamaa huyu anasema tangu awali hali hiyo ilikuwa inamtesa sana, kuona kuwa anatumika, kipaji chake kinatumika vibaya, lakini alishaingia kwenye mitego yao angefanya nini..lakini sasa  kazindukana na kaiona hiyo hali kwa mbali zaidi, kaona kuwa dunia hii ni ya kupita, kwanini asijitoe…wenzake walishamshuku na kwa mbinu zao wakahakikisha kuwa anapandikiziwa hilo gonjwa…’akasema

‘Walishampangia kuwa mwaka hata maliza, na kwa mahesabu yao wanajua keshafariki….’akatulia

‘Ni kweli kuwahivi sasa, maisha yake yapo hatarani, kwani kama bado yupo hai ataweza kutoa siri zao, lakini kwa vile na yeye ni mtaalamu wa mambo hayo ya mawasiliano ya kunasa matukio, ameweza kuwapiga chenga za hapa na pale na kwa vile alishajitambulisha kwao kuwa anaumwa, wao wameshamuweka x, kuwa haitachukua muda atakufa, hawakujisumbua sana kumtafuta…

Utaalamu wetu nao unazidi kukua, kwani madakitari wetu wamekuwa wakihangaika kutafuta tiba ya kupambana na hayo madawa yao,…magonjwa yao ya kupandikiza,  na sasa tunaweza kusema angalau wataalamu wetu wamefikia sehemu ambayo wanaweza kupambana na maradhi haya ya kutengenezwa na wanadamu…

Ni vitu vya kuogofya kweli ndio maana havitakiwi kutangazwa, lakini kwa hali lilivyo inaidi wananchi waambiwe, wawe na tahadhari….tatizo ni nani wa kumfunga kengele paka, wakati huo huo, huenda watalawa waandamizi wapo kwenye hilo kundi…..unaona ilivyo shida.

ILE NDOTO, ya dunia yangu bado inatuandama….na wananchi nao ambao ndio waamuzi wa haya,bado hawajakuwa na utashi wa kuelewa zaidi…kwani kama ni kiongozi wao ndio wachaguzi, lakini kwa vipi wataelewa hilo,…imebakia kuwa sikio la kufa….

Lakini ndio hivyo, mwanadamu kujisahau tu, ….na ndivyo ilivyo,mungu humpa mtu ujasiri, akafanya atakavyo akajenga kiburi, akajiona yeye ndiye mfalme,….mtawala wa kuogopewa, lakini hajui kuwa yeye ni kiumbe tu, kaumbwa, na mwenye mamlaka hayo, ya uhai wake anaoringia, mwenye mamlaka ya fya yake anayojivunia, mwenye mamlaka ya hali ya kipato chake…nk, ni mmoja tu, mwenyezi mungu muumba.

Na kwa wakati wake ukifika, ataviacha vyote hivyo, na anaweza akaviacha kwa udhalili wa hali ya juu, akateseka kwa maradhi, au akasubiriwa siku ile anakata roho akaonana na madhambi yake na vitu atakavyokutana navyo kaburini…..inatisha, lakini kamwe hatusikii, ..kama hatuoni huko mbali,…maana sisi ni sikio la kufa…..

‘Hao jamaa walishagundulikana kuwa watanaswa, wanatafutwa na polisi, sasa iweje, kama ilivyokawaida yao, wakuu wa kimataifa, wakaona kundi hilo wote waangamizwe, na wataangamizwaje kabla hawajakamatwa, ikatumika ile mbinu ya kuwa kila mmoja kupewa agizo la kumuondoa mwenzake,..

Huyu akaambiwa mwenzako ni msaliti, unatakia ummalize haraka, na huyo mwenzake akaambiwa hivyo hivyo kwa mwenzake, walichofanyiwa ni kuagizwa kila mmoja kwa wakati wake, kuwa mwenzake sio mwaminifu, kwahiyo anatakiwa kuondolewa, na huyo anauetakiwa kuondolewa, naye akapewa maagizo kwa mwenzake kuwa mwenzake sio mwaminifu kwahiyo anatakiwa kuondolewa..

Kwa mtindo huo, wakajikuta wote wamelishana sumu zao,na wote wamekutwa wakiwa wamekufa na hizo hizo sumu zao, na imekuwa mwisho wa kundi hilo hapo nchi jirani…..’akasema akitikisa kichwa

‘Sasa kwa kutaka kuondoa ushahidi wote, walitegesha bomu,…mmojawapo mtaalamu wa mabomu alifanya kazi hiyo, hakujua na yeye ni miongoni wa watu wanaotakiwa kufa, kwani alipoingia ndani alipigwa sindano ya shingoni na mmojawapo, na kupoteza fahamu, na baadaye kupoteza uhai,…

Bomu hilo lilitakiwa kufyatuka baada ya kuhakikisha watu wote wamemalizika na wapo humo ndani, kwani siku hiyo kulikuwa na kikao kikubwa cha wanachama wenye dhamana, wote waliitwa kutoka sehemu mbali mbali…wakijua ni kikao, hawakufahamu kuwa ndio ulikuwa mwisho wao.

Bomu hilo lilisubiria wakati muafaka,  na kiwashio chake kilikuwa huko huko kwa magaidi wa kimtaifa, ambao walikuwa wakisubiria wakati muafaka kulifyatua, ili kupoteza ushahdi wote, lakini bomu hilo likawahiwa kabla hajalipuka,na ndio tukaweza kupata ushahidi mkubwa na mambo yao waliyokuwa wakifanya yakawekwa hadharani…’akasema

‘Sasa humu nchini kwetu, kuna sehemu mbali mbali walipandikiza watu wao hao kinamna…, kwenye fani mbali mbali,na wao wanajiendesha kinamna ambayo hata wao hawajijui kuwa wanatumiwa,wao wanaona kuwa wanafadhiliwa kufanikisha hizo fani, lakini ni nini hizo fani, zina faida gani kwa jamii….ndio kitu walitakiwa kujiuliza, lakini kwa vile lengo lao ilikuwa kupata jina, na kupata ajira, hakuna aliyejiuliza hilo,…

‘Kuna ufadhili wa vikundi vya kuigiza, michezo mbali mbali…urembo, sanaa za kila aina maana wao wamelenga sehemu ambazo zinawagusa vijana, ili baadaye waje kufanya yale wayatakayo, na vijana wakiambiwa watakubali tu,….mfadhiki bwana mkubwa kasema, utabisha nini….

‘Umasikini na hali mbaya za kiuchumi zimekuwa pia silaha za hawa watu, wamejifanya ni wafadhili wa kusaidia watu wasiojiweza, ….jasho lao lililonyonywa kinamna linarejeshwa kwao kama misaada,na jamii iliyopo kwenye taabu inapokea kwa shukurani kubwa,..itafanyaje, hii ndio hali ya unyama unaendelea duniani, wenye nacho kuzidi kuwanyinya wasio nacho, na kuwadhalilisha……ni mbinu za hali ya juu sana……sasa haya yote kama jamii tunatakiwa kushirikiana sana kuyabadilisha….’akasema

‘Utajiuliza ni kwanini, ili iweje…?’

‘Ndoto zao ni kuitawala dunia,..kuwa na usemi wa kila kitu na dunia iwe na muelekeo mmoja, kwanza dunia iwe kijiji kimoja, …..hilo limeshafanikiwa, jingine tamaduni za kiutu zipotee, watu waishi kiunyama unyama, uchi…mtu apendavyo…au sio…..ili mwisho wa siku, kile kinachoitwa ushetani ndio kitawale dunia…’akaongezea

‘Sasa jamani nimewaletea huyu jamaa kwenu ili muweze kuamini haya ninayowaambia , ili mkiandika mambo yenu muwe na uhakika wa kile ninachowaambia,…kuwa hayo yapo na ndiyo wanayoimaliza dunia…baraka,zinaondoka, na kama mna maswali ya kumuuliza kabla hatujamalizana, maana baada ya hapa sitaki kuona mkilifuatilia  hili jambo tena….’akasema

Tulimuuliza maswali mengi huyo jamaa na majibu yake yalitufanya hata sisi tuogope ,kwa jinsi gani wanadamu wenzetu walivygeuka kuwa sio wanadamu tena, ni zaidi ya wanyama, na kisa ni nini, kupata utajiri, kutawala, ..kuiongoza dunia, …na jinsi alivyokuwa akielezea, nikakumbuka kile kisa cha dunia yangu…nikagundua ni wale wale….nii chimbuko lake!

 ‘Wao wanaamini kuwa kila mtu ana uhusru na utashi wa kufanya apendavyo, ajisikiavyo, na asiingiliwe, na sheria ziwkwe kutokana na utashi wa watu,..kusiwe na sheria za kumlazimisha mtu kwa viti vinavyomfurahisha, na mbora wao ni yule aliye na utajiri, …mjanja,  mwenye mamlaka, …kwaho huo ndio ubinadamu ….’akasema

‘Sasa hizo dawa za kupandikiza magonjwa zina faida gani kwao maana zinawakwanza watu wasifanye wale wayapendayo…?’nikataka kuuliza na yeye akanikatiza kwa kusema;

‘ Hizo dawa ni silaha , badala ya kutumia bastola, bomu..vitu vyenye kionekana wao wakaona ni bora kuwe na silaha za kuua kimia kimia…ina maana bwana mkubwa akisema leo huishi kweli siku hiyo unaondoka…na hakuna ushahidi, …ukichunguza hivypo vidonge ukiviweka kwenye ulimi vinayeyuka mara moja kama glucose, na kwa haraka vinakimbilia kwenye mishipa ya damu na kuathiri mapigo ya moyo, na mtu huyo haichukui muda,…anakufa!  Kama ni maalumu kwa kuua, kama ni kwa mateso vipo vya namna yake, na kama ni kwa magonjwa vipo kwa namna hiyo hiyo lakini kwa vipimo vyake, wataalamu wenyewe wanafahamu!

‘Sasa ilikuwaje kwa mdada, maana hatuoni kama alikuwa tishio, kihivyo, kwanini na yeye akawa muhanga wa mambo hayo, au alikuwa mmoja wa wanachama wa siri….?’ Tukauliza hapo yeye alikaa kimia mpaka tukaingiwa na wasiwasi kuwa anaogopa kujibu hilo swali na baadaye akasema

‘Mdada ana kipaji kikubwa cha uigizaji, ana umbo zuri lenye mvuto,…sura yake kwenye picha ni zile sura zinavutia sana, na kwa watu kama hawa wanahitaji warembo wa namna hiyo, kuvutia biashara zao…akina dada, wanatumiwa sana,wananyonywa, wanazalilishwa kwa urembo wao na nini faida wanapata…hakuna, wanaofaidika ni wao tu…mdada alitakiwa kuandaliwa hivyo….’akatulia.

Kikwazo kikubwa ilikuwa wazazi wake…wazazi wake walibobea kwenye dini, ….ikaonekana ni tatizo, …wakaamua kumtumia mchumba wake,….mchumba wake ukichunguza sana  yeye alikuwa na utaalamu wa magari , ana kipaji kikubwa sana cha ufundi, hata hajaenda shule, lakini aliweza kulifahamu gari na muundo wake…hawa ndio watu wanahitajika, wenye ufundi wa kipaji, na wakipewa shule kidogo tu wanakuwa mafundi wa hali ya juu.

Huyu jamaa akiwa na mdada watakuwa hazina kubwa ya kundi, lakini je wanaelekea, je watakubaliana na sera za kundi,…walichunguzwa kitaalamu wakaonekana ni vigeugeu…kwamba siku yoyote wanaweza kuuza siri, lakini bado wanahitajika, …ndio wakapewa kazi za muda za kufanikisha mambo , na ikifikia muda hawahitajiki tena, wanaishilia mbali….wakawa wamepandikiziwa magonjwa …..yatakayowatafuna hadi muda muafaka,magonjwa haya haya tunayoyafahamu sisi..ni nani ataligundua hilo…’akatulia

‘Mimi sikuyafahamu hayo,nimekuja kuyagundua hayo ya madawa, nilipogundua kuwa hapo kuna tatizo, nikaanza kufanya uchunguzi wangu mwenyewe..mpaka nikapata hizo siri…lakini ni siri zisizo na mshiko, ushahidi upo wapi…huwezi kusema huu ni ushahidi, wakati kila kitu kinapotea,….sumu iliyofanya hiyo kazi hufutika kabisa mwilini ,huwezi kuigundua, …wanahakikisha kuwa hakuna maandishi yoyote ya ushahidi ynabakia , mara nyingi hawatumii maandishi haya ya kawaida wanatumia maandishi ya ishara….jambo likikamilika kila kitu kinaharabiwa na hata wahusika, wanapotezwa…

Tukienda kwa mdada, yeye alikuwa kama chambo tu, japokuwa wakipenda awe mmoja wa warembo wao, kwani alikuwa na sifa zote, lakini ilionekana ni hatari zaidi kuwa naye kuliko faida yake,  siku zao zikafika..

Kuna kazi walitakiwa kupewa, majukumu ya kuhakikisha mipango yao inakamilika,  lakini ilipoonekana kuna ufuatiliaji, jamii, imecharuka, na serikali imegundua kile walichokuwa wakikifuatilia,wakaona wote waliokuwepo wapotezwe…’akasema

‘Serkali iligundua nini…?’ tukauliza

‘Hawa watu hawawekezi tu mahali bila ya kujua ni nini watakipata , pamoja na kutafuta sehemu za kuwekeza, wakitumia rasilimali watu, lakini pia mara nyingi wanatafuta na mali asili, nchi yetu hii imebarikiwa sana na kuwa na mali asili,…watu wao walishafanya uchunguzi wakaligundua hilo…’akasema

‘Wao wanajua jinsi gani watu wao watapata hizo nafasi za uwekezaji,lakini pia hawataki kupoteza hiyo nafasi ya kutumia rasilimali watu, ambao wanajulikana kuwa watafika hapo, kutakuwa na mambo ya starehe…biashara, na humo watawekeza mambo yao mengine pia.

‘Wahanga wa hayo yote ni akina mdada, wakitumika kama chambo…na ilipoonekana wanaweza kuwa mzigo badala ya tija, wakatakiwa kupotezwa, ndio  wakapewa madawa hayo ya …..kupoteza kinga….kupungukiwa damu…kwenya jamii ni magonjwa ya kawaida, hakuna atakayeshuku kuwa ni wao wamepandikiza mambo yao..

 ‘Kwahiyo…ina maana matatizo aliyo nayo mdada sio ugonjwa halisia, na ugonjwa wa kupandikizwa, na huenda anaweza kupona..au ukishapewa madawa hayo ya sumu huwezi kupona tena?’ tukauliza kwa shauku

‘Ni waambie ukweli,..hawa watu ni wataalamu kweli, wakifanya jambo lao hawakopeshi,sasa inategemea nia na lengo lao ilikuwa ni nini….kuwamaliza kabisa akina mdada na wenzake au kuwatesa kwanza hadi hatua fulani, lakini inavyoonekana lengo lao ni kuwa hao akina mdada waje kufa, kwa namna ionekane ni kifo cha kawaida,…upungufu wa kinga, na kuishiwa na damu, sasa mimi sijui zaidi labda madocta wameweza kuisafisha hiyo sumu kitu ambacho sizani kama kinawezekana,….sijui…’akasema akimgeukia docta ushauri.

‘Kwahiyo na wewe ulishajifahamu kuwa wamekuwekea hizo sumu, na ulishajua kuwa itafika muda, utaondoka, au sio, sasa ni kwanini ukajiunga na kundi la kuhamasisha, …kuishi kwa matumaini, huku ukijua wewe ni mhanga wa sumu hizo, na hauhusiki na ugonjwa asili wa kupungukiwa kinga za mwili…?’ akaulizwa

‘Najua muda utafika nitaondoka,..sina jinsi, ndio maana niliona kwa kujipa matumaini hii ndio njia pekee, ya kujikosha kutubu, na kusaidia wenzangu ili nipate cha kunisaidia huko ahera….’akasema kwa sauti ya huzuni.

‘Ni kwanini mkajiunga na makundi haya haramu….sasa mnaona athari zake, mnakuja kuwaumiza na hata ambao wasio na hatia…’mwenzangu akasema kwa hasira.

‘Nyie hamuwajuia hawa watu ni hatari,na wakikutaka watakupata tu, kwa mbinu mbali mbali…wanajua watu wengi wanatafuta, wanatafuta maisha bora, kwa kasi ya hali ya juu, na kazi hizo wanazijua jinsi gani ya kuzitengeneza, si mnataka kazi, mtaenda wapi,….’akatulia

‘Kwahiyo wengi wetu, tuna usemi kuwa ajali kazini, tutakufa tukiwa kwenye nia ya kutafuta, na tuliobahatika kujitambua ndio hivyo, tunatafuta mema ili yaje kutusaidia, ..ni kweli tulijiingiza kwenye mabaya, lakini tungefanyaje, sikio la kufa….’akasema kwa sauti ile ile ya huzuni.

‘Kwa kifupi, ndio hivyo, mimi niliyebakia, nasubiri hapo sumu hiyo ikifikia kielele chake basi nitaondoka..japokwua madakitari bado wanajitahidi kupambana, kuendelea kunisaidia kusafisha damu, sijui…’akasema akitikisa kichwa

Mimi nikaona muda unakwenda wakati hatujalipata lile tunalolitaka, nikauliza swali hili kwa kuchokonoa ili nipata huo ukweli

‘Je kwa mdada mlifikia wapi, hali yake ipoje…mliweza kumuokoa,…?’ tukauliza swali na jamaa huyo akamgeukia ofisa upelelezi, na ofisa upelelezi akamgeukia docta ushauri, na baadaye akasema;

‘Najua muna hamu sana ya kusikia kumuhusu mudada, kwani ndiye aliyewafanya hadi mkafika hapa…lakini mimi nia yangu ilikuwa kwanza muelewe hali halisi, maana mtu kama mdada ni mmoja wa wahanga kati ya wengi walionaswa na balaa hili,

‘Inasikitisha kuwa vijana nguvu kazi ya jamii  inaharibiwa,…kwa ajili ya tamaa ya wachache wenye ndoto za kupata tu kwa vyovote vile,….watu hawa wamejenga mehakalu, wana miradi mingi lakini bad hawatosheki, …maana laana ya ufisadi ipo ndani ya damu zao….ukiangalia sasa hivi maisha ya kuishi kama kijana  ni machache sana, ..ni kwanini…uwezo wa vijana kuhimili katika umri wa kijana ni mdogo sana, wanazeeka mapema sana ni ..kwanini…ni athari ya haya yote…’akatulia na kuangalia saa, halafu akasema

‘Sasa kwa kujibu swali lenu, hebu subirini kidogo…nione kama hawa watu wapo tayari,….’akasema, akachukua simu na kupiga simu, alisikiliza kidogo halafu akatabasamu na kusema

‘Kumbe wameshafika , ingieni….’akasema kwa sauti

Mara mlango ukafunguliwa, …akaingia mwanadada mmoja, shupavu, kwa unekanaji wake, nilimtambua kuwa huyo hawezi kuwa huyo mdada, bali ni askari, alikuwa kambeba mtoto mchanga, mikononi, na alipojitokeza tu pale mlangoni alionyesha ishara za kiaskari,  akasema

‘Tumeshafika mkuu…aingie…?’akasema

‘Mwambia aingie tu, tunamsubiria yeye…’akasema huyo ofisa upelelezi.

Na mara akaingia mdada mmoja akiwa akjifunika khanga, ..ile ya kuashiria kuwa huyo ni mzazi, ilikuwa haijifichi, alikuwa mama wa hicho kichanga, na alipoingia akaonyeshwa wapi akae,….kwanza alisita kufanya hivyo, akawa kasimama , lakini dakitari ushauri akasema;

‘Usiogope mpendwa, mimi ndiye nimekuhitajia,….’akasema

‘Hawa unaowaona wote hapa ni marafiki wema kabisa, kwa namna moja au nyingine, wamekuwa wakikuhangaikia wewe, kuhakikisha unafanikiwa, usiwaogope kabisa, lengo lao ni kukusaidia kila mmoja kwa namna yake, na wote wana kibali cha kufanya hivyo…nitakutambulisha kwao usiwe na shaka upo salama…’akaambiwa

Lakini mdada huyo bado alionekana kuwa na mashaka, akageuka kumwangalia Yule askari aliyembeba mwanae, halafu akageuza uso kumuangalia ofisa upelelezi, halafu akatugeukia na kutuangalia sisi wawili…sijui kwanini, kwani haikupita muda, machozi yakaanza kumtoka…

NB: Nilijua leo tutamaliza, lakini kumbe duuu..bado kuna kitu kidogo cha kumalizia, huyu ndiye nani , ..najua nyote mumeshapata jibu, lakini ni kwanini analia ?

WAZO LA LEO: Wengi wetu tunatubia makosa yetu pale tunapoona hatuna jinsi, …muda wa kuishi umekwisha, au tumebanwa kiasi kwamba hatuwezi kufanya lolote. Na ni wachache wanaoweza kuliona hilo wakafanya toba,toba ya kweli,  kwani  mara nyingi madhambi ya kudhulumu yanaziba ufahamu wetu, ubinafsi unazitawala nafsi zetu, na hata kuyaona yale tunayofanya ni ujanja wetu…..
Tukumbuke sisi ni wanadamu tu, wapiti njia, yote tuyafanyayo yanahesabiwa, na ipo siku 

yatatuhukumu, kama ni hivyo basi, tujirudi, tutubu toba ya kweli, na tutubie bado tukiwa na ufahamu wetu, …ili toba hiyo ifike kwa tuliowakosewa, waweze kutusamehe, ikibidi  tufanye jambo, turejesha mali ya watu tuliowadhulumu, tutende mema, ili hayo mema yaweze kufuta hayo maovu yetu

Ijumaa njema!

Ni mimi: emu-three

No comments :