Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeWednesday, March 16, 2016

SIKIO LA KUFA HALISIKII DAWA-19 HITIMISHO 1


Tuliamua kulifuatilia hili tatizo, kama tunaweza kuwahi, kwahiyo tukafunga safari ya kwenda hospitali aliyokuwa kalazwa huyo mdada, haikuwa vigumu kuipata kutokana na vyanzo vyetu vya uchunguzi, na kinyume cha tulichotarajia, tulijikuta kwenye matatizo makubwa, mpaka ilifikia kujuta kwanini tulifuatilia,lakini hayo ni moja ya majukumu yetu ya kusaidia jamii.

Hebu tuone mwanzo wa hitimisho hili, …ni nini kilitokea kwa mdada, ukumbuke hapa sio mdada anajieleza , haya ni mambo tuliyokutana nayo tulipoamua kujua ukweli…kweli dunia ina mambo….Tuendelee na kisa chetu

                  *********

 Tulifika hospitali ambayo alikuwa kalazwa mdada, tukajitambulisha kuwa tuna mgonjwa wetu kalazwa hapo, na sisi ni marafiki wake, lakini marafiki wa mtandao….hatukutaka kuficha jambo, kwani tulijua tunachofuatilia ni muhimu hata wao wanaweza kutushukuru.

‘Mgonjwa huyo ni rafiki wa mtandao, kiukweli hatujawahi kuonana naye uso kwa uso, ila sisi tunatokea kwenye mtandao wa `diary yangu,..’ mtandao wa mambo ya  kijamii na visaha vyenye kunasihi, ….sijui kama uliwahi kuusikia…’tukasema

‘Mhh, nausikia …sikia,unajua tena kazi zetu wengine hatuna muda wa kusoma soma visa, ila mke wangu ni mpenzi wa mtandao huo, ehe sasa niwasaidie nini…’akasema

‘Sisi hatutaki kukuficha,hapa kuna mgonjwa mmoja ambaye alilizwa akiwa mjamnzito, na yasadikiwa kaathirika, na alikuwa kwenye mipango ya ushauri nasaha…ila kwa taarifa zake alizotutumia ni kuwa alikusudia kujiua, na kwahiyo tumekuja tusaidiane kumuokoa…’tukasema

‘Kujiua…?’ akauliza huyo dakitari msemaji mwenye dhamana hiyo, maana ilibidi kumtafuta mtu ambaye ataweza kutuamini na mwenye mamlaka ya kutoa taarifa!

‘Ndio tulipokea ujumbe wake kwa barua pepe, na maelezo yake kwa ujumla yaliashiria hivyo, kutaka kujiua…’

‘Kwanini atake kujiua…lakini hayo mbona yapo sana hapa, wanakuja watu kihivyo na baadaye wanabadilika, sioni kama jambo la ajabu hapa kwetu ajabu yake ni kuwa nyie mumekuja kufuatilia…’akasema

‘Kwa maelezo yake haoni haja ya kuishi kwa matumaini kwani anajua baada ya yote ni lazima atajikuta kwenye maisha magumu, yeye na mtoto wake, sisi tunaomba tuonane naye kama hilo halijatekelezeka, maana tumefika hapa kwa haraka, ni swala la muda,…je hakuna mgonjwa yoyote aliyetaka kujiua…mkagundua?’’tukauliza

‘Hapana….wapo wanakuja wakijieleza hivyo,…lakini haijawahi kutokea akafikia hatua sasa anataka kujiua mpaka kwenda kumuokoa,…anakuja kihivyo kachanganyikiwa baadaye anaeleweshwa mapema na anakubaliana na  ushauri lakini kwa kipindi cha karibuni hakuna mgonjwa kama huyo,…labda ni taarifa za uwongo za mitandao…’akasema

‘Hapana hizo taarifa sio za uwongo, sisi huwa tunafuatilia taarifa yoyote inayokuja, tunajua hiyo ni uwongo wa kutunga au huo ni ukweli…tuna uhakika hiyo ni taarifa ya kweli na ni swala la kufuatilia kwa haraka, na hivi inawezekana tunapoteza muda…’nikasema

‘Je jina la mgonjwa huyo ni nani…?’ akauliza

‘Mhh…ndio tatizo hapo, yeye alijitambulisha kama mdada…mrembo, aka, malikia wa kijijini…’nikasema na dakitari akacheka kidogo na kusema

‘Mnaona…hilo jina tu linaonyesha dhahiri kuwa ni story za mitandao za kutunga, wayu kama hao ni matapeli wanatafuta misaada kwa njia hiyo…’akasema

‘Docta, hili ni swala la kumuokoa mtu, kama hijatokea basi kakusudia kufanya hivyo, inabidi mufanye juhudi za kumuokoa…tusaidiane tumpate , yuna uhakika yupo hapa kwenye hospitali yako…’nikasema na mwenzangu akaonyesha hamasa hiyo kwani hadi hapo tuna uhakika hakuna dalili ya tatizo , huenda hajajiua.

‘Kiukweli hakuna mtu kama huyo aliyewahi kufanya jambo kama hilo, na hakuna mwenye dalili za kufanya hivyo, hebu niambieni yupoje kwa maelezo yake, maana atakuwa kajieleza vya kutosha….’akasema na sisi tukamuelezea jinsi alivyo na yakuwa alitokea kijijini akiwa mja mnzito akafikishwa hapo kwa ushauri nasaha…

Na hata baada ya maelezo hayo dakitari huyo akasema;

‘Hatuna mtu kama huyo hivi karibuni,…’akasema akiangalia saa yake kuonyesha tunampotezea muda


‘Docta sisi tuna uhakika na hilo….na nia yetu ni kuokoa, na hatungeliweza kuja hadi hapa bila sababu ya msingi, na tunaogopa, inaweza kutokea jambo,na nyie mkawa lawamani, kwani hamkutaka kushirikiana nasi…’tukasema na yeye hapo akawa kama kaingiwa na shaka akasema

‘Mimi sina zaidi cha kuwasaidia, labda kwa sasa mkajaribu kuongea na mshauri nasaha, kama yeye atakuwa na kumbukumbu hiyo, lakini kwa utendaji wako na kwa taarifa nilizo nazo hakuna jambo kama hilo ..mnasema ni lini mlipokea hiyo taarifa….’akasema

‘Jana ….usiku……’nikasema

‘Basi hakuna kitu kama hicho, na hakuna mgonjwa mwanamama wa aina hiyo kwa hivi sasa…’akasema

‘Hakuna mgonjwa kama huyo mliyetakiwa kumfanyia upasuaji akiwa na matatizo hayo, jana …au leo asubuhi,..?’ tukauliza

‘Hakuna…nina hakika huo, kwa maelezo zaidi basi nendeni mkaongee na mhsauri nasaha yeye atawathibitishia hilo, si mnasema huyo mgonjwa alitumwa kwake…si ndio hivyo, nendeni ofisini kwake…’akasema

Basi ilibidi tuombe kibali cha  kuonana na mshauri nasaha huyo, ila tukaambiwa kwa muda huo hayupo,…tukawa hatuna jinsi ila kumsubiria, tukiombea mungu huyo mgonjwa asije akafanya hilo jambo..kama kweli hajalifanyika

Baadaye kidogo mshauri nasaha alifika, …

                   **********

‘Kwani nyie huyo mgonjwa mnayemuulizia kama kweli yupo ni nani kwanu, maana mambo yote yanayowahusu wagonjwa hapa ni ya siri ya wagonjwa na labda na familia zao husika, na sisi kama watendaji wao, tunalinda haki na usiri wa wagonjwa..?’ akauliza

‘Sisi ni rafiki zake wa mtandao, tuliwasiliana naye kwa njia hiyo, alituelezea kadhia ya maisha yake na hatua ya mwisho ndio akaandika hivyo kuwa anataka kujiua…’tukasema

‘Unajua watu kama hao wanaofikia kusema wanataka kujiua wanakuwepo hapa, wanakuja kwa dhamira hiyo, lakini mwishoni baada ya kukaa nao, tukawapa ushauri nasaha wanakuja kubadilika, sasa sijui ni yupo kati ya hao wengi,na hatujapata kadhia kama hiyo hivi karibuni mimi, sikumbuki…?’ akauliza

‘Mdada huyo alitokea kijijini na aliletwa kwako na ndugu yako…’tukasema na hapo akaonyesha kama kushituka kidogo lakini akaificha hiyo hali, na kwa macho ya kama kudharau hayo maneno akasema

‘Aliletwa na ndugu yangu, hivi karibuni, jana,juzi ….mmh, sikumbuki….’akasema

‘Sio kwamba alimleta yeye, ila ndugu yako huyo alimuagiza kwako, na wewe ukaenda kumpokea kituoni na wakati mnakuja naye kuelekea kwako, ukahisi hali yake sio nzuri, ikabidi mpitie kwanza hapa hospitalini, akaonekana ana upungufu wa damu….’tukasema na hapo akaonyesha kama kukumbuka jambo akasema

‘Mnasema yeye huyo alitokea kijijini alikuwa mjamnzito, alifika hapa kwa maelekezo ya ndugu yangu, akawa na tatizo la upungufu wa damu…au sio, mhhh… aliyemuagiza kuja kwangu ni ndugu yako, sijui kama ni huy…lakini hapana sio yeye…’akasema sasa akiwa kautulizana, akitafakari

‘Lakini kwa kumbukumbu zako yupi mtu kama huyo..?’ tukauliza

‘Ok…sijui kama ndio huyo…ila kama ndio huyo mimi siwezi kusema lolote kumhusu yeye kwa hivi sasa…’akasema kwa sauti ya huzuni, akitikisa kichwa

‘Kwanini mshauri nasaha, kwanza tukuambie kuwa tumekuja hapa kwa haraka ili ikiwezekana muweze kumuokoa kwa tatizo hilo la kupanga kujiua, na kama haijatokea mtu kujiua, au kukusudia kujiua,…basi ina maana bado yupo, na jinsi alivyotuelezea kama hakufanikiwa kunywa hiyo sumu basi mtakuwa mumeshamfanyia huo upasuaji, lakini ni vyema mkachukua tahadhari, na kama inawezekana tunaomba tuonane naye.’ Tukasema

‘Ndivyo alivyowaambia kuwa mje kuonana naye…au nyie mnapenda kufanya hivyo?,….lakini mimi bado sijakubaliana na nyie, hakuna mtu kama huyo…’ akauliza na kusema

‘Hajasema tuje kuonana naye..ila ni muhimu kama yupo tuonane naye kuna maswali ya kijamii, kama wasamaria wema tungelipenda kumuuliza na vile katuamini hadi kutuandikia sisi hayo yote tuna imani atatupokea kama ndugu zake….’tukasema

‘Sio kweli…’akasema

‘Kwanini unasema hivyo….?’ Tukauliza

‘Kama ndio huyo mnayemzungumzia, …sio kweli, kuwa atawapokea nyie kama ndugu zake,…kwasababu asingelipendakabisa hilo litokee, ..la kuonana na watu…sio kweli, na hata hivyo kamani huyo hamuwezi kumuona tena….’akasema

‘Hatuwezi kumuona tena! Ina maana tumechelewa au una maana gani,  kwahiyo alijiua kweli, keshashakufa…au …?’ tukauliza kwa mashaka.

                  **********

‘Kama nilivyowaambia mimi kama mshauri nasaha siruhusiwi kutoa taarifa zozote za mgonjwa wa hapa,..japokuwa utawala umesema nishirikiane nanyi kwani nyie mnaonekana hamna nia mbaya…’akasema

‘Ni kweli nia yetu ni kusaidiana kwa hilo, kusaidia jamii kwa ushauri, hasa kwa njia ya mtandao lakini ikibidi tunawatembelea watu kwa nia hiyo hiyo, …ikitokea jambo la kufanya hivyo, kama ni uhalifu, tunashirikiana na polisi, na kama jambo kama hili , tunawahi kuokoa kabla halijafikia kubaya,…’nikatulia kidogo

‘Tungelikimbilia polisi, lakini tuliona haina haja,ngoja kwanza tumuokoe ..ndio maana tukaimbilia huku kwa nia njema, kama hajafanikiwa kufanya hivyo basi tuongee naye tu, kumnasihi tunavyoweza…’tukasema.

‘Ndio nimeshawafahamu…. hata mimi nafuatilia visa vyenu vyenya mafunzo, msione kuwa madakitari tupo tu, tunasoma mambo mengi sana hasa yenye manufaa kwa jamii, hasa kwenye hii kazi yangu ya nasaha, ninajitahidi sana kuwa karibu na jamii, na kikweli nimependa sana mnavyoisaidia jamii kwenye mtandao kwa njia ya visa mbali mbali,….lakini hili swala kwa hivi sasa lipo nje ya uwezo wangu, kwa jinsi lilivyo…’akasema.

‘Labda utujibu kwa mkato, maana tusipoteze muda wako, …na sisi tulikuja kwa haraka kama zima moto wameitwa kuzima moto,kama tumewahi au la,..je kuna tatizo au hakujatokea tatizo, kama hilo, ?’ tukauliza

‘Kwahiyo nyie mlikuja kufanya nini hasa, kutoa taarifa kuwa tufuatilie au kuja kusaidia kuokoa,…kwanini nauliza hivi, maana kama ni huyo mnayemzungumzia mbona mumechelewa , …..?’ akauliza

‘Sisi tulipoisoma tu hiyo barua pepe, tuliamua kuchukua hatua za haraka iwezekanavyo ndio maana tumekuja hapa hata bila ya kupoteza muda baada ya kuhakikisha kuwa barua pepe hiyo sio ya uwongo ni kweli,…’tukasema

‘Basi mumechelewa….’akasema

‘Kwa vipi…?’ tukauliza kwa mashaka

‘Kama ni huyo ambaye ninajua taarifa zake, aliyetumwa kwangu na ndugu yangu mbona ni tukio la muda, ni kiasi cha wiki mbili sasa na siku kama tano  zimeshapita, ndio maana nahisi tunaongelea watu wawili tofauti, na mimi huwa nahudimia watu wengi…sasa sijui kama ndio huyo…’akasema

‘Atakuwa ndio huyo…alikuwa mja mnzito kutoka kijijini na kaelekezwa na dada yako kuja kwako, kwa ajili ya matibabu na ushauri nasaha, lakini tukio hilo ni la jana, sio wiki mbili…’tukamfafanulia vyema, akatulia akiwaza halafu akasema

‘Kuna mmoja alifika hapa akiwa na mja mnzito kweli , alifika kwa kuelekezwa na dada yangu kweli, tukampokea na kujitahidi kumsaidia kadri tulivyoweza, tulimpa ushauri nasaha, akakubaliana nasi, lakini katika hatua za kwenda kufanya upasuaji kukatokea jambo ambolo haturuhusiwi kuliongelea kwa hivi sasa kwani lipo juu ya uwezo wetu….’akatulia

‘Sawa inawezakana kumetokea matatizo au sio… na polisi wamehusishwa au sio….sisi tunachotaka ni kuwa na uhakika je tumemuwahi, je kuna baya limetokea,…au vipi kama hakuna tuweze kuonana naye tu….’akasema mwenzangu.

‘Lakini sio huyo kutokana na muda mliosema…’akasema

‘Yawezekana ndio huyo,kama tunaweza kumuona itakuwa ni vyema zaidi…tukaongea naye sisi wenyewe..’nikaongezea kusema na yeye akabakia kimia kwa muda, mimi nikauliza

‘Je aliwahi kunywa hiyo sumu…..kumeza hicho kidonge kwa nia ya kujiua au la…?’ nikauliza

‘Mimi ninachoweza kuwaambia kwa hivi sasa, kama ni huyo hamuwezi kumuona…’akasema

‘Kwanini docta, tunaomba sana basi utupe maelezo ya kujitosheleza ili tukiondoka hapa na sisi tujue la kufanya, …’tukasema

‘Nina maana yangu kubwa kusema hivyo, kama ingekuwa yupo hapa hospitalini kwanini nisiwaruhusu kwanza nyie mnafanya kazi ambayo na mimi naifanya, kusaidia jamii, japokuwa mimi ni mtaalamu zaidi yenu, na sihitaji msaada, lakini nafahamu juhudi zenu…’akasema

‘Sawa kabisa…wengi wanaotufahamu tunashirikiana kwa wema kabisa…japo kuwa tunajitolea tu…ni kazi kubwa, lakini wema hauozi…..’tukasema

‘Ni kweli…wema hauozi,…Lakini mnielewe hamuwezi kumuona huyo mtu,kwani hayupo…’akasema na kukatiza na mimi nikatafsiri moyoni kuwa alitaka kumalizia, `duniani’ kuwa keshafariki..lakini sikupenda kutumia neno hilo na mwenzangu naye akauliza kwa haraka

‘Ina maana keshaondoka…?’ akauliza

‘Siwezi kusema….’akatulia kama akiwanza na mimi nikazidi kumuuliza

‘Kwahiyo kwa kifupi, mlifanikiwa kumfanyia upasuaji salama na keshaondoka, ni bora utuelekeze wapi tunaweza kumpata ili tuongee naye asije akabakia na wazo hilo tena, ina maana hakukubali kubakia kwenye mamlaka yako tena, maana alikuwa akihitaji msaada wa kijamii wa hali na mali?’ tukauliza

‘Mnajua nasita kuwaeleza zaidi ya hapo kutokana na hali ilivyokuwa, ni nyeti na hatari, mnaelewa, ni swala la kiusalama….’akasema

‘Basi kwa msaada wako tunaomba utuamini, hebu tuambie japo kwa ufupi, Ilikuwaje, labda utufafanulie japokuwa unasema ni siri lakini tuambie yale unayoweza kuelezea ambayo hata sisi yatatusaidi ili turidhike, ilikuwaje , tusipoze muda au hilo nail huwezi kutusaidia?’ nikauliza

Mshauri nasaha huyu alitulia kwa muda,…baadaye aliamua kutuambia ukweli, tuliohitajia…

****************

‘Unajua aliyekuja kuniambia na kutusaidia kwa hilo ni huyo jamaa kutoka kijijini, na aliniambia hilo wakati tunaongea naye kuhusu aliyekuwa mchumba wa huyo mdada akaniambia kuna jambo jingine muhimu sana anataka kuniambia na kwa muda huo nilikuwa na miadi mingine kwahiyo nilimuambia

‘Sikiliza kama ni mambo hayo hayo, wewe achana nayo mimi mwenyewe nitajua jinsi gani ya kuongea naye…’nikamwambia

‘Hapana  sio kuhusu huyo mchumba wake tena, hilo linamhusu huyo mgonjwa wako mwenyewe ina maana mdada, malikia wa kijiji…..yeye anakusudia kujiua….’akasema

‘Kujiua!! ..ndivyo alivyokuambia hivyo, lini..?’ nikamuuliza kwa mshangao, japokuwa kiukweli sikuona ajabu , maana kuna wengi wanakuja na msimamo huo, lakini tunapokutana nao tunawashauri na wanakuja kubadili nia yao, nikahisi huenda alisema hayo awali kabla hajapata ushauri nasaha

‘Lakini naomba usije kumwambia ni mimi nimekuambia hilo, …kwani ni hatari zaidi akijua nimekuambia na ni hatai zaidi pia akijua mumemfahamu dhamira yake yake hiyo….’akasema

‘Kwanini, na alikuambia hayo muda gani…?’ nikamuuliza

‘Muda ule ule uliponikuta naongea naye,…na nahisi kapanga kufanya hilo kabla ya upasuaji, na nijuavyo mimi watu wa kundi hilo wakidhamiria hivyo kutokana na kiapo chao, hawarudi nyuma kwani yawezekana ni kutokana na shinikizo la kundi…sina uhakika zaidi, ila yeye kaniambia ni kutoka na kujua kuwa huko mbele  hatakuwa na maisha mazuri, yeye ni mtu wa kufa tu.. ’akasema na mimi hapo nikahisi kuna jambo, nikatulia kidogo na yeye akaniuliza swali kwa haraka

‘Ni lini mnatarajia kumfanyia upasuaji,…?’ akauliza

‘Kesho , leo au keshokutwa hiyo ni kazi ya madakitari….’nikamwambia

‘Basi ningewashari upasuaji huo muufanye haraka iwezekanavyo,na pia mumuwahi kuhakikisha hazitumii hizo dawa, ikibidi mziondoe kwenye himaya yake, kwani anaweza kuzitumia muda wowote ule kutegemeana na shinikizo la kundi hilo,...na pindi akizimeza, hamuwezi tena kumuokoa….fanyeni hivyo haraka iwezekanavyo…’akasema kwa msisitizo

‘Dawa gani hizo, zipoje….?’ Nikamuuliza

‘Wewe fuatilia hilo ni muhimu sana, ..siwezi kusema ni dawa gani hizo , ila ninachojua ni vidonge akivimeza tu vitamuua hapo hapo…..na hamtukuja kujua ni sumu….’akasema na mimi hapo nikaanza kuingiwa na wasiwasi. Kiukweli mwanzoni sikutilia maanani lakini alipotaja sifa za hiyo sumu, nikaanza kuingiwa na mashaka.

‘Niliongea naye mwenyewe akakubaliana nami kuwa kaelewa kwanini atake kufanya hivyo tena, kuna yoyote aliyokuambia ya kubadili nia yake , maana tulikubaliana naye akasema yupo tayari kufuatilia ushauri wangu...?’ Nikamuuliza

‘Mshauri nasaha, dakitari….usije kujutia kwa hili…wahini, tafuteni mbinu haraka ili muweze kulizuia hilo, kabla hamjachelewa, ..mimi nimetimiza wajibu wangu, japokuwa kwa kufanya hivyo najiweka kwenye maisha hatarishi zaidi…’akasema

‘Lakini haiwezekani , hata kama anazo hawezi kuzitumia…lakini kama unavyosema basi itakuwa ni vyema kuziondoa kwenye miliki yake….,kwani kweli huko mbele, anaweza kubadili nia….’nikasema

‘Naomba unielewe mshauri hayo ninayokuambia sio swala la kukisia, huyo anatarajia kujiua, mimi nina uhakika,…wanachama wengi wa hilo kundi walivyoapishwa kwa vitisho, na sio vitisho ni kweli wanafanya hivyo,…kwahiyo hapo japo hakuniambia hivyo, anaogopa asipofanya hivyo, wazazi wake watateswa au kuuwawa…hata hivyo yeye akijiua hatapoteza kitu kutokana na hali aliyo nayo kuwa hatapona…’akasema

‘Unasema wanachama wa kundi hilo, ni kundi gani hilo...?’ nikamuuliza

‘Mimi nawaombeni wala msipoteze muda, nendeni kwenye mkoba wake wa kike,…ni lazima zitakuwepo hizo dawa humo, sizani kama anaweza kuzificha sehemu nyingine…ziondokeni mikononi mwake…mtakuwa mumefanya jambo muhimu sana kuliko kuhangaika kujua ni kundi gani,…’akasema

Kwa kusikia hivyo, niliona nimeshindwa jukumu langu  kama mshauri na haijatokea, wengi nawasaidia,na wakikubali, haitokea kinyume chake, na kama huyo mdada atajiua mimi nitakuwa matatani,…na hata kama nitaweza kujinasua kwa hilo, lakini nafsi yangu itaumia sana, kwahiyo niliposikia hivyo, ikabidi niwasiliane na utawala wa hospitalini, na ilikuwa ni swala la muda. Je huyo mdada atazitumia hizo dawa au la na akipanga kuzitumia ni muda gani…haikujulikana .

Ikabidi tuharakishe hata upasuaji wake, ili kutokuweza kumpatia muda mwingine, lakini pia lazima juhudi za haraka zifanyike kumuokoa huyo mdada, kama alivyosema huyo jamaa kutoka kijijini kuwa mdada kwa hivi sasa kama hatafanikwia kulifanya hilo atakuwa akiwindwa, kwani wenzake watakuwa hawamuamini tena ,……

Ikabidi juhudi za haraka zifanywe kuupata huo mkoba wake ambao alikuwa habanduki nao, na ilitakiwa kufanyika hivyo bila hata ya yeye kufahamu, kitu ambacho kilikuwa kigumu sana, mdada habandukani na huo mkoba wake…

‘Je tumwambie?,….ilikuwa jambo la mwisho kufanya kutokana na alivyotuonya huyo jamaa…
                                  

                    *********

 Tukaanza mikakati ya haraka na kuhakikisha kila mara kuna mtu anakuwa karibu yake, japo kujifanya kama anahudumia wagonjwa wengine lakini ahakikishe hachezi mbali na huyo mdada….ujue hayo yamefanyika kwa muda mfupi sana. Kuna nesi wetu tunamuamini sana, tukamtumia ili tuweze kumfanya awe mbali na huo mkoba wake.

Nesi akafanya hilo, alitumwa ili amwambie huyo mdada kuna maandalizi yanatakiwa  kufanywa kabla ya kufanyiwa huo upasuaji, nesi huyo akaelekezwa cha kufanya ili watoke naye hadi huko bafuni na ajitahidi kumchelewesha ili tuzipate hizo dawa, na ikibidi tuwexe kuzibadili hizo dawa za sumu na dawa nyingine ili asije kugundua hilo.

 Kama nilivyosema nesi anayemuhudumia mara kwa mara huyo mdada, anasema Mdada huwa haachi mkoba wake hata akienda bafuni au chooni, lakini tulimwambia huyo nesi ajitahidi, awezavyo ili mdada aweza kuucha huo mkoba wake, haikuwahi kutokea tangia afike hapo kuachana na huo mkoba wake.

Nesi alifanya kazi yake na kweli huo mkoba ukapatikana, na kwa muda huo na sisi tulishatafuta dawa tunazohisi zinazofanana na hizo..kwa kukusia,.kama alivyotuelezea huyo jamaa kutoka kijijini

Lakini tulipoziona hizo dawa tukakuta haziendani na hizo tulizozipata,…, ikabidi zitafutwe nyingine kwa haraka ili kuzibadili …nia ni kuhakikisha huyo mdada haligundui hilo kuwa tumezibadilisha, lakini cha muhimu ni kuwa tulishaupata ule mkoba na zile dawa zilishakuwa mikononi mwetu….

‘Hizo dawa zipoje…?’ nikauliza

‘Ni vidonge vidogo sana, vyeupe….sisi tulipovipata mtaalamu wa dawa akaitwa na kwenda kuvichunguza, ilikuwa ni swala la muda…ziligundulakana kuwa ni sumu inayoweza kumuua mtu kwa haraka sana, na ikipita saa moja huwezi kugundua kuwa mtu huyo kauwawa kwa sumu na huwezi  kugundua mtu huyo kauwawa na aina gani ya sumu, utakachogundua ni kuwa mtu huyo kapatwa na shinikizo la damu.

Sumu au aina hiyo ya dawa hutumiwa sana na majasusi wa kimataifa…kuwaua watu wao au kujiua pale anapokuwa kwenye hatari kama hataki kusema au kutoa siri!

‘Majususi wa kimtaifa …?’ tukauliza kwa mshangao

‘Ndio hivyo, ndio maana hatukutakiwa kuwaambia hili, ila kwa vile mumeonyesha uaminifu na mpo tayari kuliweka hili kama siri hadi hapo polisi watakapofanya uchunguzi wao, nimeona niwaambie tu…ili muwe na tahadhari hiyo na muache kupekenya pekenyua..ni hatari…’akasema.

‘Sasa ikawaje ….maana mpaka hapo angalau umetupa ahueni kuwa mdada hakuwahi kumeza hizo dawa…au sio…?.’tukasema

‘Hilo halikusaidia bado…kwani hatukuwa na uhakika…kuwa humo kwenye bahasha kulkuwa na dawa ngapi kabla, kwani huenda kuna moja alikuwa keshaichukua tayari kwa ajili ya kuitumia na kwa jinsi ilivyo ndogo anaweza hata kuiweka kwenye kucha zake ndefu, na ndivyo alivyofanya…..’akasema na sisi hapo tukaingiwa na wasi wasi tena…

‘ Tulipogundua hilo, kuwa hapo tunashughulika na mtandao wa kijasusi wa kimataifa, mimi pamoja  na utawala, haraka tuliwasiliana na polisi ,…kwani ilikuwa sio swala la kusubiria tena hata kama ni mgonjwa wetu lakini kwa hali hiyo ni muhimu kuchukua tahadhari zote, lolote laweza kutokea…

Polisi walipokuja cha kwanza ilikuwa kumkamata huyo jamaa kutoka kijijini ili kuisaida polisi , wao wanajua namna yao ya kulifuatilia swala kama hilo, tunachoshukuru jamaa aliweza kushirikiana na polisi vizuri sana, sasa hatujui ni kwa nia njema au ni moja ya mbinu zao..’akasema

‘Kwanini tena, kama aliamua kumuokoa mdada, na tena akakubali kushirikiana na polisi..?’ tukauliza

‘Hawa watu ni wajanja sana…anaweza kufanya hivyo kwa lengo maalumu, ndio maana polisi walihakikisha yupo nao hadi hapo uchunguzi wao ukamilike, anasema kundi hilo lina watu mpaka madakitari….’akasema

Wakati polis wanaendelea na uchunguzi wao kwa tahadhari , maana mdada hakutakiwa afahamu lolote hadi hapo ili kutokumuongezea shinikizo lolote la moyo,  sisi tukawa na mdada, sasa kwa tahadhari kubwa…

Huko polisi jamaa wa kijijini akawa anashirikiana na polisi,

Yeye alikiri kabisa kuwa hata yeye alikuwa mmoja wa kundi hilo, na kama angekuwa nia mbaya angeacha mdada ameze hicho kidonge lakini alishaamua nafsini mwake kujitoa kabia kwenye hilo kundi na kujitakasa na toba kwa mungu, na alikuwa tayari kufa kwa ajili ya kusaidia jamii, kwani kama alivyosema anajua uhai wake ni mfupi tu.

Kwahiyo ndugu zanguni maswala yote kwa hivi sasa yapo mikononi mwa polisi….’akamalizia hivyo

Sasa ikawaje kwa mdada…?’ tukamuuliza tukiwa na hamu ya kujua zaidi na kabla hajasema neno mara mlango ukagongwa na jamaa akaingia , kwa kumuangalia tu niligundua ni mtu usalama,

Je kuna nini kinandelea

….je mdada amekufa, au yupo hai, na nini kinachoendelea …

WAZO LA LEO ;


 Msaidie mwenzako wakati wa shida, hasa akiumwa, jibidishe kumsaidia kwa hali na mali kwani kwa kufanya hivyo unaweza kumuokoa na kifo…japokuwa kifo hakikimbiwi siku ikifika…Tusipende kusubiria mtu kafa ndio tunajazana msibani na kuchanga mapesa mengi tukijifanya tulikuwa tunampenda, hiyo haisaidii tena kwa marehemu.
Ni mimi: emu-three

No comments :