Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeMonday, March 14, 2016

SIKIO LA KUFA HALISIKII DAWA-18Baada ya kumaliza mazungmzo yangu na huyo mwenyeji wangu ambayo yalianza baada ya ubishi wangu nikitaka kusikia nini Yule jamaa wa kijijini alitaka kusema, na hasa alipotamka kuwa ni jambo linalomuhusu aliyekuwa mchumba wangu. Lakini hata hivyo mwenyeji wangu alikataa kata kata na kuanza kutunga story nyingine za kunidanganya, ….

Nakiri kuwa maongezi yangu na huyu mshauri, yalinipa faraja kubwa…na niliweza kukaa na kuwazia kuishi maisha hayo ya matumaini…..lakini dhamira ilinikaa sana moyoni….labda ni kutokana na tabia yangu, nikiamua jambo langu siambiliki,….na kwahiyo nilichokuja kukifanya baadaye , msione ajabu!

                                      ***********

Katika mazungumo yangu na Mwenyeji wangu yaliyochukua muda mwingi wa kumsikiliza yeye zaidi, kuninasihi…yeye akitumia ujuzi wake wote wa ushauri nasaha, siwezi kuyaandika yote aliyoniambia,…ila nakiri kuwa wakati mwingi alipokuwa akiongea nilikuwa kama simsikilizi, akili yangu ilikuwa ikitekwa na dhamira yangu

Dhamira…..ni lazima nitende nilichokusudia , hilo ndilo suluhisho…..

Mwishowe mshauri huyu, pale alipohakikisha kuwa nimeiva akaona sasa aseme ukweli, na hapo alianza kwa kuniuliza kama nipo tayari kuyapokea majibu ya vipimo vyangu;

‘Mimi nipo tayari….nimeshajiandaa tokea jana, nipo tayari kuyapokea hayo majibu ya vipimo vyangu, na kwa hali halisi,…na uhalisia, nilishayajua matokeo hayo yapoje kabla, na zaidi nilishaoteshwa, na nina uhakika ndoto yangu haijakosea…’nikasema na yeye akaniangalia kwa macho ya mshangao, lakini hakutaka kunidadisi zaidi kuhusu hiyo ndoto, akaendelea kusema;

‘Sawa unajua nikuambie kitu, sisi tunapotaka kutoa matokea ya vipimo kama hivi, hatuangalii kuwa mtu huyu kaathirika au la,….nia kwanza ni kuelimishana, uwe na tatizo hilo au la, kama nilivyokuambia awali,..kwani kama ulivyosikia maelezo yangu ya awali ilikuwa kukujenga kukulinda na kuja kukusaidia, …uwe au usiwe na tatizo hilo….’akasema

‘Na kwa vyovyote vile, matokea  hayana maana yoyote, chenye maana kwa yoyote Yule ni juhudi zake binafasi za kujisaidia kwa kula vyema,..kujilinda na maradhi, hasa maradhi ambukizi…., na ukumbuke wewe ni mpiganaji wa kuendeleza kizazi chako, ukishindwa leo, ina maana kizazi chako kimepotea, je upo tayari kukipoteza kizazi chako…?’ akaniuliza

‘Mungu mwenyewe ndiye anajua jibu la hilo swali lako…’nikasema

‘Mungu kakupa utashi wa kuamua hatima ya maisha yako,…ndio maana mpaka leo unapumua, kakupa utashi wa kuamua uishije ndio maana leo unaishi hivi kesho vile, ..kwahiyo kujua kwa mungu utaishije ni wewe mwenyewe kwanza ulivyojielekeza…na ndio maana kila mtu anatakiwa kuweka dhamira kuwa ataishije kwa vitendo na dhamira ya kweli,…ama kufa hayo ni mamlaka yake mola huwezi kuzuia….’akasema

‘Mimi nipo tayari, nilishasema awali,usiwe na shaka na hilo, maamuzi yanguniliyodhamiria  hayatarudi nyuma…usiwe na shaka kabisa.’nikasema

‘Haya mimi nakutolea majibu yako ambayo kama nilivyokuambia yanahitajia juhudi zako,yanahitajia utashi wako, tukishirikiana mimi na wewe utaishi vyema kabisa,…maana sasa umeshajifahamu mwenyewe ulivyo…’akasema

‘Sawa nambie usizidi kunichelewesha nipo tayari…’nikasema

‘Ni kweli kuwa katika vipimo vyako kuna viini hivyo vinavyoharibu kinga za mwili za kupambana na maradhi, lakini pia wamegundua kuwa mwili wako una nguvu ya kuweza kupambana navyo, kama utafuata ushauri utakaopewa wa lishe bora, na mengineyo kutokakwa mtaalamu yaani walikuwa na maana mimi….’akasema

‘Kwahiyo kwa kifupi mimi nimeathirika…au sio?’ nikauliza nikitaka uhakika zaidi

‘Wewe una matatizo ya upungufu wa kinga mwilini, hujafikia kile kiwango cha kusema umeathirika,…naomba unielewe hapo kidogo kuna namna ilivyo kwenye tatizo hili, madaraja, hatua…….’akasema

‘Swali langu hujanijibu, nimeathirika au sijaathirika, ninao au sina huo ugonjwa…?’ nikauliza na yeye akaniangalia kwa makini halafu akasema

‘Ndio unao..unalo hilo tatizo, lakini…sio kwa kiwango hicho….unaweza ukapona…ukifuata masharti na ukiishi kwa matumaini, zaidi ya hata Yule asiyekuwa na tatizo hili…’akasema

‘Hamna haja ya kukwepesha ukweli…haina haja, ya kuogopa kuniambia ukweli, nilishakuelewa, ..’Nikasema.

‘Mimi nilishayajua hayo mapema, ila swali langu jingine nataka uniambie wazi bila kunificha,je hilo tatizo jingine ninalo….?’ Nikauliza

‘Tatizo jingine lipi hilo tena..!!..Mmh,  ni hilo la kupungukiwa damu, mara kwa mara, unajua hujanielewa, haya matatizo mengine yanatokea kwasababu ya huo upungufu wa kinga mwilini, kinga zikipungua mwilini ,kila ugonjwa utakushambulia,..kwahiyo hilo tatizo jingine lipo, lakini ni kutokana na…’kabla hajamalizia nikasema

‘Mtaalamu wa nasaha, mimi nimeshakuelewa, ninachotaka ni uhakika…nimekuuliza hivyo nikiwa na maana yangu, je hili tatizo lipo au halipo, unatakiwa unijibu ndio au hapana, …samahani kama ninakosea, ama kwa maelezo umeshaniambia si ndio hivyo…utakuwa unarudia rudia tu,mimi nimeshasema nipo tayari…usijali’nikasema

‘Ndio hilo tatizo jingine pia limeonekana, lakini kwa hivi sasa hatuwezi kuwa na uhakika mpaka ukijifungua, kama alivyosema dakitari bingwa wa mambo hayo, amesema ukijifungua itakuwa ni nafasi nzuri ya kulijua vyema, na kupamabana nalo na mengine kama yatakuwepo, mara nyingi tatizo kama hilo  kwa mama linaweza likatokea na mara mama akijifungua linakwisha, na likabakia kwa mtoto…’akasema na nilijua anayasema hayo kwa kunitia moyo.

‘Sawa nimekuelewa docta mshauri, nafahamu hayo ni kunipa matumaini, au sio…kuishi kwa matumaini au sio….nimekuelewa….’nikasema na yeye akanitupia jicho la mashaka, halafu akasema

‘Kinachotakiwa kwanza ujifungue, ..na kujifungua huko kutafaywa kwa upasuaji, natumai hilo umeshaambiwa, haiwezekani kusubiria muda wa kujifungua kwa njia ya kawaida…sawa?’ akasema
‘Sawa,…’nikasema
‘Sasa ukashajifungua itakuwa ni kazi rahisi ya kupambana na tatizo hilo, madakitari wote bingwa wamesema wataweza kushirikiana kuhakikisha kuwa wanafanikiwa kupambana na hayo matatizo na wanasema hakuna shaka utafanikiwa…utapona, utakuwa kwenye hali nzuri tu. Usiwe na shaka na tatizo hilo wewe upo kwenye nafasi nzuri ya kupona…utakuja kutuambia,….walifika watu wana hali mbaya zaidi yako…lakini sasa hivi wapo kwenye shughuli zako….’akasema

‘Sawa najua hayo ulishaniambia…najua ni kunipa matumaini au sio…sawa tumuachie mungu..’nikasema kwa sauti ya upole

‘Hebu fikiria kwanza, madakitari wote mabingwa wa matatizo hayo, wameamua kujitolea kuhakikisha wanalimaiza tatizo hilo kwako na kwa mtoto, …uone jinsi gani ulivyo na bahati, mungu kawaelekeza watu hao watumie ujuzi wao wote kwako, ujuzi walijaliwa na mola wao, nina uhakika mola wako hatakutupa,…’akasema

‘Na iwe hivyo docta…’nikasema

‘Mimi nina imani kuwa mungu kakupa mitihani hii, ili wewe uwe njia ya kuja kusaidi wengine, uwe ushuhuda kwa wengine, sasa usije kuacha jukumu hilo, utakuwa umewasaliti wale wote wanaokutegemea, pambana kwa kujipa moyo, utashinda…’akazidi kuongea

‘Sawa na iwe hivyo…’nikasema

‘Muhimu na la kushukuru ni kuwa hilo tatizo jingine linaponyeka, kama lilivyo tatizo hili la upungufu wa kinga mwilini. Mwanzoni uliona watu wengi walipoteza maisha kwa hali mbaya kabisa…kwasababu watu waliangalia ponyo la gonjwa hilo zaidi….badala ya kinga, kitu ambacho hakikuwa sahihi, ilitakiwa kuangalia kinga, na kinga ni masharti yake…kama nilivyokuambia.

Hapo nikatikisa kichwa kukubali…

‘Ujue sote tuna madhaifu ya kinga, kutegemeana na utofauti wa mwili, kutegemeana na tabia za kuishi, lishe tunayokula…na hii ndio inaleta utofauti, kinachofanyika kwa hivi mtu akionekana kaathirika ni kufuata masharti , hasa ya kula….mazoezi nk….kama nilivyosema awali, na jingine ni kupambana na vile vitu vyenye kuleta maradhi ambukizi,, na hilo ni kwa kila mtu, uwe umeathirika au la…na siku zinavyozidi kwenda kinga nayo inaongezeka…’akatulia

‘Nimekuelewa….’nikasema

‘Kwahiyo nakuomba sana, na muhimu kufuata masharti, sasa hivi kuna viini lishe, kuna dawa mbadala zamiti shamba, …vyote hivi vimefanikiwa kupambana na maradhi hayo na mafanikio yake ni makubwa…katika maisha ya yoyote Yule uwe unaumwa au huumwi, ni kuishi kwa matumaini,  kuwa utaishi maisha marefu au sio…’akasema

‘Sawa kabisa…nashukuru mtaalamu nasaha…’nikasema na yeye akaniangalia kwa makini, halafu akasema

‘MIMI nimemaliza kama una maswali mengine naomba uniulize…’akasema na mimi nikakaaa kimia kwa muda, nikizama kwenye mawazo …

‘Kwa ujumla kutokana na nasaha zake, alishaniweka njia panda…nilianza kuyeyuka na kutaka kulisahau dhamira yangu, lakini sikutaka kusema lolote zaidi kwa muda huo, nikabakiwa na maswali yangu  kichwani;…

Ndio labda watafanikiwa nikazaa salama,…je maisha ya kawaida huko mbele yatakuwaje, je wataweza kunisaidia maisha yangu yote maana matatizo hayo ni ya kudumu,…nikajijibu kwa kusema sio rahisi, nikitoka hapa ni mimi na shida zangu.

Pili nitaishije, sina kazi, sina mtu wa kumtegemea, je watu hawa wapo tayari kuniapatia ajira, sizani na zaidi wanaweza kunifanya yaya wa nyumbani na mimi inavyoonekana nina damu ya kunguni, nitaishia kusakamwa zaidi…sitaki tena kunyanyaswa sasa nitaishije,…nitapata wapi pesa za kujikimu, na kumlea mwanangu…hakuna jinsi, dunia hii sio yangu tena

Nilijua kuwa kwa vyovyote iwavyo, mwisho wa siku watasema nitarudi kwa wazazi wangu, wazazi ambao hawana mbele wala nyuma, wazazi ambao walishawekeza maisha yao kwangu, wakijua mimi nitasoma , nitakuja kuwasadia, sasa kipo wapi, nitakuwa mzigo kwao, na majonzi ya kila siku….hapana sitaki kuja kuwa mzigo kwa yoyote yule

Niliyawazia hayo na mengine mengi, na mwishowe nikamuwazia mtoto ambaye kama angelizaliwa, najua atakuwa wa kuumwa umwa tu…, kutokana na matatizo hayo ya pili, huenda hatafikisha hata miaka miwili hili ni kutokana na maelezo ya wengi niliowaulizia, mtoto kama huyo atakuwa akiumwa na kuandamwa na upungufu wa damu..hilo ni tatizo, nitaishije kwenye hiyo hali, mtoto ataishije….dhamira ikaanza kuniteka akili

Sasa kwa hali hiyo ni nani atamuweza, kama mimi nitatangulia, …itakuwa ni shida, atanyanyaswa, atasimangwa na miaka yake hiyo mwili ya uhai itakuwa ni adha kwa watu….dhamira ikaanza kuniingia akilini….
Kesho,itasema…kesho….kesho…

Hiyo...kesho kila mtu atajua….

Kwahiyo hiyo kesho nawaomba nyie watu msishangae, nitakachoamua….

Nilipobakia peke yangu nilichukua mkoba wangu wa kike, humo nilikitafuta kile nilichokitaka, BAHASHA NDOGO,..ndani ya bahasha hiyo kulikuwa na tiketi yangu, tiketi ya kutimiza dhamira yangu….nikaiona na moyo mwili ukanisisimuka,…oh, sasa kesho itasema…

Niliifungua ile bahasha…lakini nikahisi tofauti, sijawahi kuifungua hii bahasha tangia nilipopewa, na nakumbuka ilifingwa vyema, sasa mbona ipo kama ilifunguliwa…labda kwa vile ilikaa muda bila kufunguliwa, lakini nilichokitaka nilikiona,…vipo sawa sawa, na hapo nikakumbuka ile sauti  siku ile..

‘Hii ndio kinga yenu, kama ukishikwa na polisi wakakutesa ili utaje siri la hili kundi, ili ututaje sisi kamwe usije kugeuka nyuma ukafanya hivyo ukatusaliti…
Ukitusaliti, sisi tutakuandama wewe na familia yako…tutaingamiza familia yako..kama huwapendi baba na mama yako ufanye hivyo, utusaliti…

Sasa ili  usipate taabu, kuliko kutoa siri ni bora ufe.., hiki ni kiapo,..na ujue kundi hili lina nguvu, kuna viona mbali, kuna watu wanatuona hadi sasa hivi kuwa tunafanya nini….sasa ili usije kuumia, kuzalilika, wewe unachukua hiki kidonge kimoja tu, unakitia chini ya ulimi, kikiyeyuka na wewe umeshayeyuka,….hutasumbuliwa tena, na hawatakuona tena….’
Nilipumua kwa nguvu….nikasema moyoni, sasa muda umefika…sitaki kusumbuliwa tena..

                                ***********

Kama nilivyowaambia awali kundi hilo kwa pale kijijini lilijulikana kama kundi la kuigiza, na wanakijiji wengi walikuwa wakilisifia, kwa jinsi walivyoweza kuigiza kwenye majukwaa na zaidi pale tulipoweza kutoa kanda za video, lakini miongoni mwao, wateule, walikuwa wakifanya zaidi ya hayo, kuna mengina hata mimi nilikuwa siyajui.

Mimi nilikuja kuingizwa kwenye baadhi ya mambo baada ya kugundua kanda za video kwenye kabati la mchumba wangu…..ndio yeye akaniambia hicho nilichogundua ni siri ambayo alisema natakiwa kuitunnza, nikiitoa sio tu nitaangamiza kundi, lakini hata mimi nitakuwa hatarani n familia yangu , baba na mama wataangamizwa..na mimi niliwapenda sana wazazi wangu licha ya yote yaliyotokea sikuwa tayari wazazi wangu wapate shida, wateswe au kuuwawa kwasababu yangu…kwahiyo hilo nikaliweka kuwa siri

‘Na nikuambie kitu, wewe uliwahi kushirikishwa bila kujijua,..unakumbuka siku ile ulipopoteza fahamu…ukila chakula, unafikiri ilikuwa nini, na ilitokea mara zaidi ya nne, na zote hizo ulishiriki na watu tofauti..na tulipata faida kubwa hukujua kilichoendelea…’akaniambia

‘Ina maana nyie mlinifanyia nini…’nilikasirika sana siku hiyo , lakini mpenzi alijua namna ya kunipooza, siku hiyo nilipewa pesa nyingi sana na zawadi nipeleke nyumbani…

‘Usiogope mpenzi, haya ndio maisha…usione watu wametajirika, watu wana magari, wanajenga mgorofa, ukazani ni mambo ya kihalali tu,..hapana kuna mambo mabaya yanafanyika, kukwepa kodi, wengine wanaua watoto wao, wengine wanafanya vitu kama hivi ambavyo kwa jamii ni vibaya lakini vina pesa nyingi ,…sisi hatu-ui watu, ila tunafanya biashara hii, unaona tofauti yake, ila mtu akituingilia, hatusiti kum-maliza…’akasema akipitisha kidole kooni halafu akainua moja ya kanda ya video.

‘Sasa hivi wewe ni malikia wa hapa kijijini, unaona unavyosifika, wewe ni muigizaji mashuhuri, yote hiyo ni kwasababu ya haya, kuna gharama zahitajika, kufanikisha haya yote, na hizo tunapata kwa  kuuza hizo kanda…hizo za hapa kijijini ni pesa ndogo tu, …pesa nyingi tunapata kwa njia hii…’akaonyesha hiyo kanda hewani, nilichokiona pale mbele ya ganda lake nilifunika macho.

‘Hahaha unafunika macho….wakati wewe mwenyewe upo humu..’akasema

‘Eti nini…’nikataka kuangalia akazuia…na kusema

‘Sasa kuanzia leo wewe ni mwanachama halali….ungeliendelea kuwa mwanachama usiyejua kinachoendelea, lakini kwa kimbelembele chako cha kuchunguza chunguza vitu vyangu, sasa wewe ni mwanachama hai, na ole wako uje kulisema hili, wazazi wako hutawaona tena, au watakuwa wakiteseka mpaka waombe kufa….’akaniambia sasa kwa sauti ya vitisho.

Kweli sikujua,…sikujua kuwa uchafu huo na sifa hizo ndizo zilizonipandisha kwenye kilele cha ujeuri, …nikawa siwasikii wazazi wangu, sifa zilizonilemaa, nikawa namsikiliza mchumba wangu tu,…oh…
Nilipofikia kuyawaza hayo, niliinama na kuanza kulia….nilitubu dhambi zangu…nikamlilia mola wangu, nikamuomba anisamehe……nikaomba kuwa hayo nilitenda kwa vile sikupenda kabisa wazazi wangu waje kuteseka…nililia kwa muda halafu nikatulia

‘Hata nikilia nitamlilia nani kwa hivi sasa, ..’nikajiuliza
‘Oh nakulilia wewe mola wangu , wewe ndiye unaiona roho na nafasi yangu, je kweli niliyafanya haya kwa utashi wangu….hapana sikujua kuwa walinifanyia ujanja, na kuniingiza kwenye mambo machafu bila kufahamu na nilipofahamu waliniweka kwenye vitisho ndio maana ilikuwa ni siri… mola wangu nisamahe…

‘Najua …...yote sasa sio siri tena yameshajulikana, najua yote sasa itabakia ni historia …lakini sitaki mtu aje kuninyoshea kidole tena kuwa ndiye huyu alifanya uchafu huo….sitaki kiumbe hiki kije kunyoshewa kidole na kuambiwa mama yako ndiye alifanya hivyo, sitaki yeye aje kuwa tunda la uchafu huo….hapana..hapana.. ama kwa wazazi wangu najua sasa wanaweza kulindwa….sijui…mungu atawalinda.’nikasema nikishika tumbo langu

‘Nilichokitaka nimekipata, …japokuwa sikupenda iwe hivi…sikutaka , na sikujua ni kwa njia hiyo, na sasa nimevikwa hii nishani,…..hapo nikakumbuka moja ya picha niliyowahi kuigiza  huko kijijini, nikiwa kama muigizaji mkuu….niliipenda sana hiyo video ndiyo iliyonipandisha chati na kuwa kama mrembo wa kijiji

Nakumbuka walikuwa wakiniita, malikia wa kijijini , ni kutokana na kazi hiyo, kwenye kazi hiyo niliigiza kama binti wa mkulima mmoja masikini, nikiwa shambani akapita mwana mfalme akiwinda akaniona na kwa uzuri wangu akanipenda, na haraka akamwambia baba yake kuwa hatimaye kampata mke, na ikatumwa watu kuja kwetu.

Watu hawa walituma madaraka yao na pesa, hawakutambua kuwa mimi name nilikuwa na utashi wangu,  mimi nilikuwa na mchumba wangu, niliyempenda sana kijana wa jirani yetu tuliyekulia naye..

Alikuja mwana wa mfalme akataka kumposa yeye, lakini mimi sikumtaka, sikutaka ufahari wa kuitwa malikia, kwani kulikuwa na mtu aliyekuwa mfalme wa  moyo wangu,…lakini mfalme , kiongozi wa utawala alikuwa na mamlaka, hakujali kitu alitaka kukidhi matakwa ya mwanae, kwani ni nani atakataa kuolewa na mwana wa mfalme, aje kuwa malkia baadaye….lakini mimi nilikataa

‘Niliigiza vizuri sana, na ni moja ya kazi zangu iliyonipatia umaarufu pale kijijii,…nakumbuka humo, ili kuonyesha dhamira yangu ya kweli kuwa sitaki kuolewa na mwana wa mfalme tulipanga nibebe mimba ya huyo kijana… hapo kuna kipindi kilipita cha malumbano, kuandamwa na mchumba wangu akisakamwa kwa hili na lile, na wazazi nao wakishurutushwa.
Na katika sehemu hizo ndipo nilionyesha ujuzi wangu wa hali ya juu, ni kipande hicho ndicho kilinifanya niitwe malikia wa mapenzi….hahaha, kumbe ni ulimbukeni!

Ni kwel mimba ikatunga, na siku ilipofikia kuwa natakiwa kwenda kufunga harusi na mtoto wa mfalme nikamwambia huyo mtoto wa mfalme kuwa nina mimba ya mchumba wangu wa zamani,…kijana Yule wa mfalme, akapandwa  na hasira akamwendea baba yake, …na wakajadili kuwa huyo mpenzi wangu auwawe..na hiyo mimba itolewe….

‘Kama mkimuuamchumba wangu  basi na wewe utaoa maiti yangu…’nikamwambia na yeye hakunielewa, akasema nitalindwa na nitaolewa na yeye nipende nisipende, na yeye ana uhakika huyo mchumba wangu akifa, nitamsahau na mimi ipo nitajirudi kwa kuwa nitakuja kuwa malikia wa nchi hiyo..

Na kweli mchumba wangu akachukuliwa kwenda kuuwawa…..na mimi huku nyuma nikatafuta sumu ya kujiua….

Ni wakati nawazo hayo ndio nikashituliwa na sauti ikisema ;

‘Wanasema inabidi ufanyie upasuaji…’sauti ilinishtua, na kujitoa kwenye lile dimbwi la mawazo, alikuwa sio  mwingine ila Yule mwenyeji wangu alikuwa kafika kunipa habari hiyo…

‘Watakavyoamua kwangu yote ni sawa…ila nahitajia siku mbili za kujiandaa..’nikasema

‘Siku mbili …kwanini siku mbili…kesho wanaona ndio siku muafaka,…na mimi nimewaambia sawa, leo watakuwekea damu, na kesho upasuaji huo utafanyika, …hiyo ni kwa manufaa yako na mtoto..’akazidi kusema

‘Kesho……sawa kesho…’nikasema kama vile mtu yupo ndani ya ndoto

‘Ndio kesho, ila wanachotaka ni wewe kutuliza kichwa ili kukwepa shinikizo la moyo…’akasema

‘Sina shinikizo la moyo, nipo tayari kwa lolote lile..’nikasema na menyeji wangu akaniangalia kwa macho yenye udadisi…halafu akasema

‘Nikuambie kitu kuna wengi walikuwa kama wewe, na walifikia hata kutaka kujiua, lakini baadaye waliamua, wakatuliza kichwa wakajitambua,..sasa wanaishi na watoto wao..kwa matumaini…ni lazima na wewe ufanye hivyo..’akasema na nilishtuka alipotamka neno kujiua..

‘Ni kweli, lakini sizani kama walikuwa na tatizo kama hili langu, tatizo la kusubiria miaka miwili, ukiombea miaka miwili ipite ndio uwe na uhakika wa maisha, na utakuwa kila muda unaishi kwa kuongezewa damu, tatizo juu ya tatizo,…sizani kama kati yao kulikuwa na mmoja, mwenye tatizo  kama mimi….’nikasema

‘Walikuwepo wenye matatizo mabaya zaidi ya hilo..lakini matatizo kama hayo yanatokea kwasababu ya upungufu wa kinga kama nilivyokuambia, lakini dawa za kuongeza nguvu za kinga hizo husaidia kupambana na hilo tatizo, na jingine kubwa ni kutliza akili, ukalikabili lile tatizo kwa moyo mmoja,….’akasema

‘Nilimekuelewa…..’nikasema nikihema.

‘Lakini mbona ghafla umebadilika, sio hali ile uliyokuwa nayo mchana..’akasema

‘Hapana usijali mimi nipo sawa,ni kuchoka tu…’nikasema na mara nikamuona akiangalia ule mkoba wangu wa kike,nikajiuliza kwanini anauangalia, sikuwa na zaidi cha kufikiria, labda ni kwa vile kauona upo karibu name.

‘Kwanini unaweka mikoba kitandani, kuna kitu unakitafuta nikusaidie…?’ akauliza

‘Hapana..kuna kitu nilikuwa nakitafuta, hamna shida,..nitauweka, usiwe na shaka…’nikasema na yeye akaondoka akionyesha wasiwasi...

Na mimi moyoni nikasema kesho itakuwa siku nyingine,..kesho watamkuta Yule mrembo wa runinga aliyetakiwa kuolewa na mwana wa mfalme…na walipomuua, mpenzi wake, na yeye akajiua, …na harusi ya mrembo na mwana wa masikini ikaja kufanyika ahera..nilikumbuka hiyo picha huku michirizi ya machozi ikishuka shavuni

                                               *******

Siku kabla ya kufanyiwa upasuaji, ndipo niliazima simu yenye mtandao, nikakesha nikiandika yote haya niliyowatumia, niliandika kwa kifupi kifupi, lakini nafaham mwandisha atajua jinsi ya kuependesha…nilifanya hivyo kabla ya kutimiza dhamira yangu…, nilichukua muda wa kulitafakari hilo na hatimaye niliona hakuna jinsi, ni lazima nichague maoja kati ya mawili;

‘Nitimize matakwa ya dhamira yangu …ili niweze kupumzika..na taabu hizi za dunia

‘Au niishi kwa matumaini...huku nikiteseka na kudhalilika…’

 Mpaka muda huo naanza kuandika haya ….nilikuwa sijafikia muafaka….dhamira ilinisuta na nafsi ya matumaini ikawa inaniteka moyo wangu…

Niliandika nikijua mchumba wangu atakuja kuyasoma …..sikuwa na ufahamu zaidi ya kujua anaumwa, lakini sikumuweka kwenye kundi la kufa..huwezi kumdhania mwenzako kufa hata kama unamchukia.

Ila kule kunong’onezana mshauri nasaha na jamaa wa huko kijijini kulinifanya nifikirie vinginevyo na nilipowauliza ndio wakatafuta stori nyingine ya uwongo , nilijua ni ya uwongo..

Huyu mshauri nasaha aliniambia eti, huyo mchumba wangu amekubali kujiunga na kundi la matumaini na sasa anaendelea vyema, na mimi ni bora nitulie hata kama itaonekana nina matatizo basi nijiunga na kundi hili nikiwa nimeshajifungua ili niweze kuwaelimisha watu

Mimi niliwajibu; ‘Sizani kama ni kweli…, na kama ni kweli mimi sihitaji kukutana naye…na sizani kama anaweza kukutana nami tena….’nilisema hayo nikiwa sijali lolote hata kama amekufa kwangu mimi haikuwa na maana tena.

‘Kwanini unasema hivyo!..., huwezi jua mnaweza mkalewana vyema tena, mkaishi pamoja….’akasema

‘Sijui…’mimi nikasema

‘Haya wewe tuliza kichwa chako wala usiyawazie hayo,  hata mimi nimeona hayana umuhimu kwako, muhimu kwako ni wewe tu kujiandaa….’akasema na huyo jamaa kutoka kijijini akasema;

‘Ndio hivyo, nilitaka kumwambia, ila sikupenda muonane mpaka wewe mwenyewe uridhie…akukute ukiwa umeshabadilika na kuwa mtu mwingine moyo umuume….’akasema

Niliona nisiendelee kuwang’anga’ania, kwani niliiona story hiyo kama ni ya uwongo, kwa muda ule niliiona kama ni story  ya kutunga tu ili kunifanya nisiwaze zaidi, nikakubali yaishe.

Nilikubali yaishe, japokuwa nilikuwa sijaelewa ni nini kimempata huyo aliyekuwa mpenzi wangu, japo nilimuuliza huyu niliyekuwa nikiwasiliana naye kwenye mtandao, lakini yeye anasema hajawahi kumuona huyo mchumba wangu ,

‘Sina habari zaidi za kwake,…kwa mara ya mwisho nilisikia mke kamkimbia na yeye hali ni mbaya, .. ngoja nifuatilie…’akaandikiwa hivyo na baadaye akapokea ujumbe ukisema.
‘Huenda keshafariki….ila haijathibitishwa…wanafamilia hawajaweka wazi sijui kwanini….’aliandika maneno hayo baadaye na mimi moyoni nikasema
‘Kama keshafariki ni heri tu, tutakutana huko mbele ya mola huko atakwenda kujibu mashitaka …’ sikuwa na mshituko wowote….nikawa najiandaa kutimiza dhamira yangu.

                                          *****
Kabla sijaamua lipi nifanye kwanza, nilifumba macho na kuanza kumuomba mola wangu…. Aniongoze njia nichukue uamuzi ulio sahihi, Na nilipomaliza kuomba nikaanza kuyaandika haya ya mwishoni lakini kwa muda huo kidole kilishachoka kuandika, mnisamehe;

Nawaomba nyote mnisamehe..hasa wazazi wangu, kwani wao ndio niliowakosea sana, sikuweza kuwasikia, nawaomba wanielewe,ili nisiishie kwenye moto mkali wa jahanamu….lakini wazazi wangu waelewe kuwa dunia ya sasa imemejaa mitihani ya shinikizo la utandawazi, vishawishi sasa vipo vingi sana sio sawa na zama zao, nilipoingizwa kwenye huo ushawishi, sikuwa na ufahamu zadi, nilijua ndivyo ilivyo, kama walivyofanikiwa wengine…sikuelewa..

Nawashangaa sana hawa washawishi kwani siri waliyosema tuifiche,mimi nilijitahidi sana kufanya hivyo, hata maelezo yangu ya awali hakuna sehemu niliyowahi kuielezea wote ni mashahidi zangu..  wao ndio wa kwanza kuifichua….!

‘Unajua mimi toka udogoni nilipendelea sana kuangalia kanda za video, na nilipowaona waigizaji wazuri, warembo,wameinukia na kuwa matajiri, niliwazia na mimi niwe kama wao,na ilipotokea nafasi hiyo nikajua huo ndio mwanzo,…oh, kumbe …kumbe, masikini, kweli masikini haokoti, kweli….nimekuwa sikio la kufa… nikaingia kwenye mtego wao,  waliniambia hayo mengine hufanyika kwa siri hata hao huwa wanafanya ila ni kwa siri..

Mungu wangu nakuomba unisamehe …..’ nilitulia nikiwaza kuwa hayo ndio maneno ya mwishi kabla ya uamuzi, lakini baadaye nikapata nguvu na kuanza kuyaandika haya;

                                            **********

Nawaombeni nyote mlione tukio hili kama fundisho kwenu,…msije kuhadaika kama mimi, kila jambo mlionalo hapa duniani liangalieni kwa macho mawili, viapizo vya mambo machafu havina maana ni uwongo, ushirikina nk, ni uwongo,…kutapeli, kuhadaa wenzako ili ufanikiwe upate cheo, … utajiri wa namna hiyo ni wa muda mfupi tu utaishi nao kwa mashaka tu , na mwisho wake utadhalilika, utakufa kwa aibu …..wao wapo wapi sasa….walikuwepo kama hao, hivi sasa wapo wapi…

Labda mtaona mimi ni fungu la kukosa lakini haya….ila ninachowamba nyote, mniombee mola anisamehe, msiangalie machafu yangu tu mkanibeza, kuwa nimejitakia mwenyewe, kuwa mimi nilikuwa sikiola kufa…sikuwa muangalifu, lakini oneni nilipotoka, haya yanaweza kukuta hata wewe au kizazi chako, naombeni sana myaangalie haya kuweni makini na huu utandawazi, labda mimi akili yangu ya kuona iliishia hapo, haya na wewe ipambanue…

Nashukuru pia, pamoja na utukutu wangu, lakini nilikuwa binti ninayependa kuwasaidia watu, kuwasaidia watoto hasa mayatima, hasa wanyonge,nilikuwa najitolea kwenda kusomesha shule za chekechea za mayatima, nilipenda pia kuwa mwalimu,  japo nilitekwa sana kuwa muigizaji…pia nilikuwa napenda sana kuwasaidia majirani,…sifa hizo na nyingine ziwe kwenye toba zenu mkiniombea…

Najua hata mimi natakiwa kujiombea sana, basi mola kwa kutumia hayo machache ya wema niliyofanya,unisaidie, ama kwa kufika huko mbele yako mapema, au ….vyovyote uonavyo ni heri kwangu, ila hapa nilipo akili imechoka, sina jingine zaidi , zaidi ni kutimiza dhamira yangu,….

Oooh mola wangu nakuomba usiniache nikateketea kabisa, nakuomba kutokana na mema hayo machache,  uniangalia kwa jicho la huruma unisaidie,…sijui kama naweza kuishi tena,…ila wewe ndiye ujuaye zaidi….ila kama nitakuwa kwenye mitihani zaidi , nikateseka na magonjwa haya naomba aichukue roho yangu haraha mimi na mwanangu,…

Na kama mema hayo yanaweza kunisaidia, yakanikwepesha na mitihani hiyo ya magonjwa , na magonjwa hayo yakaponyeka, na kuondoka, basi naomba unipe njia sahihi, kwa kadri upendavyo…

Ni kweli kila mtu ana tamani kuishi sana, lakini kama uhai utakuwa kwenye mateso kama haya mimi sitaweza kuvumilia tena….nimechoka mola wangu, nakuomba unisaidie mola wangu, ,..Nifanikishe dhamira yangu na isiwe sababu ya kuniingiza kwenye huo moto mkali,…bali iwe saabbu ya kunipumzisha na mateso haya,…najua ni kosa , lakini nifanyeje mola wangu….

‘Nifanyeje mola wangu….! ‘ hapo nilitulia kwa muda kwani sikuweza kuvumilia, nililia sana…lakini nikagundua muda umepita

Hapa nashindwa hata kuandika zaidi, nimechoka, mwili umeanza kuchoka,… machozi yanazidi kunimiminika, macho yamekuwa mazito sijui ni kwasababu ya usingizi….lakini najua mengi mtaandikiwa, mimi naishia hapa….

Ila kabla sijawaaga naomba msije kunifuatilia,…. hamtakuta kitu zaidi ya kaburi langu, naishia hapa na kusema kwaherini wapendwa wangu, nawapenda sana….
Muda umefika wa kutimiza dhamira yangu,… ninachukua kidonge hiki kwa uchungu japo dunia naitamani…hata hivyo ni lazima nikimeze ili niweze kuyasahau haya mchungu yote…ngoja nifanye haraka maana nasikia mtu anakuja, kwaherini…..

                                                 MWISHO

Hapo ndio ilikuwa mwisho wa maelezo yake…

         ************

Sehemu hiyo ya kwanza iliishia hapo, kutokana na melezo ya muhusika mwenyewe hivyo ndivyo yalivyotufikia, sasa Maelezo mengine yatakayo fuata,ambayo yatakuwa kama hitimisho, yanatokana na uchunguzi tuliokuja kuufanya baadaye  tulipojaribu kufuatilia tukio hilo. 

Uchunguzi wetu ulianzia hapo hospitalini alipokuwa amelazwa huyo mdada, japo hatukuwahi kumkuta….

Swali je ilikuwaje....je ilitokea nini….ni sehemu nyingine ya kisa hiki..

Tuzidi kuombeana heri mola atufungulia njia za heri

WAZO LA LEO: MACHUNGU na RAHA, yote ni majaliwa ya mola wetu! Ukipata RAHA leo usisahau kumshukuru mola wako, kwani yeye ndiye mpaji wa yote na wala usijione kuwa wewe ni mjanja sana kuwazidi wasio nacho, muhumu jitahidi kuwasidia wale waliopo chini yako, kwa hali na mali, kwani kwa kufanya hivyo unajiongezea baraka, na wala usiwasimange na kuwaona wao ni wajinga,….Kumbuka kuna kupata na kukosa.

Na halikadhalika ukipata mitihani, shida zikakuandama usione kama umeonewa, huenda kwa kuzipata hizo shida, mitihani hiyo ya maisha ni namna nyingine ya kukufanya uvuke hatua, na kupanda daraja la juu zaidi, cha muhimu  usikate tamaa, unachotakiwa ni kuzidi kuwajibika, kujibidisha, huku ukimuomba mola wako, ipo siku utafanikiwa.
 Tupo pamoja
          Ahsanteni
Ni mimi: emu-three

No comments :