Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Friday, March 11, 2016

SIKIO LA KUFA HALISIKII DAWA-17




 Ilikuwa kama ndoto, sikuwa na uhakika, ila nakumbuka siku ile nilipozindukana walikuja madakitari wale wawili , kwanza walipofika walisimama wakiangalia ile mashine ya ukutani inayoonyesha mapigo yangu ya moyo, hawakuwa na haraka, wakawa wameinama kwenye meza wakiongea jambo karibu na kitanda changu,…

Mimi nikawa sasa nimezindukana vyema, na wao sasa kwa haraka wakanisogelea na kuanza shughuli zao za kuondoa vifaa walivyokuwa wameniwekea mwilini

Sina uhakika sana kama ni wao walikuwa wakiongea au niliyaona hayo kwenye njozi, lakini kuna maongezi ya watu, walikuwa wajibishana au kuelezana, nikijaribu kuyakumbuka hayo maongezi lakini kwa muda ule ilikuwa vigumu kuyakumbuka

Akili yangu iliingiwa na hamasa ya kuyakumbuka hayo maongezi, na hadi nikataka kuwauliza hao madakitari kama ni wao walikuwa wakiongea au ilikuwa ni ndoto tu lakini kwa muda ule sikuwa na sauti, koo lilikauka, na wao walikuwa wakiongea mambo yao mengine,

‘Huenda nilikuwa naota tu..’nikasema kimoyo moyo,

Kama ni kweli, nilikuwa naota au ni mazingumzo niliyoyasikia, lakini moyoni nilishajipa uhakika kuwa na mimi nimeathirika, na pamoja na hayo nina tatizo jingine kubwa , tatizo ambalo linanifanya nisiwe na uhakika wa kuishi tena mimi na mtoto wangu, ni swala muda tu.

‘Nitajua tu..’nikajipa moyo, na kiukweli kwa hivi sasa nilitaka kujua kila kitu, nilikuwa tayari kwa lolote lile.

‘Ni lazima waniambie, sitaki kufichwa tena….’nikasema

Wale madakitari waliendelea kuondoa vifaa na kuniweka sawa, huku wakiongea

‘Sasa naona yupo safi keshazindukana vyema…hana tatizo lolote….’akasema mwenzake akinikagua machoni.

‘Ok,…. natumai tunaweza kumtoa huku chumba cha wagonjwa mahututi , …’akasema mwenzake.

‘Ni kweli haina haja ya yeye kuendelea kukaa chumba hikiwakati hali yake imeshatengamaa, na mimi nimechoka nataka nikajipumzishe kidogo,…ila bado anahitajia uangalizi wa karibu…inabidi kuwaagiza manesi wafanye jazi hiyo…’akasema mwenzake

‘Lakini hili tatizo la kupungukiwa damu linahitajia uchunguzi wa kina..’akasema

‘Hilo jukumu sasa tutamuachia docta wa mambo hayo….na yule mwenyeji wake yupo wapi, maana nilimuona…ni muhimu aruhusiwe kuongea na mgonjwa wake…..’akasema na wakawa wameshamaliza kuniondoa vile vifaa wakaniuliza najisikiaje nikawaambia

‘Mimi hata sijielewi,ila najiona nipo salama….’nikasema

‘Upo salama usijali,….ni hali ya kawaida, tu, sasa tunakutoa humu unakwenda wodini kwenye vyumba vya kawaida, usijali …’akasema huyo dakitari

‘Kwani kulitokea nini….?’ Nikawauliza japokuwa akili ilishakaa vyema lakini nilikuwa sikumbuki vyema

‘Ulipoteza fahamu kidogo…,nahisi kuna mshituko ulikupata,….’akasema

‘Kwanini inatokea hivyo, ….?’ Nikauliza

‘Ni kawaida,….itaisha tu, kwani tatizo kama hili huko nyuma huwa linakutokea mara kwa mara..?’ akaniuliza

‘Lilianza kipindi hiki nikiwa mjamnzito, sijui ni kwanini….’nikasema

‘Mhh…inatokea, ila kwa vile imechanganyika na matatizo mengine….lakini itaisha tu,pamoja na hayo naona bado unaendelea kusumbuliwa na tatizo la upungufu wa damu, …na hili tatizo inabidi tulichunguze vyema tuone ni kwanini inatokea hivyo…..tukifanya uchunguzi wake itakuwa rashisi kupata matibabu stahiki…’akasema

‘Ina maana damu  yangu imepungua tena…?’ nikauliza kwa mshangao

‘Ndio lakini kwanza tunajaribu kuangalia ni sababu gani inayosababisha hilo..’akasema docta, na hapo nikakumbuka yale niliyoyasikia,…. niliyasikia kama ndoto…au watu wakiongea wakiulizana.. huenda ni wao walikuwa wakiongea,….lakini bado nilikuwa sina uhakika.

‘Vipimo vyake vinaonyesha una upungufu wa damu tana…inashangaza sana maana karibuni tulimuongezea damu, japokuwa haikuwa nyingi, lakini tulijua kiasi hicho kitaongezewa na vyakula…’nilisikia sauti hiyo

‘Kama nilivyokuambia, huyu ana tatizo la seli ….’hilo neno sikulisikia vyema, ila neno cell, nililisikia, …

‘Kwa umri kama huu, haiwezekani..’sauti nyingine ikasema

‘Inawezekana…kutokana na tatizo alilo nalo la upungufu wa kinga mwilini…’sauti nyingine ikasema

‘Mhh, yawezekana, na uwezekano mkubwa tatizo hilo litakuwa na kwa mtoto pia…’sauti ikasema

‘Uwezekano huo ni mkubwa,…. na kwa vile hali hii imegundulikana kipindi hiki , sijui kama tunaweza kumsaidia,….ilitakiwa pale ilipojulikana ana ujauzito, ndio tungeliweza kuidhibiti hii hali japokuwa kwa mtoto, …sijui…’sauti ikasema

‘Mimi nahisi alikuwa na tatizo hilo udogoni, …. lakini haikuwa na nguvu, au…yawezekana ameambukizwa,au….inashangaza kidogo,..hili tutamwambia docta anayehusika na mambo haya atupatie ufafanuzi…kwa hivi sasa tupambane na hili …’sauti ikasema

‘Muhimu tuangalia uwezekano wa yeye kujifungua,….maana kama ataendelea hivi, hataweza kujifungua kwa njia ya kawaida..na atazidi kuteseka,..’sauti ikasema

‘Lakini..hata hivyo kwa hali hii ya upunfu wa damu hatuwezi kumfanyia upasuaji,..mpaka damu iwe sawa sawa…mimi naona tumuongezee damu ili upasuaji huo uwezekane….’sauti ikasema

‘Ni bora tuangalie kwa leo kwanza, kwa kiasi hiki tulichomuongezea, na dakitarii huyo akija anaweza kutupa ushauri zaidii,…wasi wasi wangu hata tukimfanyia na mtoto akitoka salama, bado nina mashaka na huyo mtoto,…kwa tatizo kama hili, kama litakuwa kwa mtoto,sizani kama mtoto atakuwa na maisha marefu..’sauti ikasema

‘Ngoja tuone kwa leo…hayo tusubirie huyo mtaalamu wa fani hii….tusiumize kichwa, …...’sauti ikasema …

Nahisi ni watu walikuwa wakiongea kipindi nikiwa sijazindukana vyema….

                             ***********

Nilihamishiwa kwenye wodi za kawaida, na muda huo niliambiwa mwenyeji wangu anakuja kuniona,..nikawa namsubiria, lakini kabla mwenyeji wangu hajatokea mara akaingia Yule jamaa wa kule kijijini,…alionekana hana raha, sijui ni kutokana na haya yaliyotokea kwangu au alikuwa na jambo jingine.

‘Vipi unaendeleaje,…samahani sana kwa ..uzembe wangu,  kiukweli sikujua na…oh,nilishituka sana, ulipopoteza fahamu..nilijilaumu kwanini nilikuambia mambo mengi ambayo yamekushtua hivyo, sikuwa nimefahamu  …’akaanza kujitetea

‘Hapana usijali, nashukuru hata hivyo, kwani nimeweza kujua kinachoendelea ,  na kwa kwa hilo nimepata ujasiri sasa, na kwa hivi sasa nipo tayari kusikia lolote lile…’nikasema

‘Hapana kwa hali yako hiyo unahitajika kupumzika,..usiwe na mawazo mengine…unahitajia muda kurejesha afya yako, mimi nimepita mara moja, nilikuwa namtafuta Yule mwenyeji wako…’akasema

‘Ndiye namsubiria, anakuja….usijali mimi kwa hivi sasa mimi nipo tayari kusikia lolote, na akija huyo mwenyeji wangu nataka awaambie hao madakitari wanipe vipimo vyangu nijitambue kabisa, najue yeye atataka kunificha, lakini sitaki tena kusubiria….’nikasema

‘Ningekushauri usibirie kwanza…hata hivyo mbona huna tatizo kubwa, kama lingekuwepo wasingekusubirisha hivyo, wewe yuliza kichwa chako kwanza….’akasema

‘Hia haja…mimi mwenyewe nimeshajijua, ….nahisi kama niliota,..lakini nahisi nimeathirika….ninao huo ugonjwa,…na zaidi ya hayo nina hilo tatizo jingine..uhakika huo ninao kwa sasa….’nikasema

‘Hujaathirika dada …kwasaabbu nijuavyo mimi akina mama wajawazito wanapimwa mapema, na wewe ungelishajijua …wangelishakuambia hilo mapema ili uchukue tahadhari na wangetakiw akukupa dawa za kukusaidia, na kama hawakukuambia mapema ina maana huna tatizo…’akasema

‘Nahisi waliechelea kuniambia, wakiogopa hali yangu, kwani tangu awali nimekuwa ni mtu wa kushituka na kupoteza fahamu..na hili la kuniambia mtoto kakaa vibaya nahisi ilikuwa ni mbinu ya kunificha jambo…ili niweze kufika sehemu ya wataalamu zaidi, tatizo ikawa hali ya uchumi…..nauli na….sijui kwanini walinichelewesha hivyo, labda walijua sitaishi ….’nikasema

‘Hapana wala usiwaze hivyo, mimi ningekushauri sana uwasikilize madakitari wanachokushauri, wao wanajua zaidi…na ukijiwazia mabaya, unazidi kujiumiza zaidi, ..jipe moyo  kuwa huna ili mungu akujalie ujifungue salama, …maana hapo ulipo unapambana na mawili, wewe na mtoto..’akasema

‘Mtoto mwenyewe ataishi basi…..’nikasema nikijaribu kuangalia tumboni,…nikajitahidi kuondoa mawazo ya huzuni ili nisijiweke kwenye hali tete tena.

‘Kwanini unasema hivyo…?’ akauliza

‘Kama ulivyosema awali kuwa…., ndugu yako alikwua na tatizo akizaa mtoto hadumu, anafariki kabla hata hajafikia miaka miwili wakasema ana tatizo la cell, …na mimi nahisi kaniumbukiza…’nikasema

‘Lakini huna uhakika na hilo..na sio lazima,…..mimi naona usiyawazie hayo kabisa, …ngoja niende nikaonane na huyo mwenyeji wako, ninachokuomba kwa hivi sasa ni kuweka mawazo ya kwa mungu,…mungu ndiye atakuwa msaada wako mkubwa, na ujue kabisa magonjwa, shida ni sehemu ya mitihani, yakubali na na kubali kuwa yana mwisho , utapona, …na kupona kwako ni udhabiti wako wa nafsi, usijinyongeshe…na kwa hivi sasa ni bora upumzike kwanza….’akasema akitaka kuondoka.

‘Usiwe na haraka…mwenyeji wangu atakuja hapa kaa tuongee, haiwezi kutokea tena,..hilo nakuhakikishia, ikitokea ujue ndio safari yangu, na safari yangu nimeshaiona kwenye ndoto…sina muda wa kuishi tena, nimeshachoka,..haya hivyo nataka kujua kila kitu…kwanza nimeshajua kuwa nimeathirika, ….na zaidi nina hilo tatizo jingine ambalo linanifanya nijue kuwa mimi sina maana tena hapa duniani….’nikasema

‘Hapana, huwezi kujua hilo mpaka mtoto azaliwe na mara nyingi anayekuwa na matatizo hayo anakuwa ni mtoto sio mama…huenda ukahisi hiyo hali, …lakini ni ya kupita tu ,ukijifungua hali itakuwa vyema…na hata mtoto akibahatika akavuka miaka zaidi  ya miwili anakuwa keshaepukana na ugonjwa huo, mbona imetokea,..na utaalamu siku hizi upo muhimu kama nilivyokuambia ni kufuata masharti….’akasema

‘Mimi nimeathirika hilo sina shaka nalo…waniambie wasiniambie nimeshajifahamu na ni lazima waniambie… kama mchumba wangu alikuwa nao, na huyo kaka yako mshenzi …..japokuwa keshafariki lakini ….tutakutana huko ahera, ana kesi ya kujibu…..’nikatulia na mdogo mtu akawa kainama akionyesha machungu.

‘Wote hao, na hata huyo mchumba wangu ndiye kabisa, sijui kama nitamsamehe kwa hili…najua ni vyema kusameheana, lakini …..kwanini wakanifanya hivi….unajua niikuwa najiuliza ni nini kilitokea hadi nikatembea na hao wanaume wote, nimekumbuka….’nikasema

‘Achana na hayo shemeji , usiyaongee hayo tena…’akasema

‘Haina haja…nakuambia  wewe kwani wastahili kufahamu na hata ukikutana na huyo mchumba wangu mwambie kabisa aliyonifanyia,….kuniingiza kwenye madhambi nisiyostahiki nayo ana dhmabi kubwa mbele ya mungu….’nikasema

‘Msamehe,….anastahiki msamaha wako,ili…’akatulia

‘Msamaha wangu ataupata, sawa, mimi nimeshamsamehe, lakini hiki kiumbe je,…kina makosa gani,..yeye ni nani atamuhurumia, …kaingizwa kwenye shida kutokana na tamaa za watu wengine,…walitaka mali,haya walipata sasa wamefika wapi….’nikasema

‘Mimi najua tatizo hilo sikuwa nalo, sijawahi kusikia kwenye familia yetu wakiliongelea hilo, nina uhakika limetokana na huyo kaka yako…siku waliponiwekea madawa, na kuigiza mapicha yao, bila ufahamu wangu…najua hakuna atayenielewa hilo…’nikatulia

‘Hayo yamepita shemeji mimi naona usiyawazie hayo tena…’akasema

‘Ni lazima niwaze maana nilitaka kujua ni kwanini niweze kutemeba na hao wanaume wte, wakati mchumba wangu alikuwepo…ni yeye aliniruhusu…yawezekana ni yeye aliniruhusu kwa tamaa zake, au wenzake walimzunguka, ila nina uhakika nilitembea nao…niliwahi kuiona hiyo video, sikuwa nimelazimishwa inaonekana kabisa niki….kwa hiari yangu kabisa..’nikasema

‘Hayo madawa hukutoa akili kabisa…nafahamu,lakini usiyawazia sana….achana nayo, mbona huyo mwenyeji wako anachelewa kuja….’akasema

‘Mimi nimeshajifahamu …sitaishi muda mrefu, maana hayo  madhara ya ugonjwa huo mwingine, yamehamia kwangu kutokana na upungufu wa kinga mwilini, sina kinga za kuzuia, mimi na mtoto sote tupo hatarini, nahisi hivyo….na hio la kusema tatizo hilo litaondoka pale nitakapojifungua ni kudanganya tu, kwani wanawake waliowahi kuzaa na huyo kaka yako waliishi ,si walikufa wote,..’akasema

‘Nani kakuambia hayo…shemeji achana na hayo, usiyawazie hayo zaidi, huyo mwenyeji wako yupo wapi?’ akauliza akionyesha wasiwasi.

‘Nimeyasikia…hahaha, nani asiye yajaua, yeye alidanganya kuwa walipata ajali,mwingine alifariki kwakuumwa tu, akijifungua….ila ufunuo huo nimeupata kwenye njozi, mimi sina muda mrafu wa kuishi....na namuomba mungu hicho kiumbe chake kisitoke hai kisije kupata haya mateso ya dunia…ndio maana naimeingiwa na shauku moja,….’nikasema

‘Shauku gani….?’ Akaniuliza akionyesha mashaka

‘Nakumbuka wakati tunapeana viapo…tuliambizana kuwa ikitokea kushikwa na askari ikabidi kutajana ni bora unwe ile sumu…ili uachana na mateso ya polisi,…’nikasema

‘Wewe unawaza nini tena….’akasema sasa akionyesha wasiwasi wa dhahiri

‘Nakuambia wewe kama mtu uliyenifunulia ukweli nataka hii iwe siri kwako,….nakusudia kufanya hivyo,….’nikasema

‘Hapana, hapana, usifanya hivyo, tafadhali….’akasema

‘Yote yategemea  jambo moja….’nikasema

‘Jambo gani….?’ Akaniuliza

‘Ukweli halisi wa vipimo….’nikasema

‘Lakini huna matatizo….’akasema


‘Kama wataendelea kunificha hivyo, ndio sitachukua muda kutimiza maamuzi yangu…ni bora waniambie ukweli haraka, ili nisiendelee kuwapa shida….’nikasema

‘Umevunja mungu, nilitaka wewe uwe mmoja wa watu tutakaoungana pamoja kupambana na haya matatizo tuwaelimishe wanajamii…kwa nini ukate tamaa huoni mimi nipo pouwa kabisa….’akasema

‘Wewe upo pouwa,..wewe ni mwanaume, wewe hutaraji kushika mimba….wewe…lakini mimi hapa nilipo nimekalia kuti kavu, nina mimba, natarajia kuzaa kusicho riziki, maana hata nikijifungua salama, mtoto huyo hatadumu,…namuona mtoto huyo kama marehemu, hata mimi mwenyewe sio wa kuishi muda mrafu kwanini niwapatishe watu shida…..’nikatulia

‘Lakini kwanini uwe na mawazo hayo mafupi,..?’ akauliza

‘Mimi kama mama nampenda sana  mwanangu, miezi tisa ya mateso, ni ushahidi tosha, wa mapenzi ya mama kwa mtoto, nilitarajia nimbebe mwanangu anyonye ziwa, alie, nimbembeleze, lakini fursa hiyo sitaipata tena, yatakuwa maisha gani ya huzuni na kulia, maisha ya mateso, siwezi kuiona hiyo hali tena,…nimeshachoka, na pia sitaki pia watu waje kusumbuka na huyo mtoto….’nikasema nikitamani kulia…lakini nikaizuia hiyo hali ya unyonge.

‘Lakini…mbona wataalamu wamesema hilo lawezekana, kupata mtoto, na asiwe na hayo matatizo na hata kama atakuwa nayo kuna njia siku hizi za kuidhibiti, na  kwanini unakata tamaa  hivyo, hujajua lolote….hujaambiwa kuwa…?’ Akauliza na akakatiza kuendelea

‘Mimi nilitaka nimpate huyo mtoto, japokuwa kiukweli atakuwa ni kumbukumbu yenye majonzi ya maisha yangu ya taabu na mashaka, lakini hapo hapo angelikuwa ni faraja kwangu,…..lakini nimesikia hata akizaliwa huyo mtoto atakuwa ni mtoto wa kuumwa umwa tu, na hataweza kufikia miaka mitatu, ….mimi sielewi , ila njozi na maono yameniambia hivyo nd ndio ukweli wenyewe…’nikasema

‘Ni nani kakuambia hayo, umeyasikia wapi…?’ akauliza na mara mlango ukafunguliwa, na akaingia Yule mwenyeji wangu akiwa na dakitari mgeni machoni mwangu.

Tulisalimiana na mwenyeji wangu akasema;

‘Waonekana leo mchanamfu na mwenye nguvu ya ajabu, hii ni dalili njema…’akasema

‘Ni kweli kama ukiwa na mgonjwa, akiwa kazidiwa, na siku moja ukaja ukamuona tofauti ana nguvu…ujue ni dalili njema, kuwa aliyemuumba anamuhitajia, au sio….’nikasema nikicheka kama utani na wao wakacheka kuashiria ni utani, hawakuja nafsi yangu ….

‘Hapana, hiyo ni dalili njema kuwa mgonjwa anapona…na utapona tu kwa uwezo wamungu na kwa madawa, ….siku hizi utaalamu umeongezeka…’akasema mwenyeji wangu na kumgeukia Yule dakitari aliyekuja naye

‘Huyu hapa ni dakitari bingwa wa maswala ya mambo ya damu…na mambo yanahusiana na hayo, amekuja maalumu kuangalia tatizo lako hilo la kupungukiwa damu, …..na atakuwa na maswali ya kukuuliza kidogo…., ila kwa hivi sasa nataka kuongea na wewe, yeye ataonana na wewe baadaye….’akasema  mwenyeji wangu na dakitari akanisalimia,

‘Basi baadaye nitakuja tuongee, nasubiria matokea ya vipimo vyako vya damu, yakitoka nitajua tatizo ni nini, ila kuna maswala muhimu nitakuuliza baadaye ukimalizana kuongea na mwenyeji wako, matatizo kama hayo yapo na yana tiba usiwe na shaka kabisa….’akasema na kuondoka.

Alipoondoka huyo docta, mwenyeji wangu akageuka kumuangalia yule jamaa kutoka huko kijijini, akasema;

‘Vipi wewe bado upo mbona wenzako wameshaondoka…?’ akaulizwa

‘Ndio sitaongozana nao kwenye hiyo safari,  nilitaka tuonane kwanza na wewe…’akasema

‘Sasa kwanini umekuja huku,  nilikuambia usije kumuongelesha huyu mdada tena, hujasikia una nini na huyu mgonjwa unataka kumuondoa duniani kabla ya siku zake…ina maana, hukunielewa…’akasema kwa sauti ya ukali

‘Nilipitia kumuaga tu….’akasema

‘Unajua sisemi haya kwa ubaya nayazungumzia haya kwa nia njema, kitaalamu, na kwa hayo yaliyotokea, ungeliweza hata kuchukuliwa hatua za kisheria, hukutakiwa kuongea naye kabisa, kumwambia hayo uliyomwambia na kwa jinsi ilivyotokea umewapa shida sana madakitari….’akasema

‘Kiukweli….nilijua ….ana…ufahamu huo..sikuwa nime…’akazidi kujitetea na mwenyeji wangu akamkatiza na kusema;

‘Wewe huoni kuwa unaweza kumdhuru huyu mgonjwa bila kujua, na sijui kwanini walikuruhusu kuongea naye…nesi mnafanya nini...’akasema akigeuka kumwangalia nesi aliyefika akiwa na dawa

‘Hatukumruhusu sisi…walikuwa kwenye semina zao, na sijui walianza kuongea muda gani, na huyu mgonjwa….’akasema nesi

‘Samahani sana sikujua….’akajitetea

‘Hukujua eeh…! Wewe hujui kuwa wagonjwa kama hawa wanahitajia namna yao ya kuongea, hapa alipo ana mzigo mkubwa, huyu hapa ni mja mnzito, utaharibu uja uzito wake, unaweza hata kumleta tatizo kubwa zaidi hili…hili unalielewa,  kwa vile wewe upo kwenye kundi la kuhamasisha watu, si mlielekezwa haya …...?’ akasema na kuuliza

‘Mimi nilikuja kumuaga tu, natakiwa kurudi huko kijijini haraka….sikuwa na nia ya kumwambia lolote baya kwa hivi sasa, nafahamu kabisa hali aliyo nayo na uangalifu anaotakiwa kuwa nao,…kosa la mwanzo ni kuwa sikuelewa ana matatizo gani, lakini hata hivyo….’akasema na mwenyeji wangu akamkatisha na kwa kusema;

‘Tafadhali nakuomba uondoke…huyu hana matatizo makubwa kihivyo, wewe umemfanya ahisi hivyo kumbe tatizo lake ni dogo tu, na atapona bila shaka…’akasema huyo mwenyeji wangu

‘Kuna jambo muhimu nilitaka tuongee mimi na wewe, ….’akasema jamaa wa huko kijijini

‘Hilo jambo kwa hivi sasa litasubiria,…utaniambia baadaye , …ama kwa huyu mgonjwa wangu sitaki umwambia tatizo jingine lolote kwa hivi sasa, umenielewa, sitaki kosa lijirudia tena kwa hali aliyo nayo haitakiwi hiyo hali ijirudie tena, …’akasema mwenyeji wangu kwa sauti ya ya chini kama anamnongeneza ili nisisikie, wakati huo nesi alikuwa akinipa dawa.

Walisogea  pembeni kidogo, nikasikia akimuuliza

‘Kwani kuna nini……wataka kuniambia… ni kuhusu huyu mgonjwa au kuna jambo linamhusu.?’ Akamuuliza na mimi nikasema kwa sauti

‘Ni tatizo gani hilo na mimi nataka kulisikia kama linanihusu mimi…., mwacheni aniambie , mimi nipo tayari kwa lolote, na kwanini mpaka umwambie yeye, yote nimeshayafahamu, kumebakia nini tena, na hata hivyo, sasa nipo tayari kwa lolote, haiwezi kutokea tena mshtuko…’nikasema na mwenyeji wangu akatikisa kichwa kukataa, na mimi nikasisitiza kuwa aniambie

‘Ni bora asema ni jambo gani maana asiponiambia nitabakia na mashaka nikiwazia ni jambo gani na najua litakuwa linanihusu, asema tu…’nikasema

‘Wewe usijali, nitamalizana naye…tutaongea naye ofisini kwangu ni maswala yao ya kampeni za kuhamasishana hakuna zaidi au sio  ’ akasema na kumuuliza na akijaribu kumsogeza mbali kidogo jamaa ili nisiweze kusikia, na jamaa akamwambia kwa sauti ya chini chini lakini mimi niliweza kusikia hayo maneno machache

‘Ni kuhusu aliyekuwa mchumba wake….’alianza kusema na mwenyeji wangu akamzuia asiendelee , akisema;

‘Tutaongea ofisini kwangu, sasa hivi nina taka kuongea na mgonjwa ili aendelee na matibabu mengine…nimeshakuelewa, sawa..tangulia nakuja…’akasema akimsukuma aondoke, na mimi nikasema.

‘NI lazima aseme na mimi nisikie,  huyo aliyekuwa mchumba wangu kafanyaje…..aseme tu ….’nikasema nikijiinua kitandani. Na mwenyeji wangu akawa akimuashiria jamaa aondoke, lakini sikukubali……

NB: Kunani..

WAZO LA LEO: Ubaya umtendee mwenzako, na mabaya yampate mwenzako, ..ni rahisi kutamka pole, au yote mapenzi ya mungu. Ila kwa wale yaliyowakuta watajua ni nini adha na maumivu yake. Hii inatupa fundisho kuwa sote ni wanadamu na sote yanaweza yakatukuta mabaya na mazuri, kwahiyo tunahitajika kusaidiana, kuoeneana huruma tuwe kama mwili mmoja, ambao sehemu moja ikipata jereha mwili mnzima unahisi maumivu.



Ni mimi: emu-three

No comments :