Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeWednesday, March 9, 2016

SIKIO LA KUFA HALISIKII DAWA-16


Mdocta waliniuliza maswali ya afya yangu, ninavyojisikia, nilianza lini kuumwa, …na wakawa wanaandika kwenye kumbu kumbu zao,….wakawa wanaangalia ile kadi yakungu kubwa iliyokuwa imeandikwa maelezo yangu, halafu wakamuita nesi , na nesi akapewa maagizo ya dawa, halafu wakataka kuondoka , na mimi hapo hapo nikaanza kuwabana kwa maswali

‘Docta, hivyo vipimo vya mtoto kukaa vibaya mtanifanyia lini..au ndio tayari?’ nikauliza na docta wakaangaliana, halafu mmoja akasema

‘Ni nani kakuambia kuwa mtoto kakaa vibaya…?’ akaniuliza Yule docta, na mmoja, akaniambia nilale , akaanza kunikagua tumboni, akipitisha mkono wake tumboni mwangu, halafu akatikisa kichwa kama kukataa

‘Mtoto hajakaa vibaya…una matatizo mengine ambayo ndiyo tunayafanyia kazi ila kama una hisi hali ambayo inafanana na hivyo, tutakuchunguza, tutakupima kipimo cha kuangalia ndani moja kwa moja, lakini hakuna dalili yoyote ya mtoto kukaa vibaya, ni nani alikuambia hivyo…?’akasema docta

‘Huko nilipotoka walisema mtoto kakaa vibaya na nisipowahiwa naweza nisijifungue salama…na ilitakiwa nije kupelekwa muhimbili kwa ajili hiyo, walisema hilo ni tatizo kubwa na nahitajika kufanyiwa vipimo haraka iwezekanavyo…’nikasema

‘Una vyeti vyoyote …ambavyo walikupima, au waliandika maelezo yake?’ akauliza mwingine

‘Sina…’nikasema

‘Kiukweli kama ungekuwa na tatizo hilo tungelikugundua mapema tu….lakini tutalifuatilai hilo, tutakupima vipimo vyote  usiwe na shaka…’akasema na mwingine akaongeza kusema

‘Muhimu utuamini sisi,…. Kwa vipimo vyetu vya awali huna tatizo kama hilo…mtoto kakaa vyema kabisa…matatizo mengine tunayafuatilia, utapewa dawa na maagizo mbali mbali…baadaye akija Yule mwenyeji wako mtaongea, zaidi, yeye ni mtaalamu pia, utamuelezea yote unavyohisi, na ataweza kukushauri zaidi….’akasema na nikaona haina haja kuuliza zaidi na docta akaita kwa sauti

‘Nesi,…..’ alimuita nesi, na nesi akaja kwa haraka

‘Huyu nesi  atakupa dawa zako na kama una tatizo jingine lolote usisite kutuambia, ..’wakasema na  nikawaambia sina tatizo jingine kwa hivi sasa na wao wakaondoka. Nesi akanipa dawa nilzotakiwa kutumia siku hiyo,na alipomaliza akatoka.

Nilibakia nikiwa na mawazo nikijiuliza maswali mengi,  ina maana hawa madakitari hawataki kulifuatilia hilo tatizo langu, la mtoto kukaa vibaya ni kwanini, … mimi nina uhakika, mtoto hayupo sawa, na niliambiwa na madakitari bingwa wa kule kijijini, kwanini wao wanadharau, ngoja, akija huyo mwenyeji wangu nitamwambia awasisitizie wanipime, kama hawawezi  ni bora niende huko Muhimbili…

Siku ikaenda kwa haraka maana walikuwa wakija watu mbali mbali, mara wa dini mara wa kutoa misaada….wanatuhoji, na maswali yao yalinifanya nizidi kuwa na mshaka sana…na mwenyeji wangu hakuweza kuonekana tofauti na nilivyotarajia, kwani alisema atakuja mapema lakini mpaka muda huo alikuwa hajafika.

Mchana ukaingia na mara wakaja kundi la watu,  walipofika walisalimia wagonjwa na baadaye mmoja mmoja akaanza kuongea maswala ya matumaini ,…walisema wazi wazi kuwa wao wameshapima na wamejulikana kuwa wameathirika….wana ugonjwa wa ukimwi, na sasa wanaishi kwa matumaini, na wamejitolea kuwapitia wengine kuwaelimisha,…waliongea mambo mengi na baadaye wakakaribisha maswali….

Mimi nikaingiwa na mawazo, na sijui kwanini nilishindwa kuvumilia, nikauliza.

‘Kwanini mnatuhubiria hayo, kwani sisi tumeathirika…?’nikajikuta nimeuliza hilo swali

‘Kila mmoja anaweza kuathirika, na kama hujaathirika wewe na huu ugonjwa, unaweza ukawa na jamaa yako au ndugu, au jirani, anahitajia ushauri nasaha, kazi yetu nikuwapitishia huu ujumbe kila mtu…awe ameathirika au hajaathirika…’akasema mmojawapo.

Waliongea na baadaye wakamaliza, na sasa ndio wakataka kuondoka, nikagundua  mtu mmoja  kati yao ni kama namfahamu, yeye alikuwa akigawa vijarida kwa wagonjwa na jamaa waliokuwepo humo ndani waliokuja kusalimia wagonjwa wao….

‘Huyu mtu ni kama namfahamu,…atakuwa anatokea kijijini kwetu,….’nikasema kimoyo moyo nikawa na hamu ya kuonana naye, na wakati anafika kwangu kunigawia hiyo kijarida, nikaamua kumuuliza...

‘Mimi kama nakufahamu vile…wewe hutokei kijijini kimoja kinaitwa…….’nikasema na yeye akaniangalia kwa makini, halafu akasema

‘Yawezekana unanifahamu, ni kweli natokea huko, lakini sikuwa mkaaji sana, nilikuwa nafika na kuondoka…labda nikumbushe wewe ni nani….?’ Akaniuliza na alipoongea nikaweza kumtambua vyema, sauti yake ilikuwa sawa sawa na ndugu yake

‘Wewe sio ndugu yake……yule aliyekuwa na studio ya kupigisha mziki na picha kule kijijini…?’ nikamuuliza, na yeye kwanza akatabasamu halafu akatikisa kichwa , akaangalia huku na kule kama vile anawa wasi wasi na jambo, halafu akasema;

‘Ndio ni kweli, wengi wanamfahamu sana  yeye kuliko mimi,…lakini nchi ya jirani nilikuwa nafahamika mimi zaidi kuliko yeye, na mara nyingi shughuli zetu tulikuwa tunafanyia huko zaidi kuliko hapa nchini kwetu kutokana na sheria za nchi yetu,…japokuwa kwasasa hawafuatulii sana, ndio maana kaka yangu akaweza kufungua studio yake na kuanza kufanya shughuli hizo…japo kwa siri …’akasema akigeuka huku na kule.

‘Mimi nimeshaachana na shughuli hizo….lakini nisingelipenda  kuongelea shughuli hizo, …si unawafahamu wale watu ….mwanzoni walitutushia amani…na walikuwa tayari kuua, ….kwahiyo ilikuwa kazi sana, ….hata hivyo polisi wanachunguza….’akasema

‘Kwahiyo na wewe ni mwenyeji kule, au unafika mara moja moja kama mimi….?’’ akaniuliza

‘Mimi ni mwenyeji wa  huko , na nimekulia kule, hapa nimefika tu kwa ajili ya kutibiwa….’nikasema na aliniangalia kwa mashaka, sasa akaja na kukaa karibu nami,akiwa anajiamini kidogo.

‘Oh…pole sana, …ni vyema umekuja huku….huku watu wanajitambua na kuelewa zaidi ya huko kijijini…kijijini ukiumwa wanakuchukulia kama wewe ni wa kufa tu…’akasema na mimi nilitaka kumwambia kuwa mimi siumwi huo ugonjwa,lakini nikamuacha aendelee kuongea

‘Unajua , mimi nilijiunga na kundi hili katika kuhamasisha na kuwazindua watu wajielewe, waondokane na fikira hizo potovu, wabadili tabia zao…mtu akiumwa ajaribu kuwa mwangalifu asiendelee kuwaambukiza wenzake…’akatulia naona ni kama yeye hakutaka kuongea zaidi , ni kama anaficha jambo, nikahisi anaogopa.

‘Kwa mfano wewe sasa ni mjamzito, ina maana unaweza kujifungua mtoto naye kaathirika, au hajaathirika,…lakini kama umefuatilia vyema taratibu na masharti yao unaweza  kabisa ukazaa mtoto  akakwepa kuathirika zaidi…wapo wamezaa watoto hawana huo ugonjwa kabisa kwa vile walifuatilia masharti, huwezi amini, ….’akatulia

‘Unajue mimi, niligundua kuwa nimeathirika nikiwa hata sikutegemea kabisa, nilishajiamini sina na siwezi kuwa nao,…ilikuwa kazi ngumu kukubali hiyo hali, lakini sasa kama unavyoniona huwezi hata kufahamu, nina afya yangu njema kabisa zaidi ya Yule ambaye hajaathirika…’akasema akijiangalia angalia.

Ni kweli alionekana mwenye afya njema mwili wake ulikuwa umejengeja vyema kimazoezi, huwezi kumfikiria kabisa kama ana tatizo kama hilo.

‘Kwa hali hiyo, …lilipotokea kundi kama hili, na mimi nikaingiwa na  hamasa, ya kutaka kuwaelimisha wenzangu…..maana kwa hivi sasa huwezi kuwatambua wenye matatizo kama hayo, na nia yetu nikutafuta njia ya kuukomesha huu ugonjwa usisambae zaidi, na ikiwezekana uishe kabisa,…. tumetembea sana, hadi nchi za jirani kwa kazi hii, tunaigiza Michezo ya sinema na, tunaelimisha kwa njia hii ya kuongea kusambaza vijarida nk, ….na wengi wameanza kutuelewa..’akasema

‘Kwahiyo hata kaka yako amejiunga na kundi hili si nimesikia kuwa  naye kaathirika….?’nikamuuliza na nilimuona akibadilika sura, na nilihisi kama machozi yakimlenga lenga, baadaye akajitahidi na kusema;

‘Ndio kaka alikuwa nao, lakini hakutaka kuelewa,,..yeye alijijua mapema…., lakini akaficha, na bila kujali akawa anatembea na wasichana huko alipotoka na zaidi akaenda kijijini pale….oh, akawa anatembea na mabinti wa pale mimi nilikuwa bado huko ncho ya jirani, na sijijui kuwa na mimi nimeshaambkizwa

‘Ilitokea tu ikaja harakati za kupimwa bure nikaona name nikapime,….oh, nikaonekana ninao.  Unajua ujana tena, mimi japokuwa nilikuwa mwangalifu sana, maana nimesoma , nafahamu ugonjwa ulivyo, lakini kutokana na kazi tuliyokuwa tunejiunga nayo,  sikuweza kuukwepa…’akatulia

‘Lakini nimeahidi kutokana na hiyo kazi, niweze kuitumia kuelimisha watu, …’akatulia

‘Kumbe kaka alishapima, na …hakuwahi kuniambia, mimi nilipogundulikana hivyo,…nikawa mnyonge sana,..nikawa sitaki hata kuifanya hiyo kazi, siku moja kaka alikuja kuleta biashara zake, akanipa nizifanyie kazi, nikakataa..akashangaa,

‘Kwanini unakataa biashara,….hii ni biashara kali wakiiona jamaa itauzika kama njugu…’akaniambia

‘Mimi nimeamua kuachana na bisahara hii,maana najua siku yoyote nitaondoka na huko kwampla nitasema nini….’nikamwambia

‘Hivi  wewe umepungukiwa na akili, hii ndio biashara inatufanya tuonekane hapa mjini, tumejitarika kwa kupitia hii biashara, tuna magari , nyumba..sasa wewe wataka tuiharibu…’akasema

‘Utajiri, ..mali na maisha haya ni ya kupita tu….mimi naogopa mzigo wa madhambi tulioubeba, je una uhakika utapata muda wa kutubia kablsa hujakata roho….na mimi nimegundulikana kuwa nimeathirika…’nikasema na kuanza kulia,

Kaka yangu alikaa kimia kwa muda, hakutajia hilo, akaniambia

‘Kwanini hukuchukua tahadhari, nilikuambia…sasa ina maana sote tunao…’akasema akitiisa kichwa, halafu akaanza kunipa moyo na kuniambia kuwa naa yeye anao, lakini hajali kwani ni ajali kwnye mapambano.

‘Hii ni ajali kazini, lakini bao tunatakiwa kuishi, kutafuta, wewe usijali kabisa endelea na kazi siki ikifika imefika…’akaniambia, lakini mimi sikuweza kuendelea na hiyo kazi tena, akaifanya yeye mwenyewe, …nilianza kuishi kwa maisha ya mashaka nikakonda, nikaanza kuumwa, na nikalazwa, …nikiwa hospitalii nikakutana na wagonjwa wengine kama mimi wakanishauri kuwa kuna kundi la kutiana hamasana na matumaini.

‘Ndio nikaanza kuingia na matumaini kuwa wapo wengi, na wanaimani kuwa kuumwa kwa huu ugonnjwa sio mwisho wa maisha…nikaingiwa na hamasa kweli, nikaanza kujielezea
Kaka yangu akapata hiyo taarifa, akanijia na kunikanya kuwa nikimtangaza kuwa kaathirika, ataniua, na zaidi nisije kuitangaza kazi yake, ..’aliposema hapoo akageuka kuangalia huku na kule.

‘Mpaka sasa naogopa kuelezea kazi za kaka yangu, unajua  zina usiri mkubwa, na nilimuahidi kaka kuwa sitaweza kuzitangaza…japokuwa keshatangulia mbele ya haki, lakini bado nahisi kama namuona, ….kaka alikuwa mnyama kwenye kazi zake hataki mchezo…mungu amsaheme..’akatulia

‘Kitu ninacholaumu hadi leo ni kuwa yeye  alijua kaathirika….na bado aliendelea kutembea na mabinti wa watu, anawaambukiza, …., na mbaya zaidi  akapuuzia masharti ya huu ugonjwa,..huu ugonjwa ukifuatilia masharti yake unakuwa huna shaka,….unaishi nyema kabisa….ndio hivyo labda siku zake zilipangiwa ziwe hivyo,  na bahati, siku zake zimefika keshatangulia mbele ya haki….’akasema

‘Oh….una maana….’nikasema

‘Ndio ameshafariki kaka yangu, nilimpenda sana..ni mtu wangu alikuwa karibu sana nami lakini ndio hivyo mungu kampenda zaidi….’akasema akianza kububujikwa na machozi…na  mimi pale nilipo hali yangu ikawa imebadilika ghafla, nilianza kuhisi vibaya, mwili ukaniisha nguvu, nikanywea, nikataka kutapika….sijui kwanini nilijihisi vile ghafla baada ya kusikia taarifa ile.

Kwa ujumla kaka yake alijulikana sana hapo kijijini, na kutokana na kazi yake wengi walimzoa sana alikuwa mcheshi sana na kwenye shughuli akiitwa anaipendezesha vizuri sana….alikuwa msanii wa shughuli. Na kutokana na kipaji chake hicho, kila mtu alitaka kumuita kwenye shughuli yake kama mwendesha shughuli. Alikuwa mtanashati anayejipenda, na alikuwa na sura nzuri yenye mvuto na kwa hali hiyo wasichana wengi walimpenda sana. Kumbe…oooh

‘Oh, ina maana Msanii amekufa,….oh, hata sikuwa kuambiwa, alikufa lini? Hapana sio kweli mbona mimi sijui…’ nikasema  huku nikijaribu kutafuta namna ya kujizuia, ila pale nilikuwa sijisikii vizuri kabisa.

‘Ndio, ameshafariki, na alifariki akiwa na hali mbaya sana, aliishiwa ghafla, kuhara , kutapika…ni magonjwa hayo yaliharakisha kummaliza, akatokwa na madonda, aah, inatisha …akapoteza wajihi wake kabisaka maana maradhi yote yalimuandama….hakutaka kufuata masharti….hajafariki muda mrefu, hata mwezi haujaisha,..ubishi wake bwana, halafu alifanya mambo ambayo hayastahiki, na zaidi alijua kuwa ana tatizo la ziada ….’akasema akitikisa kichwa  kwa uchungu

‘Tatzi gani la ziada…?’ nikaweza kumuuliza

‘Tabia yake hiyo ya kujitambua kuwa anao huo ugonjwa , na ya kuwa ana hilo tatizo na bado akaendelea kutembea na mabinti  mbali mbali,hata bila kuwafahamisha, wakachukua tahadhari…kiukweli kama mtu unajijua una huo ugonjwa ni muhimu amuelezee mwenza wake,…kwanini utembee na watu wengine ukijua utawaambukiza mimi inaniuma sana,..sio vizuri, na pale kijijini alitembea na mabinti wengi sana, wengi walimpenda, kwa vile alikuwa msanii mnzuri hadi kwenye mambo hayo, ooh,….’ Akasema

‘Alikuwa na tatizo gani la ziada…..?’ nikauliza

‘Mhh…aliwahi kuoa , lakini kila akizaa mtoto hafikishi mwaka.  na ikafikia hatua wakaachana, yeye
aliambiwa damu yake ina athari na kabla hajaoa inabidi mchumba wake apimwe kwanza ili ijulikane kama anaweza kuzaa bila mtoto kuambukizwa, ….

‘Ndio huo ugonjwa wa ukimwi…?’ nikauliza

‘Hapana hilo ni tatizo jingine kablsa,…mtoto anakuwa na upungufu wa damu…mara kwa mara, na haishi kwa muda mrefu, ….yeye analijua hilo kwani walihangaika sana na mkewe na ilifikia muda wakaachana, na akapewa hiyo tahadhari kuwa asije kuoa, au kuzaa bila huyo mwenza kupimwa….. analijua hilo, lakini hakujali,…’akasema

‘Mhhh mimi hata sielewi….;nikasema

‘Yeye anaelewa sana…lakini zaidi wanachojua watu kwa hivi sasa ni huo ugonjwa wa ukimwi….’akasema

‘Oh….’nikaguna na yeye akasema

‘Kwahiyo kama ikatokea kampa mtu mimba,….inabidi awe makini kweli, kama inatokea anapungukiwa
na damu, hiyo ni dalili mojawapo, lakini mara nyingi matatizo hayo hutokea kwa mtoto….na hali inazidi kuwa mbaya kama akiwa na huu ugonjwa wa kupunguza kinga, …’akasema akitikisa kichwa.

‘Oh mungu wangu….’nikasema

‘Hili lilikuja kujulikana pale kijijini, wakati kaka amezidiwa,..yeye mwenyewe ilibidi aanza kusema, kukiri, kuwa kaathirika, akajitahidi kutubu, na watu waliposikia hivyo, wengi wakawa wanaishi kwa mashaka, hata wale waliopo kwenye ndoa…’akasema

‘Kwanini …?’ nikauliza

‘Kwanini…unauliza kwanini,…. huwezi jua, baba katembea na binti wa ndani,…binti wa ndani alihadaiwa na kaka akatembea naye…..sasa huyu baba wa ndani akikutana na mkewe itakuwaje, ni mnyororo ambao unamfuata hata na asiyekuwepo…kwahiyo hali hiyo iliposikika, hakuna aliyekuwa na amani…na tuliwasaidia sisi tulipofika hapo kijijini tukawahamsisha kuwa wakapime,….’akatulia

‘Kupima, ….pale kijijini ni kazi….wengi walikuwa wanapinga kupima…’nikasema

‘Mwanzoni wengi waliogopa kujitokeza…kidogo kidogo wakaanza kuja vituoni, na walioanza ni wavulana, wasichana kidogo ,nguvu kazi ya kijiji, na baadaye kidogo kidogo wakaanza kujitokeza, na ambao hawakuwa na jinsi ni akina mama wajawazito ni lazima wapime, …ni baada ya kazi kubwa ya kuwaelimisha, kuigiza michezo mbali mbali ya hamasa….ndio wakaanza kujitokeza kwa wingi…..na wengi wakagundulikana wameathirika…’akasema

‘Oh balaa gani hilo…na yote hayo ni sababu ya nini, umasikini….maana vijana walijiunga huko ili kutafuta ajira, ….na ina maana basi aliyeambukiza watu ni huyo kaka yako aui?’ nikauliza nikiwa na wasiwasi

‘Ni yeye na kundi lake…..wengi walihadaiwa walipofika hapo kwenye mazoezi ya michezo, na….ndio hivyo…, na najua alipofika kitu cha kwanza aliwatafuta, vijana mashababi, wasichana warembo ili wajiunge  kwenye michezo ya kuigiza,  michezo ya sinema na kutengenza kanda za video si ndio ilikuwa hivyo,…lakini ndani kwa ndani wakaingizwa kwenye kuigiza mapicha mabaya, …’akasema na kugeuka huku na kule.

‘Mapicha mabaya….?’ Nikauliza nikionyesha mshangaoo akili yangu ikaenda mbali zaidi.

‘Ndio michezo ya kutengeneza picha za ngono, video hizo zilienda kutengenezwa vyema nchi ya jirani kwani huko kuna  mitambo mizuri, tulikuwa nayo huko na tulikuwa wakala wa kimataifa……mimi mwenyewe nilikuwa nairatibu….’akasema na hapo nikakumbuka zile kanda za video nilizowahi kuziona kwenye kabati la mchumba wangu,..kumbe!

Mimi pale akili yangu ilianza kuwanga, nikijiuliza ilikuwaje nikaingizwa kwenye mpango huo bila ya mimi kujijua, …bila ya mimi kujitambua, nikataka kumuuliza swali lakini yeye akaendelea kuongea

‘Hii ilikuwa siri ya kundi….wazazi walikuwa hawajui, vijana wanasema wanakwenda mazoezini huko kinachofanyika hawakijui, ni tatizo kubwa sana, sijui serikali watafanyaje kumaliza huu uchafu, …ni kutu inayokula chuma taratibu, hili na tatizo la madawa ya kulevya….kwani makundi kama haya yanazidi kuongezeka na sasa wameingia hadi huko viijijini,…’akasema

‘Sasa kwanini hawakuchukuliwa hatua…’nikasema

‘Nyie mliowahi kuona mlitakwia mseme, lakini mkiuliza mnaogopa, …kwani mlilishwa kiapo cha siri,mkiahidiwa mapesa mengi, si ndivyo hivyo….kaka alishachukuliwa hatua, sema kwa vile alishaanza kuumwa, lakini wazazi na serikali ya kijiji, ilishaanza kuchukua hatua za kumshitaki na ilikuwa karibu afikishwe mahakamani, …’akasema

‘Masikini Msanii,…..ina maana hata mimi nitakuwa nao basi…lakini ilikuwaje na mimi nikakubali kirahisi hivyo, mimi sielewi….’nikajikuta nimesema

‘Kwani na wewe uliwahi kutembea naye…oh, …wao walikuwa na mbinu nyingi sana, kama wanakuhitajia kwenye kundi…..watakupata tu…..je wewe uliingia kwa hiari au ?’ akaniuliza na mimi nikabakia kimia nikianza kuwazia  jinsi gani niliweza kuingizwa kwenye mtego wao. Sikujua…mchumba wangu….yeye ndiye ..oh, kichwa kilianza kuniuma.

‘Kwanza ukihitajika humo kama una sura nzuri kwa msichana wanaweza kumtumia mchumba wako, au ikishindikana wanatumia mbinu nyingine ya kukulewesha madawa ….’akasema

‘Kuna madawa wakikiwekea, kwenye kinywaji unakuwa kama zezeta, utaweza kufanya yale ambayo ukiwa katika hali yako ya kawaida huwezi kuyafanya…’akaendelea kuongea lakini mimi kwa wakati huo akili haikuwa yangu  sikuwepo kabisa , nilikuwa nimezama kwenye lindi la mawazo..

Nilianz kuwazia kuwa na mimi sasa nina huo ugonjwa, nikawazia nipo kwenye hali mbaya, nimeisha , nina madonda mwili mnzima….,nikiwakumbukia wale waliowahi kuumwa walivyoisha, kuna  watu niliowahi kuwaona wakiteseka na huo ugonjwa nikajihisi na mimi nitakuwa hivyo pia,….nilianza kuwanza jinsi gani nitaweza kujifungua mtoto naye akiwa kaathirika, na huenda hataishi muda mrefu, kisa ni mimi…niliwaza mengi, mengi sana…nikaanza kulia, ..nikaanza kuwakumbuka wazazi wangu,….

‘Usijali…wewe umeshajitambua, kama umeshajitambua, ishi kwa matumaini, fuata masharti utapona kabisa..hunioni mimi…nimeshapona,…japo kuwa nimeathirika…’akasema

‘Mhh..hata sijui…kiukweli naanza kujijutia, wazazi wangu walinikanya sana,….walinielimisha, na hata kunichapa, lakini nilikuwa mkaidi,nilimsikiliza mpenzi wangu zaidi,…yote niliyoambiwa hayakuweza kuingia akilini mwangu, sasa ..ooh, lakini hata hivyo mimi kiukweli sijui,..kama kweli ninao au la…sijawahi kupima, au kuambiwa…’nikasema

‘Kama hujapima usiwe na mashaka, …na ni vyema uingiwe na moyo, wa kupima,ujenge ujasiri, uone kama unapima ugonjwa kama ugonjwa mwingine, na uwe tayari kupokea matokea yake, ukiweza kuweka ujasiri huo, hata ikipima utakuwa kama unatimiza wajibu tu,….hutaumia, utaweza kupona kwa haraka…’akasema

‘Kupona kwa haraka…hahaha…! Ugonjwa huu hauna dawa, utaponaje, nitaponaje, na wakati umeshasema kuna tatizo hilo jingine la ziada, mtoto akizaliwa, …ooh, kwanini mimi, kwanini …...Mimi namlaumu sana mchumba wangu ndiye alisababisha yote haya…alinirubuni, ….sikujua, ..’nikaanza kuongea kama mtu aliyepagawa, na yeye akawa na wasiwasi akiangalia huku na kule akaongea kwa sauti ya kunong’ona

‘Kwani mchumba wako ni nani…mbona wasema kaka halafu …..?’ akaniuliza

‘Ni …handsome boy…’nikamtaja kwa jina lake la utani wanavyomuita hapo kijijini na aliposikia hivyo akaniangalia kwa macho yenye wasiwasi.

‘Una maana Yule...mwenye gereji pale kijijini...yule alikuwa rafiki mkubwa wa kaka yangu, …yeye alikuwa mmoja wa kundi la biashara hizo haramu,…kwa siri alikuwa akienda nchi ya jirani kufuata vipuri vya magari na humo aliweza kuficha hizo biashara…si ndio yule mwenye gereji kubwa…?’ akauliza
‘Ndio huyo…..’nikasema
‘Oh, unajua huyo mke wake aliyemuoa, alikuwa mpenzi wa kaka yangu, kumbe kila akija huko nchi ya jirani, walikuwa kwa siri wana mahusiano, kaka akaja kuyagundua hayo,….na hilo ndilo lilifanya yeye na kaka wakosane baadaye…yaani kulitokea ugomvi siku moja, …we acha tu…’akasema.

‘Eti nini, ina maana handsome na huyo binti walikuwa wanajuana muda, na muda huo kaka yako alikuwa keshatembea naye na anajijua anao…kwanini lakini…ina maana,….’nikashindwa kuendelea nikishika kichwa!

‘Walikuwa wapenzi wa siri siku nyingi, si walijuana toka huku, kaka naye hakuwa na wasiwasi aliwaamini, kumbe …wanazungukana wenyewe kwa wenyewe…hebu nikuulize swali  Je uliwahi kuwasiliana na huyo aliyekuwa mchumba wako hivi karibuni…?’ akaniuliza akiniangalia kwa macho yenye masikitikio.

‘Hapana nina muda kama miezi eeh…., niliondoka hapo kijijini miezi miwili sasa….’nikasema.

‘Oh,..huyo  jamaa yupo hivi sasa ana hali mbaya sana na mkewe wake ameshamkimbia,…mimi  nilijua tu wataachana,namfahamu Yule mwanamke hakaagi na mume….., ana tabia chafu, na watu kama hao wana roho ya paka, kazi yao ndio hiyo kuambukiza tu. Mimi niliwahi kumshauri huyo jamaa akaona mimi naingilia mambo yao na nafanya hivyo kwa kumsaidia kaka yangu….’akasema.

‘Ina maana na yeye kwa hivi sasa anaumwa ….? Au yupo na hali mbaya kwa vipi….?’ Nikauliza kwa mashaka.

‘Huyo aliyekuwa mchumba wako sio….? Tatizo lake alikuwa kama kaka yangu,..hakutaka kusikia, hakutaka kukubali ukweli, yeye na kundi lao ndio waliokiharibu hicho kijiji…nawalaumu sana kwa hilo…na hiyo nahisi ni adhabu kwao kwa makosa waliyofanya japo kuwa sasa wanaadhibiwa na wasiostahiki…mungu mwenyewe anafahamu ni kwanini, watu wanakanywa hawasikii, imekuwa ni sikio la kufa,…’akataja msemo huo ulionigusa sana moyoni.

‘Nakuuliza na yeye anaumwa…au …?’ nikauliza hilo swali tena

‘Ndio anaumwa,  hali yake ni mbaya,…na hutaamini, alianza ghfla, na kwa muda mfupi tu akawa hajiwezi, niliondoka akiwa kalazwa, na japo kuwa kakubali ukweli, lakini naona kama keshachelewa sana, kiujumla nimemuacha akiwa kwenye hali mbaya ukimuona utamuhurumia….’aliposema hivyo mwili wote ukanyong’onyea, nilishindwa kuvumilia, nikahisi vibaya …..

Pale nilivyo kaa, nilianza kuona giza likitanda machoni, na kwa mbali nilimuona Yule mwenyeji wangu akija, lakini  sikujua kilichotokea baadaye, kwani nilikuwa tayari nimeshapoteza fahamu.

NB: Inabidi niishie hapa ili tuweze kuyatafakari hayo…mengi yametokwa kwa muda mfupi, lakini tupo pamoja.


WAZO LA LEO: Tunaposhauriwa kuhusu magonjwa ya kuambukiza tuwe makini na kufuata ushauri wa wataalamu, ni vyema tukapima kabla ya kujiingiza kwenye mahusiano, kuna magonjwa tunaweza kuyakwepa, kuna maambukizi tunaweza kuyakwepa, kuna matatizo ambayo tunaweza kuyakwepesha kwenye familai zetu na vizazi vyetu,..haya kwa wazee wetu waliyafanya mtu akitaka kuoa, au kuolewa wazee wetu walifanya uchunguza kwa familia husika kama familia hiyo haina magonjwa ya kurithi, nia ni kukwepa matatizo hayo kwenye familia, siku hizi kuna vipimo, je hatuwezi kuanza kuyafuatilia haya. Tunapuuzia, na matokea yake inakuwa sikio la kufa…

Ni mimi: emu-three

No comments :