Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Monday, March 7, 2016

SIKIO LA KUFA HALISIKII DAWA-15

Ikawa ni safari kuelekea Dar…..

Sikusumbuka kufika…gari halikuleta matatizo…, namshukuru mungu kuwa pamoja na hali yangu, mwili hauna nguvu, lakini niliweza kufika salama, na niliposhuka kituoni nikawasiliana na mwenyeji wangu, akaniambia yupo tayari keshafika hapo kituoni kunipokea.  

‘Nimeliona gari ulilokuja nalo….’akasema

Mwenyeji wangu huyu alikuwa na usafiri wake, hakuingia na hilo gari ndani, aliingia kunifuata tukatembea kutoka nje, hadi kwenye gari lake, …na ila hatua  ya kutoka kwenye basi hadi kwenye gari lake hali ikabadilika, nilianza kujisikia vibaya na yeye akaligundua hilo, japo nilijitahidi sana kutokujionyesha…

‘Oh,nakuona haupo safi..kwa hali hiyo siwezi kukuchukua nyumbani ni vyema tupitie hospitalini kwanza,…’akasema

Mimi  sikusema lolote maana kiukweli nilikuwa najisikia vibaya, nikawa kimia tu,yeye akaendesha gari lake kuelekea hospitali, tulipofika tu madakitari wakanihangaikia, kitu cha kwanza nikawekewa maji (drip), huku wakichukua vipimo vya haraka,na vipimo hivyo vikaonyesha  nina upungufu wa damu,..tatizo lile lile.

Nikalazwa…

 Na siku ya pili ndio nikapata muda wa kuongea na mwenyeji wangu nikiwa kitandani, hali kidogo ilikuwa inarizisha,..niliweza kusimama na kutembea mwenye kwenda chooni, tofauti na jana yake nilipofika hapo hospitalini hata kutembea nilishindwa.

‘Naona leo haujambo…’akasema

‘Najisikie nafuu…’nikasema

‘Sasa mimi nimepitia hapa mara moja, hebu nambie, hali yako kwa ujumla…ndugu yangu alinielezea juu juu tu akiwa kachanganyikiwa,  yaonekana alikuwa kataharuki.., mpaka nikaogopa,’akasema.

‘Mimi siwezi kujua zaidi,..labda nisema tangu nipate ujauzito huu nimekuwa nikiumwa tuu,..na kila mara naambiwa damu imepungua na zaidi natapika sana,…naskia kizungu zungu, kula kwa shida…ndio hivyo tu..’nikamwambia.

‘Basi usijali, ilimradi umefikia hapa hospitalini, utachunguzwa vyema, watakupima kila kitu ili kuona tatizo lipo wapi…ila kwa hivi sasa upo safi…muhimu tu utulize kichwa chako, ondoa mawazo,  ukijua kuwa upo kwa wataalamu, au sio’ akasema akiniangalia kwa tabasamu mdomoni.

‘Sawa mim nakusikilizeni nyie, maana hapa nimekuja kwa kupitia, sina mbele wala nyuma, sina ndugu wala rafiki…’nikasema

‘Usijali, …wewe tambua kuwa kila mtu ni ndugu wa mwingine, na kusaidiana ni wajibu wa kila mtu, hatutakiwi kubaguana, …ukiwa na nafasi, saidia mwenzako,maana kusaidia ni akiba yako ya huko mbele,ndivyo imani yangu inasema hivyo…’akasema

‘Nashukuru, …kama wapo wenye moyo huo…imefikia hatua hata naogopa,naona kila mtu hanipendi….’nikasema

‘Sio hivyo,..ni hulka tu….sasa naona nikuache, nipitia kazini mara moja, halafu nitakuja, tutaongea , nataka tuongee kidogo..’akasema na kuondoka.

Kwa muda ule nilipatiwa dawa, na haikuchukua muda nikashikwa na usingizi, nilipoamuka nilimuona mwenye wangu ameshafika.

‘Haya nimekuja, nimeona nije tuongee kidogo na nifahamu kinachoendelea, nimeongea kidogo namadakitari sasa naona niongee na wewe, japo sio kwa mapana, nataka kujitambulisha kwako na wewe ujiatmbulishe kwangu….’akasema

 ‘Mimi ni ofisa wa kampuni zisizo za kiserikali za kuhudumia wagonjwa wa magonjwa ya kifua kikuu na ukimwi…’alipotamka ukimwi nikahisi mwili ukiniishia nguvu,ikabidi niulize hapo hapo

‘Ina maana mimi nina ukimwi?’ nikamuuliza na yeye akaniangalia kionyesha tabasamu lake.

‘Oh, kwannii  unaniuliza hivyo, kwani huko wakati unatibiwa walikuambiaje..?’ akaniuliza kwa mshangao

‘Hapana mimi sina ukimwi, watu wanasema hivyo kuwa ninao huo ugonjwa, lakini sijawahi kupima au kuambiwa na dakitari hivyo..’nikasema

‘Hilo tutaliangalia,..usijali kabisa, usisumbue kichwa chako kuwaza kitu ambacho huna uhakika nacho,…wanasema usijitwike mzigo kabla haujatua kichwani…unasikia,..na ukumbuke kuwa ukimwi ni ugonjwa tu kama magonjwa mengine, …na huwezi kujua kuwa unao ugonjwa wowote mpaka upimwe au sio,..kama hujawahi kupimwa,basi huna, …’akasema

‘Sasa kwanini naumwa umwa hivyo,na watu wengi, hata huyo ndugu yako anasema mimi ninao…ndio maana akataka nije tuonane na wewe?’nikasema na kumuuliza

‘Nikuulize swali wewe unahisi ni kwaninii wanasema hivyo?’ akauliza

‘Wanahisi kwa vile ….’nikasita kidogo halafu nikaendelea kuongea

‘Labda ni kwa vile….kuna mwanaume wanasema anao, huenda kaniambukiza…’nikasema

‘Ni nani kwako huyo mwanaume…..?’ akaniuliza

‘Aaah, ni hadithi ndefu hata sielewi…..’nikasema

‘Usijali, ukumbuke kitu, kutembea naye sio tatizo..unaweza ukaambukizwa au usiambukizwe,na unaweza ukaambukizwa kwa njia nyingine tofauti, kuna sindani, viwembe, kuchanga vitu kwa hivyo vikiwa na maambukizi, sasa nikuulize wewe,je wewe uliwahi kutembea naye huyo mtu?’ akaniuliza na mimi hapo nikakaa kimia

‘Usijali…eeh, nikuulize kitu, wewe uelewi wako, ukiumwa na mbu,unaweza kuwa na malaria,… kwa ufahamu wako?’akaniuliza akiniangalia kwa makini usoni

‘Kama mbu hao wana malaria unaweza kuambukizwa, lakini kama hawana huwezi kuambukizwa ndivyo nijuavyo mimi…’nikasema

‘Sawa kabisa….sasa nikuulize swali moja, usijali lakini,  je huyo mwanaume wanayesema ana ukimwi, una fahamiana naye…unamfahamu vyema?’ akaniuliza

‘Ni majirani kijijini, ila yeye alikuwa akifanyia kazi nchi ya jirani baadaye akarudi hapoo kijijini, wengi wanamfahamu kwa vile…ana shughuli inayowavuta sana vijana, ana biashara ya studio ya kupiga picha, anachezesa madisco,…ana..tengeneza kanda za harusi…ni vitu kama hivyo….’nikasema

‘Ok…..kwahiyo wewe unamfahamu kwa kazi yake hiyo , na ndiyo iliyofanya muwe naye karibu au sio?’ akaniuliza…’nikatulia sikumjibu kichwani nilikuwa naanza kuhisi uwoga…maswali yake yalikuwa na maana Fulani,

‘Usijali…..usifikirie sana kujiumiza,kamahuwezi kujibu acha…usiumize kichwa, ila nimekuuliza kuhusu huyo mtu ili nijue mlivyofahamiana…mnaweza mkawa mnafanya shughuli moja, mkawa mnachangia vitu…au mkawa marafiki,ikatokea tu mkapendana au sio…sasa hamasa yangu ni kujua kwanini watu wakasema kakuambukiza je mna urafiki naye wa karibu, hata wa siri, usiogope kuniambia…?’ akaniuliza.

‘Mhh, sio kihivyo…zaidi ni kuwa alikuwa rafiki wa mchumba wangu..’nikasema

‘Kwahiyo kumbe yeye sio mchumba wako, wala rafiki yako ,?’ akaniuliza

‘Sio mchumba wangu, ni jirani tu, na rafiki wa mchumba wangu…’nikasema

‘Sasa kwanini watu wahisi kuwa yeye kakuambukiza,..?’ akaniuliza

‘Hata mimi sijui…’nikasema na yeye akatabasamu na kusema

‘Usijali, hayo na mengine mengi tutayaongea, muhimu nichukulie mimi kama rafiki yako,rafiki yako anayetaka kukusaidia kuvuka mto wenye fito moja, na unaogopa kuvuka,sasa mimi nimeamua kukushika mkono..ili usije kuanguka,…ina maana unatakiwa uniamini mimi..unieleze kila kitu,bila kuogopa au kunificha ili tuweze kuvuka hadi ng’ambo…itakuwa siri yangu na wewe tu.’akasema

‘Sawa..’nikasema nikiwa sina amani, sikutaka kuendelea kuongea tena, nilihitajia muda wa kutafakari.

‘Mimi nimekuwa nikiifanya hii kazi kwa muda sasa, na wengi walioamua kunielezea ukweli sasa hivi wamepona,wanafanya shughuli zao tu, kwa vile wamejitambua, sasa na wewe kitu kikubwa kwanza ujiamini, ujitambue, uwe na matumaini, kuwa magonjwa yapo, na yana tiba, lakini kwanza uyafahamu, ufahamu masharti yake..nikuambie ukweli, ukiwaona wengine niliwahi kuwahudumia, walikuwa kwenye hali mbaya sana, lakini sasa..huwezi kujua kuwa walikuwa na tatizo…’akasema

‘Kwani ukimwi unadawa, una maana gani ukisema wamepona…?’ nikamuuliza

‘Mhhh…ndio ukimwi una dawa na unaweza kupona…’akasema na mimi nikamuangalia kwa macho ya mshangao nikataka kumuuliza hiyo dawa imegunduliwa lini, yeye akaendelea kuongea kabla sijamjibu

‘Dawa ya UKIMWI,  ni kufuata masharti yake, hiyo ndiyo tiba yake muhimu, dawa nyingine ni za kuongezea nguvu tu mwilini, …lakini muhimu ni masharti yake,…’akasema na kuangalia saa

‘Unamuona Yule mdada anayepita pale…unaweza kumuhisi vipi, ?’ akaniuliza na kunionyesha mwanadada mmoja akiwa mnene, ana afya nzuri kabisa alikuwa akiongea na wenzake kwa furaha.

‘Kumuhisi vipi, kwa vipi…?’ nikamuuliza, na baadaye nikagundua ana maana gani kwenye swali lake nikasema;

‘Mhh, sizani kama anaumwa Yule kwani ni mgonjwa…ameathirika?’nikasema na kuuliza

‘Na wewe ukifuata masharti, …kama una matatizo hayo wanayokuambia unayo, maana hujapimwa, maana hujui au sio, kama hujapimwa huwezi kujiaminisha, yoyote anaweza kuwa nao…na ukijijua ukajitambua, ukajiamini, ukawa na matumaini, …utakuwa vile..’akasema akionyeshea ishara kwa huyo mwanadada.

‘Ni muhimu kwa hivi sasa kwanza ujiweke kwenya nafasi ya kujiona mwenye bahati,..kwanini nasema hivyo…wewe hapa una ufahamu, unaelewa, unapumua, …au sio, una akili ya kuweza kutafakari nzuri na baya,…hiyo ni bahati, …kuna Yule ambaye anapumulia  mipira, hajiwezi ,hajitambui, …huyo ndiye wa tunakuwa na mashaka naye…..umenielewa,..sasa wewe kwanza mshukuru mungu wako kwa hilo,na kwa vile umekutana na mimi, nataka uniamini , mimi nitakushika mkono tutavuka pamoja….je upo tayari kuniamini…?’ akaniuliza

‘Mimi nipo tayari kwa lolote lile..ila siwezi kuamini kuwa ninao, kama wanavyosema watu…sijawahi kupimwa,mimi najiuliza ni  kwanini watu wanishuku tu…..kwani mimi naonekana ni nao, mbona wengi walitembea na huyo jamaa wamepima na wanasema hawana…’nikasema

‘Ni kweli ndio maana nasema wewe huna,…subiria upimwe kwanza, na kama unao usijali, hilo ni tatizo lakawaida,  ni ugonjwa kama magonjwa mengine,…’akasema na mimi nikabakia kimia

‘Nikuulize.unajua ugonjwa wa kisukari, shinikizo la damu, ….na ‘akasema sasa akisimama huku akiangalia saa yake

‘Ndio nimesikia kuhusu magonjwa hayo, wanaambiwa wasile chumvi nyingine wengine sukari, vyakula vya mafuta…’nikasema

‘Ehee, kumbe unajua hayo,…hayo yote ni magonjwa yanawasumbua sana watu, lakini wale wanaofuata masharti  yake wanapona wanakuwa hawana matatizo nayo tena..na ugonjwa huo, wa ukimwi nao kinachotakiw a ni kufuata masharti yake..na sharti  mojawapo , usifanye tena ngono….jitulize’akasema

‘Kwa hali kama hii ni nani atafanya ngono…’nikasema nikijiangalia, huku moyoni nikijiuliza kwanini akazungumzia maswala ya ngono, au ni…..ndugu yake kamwambia awe makini na mimi..

‘Sasa sikiliza wewe kwa hivi sasa utakuwa hapa hospitalini…na karbu kila siku tutaongea na wewe, nataka tufahamiane vyema, …wewe uniamini mimi…mimi niwe rafiki yako mwenza…ili uweze kuvuka huo mto wenye fito moja,…na ukumbuke wewe una ujazito, kwahiyo unatakiwa usijifiirie wewe mwenyewe  tu, fikiria na hicho kiumbe kilichopo tumboni mwako…na kiukweli ukifuata masharti utajifungua salama…’akasema.

‘Lakini pamoja na hayo…huko nilipotoka, madocta waliniambia mtoto amekaa vibaya, kunahitajika vipimo vikubwa…je humu hivyo vipimo mnavyo?’ akaniuliza

‘Kuna vyeti vyovyote umekuja navyo…?’ akaniuliza

‘Vyeti!!!?’ nikauliza kwa mshangao, na hapo nikakumbuka, inawezekana yule mzee na baba mwenye nyumba walikuwa wakinitafuta ili kunipatia hivyo vyeti…nilisikia wakisema hivi vyeti ni muhimu aende navyo…kwa muda ule sikuwa nimejua wana maana gani kusema vyeti, nakumbuka baba mwenye nyumba alikuwa kashikilia bahasha kubwa..oh, sikujua,….kama ningelijua ningelijitokeza,

Nakumbuka nilivyojificha kwenye kile kitu nikiwa nimejifunika baba mwenye nyumba akapita kwenye kile kiti na hakushuku kitu baadaye iakbidi ateremke kwani gari lilikuwa linaondoka, …na sikuweza kujua walichokuwa wananitafutia..

‘Vyeti ulivyokuwa ukitibiwa huko, nilimwambia ndugu yangu akupe uje navyo, akasema atafanya huo mpango huko hospitalini ili vipatikane hivyo vyeti, na utakuja navyo…hukupewa bahasha yoyote, yenye nyeti ndani…?’akauliza

‘Mhh, hapana hakuwahi kunipatia bahasha yoyote au vyeti,…alikuwa kakasirika tu…’nikasema

‘Basi usijali , kila kitu kitaenda vyema tu,hapa umefika, …japo kiukweli hii hospitali ni ya pesa, ila kuna udhamini wa magonjwa maalumu ambapo tunategemea misaada, na mimi ni mmoja wa watu wanaousimamia hilo..’akasema

‘Kwahiyo kuna malipo yanahitajika, kwanini nisiende Muhimbili, niliambiwa niende huko..’nikasema

‘Ikibidi utaenda huko..ila nilihitajia ukae hapa ili niwe nawe karibu,kuna mambo nafuatilia, tunafanay utafiti wa magonjwa, namahusiano yake na maisha ya watu,…vyanzo vyake,na jinsi gani ya kupambana na maambukizi,..’akatulia

‘Kwahiyo mimi nitajitahidi kukusaidia, ila tusaidiane, ..ukificha, unajiumiza mwenyewe, na ufuate kile ninachokuambia, nikisema usifanye uache…unasikia haya ni kwa manufa yako,..kitu ambacho sitapenda, ni wewe kuwa mkaidi na kuwa msiri…niambie kila kitu ili iwe rahisi kwangu kufuatilia, na kuhakikisha unaondokana na hilo tatizo…’akasema

‘Kwahiyo hapa kuna hivyo vipimo, vya kuonyesha kuwa mtoto kakaa vipi na jinsi ya kumweka sawa…?’ nikamuuliza na yeye akaniangalia kwa macho ya udadisi, halafu akasema

‘Ndio …hivyo vipimo vipo…usijali….ndio maana ndugu yangu akafanya juhudu uje tuonane…hapa umeshafika kila kitu kitakuwa shwari, usijali, je  utaniamni…?’ akaniuliza huku akitabasamu, kiukweli alijulia kuonyesha hisia za usoni, tabasamu lake liliweza kukufanya umwamini tu.

‘Ndio nitakuamini…lakini nitakuwa na amani pindi nikipata vipimo vyangu na kuambiwa ukweli kuhusu mtoto wangu…je kwanini wanasema kakaa vibaya…’nikasema

‘Usijali….wewe sasa pumzika…na madocta wanasema walishachukua damu yako,na pindi wanaweza kuja kukupa dawa, ..na mengine tutaongea nao nikirudi, huna haja ya kuwauliza maswali mengi, maswali mengi nitawauliza mimi na mimi nitaweza kukupatia majibu yenye kukusaidia…’akasema

‘Ina maana nisiwaulize chochote, kama wakileta vipimo, kuwa mtoto kakaa vibaya….?’ Nikauliza

‘Usiwaulize chochote,…wanaweza kuuliza maswali ya kawaida tu,…umenielewa, madocta wana sehemu yao,… si unajua madocta wengine wanaweza kuongea ukatishika…lakini mimi nimesomea kuongea na wagonjwa wakahisi vyema…kuanzia sasa mimi ni wakili wako wa haya matatizo, mimi ndiye nitakuongelea kwa niaba, hilo la mtoto kukaa vibaya sio tatizo, na wala usijali,…sawa…’akasema na kuanza kuondoka

‘Sawa…’nikaitikia na akaondoka, mimi nilibakia kujiuliza, iweje yeye anasema hilo la mtoto kukaa vibaya sio tatizo, wakati huko nilipotoka walikuwa wakisema ni tatizo kubwa na nisipowahishwa kurekebishwa naweza kupata matatizo, na kumpoteza huyo mtoto, na mimi maisha yangu yatakuwa hatarini…niliwaza sana hilo,na nikasema kimoyoni;

‘Mimi nitawauliza madocta nijue ukweli…., hata kama yeye kasema nisiwaulize, kwanini nisiwaulize wakati mimi ndiye ninayeumwa ….nitawauliza tu,ili nijue huyo mtoto kakaje, na kwanini damu inapungua mara kwa mara, je ni kweli mimi nimeathirika…ngoja waje,….’nikasema

Na baadaye kidogo  madocta wakafika, walikuwa wawili…


WAZO LA LEO: Kuishi vyema na salama, ni pamoja na kujitahidi kuwa na tahadhari na vile vitu vyenye kuathiri afya zetu.Kama kuna walakini na kitu, vyakula, vinywaji na miendendo yetu ya kila siku basi hata maisha yetu yatakuwa na walakini. Vyakula. Tukichunguza kwa makini, vyakula, vinywaji  na matendo yetu yamekuwa ndio sababu ya kuathiri afya zetu, tujaribu kufuata masharti,  kula vyakula bora, na kutenda yaliyo mema, ili iwe sababu ya kufaulu kwetu.
Ni mimi: emu-three

Ni mimi: emu-three

No comments :