Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeFriday, March 4, 2016

SIKIO LA KUFA HALISIKII DAWA-14 Mke mtu alipofika chumba cha mdada hakupiga hata hata hodi akasukuma mlango na kuingia ndani, akamkuta mdada akiwa kainama akikunja nguo tayari kuweka nguo hizo kwenye mfuko aliokuwa nao… na mdada aliposikia mtu akaingia ndio pale aligeuka na kumuoana mwenyeji wake, mama mwenye nyumba…..Tuendelee.

Mke mwenye nyumba alipoona ile hali hata yeye ilimshitua kidogo, akijiuliza huyu mtu ana nini,  kwanini huyu mdada anamuangalia kwa macho ya uwoga, tena ni kama vile anataka kupiga yowe,kukimbia  na huku anarudi kinyume nyume….kwanza alitulia pale mlango akimtizama tu, akihisi kuwa huo unaweza kuwa ni usanii tu, baadaye akaingia ndani, huku akisema;

‘Haya wewe mtu,…mwizi wa waume za watu , Malaya….naona nikuite hivyo, maana hatua uliyofikia unadiriki kuitwa hivyo….’akasema na sasa akiwa keshaingia ndani kabisa.

‘Sijui kwanini unaigiza kuniogopa, …mbona jana wakati mnashikana na mume wangu, ulikuwa huogopi , pale nilipowafuma ndio ilikuwa sehemu ya kuogopa,…sasa hivi waogopa nini, kuwa nimekuja kukupiga,….hahaha, kupigwa utapigwa, lakini sio mimi…..ila ikibidi, ukijifanya mkaidi, sitasita kufanya hivyo…’akasema huku akitikisa kichwa

‘Wazazi  wako mwenyewe walikushindwa, wakatupiwa dunia,…na watu, jamii nayo sasa inakushindwa, uone jinsi gani ulivyo kinyaa, tabia hiyo ni mbaya, sijui kwanini mnajiabisha kwa mambo hayo, binti mnzuri kama wewe…ooh, kweli kila kizuri hakikosi kasoro…ok, mimi sitaki nikuambie mengi maana muda unakwenda mbio, walishakuambia wengi, lakini masikio yako yamekufa……ila ninachotaka kusema kwako hivi sasa ni kuwa unaondoka…’akasema

‘Muda wako wa kukaa hapa umekwisha….., kama uliona hapa ni gesti ya kufanyia ufusuka wako , sasa umekwisha, …hatuhitaji malipo yoyote kutoka kwako, …kwenye madanguro si mnalipia, hapa umekaa bure tu…..sasa unaondoka ….’akasogelea hatua chache kunikaribia, na mimi bado ile hali ya kuogopa, ile ndoto ilikuwa bado inanicheza kichwani nikashtuka pale aliponyosha mkono, na yeye akashituka pia.

‘Vipi wewe…ndio usanii gani huo, …hahaha, hata ufanye visa gani utaondoka tu…, hii hapa ni teketi yako ya kusafiria, na huu ni mkoba wako utawekea nguo zako, chukua kila kilichokuwa chako kinachokuhusu uondoke nacho,mimi humu ndani , sitaki kuona dalili yoyote ya mtu kama wewe, maana nikiiona nitatapika…’akasema akiwa kamkazia macho mdada

Mdada sasa akili ikakaa sawa akanyosha mkono kupokea kile alichopewa, kaambiwa ni tiketi, lkini tiketi ya nini, …kijijini kwao hakuhitaji tiketi, tiketi unapewa ndani ya gari…akaipokea hiyo tiketi na sasa alikuwa akitaka kunyosha mkono kupokea  hilo begi la safari….

Lilikuwa begi kubwa tu,…moyoni akafurahi,…hata hivyo angefanya nini, hakuwa na jinsi,alishukuru, lakini hakuweza kutamka neno kwa muda huo, …alipindisha macho kuungalia mkoba aliokuwa nao,ulikuwa umechakaa, na ni mdogo, …hata hivyo, akajiuliza hiyo tiketi ni ya kwenda wapi, lakini hakufungua mdomo,….hakuikagua ile tiketi kwa muda huo kwanza, akatulia.

‘Wewe ulifikiria mimi nitaondoka nikuachia mume, nikuachie nyumba yangu,unajua imejengwaje hii….hahaheee, ndio ilikuwa lengo lako au sio….hahahee…umenoa….’akasema

‘Nikuambie kitu huyo mume ni mume wangu wa ndoa,..na wewe nenda ukatafute mume wako hata kama ni hawara, lakini sio hapa…nikishauri kitu, mume hatafutwi kwenye majumba ya watu,kwenye ndoa za watu…mume mwema anakuja kwenu kukuchumbia sio wewe ukamtafute..huko nikujizalilisha…’akatulia

‘Hata hivyo,…labda nia yako ilikuwa hiyo…kuusambaza..ndio unalipiza kisasi au sio…na  sijui mlifikia wapi,…hawa wanaume jamani, mbona wanataka kutuua ninachojua ni kuwa mlishaingia kwenye mahusiano, kwahiyo uwezekano mkubwa kuwa umemuambukiza huo ugonjwa uliona nao ni mkubwa, tutakwenda naye akapime….’akatulia

‘Hata hivyo, siwezi kuvunja ndoa yangu kirahisi hivyo, ila kama kaathirika, basi sitasita kuachana naye, …ila kwa hivi sasa ni lazima nilinde ndoa yangu, hadi hapo nitakapothibitisha hilo,….ni lazima akapime…’akasema

Hapo mdada alitaka kusema neno, alitaka kumkemea kwa kauli kama hizo, hilo la kusema yeye kaathirika kalipatia wapi…lakini akaona atulie kwanza, ….hakutaka shari,hata kama angelitaka shari nguvu za kuongea, kupambana angezipatia wapi,mwili ulikuwa kama sio wake..akahisi machozi mawili yakitoa machoni.

Mke mwenye nyumba hakujali ile hali,hakujali hayo machozi akaaendelea kuongea…

‘Sasa sikiliza mimi sio mnyama kihivyo…sina chuki nawe kihivyo….hapana,, najua utanielewa vibaya, na haya machozi ni ya kinafiki mimi hayanitishi, kama ungelikuwa umewahi kuolewa ungeleewa jinsi gani nimeumia, lakini….shukuru mungu , sijui hasira zangu zilikwenda wapi….’akatulia

‘Yaani we acha tu…ila nilikionea huruma hicho kiumbe, hakina hatia masikini ya mungu wenye hatia ni wewe na hao mabwana zako…moyoni nimechukia, ….kwa hayo matendo yanayohatarisha uhalali wa ndoa yangu, …mimi kama mke lazima niilinde ndoa yangu kwa kila hali,…’akatulia

‘Unajua nilipokuona siku ile ya kwanza…pamoja na huruma, lakini mwili wangu ulisisimuka,….sijui kwanini, hisia ziliniambia kuna kitu…sikuweza kukuamini kabisa, nilikubali tu tukae pamoja, ili tuweze kukusaidia hadi hapo utakapojifungua, lakini za mnafiki hazicehelewi, …ukaanza kuonyesha makucha yako,…..na tena ukazidisha hadharani unakumbatiana na mume wangu,….wewe ni nyoke, ..na hakuna anayaweza kukaa na nyoka nyumbani kwake….wewe ni kunguru  asiyefugika,….na nimesikia hata wazazi wako walisema wewe ni sikio la kufa…’akasema sasa akiwa ananiangalia moja kwa moja usoni.

‘Sasa kwa kukuthibitishia kuwa mimi sina roho mbaya, nimefanya mambo ya kiutu, kiubinadamu,…mimi kwa pesa zangu nimewasiliana na dada yangu, yupo huko Dar, yeye anashughulikia kitengo kimoja cha walioathirika, yeye ni mtaalamu wa mambo hayo, …nimeongea naye akasema usafiri uende kwake, atatafuta namna ya kukusaidia, yeye ni kazi yake,analipwa kwa kazi hiyo, ana mume, sasa uende ukatembee naye, ….’akatulia

‘Nikishauri kitu kama dada yako, ukifika huko,acha tabia hiyo mbaya, uwe na lengo moja, kujiokoa, kuangalia afya yako,…ili uzao kwa amani….yeye anajua jinsi gani ya kuishi na watu kama nyie, najua atakupa ushauri nasaha, na watafanya taratibu za kuhakikisha unajifungua salama….’akatulia

‘Huyu mume wangu niachie , nitajua jinsi gani ya …….Najua,najua tu…utakuwa umemuambukiza mume wangu inaniuma sana…tumetoka naye mbali, kajituliza miaka nenda,leo hii, kakutana na wewe …siwezi kukusamehe….kama nikisia naye anao….sijui…, mungu mwenyewe ndiye anajua zaidi, lakini, ……aah, we nenda tu…’akasema

Aliposema hivyo, nikaichunguza ile tiketi, kweli ilikuwa ya kusafiri kwenda Dar, na muda wa kufika kituoni ulikuwa unakaribia,…nilishindwa hata niseme nini…nikataka kuinama sasa kuendelea na kupanga nguo kwenye huo mkoba, na yeye akaendelea kuongea.

‘Haya fanya haraka,  muda umekwisha,  weka nguo zako humo kwenye mkoba huo, achana na huo uchafu wako,….tutatupa jalalani…., ila…, nakuomba,…tena sana, usije kufanya ujanja, badala ya kusafiri ukashukia njiani na usije kukanyage tena hapa kijijini, maana popote nitakapokuona nitakupigia debe mpaka uondoke, wewe hufai….wewe ni nyoka mwenye sumu…’akasema na kunisogelea, akinisaidia kuweka nguo kwenye mkoba,kwani nilikuwa siwezi kuinama vyema.

Nguo zikawa ndani ya hilo begi,sasa naanza kuhisi vibaya,…..nahisi kutapika,kizungu zungu, lakini nikamuomba mungu niondoke tu humo ndani,….nikawa sasa nataka kwenda angalau kunywa maji,yeye akasema, akinikabidhi karatasi, …

‘Hii ni ramani itakusaidia kufika eneo, sio sehemu ya kupotea, lakini ni kwa tahadhari,…ila ukiona huelewi, ni bora uulize watu watu, na hapa nimeandika namba ya simu ya huyo dada yangu kasema kama atapata nafasi atakuja kukupokea, vinginevyo,ukifika pale ubungo, tafuta mabasi ya kwenda Sinza…huko kuna ofisi yao ndogo na ndipo utafikia kwa muda…’akasema

Humo kwenye karatasi kuna maelekezo yote…na kwa kukuonyesha kuwa mimi sina roho mbaya kama wewe, nimejitolea kukupa simu hii ndogo, ninakupa  ni yako na hiyo namba nimeandika hapa, hii hapa…’akasema akionyesha hiyo namba

‘Na zaidi….hii ni pesa kaitoa mume wangu, wakati nakuja huku kanikimbilia akanipa,…mimi nilitaka usipewe hata senti moja, lakini ubinadamu umeniingia…. sina roho mbaya kihivyo…..chukua hii pesa itakusaidia mbele ya safari,  zaidi ya hapo tusijuane…usije kukanyaga tena hapa, hili nazidi kukusisitizia, haya safari njema….’akasema na kuchukua hilo begi akatangulia nalo nje.

Pale nilipo mwili haukuwa na nguvu,….kiuono kimekakamaa….nikijaribu kuinua mguu inakuwa shida,nikatulia kwa muda nikimuomba mungu, lakini awapi…nilihisi kitu kikakata tumboni,…nilihisi maumivu makali, nikapiga ukulele wa mara moja

‘Aaaah…..’

‘Wewe mdada , toka humo ndani haraka,  usitake niingie humo, nikutoa kwa mapanga … tunachelewa…’sauti ile ilikuwa kama ina nguvu Fulani, hasa alipotaja panga,na mguu ukaweza kuinuka,..nikaanza kujikongoja kuelekea nje….kila hatua ilikuwa ni taabu, giza lilishaanza kutanda usoni

                             ***********

Nina uhakika kama asingeliwahi kunishika ningeanguka na sehemu ile ya mlango ukitoka nje kuna ngazi za nyumba, ..hapo ndipo nilihizi kabisa nimepotewa na fahamu, nilichoshtuka nacho ni mtu kuja kuniwahi na kunishika halafu akanishika mkono..

‘Taratibu mama….kuwa mwangalifu hizi ngazi ni hatari..’ilikuwa sauti ya mume mtu.

‘Nani kakuambia uje huku,…nilishakuambia haya hayakuhusu, wewe nenda kamsubiria mzee, ….huyu anakwenda mwenyewe…na hii bajaji itamfikisha kituoni…’akasema

‘Kwa hali kama hii, sizani …ngoja nimpeleke..’akasema baba mwenye nyumba, na mama mwenyenyumba akaja na kunishika mkono , akawa kama ananikokota hadi kwenye bajaji,akanisikumia niingia halafu na yeye akaingia

‘Haya mimi nitampeleka mwenyewe…wewe kamsubiri e mzee….’akasema na kumuamrisha mwenye bajaji aondoke tuwahi kituoni.

Kiukweli hali ilikuwa mbaya,..hadi tunafika kituoni ilikuwa kama nipo kwenye njozi..maumivu,kujisikia vibaya ndivyo vilitawala akili yangu. Na Tulipofika,gari lilikuwa limeanza kunguruma na kupiga honi.

‘Haya haya..gari lile kule linaanza kunguruma,…unaona tungelichelewa, akasema mama mwenye nyumba huku akichukua mkoba na kuanza kutangulia nao, mimi nilitoka pale kwenye bajaji kwa shida, na aliyenisaidia ni dereva wa  hiyo bajaji,…akanishika mkono.

‘Hivii hii kweli hii safari utafika,..unaenda kutibiwa nini..maana hii hali usingelitakiwa kusafiri..’akasema dereva wa bajaji akinisaidia, na mama mwenye nyumba alipoona ile hali akasimama mapakatukamfikia, akanishika mkono na kuanza kunikokota.

Tulifika kwenye basi nikaingia ndani…alihakikisha nimekaa kwenye kiti changuu , ndio akasema;

‘Haya sasa safari ndio hiyo….ufanye ujanja wako utoke mimi sitakusamehe kwa hilo, na ujikaze mwanamke wewe,unajilegeza, unataka nani akuonee huruma, wakati unastarehe na mabwana zako hukulijua hili…’akasema kwa sauti mpaka watu wakageuka kuniangalia. Yeye hakujali akateremka na kupanda ile bajaji kurudi nyumbani kwake.

***********

Nilibakia ndani ya lile basi lilikuwa bado lipo kwenye mwendo wa kutaka kuondoka. Mimi nikaanza kujiuliza huko Dar wanapotaka niende, nitaishije,…si ndio itakuwai ndani ya familia ya mke na mume kama huku, au nitakuwa sehemu gani,  …ni sawa nitakutana na huyo mtaalamu kama walivyotaka wao, sijui wa nini,…?

Je huyo mtaalamu atanipokeaje, maana atakuwa keshapandikiziwa ubaya mwingi…ina maana ataishi kwa mashaka akiwa haniamini..

‘Hapana  siwezi kwenda kuzalilika tena….’nikasema lakini nikajiuliza nifanyeje mimi , maana kwa hali niliyo nayo,sina mbele wala nyuma, sina jinsi yoyote ya kujitegemea, kwahiyo mimi ni ….’nikatulia nikiangalia nje, nilishangaa kuona basi haliondoki …labda kuna jambo limetokea…

‘Mhh…’ niliguna maana nilikuwa sijisikii vyema, nilitaka angalau nijilaze ninyooke, lakini kwenye kiti unakaa kwa shida. Ile hali ya kukaa kusubiri  ilinichosha, nikaona Napata shida, isitoshe sikupendelea kwenda huko.

Mwishowe nikaona nighairi,…labda nirudi kijijini kwetu tu…lakini hilo halikutulia, nilishaapa sitarudi tena  kijijini kwetu mpaka niwe nimejifungua,….sikutaka kukutana na wazazi wangu katika hiyo hali….lakini hata hivyo nilitaka kukutana na hao wanaume wanne walioniharibia maisha yangu, na sasa wamekuwa wakinitangaza kwa ubaya..

‘Hawa watu ni lazima nije kukutana nao…’nikasema kwa sauti kidogo

 Ni kweli nilihitajia sana kukutana na hao wanaume wanne wanijibu  maswali yangu,… ilikuwaje,…na pili nionane na huyo aliyekuwa mchumba wangu, kwanini kanifanyia hivyo, najua uchumba  haupo tena kwani ameshaoa,  lakini kuhusu hiyo siri….au niende polisi,…wakafungwe tu,….lakini nikifanya hivyo hata mimi nitahusika…

‘Potelea mbali, hata mimi nikihusika lakini nitakuwa nimetubu, nitakuwa nimejikosha, …hawa watu sio wakuhurumiwa,…mhh, mimi huko Dar, siende, ngoja nikaonane nao niwaambie naenda polisi,…lakini ni lazima niwe na ushahidi, na ili niwe na ushahidi ni lazima nionane na hao wanaume wanne…’nikasema nikaanza kusimama.

Bahati nzuri jirani wa kiti change alikuwa hajakaa kwenye kiti chake, kwahiyo niliweza kusimama japo kwa shida…nikajisogeza ili kutoka pale lakini kitu kikaniambia niangelia dirishani kwa nje,…nikashtuka

Nje ya gari,  nikamuona yule mzee aliyejitolea kunidhamini akiwa na mume mwenyenyumba ,walikuwa wakiangalia huku na kule, sijui walikuwa wamekuja kufanya nini…nikarudi kwenye kiti change na kuende;ea kuwachunguza kwa macho.

Walionekana wakitafuta kitu , na mara nikawaona wakija kwenye hili basin a kuingia  na mimi kwa haraka nikachukua khanga nikajitanda sehemu yote ya uso,kama kujifunika gubi gubi kinamna ambayo mtu hawawezi kunigundua kirahisi…nikakaa na kutulia

Jirani yangu wa kiti naye alishafika na jinsi alivyokaa aliweza kunikinga vyema …..Hawa jamaa wawili wakaingia kwenye lile basi, nilisikia kabisa wakinitaja na kuanza kukagua kwenye viti  kwa macho wakiwa wamesimama pale mlangoni, na kwa muda gari lilishaanza ile hali ya kutaka kuondoka, nilimuona Yule mzee akiongea na kondakita;

‘Mbona simuoni….’akasema mume mwenye nyumba

‘Una uhakika ni gari hili au yapo kwenye gari la pili..?’ akauliza mwenyekiti

‘Ni hili hili… ngoja nikague vyema,…’akasema mume mwenye nyumba, akaamua kutembea ndani sasa akikagua kiti kimoja kimoja na yule mzee akabakia pale mlangoni akiendelea kuongea na kondakta na otingo wa hilo basi.

NB: Haya ndio mwanzo wa maisha mengine yam dada au kuna nini kitatokea, tuwepo kwenye sehemu ijayo


WAZO LA LEO: Uwongo , kusingiziana ubaya kwa minajili ya kupata au kushinda kwenye jambo lolote ni sawa na wizi, ukumbuke kuwa hiyo ni sehemu ya dhuluma, na kamwe dhuluma haidumu, ipo siku utalipizwa, acha,….na kama una tabia hiyo tubu na mrejee mola wako kabla kitabu chako hakijafungwa.

Ni mimi: emu-three

1 comment :

Anonymous said...

duuuh