Nilimtizama aliyeingia pale mlangoni jicho la kwanza lilitua
kuangalia kile alichokibeba,….hisia zilikwenda mbali sana, akili yangu haikuwa
sawa, …mawazo, na hisia zangu za kwanza, nikajua sasa ni shari, akili ikajenga taswira ya hofu, ….woga ,
ukanitanda…akili ikaona hivyo , kile kilichotokea nikajua ndio hicho….ubongo haukuona hali halisi uliona taswira , tukio la
usiku,….
Aliingia mtu, ….na mtu huyo alikuwa kajifunika usoni, lakini
baadaye akaondoa ile nguo….mimi sikuweza kumuangalia usoni moja kwa moja,
niliangalia kile alichokuwa kakibeba,…..silaha…kwa muda ule nilikuwa nipo peke
yangu chumbani, nikitandika kitanda!
Nilichofanya nikuachilia kile nilichokua nimekishika, na
kuanza kusogea nyuma, nikitaka kupiga yowe, lakini sikuweza kufanya hivyo, mdomo
ulikuwa mkavu, kiu na njaa vilikuwa vimeniandama…kwahiyo hata sauti haikuweza
kutoka, ilibakia kufungua mdomo tu,…
Nilisogea kinyume nyume, na huyo aliyeingia akawa kasimama
pale pale mlangoni, ni kama kunipima au kunizidishi aliendeela kasimama kwa muda huku akinitizama mimi…lakini cha
ajabu mimi sikutaka hata kuangalia uso wake…ili nilijua ananitizama mimi…macho
yangu yalikuwa yakitizama ile silaha;
‘Mhhh, naona unaogopa eeh…hahaha, kumbe na wewe ni mwoga
eeh…’akasema huku akicheka, na alipocheka ndio nikamtizama, maana kicheko chake
kilikuwa kama mwangwi..ooh, huo mdomo, oh, hayo meno….na kila akicheka meno
yake yalionekana kama ya shetani , na nilipoona hayo maumbile ndio nikazidishia
kuwa na wasiwasi, woga…yeye alikuwa bado kasimama pale pale mlangoni.
‘Mimi naona ajabu sana,inawezekanaje utembee na mume wa mtu na
tendo hilo ni hatari zaidi ya hii silaha, na hukuogopa, ….eeh hebu nambie,
maana tumeambiwa mke wa mtu au mume wa
mtu ni sawa na kaa la moto huwezi kulifumbata mkononi….lakini wewe uliweza, huogopi,
.sasa iweje, kuiogopa silaha hii, hii ni kitu zaidi ya tendo hilo, ….’akasema
sasa akiizungusha hewani ile silaha.
Nilitaka kumwambia mimi sijatembea na mume wake..na wala
mume wake simjui, lakini sikuweza kutamka neno….mdomo umefunguka, lakini sauti
haitoki….
Akaanza kusogea kuingia ndani, huku akitikisa kichwa huku
akichezesha ile silaha kuonyesha jinsi ya kuitumia, naona lengo lake ilikuwa
kunijenga hofu tu… huenda hatanidhuru…nikajipa matumaini.
‘Nikuambie ….basi kuhusu hii silaha, unaona ilivyo tofauti
na silaha nyingine... ‘akainua juu na
kila ikifika hewani inameta meta kuonyesha yale makali yake. Ungeliweza kuona
yale makali yake na kuyahisi…nikahisi kuwa yaweza kuukata mwili wangu, na hapo mwili
ukasisimuka.
‘Siku mimi naolewa, nilipewa silaha hii na babu yangu, babu
yangu alinipenda sana, kwasababu ,mimi nilikuwa jasiri yeye alipenda kuniita
mke-dume, sikuwa napenda sana kucheza na wanawake wenzangu mimi nilikuwa
napenda kucheza na midume, na nilikuwa napambana nayo kidume. Ndio maana muda
wote nipo kama dume…sio ….lege lege..si unaniona, akainua mkono ulioshika hiyo
silaha kiujasiri.
‘Nashukuru kuwa babu
yangu aliweza kuishi hadi kuhudhuria ndoa yangu na siku naolewa ndio nikashangaa
ananikabidhi silaha hii…, akaniambia mjukuu wangu mimi sina cha kukupa, ninachoweza kukupa ni silaha
hii…’akatulia na kuinua ile silaha hewani.
‘Silaha,!!! Silaha ya nini babu…?’ nilimuuliza
‘Ya kulindia ndoa yako….usikubali mtu aiharibu ndoa, yako,
na muhimu kata magugu na mizizi kabla mtu haujashika chini…hakikisha unangoa na
mizizi yote…’alisema hivyo kimifano….mhh, unajua sikumuelewa kipindi hicho,
kipindi hicho ningeelewa nini zaidi ya kuolewa,…nilijua ndoa ni ndoa tu, najua
huko ni upendo tu, hakuna chuki, hakuna wabaya kama nyie, ….hata nilipofika kwa
mume wangu sikuwa nimeelewa ni nini lengo la babu kunipa silaha hii na maneno
yake.
‘Lakini siku nilipowafumania, …..kumbukumbu za kauli ya babu
zikanirejea...nilishaisahau, kumbe, silaha hii ilitakiwa ifanye kazi yake, na
unajua silaha hii niliiweka kwenye vifaa visivyotumika nikawa nimeishahau,
nilipokumbuka tu nikaanza kuitafuta nilihangaika sana kutafuta hii silaha, na
mara nikaiona…siku nilipowafuma, sikuwa na …kumbukumbu hii, ila leo nimekumbuka…’akasema
‘Kunifumania…!’ nilisema kimoyo moyo..
‘Sasa natumai wakati wakuifanyia kazi silaha hii umefika,
bado sijachelewa..…’akasema na sasa akaingia ndani, na mimi nikazidi kurudi
nyuma nikiogopa, ..na yeye akaniangalia kwa macho yaliyojaa chuki, …chuki kweli ya kuua, ….alinikazia
macho halafu akasema:
‘Unajua ….sisi wanawake ni wema sana, lakini ikifikia kwenye
chuki, chuki ikatawala nafsi zetu ….mioyo yetu inageuka kuwa mibaya sana, roho
mbaya inachukua nafasi…na mwanamke akiwa na roho mbaya anakuwa mkatili kweli,mimi
sikuwa na roho mbaya, lakini kwasababu
yako sasa nina roho mbaya…wewe hujui tu, hivi sasa nakuchukia,..unajua
kuchukia,…nakuchukia…’akasema na sauti yake ilikuwa kali mpaka nikahisi kichwa
kikiuma.
‘Sasa nataka kuhakikisha silaha hii inamaliza hasira
zangu,…wewe unatembea na mume wa mtu, halafu umeshamwambukiza ukimwi , ….ili na
mimi aniambukize…hahaha…sasa kabla sijaambukizwa nataka kwanza wewe ufe…’akasema
akinisogelea.
‘Ukimwi….! Mimi nina ukimwi….?’ Nilijiuliza kimoyo moyo,
sasa akawa anasogea kunikaribia
Na mimi nikawa nasogea kinyume nyume mpaka ikafikia sehemu siwezi
tena kurudi nyuma, kukawa na kitu kimeziba kwa nyuma, …sijui ni ukuta au…sikutaka
hata kugeuka nyuma, niliogopa nikigeuka nitavyekwa na ile silaha nikabakia
kutoa macho tu ya uwoga,..alipokuwa hatua chache kutoka nilipo, ni karibu sana,
akasimama na kusema;
‘Unajua hadi sasa najilaumu, ni kwanini sikufuata usia wa
babu,sasa ni lazima nifanye hivyo, nikate shina kabla halijaweza mizizi, na
hatimaye ning’oe mizizi kabisa (akainua
lile silaha juu kama anataka kuitumia)
Akanisogelea sasa akiwa kainua ile silaha juu….
Nikafunua mdomo kutaka kupiga yowe, …lakini mdomo
haukufunguka….yeye sasa keshapandisha hasira anakuja kwa kasi kunikabili…nikajua
kweli kadhamiria nisipojitetea huyu mtu kweli anaweza kunidhuru, aliponijia kwa
kasi, huku silaha ipo juu nikajitutumua na kusogea pembeni, huku nikitumia
mikono yangu miwili kumsukuma pembeni. Ilikuwa nusura ya mungu tu,…akapepesuka,
na kwenda upande.
‘Kumbe…wajifanya mjanja sio, ngoja sasa nikuonyeshe, na ole
wako upige yowe, sasa hivi hakuna wa kukutetea, sitakubali kamwe kuingiliwa, ni
lazima nikuumize…kabla hujaondoka, nataka nifyeke magugu yote,nakutoa na
mizizi, na kuhakikisha kuwa hutaweza kuota tena…..’akasema na sasa akaishusha
ile silaha kuelekea kichwani nilikwepa
na nikakoswa koswa na ile silaha akanikate begani, nilihisi maumivu makali kweli. Nilijua
bega limetoka!
Silaha ile ilikuwa ni aina ya panga, lakini ni
nyembamba…kama jambia…
Alipokuja kwa kasi safari hii, kutokana na maumivu kwenye
bega sikuweza kumzuia , sikuweza kumsukuma kama awali, akaniweka kwenye usawa
wake,….macho ya ukatili, ya uuwaji yakawa yananiangalia moja kwa moja usoni…huku
akiwa kainua ile silaha juu, silaha ile ikawa inakuja sawa sawa na paji langu
la uso, niliyaona makali yake …nikajua sasa nimekwisha, kichwa sasa
kinapasuliwa vipande viwili….
Na mara nikasikia sauti ….oooh, nilikuwa usingizini, nikazindukana…kumbe
nilikuwa naota..na hapo nikasikia mtu akigonga mlango wa nje, kumbe ilikuwa ni asubuhi, kumbe ilikuwa ni ndoto ya
kutisha, nikakumbuka tukio la jana,….oh, nilipokumbuka hilo tukio niikamuka haraka,
nikijua natakiwa kuondoka hapo nyumbani,…
‘Hii ndoto ina ishara mbaya…’nikasema
**********
Aliyekuwa kasimama mlangoni ni mama mwenye
nyumba,….akinitizama kwa udadisi, akaniona ninavyoogopa,…nilivyo na wasiwasi,
nikiwa na uwoga usiofichika….akatikisa kichwa kama kunisikitikia vile au
kunidharau..
Kumbe wawili hawa hawakuwa bado wameelewana, japokuwa mzee
alipoondoka alikuwa kawaweka sawa, lakini mzee alipoondoka mume alianza kuongea
na ndio ikawa sababum mke mwenye nyumba akataka nifukuzwe humo ndani haraka
iwezekanavyo, lakini mume mwenyenyumba akasema ni bora wasubiria maamuzi ya
kikao
‘Mzee kasema tusubiria maamuzi ya kikao, kama tutamfukuza
tutakuwa tumempuuza, subiria kwanza..’akasema
‘Je kikao kikiamua kuwa aendelee kukaa humu mpaka ajifungue,
unafikiri nani ataweza kuishi na mtu kama huyo….nani atamuhudumia, unajua watu
kama hao wanahitajia huduma zao tofauti…hapana mimi siwezi kukaa naye tena,
najua unamtetea kwa vile keshakuwa hawara wako..’akasema mke mtu.
‘Kwani kuna tatizo gani ukimsubiria huyo mzee..?’ akauliza
mume mtu
‘Mimi nilishaweka mipango yake tayari…’akasema
‘Mipango gani…mke wangu..?’ akauliza mume mtu akionyesha
mshangao
‘Huyu mtu anatakiwa kuondoka hapa nyumbani haraka,…akiondoka
ndio tunaweza kusikilizana mimi na wewe la sivyo, msimamo wangu utakuwa ule
ule..unipe talaka yangu….’ akasema
‘Mke wangu maswala ya talaka achana nayo, mimi ninachoona
cha muhimu tunamsubiria mzee arudi, yeye ndiye atatuambia la kufanya..najua
kikao kitaweza kutafuta ufumbuzi wa haya na mambo mengine ya ndani hayana tija
kuyaongea kwa watu….mimi sivyo kama unavyofikiria wewe…..ilitokea tu..kana
nilivyosema awali, na wewe ulifika muda nikiwa namtuliza alale…..’akasema mume
mtu
‘Sikiliza mimi siwezi kurudi nyuma, kwani tulikubaliana au
sio, mengine ni yenu, na niwaambie kitu, huyu hapa anaondoka, na ahame kabisa
hiki kijiji, maana nikimuona nitakumbukia, na hata watu watanicheka,
nimeshachukua maamuzi na ni lazima yafanye kazi…’akasema mke mtu
‘Kwani mke wangu una haraka gani, huyu mtu ataondoka kama
ulivyotaka wewe, lakini hatuwezi kumfukuza kama mwizi….tujaribu kuwa
waungwana..’akasema mume mtu
‘Waungwana eeh, nyia mliyokuwa mkiyafanya mlifanya kiungwana
eeh, huo ndio uungwana sio….?’ Akasema
‘Haya hebu niambie wewe unataka tufanye nini….?’ Akauliza
mume mtu alipoona mke kadhamiria
‘Kama nilivyokuambia mimi nilishamuandalia huyu hawara wako kila
kitu,…anatakiwa kuondoka, tena sasa hivi, hata tiketi yake ya kusafiria
nilishaiagizia kwa simu….siwezi kusubiria tena, …
‘Unakumbuka yule mtu aliyekuja kugonga mlango asubuhi asubuhi ni wakala wa usafiri,
alileta tiketi ya basi, ….sasa haya ya kumsubiria huyo mzee yatachelewesha,
muda unakwenda na mzee hajarudi, sijui wameamua nini huko, …vyovyote iwavyo
huyu mtu anatakiwa kuondoka, na tukiendelea kusubiria hapa huyu mdada atakosa
usafiri na pesa yangu itapotea…’akasema
‘Mke wangu tiketi ya kwenda wapi…?’ akauliza mume mtu kwa
mshangao
‘Anakwenda huko kunakomfaa, anakwenda sehemu ambayo najua
atapata huduma zinazomstahiki….’akasema
‘Mke wangu…..’mume akatakakuongea lakini mke akasimama
akaingia chumba kingine na mara akatoka, akiwa kashikilia begi la safari..’
‘Mimi nataka kukuonyesha kuwa mimi namjali huyo hawara wako kuliko
nyie, wewe kinachokuongoza hapo ni tamaa zako za kimwili, lakini mimi
kinachoniongoza hapa ni upendo wa mstakabali wake wa baadaye..jinsi
tutakavyoweza kumsaidia huyu ili aweze kusogeza siku zake za kuishi, na hicho
kiumbe huko tumboni kizaliwe kikiwa salama…’akasema mke mtu
‘Unajua mke wangu, hayo mnayozaungumza ni maneno ya kusikia
tu..hayana ushahidi, …na nikuambie kitu, kauli hiyo ya kuwa kaathirika, ni bora
usiiongee kabisa una uhakika gani, ….je kama sio kweli, huoni mtakuwa kwenye
dhambi kubwa sana…’akasema mume mtu
‘Hahaha……nikuambie kitu, hilo mimi nina uhakika nalo…huyo mtu kaathirika,…hilo
sana shaka nalo, nimethibitisha…. ndio maana nataka na wewe , huyo hawara wako akiondoka tu, mimi na wewe mguu kwa mguu
tunaende ukapime. …hilo sharti lazima litimizwe kama nilivyomuambia mzee…’akasema
‘Lakini sasa kwanini hukumwambia mzee kuwa umeshakata tiketi
ya basi, na….?’ akauliza
‘Najua Mzee asingekubali,. ..sijui huyo mwanamke kawapa nini
nyie wanaume…huyu mzee kabadilika kweli,…kisa huyo mwanamke humwambii kitu,…hebu wewe fikiria alisema nikipata ushahidi
tu..yeye hatasubiria nini wala nini…atamfukuza huyo mwanamke, sasa kipo wapi…,
sasa eeeh, mpaka kikao eeeh, subirini eeeh…nimechoka! Sasa nyie sisubirini , mimi
nachukua maamuzi, hapa sasa ni kazi tu, aondoke….’akasema
‘Mke wangu…..sio vizuri hivyo, wema wetu wote utakuwa hauna maana, ..hebu
niambie utamwambia nini,…aondoke?, unamfukuza?.....mimi sipendi tabia hiyo
kabisa, basi mpe pesa hii ije imsaidie, kama umeamua hivyo….’ Akauliza na
kusema mume mtu
‘Wewe subiri tu utaona nitakachokifanya, ….ataondokana akiwa
anajuta,…na kwa hili….sitaki uniingilie,
wewe ukae humu humu ndani…huyu atatoka na hatarudi tena, na hutamuona tena
maishani mwako…..’akasema na kutoka akimuacha mumewe akiwa kaduwaa tu,…
Mume mtu alishika kichwa akiwa kajiinamia, na baadaye akaona
hawezi kuvumilia, akashindwa kujizuia, akasimama na kuanza kumfuatilia mkewe
kwa nyuma….
‘Huyu anaweza kuzua balaa, ngoja nikamuwahi kumzua, ….’akasema
NB: Hivyo ndivyo ilikuwa, je na hapo kuna rejea nyingi! Visa vyangu ni maandalizi ya tamithilya, …movies
!
WAZO LA LEO:
Uchungu wa kuibiwa ndoa, aujuaye ni mwanandoa, huwezi kuutathimini uchungu huo mpaka siku
likukute. Hala hala, wale wenye tabia hiyo, ndoa ni kitu kitakatifu, hakitakiwi
kuchafuliwa ovyo, na ikitokea kuchafuliwa madhara yake ni makubwa sana…acha, na tubu
kwa mola na kama hujaoa au kuolewa muombe mola wako akusaidie umpate mke au mume mwema.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment