Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeMonday, February 29, 2016

SIKIO LA KUFA HALISIKII DAWA- 12‘Aliyeingia alinifanya nitoe macho….’  Mdada aliendelea kusimulia

‘Lakini  kabla sijawaelezea ni nani huyo aliyeingia, ngoja kwanza niwaelezee kuhusu kikao kilichokuja kufanyika baada ya mzee kuondoka….ni kikao kilichokuwa na msitakabali wa maisha yangu, na maelezo haya niliyapata baadaye, lakini yanahitajika kuelezewa kabla sijaendelea mbele.

Ni kikao kilichonigusa sana, na siku niliposimulia, nililia,..nililia nikimkumbuka huyo mzee, sikuelewa ni kwanini nililia, lakini nahisi ni kwa jinsi alivyoonyesha moyo wake kwangu….nilimuona zaidi ya baba yangu!

**********
 SIKU ILE mzee  alipotoka pale ndani na kuniacha nikilia na kuwaza ya kuwaza, kumbe mzee yeye alikwenda moja kwa moja kwenye ofisi za kijiji na kumtuma tarishi kuitisha kikao cha wajumbe wa kijiji, na wajumbe walipofika akaanza kuelezea;

‘Nimewaita wajumbe na wazee wa kijiji kuhusu zile shutuma zenu kumuhusu yulebinti…Yule bint, ambaye tuliambiwa kuwa ana tabia mbaya na mwovu na ya kuwa kaja hapa kijijinu kwa lengo baya, kuwa anataka kuusambaza ugonjwa mbaya  wa ukimwi, kwa kulipiza kisasi….hapa kijijini kwetu..kwa watoto wetu,

‘Mimi nikajiuliza, ina maana kumbe hapa kijijinu kwetu ugonjwa huo haupo, …na tumeamua kuchukua tahadhari hiyo ili usiingie, ni jambo nzuri,…kama ni kweli ,… tuliache hilo kwanza…,

‘Labda nianza kwa kusema… mimi mwenyewe niliamua kufanya uchunguzi wangu binafsi maana huyo binti alikuwa kwenye dhamana yangu…na japo nina matatizo yangu mengi, lakini ilibidi nifanya hivyo, ukubwa jalala..’akatulia

‘Na hata hivyo, mtu hujikuna pale mkono unapofikia, ….japokuwa ni kiongozi, japokuwa mimi ni mzazi, lakini inafika mahali, unaona hapa sasa nahitajia msaada, na kwa hili, …la huyo binti, nakiri kwa kusema kuwa sasa nahitajia msaada wenu…’akasema na watu wakaguna.

‘Nimeona kiujumla,..sio vyema kuendelea kuishikilia dhamana hiyo  kwa huyo ..binti….kwani kwangu mimi mwenyewe nimeona inaleta picha mbaya, na tafsiri ziziszo na msingi zinazidi kuenea, kwahiyo leo nimewaita hapa ili  tuwe na maamuzi ya pamoja, kama kuendelea kumlea huyo binti kama mgeni wetu ama ….yote inategeema maamuzi yenu , ila mimi kutokana na shutuma na ….kuhisiwa vibaya nimeona leo nije kuivua dhamana hiyo….’akasema

‘Tulijua tu mzee, utaujua ukweli na hatimaye utatoa maneno ya busara…huyo binti hastahiki kuishi hapa kijijini kwa yoyote Yule, na tulishangaa mzee wetu wewe kumtetea, na kumkingia kifua, sasa natumai umeugundua ukwelihebu jiulize mzee….kama wazazi wake walimshindwa, sembuse sisi…..’akasema mama mmoja.

‘Kwahiyo ndugu mwenyekiti hiyo ndio ajenda muhimu niliyowaitia na samahanini kwa kuacha shughuli zenu…’akasema mzee. Na mwenyekiti, kwanza akatulia akiwakagua wajumbe, na baadaye akamgeukia mzee na kumuuliza

‘Je mzee umechukua hatua hiyo kutokana na uchunguzi wako au kuna jambo jingine?’ akaulizwa

‘Nisingelipenda kuingilia undani wa uchunguzi wangu,….kwani msimamo wangu mnaufahamu, ….mimi sipendi mambo ya kusikia tu, na kuyakubali hapo hapo…mimi huwa napenda ushahidi wa wazi…na nilipokwenda huko kijijini sikuweza kuupata huo ushahidi wa wazi wakunisaidia hilo, hapo lazima nikiri kwenu,…,

‘Na kwahiyo basi, nisingelipenda kuongea uvumi, maneno ya watu walivyokuwa wakisema,..hapana, mimi sipendi hiyo tabia,..na nilipoona mambo yalivyo huko kijijini , sikutaka kuendelea kuchunguza zaidi. Kiukweli,…nakiri pia hisia zangu bado zinanituma kuwa huyo mdada huenda hana hatia, lakini kwa hilo, hata mimi siwezi kujiaminisha kihivyo, ndio maana nikaona niutue huu mzigo, kwani nami nina yangu yananitoa jasho….’akasema na wajumba wakaguna. Na mwenyekiti kabla hajasema neno mjumbe mmoja akasema;

‘Lakini mzee unataka ushahidi gani zaidi…au mpaka likukute tatizo, …itokee kijana wako atembee na huyo binti, aumbukizwe ndio utaamini, au…na ni kwanini unamtetea sana huyo binti, ni jamaa yako,…unamtaka awe mkweo nini……hahaha mzee, tuamini sisi hayo tunayokuambia huyo binti hafai?.’akasema na kuuliza mjumbe mwingine.

‘Mnielewe vyema,…. kwa kusema hivyo, sio kwamba namtetea huyo binti…kama ni mwovu, kama ana makosa tunatakiwa tuyaonyeshe makosa yake, huwezi kumuhukumu mtu kwa kauli tu….ndivyo ilivyo kisheria na kiimani,…ni kweli huko kijijini kwao niliwauliza watu wakakubali kuwa huyo mdada alikuwa hasikii, alikuwa na tabia chafu…hilo hata wazazi wake walilithibitisha,…. lakini niwaulize nyie,  hivi hapa kijijini hawapo mabinti wa namna hiyo, au hawapo vijana wa namna hiyo….wapo wengi tu…’akasema huku akiwaangalia wajumbe kusika kauli…

‘Mzee ukisema hivyo unakosea,…tunajua hilo, lakini ni bora kukinga, na huku tukiendelea kutibia matatizo yetu…hiyo sio hoja mzee….unajua harakati zetu za kukibadilisha hiki kijiji kiwe kijiji bora chenye maadili mema,….huyo anakuja kuharibu’akasema kijana mmoja mjumbe anayewakilisha vijana,

Kauli hiyo ya mzee ilionekena kutakwa kupingwa na wajumbe wengi, maana wajumbe mbali mbali walinyosha vidole kutaka kuongea lakini mwenyekiti akasema ….

‘Mzee tunakumbuka kuwa wewe mwenyewe kwenye kauli zako ambazo zilifanya mpaka ukawa kiongozi  muadilifu wa kijiji na kiongozi wa kushauri kwenye nyumba za ibada uliahidi kuwa utakuwa msitari wa mbele kupambana na tabia chafu zinaongezeka hapa kijijini kwetu, na mojawapo ni ujio wa wageni wenye malengo mabaya…sasa huyu ….kwa taarifa hizo na matendo hayo huoni kuwa ana malengo mabaya…’akaulizwa

‘Sawa mwenyekiti, mimi nataka mnielewe,….katika maswala ya imani, tunaambiwa wageni ni watu wakuenziwa,…. anapokuja mgeni  kwanza ni baraka bila kujali ana nini,…na pale anapokuwa ana shida, hana pa kwenda, inatakiwa tumkirimu, na mimi kama kiongozi mshauri  wa imani za dini, nilitimiza wajibu wangu…je haya hayakuwepo zamani …wazee wenzangu mniunge mkono kwa hili, sio kweli kuwa enzi zetu, baraka hazikuwa nyingi, hali ya maisha ilikuwa nzuri, watu hawalalamiki njaa…ni kwanini , ..?’ akauliza na watu wakawa kimia.

‘Muulizeni huyu mfadhili wa huyu binti….japokuwa alijitolea kumchukua huyo binti, lakini hali yako ya kiuchumi ilikuwa inayumba, chakula cha shida…lakini siku alipoingia huyo binti hapo kwao, walishangaa, kipato, hali ya kiuchumi ilitengemaa, hawakuiona tena ile shida na siku kukosa pesa ya kula…hili hawakuliangalia kwa mtizamo huo maana shetani alishawaingilia….haya sasa huyo binti ataondoka, tuone itakuwa….’akatulia.

‘Sawa mzee lakini pia tuangalia na upande mwingine wa shilingi , athari za mgeni huyo…na hayo mzee unayoongea ni nadharia tu….huwezi kuthibitisha kwa vitendo na ushahidi kama unavyotaka wewe…’akasema Yule kijana.

‘Sawa hayo yamepitwa na wakati…..muonavyo nyie…wa kisasa, kama hayo mnayaona yamepitwa na wakati hebu tuangalie utu, siku hizi mnaita haki za binadamu eeh…. hebu tuangalieni hali ya huyo mdada…ni mjamnzito, anaumwa, hana jamaa, hivi kweli kama angelikuwa ni binti yenu mngelimuacha tu,…kwanza ilibidi tutimize wajibu wetu, na ndicho nilichokifanya mimi , hapo nilikuwa na kosa gani…nawaulizeni nyie….?’akasema

‘Sawa hilo hata sisi tulikubaliana nalo pia mzee, ndio maana awali tuliliunga mkono…., lakini ndio zikaja hizo taarifa za tabia zake mbaya,  na kwa ushahidi yule aliyejitolea kumuhifadhi, aliweza kushuhudia tabia isiyofaa ndani ya familia yake, .mke wa mfadhili, amekuwa akilalamika kuwa binti huyo ana vitendo vya kumshawishi mume wake na ndoa yake ipo matatani….je hayo hayatoshi kuchukuliwa hatua…’akasema mama mmoja

‘Na kwa kuongezea hilo mzee mwenzangu, huyo mama mfadhili alisema anaweza kuleta ushahidi  wa picha anasema aliwafuma wazi wazi wakiwa kitandani wakishibana kimahaba…na kasema hiyo picha ameshakuonyesha mzee…, mzee sasa  unataka nini tena hapo, hebu chukulia kama huyo mke mfadhili angelikuwa ni binti yako , ungekaa kimia mtu wa kuja aje kuvuruga ndoa yao….?’ Akaulizwa

‘Ndio maana nikawaita, maana naona mambo haya sasa yananizidi, mimi kama mzazi, nina watoto, nina wajukuu, nina matatizo yangu mengi tu, nilijitahidi kutimiza wajibu wangu  kama kiongozi, kama muumini, sasa nimeona hili niliweke mikononi mwenu….ila mnielewe, mimi nimeosha mikono yangu, ….mimi sitaki kuwa mhanga wa kuamua kile ambacho ninajua kinaweza kuwa laana,..

‘Hahaha..... mzee, mbona una kuwa na imani haba, kuna laana gani kutoka kwa mtu ambaye anafanya kazi ya ukahaba….au huo sio ukahaba …ni uhuni, ni umalaya…., mtu aliyetembea na wanaume wengi bila ndoa tutamuuitaje….na mambo yao waliamua kuyaweka hadharani,kila mtu aone….mzee  mtu aliyefukuzwa na wazazi wake unaogopa eti ataweza kuleta laana, mzee acha huo udhaifu ….’akasema mjumbe.

‘Mimi naongea haya kwa uzoefu,….laana mnaweza msizione hivi hivi tu….zinatokea baadaye mkiwa mumejisahau kabisa, na mnaweza kabisa msijua chanzo ni nini….maana ukimtendea mtoto wa mwenzako, ukumbuke nawe una watoto, kama huna watakuja…na yale yale yanaweza kutokea kwako..hayo tumeyashuhudia hapa kwetu…mnakumbuka visa mbali mbali viliwahi kutokea hapa kijijini wenye hekima zao waliliona hili,….jamani ujanja wa dhuluma hauna tija kabisa…sitaki kuelezea hayo.’akasema mzee

‘Sasa mzee wewe unataka kusema nini….maana umesema ulikwenda huko kijijini ukafanya uchunguzi, je …wewe huko kijijini uligundua nini,….?’ Akaulizwa

‘Mimi nilifanya uchunguzi wangu kwa ajili ya kujirizisha,…unajua jambo likishatendeka, unachobakiwa nacho ni kauli za watu,ushahidi halisi unakuwa umeshachakachuliwa…sasa inategemea watu wanamuelewaje  huyo mtu, kihali ….kihisia,… na ushahidi kama huo unaweza kuwa na utata…ukiwa kiongozi muadilifu, unatakiwa uwe makini sana na ushahidi kama huo, ni vyema ukijirudisha na kujiangalia wewe mwenyewe kwanza kabla hujamnyoshea mwenzako kidole….kufukuza , kutoa adhabu kali…wakati wewe mwenyewe unanuka ni dhuluma, na hili linaondoa baraka,…tuweni makini jamani....'akasema mzee.

‘Sasa mzee …kwa hali kama hii ulitaka tufanye nini, tukae kimia….hapana hiyo hatuwezi….’akasema mjumbe mwingine.

‘Sijasema tukae kimia, ila ni vibaya sana ukawa unatoa hukumu wakati wewe mwenyewe una mauchafu yako,..nia eti kuonekana, au kujijengea jina, au kujitwalia madaraka…ni kweli utapata hicho ukitakacho, utaonekana muwajibikaji,…. , utachuma,…lakini  unamdanganya nani,…jamani ole wetu wenye tabia hizo, haya machumo ya kutafuta sifa, ni sumu ndani mwako,….ipo siku na wewe yatakukuta hata kwenye kizazi chako mwenyewe, mimi naogopa sana’akasema

‘Sasa mzee tuambie, ….kutokana na hilo wewe unatakaje….maana hatukuelewi…?’ akaulizwa

‘Mimi huko nilipokwenda…niligundua mambo ambayo bado yananipa mashaka,…ni kweli, kuna walakini mwingi tu, na maswali mengi ya kujiuliza..lakini kwanini nibebe hili jukumu peke yangu, ndio nikaona kabla sijasema langu,….kabla sijang’ang’ania maamuzi yangu nikaona tusaidiane kwa nia njema kabisa…sasa mimi nimelileta rasmi mbele yenu, maana huyu binti alikuja hapa kijijini kwetu, ni mgeni wa wote, au sio….sasa nataka kusikia kutoka kwenu, labda mna ushahidi wa matendo na vienzi vyake….’akasema

‘Kwahiyo mzee, unataka kusema wewe hukupata ushahidi wa matendo na vienzi vyake…ili tuweze kuwa na maamuzi ya pamoja, maana wengine walishaweka bayana,….iliyobakia ni wewe tu mzee, unasemaje sasa mzee?’ akaulizwa

‘Kiukweli, …hakuna ushahidi bayana, hakuna ushahidi wa matendo na vienzi vyake, sikuwahi kuuona,,…hata hivyo kwa vile raia wengi hapa kijijini wanalalamika, na wengi wananilalamikia mimi, …na akiwemo mke mfadhili, ambaye alifikia kwangu na hata kunionya kuwa kama ndoa yake itavunjika mimi nitabeba lawama,….sasa nimeona tulizungumze hili na tuchukue hatua sitaki kama mlivyotaka nyie…kwa pamoja…’akawaambia wajumbe.

‘Hapo mzee tupo sawa,…tuchukue hatua kwa pamoja, umesikia mwenyekiti, mimi naona ndugu  mwenyekiti  tuingie kwenye hoja yetu,…je huyo mdada, anastahiki kuendelea kukaa hapa kijijini…au andoke hapa kijijini….’akasema mwanamama mmoja na wajumbe wakasema kwa pamoja

‘Aondokeeee’ wakasema kwa sauti

‘Tufuate utaratabu kwanza…’akasema mwenyekiti, na kumgeukia mzee.

‘Mzee wewe unasemaje kabla hatujaingia kwenye hatua nyingine, bado una pingamizi…?’ akauliza mwenyekiti.

Mzee alitikisa kichwa kwa kusikitika,hakusema neno na mwenzake, aliyekuwa karibu naye akasema;

‘Mzee mwenzangu, sisi kama tulivyokuambia, tumejiridhisha, hatubabaishwi na urembo wa huyo binti,kama wewe mzee urembo umekuzuzua,…labda una malengo yako ,  sisi hatutaona haya kuyakemea maovu,…angalia mzee weupe ule, una walakini wewe hujui tu…sasa ngoja kijana wako mmoja aingie kwenye anga za huyo binti, …..shauri lako’watu kusikia hivyo wakacheka, na mzee  akasema

‘Hizo ni hisia zako,  mimi nilitaka niwe muwazi na pia nitimize wajibu wangu kiadilifu na kihekima kama mzee…nisingeliweza kuamua bila ya ushahidi, bila kuwa na uhakika….na hata hivyo hili tatizo sasa lipo mikononi mwenu….’akasema mzee.

‘Sawa mzee…..hilo jukumu sasa lipo mikononi mwa kikao, je kuna mjumbe mwingine mwenye hoja kabla hatujaendelea na hatua nyingine...mzee wewe hapo hujasema neno, hebu tuambie maoni yako..’mwenyekiti akamuuliza mzee mmoja aliyekuwa kimia kwa muda mrefu.

‘Kiukweli,…kutokana na waliyosema wenzangu na kutokana na maelezo ya hao waliokwenda huko wakafanya uchunguzi, mimi sioni kama kuna utata hapo,….mimi naonelea huyo binti, achukuliwe hatua stahiki na ni wajibu wa kikao sasa kuamua kama ni aondoke hapa kijijini au tutafute njia nyingine, kama zipo, nila nionavyo mimi kwa masilahi ya raia , na watoto wetu ni bota tu aondoke haraka…tusisubirie shari…na tukifanya hivyo wengi watakaogopa kuja hapa kwetu,…na tutaweka mfano bora’akasema huyo mzee na wajumbe wakashangilia, hasa akina mama.

‘Sasa tunakuuliza mzee wetu wewe uliyejitolea kuwa mdhamini wake, maana wewe ndiye uliyeweka pingamizi awali ukasema una uhakika huyo binti ni mwema…je  una zaidi au tuanza mchakato wa kupiga kura…?’ akaulizwa mzee aliyenidhamini.

‘Kama nilivyosema hili swala sasa ni lenu , ni la kikao,  mimi sina zaidi ….siwezi kuendelea kushikilia msimamo wangu, huyo sasa ni mgeni wetu sote, kwahiyo kama ni dhambi kama ni maamuzi, yapitishwe kwa kauli zenu, ila mimi ningewaomba kitu kimoja…..naombeni mnielewe kwa hilo, mimi kwa mchakato huu,  nitajiweka pembeni kidogo ….’akasema na kutulia, na mwenyekiti wa kikao hicho akasema

‘Kwa vipi mzee….?’ Akauliza mwenyekiti

‘Mwenyekiti endelea…achana naye, ataturudisha nyuma huyo’akasema mzee mwingine
‘ Sawa, hata mimi naona…kikao kiendelee, sasa ni hivi ki- kawaida yetu ikitokea jambo kama hili, tunapiga kura, …, na wazeewetu kikawaida tunawaheshimu na ndio maana tukawapa nyie kauli za turufu ya kuwa  kama kuna mwenye pingamizi kati ya nyie wazee waadilifu, anaruhusiwa kuweka pingamizi, na ikitokea hivyo, hatuwezi kupiga kura, sasa nyie wazee kama yupo mwenye pingamizi, tunamuomba aseme,….(kukawa kimia)

‘Je yupo mwenye kura turufu ya kupinga?’ akauliza mwenyekiti tena, na wazee wote wakabakia kimia baadaye mzee aliniyenidhamimi akakohoa na kusema;

‘Mimi nimeshaondoa kura yangu  turufu  niliyokuwa nimeweka awali,…nilisema mimi nijiaweka pembeni kwa mchakato huo,nikiwa na maana sitapiga kura…’akasema huyo mzee aliyekuwa akinitetea na kuwafanya wajumbe washangae,….

‘Kwanini mzee, hujui kwa kufanya hivyo unatusaliti…! Ina maana bado unapinga kuwa huyo binti hana hatia, hana makosa au? Na kama bado unapingamizi  useme mzee, na unafahamu hilo fika kama una pingamizi hatuwezi kupiga kura,..unajua kabisa nyie wazee mmoja akikataa basi kura haina umuhimu tena…’akaambiiwa

‘Mimi ninajua sana hilo,…na sijawa msaliti kwa hilo, huo ni uhuru wa mtu kufanya hivyo… ndio maana nimeondoa pingamizi langu, hata hivyo, mimi sijakataa wala sijakubali…naomba mniamini hivyo, na nawaahidi kuwa matokea ya kura zenu nitayaafiki…ila mimi sitapiga kura kwasababu zangu binafsi.’akasema huyo mzee

‘Sawa mzee naona huruma zimekuzidi, au kwa vile ulitaka aolewe na kijana wako nini…hahaha, sisi tutaendelea  na hili zoezi kwa masilahi ya kijiji chetu naombeni msimuulize tena mzee wetu ni kwanini ni kwanini itatukwamisha…tumeelewana…’akasema mwenyekiti na wajumbe wakasema ;

‘Tumeelewa ,  tupige kura….’

‘Ni haki yake…..na tunamfahamu mzee wetu, kwa hekima zake ni lazima ana maana yake…. na uamuzi wake tunauheshimu…mimi nafahamu ni kwanini,….hahaha’akasema mwenyekiti na kucheka.

Sasa tunapiga kura, katibu pitisha vikaratasi…najua wote mnafahamu kuandika,  kura zipo hivi, kama wewe unataka mdada aondoke, wewe andika AONDOKE, kama hutaki andika ABAKIE.. tuemelewana…’ akasema mjumbe

‘Tumelewana mjumbe sote hapa tumeenda shule….’wakasema na kweli zoezi la kupiga kura likaanza

Matokea ya kura ….,

‘Wengi wamesema ….kutokana na kura zenu, AONDOKE…kwahiyo ina maana mdada anatakiwa kuondoka hapa kijijini…haya ni kwa kura zenu…’akasema mwenyekit.

‘Lakini kwa hekima, na busara, …sisi sio kwamba tunamchukia huyo binti….na sio kwamba hapa kijijini ni watakatifu kihivyo….hapana, lakini heri nusu shari kuliko shari kamili,..hata mzee kaliona hili, kila siku tatizo, matatizo, kesi..haya ndoa za watu sasa matatani,…kisa ni nani…’akasema mwenyekiti kabla hajamaliza wajumbe wakasema

‘Mdada..’

‘Ehee ndio hivyo, sasa kihekima, hatuwezi kumwendea na kusema ONDOKA, ONDOKA…kuna taratibu zetu, zinajulikana,….mzee uliyamdahamini, ..tunakuomba kwa hili utusaidie, mimi na viongozii wenzangu tutakaa tuone jinsi gani tutamuondoa hapa, …hatutaki kutumia nguvu…’akasema mwenyekiti

‘Mzee, unasemaje…?’ mwenyekiti akamuuliza mzee aliyenifadhili

                                                           ********

Wakati hayo yakiendelea huko kwenye kikao….

Huku nyumbani kwa mfadhili, kwa baba na mama mwenye nyumba  kwanza mzee alipoondoka wawili hawa walikuwa wamenuniana tu, bifu kwa bifu, hakuna kuongea, baadaye baba mwenye nyumba akafunua mdomo kujaribu kujitetea,kubembeleza ….ooh, ndio akajichongea, mama mwenye nyumba akaanza kuongea,….aliongea mpaka basi.

Baadaye mke mtu akaanza kulia….na alipochoka, akasema,

‘Inaniuma sana, …lakini kwanini niumie, kwanini nilie, kwanini…hapana sasa, kabla huyo mzee anayekutetea hajarudi hapa, nataka nifanye jambo, ni lazima nifanya jambo, mimi si mnaniona mjinga, sasa ngoja uone vumbi langu. Na hili … itakuwa fundisho kwa watu kama ho..’akasema na kusimama.

‘Mke wangu….’mume akajaribu kujitetea

‘Na kwa hili naomba ten asana usiniingilie, ukitaka salama yako,…ukae mbali na mimi…’akasema

‘Unataka kufanya nini…?’ akauliza mume sasa akionyesha wasiwasi

‘Utaona mwenyewe nitakachokifanya…na hili litakuwa fundisho kwa watu kama hawa kuja kuingilia ndoa za watu….’akasema huku akitembea kutoka nje

‘Mke wangu mzee alisema tusifanye chochote, tuwe na subira , tusimruhusu ibilisi akatuteka akili zetu,.hebu kwanza tusubiri mzee arudi, ….nakuomba utulie kwanza,...!’ alisema mume mtu lakini ilikuwa kama ndio anachochea moto. Mke mtu akatoka kwa jaziba, na mume mtu alijua kabisa mke anataka kwenda kuleta fujo kwa mdada!

                                                                *******.

Haya na huku kwa mdada je, mdada ambaye hadi hapo alikuwa hajui ni nini kinachoendelea, alikuwa kaachwa chumbani kwake baada ya mzee kuondoka, tuliishia pale Mlango ulipofunguliwa, akaingia mtu….

Mdada anaendelea kusimulia kwa kusema;

‘Mlango ulipofunguliwa, niligeuka kuangalia ni nani aliyeingia…nikijua sasa ndio nimefuatwa kufukuzwa,..na kwa muda huo sikuwa na uhakika ni nani angeingia kwani nilikuwa nimeinama nikianza kukunja nguo zangu ili niweke kwenye mfuko, tayari kwa kuondoka.

Na niliposikia mlango ukifunguliwa, fikira zangu za haraka haraka zikawa zinajiuliza,….ni nani huyu kaingia bila hata hodi,…ni mama mwenye nyumba, au baba mwenye nyumba, ….au ni mzee karudi tena, lakini kwanini asipige hodi…

Taratibu kwa mashaka nikageuka kuangalia mlangoni…,nikamuona aliyeingia,  lakini macho yangu yalipoangalia hicho alichokishika huyo aliyeingia, nilijikuta nikitoa macho,….macho ya uwoga,…
Kwanini atoe macho ya uwoga….tutaona sehemu ijayo…


NB Tuishie hapo kwa leo, ama kwa wale wanaosema narudia rudia ya nyuma, …kufanya hivyo ni namna ya kusherehesha kisa hiki, mtindo wa rejea kujikumbusha …na hivyo ndivyo yalivyotokea kwa MUHUSIKA, ili kukidhi haja ya mawazo yake kiuhalisia….na hata ilivyo kwenye ubongo wa mwanadamu ndivyo ilivyo, kuna ile hali,ya KUKUMBUKIA, yaliyopita pale tukio likitokea, hata mnaoangalia `movies’ mtasadikisha hilo, na hup ndio mtindo wa emuthree (emuthree style) katika kuandika visa vyake…..TUPO PAMOJA.
Ni mimi: emu-three

1 comment :

Anonymous said...

Hi there mates, how is all, and what you wish for to say concerning this paragraph, in my
view its actually awesome designed for me.