Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Friday, December 25, 2015

RADHI YA WAZAZI-62






Ilikuwa kazi kubwa sana kumshawishi kijana wetu kukubali kuhudhuria kikao cha maridhiano,kama ilivyopendekezwa na hakimu.

Ilibidi, wakili mtetezi kufanya kazi ya ziada, na hakuchoka, kumuendea jamaa wetu huyu, ambaye kila mara alipofikiwa alidai kuwa hana nafasi, lakini sasa hakimu akawa katoa agizo kuwa anahitajia hayo makubaliano ili aweze kumaliza hiyo kesi,

Wakili baada ya kupata maagizo hayo, alikwenda moja kwa moja kwa jamaa yetu, na kumwambia kuwa sasa asipokubali kuwepo hicho kikao, kesi itaendelea na itambidi awe anahudhuria mahakamani mara kwa mara…

‘Mimi sina muda huo….’akasema

‘Ndio maana tunahitajika kuwepo hicho kikao cha maridhiano, ili hakimu aweze kuimaliza hiyo kesi…’akaambiwa

‘Kwani kuna tatizo gani, kwanini hakimu asitoe hukumu tu, maana kila kitu kipo wazi, mkosaji anajulikana alichokifanya, atoe hukumu….’akasema

‘Wewe unafahamu wazi kwanini hakimu alisitisha kuendelea na  kesi hiyo kwanza…..’akasema

‘Mimi sifahamu ….’akasema

‘Hakimu hakutoa hukumu kutokana na halii halisi, wewe ulikuwa huwafahamu wazazi wako, na umewafahamu kati kati ya matatizo kama haya, yeye akachukulia hayo kiubinadamu ili mfahamiane kwanza….’akaambiwa

‘Tunarudi kule kule, hayo hayana maana kabisa, anyway…haya nambieni mnataka mimi nifanye nini,….?’akasema na kuuliza

‘Tunataka tukutane wewe na wanafamilia, tuone yale mnayohasimiana, ili tuyamalize haya matatizo, na ikibidi ….kutokana namaridhiani hayo kesi ifutwe, na nyie make kama familia, unaona hekima ya hakimu…’akaambiwa

‘Nikae meza moja na huyo mzee, sizani kama tutaelewana…yule mzee ana hasira, na mimi siwezi kuvumilia, kama anajifanya ana hasira mimi ni zaidi, sitajali kuwa ni mzee…..ndio maana sitaki kabisa kukaa naye meza moja….’akasema

‘Inabidi, ukumbuke yule ni mzazi wako, na inabidi tukae tuyamalize…ili kesi ifikie mwisho,ikiwezekana kesi hiyo ifutwe,… ili wewe usisumbuliwe sumbuliwe tena….’akaambiwa na yeye akatulia akiwaza jambo,halafu akasema;

‘Tutakutana wapi na lini, ujue mimi nipo kazini, siwezi kuacha shughuli zangu kwa mambo haya yasiyo na maana kwangu, nambie…’akasema akiangalia saa yake

‘Wewe unataka tukutane wapi, nyumbani kwako, au ofisini kwangu, au twende kabisa huko kijijini, unaonaje hilo, ukienda kijijini wataona wewe kweli ni muungwana, mtoto mwema unasemaje…?’ akaulizwa

‘Nitakuja ofisini kwako…siwezi kwenda huko kijijini, hao watu sio wema kwangu.  Kijijini….! Hahaha,….. hapana huko siwezi kwenda kabisa….’akasema

Basi siku ya kukutana ikapangwa,lakini kwa bahati mbaya mzee huyo, yaani baba yake jamaa, hakuweza kufika kutokana na hali yake kuwa sio nzuri, lakini wakili mtetezi, akasema kikao kinaweza kuendelea na Profesa atamuwakilisha kaka yake...yatakayokubaliwa yeye atayawakilisha kwa kaka yake.

‘Kwanini tusiende huko kijijini, alipo huyo mgonjwa ili yeye mwenyewe, kijana aweze kumuona baba yake na baba yake atasikia faraja,…..?’ Profesa akasema

‘Kijana wako kasema yeye hawezi kwenda huko,….’akasema wakili alipokutana na Profesa kumpa taarifa hiyo.

‘Mimi nataka kuongea naye kwanza kuhusu hilo, maana ni muhimu ninawe mikono, nisije kuonekana mimi sikutimiza wajibu wangu…’akasema Profesa

‘Unataka kuongea nini na yeye, nachelea usije kuharibu, ukafanya jamaa akatae kabisa kukaa hichi kikao…?’ akaulizwa

‘Yule ni baba yake, ni lazima nimueleze hali halisi,…’akasema na wakili baadaye akakubali, lakini alitaka na yeye awepo, kwahiyo wakaongozana hadi ofisini kwa jamaa na bahati nzuri, akakubali kuongea nao

‘Mnasemaje tena, na kwanini umekuja na huyu mtu…?’ akauliza akimnyoshea mkono Profesa

‘Yeye ana ujumbe muhimu anataka kuongea na wewe kwanza…’akaambiwa

‘Kwahiyo kikao hakipo tena…?’ akauliza

‘Kikao kipo, ila yeye alitaka kuongea nawe kidogo…msikilize tu…’akasema wakili,na Profesa akasema;

‘Mimi nilionelea kikao hicho kikafanyike huko kijijini, kwa kaka,….kwa baba yako ili wewe mwenyewe uone hali ya baba yako, na ukifanya hivyo , ni kwa faida kwako, utampa faraja yule mzee,hebu jaribu kulifikiria hilo kama mtu uliyekomaa…’akasema Profesa

‘Unaanza kuleta yale yale…mlitaka niende kuonana na yule mama, ….nikapoteza muda wangu hakuna kilichosaidia, sasa unataka niende kuonana na huyo mzee, ili iweje,…kama anaumwa, mpelekeni hospitali, mimi siwezi kufanya apone, kwani mimi ndiye nimempa huo ugonjwa….’akasema akiwa kasimama ameegemea mlango.

‘Sikiliza bwana mdogo, kwa mama yako umefanya makosa….wewe hujui tu….sasa mimi niliona yaliyopita yamepita, sasa jirudi,…hujachelewa bado,…mimi.., alitaka mkutane naye akupe hata wosia, moyo wake uwe radhi na wewe….umefanya kosa kwa mama yako,  ..hujui mama yako kaondoka na kinyongo gani, …’akaambiwa

‘Usielete visingizio hapa….yule mama yote alijitakia mwenyewe, au tusema ni ajali, ni bahati mabaya, mimi sihusiki lolote,…na nilifika, na siku nilipofika alikuwa hajitambui,….sasa unarudia rudia,..mama, mama….awe na kinyongo na mimi kwa lipi, ..acha ujanja ujanja wako hapa…’akasema

‘Sikiliza nikuambia….’akasema Profesa na jamaa akaangalia saa , halafu akasema

‘Hebu nambie wewe ulitaka mimi nikae pale hospitalini mpaka lini…unafikiri mimi sina kazi kama wewe, kazi kwanza…kazi nimuhimu, unasikia,mimi sio tapeli kama wewe, kuishi kiujanja ujanja siwezi,…nafanya kazi ili nipata pato halali….’akasema

‘Sijakataa hilo…lakini mzazi wako naye ni muhimu kwako, ulitakiwa uonyeshe dalili kuwa unamjali, uonyeshe kuwa ulimkubali, lakini ilionyesha kwa kila mtu kuwa hukumtaka mama yako, …hiyo ni balaa mbele ya safari,…’akaambiwa

‘Hebu niambieni, kikao kipo au hakipo….?’ Akauliza akiwa sasa anataka kuondoka

‘Kikao kipo, ila ilibidi nije na Profesa ambaye alitaka kuja kukupa huo ujumbe, kama nilivyokuomba mwanzoni na yeye alikuja na wazo hilo, kuwa ni muhimu kikao hicho kifanyike huko kijijini….’akaambiwa

‘Sikilizeni, kama ni lazima kifanyika huko kijijini…., basi tuachane na mazungumzo haya, maana kwangu hayana tija yoyote, siwezi kupoteza muda wangu hadi huko kijijini, siwezi , siwezi, mumenielewa, sasa muamue wenyewe….’akasema jamaa

‘Hayo mazungumzo mbele ya baba yako yana tija kwako sana, ujue hao ni wazee wako, huyo ni baba yako, mzazi wako,..na kuridhia naye, itakusaidia sana katika maisha yako ya mbeleni…’akasema Profesa.

‘Kauli yangu umeisikia sio…Ndio hivyo…., kama kikao hakiwezi kufanyika hapa mjini,huko kijijini siende, kwanza mimi natafuta nini huko, haya ni kwa manufaa yao wao wenyewe wanaotaka hii kesi ifutwe, ndio wahangaike, ….mimi ningelipendelea haki itendeke, sema tu sina muda wa kwenda mara kwa mara mahakamani, lakini ikibidi, kama watajifanya vichwa ngumu, nitahakikisha haki inatendeka….’akasema

‘Kwahiyo upo tayari baba yako afungwe?’ akaulizwa na Profesa na hapo kijana akaangalia saa yake, baadaye akasema…

‘Sasa mniambie moja, hicho kikao kipo au hakipo….?’ Akauliza

‘Kikao kipo tutafanya utakavyo wewe….’akasema wakili na kumuashiria Profesa waondoke, na Profesa akawa anataka kuongea lakini jamaa akaondoka kuendelea na kazi zake.

                **********

 Basi siku iliyopangwa kufanyika kikao ambayo ilikuwa ni kesho yake, wakili na wakili msaidizi wakiwa ofisini kwako, na muda mfupi baadaye akafika kijana wetu kama walivyozoea kumuita, alifika peke yake, mkewe hakuwepo,..

‘Unaona hawa watu walivyo, hawajali muda, sasa huyu Profesa na ndugu yake wapo wapi….’akaanza kulalamika baada ya kufika na kusubiri kidogo.

‘Kwa taarifa nilizozipata, baba yako hataweza kufika, ndio maana walitaka kikao kifanyike kijijini,lakini Profesa atafika, akimuwakilisha ndugu yake, .’akaambiwa

‘Baba yako, baba yako, mimi sipendi hiyo kauli….’akasema akikunja uso

‘Lakini tulishakuambia, kama hujarizika, basi tufanye vipimo vya kitaalamu ili ujirizishe mwenyewe kuwa huyo ni baba yako mzazi…ukagoma, lakini hata hivyo, kwa ajili ya kumbukumbu hilo litahitajika …kama kesi itarudishwa mahakamani...’akaambiwa

Profesa akawa kama hajasikia hilo, au kuyazarau hayo maneno aliyoambiwa yeye aliangalia saa yake halafu akasema;

‘Mimi nitasubiria nusu saa baada ya hapo, nitaondoka, na msije kunisumbua tena….’akasema

 Baadaye Profesa akafika na wazee wawili

**********

Kikao kikaanza, wakili mtetezi alirejea yake aliyoagizwa na hakimu na ya kuwa hakimu kasema hayo makubaliano yafikishwe kwake haraka iwezekanavyo, kwani kesi hiyo imesubirishwa kwa muda mrefu, na huenda hakimu huyo anaweza kupata uhamisho…

‘Kwahiyo kwanza ni wewe ulitendewa kosa, hadi kesi ikafikishwa mahakamani kukubali kuwa umesamehe, na huna haja ya kuendelea na kesi hiyo, lakini kabla ya hilo…’akatulia akifungua makabrasha yake

‘Rejea yale aliyopendekeza hakimu, …hakimu alitaka wewe na mshitakiwa mfahamiane, kutokana na ombi kuwa wewe ulikuwa humfahamu baba yako..’akasema wakili

‘Je wewe umeshamfahamu baba yako na kumkubali ….?’ Akaulizwa

‘Hilo linahusiana vipi na kesi,…hebu niwaulize, baba akimkosea mwanae, mtoto haruhusiwi kumshitaki baba yake…?’ akaulizwa

‘Anaruhusiwa, ….lakini sisi tuliyafanya haya kutokana na historia yenyewe, kuwa wewe ulikuwa humfahamu baba yako, ndio tukaona kuna umuhimu wa kuwakutanisha kwanza, huwezi kujua mioyo ya watu hutofautiana,kwa furaha ya kumtambua baba yako unaweza kusamehe kila kitu,….’akasema

‘Lakini sheria si ipo wazi…ni nani aliyemletea mwenzake fujo,ni mimi au ni yeye….?’ Akauliza

‘Kwanza tulimalize hili, je umeshamfahamu kuwa huyo mzee ni baba yako, na ukakubaliana na hilo?’ akaulizwa

‘Mimi nimeshamfahamu huyo mzee …na kama mnadai kuwa ni baba yangu, mimi siwezi kusema lolote kwa hilo ninachotaka twende moja kwa moja kwenye swala muhimu, kuhusu hiyo kesi, ….’akasema

‘Hatuwezi kwenda huko mpaka hili swala limalizike, kwani lipo kwenye mapendekezo ya hakimu na tunahitajika kuepeka marejesho kwa hakimu….’akaambiwa

‘Ngojeni kwanza, …nyie mna wakili wenu mtetezi, lakini mimi sina wakili hapa, je mawazo yangu na hoja zangu atazisimamia nani…?’ akauliza

‘Ukumbuke kuwa hiki ni kikao cha kifamilia, ,…hatuhitajii wewe kuwa na wakili wako, tunaongea haya familia, mimi wakili nimeitwa hapa niwe shahidi tu, na mtakayokubaliana niweze kuyawakilisha kwa hakimu, lakini kwa vile mimi ndiye ninayefahamu ni nini hakimu anahitaji, nimeona niwe msimamizi wa kikao ili mambo yaende vyema…’akasema wakili mtetezi

‘Sikilizeni, …mimi nataka haya mambo tuyamalize, na nipo tayari kesi hiyo ifutwe,…’akasema na kila mmoja akashusha pumzi ya kuonyesha kuwa hatimaye mambo yanakwenda vyema

‘Lakini… baada ya hapo, sitaki kujuana tena na hawa watu, siwataki hata kuwaona kwenye macho yangu….’akasema na wote wakaguna

‘Kwa kusema hivyo una maana gani,…ina maana hujamkubali huyo mzee kuwa ni mzazi wako, ina maana mlikuwa hamjakubaliana, hukuchukua taratibu zozote za kuongea naye?’ akaulizwa

‘Sikilizeni, kimaandishi, …kama ni muhimu kuwa hivyo, …narudia kusema hivi, kimaandishi kama ni muhimu,  ile iwe hivyo, ….ili kesi ifutwe, andika na nitasaini kuwa nimekubaliana na hayo, ..’akasema

‘Unajua hapo hujaeleweka, kwani nia nini, hatuhitaji kuanya mambo kihivyo, kuwa tuhadae ili kesi iishe,..nia ni kutaka mambo haya yaishe kwa nia moja, wewe ujumuike na familia yako, ni faraja, eti, wewe hukuwahi kuwafahamu wazazi wako, na sasa umewapata,, bahati mbaya mama kafariki,….pole sana….’akasema wakili

‘Muheshimiwa tusifanye mambo yawe marefu,…unajua kwa kukusaidia tu , kama alivyotaka hakimu, tutafanya,….’akatulia kama vile anachotaka kuongea ni jambo lenye thamani kubwa, lakini halitakiwi kusikiwa na watu wengi

‘Mimi ni mwema sana, unasikia,…. Kimaandishi tutafanya hivyo…au sio, kama mnayotaka nyie, si mnataka kesi iishe, isiwe shida,…lakini tuelewane hapo,….’akatulia kidogo

‘Kuna mambo muhimu nataka tuelewane hapo,….unajua, ndio maana nilitaka wakili wangu awepo, lakini sio mbaya, …wewe utawakilisha inatosha…’akasema

‘Wewe ulitaka nini, ili wakili wako ashuhudie, au akuwakishe, ulitaka nini…?’ akaulizwa

‘Unajua hawa watu ni wajanja sana, na siwaamini katu….sasa nitakubali kuweka sahihi yangu, lakini ….,’ akatulia kidogo

‘Lakini,  nina masharti, ambayo nataka hawa watu wayakubali, mbele yako wewe kama wakili wao…’akatulia

‘Hatujakuelewa, masharti, masharti ya nini….! Kwasababu nia yetu ni maelewano, na maelewano manzuri ya kifamilia ni udugu, sioni kwamba udugu, hasa wa mzazi na mtoto wake kunahitaji masharti , labda , hebu tueleweshe hapo ni kwanini unaweka masharti …..’akasema wakili mtetezi

‘Ni hivi, kama mnataka mimi nikubali kuwa  hiyo kesi ifutwe, si ndivyo mnavyotaka ?’ akawauliza na kabla hajajibiwa akasema….

‘Sasa ili nikubaliane na matakwa yenu, mimi nina masharti yangu,…mkikubaliana nayo,mimi nitaweka sahihi yangu na mambo yataisha,…kwani hata mimi nataka yaishe ni malizane na hawa watu,….lakini bila namna, bila kuwepo na hayo masharti, najua itakuwa mwanzo wa usumbufu….’akasema na kutulia kidogo

‘Mimi sitaki tena usumbufu na hawa watu, nataka amani , unajua wamesababisha naanza kukosana na mke wangu, hivi sasa mimi na mke wangu hatuelewani, ukiangalia sababu hasa …ni hawa watu…..’akasema akimnyoshea kidole Profesa.

‘Pole…lakini matatizo ya mke na mume ni kawaida, …muhimu ni nyie kuelewana, na kama ungekuwa iumeshaelewana na wazazi wako hawa wangekusaidia ….wazee wana hekima zao…’akaambiwa

‘Hahaha…hawa wanisaidie wakati ndio sababu, na wanataka iwe hivyo..lakini hawataweza…nikuambie kitu, huyu kaweka fitina mpaka kwa mama mkwe wangu, naonekana mimi sifai…..sasa nitamuonyesha mkwe wangu kuwa nafaa, hata bila yeye naweza….’akasema

‘Kumbe….’akasema Profesa akitabasamu

‘Unaona….Hawa watu sio watu wema,….hasa huyu, ….usimuone hivi, ni mwerevu sana, katika kutafuta jambo atajifanya mwema hujawahi kuona,ngoja apate…kiburi kinajitokeza,….namfahamu sana, kama ndiye yeye, maana mpaka sasa sijaamini…’akasema akimnyoshea kidole Profesa

‘Haya hebu tuambie ni masharti gani hayo…..?’ akaulizwa na wakili akimuangalia jamaa kwa macho yenye shauku

‘Ehee, sasa tunaanza kuelewana, …nataka uyaweke sawa, ni mashrti muhimu ambayo yatahakikisha kuwa hawa watu hawanisumbui tena….wakiyakubali, aaah, basi sina shaka, mimi nitakubali kuweka sahihi yangu kwenye hiyo taarifa inayokwenda kwa hakimu…..’akasema, na wakili akamwangalia Profesa aliyetaka kuongea jambo….

NB: Naishia hapa muda …mb, hizo zimekwisha,….

WAZO LA LEO: Katika kumaliza matatizo ni muhimu kila mmoja akapewa nafasi yake, na kwenye meza ya makubaliano kila mmoja ana nafasi sawa….tusiweke vikwanza kwa kuangalia masilahi binafsi. Na maongezi yenye nia njema, huleta tija, kuliko kutumia mabavu,..kwani wakipambana mafahali wawili zinazoumia ni nyasi.
 


Ni mimi: emu-three

1 comment :

emuthree said...

Msione tupo kimia, jembe(laptop) imeharibika, pia mitihan ya hapa na pale, lkn mungu yupo, atatusaidia,zaidi tutembelee facebook