Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeFriday, December 11, 2015

RADHI YA WAZAZI-60Ni kipindi kifupi, lakini matatizo yaliyotokea yalileta athari kubwa, huenda ilikuwa sehemu ya mwisho ya kupimwa , mtu huwa anapewa nafasi zote , lakini yeye mwenyewe ndio anaamua kutenda madhambi...

Ni kipindi kifupi cha kila mwenye utashi kuamua,...na hata  kwa upande wa wazazi, ilikuwa ni kipindi kigumu kwao, wakiumia moyoni, ..lakini wangelifanya nini

‘Huku kwa huyu mama mgonjwa hali yake haikutengamaa...hali yake iliziidi kuwa mbaya, na hata hiyo safari ya kupelekwa huko Muhimbili ilibakia kusubiriwa tu, atapelekwa, atapelekwa,, ilionekana ni kama vile madocta walishaona ni jambo lisiloweza kuponyeka, kwahiyo wakawa wanatumia mbinu za kuchelewesha chelewesha tu...

Ndugu na jamaa wakakutana na wakaona ni bora mtu awaone madakitari, na Profesa akajitolea kwenda kuongea na madakitari,.....

‘Hivi kwanini mgonjwa wetu hapelekwi huko Muhimbili, si mlisema kuwa tatizo hilo linahitajika upasuaji, na upasuaji huo ni mpaka Muhimbili, sasa siku zinapita na hali ya mgonjwa wetu inazidi kuwa mbaya, je kuna tatizo gani..?’ akauliza Profesa akiongea sasa na docta. Docta akachukua kabrasha la mgonjwa na akawa kama anasoma, halafu akasema;

‘Huyu mgonjwa, kuna vipimo...eeh, keshapima, na kuna dawa anatumia, hata hivyo, kila kitu kina utaratibu wake,...hatuwezi kumchukua kwa haraka mpaka hiyo tiba tunayomfanyia ikamilike...subirini tutawaambia....’akasema

‘Lakini wewe mwenyewe mwanzoni ulisema mgonjwa anahitajika upasiuaji, ili kuondoa hiyo damu ilionekana kwenye ubongo, au ilikuwa ni kauli tu...?’ akauliza Profesa

‘Kama nilivyokuambia, kuna matibabu tunamfanyia ambayo yatasaidia, ila kwenye wiki hii inaykuja, kama tutaona kuna umuhimu huo tutampeleka huko, nyie mjipange tu kusaidia, kama mlivyooambiwa....’akasema docta

‘Lakini kama shida ni gharama za usafiri, watu wameshachangishana, mtuambie tu ni kiasi gani, ...’akazidi kusihi.

‘Subirini mtaambiwa msiwe na wasiwasi....’akasema docta akionyesha kuwa ana haraka kuwahi kwenye kazi zake, na ikawa haina jinsi Profesa akarudi kwa watu wake waliomtuma kutoa taarifa...

                        ************

Huku kwa kijana wetu au jamaa yetu, akiwa ofisini kwake, akiwa anatafakari jambo, akasimama na kwa haraka akatoka na kuelekea sehemu nyingine, na mara simu yake ikalia, akaangalia mpigaji, alipoona ni nani, akabonyeza sehemu ya kukata simu....

Pamoja na juhudi za watu, ....kuombwa na kushauriwa kuwa aitikie wito wa kukutana na wazazi wake, yeye alibakia na msimamo wake ule ule....sasa ikawa mara kwa mara anapigiwa simu kuwa mama yake anaumwa sana, anahitajika kwenda kumuona, lakini hakuweza kufanya hivyo kwa haraka, zikapita siku mbili, na siku ya tatu, ndio akafika hospitalini na siku hiyo aliyofika, mama huyo alikuwa hajiwezi kabisa...

Alifika kwenye wodi aliyolazwa huyo mama, akamsogelea, na muda huyo alikuwa dakitari akimuhudumia kwa kumwekea dripu, kwani hali ya mama ilikuwa imebadilika, akawa anahangaika, dakitari akaitwa, na alipofika akamkagua na kuanza kutoa huduma stahiki na muda anafanya hayo ndio jamaa yetu akafika......

‘Nyie mliataka mimi nifike, haya nimefanya hivyo, niambieni nifanye nini sasa na hali ya huyo mgonjwa mnaiona ilivyo, ...’ akasema alipoona dcta akihangaika na mgonjwa

‘Mimi sio docta wa binadamu, ingekuwa ni komputa, aah, ningesaidia,.... sasa kwa hali kama hii mimi nitasiadia nini,...tumuachie docta afanye kazi yake,....’akasema huku akiwa haonyeshi kujali.

Na kuna jamaa wa mgonjwa walikuwepo, mmoja akasema;

‘Lakini uliambiwa mapema kipindi mgonjwa akiwa hajazidiwa kihivyo,  huyu mama alitaka kukuona wewe hukufika....’akasema na jamaa akaangalia saa yake

‘Lakini subiria, atazindukana tu, huwa inatokea hivyo, na akizindukana anakuwa na hali nzuri na mnaweza hata kuongea japokuwa wakati mwingine kwa shida, si unajua hata macho yake hayana nguvu, kwahiyo ni mpaka ujitambulishe.....’akaambiwa

‘Kwa hali kama hiyo kuna kuzindukana hapo,...hiyo ni pamoja na uzee tena, unajua mpaka sasa najiuliza ni kwanini alijiingiza kwenye gari, mimi sina kosa kabisa, niliangalia kote kulikuwa hakuna mtu, ghafla huyu hapa, nilikanyaga break lakini wapi....’akasema kama kujitetea

‘Tatizo sio hiyo ajali, tatizo ni kuwa huyo mama anataka kukuona wewe, ...’akaambiwa

‘Haya sasa ndio hivyo nimefika anione sasa, mnaona hali aliyo nayo, na mnasema hata kuona ni shida, atanitambuaje? eeh....labda anadai fidia,..au.....’akasema na docta akawa keshamaliza kumuhudumia mgonjwa, na sasa alikuwa kasimama akionyesha kutaka kuongea jambo

‘Wewe ndiye nani....?’ akauliza

                   ***********

Docta alipoona huyo mama katulia, kwani alikuwa akihangaika sana, na alipompima akaona ni tatizo la shinikizo la damu lipo juu, akajitahidi kulishusha,...na baadaye, alipoona huyo mama katulia, ndio akasogea kumuangalia huyo jamaa

‘Wewe na huyu mama mpoje?’ akaulizwa

‘Tupoje kwa vipi,....kiujumla mimi simjui..., ila nasikia kuwa anataka kuonana na mimi, ...nahisi, labda ni kwa vile mimi ndiye nilimgonga kwa bahati mbaya..., labda anataka kunilalamikia,..lakini kiujumla kosa ni lake, zaidi ya hapo mimi simfahamu....’akasema

‘Una uhakika na unachokisema, maana huyu mama hadi sasa shinikizo hilo la damu, ni kuashiria kuwa kuna kitu kinamsumbua, na huenda ni hiyo hali ya kutaka kukuona  wewe.....’akasema docta

‘Si ndio hivyo nimekuja docta, sasa kwa hali hiyo docta anaweza kunifahamu, .....au niwaulize mnataka mimi nifanye nini....’akasema

‘Huyu mama alikuwa akisema anataka kumuona mtoto wake, ...na watu wamekuita hapa wakijua wewe ni mtoto wake,je wewe sio mtoto wake?’ akauliza

‘Mimi sio mtoto wake kabisa ..’akasema

‘Oh, kwa hali hiyo mimi .nashangaa ... sisi tunayemuhitajia hapa ni mtoto wa huyu mama...’akasema docta akiwaangalia jamaa wengine

‘Mimi sijui, na siwaelewi hawa watu, kwanini wanasema mimi ni mtoto wa huyu mama!, ....kwanini wanitafute mimi, kwanini wasimtafute mtoto halisi wa huyu mama, nilishaamwambia mimi sio mtoto wake....’akasema na jamaa wakawa kimia, na docta akasema

‘Kwahiyo wewe ulishawahi kukutana na huyu mama kabla, watu wakakuambia huyu ni mama yako, na wewe ukakataa, au sio?’ akaulizwa

‘Ndio...na niliwaambia kabisa ....tatizo hawa watu hawataki kunielewa...’akasema

‘Sasa kwa kukuuliza tu, wewe wazazi wako wapo wapi, na kwanini wakuambie wewe kuwa huyu ni mama yako,...?’ akauliza na kwa muda ule Profesa, akafika,
Mara kwa mara Profesa huwa anafika,  ila kaka yake hakuweza kufika kwani hali yake  naye haikuwa nzuri, huko nyumbani kijijini.....

‘Docta samahani naomba niingilie kati haya mazungumzo yenu kidogo, maana mimi ndiye ninayefahamu haya yote, huyu kijana,...namuita hivyo kijana kwa vile mimi ndiye niliyemlea, namfahamu sana...’akasema na docta akatulia kusikiliza

‘Kiukweli huyu kijana ni kweli alikuwa hawafahamu wazazi wake,...kutokana na sababu sio muhimu kuzitaja hapa...ila sasa imetokea hivi,...na ni bahati kuwa kawakuta watu wema, wamembainisha wazi kuwa hawa kweli ndio wazazi wake, yaani huyu mama na kuna baba yake yupo huko kijijini naye anaumwa...’akasema Profesa

You again....unawadanganya watu....’akasema huyo jamaa, akimuangalia Profesa kwa macho ya hasira na mshangao!

‘Una uhakika kuwa ,mimi nawadanganya watu...kijana angalia sana, hii ndio nafasi yako ya mwisho utakuja kuijutia...’akasema Profesa na docta akawa anawaangalia hawa watu wakijibishana kwa hamasa

‘Kwanini unasema hivyo, kuwa nina uhakika, na wewe mtu, ..kwanza.mimi sikujui,....kama umewadanganya watu kuwa mimi ni mtoto wa huyu mama, na yule mzee,...aliyeniletea fujo nyumbani kwangu umekosea sana,...kwanza wewe, wewe, siamini kuwa wewe ndio yule marehemu....’akasema

‘Sikiliza nikuambie kitu,...unaweza kuukana ukweli, lakini ukweli ukawa pale pale, ni kama kutwanga maji kwenye kinu,...sijui kwanini bado hujazindukana,... na umri huo ulitakiwa uelewe ukweli halisi, ....yale ya zamani ulikuwa ni utoto, sasa kwa umri huu, bado unakataa ukweli , ili iweje, hawa ndio wazazi wako hata kama wana hali ambayo huitaki wewe, hutakiwi kuwakana....niambie wewe umezaliwa na nani, umetoka mbingunu....?’ akauliza profesa

‘Na nikuulize wewe, kwani nyie mnataka nini kwangu, nikubali hayo kirahisi tu, ili iweje, hiyo ili iweje ulitakiwa wewe, ujiulize....au eeh, mnataka mpate nini kwangu,...niambieni wazi ni nini mnachokihitajia kwangu....?’ akauliza

‘Tunataka nini kwako!!...?’ akauliza Profesa,

‘Ndio mniambie....’akasema

‘Yaani kukutambulisha kwa  wazazi wako ni kosa, ni kuwa kuna kitu tunahitajia kutoka kwako....unajidanganya kweli kweli...., mimi naweza kusema kuna kitu labda nataka...., lakini hawa ni wazazi wako wana haki,...’akasema

‘Unaona eeh, wewe unasema nini, kuwa labda kuna kitu unataka kutoka kwangu, kitu gani...nilijua kabisa wewe ndiye chanzo cha matatizo haya yote, nafahamu wewe unachotaka ni nini, kama kweli ndio wewe...lakini sheria ipo wazi, hakuna aliyekulazimisha kuuza ile nyumba, uliuza kwa shida zako...sasa wewe unataka kuwaingiza watu wengine kwenye shida zako....’akasema

‘Hahaha...hilo lina wakati wake muda ukifika,...,sio sasa...’akasema akiashiria kwa mkono kukataa

‘Muda gani ukifika wakati kila kitu kipo wazi....’akasema

‘Kijana, wajifanya huelewi, wamekuharibu kiakili au sio ...sheria zipo ndio, lakini kwa ujanja zililazimishwa ziendane na,shida iliyotengenezwa itokee....’akasema

‘Shida zikatengenezwa, ili sheria ziweze kufanya kazi yake,..unasikia mimi sio mtoto mdogo, mimi sio mjinga...najua mipango yote na yote nimeshayaweka sawa,.... muda utafika tutapambana kisheria..., lakini kwa sasa ni hili, ....’akasema akionyesha kidole kule kitandani.

‘Kijana hili litakupeleka kubaya, na utakuja kuumia kweli, hata hayo maisha unayoringia usiyaone , nakuambia ukweli...’akasema

‘Unanitisha,....hahaha, unanitisha mimi, unanifahamu sana kuwa mimi sitishiki,...kwanza kwani nimemuibia mtu, kwani nilikuja nyumbani kwenu nikawasumbua, ...nyie ndio mliokuja kwangu na kuniletea fujo, na kama ni wivu, sijui...’akasema huku akitikisa kichwa

‘Wivu wa nini, nani akuonee wivu wewe.....kwa utapeli, au..au wajifaya hujui kuwa kilichofanyika huko ni utapeli...’akasema Profesa

‘Tapeli ni wewe, ukazidiwa ujanja,..lakini hata hivyo,...kama ni mali, mbona vyote nimevifanya kwa akili zangu, kwa juhudi zangu......sikuelewi, ni nini unataka kwangu,,,,wewe ulishatambulikana umekufa,,...’akasema akitaka kuondoka

‘Nimekufa eeh, sasa nimefufuka, tutapambana ....najua sasa matumbo joto, huyo mama mkwe wako, atakuja huku kutoa ushahidi....’akasema na akaona kaongea sana akakatisha

‘Mimi sikuogopi, nenda kokote , na wala simtemgemei yeye, ....usinitishe kwa hilo,.....’akasema

Sikiliza kijana kwa kukusaidia, kwanza malizana na hawa wazee, msikilize huyo mama yako anakuhitajia, huyo ni mama yako,....ni mama yako nakuambia tena na tena....’akasema na jamaa akatiksia kichwa kukataa

‘Nakuambia tena huyo ni mama yako, na nilishakuambia mara nyingi, wazazi wako wapo na utakuja kukutana nao,  mimi ndiye ninayefahamu,...na mimi ndiye nafahamu wapi ulipotokea, huyo mama mara kwa mara akizindukana anakutaja wewe,...’akasema akiashiria kwa kidole, na jamaa akawa anatikisa kichwa kukataa.

‘Kataa lakini huo ndio ukweli, huyoo mama anakutafuta wewe, toka ulipotoweka machoni mwake, na yote unayoyaona hapo, kapofuka macho, haya sasa umemgonga ni kwasababu yako wewe,anahangaika kukutafuta ,...huyo ni mama yako aliyekubeba tumboni miezi tisa, akahangaika na wewe, huyo huna ujanja wa kumkataa...hujazaliwa hewani...’akaambiwa

That is your style men...i know you,...hahaha, Mama, mama.. kwanini sasa mama, hebu nambie,  wakati naitwa chokoraa, mtoto wa mitaani, yatima,....asiye na wazazi, wewe kama kweli ndio wewe, hukuwepo...ulikuwepo, kwanini hukusema wazazi wangu wapo,...wewe, ukasadikisha hayo kuwa kweli mimi ni mtoto yatima, ..je huyo mama hakuwepo?’ akawa kama anauliza

‘Nilishakuambia ....’akasema Profesa

‘Ulishaniambia nini, wewe sema kwa vile una lango jambo, unataka kuwatumia hawa wazee kwa vile ni jamaa zako, au sio, sasa hivi nashangaa,..kila mtu sasa anaweza kusema yeye ni baba yangu, yeye ni mama yangu,...sikubali....’akasema akikunja uso wa kutafakari

‘Hayo ni mawazo yako kijana ya kujaribu kuukwepa ukweli,...mimi kila kitu nilishakuambia ni kwanini ilitokea hivyo, hebu nambie nigeacha ungelifika huko ulaya wewe, ungempata huyo mke wa kizungu, au hilo hulioni, leo wajiona msomi, mtaalamu, ni kwa juhudi hizo,.... sawa, uliitwa hivyo, lakini kwa masilahi fulani,.... usitake niongee sana, huu sio muda wake ...’akasema Profesa

‘Huo sio muda wake kwa sababu ni uwongo....’akasema kwa hasira, na docta akawa keshaondoka, na Jamaa aligeuka na kuangalia pale kwenye kitanda, akageuka kuangalia nje, halafu akageuka kuwaangalia watu waliokuwepo, akaangalia saa yake halafu akasema

‘Huwezi kunihadaa kirahidi hivyo, mimi nilishawauliza , so what....tuweni wahalisia, ili iweje, hebu niambieni mnataka mimi nifanye nini....ok, kama ni msaada wa gharama nitatoa, kwa vile nimemgonga kwa bahati mbaya, then...?’ akauliza akionyesha mkono wa kukata tamaa

‘Jibu unalo wewe mwenyewe, sisi kazi yetu ilikuwa hiyo, tumeshakuambia kuwa huyo ni mama yako mzazi..wewe sasa sio mtoto mdogo, unayo akili, msomi..., sasa ni kazi yako wewe kutimiza wajibu wako kama mtoto wa huyo mama, unachotakiwa hapo ni kusubiria, au kufanya vyovyote uwezavyo, ili akizindukana akuone, vinginevyo, ....’akasema Profesa akionyesha kwa mikono

‘Mimi nina kazi  zangu, ...siwezi kukaa hapa kusubiria,.... nyie kama mna mda, ok ...basi akizindukana mtanipigia simu nitakuja, ...sawa? ‘ mara simu yake ikaingia ujumbe wa maneno akaiangalia akasema

‘Unaona sasa hivi nahitajika ofisini nilitoka kidogo tu....kwa kujiiba,’ akasema huku akiangalia saa yake,

‘Halafu linguine niwaambie ukweli, mimi siwezi kukubali kirahisi hivi, hasa baada ya haya yote...’akasema na kumgeukia Profesa, wakawa wameangaliana usoni

‘Hasa ...wewe, wewe ni tapeli, hata Ulaya wanakufahamu hivyo, ndio maana ulifukuzwa, na na nahisi hata familia yenu  muelekeo ni huo huo...kwahiyo, eeh,  kama ni kuja nitakuja tu kibinadamu kwa vile mimi nimemgongwa huyu mama kwa bahati mbaya, na sivinginevyo....’ akasema akageuka huku na kule kama anatafuta kitu

‘Eti,...mama, eti huyu ni mama yangu, sikubali,...nitakuja tu, nyie nipigieni simu, call me, please,...’akasema na kuanza kuondoka

‘Kijana....’akasema Profesa akiangalia kitandani alipolala huyo mama, nahisi aliona kitu, lakini huyo anayemuita kijana alishaondoka
Ilikuwa ni nafasi ya mwisho ya huyo kijana, kwani wakati ule anaondoka, huku nyuma huyu mama alizindukana,na cha ajabu akawa anaongea vyema, kiasi kwamba watu waliingiwa na furaha kuwa hatimaye mama huyo keshazindukana kabisa

‘Mtoto wangu yupo wapi, nilimsikia...., keshaondoka...?’ akauliza

‘Ndio....lakini atarudi...’akaambiwa

‘Mhh....sijui kama ataniwahi..masikini....haya nitafanya nini mimi, sikupenda iwe hivyo.....’akasema na mazungumzo hayo yalikuwa ya mwisho kwa huyo mama , kwani usiku ule taarifa za huzuni zikazagaa....

Tuishie hapa leo


WAZO LA LEO: Mabadiliko ya kweli hutokana na wewe mwenyewe hasa unapofikia umri wa kujitegemea, Wewe au mimi, ukiwa na utashi, na akili zako timamu, huwezi kusubiria mpaka usukumwe, au usikie kauli ya mtu fulani, ndio ujitumem hata kile unachoweza kukifanya, au kukiona, na hata ukweli ukiwa wazi machine mwako ...huo sasa utakuwa ni utumwa, muhimu ni kujituma wenyewe., hiari yashinda utumwa.... 

Ni mimi: emu-three

No comments :