Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeMonday, December 7, 2015

RADHI YA WAZAZI-59


Mara kukasikika kelele za watu wakisema ......

‘Amegonga, kaua, kaua....’, na kelele zilipozidi zikafanya vikao vilivyokuwa ndani ya  mahakama kukatishwa na watu wakatoka nje kwa haraka, kila mmoja akitaka kuangalia ni nini kilichotokea. Na kwa ujumla, kwa muda ule ndani ya mahakama kulikuwa hakuna shughuli zozote za kesi zaidi ya hivyo vikao viwili ambavyo vilikuwa vinamaliza maliza kile walichokuwa wakiongea.

Watu wale waliokuwa mahakamani  walitoka na kukimbilia nje, na kukuta kundi la watu wakiwa wamejikusanya pembeni mwa bara bara , ni sehemu magari yanayotoka kwenye mahakama yanapopitia ili kuingia kwenye barabara kuu.

‘Kumetokea nini jamani....’Profesa akauliza, na swali hilo likaulizwa na karibu kila mtu aliyekuwa katokea ndani, na hata wale waliokuwa nje, walikuwa wameshaanza kundoka, kuelekea kwenye shughuli zao, kwahiyo hao wachache waliokuwepo wakitembea kutoka eneo la mahakama hakuna aliyeweza kuona hilo tukio zaidi ya kuhisi tu, kwani ni tukio lililotokea kwa haraka sana.

Ni kweli wegi hawakuliona hilo tukio, japokuwa walikuwepo hapo nje, sana sana walikimbilia pale barabarani kuangalia nini kimetokea na ndipo wakamkuta huyo mama kalala pembezoi mwa barabara.... ,

Ni mtu mmoja tu, naye alikuwa akitoka mlangoni mwa mahakama, huyu alikuwa mmoja wa wazee wa mahakama, anayeaminika, ndiye aliyebahatika kuliona hilo tukio na ilikuwa ni kwa bahati tu, kwani wakati tukio hilo linatokea mtu huyo alikuwa anatoka kwenye mlango wa mahakama, na wakati anatoka ndio akaliona hilo tukio.

‘Wakati natoka tu, macho yangu yakaona ...nilihisi mwili ukiniisha nguvu, nilishindwa hata kupiga kelele kumwambia dereva, hata hivyo gari lilikuwa kwenye mwendo ule wa kasi wa kuzunguka,, ....’akaanza kusema.

‘Huwezi kumlaumu dereva kabisa,....kwani huyu mama ni kama alijipeleka...ila dereva, sijui kwanini, hakusimama, mimi sikupoteza muda nikawapigia hospitali, kijana wangu anaendesha gari la wagonjwa......’akasema huyo mzee

Kwa muda huo, wengi walikuwa wakihangaika kupata nafasi ya kuangalia ni nini, na japokuwa walishahisi kuwa ni ajali, lakini wengi walitaka kuhakikisha ni nani aliyegongwa,...

Hawa walitoka ndani ya mahakama walichelewa, kwani gari la wagonjwa lilishafika,... na wahudumu wakawa wameshaanza kumuhudumia huyo mhanga, na maaskari wakaanza kazi ya kuwaondoa watu wasogee mbali na eneo hilo

‘Kwahiyo ni ajali ni mtu kagongwa....’akasema Profesa sasa akimsogelea yule mzee aliyeona kilichotokea, na kwa muda huo alikuwa akitoa maelezo kwa maaskari usalama

‘Ndio ni ajali mama mmoja kagongwa.....’akasema huyo mzee akimjibu Profesa

‘Kagongwa vipi ...hapa ni sehemu ya kumgonga mtu, huyu mtu alilewa?’ ni swali jingine kwa mtu mwingine

‘Ni ajali kiukweli,...ila kinachonishangaza ni huyo dereva, baada ya tukio , sijui kwanini hakusimama,....’akasema huyo mzee

‘Ilikuwaje kwanini, ikawa ni maswali mengi na sasa waliokuwa wakielezea ni watu wengine waliomsikia huyo mzee akisimulia...?’ akaulizwa na kwa muda ule gari la wagonjwa lilishaanza kuondoka na huyo mhanga wa hiyo ajali.

‘Ni mama gani huyo aliyegongwa?’ swali likauliza na huyo mzee akawa anashindwa amjibu nani, amuache nani, ikabidi aanze kuelezea tu

‘Ni mama mmoja hivi....’akasema huyo mzee


                          **********

‘Mama mmoja,..mama yupi huyo....’aliyeuliza sasa alikuwa mshitakiwa , huku akiangalia huku na kule kama anamtafuta mtu anayemfahamu.

Profesa naye akawa anaangalia huku na kule na wazee wengine wakawa wanafanya hivyo hivyo, ikionyesha kila mtu alikuwa akiliwaza hilo

‘Yule mama aliyetuacha pale kwenye kikao yupo wapi...?’ akauliza jamaa mmoja

‘Kweli, na si ana matatizo ya kuona, yule binti anayemsaidia na yeye yupo wapi?’ akauliza Profesa

‘Mzee huyo mama aliyegongwa yupoje....?’ akauliza mshitakiwa

‘Mimi simfahamu vyema, ila wakati natoka ndio nikaona hilo tukio ..niliona lile gari likirudi kwa nyuma, na.jinsi lilivyojigeuza kwa haraka ili kuelekea barabarani, na wakati linaigeuza kwa haraka ndio huyo mama akatokea na kujipeleka, alikuwa anakimbia ....’akatulia

‘Likamkanyaga..?’ akauliza

‘Halikumkanyaga, lilimgonga, na kumrusha juu, akaenda kudondokea bara bara kuu....Lilimkosa kosa,....’akasema

‘Akadondokea kwenye lami? ‘akauliza mtu mwingine

‘Kichwa kiligongwa kwenye lami, hilo nimeliona kabisa, yaani ni hatari....’akasema huyo mzee

‘Kwahiyo kupona ni bahati...?’akauliza mwingine

‘Ya mungu mengi, maana nilimuona akitikisika mara mbili kama mtu anakata roho akatulia huyo mzee akionyesha masikitiko

‘Mungu wangu.....’aliyesema hivyo alikuwa mshitakiwa

Mara akatokea binti mmoja akiwa kabeba kikapu akioyesha kuwa alitokea kununua vitu sokoni, alipoona watu wapo nje wanaongea kuhusu ajali, akasimama akiwa kaduwaa, na aliyemshitua alikuwa Profesa...

‘Wewe yule mama yupo wapi?’ akaulizwa

‘Nilimuacha ndani ya mahakama, nilimuambia asitoke mpaka nirudi, kwani nilitumwa kununua hizi bidha, ili muda wa kuondoka tuondoke nazo, atakuwa yupo ndani...’akasema huyo binti akitaka kuingia mahakamani

‘Mungu wangu....’ilikuwa sauti ya mshitakiwa aliyekuwa kashikilia kichwa

‘Huyo mama aliyegongwa yupoje..?’ akaulizwa mzee aliyeona hilo tukio. Na yule binti alirudi kutoka ndani akiwa sasa kachanganyikiwa, akawa anaanza kulia...

‘Oh, dada yangu,......oh dada yangu....’akawa anahangaika na watu wakafanya kazi ya kumtuliza, na ikaonekana hakuna zaidi ila kuelekea huko hospitalini

                       ***********

Hospitali yenyewe hakikuwa mbali nimwendo wa kutembea tu, ila wale wenye usafiri, wakasaidia kutoa msaada wa gari, na aliyeweza kusaidiwa alikuwa mshitakiwa akiwa na 
Profesa na yule binti anayetembea na huyo mama na wazee wengine

‘Mpaka sasa tunahisi tu kuwa ndio yeye, maana watu wengi wa huku hawamafahamu huyo mama, na .....’akasema mzee mmoja

‘Atakuwa ni yeye.....’akasema mshitakiwa

‘Kwanini unasema hivyo, wewe ulikuwa ndani kama sisi.....’akaambiwa

‘Hiyo ajali niliiona kwenye ndoto....nilishaawaambia kuna mambo yatatokea...mimi nikiota jambo fulani ujue kuna jambo litatokea,....na sijui....’akasema na watu wakamuangalia kwa mashaka

‘Ndoto,...ndoto inatokea ukiwaza, ...bro achana na imani yako hiyo kwani hiyo ndoto ilikuwaje,,,?’ Profesa akasema na baadaye akauliza

‘Ndoto kama hiyo, inaashiria mikosi tu,...tumuombe mungu ...’akasema kaka mtu akiwa kama vile yupo kwenye njozi

Na kwa muda huo wakawa wameshafika hositalini, na haraka haraka wakaelekea chumba cha wagonjwa mahututi, na madakitari ndio walikuwa wametoka kuhangaikia wagonjwa waliofika muda huo

‘Samahani dakitari kuna mama mmoja aligongwa na gari,.....’akaanza kusema Profesa

‘Nyie ndio jamaa zake....?’ akauliza huyo dakitari akiwa na haraka za kuondoka

‘Ndio, tulikuwa mahakamani ajali hiyo ikatokea....’akasema Profesa

‘Huyo mama bado, hajaweza kuzindukana,....’akasema docta akiwa kasimama sasa

‘Oh, tunaweza kumuona mara moja maana hatuna uhakika kama ni huyo tunayemuulizia...’akasema Profesa na huyo dakitari akaonyesha uso wa kushangaa

‘Hamna uhakika...?’ akauliza

‘Ndio wakati ajali hiyo inatokea sisi tulikuwa ndani ya mahakama, na tulipotoka alishachukuliwa, ndio maana tunataka kuhakikisha tu kama ndio yeye huyo mama jamaa yetu....’akasema mshitakiwa

‘Sawa nimewaelewa, twendeni huku...’docta akasema na wote wakamfuata nyuma, na alipoona hivyo, akasema

‘Sio wote jamani, wawili au watatu wanatosha...’akasema na Profesa , kaka mtu na yule binti naye akataka kwenda kuthibitisha, na mzee mwingine akajichomeka

Walifika kwenye chumba, wakaambiwa, watamuona kwa kupitia kwenye dirisha kuna kiyoo kinaonyesha kwa ndani, lakini hawaruhusiwa kuingia ndani, kweli alikuwa ndio yeye, na kilio cha yule binti anayemsaidia kikatanda ikawa ni kazi ya kumliwaza tena

‘Nitasema nini mimi nyumbani....niliambiwa nisiachane naye hata mara moja..sasa nimemuacha na haya yametokea,....’akasema kwa uchungu huku akilia!

‘Lakini ni bahati mbaya....’akaambiwa na wakati huo huyo dakitari alikuwa kaingia kule ndani, na muda baadaye akaja kuwaona....

‘Hali ya huyo mama bado haijawa vyema , kwani kwa vipimo vya haraka aliumia kichwa na sasa hivi tunafanya uharaka wa kupata picha.....tuone kama dawa imeingia ndani, tutamchukua kwenye vipimo vya   cit-scan, ili tuone kuna athari gani, baada ya hapo ndio tutajua utaratibu mwingine...’akasema docta na kuondoka

Na baada ya muda huyo mama akachukuliwa kupelekwa chumba cha vipimo hivyo, na jamaa zake hawa wakawa wamesimama pale pale wakisubiria, na wakati wanasubiria ndio sauti ikatoka...

‘Masikini ....mtalaka wangu.....sasa najilaumu sana, sikutakiwa kumfanyia hivyo, huenda haya yote yasingelitokea,.....mmh ’ilikuwa sauti ya mshitakiwa, akiwa kajiinamia alionekana kabisa analia, na Profesa alimuangalia ndugu yake huku na yeye moyoni akawa anajilaumu, hakusema kwa sauti, lakini akilini alisema

‘Yote haya kosa ni langu....nisingefanya niliyoyafanya, labda haya yasingelitokea...ujanja ujanja wangu ndio huu,...nilijua nitapata , nilijua nitamtumia nipate nay eye apate na familia yake ipate, lakini kumbe haikuwa njia muafaka...nafahamu kabisa hakuna atakaye lielewa hilo kila mtu atakayefahamu yote yaliyotokea ataishia kunilaumu mimi....’akawa anawaza huku akitikisa kichwa

‘Lakini hata hivyo, kosa sio langu....huenda mambo yangeenda vyema,..., kosa ni la hawa watu, mama mtemi na watu wake,....wamemrubuni huyu kijana wakamuharibu, ..na huyu kijana wangu, hata hataki kufikiria wapi alipotokea, kaamua kunisaliti,.....sitamsamehe kwa hili, nitapambana naye....’akawa anazidi kuwaza

Haikuchukua muda docta akaja, na hakuongea na wahusika alipitiliza kwanza, na aliporudi akaingia tena kwenye hicho chumba na alipotoka, sasa akawajia na kusema

‘Nyie ni ndugu zake huyo mama wa karibu au sio..?’ akauliza

‘Ndio.....’wakasema

‘Kipimo kinaonyesha damu imepenya kwenye ubongo, kidogo....lakini kiutalamu, damu ikigusa ubongo, kuna athari zake...., na bado tunahangaika, tuone zaidi, ila kwa hali aliyo nayo, inabidi kuhamishiwa hospitali kubwa zaidi...’akasema ni kama hakutaka kuulizwa maswali zaidi akaondoka

‘Sasa docta.....’alikuwa Profesa lakini docta alishaondoka na baadaye akarudi na kusema

‘Nilikuwa nataka kuongea na ndugu yake  wa karibu sana....’akasema na aliyejitokeza ni Profesa na kaka mtu naye akafuata nyuma

‘Bro, wewe pumzika, naona kwa hali yako hutakiwi , niache mimi nikaongee na docta ...’akasema Profesa, lakini kaka mtu hakutaka kuitikia wazo hilo akaelekea huko kwa dakitari
Dakitari hakutaka kupoteza muda, akasema

‘Ndugu zanguni, kutokana na vipimo, yanekana damu imeingia na kugusa ubongo, mmmh, kwa hivi sasa siwezi kusema kuwa kuna athari zozote, tunajitahidi kadri ya uwezo wetu kupunguza hilo, na tunachoshukuru ni kuwa  mgonjwa kazindukana, japokuwa akili haijawa sawa ...’akasema

‘Oh, kwahiyo anaweza kungea....?’ akauliza mshitakiwa

‘Mhh, hapana,bado  ..ila, ni kawaida, hutokea hivyo, mgonjwa kama huyo akizindukana huwa wengine hawawezi kusema kabisa, wengine mwili mnzima unakuwa haufanyi kazi,....na tungesema upasuaji, lakini hapa kwetu hatuna utaalamu huo...’akasema

‘Kwahiyo kama damu imegusa ubongo, itakuwaje...tunaweza kutumia tiba mbadala, zipo dawa zinasaidia...’akasema Profesa

‘Hizo dawa haziwezi kusaidia,...tumekaa na wenzangu tukaona ni bora mtu huyu asafisrishwe kupelekwa Muhimbili...’akasema docta

‘Muhimbili...hatafika, mnapoteza muda bure...’alikuwa mshitakiwa akitikisa kichwa, na docta akamwangalia halafu akayazarau manen yake akasema;

‘Sasa tulikuwa tunahitajia msaada wenu,..gari lipo...lakini...gharama za mafuta....hata hivyo, nilikuwa nawaambia tu, muanza kukusanya kusanya, ili tuweze kuona ....kwa hivi sasa bad tunajitahidi ,tutakuja kuwaambia cha kufanya,...’akasema docta

‘Umesema keshazindukana, naweza kuongea naye....?’ akauliza Mshitakiwa

‘Ndio, ...na hilo limetupa faraja, na kuna muda aliweza kuongea na alichoweza kusema ni maneno machache...’mtoto wangu namtaka haraka..mtoto wangu, ....’ lakini hatuwezi kuruhusu mtu kuongea naye kwa sasa,...’akasema

‘Na huyo mtoto wake ataongeaje naye...?’ akauliza Profesa

‘Kwani huyu mtoto wake yupo hapa, ndio huyu binti mliyekuwa naye?’ akauliza doctor

‘Hapana huyo binti ni mdogo wake sio mtoto wake....’akasema Profesa

‘Ni vyema mkamuita huyo mtoto wake, inaweza kusaidia sana....’akasema docta na Profesa akamuangalia ndugu yake aliyekuwa kainama chini, akiashiria kuwa kwenye mawazo manzito, na alionekana kama hayupo kwenye hali nzuri

‘Vipi bro, upo sawa.....’akauliza na kaka yake akasimama, na alionekana kama sio yeye, akawa anaangalia hewani, halafu akasema ;

‘Mungu wangu, nilijua tu...ile ndoto...nilijua tu...’.na ghafla mara akatikisa kichwa, akainua mikono na kushika kichwa akiashiria maumivu, na docta akasimama haraka, lakini alikuwa kachelewa, mzee akadondoka chini, ....

Tuishie hapo kwa leo, tunamalizia malizia msichoke, tuzidi kuombeana heri,....


WAZO LA LEO: Jinsi umri unavyokuwa mkubwa, na ndivyo uhimili wa matatizo unavyopungua, Ukiangalia maisha yetu ya Kiafrika, kuhangaika hakuwiani na kipato, kiasi kwamba mtu anafikia utu uzima hata kujiwekeza anakuwa bado, na zile zinazitwa akiba ya uzeeni zinakuwa hazina thamani sawa na uhalisia wa maisha kutokana na kushuka kwa thamani ya pesa,.. na  utakuta muda unavyozidi kwenda ndio matatizo yanakuwa mengi, kwa uoni wangu, labda sasa pensin iangaliwe upya thamani wakati inapochangwa iwe sawa na kipindi inapolipwa kama mafao
Ni mimi: emu-three

No comments :