Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Wednesday, December 2, 2015

RADHI YA WAZAZI-58


‘Mimi kamwe sijakubaliana na hilo mnanilazimishia tu, kwa vile mumeamua wenyewe fanyeni mtakavyo, msinishirikishe tena, lakini msije kuja kusema mimi  nimekubaliana na nyie hapana, vunjeni sheria wenyewe,....’akasema shahidi,

‘Hutujakulazimiaha shahidi,huo ni uamuzi wako, sisi tulichokuwa tunataka ni kukutanisha wewe na baba yako, ambaye ulikuwa humfahamu, mfahamiane, na muafikiane, ...japokuwa kosa limefanyika, lakini kwanza hebu fahamianeni,...ni muhimu hilo kiubinadamu...’akaambiwa na

So what..?’ akauliza kwa mshangao,

‘Ili iweje!...haah, tulifanya hivyo, tukijua kuwa hilo laweza kuwa ni muhimu kwako, kuwa wewe hatimaye umemfahamu baba yako, ni vyema mkakaa mkaongea mkajuana na makosa ni makosa yanaweza kuangaliwa upya, ina maana wewe hujafurahi kumtambua baba yako, uliyekuwa humfahamu, ....?’

‘Ili iweje? Ndio nawauliza hivyo,..., hata kama yeye ni baba yangu, so what,..., hawa wababa wanajitokeza kwenye raha tu, wababa gani hao,....huyo sio baba yangu, huyo ni muhalifu, hebu niwaulize ina maana sheria haitafanya kazi yake kwa vile huyo ni baba yangu, ....na ni nani kawathibitishia hilo kuwa ni kweli,...’akasema akiangalia saa yake

‘Jamani nyie watu,... hebu angalieni wenyewe, muda mliotumia, gharama, bado mnatafuta njia ya kukwepesha haki isifannyike, kwa vile...no siwezi kuamini hili, yeye ni nani kwenu....?’ akauliza

‘Tulijua labda kwako itakuwa ni faraja kumpata mzazi wako, tulijua baada ya hilo, wewe utabadili nia, utapenda kwanza mkae na baba yako mfahamiane vyema....ndio mawazo yetu, ..na kama ni baba yako kweli, kihekima ni vyema mkakaa kwanza mkajuana,..ina maana hilo kwako sio muhimu,....? ‘ aliulizwa

Yeye alitikisa kichwa kuashiria kushangazwa

‘Ina mama kumbe wewe  humtaki mzazi wako,..inashangaza kabisa kuna nini hapa,..’akasema muendesha mashitaka  akitikisa kichwa

‘Huyo sio baba yangu, huyo ni mhalifu, mbele ya mahakama huyo ni mhalifu, nilishaongea mbele ya hakimu, hao watu ni matapeli,...,  je alichofanya ni kizuri, hajakosea, haijalishi kamfanyia nani....’akasema huyo jamaa, huku muendesha mashitaka akiwa haamini, kaduwaa....

Muendesha mashitaka huyo alipoona shahidi huyo kadhamiria anachokiongea akaamua kumuuliza swali ambalo alishawahi kumuuliza kabla

 ‘Nakuuliza tena, je upo tayari.mzazi wako, baba yako afungwe, na hata baada ya kuthibitishwa kuwa huyo ni baba yako mzazi, ?’ akamuuliza

‘Muheshimiwa, kwanza huna uhakika kuwa huyo ni baba yangu, unao uhakika huo? ...huna,.... pili, hata kama ni baba yangu, tusema hivyo, ila sio baba yangu, siwezi kuwa na baba kama huyo,..mfano  akikosea ina maana hastahiki kushitakiwa,...?’ akauliza shahidi

‘Sijakukatalia hilo,...ila huyo ni baba yako, ulikuwa humfahamu,....kutokana na wakili mtetezi,  na tulitaka kulithibitisha hilo kisheria kwa kupata vipimo vya kitaalamu,kama vielelezo,ambavyo vitathibistiha kuwa huyo ni baba yako, na tulitarajia hilo linaweza kuwa furaha kwako, na ungeliweza kubadili nia,....’akaambiwa

‘Ndivyo sheria inavyotaka hivyo,...?’ akauliza huyo shahidi kwa mshangao

‘Kuthibitisha ndio...sheria inataka tuthibitishe hilo, tutafanya hivyo,ili na wewe ujirizishe...’akaambiwa

‘Kuwa mhalafu akidhaniwa kuwa ni mzazi wako, wewe mtoto uliyetendewa makosa huna haki tena,..si ndivyo mnavyotaka kufanya, sheria ndivyo inavyosema.....?’akasema na kuuliza

‘Oh,....labda wewe hujatuelewa,...tulichotaka kukifanya  ni kuja kuondoa lawama, ....kama wewe bado unashinikiza, hata baada ya kufahamu kuwa huyo ni baba yako, basi sisi tutafuata taratibu, lakini kuna hayo mambo lazima yafanyike, hayo ni maagizo ya muheshimiwa,....’akaambiwa

‘Maagizo gani?’ akauliza

‘Kwanza kuthibitisha kuwa kweli huyo ni baba yako, ushirikiano wako unahitajika, hilo tutalifanya kwa kuchukua damu yako na ya mshitakiwa, kuhakiki hilo, na pili kuwemo na kikao cha mariziano, kama kweli ni baba yako, ...na baada ya hapo, kesi itaendelea...tutaona .....’akaambiwa

‘Mnapoteza muda bure for nothing, am sory...’akasema na kugeuka kuanza kuondoka

‘Sikiliza kijana, wewe bado mdogo, hujui athari ya haya yote, sisi tumefanya haya kwa nia njema kabisa, kwa ajili ya maisha yako ya baadaye, sio kwamba tumeshindwa kutimiza wajibu wetu, lakini tusije kufanya hivyo,  baadaye yatakayotokea nije mimi kulaumiwa,...nakuuliza tena, upo tayari kumfunga baba yako baada ya kuthibitisha hilo?’akaulizwa shahid.....

‘Sikuelewi muheshimiwa.......

Yule shahidi, ambaye kutokana na wakili mtetezi  ‘ni mtoto wa mshitakiwa’, hakutaka kuendelea kusikiliza akaanza kutoka nje akiwa na hasira hakujali muito wa muendesha mashitaka ambaye alikuwa hajamalizana naye,...

Na wakati huo kukatokea tukio upande wa pili, tukio lililomteka akili muendesha mashitaka badala ya kuendelea na mtu wake, akawa anaangalia jambo, upande huo wa pili huku akiwa kanyosha mkono wa kumuashiria huyo shahidi asubiri....asiondoke

Lakini shahidi huyo hakusubiri...aliondoka!

Ni wakati huo huo, ....wakati shahidi huyo anaondoka

Upande ule wa pili, upande ambao sasa wakili muendesha mashitaka alikuwa akiuangalia..., akatokea mama mmoja, aliyekuwa akionekana kutaka kuongea na wale watu kwenye lile kundi, lakini ilionekana watu wale hawakuwa tayari kumsikiliza,...

Lakini cha ajabu, alichoona wakili huyu, ni pale yule mama, ghafla alipogeuka, kipindi kile kile huyu shahidi akiwa anatembea kutaka kuondoka, na ndipo wakili muendesha mashitaka akagundua kuwa mtu wake keshaondoka, ...na kujaribu kumsimamisha lakini alikuwa keshachelewa.

Muendesha mashitaka akawa sasa anatoa simu yake kutaka kumpigia mlinzi kuwa asimruhudu huyo shahidi kuondoka, na alipotoa simu yake akakuta haina chaji, imezimika, ..
                                                 *********

 Yule mama akiwa katulia, akiwa katega masikio, akasikia wakisema;

‘Mimi siwezi kukaa na huyo muhuni,  labda kama yupo mzazi wake mwingine atalifanya hilo,...’ sauti hiyo ilimuuma sana, akasimama, japokuwa aliambiwa asije kuondoka hapo, lakini alihisi vibaya

‘Mimi kama sio baba yake na ameshasema hivyo,  sitaweza kukaa na huyo muhuni, huo ndio msimamo wangu, ....’ sauti ile ambayo anaifahamu vyema ikasema tena

Oh, wewe usiseme hivyo huyo ni mwanao....akawa anasema kiakili, akaona anahitajika kuliongea hilo, yeye anahitajika kuchukua hatua kabla hajachelewa,

Akaanza kutembea kuelekea hapo wanapozungumza hao watu, haikuwa mbali ana pale alipokuwa amekaa..

‘Kama mimi nilivyosema ,.huyu ndiye baba yake, atakaa naye watakubaliana...’sauti ikasema na huyo mama akazidi kujisikia vibaya, kwani hajui baba mwingine zaidi ya huyo anayeongea, kwanini leo amkane mwanae,....hapana ni lazima ni mwambie ukweli...akawa sasa anatembea

‘Kama mama yake angelikuwepo hapa, basi angejumuika naye, kwenye hicho kikao, wakakubaliana lakini sio.....’ sauti hiyo ilisema na yeye alishafika karibu, na ndipo akaona asizidi kunyamaza akasema;

‘Mimi mama yake nipo nitakaa naye meza moja nitaongea naye, ....’na wote wakageuka kuangalia sauti ilipotokea, na waliomsikia , waliokuwa karibu naye wakamuona, lakini cha ajabu wakampuuzia....

                               **********

Mama yule moyo ukawa unamuenda mbio, kwani kuna hisia nyingine zilikuwa zikimuhitajia, alihitajika kufanya jambo, na akiendelea kukaa na hao watu, atachelewa, kwa haraka akazifuata hizo hisia, akageuka kwa jinsi hisia zilivyomtuma,....haraka, fanya haraka,...hisia zikamwambia hivyo...

Kweli kwa haraka akaanza kutembea,  akahisi kuna jambo jingine muhimu zaidi ya kuongea hapo, akatembea kuelekea huko hisia zinapomtuma,...akahisi, akamuhisi, mwili ukaingia na kitu kama msisimuko, akahisi ile hali ya uzazi, mama na mwanae,.... akasimama, akanyosha mkono wa kutaka kumshika  alijua kuwa ndio yeye....lakini aliikuta akipigwa kikumbo, akapepesuka...lakini hakuanguka

Akaitahidi, kwani alijua asipofanikiwa hapo, ndio basi tena.......lakini hisia, na ule msisimuko ukaanza kumuisha, ina maana keshaondoka.....hisia zikamtuma akimbie kuelekea huko...akatembea kwa haraka kuelekea huko, huku akisema;

‘Subiri, usiendoke....subiria wewe mtoto, utaangamia...’ huku akitembea na mara akapigwa kikumbo na mtu mwingine, lakini alijua kabisa huyo sio anayemtaka, akazizoa zoa, na akajihisi yupo mlangoni, akahisi hali ya hewa ya nje, akajua yupo nje,, hata mwanga ulipenya kwenye mboni zake, ....mwanga unamsaidia kuona,...lakini sio sana, anaweza kuona giza akajua ni mtu kamkaribia, lakini hawezi kumtambua

Ila cha ajabu, ....aliyekuwa mumewe, ...hata akipita nje ya nyumba atamtambua, ...hata akiwa kwenye kundi la watu atamtambua,...lakini keshakuwa mbali naye tena, inabakia kumbukumbu za maisha yao ya upendo enzi hizo.....

Hisia hizo za ajabu, pia zipo kwa mwanae, mtoto wake aliyemuona kama sehemu ya mwili wake, siku alipompotea alihisi kupotewa na sehemu ya mwili wake, na kweli aliliona hilo, kwani uafahamu wa kuona ukaondoka, mwili ukawa hauna nguvu, na alijua kama mwanae ataweza kurejea akawa karibu naye, huenda ufahamu huo utarudi...

Siku aliondokewa na ufahamu huo, alilia sana, alitaabika, akawaambia ndugu zake wajitahidi wampate mtoto wake, lakini hakupatikana, na akawa akilia usiku na mchana,..hadi akawa haoni kabisa, ikawa imebakia hisia, na kumbukumbu wakati anamlea mtoto wake, hadi siku ile kule kisimani alipokwenda kuchota maji,

Anakumbuka vyema, siku ile ilimjia ile...akapatwa na kizunguzungu akaanza kuvutwa, na hali ili ikitokea fahamu humpotea na kinachoendelea baadaye hakifahamu mpaka kupute muda, fulani, akizundukana huambiwa tu alifanya hivi na vile

‘Hiki ni kifafa, lakini kinatokana na urithi,ila kilikuwa hakina nguvu sana, nguvu yake ilisababishwa na msomgo wa mawazo, kama ataweza kudhibiti mawazo yake, hili tatizo linaweza kupoa, lakini sio kupona...’anakumbuka siku alipokwenda na mama yake akimuhangaikia, kipindi hicho alishajifungua...na kauli hiyo ilimkatisha tamaa moja kwa moja

‘Mimi sasa kiburudisho changu ni mwanangu,  huyu ndiye atanipa tumaini...nikiwa naye sitakuwa na mawazo.....’akasema akiwa akimlea mwanae, lakini cha ajabu kipindi hicho tatizo hilo lilimuandama sana,....na ikawa ndio sababu ya kumpoteza mtoto wake....

Kupotea kwa mtoto wake ikawa ni pigo kubwa sana,.....macho yakawa hayaoni, ..kuna muda kunakuwa na unafuu anaweza akaona kwa mbali,... lakini hali hiyo haidumu kwa muda mrefu, maana mawazo ya mtoto wake yakimjia basi hisia za kuona hufifia kabisa...

‘Sasa usichelewe, kumuona mtoto wako,  huko mahakamani ndio sehemu yako yam wish ya kumsaidia huyo mtoto wako, hakikisha unamzuia asitoke hapo mahakamani kabla hajashikana mikono na baba yake, kabla hamjashikana mikono wewe na mtoto wako kuashiria kukubaliana, muhimu mridhiane, ukifanikiwa kwa hilo matatizo yote yatakwisha,....

'Nakuonya, ukichelewa huyo mtoto akitoka hapo mahakamani, kitakachokuja kutokea huko mbele, ni hatari,...nasikitika... hutaweza kumsaidia tena huyo mtoto wako na wewe mwenyewe...’alikumbuka ndoto hiyo iliyokatishwa kwa yeye kuzindukana kwenye usingizi,  na aliyekuwa akimuambia hayo, alikuwa hamjui....

Na alipozindukana, akakumbuka kuwa siku hiyo ndiyo siku ya kesi, akawaambia ndugu zake ni lazima afike huko mahakamani,.....

‘Uende kufanya nini, hujaitwa kama shahidi, ...’akaambiwa

‘Ninakwenda kusaidia, nakwenda kumuokoa mtoto wangu, na baba yake, nisipofika nikasaidia, hakuna msaada mwingine wa kulitatua hili tatizo ...’akasema

‘Kwa vipi, ...wewe unakwenda kuleta matatizo huko.....’akaambiwa

‘Ni lazima niende, ni muhimu sana niwepo....’akasema na ndugu wakashindwa kumzuia, basi  akaambiwa wataondoka na mdogo wake ambaye amekuwa msaada mkubwa kwake.

Mdogo wake huyo ndiye anayemsaidia kila anapotaka kwenda na amekuwa sasa yeye ndiye macho yake , kumuelezea kile kinachoendelea, na ndiye muongozaji wake kwa kila anachotaka kukifanya, kama inahitajika kutembea au kufanya chochote, na kiukweli, ...walipendana sana.

Basi mdogo mtu alipoambiwa kuhusu hiyo safari, alikubali mara moja akasema;

‘Mimi nitaenda naye.....’

Na wanandugu japokuwa hawakutaka hiyo safari, lakini kwa vile huyo mdogo wake atakuwa naye, wakawa na amani kidogo, kwani yeye anamjulia huyo mama, hasa ikitokea tatizo la kuanguka kwa matatizo hayo ya kifafa, huyo mdogo wake alikuwa anafahamu amfanyie nini dada yake...

‘Hakikisha huachani naye, na ukienda sokoni kununua hizo bidhaa uwe naye, usimuache....’akaambiwa, na kosa alilolifanya ndio hilo, aliondoka akamuacha dada yake, akiendelea kusikiliza kinachoendelea mahakamani, dada yake hakutaka kuondoka kabisa mpaka akamilishe kilichompeleka hapo, na kukamilika kwake ni mpaka akutane na mshitakiwa na huyo shahidi aliyekuwa kasimamishwa siku hiyo

Huyo Mama alishindwa afanye nini, akamwambia mdogo wake:

‘Unajua mdogo wangu, ni muhimu nionane na huyo mshitakiwa,...kama nilivyokuambia wakati tunakuja’akasema huyo mama.

‘Kwa hivi sasa itakuwa vigumu sana, alipofika tu aliambiwa aende akakae kule mbele, nilishindwa kumuambia kuwa unataka kuongea naye...’akasema mdogo wake

‘Sasa nitampataje, maana ni muhimu sana...’akasema huyo mama

‘Kwahivi sasa ni vigumu sana, kwani haruhusiwi kuongea na mtu mpaka kesi imalizike....’akasema mdogo wake,na huyo mama akasikitika kweli, lakini hakuwa na la kufanya, baadaye ndio akaitwa huyo shahidi huyo mama alishahidi kitu, ...na hata alipoitwa huyo shahidi hali yake na shauku ikawa ipo juu, na akamuuliza mdogo wake;

‘Na huyo shahidi, nitampataje.....’akauliza akimshika mdogo wake kwenye vigana vya mkono.

‘Huyo anayehojiwa sasa hivi huwezi kumuona pia, inabidi tusubiria amalize kuongea na wakati anatoka ndio nimfuate....’akasema mdogo wake

‘Oh, kila mtu muhimu kumuona mpaka kesi imalizike, na ikimalizika hapo kila mtu anaondoka mbio mbio, huu kweli ni mtihani, kukosa nguvu za haya macho sina ujanja, sijui sasa tutafanyaje maana muda wa amani unakwisha, kitakachofuata ni hatari...’akasema dada yake, na mdogo wake hakumuelewa, alichukulia ni maneno ya dada yake ya kila siku, akazarau.

Wakati kesi inaendelea huyo mdogo mtu akaona atumie nafasi hiyo akanunue vitu, ili wakiondoka wasiende sokoni, kwani muda utakuwa sio mnzuri kwenda sokoni na kurudi kituoni, akasema

‘Sasa dada sikiliza kesi bado inaendelea, mimi nakimbia sokoni, kununua vitu, nitarudi kabla kesi haijamalizika, nikirudi nitahakikisha hao watu wako mnaongea nao, mmoja baada ya mwingine...’akasema

‘Kweli...sijui, haya nenda haraka usichelewe, utanikuta hapa hapa,...mimi nimeshakata tamaa,na huyu shahidi hamalizi tu, mbona wanamtesa tu...maswali mengi...hawajui tatizo ni nini, wangeniita mimi....’akasema huyo mama

‘Haya wewe usiondoke, ....ukae hapo hapo, ....’akasema mdogo mtu na kuondoka kwa haraka...na aliporudi, alikuta kesi imekwisha kinachoendelea hakieleweki kila mtu kashika shavu, huyu anaongea hiki yule anaongea kile...

Akaingia ndani ya mahakama, hakumkuta mtu, akatoka mbio na kuanza kuulizia,

‘Jamani kuna mama mmoja nilikuwa naye humu ndani ana matatizo ya macho mumemuona wapi...?’ akaanza kuulizia..hadi alipokutana na Profesa akiwa na ndugu yake, na ndipo akawaelezea kuwa huyo mama alikuwa akitaka kuongea na huyo mshitakiwa

‘Mhh...kuna tatizo limetokea....’akaanza kuongea Profesa, kaka mtu alikuwa hawezi hata kuongea

‘Tatizo gani, dada yangu kapatwa na nini....?’ akauliza na wakati huo gari la wagonjwa lilikuwa linaondoka kuelekea hospitalini

                                        *********
Kwani ilikuwaje...swali aliloulizwa aliyekuwa shahidi, na hapo kumbukumbu zikamreea wakati akiwa mahakamani wakati alipokuwa akiongea na muendesha mashitaka, na sasa akawa mbio mbio kutoka nje.....

Ni wakati ule, akiwa anatoka mbio,..na wakati anatoka akageuka kuangalia kundi lile, kundi lile ambalo lilimnyima raha, lakini cha ajabu macho yake yakamuona mama mmoja, aliyekuwa akigeuka , na kuanza kutembea muelekeo wa mlangoni....huko anapoelekea yeye, hakuwa na muda wa kumuangalia huyo mama  ni nani, japokuwa hisia zake zilimvuta kufanya hivyo, akazizarau, nia ni kutoka mle ndani kwa haraka, kabla muendesha mashitaka hajamzuia tena

‘Huyu muendesha mashitaka lazima nimkimbie haraka..atanichelewesha hajali muda huyu, hanielewi....’akawa anaongea kwa sauti ndogo, huku akitembea kwa mwendo wa haraka, hakutaka kizuizi kingine mbele,...oh, huyo mama!

Cha ajabu alichokiona ni kwa jinsi yule mama alivyotembea kwa haraka na kuja kuweza kusimama katika ya njia, ambayo yeye alitakiwa kupita, ili aufikie mlango na kutoka nje.

Kwa hasira , kwa kuchanganyikiwa hakutaka hata kufahamu huyo mama ni nani, akamfikia yule mama na kumpiga kikumbo, na yule mama akapepesuka, lakini huyo mama hakuanguka, na huyo mama hakuacha,kunyosha mikono kama kutaka kumzuia, na wakati anampiga huyo mama kikumbo, ndio alisikia sauti ya huyu mama akisema;

‘Mwanangu kubali, ...kubali yaishe, shikana mkono na baba yako, usipofanya hivyo,...utapata taabu, acha ukaidi.....’sauti hiyo aliisikia masikioni mwake,ilikuwa ya huyo mama, lakini hakusimama akawa ameshatoka nje,

‘Mwanangu mwanangu, kila mtu ananiita hivyo, nitakuwa na wazazi wangapi....’akasema huku akiingia kwenye gari lake..hakutaka kugeuka nyuma, hakutaka kuongea na mtu, alikuwa akikimbizana na muda!

Akili ilikuwa kama sio yake, kwanza alishachelewa, alitakiwa kumpeleka mkewe kwenye sherehe za akina mama, akina mama wanaotoka huko ulaya walipokuwa wakiishi, na mkewe ni kiongozi wa hilo kundi, kwahiyo ilikuwa ni muhimu sana kwa mkewe, na zaidi walitakiwa kwenda na waume zao!

‘Nitafika mahakamani, nikiona wananichelewesha nitaondoka tu....’alimwambia mkewe, na mkewe akasema;

‘Sawa usiniangushe, nikifika pale bila mume, sijui nitajisikiaje...’akasema mkewe

‘Ni lazima tutakwenda wote, sizani kama kesi hiyo itachukua siku nzima, ushahidi wangu upo wazi....’akamuhakikishia mkewe

Na bahati mbaya, ikatokea hivyo, muda ukawa ni kitendawili kwake,  na alipoona saa zinazidi kwenda na muendesha mashitaka anazidi kumbana, akaona hana jinsi , ndio akatoka mbio, ....hakujali cha nani tena....alishaamua,

Aliingia kwenye gari, akawasha gari tayari kwa kuondoka, akageuza kichwa kuangalia nyuma, akaona kweupe,.. na kwa haraka, akarudisha gari nyuma, akaangalia kwa haraka kushoto, halafu kulia, akaona hakuna mtu, akaligeuza gari kwa haraka,muundo wa U,....na wakati analigeuza kwa haraka, ndipo akamuona yule mama...akitembea kwa haraka na kuliingia gari....

Alishachelewa, akajaribu kukanyaga breki, lakini gari lilishakubali, alichoona ni yule mama akirushwa hewani, na kutupwa pembeni mwa barabara kuu....

Gari lilishageuka kwa jinsi alivyochanganyikiwa akakanyaga mafuta, gari likaondoka kwa mwendo wa kasi, na kuingia barabara kuu, hakusimama wala kuangalia kushoto au kulia, kichwani alikuwa anakumbuka miadi yake na mkewe, alishachelewa, akazidi kuongeza mwendo.... kuelekea nyumbani kwake!.

‘Nitajibu hilo tatizo baadaye....sio kosa langu, walioona watanisaidi...’akasema huku akiendesha gari lake kwa mwendo kasi,...na alipofika nyumbani alimkuta mkewe mlangoni, akiwa kakasirika, alishajiandaa kuondoka na gari lake mwenyewe,

‘Samahani mke wangu,....’akasema na mkewe hakusema kitu, akaingia kwenye gari, kwa haraka wakaondoka kuelekea huko kwenye hiyo shughuli!

                                   **********

Waliporudi tu, wakakuta ujumbe, jamaa anatafutwa na polisi, ...kabla hajakaa sawa polisi wakaingia, jamaa akakamatwa...hadi kituo cha polisi, kwenda kujieleza!

‘Kosa lako umegonga, na baada ya kugonga ukaondoka,...japokuwa uliyemgonga ndiye mwenye makosa, mashahidi waliona....yule mama haoni vyema, aliiingiza mwenyewe wakati gari linapiga kona kuingia barabara kuu....

‘Kosa lako kwanini hukusimama....?’ akaulizwa

‘Ni kweli nakubali ajali hiyo ilitokea,.... lakini sio kosa langu, na sikuweza kusimama kwasababu nilikuwa na dharaura ya muhimu sana, nilikuwa na miadi isiyoweza kusubiria mke wangu alitakiwa kuwahi kwenye mkutano muhimu wa wanawake wa waliowahi kuishi nchini mwao, kuna msaada wa kuwekeza hapa nchini kwetu, kwa kupitia kwa hao akina mama, ...na mgeni rasimi ni mke wa mkuu wa nchi, hebu angalia umuhimu wake...’akasema akitabasamu kuonyesha alikuwa akiongea jambo la muhimu sana.

‘Lakini uligonga...na ...’afande akawa anaongea na jamaa akamkatisha akisema;

‘Halafu afande, Mke wangu ni kiongozi wa umoja huo, na mimi nilitakiwa niwe naye, walitakiwa kuongozana na waume zao, kwahiyo nilikuwa na haraka,...haraka, ... na ukumbuke muda ule nilitoka mahakamani kutoa ushahidi, nilikuwa nimechanganyikiwa...maswali yalinichosha kichwa changu!

‘Umeona afande...Ikizingatiwa muda wa kuondoka na mke wangu ulishapita, alikuwa akinisubiria, .....’akatulia akimwangalia afande kwa makini

‘Hata kama ulikuwa na haraka gani, inapotokea ajali, unatakiwa usubirie...si unaelewa hilo?’ akauliza

‘Afande mimi nilifuata kanuni zote za barabarani,niliangalia kote kulikuwa hakuna mtu,  na wakati nageuza gari, ndio...., huyo mama akaliingia gari, ni kama vile alitaka agongwe, gari lilishakuwa kwenye mwendo...kiukweli huo ni uzembe wake mwenyewe..’akajitetea

‘Umeelewa kosa lako?,...., kwanini ulipogonga hukusimama, kisheria na kiubinadamu, ilitakiwa usimame, uone hali ya huyo mama, ili asaidiwe, ...baadaye ungelitoa huo udhuru wako, baada ya trafiki kufika na kupima,... wewe uliona mkutano huo ni muhimu kuliko maisha ya huyo mama,...?’ akauliza afande

‘Hivi nikuelezeje afande,...wawezekezaji toka nje, ...hilo sio muhimu,  ...., na mgeni rasmi ni mke wa mkuu wa nchi, na mke wangu ndiye mwenyekiti wa umoja huo, sasa hebu jiulize mgeni rasmi afike, na mwenyekiti hayupo....angeelewekaje, ....na kwa ujumla mimi sikuwa na makosa, huyo mama ndiye mwenye makosa...’akasema akiashiria kwa mikono

‘Unamakosa,  kwanza, wewe mwenyewe umekiri kuwa ulikuwa umechanganyikiwa ukiwa umetokea mahakamani, sawa si sawa...?’ akauliza na jamaa akaonyesha mikono ya kuashiria anapotezewa muda

‘Sheria zinasema huwezi kuendesha gari ukiwa unahisi umechanganyikiwa, pili ukagonga hata kama kosa sio lako lakini ulitakiwa kusimama, ili trafiki afike kukagua,...hilo kosa, nakuandikia makosa hayo, utakwenda kujibu mahakamani...sawa?’akaambiwa na huyo askari

‘Mahakamani, niende mahakamani wakati nimeshakuelezea, na ushahidi upo kuwa mimi sina makosa,....haiwezekani.....hilo sikubali na mimi naondoka afande, nimechoka, na uzembe wa nyie watu, hivi hii nchi ina watendai gani, makosa na sheria ipo wazi, mnataka kupindisha, mnataka nini  ...’akasema akitaka kuondoka

‘Sikiliza huwezi kuondoka, unatakiwa kwanza uweke sahihi yako hapa kuthibitisha makosa yako,nipe leseni yako ya gari kwanza...’ akaambiwa

‘Leseni yangu ya nini....?’ akauliza na huyo afande akawa anafunua kikaratasi, akasema

‘Na pili nimekuambia, huyo mama hali yake ni mbaya sana...anataka uende ukaonane naye anakuhitaji, huo ni ujumbe kutoka huko hospitalini...huu hapa’akasema huyo askari akimuonyesha huyo jamaa karatasi, jamaa hakutaka hata kuuangalia, akasema;

‘Hali yake ni mbaya ok, ,... am sory, sio kosa langu,....na kwanini atake kuniona mimi, mimi sio dakitari,....isitoshe mimi sikumgonga kwa makusudi, kwenda nitakwenda, lakini sio leo...kwa hivi sasa nina miadi, nina wageni muhimu nyumbani....kesho, eeeh, kesho, naweza kwenda, ...’ akasema, na yule askari akamuangalia kwa macho ya kushangaa.

‘Wewe ni mtu wa ajabu sana, umesema ulimgonga huyo mama kwa bahati mbaya, au sio..? basi kiubinadamu, kiutu, ulitakiwa kufika kumuona huyo mama, na kumuomba msamaha, angalau kutoa msaada wa kiutu....’akasema huyo askari

‘Afande, ukisema mimi nikamuomba msamaha unakosea,...na nahisi yule mama ana matatizo...’akasema akiashiria kichwani

‘Ndio ana matatizo ya macho haoni vyema....’akasema askari

‘Nilijua tu....’akasema huyo jamaa

‘Ulijuaje,....unaona kumbe ulifahamu huyo mama ana matatizo hayo, kwanini hukuchukua tahadhari, halafu ungesimama basi.....,lakini kwanza tuyaache hayo unahitajika uende huko hospitalini....hapa utaniachia leseni yako ya gari’akasema afande

‘Nilimuona huyo mama wakati tupo ndani, mimi natembea akazuia njia, ...lakini sikumuona jinsi alivyotaka, .... nilishutukia tu nimeshamgonga, ,....kwa leo afande, am sory, siwezi kwenda huko afande...na leseni yangu siwezi kukupa’akasema

‘Taarifa imesema hivyo, kuwa leo ni muhimu uende huko ukamuone huyo mama, ...taarifa ilikuja hapa mara mbili, wanasema hali ya huyo mama ni mbaya, na muda mwingi amekuwa akikuhitajia wewe,....’akaambiwa

‘Ananihitajia mimi kuwa ananifahamu au kwasababu ya hiyo ajali....?’ akauliza

‘Ndio tunajiuliza na sisi, je wewe huyo mama uliyemuona ndani humfahamu  kabla, je kabla ya siku hiyo, hukuwahi kuonana naye, huna mahusiano naye,.....?’akaulizwa

‘Simfahamu,....afande, mimi simjui kabisa,... kama nilivyowaambia huyo mama kumuona kwangu ni wakati nataka kutoka nikiwa ndani mahakamani, ...na kwa jinsi nilivyomuona nahisi kama ana matatizo ya akili.....’akasema

‘Mbona nasikia, wamesema huyo mama anasema anataka akuone wewe ni mwanae, ametaja hivyo,kuwa wewe ni mtoto wake, ....’akaambiwa

‘Mtoto wake,! Hahaha, huyo kachanganyikiwa, ....mimi sio mtoto wake!...mimi naondoka nasubiriwa nyumbani nina wageni muhimu....’akasema na kwa haraka akasimama na kutoka nje akitaka kuingia kwenye gari lake....lakini akazuiwa

‘Lete leseni, hiyo ni amri...utakuja kuvipata mahakamani...’akaambiwa na kukatokea mzozano, lakini baadaye jamaa akakubali, akijua ni faini tu inahitajika, na akiendelea kukaidi atazidi kuchelewa. Akaitoa leseni na kutaka kuingia kwenye gari...

‘Gari hilo huwezi kuondoka nalo ...’afande akasema kwa sauti, na jamaa akabaki kaduwaa
Tuishie hapa kwa leo...kwani inasikitisha, tutaona itakavyokuwa,


WAZO LA LEO: Vyovyote itakavyokuwa thamani ya mtu yoyote huwezi kuilinganisha na kitu ...mali, au kuithaminisha na kitu! Utu wa mwanadamu ni kitu pekee. Inapotokea jambo, kuchagua mtu, utu wa mtu au mali,...usiangalie mali kwanza, wengi wapo tayari kuhatarisha maisha ya watu, hata kuua, kwa ajili ya mali, ni nani kakuambia hiyo mali unaweza kuipata ukaitumia kabla  umauti haujakushika!

Ni mimi: emu-three

No comments :