Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeTuesday, November 10, 2015

RADHI YA WAZAZI-53Siku ikafika na kesi ikabidi ifanyike, baada ya juhudi ya kutaka kesi hiyo ifanyike nje ya mahakama kushindikana, baada ya juhudi ya kuwakutanisha wahasimu hawa wawili mshitakiwa na mlalamikaji kushindikana, na wakili ambaye alijitahidi sana kuona jambo hilo linamalizwa kwa amani ikafika mahali akasema kashindwa ,iliyobakia mahakama ndiyo itaamua, ...

‘Ndugu yangu wewe ni rafiki yangu, nakumbuka ulinisaidia sana dawa kipindi kile naumwa sana pumu, na ugonjwa huo nimeshausahau,...nakumbuka ulinisaidia mengi enzi zile, ndio maana nikihakikisha nafuatilia hili swala lenu nione kama litaweza kumalizwa kwa amani, lakini naona imeshindikana....’alisema wakili akiwa kashikilia barua mkononi

‘Lakini hujaongea na hakimi ukamuelezea hali halisi,unaona kaka yangu anaumwa.....’akasema Profesa

‘Sasa hivi nimetoka mahakamani na nimepewa barua hii, kuwa kesho kutwa ni siku ya kusikiliza kesi yenu....’akasema

‘Na nilijaribu kuongea na waendesha mashitaka , wao ndio kabisa hawataki mazungumzo yoyote kwani wao wanadai kuwa wana ushahidi kuwa tendo lililofanyika lilikuwa la kudhamiria, na pia kumekuwa na vitisho kwa wenye nyumba, ambao ndio walalamikaji  ....’akasema

‘Lakini hivyo vitisho ni nani amevifanya mbona sisi hatujawahi kufikiria kufanya kitu kama hicho...?’ akauliza profesa

‘Wao wanasema wana ushahidi kuwa nyie ndio mnaofanya hivyo,...mumetuma watu kuwatishia amani, na sasa hivi wanaishi kwa hofu,.... ndio maana wanataka kesi hii ifanyie hukumu itolewe ili iwe fundisho kwa watu wasiotii sheria....’akasema wakili

‘Hakuna namna nyingine ya kusaidia hii kesi, maana kama kesi ni kesho kutwa, na barua imeshotoka, unafikiria sisi tutafanya nini...je tutawezaje kushinda....’akasema Profesa akionyesha kukata tamaa.

‘Yote sasa inategemea mashahidi wao wa mwisho ambao watahitajika kufika kuthibitisha hilo tukio, kwani siku za kesi zilizopita walifika walinzi tu, sasa wenye nyumba wanahitajika kufika kuthibitisha hilo kuwa hivi sasa wanaishi kwa hofu kwa kutishiwa amani...’akasema

‘Kwahiyo tufanyeje...kwa hivi sasa na hali ya kaka kuna siku inakuwa mbaya,...siku nyingine nzuri, haeleweki nahisi ni kutokana na hii kesi?’ akauliza profesa

‘La kufanya hakuna kwa hivi sasa....labda nikusikilize wewe, ulisema kuna jambo ulitaka kuniambia ...ni jambo gani hilo....?’akasema wakili na kuuliza

‘Mhh...ni kweli kuna jambo ninalotaka kukuambia, sijui kama litasaidia, ni jamboo ambalo sikupenda lijulikane kwa hivi sasa, kwani linaweza kuendeleza chuki badala ya kusaidia lakini kwa hali ilivyo sasa ni bora nikuambie ili uone kama linaweza kusaidia kwenye hii kesi, japokuwa kwa jinsi ninavyomfahamu huyo jamaa sizani kama ataweza kulichukulia maanani...’akasema Profesa

‘Ni jambo gani....lolote laweza kusaidia lakini mpaka nisikie ni jambo gani?’ akauliza wakili, na 

Profesa akaanza kumuelezea jambo hilo kwa kirefu

Tuendelee na kisa chetu

******************
Kesi ilianza kwa taratibu zake na waendesha mashitaka wakatakiwa kutoa mashahidi wao ambao walihitajika siku hiyo, na ndipo akaitwa shahidi ambaye alijitambulisha jina na baada ya taratibu za kimahakama kufuatwa, na baada ya kutaja jina lake akaanza kuulizwa maswali...

‘Haya tuambie wewe siku ile ya tukio ilikuwaje...?’ akaulizwa

‘Mimi nilitokea kazini na nilipofika getini, nikapiga honi kama kawaida na wakati geti linafunguliwa mara akatokea mtu mbele ya gari langu akiashiria nisimame, na baadaye mtu huyo akasogea kwenye kiyoo cha gari na kuanza kugonga kwa nguvu....’akasema

‘Alikuwa akigonga na nini....?’ akaulizwa

‘Ni jiwe alilokuwa nalo mkononi...’akasema

‘Alikuwa akigonga kiyoo na jiwe...?’ akaulizwa

‘Ndio, ndio maana nikafungua mlango kwa hasira,...na nilipotoka kwanza niliangalia mlinzi yupo wapi,...., maana nilishaingiwa na wasiwasi, na muda ule mlinzi alikuwa kwa ndani akifungua geti, likawa wazi, na mlinzi alipomuona huyo mtu kasimama pembeni ya gari langu, akaja , na kwa muda huo na mimi nikawa nimeshatoka nje ya gari.....’akasema

‘Ukisema huyo mtu una maana gani...?’ akaulizwa

‘Mshitakiwa huyo hapo...’akasema akimnyoshea mkono mshitakiwa

‘Ikawaje?’ akaulizwa

‘Nilishikwa na butwaa pale nilipomuona mlinzi wangu akivuja damu.....’akasema

‘Akivuja damu sehemu gani...?’ akaulizwa

‘Kichwani,....’akasema

‘Ukafanyaje...?’ akaulizwa

‘Kiukweli nikahisi kuna jambo la hatari, nikamuuliza mlinzi kulikoni maana alihitajika kupata huduma ya kwanza, kwa jinsi alivyokuwa na damu,... lakini huyo mshitakiwa hakunipa muda huo akaniandama kwa madai yake , ..’akasema

‘Madai gani hayo....?’ akaulizwa

‘Anasema alikuwa akitaka kuongea na mwenye nyumba kwani kuna ndugu yake kaambiwa aliwahi kuingia humo ndani, na kuhusu mlinzi kwanini anavuja damu akasema ni kwasababu alimfundisha adabu kwa vile hakuwa na majibu mazuri kwa wageni........’akasema

‘Ni kweli kuwa kulikuwa na ndugu yake humo ndani?’ akaulizwa

‘Kulikuwa hakuna mtu yoyote humo ndani kwa siku hiyo, ...’akasema

‘Sasa kwanini akasema hivyo?’ akaulizwa

‘Kwa maelezo yake nikakumbuka kuwa kuna jamaa mmoja alifika siku tatu kabla ya tukio hilo, jamaa huyo alifika akijifanya yeye ni profesa, na kwa vile mimi nilikuwa nimetarajia kutembelewa na rafiki yangu wa chuo kikuu ambaye ni profesa nikajua ndio yeye, kwahiyo mlinzi aliposema kuna mgeni wangu profesa sikusita kumwambia amruhusu, na mara akatokea jamaa mmoja ambaye kwa maelezo niliyoyapata baadaye ndiye aliyekuwa akitafutwa na huyu mshitakiwa....’akasema

‘Huyo jamaa alikuwaje?’ akaulizwa

‘Huyo jamaa alikuwa mgonjwa kwa jinsi alivyoonekana, mimi sikuweza hata kuongea naye, kwani nilikuwa nje siku hiyo, nilipoingia kwa ndanii ili niweza kuongea naye, mara ghafla al
akadondoka na kupoteza fahamu ikawa ni kazi ya kumpeleka hospitalini, tukamtibia kwa gharama zetu japokuwa hatumfahamu...’akasema

‘Kwahiyo shahidi kwa jinsi ulivyosikia alisema alikuja kumuona huyo jamaa yake mgonjwa?’ akaulizwa

‘Hayo sasa tulikuja kuambiwa baadaye, ...’akasema

‘Kwanini alitumia nguvu badala ya kuulizia yaliyotokea kwa huyo ndugu yake, ..?’ akaulizwa

‘Mlinzi alisema jamaa huyo hakutaka kuhojiwa, yeye aliofika alielekezwa wapi ndugu yake you hositalini kama tulivyoacha maagizo, lakini mshitakiwa yeye alidai anachotaka ni kuingia ndani na kuonana na wenye nyumba, na katika heka heka za kumwelewesha  huyo mshitakiwa yeye kwa ghadhabu zake akakimbilia kumiga mlinzi, ......’akasema

‘Ni kwanini ampige mlinzi ...?.’akasema

‘Ndio hapo mlinzi alishikwa na butwa kwani mlinzi wakati anarudi kwenye lindo lake , mshitakiwa ndiye alimvamia kwa nyuma,....

‘Je unahisi labda jamaa huyo alifanya hivyo kwasababu ya kuchanganyikiwa kuwa labda ndugiu yake kashikiliwa humo ndani?’ akaulizwa

‘Hapana ilionekana kabisa jamaa alifika hapo kwa shari,...kwani alielekezwa wapi ndugu yake yupo kama angekuwa akimjali ndugu yake angekimbilia hospitalini kumuangalia, lakini yeye alitaka kuingia ndani wakati sisi wenye nyumba hatukuwepo, na kwanini alishikilia jiwe, ....’akasema

‘Je kuna mambo gani mengine yalikuja kutokea baadaye kuonyesha kuwa jamaa hakuwa na nia njema ...’akasema

‘Baada ya hilo tukio, walifika askari, na walimkuta akiwa anapambana na mlinzi wangu, na mimi nikiwa najaribu kumtuliza, hakusikia akaendelea kumpiga mlinzi, maaskari waliokuja siku hiyo wanaweza kulithibitisha hilo...’akasema

‘Wakati anafanya fujo alitamka maneno gani labda?’ akauliza

‘Alisema na bado nitahakikisha mnahama kwenye hii nyumba,.....’akasema

‘Unahisi kwanini alisema hivyo?’ akaulizwa

‘Kiukweli sijui, maana hata huyo ambaye anadai ni ndugu yake wakati anaongea na walinzi, walinzi waliniambia alizungumzia maswala ya nyumba,  sasa sijui walikuwa na lengo gani na nyumba....’akasema

‘’Kwani wewe hiyo nyumba ni yako?’ akaulizwa

‘Ndio hiyo nyumba ni nyumba yangu, niliinunua nikiwa ulaya kwa pesa zangu, kwani nilijua nikirudi huku nyumbani, nahitajika kuwa na nyumba yangu mwenyewe, nina hati zote za umiliki ....’akasema

‘Ulinunua kama ilivyokuwa au ulinunua kiwanja?’ akaulizwa

‘Nilinunua ikiwa na nyumba ndogo tu, nikaijenga upya kama ilivyo sasa, .....’akasema

Baadaye akaja wakili mtetezi, na kuanza kumuhoji huyo shahidi

‘Unasema ulipofika getini kwako ulishangaa kuona mtu kasimama mbele ya gari lako na kugonga kiyoo kwa jiwe,...’unaweza kuonyesha jinsi alivyogonga kwa jiwe

‘Nipeni jiwe nionyeshe alivyogonga.....’akasema na watu wakacheka

‘Unamuona yule pale mshitakiwa ni mzee wa miaka zaidi ya sitini, anaweza kweli kufanya jambo kama hilo?’ akaulizwa

‘Swala sio umri, mtu anaweza kuwa na umri mkubwa akafanya mambo ya kitoto....’akasema

‘Unasema ulimuona mlinzi akivuja damu , alikuwa akivuja damu sehemu gani?’ akaulizwa

‘Kichwani....’akasema

‘Sehemu gani ya kichwa, mbele au nyuma?’ akaulizwa

‘Nyuma....’akasema

‘Tusema mimi nimesimama hivi nakuangalia wewe hivi kwelii unaweza kuona damu zikivuja kutoka nyuma?’ akaulizwa

‘Alikuwa kashikilia kichwa, na mkononi kulikuwa na damu...’akasema

‘Kwahiyo damu uliziona mkononi sio kichwani....?’ akaulizwa

‘Mkono ulikuwa na damu zilizotoka kichwani...’akasema

‘Unasema mlinzi alikuja pale alipokuwa kasimama mshitakiwa,....na wewe ulikuwa umeshatoka nje ya gari,...wakati huo mshitakiwa bado alikuwa na jiwe mkononi...?’ akaulizwa

‘Ndi....ndi....sikumbuki,...ninachkumbuka ni kuwa yeye alianza kumpiga mlinzi....’akasema

‘Ina maana mlinzi alipofika tu, yeye mshitakiwa akaanza kumpiga huyo mlinzi au kulitokea mazungumzo yaliyofikia mtafaruku huo?’ akaulizwa

‘Wakati namuuliza mlinzi kulikoni,...ndio kukatokea mtafaruku huo, ....’akasema

‘Kwahiyo sio kuwa mshitakiwa alianza kumpiga mlinzi kama ulivyosema awali, ..?’ akaulizwa

‘Mlinzi alipofika wakati nauliza kulitokea nini ndio mshitakiwa akamkabili mlinzi na kuanza 
kumpiga...’akasema

‘Kwa jiwe?’ akaulizwa

‘Ha....hapana, walishikana...’akasema

‘Kwahiyo hakuwa na jiwe mkononi...?’ akaulizwa

‘Kwa hali kama ile sikumbuki vyema...maana mimi niliingilia kuwaamua...’akasema

‘Mlinzi alikuwa na nini mkononi?’ akaulizwa

‘Na fimbo yake anayokuwa nayo akiwa lindoni ni kama rungu hivi ...’akasema

‘Je yeye wakati kunatokea vurugu hizo fimbo alikuwa nayo mkononi

‘Ndio....’akasema

‘Lakini hukumbuki kuwa mshitakiwa alikuwa na jiwe mkononi...?’ akaulizwa

‘Sikumbuki....sikuchukulia maanani kukumbuka hilo....’akasema

‘Yule ni mzee, ni baba yako, hivi kweli kwa mtizamo wako mtu kama huyo anaweza kufika kwenye makazi ya mtu bila sababu maalumu, aanze kuleta vurugu kama ulivyodai...?’ akaulizwa

‘Kwanza ondoa hiyo kauli yako....’akasema

‘Kauli gani...?’ akauliza wakili akionyesha kama kushangaa

‘Hiyo kauli kuwa mzee  huyo ni baba yangu, huyo mzee sio baba yangu...na siwezi kuwa na baba mkorofi kama huyo....’akasema

‘Huyu mzee sio baba yako...?’ akauliza wakili

‘Ndio huyo mzee sio baba yangu, na siwezi kuwa na baba kama huyo hunielewi...’akasema kwa hasira

‘Unasema huwezi kuwa na baba kama huyo kwasababu ni mkorofi, au kwa sababu sio baba yako wa kukuzaa...?’ akaulizwa

‘Kwa yote mawili , kwanza sio baba yangu wa kunizaa na pili sio baba yangu kwa tabia zake, nashukuru kwa hilo, wenye baba kama huyo wana shida ...’akasema na watu wakacheka

‘Je kwa kutaka kuthibitisha kauli yako hiyo, nikuulize baba yako yupoje?’ akaulizwa, wakili muendesha mashitaka akalipinga swali hilo, na wakili mtetezi akasema

‘Swali hili limetokana na kauli yake hiyo kuwa hawezi kuwa na baba kama huyo mimi nataka kutambua vyema baba yake yupoje kiasi kwamba awe tofauti na huyo mshitakiwa...’akasema

‘Je hiyo inahusiana vipi na kesi hii.....?’ akauliza wakili muendesha mashitaka

‘Nataka kuthibitisha kauli, kuwa ina ukweli ,....’akasema

‘Ili iweje kwenye kesi hii...?’ akauliza na hakimu akaingilia kati, na kwa mshangao hakimu akataka swali hilo lijibiwe

‘Baba yangu ni muungwana, aliyesoma, na hawezi kuwa na tabia kama hiyo...’akasema

‘Baba yako amesoma,ni muungwana, alishawahi kukutembea hapo nyumbani kwako...?’ akaulizwa

‘Hapana.....’akasema

‘Kwanini?’ akaulizwa

‘Kwasababu hayupo....’akasema

‘Kaenda wapi?’ akaulizwa

‘Hayupo duniani....’akasema

‘Pole sana, ina maana keshafariki ..si ndio...?’ akaulizwa

‘Ndi-o, aah,Sijui yawezekana....’akasema

‘Ndio halafu hujui, kipi ni sahihi hapo.....umesema baba yako ni muungwana, msomi kuonyesha kuwa unamfahamu , kuwa enzi za uhai wake alikuwa hivyo....au sio?’ akaulizwa

‘Nimesema sijui, sikuwahi kumuona, na simjui....enzi za uhai wake alikuwaje.....maana sikuwahi kuishi nao,......’akasema na watu wakacheka

‘Unasema humjui, na hukuwahi kumuona,je ulifahamu vipi tabia zake?’ akaulizwa na wakili akaweka pingamizi, na wakili huyu akajitetea na kuelezea kwanini kauliza swali hilo

‘Huyu  shahidi kapinga kuwa huyo hawezi kuwa ni baba yake na baba yake ni msomi, muungwana, lakini baadaye anasema baba yake hamjui,hakuwahi kuishi nao....kuonyesha kuwa huyu shahdi ni muongo,...’akasema wakili

‘Mimi sio muongo, ila maswali yako hayana msingi wa hii kesi , unanichanganya tu akili yangu.....’akasema shahidi akimuangalia muendesha mashitaka kama kuomba msaada, na muendesha mashitaka akaweka  pingamizi kuwa maswali ya wakili hayaendani na kesi

‘Yana msingi , kwa vile nataka kulithibitisha hilo, kuonyesha kuwa huyo shahidi ni muongo, hana heshima kwa wazee, na kuonyesha kuwa kauli zake chafu ndizo zilimfanya mzee, mshitkiwa kupandwa na hasira....’akasema

‘Mimi sikuwepo wakati wanaongea na mlinzi....’akasema shahidi

‘Hukuwepo ila ulifika baadaye na wewe na mlinzi wako mkaanza kumpiga huyo mzee hadi kumvunja mbavu,....kuonyesha jinsi gani unavyowachukia wazee, wazee ambao ni wazazi wako.....’akaambiwa

‘Sio mzazi wangu huyo mzee....’akasema

‘Kwahiyo ulifanya hivyo, kwa vile sio mzazai wako?’ akaulizwa

‘Nilifanya nini....mimi nilipoona huyo mzee analeta vurugu, kwanza alimuumiza mlinzi na bado alitaka kunipiga na mimi, tukawa tunamzuia kwa pamoja....’akasema

‘Ndio mumupige mzee, ambaye ni sawa na mzazi wako hadi kumvunja mbavu...?’ akaulizwa

‘Sikumvunja mbavu mimi,...sikumpiga, na yeye sio sawa na mzazi wangu, .....’akasema

‘Wewe ili awe sawa na mzazi wako ulitaka aweje....?’ akaulizwa

‘Awe muungwana, asifike kwenye nyumba za watu na kuanza kuleta vurugu...’akasema

‘Kwahiyo wewe na mlinzi mlimpiga huyo mzee kwa vile tu, hafanani na jinsi utakavyo wewe?’ akaulizwa na muendesha mashtaka akaweka ingamizi kuwa wakili anamlazimishia shahidi kauli ambayo hajaitamka.

‘Shahidi anasema ili amkubali mzee kuwa ni mzazi wake anataka awe vile anavyotaka yeye, hajui kuwa uzee, na uchakavu,au uduni wa maisha  umetokana na  wazee hao kuhangaika ili wao wapate, ili wao wasome, na kuhangaika kwao ndiko kumewafanya  wazee hao wafikie hapo walipo, waonekane wamechoka, ...’akasema wakili

‘Je wewe hutazeeka...?’ akaulizwa

Watu wakaguna , wengine wakacheka na hakimu akagonga rungu kutuliza watu, na akasema

‘Shahidi jibu swali..lakini wakili hakikisha kuwa maswali yako yanalenga kwenye kesi, sitaki nikufundishe wajibu wako....’akasema hakimu

‘Swali gani, muheshimiwa hakimu....?’ akauliza hakimu akimuangalia wakili mtetezi kwa mashaka

‘Wewe unasema humjui baba yako na ya kuwa hujui kama baba  yako yupo hai au la  nauliza tena kama ni hivyo unawezaje kusema baba yako hana tabia kama ya huyo mshitakiwa vipi ulijua tabia ya baba yako,....?’ akaulizwa

‘Mimi simjui baba yangu maana sikuwahi kumuona....hata hivyo, baba yangu hata kama ningemuona hawezi kuwa na tabia kama za mshitakiwa .....’akasema

‘Kwahiyo kauli ya kusema kuwa baba yako kafariki sio sahihi huenda yupo hai, ila hujawahi kuonana naye...?’ akaulizwa

‘Kwani hayo ya baba yangu kuwa hai, yahusiana gani na hilo tukio, mtu aje kwangu, hata kama ni baba yangu afike kwenye nyumba ya mtu na kuleta vurugu, haikubaliki tabia kama hiyo, na isitoshe huyo hawezi kuwa baba yangu, nimeshasema hilo...’ akasema shahidi.

‘Kwasababu nataka kukuonyesha kuwa huyo mshitakiwa hakuyafanya hayo kwa makusudi, mzee kama yeye alikerwa na kauli zenu chafu, akakasirka na nyie kwa kuonyesha ujana wenu mkaanza kumpiga...’akasema wakili

‘Hiyo sio kweli....yeye ndiye aliyeleta vurugu,...usibadilishe mada.....usimtetee kwa kitu ambacho hakikuwa hivyo....yeye kashtakiwa kwa kuleta vurugu,.....’akasema

‘Yeye sasa hivi ni mgonjwa kavunjika mbavu, kategeuka miguu, ni kutokana na nini...?’ akaulizwa

‘Kutokana na uzee wake.....’akasema na watu wakacheka

‘Kwahiyo mtu akiwa mzee anavunjika mbavu anategeuka miguu....?’ akaulizwa

‘Sio lazima iwe hivyo, ila kama mzee ni mkorofi, hajitulizi nyumbani kwake, kazi yake ni kupita kwenye majumba ya watu na kuleta vurugu, matokeo yake ndio hayo, ataumia miguu, na hata kuvunjka mbavu, maana anaweza kudondoka, akaumia.....’akasema

‘Hizo mbavu zitavunjikaje kama sio kupigwa mateke, ....wewe na mlinzi hamkumpiga huyo mzee mateke....mkamchangia kwa pamoja, mkampiga kama mwizi, wakati mzee huyo alifika akimtafuta ndugu yake....’akauliza wakili

‘Mimi sijui aliumiaje hizo mb\vu, huenda alifika hapo akiwa na matatizo yake akatafuta kisingizio tu......’akasema na watu wakacheka

‘Wewe unasema humjui baba yako, hujawahi kuonana na baba yako, au sio? lakini huyo aliyefika hapo siku hiyo anaweza kuwa ni baba yako mzazi na alifika hapo akimtafuta ndugu yake ambaye pia anaweza kuwa ni baba yako mdogo...’akasema wakili huyo kwa haraka kabla wakili muendesha mashitaka hajaweka pingamizi.

‘Anaweza kuwa hahaha,..... anaweza kuwa kwa wengine, lakini sio kwangu mimi,....na wazazi wangu hawawezi kufanya hivyo .... hata hivyo, hayo ya kumtafuta ndugu yake ilikuwa ni sababu tu....muheshimiwa kwanini unakwepesha kesi ya msingi ya wao kuleta vurugu.....’akasema

‘Hujajibu swali langu, anaweza kuwa au hawezi kuwa mzazi wako, ....?’ akauliza wakili

‘Mbona nimeshakupa jibu tayari, nimesema hawezi kuwa mzazai wangu huyo, hata siku moja.....’akasema kwa dharau

‘Kwanini hawezi kuwa mzazi wako....?’ akaulizwa swali na aliona kama anakerwa kwa kurudiwa maswali yale yale.....

‘Kwasababu ningewajua na kuwatambia, kwa kifui mimi nimekulia hadi hapa nilipo simjui baba wala mama nimeishi kivyangu, hata mlezi..sikuwahi kuwa naye....na....’akasita na kutulia kuongea kwani mlangoni aliingia mtu akitembea taratibu kuelekea kiti cha mbele walipokuwa watu wamekaa kiti cha mbele

Ile hali ya kunyamaza kwa ghafla, iliwafanya watu wageuke kumuangalia huyo mtu aliyeingia, na hakimu naye akaangalia kuelekea kwa huyo mtu,..na hapo wakili mtetezi akasema...

‘Hebu nikuulize huko ulaya ulifikaje...na ulikuwa ukiishi na nani ulipokuwa mdogo?’ akaulizwa na wakili muendesha mashitaka akaweka ingamizi kuwa swali hilo halina msingi , halihusiani na kesi na wakili mtetezi akasema yeye anataka kuonyesha wazi kuwa mshitakiwa alifika hapo kwenye nyumba kwa lengo gani, na hayo yaliyotokea ni utomvu wa nidhamu, kwa vijana kwa kutowaheshimu wazazi wao,kwa kutoa lugha chafu na dharau....’akasema wakili

‘Unasema wewe humjui baba wala mama, huyo aliyekulea ukiwa huko ulaya alikuwa ni nani,,,,sio baba yako mdogo,...?’ akaulizwa

‘Sio baba yangu mdogo ni msamaria mwema tu,.....’akasema

‘Hata kama ni msamaria mwema, wewe wakatii unaishi naye hukumuheshimu kama mzazi wako na je sasa, huyo unayemuita msamaria mwema yupo wapi ?

‘Yeye  alishakufa,...’akasema

‘Alishakufa,!  unahakika kuwa alishakufa au ulimuua wewe.....?’ akauliza wakili , na watu wakacheka na wengine wakawa wanaongea kwa kunong’ona, na minong’ono ya wengi huleta kishindo

‘Taratibu zifuatwe....’Hakimu akasema akigonga rungu lake ..halafu akasema

‘Alkufa mwenyewe kwa maradhi yake......’akasema na wakili akageuka kwa yule mtu aliyeingia na kusema;

‘Basi huyo uliyemuona akiingia ndiye mlezi wako, uliyekuwa ukiishi naye Ulaya......’akasema wakili, huku akinyosha mkono kuelekea pale alipokaa huyo mtu.

‘Sio kweli huyo aliyekuwa nami huko ulaya alishafariki dunia....hawezi akawa huyo wanafanana tu......’akasema

‘Mlikuwa mkiishi naye kwa vipi.....huko Ulaya?’ akaulizwa

‘Kama msamaria mwema tu......’akasema

‘Hakuwahi kukuambia kuwa yeye ni mzazi wako...?’ akaulizwa

‘Hayo hayahusiani na hii kesi....hata kama aliniambia...’akasema

‘Ni kazi yako kujibu swali, kama hayahusiani na hii kesi wakili wako angesema hivyo, jibu swalii langu, je huyo uliyekuwa ukiishii naye huko ulaya hakuwahi kukuambia kuwa yeye ni baba yako mdogo....?’ akaulizwa

‘Baba yangu mdogo kwa vipi....?’ akauliza shahidi kwa mshangao

‘Unajifanya hujui,....eeh...hujiu baba mdogo anakuwa vipi au hujui Kiswahili vizuri kwa vile ulaya baba mdogo mnamuita Uncle, au....?’akasema wakili na kuuliza na watu wakacheka

‘Ndio sijui.......huyo hakuwa baba yangu mdogo....’akasema akimtupia jicho yule mtu aliyeinga halafu akamkazia macho wakili

‘Hakuwahi kukuambia kuwa wewe una wazazi wako, mkaja naye kutoka Ulaya akakutambulisha kwa wazazi wako, bado ukawakana.....?’ akaulizwa

‘Haya yanahusiana vipi na hii kesi....?’ akauliza akimuangalia muendesha mashitaka ambaye alikaa kimia, alikuwa akiandika kitu kwenye makabrasha yake.

‘Jibu swali langu , je haikuwah kutokea hivyo...yeye kukuleta huku Tanzania akakutambulisha kwa wazazi wako, kwa baba na mama yako ukawakana....?’ akaulizwa

‘Hata kama ilitokea hivyo, lakini sio kweli, hao hawakuwa ni wazazi wangu, na huyo hakuwa ni baba yangu mdogo, alitumia mbinu tu ili kujipatia alichokitaka, yeye maisha yake yalikuwa hivyo, aliwahi hata kufungwa kwa utapeli....’akasema na watu wakacheka

‘Basi kwa taarifa yako huyo ni baba yako mdogo halisi, muangalia vizuri ....’akasema akinyosha mkono kwa yule mtu, halafu akaendelea kusema

‘Na ndiye aliyekuwa akitafutwa na kaka yake,kaka yake ambaya alikuja kwako, mkampiga wewe na mlinzi kama mnapiga mwizi, ...kaka yake ambaye ni baba yako mzazi haswa, ambaye leo mumemfanywa awe mshitakiwa....’akasema wakili akimuonyeshea sasa mshitakiwa na watu wakaguna

‘Sio kweli.....huo ni uzushi,...huyo hawezi kuwa ni mzazi wangu, nilishasema na nitasema tena....achen uzushi, ....familia hiyo naifahamu vyema mimi, ni ya wazushi, mtu anajiita Profesa hata kusoma hajasoma,...watu wanakuja kwenye majumba ya watu na kuleta vurugu kutafuta visingizio....’akasema kwa hasira na watu wakawa wakacheka kidogo halafu kukawa kimia, na kukatokea kitambo cha ukimia halafu hakimu akasema...

‘Wakili una uhakika na unachokisema, ?’ akauliza hakimu na kabla wakili hajijibu hakimu akasema; `Wakili mtetezi,huyo mshitakiwa ni kweli kuwa ni baba mzazi wa shahidi?’ akauliza hakimu na kabla wakilii hajajibu shahidi akasema;

‘Huyo sio baba yangu mzazi muheshimiwa hakimu, huyu wakili, anajaribu kunichanganya kiakili, anajua kabisa kuwa huyo sio baba yangu mzazi, hebu angalieni, hatufanani kabisa, asipoteze ukweli wa hii kesi...’akasema shahidi, na wakili akasema;

‘Muheshimiwa hakimu, nina uhakika na ninachokisema, huyo mshitakiwa ni baba mzazi wa huyu shahidi...., lakini kutokana na tabia mbaya za vijana wetu wanafikia hatua ya kuwakana wazazi wao kwa vile tu wanauwezo.....mzee huyo alifika.nyumbani kwa huyo kijana akimtafuta mdogo wake, na ...’wakili muendesha mashitaka akaingilia akisema wakili mtetezi anajaribu kukwepa kesi ya msingi na kuleta hoja nyingine..ili kupoteza muda

Hakimu kwanza alimuangalia wakili muendesha mashitaka halafu akamuangalia wakili mtetezi, akasema.

 ‘Natoa mapuziko mafupi, na wakati huo nawahitajia mawakili wote hapa mbele nataka kuteta na nyie kidogo....’akasema

‘Huyo sio baba yangu mzazi hawa watu ni waongo, na Profesa alishafarki zamani hawa tu ni matapeli....’akasikia shahidi akisema kwa sauti


WAZO LA LEO: Hata jani la mgomba lililokauka lilikuwa kikonyo, ...na wewe kijana ipo siku utakuwa mzee, usidharau wazee wako kwa vile sasa weweuna umbo nzuri , waheshimu wazee huku ukimuoma mungu na wewe ufikie hapo kwenye uzee ukiwa salama na afya kwani uzee hauombwi

Ni mimi: emu-three

No comments :