Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeFriday, November 6, 2015

RADHI YA WAZAZI-52Pamoja na hayo wakili alijitahidi kupeleka maombi kuhusu hiyo kesi akielezea mambo mengi, ikiwemo hali ya afya ya mshitakiwa , na ombi likawa ‘ikiwezekana kesi hiyo iwe ni ya madai tu’ na ikiwezekana kesi hiyo imalizwe nyumbani, lakini hilo halikuwezekana, Na wakili alipokutana na Profesa kuyaeleza hayo akasema;

‘Kwanza waliofanyiwa hivyo, hawajaonyesha ushirikiano, siku ya kusikilizwa ombi letu, walihitajika wawepo, hawakufika,... na hakuna maelezo yoyote kutoka kwao kuwa wamekubali kuwa kesi hiyo imalizwe nyumbani...’akasema wakili

‘Lakini uliongea nao kama nilivyokuomba...?’ akauliza

‘Nilifika nikaongea nao lakini hapo hapo walikataa hilo ombi, nikaona nipeleke ombi hilo kwa hakimu, na nikajua wakitwa kulisikiliza hilo ombi watafika tu, lakini cha ajabu hawakufika kama walivyosema...’akasema wakili

‘Sasa hakimu kwanini hakuwachukulia hatua kukaidi ombi lake...?’ akauliza Profesa

‘Hilo sio ombi la hakimu, hilo ni ombi letu, na nia ni kujenga ushawishi, uelewe hapo, nilitaka wao wakiwepo kuwe na uzito wa kumshawishi hakimu, hakimu asingeliweza kuwaita kwa ombi letu, yeye anasubiria hayo yafanyike mahakamani...na tunachofanya sisi ni kuyamaliza kwanza nje....’akasema wakili huyo

‘Halafu kuna jambo jingine, wameniambia, sasa sijui ni nyie mlifanya hivyo, au wao wameamua kutunga tu....’akasema

‘Jambo gani...?’ akauliza

‘Wanasema wametishiwa amani , eti kuna watu walifika wakatoa vitisho kuwa wasipofuta hiyo kesi nyumba yao itachomwa moto, na mambo mengi tu, sasa sijui ni nani alifanya hivyo...’akasema wakili

‘Hakuna mtu aliyefanya hivyo, wametunga uwongo wao...namfahamu yule anaweza kuzusha mambo tu....’akasema profesa

‘Mimi nilikuwa na ushauri mwingine japo umekuwa ukiukataa, mimi naona sasa ni wakati muafaka wewe kwenda kuonana na wao huenda italeta uzito fulani, ninachotaka ni wao watoe ushirikiano, utakaoweza kumshawishi hakimu akibali ombi letu....’akasema wakili

‘Kwakweli kwa  hivi sasa siwezi kuonana nao, nitazua makubwa zaidi, ....’akasema Profesa

‘Basi kaka yako afanye hivyo, kwa hali yake kwa hivi sasa anaweza kufika huku mjini, au sio afike akawaombe msamaha..huenda itasaidia...’akasema wakili

‘Kaka amesema hawezi kwenda kuwaomba msamaha kwa vile yeye anaona hana kosa....’akasema Profesa

‘Sasa hilo ndilo linaleta utata, maana kama nyie pande mbili hamjaafikiana, mnatarajia nini mbele ya hakimu, yeye ataliona hilo ombi ni muafaka kama nyote mumeafikiana,, mimi inaniwia vigumu sana, ...’akasema

‘Mhh, kiukweli ni jambo lenye utata, na najaribu kukwepa maafa zaidi....’akasema Profesa

‘Basi ....iliyobakia tusubirie mahakamani...’akasema wakili

Kisa kinaendelea

*********

Siku kabla ya kesi mama mmoja alifka kwenye nyumba ambayo wanaishi watu hao waliofanyiwa fujo, mama huyo akiwa na binti mdogo anayemuongoza akagonga mlango na mlinzi akajitokeza na kuuliza

‘Nyie nani na mnataka nini....?’

‘Mimi naomba kuonana na mwenye nyumba hii....’huyo mama akasema

Yule mlinzi akamuangalia huyo mama, na huyo binti ambaye alikuwa naye, halafu akasema

‘Mna shida gani na mwenye nyumba....?’ akauliza

‘Nataka kuongea naye kuhusu kesi iliyopo mahakamani....’akasema huyo mama

‘Jamani mumeshaambiwa kesi hiyo ipo mahakamani hakuna lolote linaloweza kufanyika kwa hivi sasa, ...wewe wataka kuongea nini zaidi na mwenyenyumba kama unataka kuongelea hiyo kesi nenda mahakamani....’akasema mlinzi

‘Mimi ninataka kuongea na huyo mtu, kwanza nataka nimuone,...ninahisi namfahamu tafadhali kabla mambo hayajaharibika nataka nionane naye......’akasema na mara mwenye nyumba akatokea

Kumbe kwa muda huo mwenye nyumba alikiuwa akitembea tembea nje kunyosha miguu na ndio akasikia mlinzi akiongea na hao wageni, akaona afike kuona ni akina nani
Akasogea hadi pale mlangoni, ndipo akamuona huyo mama akiwa na binti, wakiongea na mlinzi

Ni nani hao na wanataka nini....?’ akauliza

Na yule mama aliposikia sauti ya kiume , maana huyo mama haoni vizuri, akashtuka, akageuka kuelekea kule sauti ilipotokea, akasema

‘sio wewe kweli,....’akasema huyu mama akitaka kusogea lakini mlinzi akamzuia

‘Sio wewe maana yake nini, wewe mama unataka nini...?’ akaulizwa na mlinzi

‘Ndio wewe nimekutafuta na sasa nimekuona, mungu wangu, ndio wewe, ndio wewe kabisa, nahisi sauti yako moyoni mwangu....’akasema huyo mama

‘Wewe mama vipi umechanganyikiwa nini....’akasema mlinzi na yule mwenye nyumba akawa kasimama kaduwaa akawa anamuangalia huyo mama, halafu akageuka kuondoka.

‘Waondoke zao,mimi siwajui...’akasema mwenye nyumba, na huku nyuma yule mama akawa 
anaongea

‘Ndio wewe, nilikuota jana kuwa umekuja upo hapa kwenye nyumba nzuri...., ndio wewe kabisa, ngoja nisogee nikuguse nihakikishe....’yule mama akasema na wakati huo huyo mwenye nyumba alishaondoka, na aliyemjibu ni mlinzi akasema

‘Wewe mama mwenye nyumba hakutambui, kasema muondokei, ....’akasema

‘Kwani wewe mama una shida gani,....?.’akasema mlinzi

‘Shida gani nyingine niliyo nayo mimi, jiulize kwanini nitokea kote huko nije mpaka hapa, huyo binti hajui lolote nimeongozwa na hisia zangu hadi nikafika hapa, ..namtaka huyo niongee naye nahisi you matatani, .....’akasema huyo mama

‘Ujanja wenu huo ...mnatumia ujanja wa kuja hapa kuomba omba,leo mwenye nyumba hana pesa za kutoa , ...kwahiyo ondokeni hapa la sivyo mtakwenda kulala jela,,,,.’akasema huyo mlinzi na kufunga mlango

***********

Mwenye nyumba akarudi ndani akawa anaongea na mkewe

‘Unajua kuna mama mmoja kafika hapo getini akawa anaongea maneno ya ajabu, eti anasema ndio wewe, nilikuota,...’akasema huku akicheke kwa dharau, na mkewe akashituka na kugeuka kumuangalia

‘Mhh...kwanini asema hivyo, ulimuuliza aliota nini, na huyo mama katokea wapi,i?’ akauliza mkewe

‘Ndivyo walivyo watu wa huku, wanaweza kutumia kila mbinu kutafuta misaada, mimi simjui kabisa huyo mama, halafu nashangaa ....huyu mama , lakini sio yeye, kipindi hicho nilikuwa mdogo, huyu mama ni mzee zaidi, na cha ajabu anaonekana haoni, ndio hapo naona ajabu, alitambuaje,....’akasema akibenua mdomo kwa dharau

‘Kwanini unasema haoni?’ akauliza mkewe akionyesha uso wa huruma

‘Anaongozwa na binti mdogo kashikwa mikono....’akasema

‘Jamani sasa kwanini usingelimkaribisha ukampa chochote,,...nahisi alikuwa anahitajia msaada, tatizo la nchi yenu hakuna taratibu za kuwasaidia watu kama hao wasiojiweza, inabidi nyie raia musaidie...’akasema mkewe

‘Nimechoka na hawa watu ,...kila siku anakuja huyu mara yule wote wanaomba omba, tutapatia wapi pesa za kutoa kila mara, achana na hao watu kabisa....’akasema

‘Lakini nikuulize je yeye alisema amekuja kwa nia ya kuomba msaada au alikuja kwa swala gani?’ akauliza mkewe

‘Nilisikia akimwambia mlinzi eti amekuja kuhusiana na hiyo kesi, nikajua huenda ni mke wa yule mshitakiwa, nikawa na hamasa ya kumuona huyo mwanamke yupoje...., na nilipofika tu, huyo mama akashikwa na kitu kama mshituko aliposikia sauti yangu ndio akasema maneno hayo:

‘Ni wewe....ni wewe,...nilijua tu,..ni wewe nilikuota....alikuwa anaongea kwa hisia za ajabu, nikahisi amechanganyikiwa.....’

‘Kuna jambo hapo, huenda kweli ni mke wa mshitakiwa huyo, lakini huyo mshitakiwa yeye siku ile hukumtambua vyema ni nani......?’ akauliza

‘Hatukuweza kuongea zaidi, yeye alidai kuwa yule mtu anayejiita Profesa ...kama hivyo, maana sijawa na uhakika, eti alikuwa ni ndugu yake, aliyepotea....na kwa hali ilivyokuwa, sikuwa na muda wa kumtambua vyema yeye ni nani.....hata wewe ungekuwepo, ukashikwa na hasira,...kamuumiza mlinzi na bado analeta kiburi, ...nikampa kichapo, nahisi nilimvunja mbavu, maana ni mbishi hasikii, ....’akasema

‘Hapo na wewe ulifanya kosa ...’akasema huyo mkewe

‘Kwa hali kama ile ungelifanya nini, ni mbishi, lakini alichokipata sasa atakuwa keshajifunza adabu, hii mijitu ni sugu kweli hata ukipiga haiskii kipigo....’akasema

‘Kama huyo mama anadai kuwa alikuota....mmh, kuna kitu hapa...tatizo wewe hujataka kulichunguza hili swala kwa undani zaidi, nahisi hawa watu wanaweza kuwa wanandugu wa marehemu...?’’akasema mkewe

‘Hahahaha....ungeliona sura ya huyo baba, ..hahaha sura mbaya, jitu jeusi, sijui wanaweza kuwa na ndugu naye, sasa kwanini niwachunguze ili iweje....labda kama ni ndugu zake marehemu naweza kukumbuka aliwahi kuja mzee mmoja mimi nikiwa mdogo, akaai yeye ni baba yangu, siwezi kujua kama ndio yeye au la,....’akasema

‘Lakini mimi ninahisi hii kesi inaweza kuzua mambo mengine ....kwanini tusisaidie hii kesi iishe, tuachane na hawa watu kwa amani....’akasema huyo mkewe

‘Unanishangaza kweli mwenyewe ulisema umechoka na huo usumbufu wao, jinsi wanavyokuja hapa mara kwa mara, dawa yao ndio hiyo, akifungwa mtu mmoja watakaoma kabisa kuja hapa tena, lakini kama hakutafanyika jambo la fundisho, kila siku utakuwa ukipokea wageni hapa. 

Hawa watu hawataki kufanya kazi , wao kuomba omba tu....’akasema

‘Mhh, kweli watu wenu wamezidi,....kuomba omba, halafu wanakuja kwenye makazi ya watu, bila hata taarifa, hawajali muda,..kweli nimechoka na usumbufu wao,’akasema mke mtu

‘Ndio maana nataka wahukumiwe iwe ni fundisho kwao....’akasema

‘Na kama ni kesi huwezi kukwepa kwenda mahakamani..kama ukiitwa utafanyaje...?’ akauliza mkewe

‘Mimi siendi.....na yule wakili wao akija hapa sitaki kuongea naye tena.....’akasema

‘Ili kulimaliza hili inatakiwa utoe ushahidi kuwa watu hawa ni wakorofi....’akasema mkewe

‘Kama wewe una muda wa kufuatilia mambo hayo nenda, mimi sina muda huo, kwanza sasa hivi tunafunga mahesabu ya mwaka huko kazini ,, ..leo tu nilitakiwa nifike , nimeomba ruhusa tu, nilitakiwa niwepo huko, baaaye nitaondoka, sijui wewe.....’akasema

‘Hata sisi ni hivyo hivyo....ila leo mimi napumzika siendi huko kazini....’akasema mkewe

‘Unaona eeh, sasa kwanini tupoteze muda na mambo hayo ya kujitakia, waache wenyewe mahakama na hakimu wao, wataamua , hiyo kesi ipo mahakamani, na kama nitasikia hakimu kawasamehe nitaona ajabu kweli, ndio nitajua hawa watu hawafuatii sheria,...’akasema

‘Kwanini....ina maana unataka wahukumiwe wafungwe?’ akauliza mkewe

‘Wewe unaona walichokifanya ni sahihi, mtu afike kwenye nyumba ya watu alete vurugu, ampige mlinzi ..wewe unaona hiyo ni sahihi kweli ?, kama ingekuwa huko ulaya unafikiri ingekuwaje...?’ akauliza kwa msisitizo.

‘Kiukweli walichokifanya sio sahihi,....lakini mpaka sasa najiuliza kwanini hayo yote yatokee,’akasema mkewe

‘Ni wahuni tu....’akasema mumewe

‘Lakini nikuulize kitu, yule mtu aliyekuja na kujiita Profesa, kweli sio ndugu wa yule marehemu,...mimi bado naliwazia hilo, japokuwa nilipompigia mama alisema yule Profesa alifariki, yeye ana uhakika huo,...’akasema

‘Sasa una wasiwasi gani naye...’akauliza mumewe

‘Wanafanana sana.....nilimwambia mama akasema yule mtu asingeliweza kupona, na aliwasiliana na watu anaowafahamu huku, wakamthibitishia hivyo,... ila mimi nahisi kuwa huyu, anaweza kuwa ni ndugu yake,maana wanafanana kweli kweli...hivi kwanini wewe ..haujalifuatilia hilo kuwafahamu hao watu vyema....?’ akauliza

‘Sina muda huo kabisa...na kama ni hiyo familia sitaki kabida kujuana nayo, na huyu mzee, mmmh, labda ndio yeye,aliyekuja kipindi kile nikiwa mdogo, na kama ni yeye, .....sitaki kabisa kufahamiana naye...’akatulia

‘Unakumbuka nini ulipokuwa mdogo, huyo mzee alikuwaje, kwanini hutak ufahamiane naye...?.’akauliza mkewe, na mara simu ya huyo jamaa ikalia, na alipoangalia akaona ni namba ngeni kwenye simu yake,akaipokea,

‘Halooh ni nani mwenzangu, ....’akasema na akawa anasikiliza kwa muda halafu akasema

‘Kwa kweli mimi sina muda wa kufika mahakamani, nawaambia hivi, nyie mnafahamu sheria si ndio..., na mahakama ndio mwamuzi au sio, basi sheria ifuate mkondo wake, ....nyie ongeeni ilivyokuwa na  hukumu itolewe kwani kuna tatizo gani,... lakini mimi siwezi kufika huko kabisa, ....’akasema akatulia kusikiliza , halafu akasema

‘Mimi nitaona ajabu sana,....’akasema na kutilia akisikiliza na baadaye akasema

‘Ni kweli alikuja mtu hapa akisema yeye ni wakili, amekuja kuleta maombi ya mshitakiwa, kiukweli sikuweza kukubaliana na hayo maombi yake, kwa vile hayana msingi,...’akasema na kutulia kusikiliza

‘Hapana....siwezi kukubaliana na hilo ombi lao, kwa vile kweli alileta vurugu, alimuumiza mlinzi wangu,kama nitakualiana na hilo ombi, watakuwa wanakuja tena na tena,mimi naona ni bora adhabu itolewe ili iwe ni fundisho, lakini zaidi ya hayo kiukweli nimechoka na hao watu.....’akasema na kusikiliza

‘Ndio alisema ni wakili wao...’akasema na kutulia

‘Unaona eeh,kama wamefikia kutafuta wakili basi ujue wamejiamini,....sasa mimi nifanyeje....?’akasema na kuuliza, akawa anasikiliza kwa muda halafu akasema

‘Muda, sina .....ooh,.....nilishawaambia mimi sina muda wa kufika huko, ....’akasema na baadaye akamaliza kuongea na hiyo simu na kukaa kimia, mkewe akawa anasubiria kusikia ni nini mumewe aliambiwa kwenye simu.

‘Huyo ni muendesha mashitaka anasema natakiwa niwemo mahakamani kutoa ushahidi siku ya hiyo kesi...’akasema

‘Nilijua tu,...sasa itakuwaje...?’ akauliza mkewe na mumewe akajipiga na mikono kama kukata tamaa, halafu akasema;

‘Anasema kuna barua italetwa ya mahakama, ni lazima niwepo,...’akasema

‘Kwahiyo ni lazima uende,.....hao umepatikana, sasa utafanyaje...’akasema mkewe na jamaa akatulia akiwaza jambo, baadaye akasema

‘Nitaangalia.....’akatulia akiwa anawaza jambo, na mkewe akataka kuongea jambo, lakini 
kabla hajasema neno mara mlinzi akagonga mlango na kusema

‘Kuna mgeni getini anataka kuja kuongea na wewe.....’akasema mlinzi

‘Ni nani tena, si nilishakuambia......?’akauliza mwenye nyumba na kabla hajamaliza, sauti ikasema kwa nje...

‘Ni mimi.....’ mlinzi aligeuka nyuma kwa mshituko


WAZO LA LEO: Kusameheana ni jambo jema na lenye busara,na hujenga upendo na mshikamano wa dhati,... lakini tabia ya kusamehe ianzie moyoni mwa mtu kwanza, uwe nayo katika maisha yako, kwani huwezi kutazamia kusamehewa, kama wewe mwenyewe huna tabia ya kusamehe. Usitarajia kutendewa mema kama wewe sio mtenda mema, ....kumbuka mwenye tabia ya kusamehe naye husamehewa.

Ni mimi: emu-three

No comments :