Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeFriday, October 30, 2015

RADHI YA WAZAZI-50
Profesa alikataa kata kata kuongozana na wazee kwenda mjini, ili kuonana na watu waliomshitakia kaka yake, ili ikiwezekana keso ifutwe na mambo yaongelewe nje,....
Wazee kuona hivyo wakaamua kwenda huko mjini wenyewe ili kuona jinsi gani wanaweza kusaidia hili tatizo kihekima zaidi, je itawezekana

Tuendelee na kisa chetu.....

Wazee  wakasafiri kuelekea huko mjini......

Na moja kwa moja  walikwenda kwenye hiyo nyumba  kama walivyoelekezwa, na kama ilivyotarajiwa, hawakukaribishwa moja kwa moja, walikataliwa kuingia ndani na mlinzi, kwa maelezo kuwa wao hawaruhisiwi kuingia ndani kutokana na yaliyotokea huko nyuma.

‘Lakini sisi tumekuja kuonana na hao watu kwa nia njema kabisa...’wakasema

‘Wenyewe wametoa agizo kuwa tusiruhusu mtu yoyote kuingia, hususani anayetoka huko kijijini kwa hao watu waliokuja hapa na kuleta vurugu,....’akasema mlinzi

‘Lakini wenyewe si wapo ndani?’ akaulizwa mzee akijaribu kuchungulia ndani kwa kuitia mlangoni na mlinzi akasogea kati kati ya mlango kama vile anazuia huyo mzee asione huko ndani

‘Nimeshawaambia hivyo wazee, inatosha nafikiri nimeleweka wazee wangu.....’akasema mlinzi
Wazee hawakukata tamaa, wakamsihi mlinzi,  hatimaye mlinzi akaona isiwe shida japo alishaagizwa hivyo, akaona aingie aonane tena na bosi wa nyumba, na bahati nzuri siku hiyo walikuwepo wenyewe.....

‘Nilikuambia hao watu wakija waambie sitaki kuonana nao, hukunielewa...’ akaambiwa

‘Wamesema ni kuhusu,  kesi iliyopo mahakamani...na wamefunga safari ya mbali kutoka huko kijijini hadi hapa lengo ni wao kuonana na nyie...’akasema mlinzi

‘Kama ni kuhusu hiyo kesi, waambie mimi siwezi kuizungumzia lolote maana hiyo kesi ipo mahakamani.....wewe si unaelewa hilo, ....’akaambiwa mlinzi, hatimaye mlinzi akarudi kwa wazee na kutoa taarifa hiyo kwa hao wazee, wazee wakazidi kusihi kuwa ni muhimu kuonana na mwenye nyumba.

‘Unajua sisi tumetoka kijijini tumefunga safari hadi hapa, hivi kweli hamuoni kuwa ina muhimu sana kuonana na hao watu, mwambie hata kama ni hivyo, aje tuonane naye tuongee kidogo, asikie ombi letu...’akasema mzee mmojawapo, na mlinzi alishindwa kurudi tena kwenda kumuona bosi wake akakaa kimia, wazee wakasubiria hapo wakizidi kusihi...lakini hakuna kilichofanyika...

Ilipita muda mara mama mwenye nyumba, huyo mama wa kizungu akawa anataka kutoka nje na gari lake, ndio akawaona hao wazee, ikabidi asimame kuwaulizia wanachotaka ni nini....

‘Kwani nyie ni nani na mnataka nini ?’ akauliza huyo mama akiwa ndani ya gari lake akiongea kwa kuchungulia kwenye dirisha la gari

‘Sisi tumetokea kijijini, tumefunga safari hadi kufika hapa nia ni kuonana na anayemiliki hii nyumba, ambaye alishitakia kuwa kafanyiwa fujo. Na jamaa yetu .tafadahali tunahitaji, tuongee na wewe au mwenye nyumba....maana mwenzetu anaumwa, ...’akasema mzee

‘Lakini hiyo kesi ipo mahakamani, ipo mikononi mwa mahakama, sisi hatuna la kufanya, si mnajua sheria ilivyo, ...’akasema huyo mwanadada wa kizungu

‘Hebu niambie mna shida gani?’ akauliza huyo mama mwenye nyumba akiwa ndani ya gari lake akiongea kwa kupitia dirishani kwenye gari lake.

‘Wewe ndiye eeh mwenye hii nyumba, wewe na mume wako, ambao ndio mliyemshitaki mzee mmoja aliyefika hapa na akawaleta fujo?’ akaulizwa

‘Ndio......’akasema huyo mwanadada wa kizungu

 ‘Tunafahamu sana kuwa kesi io mahakamani,..., ndio maana tumefike tuongee, tuone jinsi gani tutasaidiana, kiubinadamu, unajua haya yanaweza kuwatokea hata nyie, ni makosa yamefanyika,  tunakubali hilo,  nia yetu pia ni kuwaomba msamaha kwa hayo yaliyotokea....’akasema mzee mmojawapo.

‘Msamaha hakuna shida...muhimuu ni huko mahakamani watakavyoamua...lakini anyway...’akasema huyo mama wa kizungu

Yule mama wa kizungu akageuza gari na kurudisha ndani, akamwambia mlinzi awafungulie hao wazee waingie ndani, yeye akatangulia kuingia ndani kuanza kuongea na mume wake, ..

‘Kwanini umewaruhusu hao watu waingie,....kwanini umefanya hivyo, tulielewana nini, na umefanya nini, unawafahamu hao watu walivyo, itakuwa ndio mwanzo wa usumbufu, kila wakiwa na shida watakwa wakija hapa, mimi nawafahamu sana hao watu.....’mumewe akaja juu kweli, lakini mbele ya mkewe ikabidi baadaye akubali, na wakati huo wazee walishaingia ndani.

Wazee wale wakaingia na kukaribishwa kukaa kwenye viti....
Ikawa sasa ni kikao  cha hao wazee na yeye mwenye wakati huo mkewe alikuwa kasimama kama msikilizaji tu, alikuwa na haraka ya kuondoka.

‘Nyie ndio wenye hii nyumba?’ wazee walianza kuuliza swali hilo mapema kabisa.

‘Ni nini lengo lenu wazee...., sioni umuhimu wa kujibu swali lenu hilo, labda kama nyie ni watu wa serikali mnataka uhakiki wa kuhusu anayemiliki hii nyumba, je nyie na maofisa ardhi..?’akauliza

‘Hapana sisi sio maofisa ardhi, sisi ni wazee tumetokea huko kijijini...’wakasema

‘Sasa kama nyie sio watu wanaohusika na umiliki wa majengo, au  kama hamuhusiani na hayo mambo ya umiliki wa nyumba, mimi siwezi kuwajibu hili swali kwa sasa, je mna shida gani..?’ akuliza huyo mwanaume

‘Kwasababu walioshitaki ni wamiliki wa hii nyumba,...tumeambiwa mahakamani hivyo, kwahiyo lengo letu ni kuonana na hao wamiliki...’wakasema

‘Sisi ndio tuliowafanyiwa fujo, mlinzi wetu akajeruhiwa, mimi mwenyewe nikapigwa, ikabidi tujitetee, na kwa vile tuliona tumevamiwa tukawaita polisi, na polisi wakafika wakafanya kazi yao, je sisi tuna kosa gani...’akasema huyo jamaa

‘Poleni sana, na tunawaomba sana msamaha kwa hilo, ....ni kweli mwenzetu alikosea alikuwa kachanganyikiwa kwa vile alikuwa akihangaika kumtafuta ndugu yake, ambaye aliambiwa alifika kwenye nyumba hii...na tungelikuja naye, lakini anaumwa, ....’ wakasema

‘Huyo mzee aliyeleta fujo hakuwa amechanganyikiwa, kabisa, kama aliwadanganya hivyo, alikuwa akiongea vyema, na akili yake timamu,...’akasema

‘Nilipofika nilimkuta mlinzi wangu akivuja damu, mlinzi aliniambia, yeye alimsihi huyo mzee asiingie ndani maana sisi hatukuwepo kwa muda huo na mzee akasihi kuwa ni lazima atuone sisi, na mlinzi alipojaribuu kumuelewesha ndio akavamiwa kwa nyuma...., akidai kwanini ndugu yake alipoteza fahamu humu ndani, anataka kujua hilo, ...kwahiyo kwa kifupi ni kusema kuwa huyo mzee alileta vurugu, akamjeruhi mlinzi pale alipomzuia asiingie ndani....’akasema

‘Ndio tunasema alichanyikiwa,...kwani  siku mbili kabla amekuwa akihangaika huku na kule, kumtafuta ndugu yake...na alijua huenda kazuiliwa humu ndani,.. na asingeliondoka mpaka ajua ni kitu gani kilimsibuu ndugu yake..ndio maana alitaka kuonana na nyie.....’wakasema

‘Mlinzi alimwambia sisi hatupo, na alimwambia ndugu yake kalazwa hositalini ila yeye aling’ang’ania kuwa ni lazima aingie ndani kuongea na sisi.....’akasema

‘Ndio maana tumekuja kuwaomba msamaha, maana kwa hivi sasa mzee huyo anaumwa, alikuwa kalazwa hospitalini,...hali yake sio nzuri, na kiujumla kama ataendelea na usumbufu wa hii kesi itamuathiri sana, kiubinadamu tunaomba mlione hili, ....’akasema mzee mmojawapo

‘Kwahiyo sisi mnataka tufanye nini,..mkumbuke kaleta fuko, kavamia nyumba ya watu, kamjeruhii mlinzi wetu akiwa kazini, mlinzi  kashonwa nyuzi sita kichwani,...’akasema jamaa

‘Poleni sana.....’wakasema wazee

‘Mimi mwenyewe nilipofika, nilijarabu kumsihi, akaanza kunivamia na mimi, akaniumiza na mimi, unaona hapa...’akanyosha mkono na mguu kuonyesha mchubuko,....

‘Sasa mtu kama huyu asiyejua sheria mlitaka sisi tukae kimia tu, yeye ni nani, acheni sheria ichukue mkondo wake...ili ajifunze.’akasema

‘Tunakukubalia kuwa kafanya makosa, ...ndio maana tumekuja kuwaomba msamaha, ....na tupo tayari kuwapigia magoti kwa niaba...’akasema mzee mmoja akielekea kupiga magoti

‘Aaah, mzee... usifanye hivyo mzee, maana haitasaidia kitu, ..kama mnaweza nendeni mkawapigie magoti watu wa usalama, polisi na mahakama, maana kesi hiyo kwasasa ipo mahakamani....sisi hatuna la kufanya, hata ukitupigia magoti haitasaidia lolote,...’akasema jamaa

‘Mnaweza kusaidia sana, na mnalifahamu hilo, ni kiasi cha kuonana na muendesha mashitaka kuwa nyie mumesamehe, na kwa vile yule ni mzee, nyie mna uwezo kidogo, msaidieni kesi ifutwe, mtapata baraka...hata kama ni mahamani msema kuwa mumeshamsamehe mzee wetu huyo, na mpo tayari tuyaongee hayo nje ya mahakama...’akaambiwa

‘Unajua kuna watu hawana busara, wanakuja kwenye majumba za watu bila hata taarifa huyo mwenzake anayesema anamtafuta allikuja hivyo hivyo, ....akajifanya yeye ni Profesa, mimi nilijua labda ni profesa wa chuo kikuu ninayemfahamu mimi....’akasema

‘Kwa vile nilitarajia kuonana na huyo Profesa wa chuo kikuu rafiki yangu, alipokuja mlinzi na kutoa taarifa hiyo nikawaambie wamruhusu,, kumbe ni huyo muhuni fulani tu, mgonjwa mgonjwa,...kaja humu ndani ghafla kadondoka na kuoteza fahamu,sisi, tukaingia gharama ya kumtibia, kwa gharama zetu.....’akasema na kugeuka kumuangalia mke wake akasema

My wife wewe unaweza kuondoka, hawa tumemalizana nao waondoke tu...’akasema akimuambia mkewe, na mkewe akawa anasita kuondoka.

‘Huyo alikuwa ni mdogo wake huyo mzee akiwa anamtafuta ndugu yake , aliyepotea siku mbili, ndio maana akafika hapa kumtafuta...aliambiwa alikuja humu ndani na alipofika humu hakuonekana tena akitoka.nje kutokana na maelezo ya majirani...’akaambiwa

‘Hakuonekana akitoka wakati sisi tulimchukua na kumpeleka hospitalini, sema tulipokuwa tunatoka hakuna aliyeona,..tulitokea mlango huu wa nyuma, tukamuingiza kwenye gari, kwahiyo hata walinzi hawakumuona kuwa yupo ndani ya gari wakati tunatoka,..viyoo vya gari havionyeshi ndani, kwa hali aliyokuwa nayo, sisi tulijua keshakufa...’akasema huyo jamaa

‘Huyo mzee sio muhuni, ni mtu na heshima zake, alikuja kama tulivyokuambia kumtafuta huyo ndugu yake, sasa inategemea alipata majibu gani kutoka kwa mlinzi, huo ndio wasiwasi kwa kujitetea...hatujui, na hayo tumeona yapite tu,...kosa limeshafanyika,  muhimu ni hili, tusaidiane kulimaliza,.....tafadhali tupo chini ya miguu yako...’akasema mzee

 ‘Kama nilivyowaambia, ..hayo mambo sasa hivi yapo mikononi mwa mahakama, na mimi siwezi kupoteza muda kwa kwenda mahakamani, au kwenda sijui kwanani, muda huo sina kabisa, mke wangu ndio kabisa, sisi tukitoka hapa ni ofisini, na huko ofisini hatuna muda wa kutoka toka, kazi zetu hazituruhusu...’akasema

‘Kwahiyo kwa kifupi, mimi siwezi kabisa kufuatilia hilo jambo, yeye amejitakia mwenyewe, nyie kama mna nafasi hiyo nendeni mkafuatilie wenyewe, huko mahakamani....’akasema na kuongezea

‘Hata hao watu wa mahakamani niliwaambia mimi sina muda wa kufika huko mahakamani, wao waisimamie wenyewe, wao wafanye wajuavyo wenyewe....’akasema

‘Hapo bado hujatusaidia kwa hilo....nyie ndio mlifanyiwa fujo, nyie ndio mliwaita askari, na nyie ndio mnaweza kwenda kuwaambia hilo swala limekwisha, mumeona tulimalize nje ya mahakama, hiyo inawezekana na kesi ikafutwa....’akasema mzee

‘Hivi wazee hamunielewi, muda huo sina kabisa...nyie nendeni mkaongee  na hao wahusika wenyewe, waambieni mimi nimeshasamehe, basi inatosha ....’akasema

‘Bila nyie kuwepo, hawawezi kuamini...’wakasema wazee

‘Waamini wasiamini sisi halituhusu tena, mimi sitainua mguu wangu kwenda kuonana na na...eeh, sijui na nani....wao wametimiza wajibu wao, ...mlinzi wangu ameshatibiwa nimemwambia aachane na mambo ya mahakama, walimuita sijui kutoa ushahidi, mnataka bado mimi nihangaike eti kufuta kesi, hivi sisi tutaonekanaje ...kwanza muda huo sina 
.’akasema sasa akiangalia saa yake

‘Unajua tumetoka kijijini, mbali, kuja kuwaona,...kutokana na hili mchukulie huyo kama mzee wao, mzazi wako....’akasema mzee mmoja, na jamaa akasimama

‘Jamani kwaherini, mke wangu alikuwa na kikao mumemkatisha na mimi nahitajika ofisini,....kwaherini, huko mahakamani sitakuja au na siwezi kwenda kuonana na huyo anayesimamia hiyo kesi, hilo mnielewe hapa....sina muda huo, leo mumenikuta nyumbani kwa dharura tu....na mtu kama huyo hawezi kuwa kama mzee au mzazi wangu...abadani..’akasema huku akiwa ananyosha mkono wa kuwaelekeza hao wazee watoke nje.

‘Tafadhali kwa hisani yako....’akazidi kusihi mzee lakini jamaa akawa anazidi kuonyesha mkono kuwaashiria watoke.

Wazee, wakaona hawana la kufanya wakasimama na kuanza kuondoka, na walipofika getini yule mlinzi aliyeumizwa alikuwa kafika, wakajitambulisha kwake na kujaribu kuongea naye kama anaweza kusaidia lolote na yeye akawaambia

‘Mimi sina tatizo, nimeshangea na muendesha mashitaka kuwa nimeshamehe tu, najua ilikuwa ni hasira, na watu wa namna hiyo wapo, lakini wamesema hiyo ni kesi ya kujeruhi, ni lazima isikilizwe hadi mwisho....’akasema huyo mlinzi

Wazee wale hawakuishia hapo, walikwenda moja kwa moja kwenye mahakama inayosimamia hiyo kesi, na majibu waliyoyapata ni yale yale, kuwa hata kama hao waliotendewa hivyo wamesamehe, lakini kesi hiyo imeshafika mahakamani ni lazima isikilizwe na hakimu ndiye ataamua vinginevyo....

‘Muhimu hao waliotendewa wafike mahakamani waseme wenyewe kuwa wamesamehe...inaweza kusaidia kupunguza adhabu....’wakaambiwa
Ikabidi wazee warejee kijijini wakiwa wamekata tamaa,

Profesa alipoambiwa hivyo, akahisi mwili ukimchemka kwa hasira, akikumbuka mambo ya gerezani, akikumbuka kaka yake kapatwa na matatizo hayo kwa ajili yake, akasema

‘Nitaenda mjini kuonana na wakili mmoja, najua atasaidia kulimaliza hili tatizo ..huyo jamaa hajui wapi katokea,siku akijua ataumbuka ....lakini kwa hivi sasa sitaki kuonana na yeye kwanza..’akasema

‘Utakwenda kwa huyo wakili peke yako?’ akaulizwa

‘Haina haja ya kwenda watu wengi nitaonana na huyo wakili peke yangu na yeye  atashauri tufanyeje...’akasema
Na wakati wanaongea kaka mtu alikuwa ndani,na mara Profesa akaitwa na huyo kaka yake...

‘Bro unasemaje...’akasema

‘Nimekuambia usiende huko mjini, haina haja....mimi nitaongea mwenyewe mbele ya mahakama, nitajitetea mwenyewe...kama ni hukumu acheni itolewe,......’akasema

‘Bro wewe hujui kesi hiyo ni mbaya, umevamia nyumba ya watu, umeumiza,...hilo ni kosa kubwa sana...’akasema Profesa

‘Wewe ungelisikia kashfa alizokuwa akizitoa huyo mlinzi usingelikaa kimia...nilitaka kumfunza adabu yule mlinzi ili ajue jinsi gani ya kuongea na wageni...wakubwa waliomzidi umri...’akasema

‘Haya umepata faida gani....?’ akauliza

‘Ndio maana sitaki msumbuke...halafu hebu njoo kuna kitu nataka kukuulizia,...’akaambiwa, na yeye baada ya hao wazee kuondoka akaingia ndani kuongea na kaka yake

‘Unajua nimeota ndoto....sikumbuki vizuri, ila ile sura ya huyo mwenye nyumba, sijui ndio mwenye nyumba au mpangaji, kama sio ngeni kwangu....imenijia kwenye ndoto....aah, ile ndoto sijui ilitaka kunielezea nini.....’akasema kaka mtu.

‘Mhh,...mimi sijui, yawezekana unamfahamu ..., ndio maana nataka nikaogee na wakili, ikishindikana itabidi mimi na wewe tuongezane mguu kwa mguu kwa hao watu , lakini hilo ni baada ya mimi kuongea na huyo wakili, tuone atatushauri nini...’akasema profesa

‘Mhh...hiyo sura....nikikumbuka hiyo ndoto nitakuambia....lakini.....’akasema kaka mtu na Profesa akawa anakuna kichwa akiwaza akamsogelea kaka yake akitaka kumuambia jambo...

NB: Tuishie hapa kwa leo


WAZO LA LEO:Kiongozi mwema anayewajali raia wake, hayupo tayari kuona raia wake wanatesea, au wanaumia... ni bora yeye mwenyewe kama kiongozi aumie kuliko raia wake, hata mmoja tu kuumua, ilivyo kiongozi anatakiwa awaone raia zake kama sehemu ya familia yake, je baba au mama yupo tayari kuona watoto wake wanateseke?, ..Kama haweze kuliona hilo kwa familia yake basi kwa raia zake iwe ni hivyo hivyo,!
Ni mimi: emu-three

No comments :