Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Tuesday, October 27, 2015

RADHI YA WAZAZI-49


Mlinzi akiwa kashikilia kichwa kikivuja damu, akifungua mlango ili yale magari yapite, akiwa kajaa hasira,...alitaka afanye hayo magari yapite kwa haraka ili atoke akapambane na huyo mzee,  kichwa kilikuwa kikimuuma kweli damu zikiwa zinaendelea kuvuja,....

Tayari akiwa keshafungua mlango, akashangaa kuona hayo magari hayapiti, akasogea kuangalia kuna tatizo gani, huku akiwa kashikilia kichwa,  ...akamuona yule mlinzi kasimama pembeni ya gari,.....akigonga dirisha la gari!

‘Sasa utakiona....’akasema akiwa kaona sababu ya kulipizia kisasi
Kwa hasira sasa akiwa na rungu tayari mkononi, akamuendea yule mlinzi akilini akitaka kulipiliza kisasi , akishushe kile kirungu kichwani kwa huyo mlinzi lakini alikuwa kachelewa.....
Mlango wa gari la bosi wake  ukafunguliwa, na aliyetoka ni bosi wake mwenyewe akiwa kaiva kwa hasira......

‘Huyu mtu vipi....?’ akauliza akimuangalia mlinzi, lakini akajikuta akibakiwa na mshangao,  damu zilikuwa zinamvuja huyo mlinzi, akageuka kumuangalia huyo mzee....

‘Kuna nini kinaendelea hapa....?’ akauliza akimuangalia mzee , halafu mlinzi

‘Muulize mwenyewe tatizo, hajui jinsi gani ya kuwakaribisha wageni, ...hapo kajigonga kwenye mawe asije kusingizia ni mimi nimemuumiza hivyo...’akasema mzee

‘Ila mimi nilikuwa nataka kuongea na wewe, ....hapa au ndani, utakavyoona wewe...’akasema

‘Wewe mzee, umemuumiza mlinzi wangu halafu unasema unataka kuongea na mimi....?’ akauliza

‘Nataka kuongea na wewe kuhusu ndugu yangu aliyefika hapa, akapoteza fahamu mengine hayanihusu,...kilitokea nini mpaka akapoteza fahamu nataka kulijua hilo,...’akasema akiwa kakunja uso

Yule jamaa mwenye nyumba, akawa akimuangaia mlinzi , kwa hiyo hali inabidi apate huduma ya kwanza, lakini mzee naye inabidi afundishwe adabu....akasema

Ina maana wewe ndio umemuumiza mlinzi wangu kiasi hicho....?’ akauliza akimuangalia mlinzi halafu akamuangalia huyo mzee, na wakati huo mlinzi alikuwa kashikilia kichwa akionyesha hasira , damu zikiwa zimelowesha mpaka sare yake ya kazi.

‘Ndio bosi,..huyu mzee ni tapeli amekuja hapa na maneno yake ya kitapeli, eti anataka kuingia ndani kuonana na wenye nyumba, nimemzuia kuingia ndani na kilichotokea ndio hiki,..kaniumiza ngoja nimfunze adabu...’akasema mlinzi akimuendea huyo mzee. Mzee akatabasamu ile ya dharau, akijiandaa kupambana na huyo mlinzi

‘Wewe mzee...’Jamaa, yaani huyo bosi wa nyumba, akiwa na hasira akamsogelea mzee,  kumsukuma kwa mkono, ili asogee mbali na gari lake, mzee hakusogea ilikuwa kama mti umepandwa, macho yake yalikuwa hayabanduki kwa mlinzi,....

‘Wewe mzee una akili kweli, unakuja kwenye nyumba za watu na kuanza kupiga walinzi, ....’akasema

Na aliposema hivyo, ndipo mlinzi akapatia mwanya, akainua kirungu chake hewani  akikilenga kichwani mzee, lakini mzee alikiona, akakikwepa,. Kikamgonga begani, mzee akageuka, upande, na akangurua kwa simba.....

‘Mhh.....’ akaguna, akigugumia yake maumivu ya kirungu, mzee akamwendea mlinzi mnzima mnzima, mlinzi arusha teke, kumtega mzee, mzee akaserereka kutaka kudondoka, akawahi kushika chini na mkono mmoja,.....mwenye nyumba akasogea na kumsaidia mlinzi na hapo mapigano, yakaanza mapigano.....

Tuendelee na kisa chetu

*************

Ni siku ambayo Profesa alifika sehemu ambayo huwa anauzia dawa zake akitokea hospitalini, na alipofika hakumkuta huyo rafiki yake wanayeuza naye dawa, na hata wale aliozoeana nao ambao hufanya biashara maeneo ya hapo hawakuwepo, kwanza aliona ajabu mbona kumekuwa kweupe..

‘Kuna nini kimetokea.....?’ akauliza akigeuka huku na kule..na bahati jamaa mmoja aliyekuwa karibu na gari, kuonyesha ni gari lake akasema;

‘Jiji limeanza mpango wa kuhakikisha, wauzaji wa biashara ndogo ndogo wanauzia sehemu rasmi, walizopangiwa ndio maana unaona leo kupo hivi...’akaambiwa

‘Oh, sasa kuna jamaa mmoja huwa alikuwa anakaa hapa, ....sijui atakuwa kaelekea wapi?’ akauliza

‘Nimesikia , hata leo alikuwepo...yeye ana kibali, lakini ndio hivyo wameambiwa wasiwe wanauzia eneo hili, lakini kwa vile kazoea kuja hapa, anafika akiangalia upepo unavyokwenda...’akaambiwa

‘Sijui tutauzia wapi dawa zetu...’akasema Profesa

‘Na wewe unauza dawa, ...unauza dawa gani, maana hata mimi nilikuwa namsubiria yeye...toka juzi haonekani, kila nikifika naambiwa katoka sasa hivi...’akasema huyo mtu

‘Sasa....atakuwa kaenda wapi ...?’ akauliza

‘Nasikia eti kaenda kituo cha polisi....’akaambiwa

‘Kituo cha polisi kuna nini!?’ akauliza sasa akionyesha mshangao, moyoni akahisi huenda polisi wamekishika kibali chake ......

‘Kwa jinsi nilivyosikia eti kuna tatizo linamhusu jirani yao wa huko kijijini anakotokea, yeye.....’akaambiwa

‘Tatizo gani, na jirani yao gani huyo?’ akauliza akionyesha shauku ya kutaka kusikia zaidi

‘Kwani.....’huyo jamaa akataka kusema na macho yake yakatua kwenye mkoba alio nao Profesa, halafu akasema;

‘Niliambiwa kuwa kuna jirani yao kashikiliwa na polisi kwa kuleta vurugu kwenye makazi ya matajiri....’akaambiwa

‘Mhh, ....kwanini sasa,..huyo jirani yao, ana akili kweli, kwanini aende kuleta vurugu, kwenye makazi ya watu, ni lazima kuna sababu au sio...sasa ‘akatulia

‘Ndivyo nilivyosikia...’akasema huyo mtu

‘Oh, sasa atakuwa nani huyo...jirani yake, au wanatoka kijiji kimoja to.....!’ Profesa akasema akiwaza

‘Wanasema ni jirani yao, sasa sijui kwa vipi, yeye alikuja hapa akiwa anamtafuta ndugu yake, ambaye alipotelea kwenye nyumba ya huyo tajiri, alipokwenda kuleta fujo, ....ni mambo ya kusikia tu, sasa sijui zaidi...’akaambiwa

‘Unasema.....alikuwa akimtafuta ndugu yake!?....’akasema Profesa akionyesha kushituka,

‘Sisi ndivyo tulivyosikia, si unajua tena, mambo ya kusikia,zaidi labda ukionana naye lakini kiujumla ndio hivyo, anahangaika kuona jinsi gani ataweza kumtoa, au kumuwekea dhamana huyo jirani yao,...kwani kachokoza wenye nazo....’akasema

‘Mhh,  sijakuelewa...’akasema Profesa sasa akiwa hana amani kabisa alishahisi jambo

‘Ndio maana natanguliza kukuambia kuwa nimesikia,.mimi sio mkaaji wa hapa, nakuja na kuondoka, kwahiyo sijaelewa zaidi,maana hata haya ninayokuelezea nilisikia huyo jamaa niliyemkuta hapa akimuhadithia jamaa mwingine aliyekuja naye kuulizia dawa....kama mimi...’akaambiwa

‘Kwahiyo....kaenda polisi kumfuatilia huyo jirani yake...’akasema Profesa sasa akitaka kuondoka

‘Ndio hivyo, huyo muuza dawa anafuatilia dhamana ya huyo jirani yake, aliyeleta vurugu kwenye makazi ya watu, akimtafuta ndugu yake inayesemekana alipotolea humo, sasa katika kuulizana huyo jamaa akaleta vurugu, akaitiwa polisi akakamatwa...’akasema

‘Mbona balaa hili....’akasema Profesa

‘Na huyo muuza madawa asingelijua hilo, ni kwa vile, huyo jirani yake aliacha mzigo wake hapa, kuwa akitoka huko ataupitia hapa, sasa muuza madawa alipoona jirani yake anachelewa kurudi, akaona na yeye amfuatilie huko anapohisi alikwenda akijua na yeye huenda kapotelea huko,...’akasema huyo jamaa

‘Ile anafika huko ndio akakutana na hiyo taarifa kuwa huyo jamaa kaswekwa ndani kwa kuleta vurugu, na hata kumuumiza mlinzi wa nyumba....’akasema

‘Balaa gani hili tena....!’ akasema Profesa akionyesha kuchanganyikiwa

‘Wapo kituo gani cha polisi?’ akauliza

‘Nahisi kitakuwa hicho kituo kikuu cha polisi cha hapo mbele...., ‘akaambiwa

‘Oh, inabidi niende huko kumuona, wewe ulikuwa unahitajia dawa gani..?’ akamuuliza na huyo jamaa

Huyo jamaa  akamuelezea tatizo lake, na Profesa akamuambia dawa hizo anazo, akamtolea huyo jamaa dawa anayoihitajia, na alipopewa pesa akashukuru maana hapo alipo hakuwa na kitu mfukoni, na kwa haraka akaondoka mbio mbio kuelekea  huko kwenye kituo cha polisi

*************

Profesa alifika kituo cha polisi na alipofika, akakutana na rafiki yake, akiwa kasimama nje ya kituo, akiwa anasubiria, na alionekana kama anataka kuondoka, akamsogelea na kumshika bega, na kitendo hicho kilimfanya rafiki yake kushituka na kugeuka kwa haraka, na alipomuona kuwa ni Profesa akasema;

‘Ulikuwa wapi wewe, umesababisha mpaka kaka yako kashikwa na polisi?’ akauliza

‘Kwanini sasa...yeye anakwenda kuleta ubabe kwenye majumba ya watu...kwanini kafanya hivyo, kaka naye bwana, sasa hili balaa’ akasema

‘Umesikia eeh,...kaleta vurugu kwenye nyumba za watu, matajiri, ...kaka yako unafahamu mihasira yake, sasa ananyea ndoo humo ndani, akitoka hapo ni gerezani...., ukimuona utamuhurumia..’ akasema

‘Sasa umefikia wapi, kwani kaumizwa....?’ akauliza Profesa akionyesha wasiwasi

‘Siunajua tena kuingia polisi ni bure, ...lakini kutoka, ni kazi...na mimi hapa sina chochote, unajua leo ni sikuu ya pili nahangaika,....isingelikuwa shemeji, mke wa kaka yako, ningeacha jamaa ajifunze adabu kidogo....’akasema

‘Oh ndio ujirani mwema huo ni lazima umsaidie..’ akasema

‘Ndio hivyo, ....lakini Kaka yako kazidi na mihasira yake ya kizamani.....wewe utakwendaje kwenye nyumba ya mtu ulazimishe kuingia, eti alitaka kuhakikisha, na kujua kwanini ndugu yake alipoteza fahamu,..akakutana na vichwa maji,...nasikia eti kwanza alimuumiiza mlinzi,...na haijatosha, akaanza kuoigana na mwenye nyumba...’akaambiwa

‘Kapigana na mwenye nyumba, mungu wangu,....’akasema profesa akitikisa kichwa

‘Wanasema awali mlinzi alimzuia kaka yako asiingie, kaka yako....hakusikia akatumia nguvu na ndipo akamuumiza mlinzi,, mwenye nyumba aliporudi akaona hiyo hali, akahamaki kwanini huyo mtu kampiga mlinzi wake....’akawa anasimulia

‘Kaka yako akataka kuendelea kupigana na mlinzi, nahisi ni kutokana na majibizano, sasa mlinzi akapata sababu, akishirikiana na mwenye nyumba, wakamweka mzee sawa,wakamchangia...mzee chali...lakini mzee bado akawa anazidi kuleta vurugu, wakaona wanaweza kuua, ikabidi waite polisi, ....’akasema

‘Ina maana kaka yeye atakuwa hana akili kupigana na mlinzi hata kama alikuwa na sababu ya muhimu haitaonekana tena...’akasema Profesa

‘Unaambiwa hata polisi walipofika, mzee badala ya kujisalimisha anataka kuendelea kupigana mbele ya hao watu wa usalama, wakaona kumbe mzee huyu mjeuri, wakamgonga virungu miguuni, nasikia walimfikisha hapa hata kusimama hawezi....’akasema

‘Mhh....sasa umefikia wapi, kipi kinahitajika, dhamana, au ...?’ akauliza na mara askari mmoja akafika na kusema;

‘Nyie ndio jamaa wa huyo mbabe hapo ndani?’ wakauliza

‘Ndio afande, akasema rafiki yake Profesa, na profesa alikaa kimia, akiogopa kujionyesha kwani huko alipotoka hospitalini katoroka, isije ikawa taarifa zimeshafika hapo.....

‘Ni hivi, ..ndugu yenu kakiuka sheria, kwenda kuleta vurugu kwenye nyumba za watu, kumuumiza mlinzi... pili alikataa kutii amri za za watu wa usalama, ...kwahiyo ana kesi ya kujibu, anahitajika kupelekwa mahakamani...’akasema huyo askari

‘Lakini afande tunaomba haya mambo tuyaongee nje tu, tutaongea na hao watu waliofanyiwa fujo tuyamalize kienyeji, hakuna haja ya kwenda mahakamani...’akasema jirani

‘Hilo halipo, ...kwa mujibu wa sheria, ndugu yenu anahitajika kufikishwa mahakamani, na huko ndio mtamuombea dhamana, lakini sisi hapa hatuna zaidi, hatuna cha kuwasaidia...’akasema huyo polisi, wakajitahidi kuongea naye lakini haikusaidia kitu,

‘Mkuu wangu ambaye mwenyewe ndiye alikwenda huko kwenye tukio, aliona ukaidi wa ndugu yenu, kwahiyo mimi nitafanya nini...’akasema huyo askari

‘Unaweza kutusaidia tu afande, ujue huyo mzee katokea huko kijijini..’akasema Profesa

‘Ndugu yenu mkorofi, anadai kuwa aliwahi kuwa kiongozi wa kijiji, kiongozi gani hana  hata hekima, unafikaje kwenye makazi ya watu na kuleta vurugu....anadai alitukanwa na kukashifiwa, sasa kwanini achukue sheria mikononi mwake...kwahiyo hii ni kesi ya vurugu na kujeruhi....zaidi mimi sina...mkuu keshaondoka, ,,,’akasema polisi huyo

‘Sasa tutafanyaje afande...?’ akauliza Profesa

‘Muhimu kesho mfike mahakamani huko mtaomba dhamana, ...kwa hapa, mtapoteza muda wenu bure...’akasema huyo polisi

‘Afande,,...tunaomba basi tuonane naye ...’akasema Profesa

‘Kwa hivi sasa muda umekwisha , ...kama ni kuonana naye utaonana naye hiyo kesho...na ni huko mahakamani, na baada ya hapo inabidi kupelekwa gerezani, sio hapa tena....kama mumemletea chochote cha kula tutampokelea....’akasema huyo askari

 Walijitahidi kuongea lakini haikuwezekana, ikabidi waondoke, na kesho yake wakafika mahakamani wakati kaka mtu huyo akisomewa mashitaka yake na dhamana ikahitajika hati ya nyumba, ..na wadhamini watatu..ikabidi wanafamilia hao kuhangaika kuzipata hizo hati na wadhamini ...mpaka wanakamilisha muda ukawa umekwisha, ikabidi warudi tena kesho yake..

Dhamani ilikuja kukubaliwa wiki imeshapita, na kaka mtu alishapelekwa gerezani, kwani hapo kituoni, alitakiwa kukaa siku moja tu,..na huko gerezani alitolewa akiwa magonjwa, akapelekwa moja kwa moja hospitalini, hata siku ya kesi yake inatajwa, yeye alichukuliwa kutoka hospitalini aliokuwa kalazwa.

Kesi ikasomwa kwa mara ya kwanza na kwa maelezo yalivyotolewa, ilionekana kaka mtu yupo hatiani ana kesi ya kujibu, hata mwenyewe alipoulizwa alikubali kuwa alifanya makosa kwa vile alikuwa kachanganyikiwa akimtafuta mdogo wake aliyepotea siku mbili...

‘Ndio ufanye fujo kwenye makazo ya watu ujeruhi...’akaambiwa
Kesi ikahirishwa na kupangwa tarehe nyingine, na kwa vile alishakubali kosa kilichoratajiwa  ni hukumu,...hata hivyo, dhamana ilishakubaliwa....akaruhusiwa kwenda nyumbani. Japokuwa hali yake ya kiafya ilikuwa sio nzuri, na hata aliofikishwa nyumbani  akawa mtu wa kitandani...

Ya kaka kama ya mdogo mtu...japokuwa yeye hakuwahi kufanyiwa ukatili huko gerezani, lakini 
kwa tukio hilo, alisononeka sana moyoni.

***********

‘Ilivyo, ili hii kesi ifutwe, inabidi kuongea na hawa watu,....’akasema Profesa

‘Kesi ifutwe! Wewe kesi kama hiyo haiwezi kufutwa, nani kakuambia inaweza kufutwa...?’ akauliza mtu mwingine

‘Kuna kinachoshindikana...ni kumpata wakili mnzuri tu, na kama tungelikuwa na pesa..kesi kama hii ni ndogo tu....’akasema Profesa

‘Unasema kuongea na watu gani sasa...?’ akauliza jirani yake

‘Hapo kunatakiwa kuongea na hao waliofanyiwa fujo, wenye nyumba huko mjini, hao watu waliofanyiwa fujo, wao ndio walioshitaki,...’akasema

‘Hata kama ingelikuwa wewe ungekaa kimia, mtu aje kwenye nyumba yako alete vurugu....’akaambiwa

‘Ile nyumba kwanza sio ya kwao...wameipata kwa dhuluma tu....’akasema Profesa

‘Unajuaje kuwa sio yao, kisheria, ni yao, hata kama ni wapangaji....’ akaseme mwenzake

‘Najuaje, najua sana, lakini hayo tuyaache...ndio maana sitaki kabisa mimi kuongea nao watu...’akasema profesa .

‘Sasa ni nani wa kuongea nao....?’ akaulizwa

‘Inabidi wazee wenye hekima wakakutane na hao watu, wawashawishi, wakubalia kufuata hayo mashitaka...’akasema

‘Hilo ni kweli, ..tunaweza tukazunguka kumbe kweli kuna njia ya mkato,...inabidi kuongea nao, wao wanaweza kuimaliza hii kesi,ikibidi hata kuwapigia magoti...ili kaka yako atulize kichwa, unajua hata kuumwa huko kunatokana na mawazo...’akasema huyo jirani  rafiki wake wa biashara.

‘Lakini mimi siwezi kwenda kuongea nao, eti niende kuomba...nimpigie magoti, hapana, mimi nitakwenda kuongea nao, siku maalumu lakini sio sasa, natayarisha mambo yangu , yakiwa tayari, tutapambana nao, tena mahakamani..’akasema Profesa

‘Lakini kwa hivi sasa rafiki yangu, hakuna jinsi,....wewe upo tayari kaka yako atesekee, na ukicheza anaweza kusweka jela, akienda jela atafia huko, sasa umefanya nini, ni bora uwe mnyonge kwa hivi sasa kwa ajili ya afya ya kaka yako, ,..’akaambiwa

‘Kwa kuongea nao sio lazima mimi.....’akasema

‘Sawa sasa unataka tufanyehe...., lakini ngoja, hilo niachie mimi, nitaongea nao...najua jinsi gani ya kufanya...’akasema jirani yao huyo.

Na kweli jirani yao huyo, akakutana na jopo la wazee, wakachaguana, na baada ya kujua ni nini kinachotakiwa kufanywa baadhi ya wazee wakatumwa mjini, kwenda kuonana na hao walioshitaki polisi...

‘Itabidi tukifika huko cha kwanza tuombe msamaha kwa kilichotokea  na wa kuomba msamaha ni mdogo mtu, na pili kuwaomba wao wasaidie hiyo kesi ifutwe....’akasema mzee mmoja mwenye busara, kauli hiyo ilimfanya Profesa kuja juu, akasema

‘Nimeshawaambia mimi siwezi kwenda huko kwa hivi sasa...siwezi..’akasema

‘Unatakiwa wewe kwa niaba ya kaka yako, kaka yako hawezi kwenda huko mjini kutokana na hali yake ilivyo...’akasema

‘Hata kama kaka angeliweza kwenda asingelikubaliana na ombi lenu hilo...’akasema Profesa

‘Sasa kwanini,? Mbona hamtaki kuliweka wazi hili jambo..kuna nini, kwani kaka yako hakuenda kufanya fujo kwenye nyumba ya watu,..mnatakiwa muwe na uelewi wa sheria, hata kama kuna mambo mengine kati yenu, lakini huwezi kwenda kwenye nyumba za watu na kufanya fujo....’akasema mzee

‘Hebu Profesa tuambie wazi, wewe ulipokwenda huko kulitokea nini, maana chanzo kikubwa ni wewe, isingelikuwa wewe kaka yako asingelifika huko akikutafuta?’ akauliza mzee mmojawapo

‘Ni kweli kaka yako anaugulia, anaumia , kateseka kawekwa ndani kwasababu yako,....sasa kuna nini mbona hili jambo mumelifanya liwe la siri sana....’akaongeza mwingine

‘Lakini nilishamwambia bro, mambo yangu asiyafuatilie kabisa yeye hayawezi, sijui kwanini hakunielewa....’akasema

‘Hivi kweli una akili wewe...ina maana kweli kaka yako mwenyewe angetulia tu, wakati siku mbili ulikuwa haupo, haijulikani wapi ulipo....’akaambiwa

‘Ya kwangu yaacheni, yaacheni kabisa, yeye mwenyewe nilishamwambia,mambo yangu ni ya kimataifa, nayafahamu mwenyewe ...’akasema

‘Unajua wewe ndugu hatukuelewi, ina maana hata likitokea tatizo kaka yako asikufuatilie,...kama angefanya hivyo, basi angekuacha kuja kukuchukua kipindi kile wakati umelazwa, kama si ungelifia huko hospitalini.....’akaambiwa

‘Niwaambie kitu, yangu yana muda wake, muhimi tuendelee na hayo ya kaka, ...’akasema

‘Lakini si ndio tunataka kujua chanzo ni nini...’akaambiwa

‘Nimeshawaambi mimi sitaki kuongea lolote kuhusu mambo yangu kwa watu, hata kaka nilishamuambia kuwa mambo yangu asiyaongee kwa yoyote yule,...kwa hivi sasa, maana nitazidi kuumia, nawajua watu walivyo...’akasema

‘Mimi nijuavyo ni kuwa wewe unafuatilia maswala ya nyumba yako ya mjini, au sio, kwani imekuwaje kuhusu hiyo nyumba, nasikia ni nyumba kubwa tu....na sasa inamilikiwa na watu wengine uliuza au ilikuwaje?’ akaulizwa

‘Hayawahusu....’akasema Profesa

‘Kwasababu mara nimesikia, kuna watu walifanya njama ikauzwa ukiwa jela huko ulaya, au sio ...na ulikwenda kuonana na hao watu waliopo sasa...,  sasa ilikuwaje huko, maana uliokwenda huko ndio ukapotelea huko...’ akaulizwa na jirani rafiki yake

‘Nimewaambia hayo yangu kwa hivi sasa hayawahusu, siwezi kuyaongea maana nikiyaongea yatazua mambo mengine makubwa, kwanza tuangalie hili la kaka, ndilo muhimu, haya yangu kiukweli hayawahusu kabisa,  mimi nitajua la kufanya, muda ukifika...’akasema akionyesha kuchoka.

‘Hao wenye nyumba, tutaenda kuongea nao, hilo halina shaka, lakini wewe unatakiwa uwepoo kwa niaba ya kaka yako,....usipokuwepo wewe wao watatuamini vipi, huwezi kuomba msamaha kwa niaba wakati mwenyewe yupo, kama kaka yako angelikuwa mzima, ana weza kusafiri tungeenda naye, lakini kwa hali yake ilivyo, hatuwezi kumchukua,  inabidi wewe  ndio uifanye hiyo kazi , ukaombe msamaha kwa niaba yake...’akaambiwa

‘Na tena ikibidi hata kuwapigia magoti maana kesi hii ni ngumu...’akasema rafiki yake

‘Eti nini....mimi Profesa niende kuwapigia hao wahuni magoti, kuwa naomba msamaha,...hahaha, nyie watu, ...hapana, hilo kama mnaweza mbebeni kaka akalifanye yeye mwenyewe, kama atakubali...lakini sio mimi...’akasema

‘Kwanini sasa.....?’ wakamuuliza wakionyesha kushangaa

‘Mimi siwezi kwenda kuonana na hao watu kwa hivi sasa, nina sababu zangu chungu nzima, nyie nendeni, kama atagoma, sasa nitajua kweli yeye ni kidume, ..nawaambia ukweli, mimi siwezi kwenda kwa hivi sasa kuonana na hao watu, hatutaelewana kwa hayo yaliyotokea.... hata kaka, akisikia hivyo, hatanielewa...’akasema

‘Kwanini..mbona hatuwaelewi....mnajua hii kesi ni kubwa, mtu kuleta fujo na kujeruhi,...unajua kesi kama hiyo hapo ni kifungo na faini...hivi nyie watu mpoje...! ‘Akasema mzee mmoja kwa sauti ya hasira.

‘Kwahiyo nyie mnataka nisema nini...?’ akauliza

‘Utuambie kila kitu...ambacho kilifikia hadi kukatokea hilo, sizani kama kaka yako angelifanya fujo tu,lazima kuna sababu..na je swala la nyumba limefikia wapi, maana wewe ulikwenda huko kulifuatilia, na ndio ikawa sababu ya kupotelea huko, yote hayo tunahitajika sisi kuyafahamu kwanza kabla hatujafika huko...’akaambiwa.

Profesa akatulia kimia halafu baadaye akasema

‘Nyie nendeni huko mjini mkaonane na hao watu...mimi sitaenda...kama watakataa sasa mimi nitajua ni nini la kufanya, lakini siwezi kwenda huko kwa hivi sasa...’Profesa akaishia hapo,

Wazee walipoona hivyo, wakainuka na kuanza kuondoka...

Ni nini kitatokea?

WAZO LA LEO: Vurugu, uhasama huanzia na jambo dogo tu, kutokuvumiliana,kutokusikilizana, na kutokusameheana. Kipindi cha kutofautiana ni kipindi muhimu sana kwa kila mmoja kuzishinda nafsi zake, kuweka hekima mbele, na kujua kuwa chuki na uhasama yaweza kuwa chimbuko la vita,tukiangalia kinachoendelea sasa kuhusu uchaguzi na sasa matokeo yake huu ni muda tunahitajika tuwe pamoja tujenge uvumilivu, tukubali kuwa kwenye ushindani kuna kushindwa na kushindwa ...ya wenzetu yalianza hivyo hivyo,...wao ni wanadamu kama sisi. Kinachotakiwa kwa watendaji ni haki na ukweli ...
Ni mimi: emu-three

No comments :