Ni siku ya pili Profesa haonekani huko
kijijini.....
‘Huyu mtu kaenda wapi...?’ kaka mtu
akajiuliza
Kaka mtu akajaribu kuwauliza majirani na hata watu wanaomfahamu huyo ndugu
yake huko anapofanyia biashara zake huko mjini, lakini hakuna aliyeweza
kumsaidia,kila alijubu sijui,...
Mwisho wa siku uamuzi ukapitishwa, kuwa ni bora kwenda kumtafuta huko huko mjini...mji una mengi, na isitoshe ndugu yake huyo ni mgonjwa, huenda alizidiwa, huenda.....
Tuendelee na
kisa chetu...
Siku
iliyofuata kaka yake Profesa alifika mjini na kwenda kwenye nyumba ambayo
alielekezwa kuwa profesa alionekana akiiingia hapo, na watu hawakumuona akitoka
‘Ataingiaje
apotelee humo humo....’akauliza kaka mtu
‘Labda ufika
ukawaulizie walinzi...’akaambiwa na watu waliowahi kumuona mtu akiingia humo
ambaye anafanana na maelezo ya huyo kaka mtu.
Akaikagua
hiyo nyumba, akiona mabadiliko makubwa, nyumba aliyokuwa akiifahamu zamani
haikuwa hivyo, ina maana nyumba hiyo imefanyiwa ukarabati mkubwa hadi
kubadilika, lakini alikuwa na uhakika ni hapo ndipo ilikuwepo nyumba ya ndugu
yake...
Japo
hakupenda kufika kwenye nyumba hiyo, hakupenda kabisa kuyaingilia maisha ya
Profesa na watu wake, hasa baada ya kusikia maelezo aliyosimuliwa na mdogo
wake,...lakini hakuwa na jinsi , ndugu yake hajaonekana leo siku ya pili, na
sio kawaida yake na mtu mwenyewe ni mgonjwa.
‘Ni lazima
niwaulize nijue .....huenda, yupo humo ndani, au...., na kwanini kama kapatwa
na tatizo, mbona hajapiga simu, ...’akawa anajiuliza huku akielekea kwenye hiyo
nyumba.
Wakati
anaondoka huko kijijini alipitia kwa jirani yake mmoja ambaye naye ana biashara
mjini,kama anaweza kuwa na taarifa yoyote...
‘Hapana,
kiukweli sina chochote nikijuacho kuhusu yeye....kwani hajafika huko nyumbani
kwake,....?’ akauliza huyo jirani
‘Hajafika siku
ya pili sasa...’akasema kaka mtu..
‘Muhimu ni
kwenda huko mjini, mtu mwenyewe mgonjwa labda kazidiwa, na wengi wa pale
hawamfahamu sana, watu waliopo sasa ni wageni wageni tu..’akaambiwa na jirani
‘Lakini hali
yake sio ya kuzidiwa, kajaribu kufuatilia masharti, ..hakuwa na hali mbaya, si
mnamuona mwenyewe alivyo, kanenepa, sio yule maiti aliyefika hapa....’akasema
kaka mtu
‘Hahaha, na
wewe bwana ina maana ulifikia kumuita ndugu yako maiti..’akasema jirani yake
‘Wewe
ulimuona alivyokuwa,kipindi anafika ...aliisha ya kutisha hadi mifupa yote
unaihesabu..kweli kuumwa sio kufa, na mungu kamjalia, sasa kanawiri, na alivyo
mshari, huenda kafika mjini kalianzisha...’akasema kaka mtu
‘Ina maana
unajua kaenda huko kwa shari?’ akaulizwa
‘Hapana,
hajasema hivyo, huwa anakwenda kuuza uza dawa zake, ili apate kujikimu..dawa
zake zinatibu, watu wanazitafuta....lakini huwezi jua, ya mjini mengi....’akasema
‘Sasa kwanini
hajapiga hata simu?’ akauliza jirani
‘Ndio hilo
linanitia mashaka, na kwa vile nina safari ya mjini, nitayajua huko huko, na
kama kuna mtu kamnyanyapaa ndugu yangu tutapambana huko huko, nasikia kuna watu
wenye tabia hizo chafu..’akasema kaka mtu
‘Siku hizi
mambo hayo hayapo bwana...kwanza sasa hivi mtu anaumwa na mwili wake, na huwezi
hata kumdhania kuwa mtu huyo ni mgonjwa, ....’akasema jirani
‘Kuna watu
wanaweza kumfahamu alipotokea, si unajua tena, lakini hayo nawazia tu sina
uhakika nayo ....’akasema kaka mtu
‘Sizani,..tuombe
mungu kuwa yupo salama, labda kuna mengine kakutana nayo,..au watu wa manispaa
wamemkamata, kwani biashaar zake zina kibali cha kuuza hayo madawa...?’
akaulizwa
‘Tena cha
kimataifa...ana kadi yake ya kuhalalisha biashara yake, imethibitishwa huko
ulaya, hilo la kukamatwa na watu wa manisipaa, sizani,...lakini nitajua yote nikifika
huko...’akasema
Basi kesho
yake asubuhi na mapema akapanda gari la kwanza na kufika mjini, wakati
anahangaika kutafuta vifaa vyake huku anaulizia, na baadaye akafika sehemu maalumu
ambayo aliambiwa kuwa ndugu yake huyo huwa anauzia dawa zake, mara kwa mara
Na akakutana
na jamaa mmoja ambaye alimuelezea ilivyokuwa;
‘Ndugu yako
jana alipomaliza kuuza dawa zake alisema kuna sehemu anapitia...’akaambiwa
‘Sehemu
gani?’ akauliza kaka mtu
‘Hajasema,
lakini nahisi ni pale ilipokuwa nyumba ambayo anadai yeye alikuwa
akiimiliki....ina maana hayupo nyumbani ?’ akasema jamaa na kuuliza
‘Hajafika leo
siku ya pili, Una uhakika atakuwa alikwenda huko?’ akauliza kaka mtu
‘Sina uhakika
sana...., lakini kinachonifanya nihisi hivyo, yeye siku ile, aliondoka
mwanzoni, akafika huko, na baadaye akarudi akasema huko alipokwenda hakuwakuta
wenyeji,...’akasema
‘Wenyeji
gani?’ akauliza kaka mtu
‘Mimi hapo
sijui,..ila yeye alisema alitaka kuonana na watu wanaoishi kwenye nyumba hiyo...mimi sijui ni nyumba
gani...’akasema mtu ambaye naye anauza madawa, na huwa wanajuana na Profesa,
kwa kipindi hiki, japo hajui maisha ya nyuma ya Profesa.
‘Ilikuwa muda
gani alipokwenda huko?’ akauliza kaka mtu
‘Ilikuwa
muda wa mchana hivi, ni kama saa nane hivi,...nahisi kuna kitu kilikuwa kikimsumbua, hakuonekana
kama ilivyo siku za kawaida...’akasema
‘Hakusema
anaumwa?’ akaulizwa
‘Hapana,
alisema yupo na afya njema kabisa,...ila mimi nilihisi kuna kitu anafikiria
sana...’akasema
‘Kwahiyo
alipokwenda mchana akarudi, halafu akaenda tena muda gani, jioni,..kwanini?’
akauliza
‘Bro kiukweli
mimi sijui mambo yake, jamaa ni msiri sana na mambo yake, unajua hata jioni
mara nyingi tunaongozana, lakini siku ile,...hatukuongozana kituoni kama
kawaida, yeye alisema kuna sehemu anapitia, sikuwa na muda wa kumuuliza maana ilikuwa
ni muda kila mmoja anahangaika kutafuta usafiri....’akaambiwa
‘Kwahiyo ni
vyema niende huko nikaulizie..ooh, sipendi kabisa kwenda huko,...kujiingiza
kwenye mambo yake, lakini sina ujanja , ni lazima niende nione kama alifika
huko..’akasema
‘Sawa utatufahamisha
basi kinachoendelea kama kuna msaada unahitajia, utatuambia, maana yule ni
mwenzetu japo hatujaanzisha ushirika, tuna wazo hilo la kuanzisha ushirikiano
wa kuuaza madawa, ngoja tukae vyema...’akaambiwa
‘Sawa ni wazo
zuri, ngoja nifike, nitakuja kuwapa taarifa.....na huu mzigo wangu nauacha
hapa...’akasema
Ndipo
akaelekea huko....
Akafika
kwenye hilo jengo na kugonga mlango, na mlinzi akafungua mlango mdogo wa
kupitia watu, akamuangalia huyo mzee juu hadi chini, akauliza
‘Una shida
gani mzee?’ akauliza
‘Ndio salamu
hiyo...?’ akauliza huyo mzee naye akimkagua mlinzi kama alivyofanya yeye
‘Shikamoo
mzee, nikusaidie nini...?’ akauliza huyo askari
‘Kuna ndugu
yangu alifika hapa siku mbili zilizopita, nasikia aliingia humu, na hajaonekana
akitoka tena, ...je humo ndani anafanya nini?’ akauliza na huyo mlinzi akatulia
kama anawaza
‘Una uhakika
na unachokisema,...mtu aingia halafu asionekane, ni nani huyo, au umekosea
nyumba...’akasema
‘Sijakosea ni
hapa hapa....’akasema
‘Yupoje huyo
ndugu yako?’ akauliza huyo mlinzi akionyesha uso wa mashaka.
‘Ni mwembamba-mbembamba
hivi,....ananyoa kipanki..kimtindo
wake....’akasema na huyo mlinzi akamchunguza huyo mzee halafu akasema
‘Mhh,....’akaguna
hivyo, na akawa anaendelea kumkagua huyo mzee, halafu akasema
‘Naona kidogo
mnafanana naye, ...ndio alifika mtu kama huyo, alifika hapa akitaka kuonana na
wenye nyumba, na bahati mbaya, ...’ hapo akatulia kidogo, halafu akasema
‘Hivi huyo
ndugu yako ana matatizo gani?’ akauliza
‘Bahati mbaya
nini, kapatwa na nini?’ akauliza mzee huyo akionyesha wasiwasi
‘Alidondoka
tu na kupoteza fahamu....tuliambiwa na mabosi zangu walipotoka hositalini, maana
walitoka na gari kwa haraka hatujui kuwa ndani kuna mtu, kumbe ndio yeye
alizidiwa huko ndani, ni mgonjwa mgonjwa eeh,...’akasema kama anauliza
‘Hospitalini,
kalazwa, au imekuwaje na alidondokaje, ....hadi kupoteza fahamu, hivi hivi tu ..bila
sababu. yoyote...?’ akauliza
‘Ndio kwa
maelezo ya mabosi zangu ndivyo ilivyokuwa, kama una zaidi nenda hospitali hii
hapa....’yule mlinzi akatoa karatasi aliyopewa, na mabosi zake kuwa kama
atakuja ndugu akiulizia kuhusu huyo mtu, aelekezwe huko, ya kuwa huyo mgonjwa
kalazwa kwenye hiyo hospitali zaidi watapatia maelezo huko...
‘Nataka kujua
kilichomtokea hapa hadi akadondoka na kupoteza fahamu...lazima kuna sababu...’akasema
huyo kaka mtu
‘Sisi kazi
yetu ni ulinzi, yaliyotokea huko ndani hatujui,..tunachojua na tulichoambiwa ni
kuwa ndugu yenu alidondoka na kupoteza fahamu, na ikafanyika juhudu za
kumtibia, kwa kupelekwa hospitalini,...na yuko huko akiendelea na matibabu,
mengine zaidi utayapatia huko huko hospitalini...’akasema mlinzi
‘Naweza
kuonana na wenyewe, wapo ndani au sio....?’ akauliza
‘Hujanielewa mzee,kiachotakiwa
ni wewe.uende hospitalini, huko ndipo utamuona mgonjwa wako, na huko ndipo utayapata
maelezo zaidi, hapa huwezi kupata lolote, na wenyewe hawapo, wamekwenda
kazini....’akasema mlinzi
‘Wanarudi saa
ngapi?’ akauliza Mzee akiwa kamkazia macho huyo mlinzi
‘Kwani lengo
lako ni nini, kuwaona wenyeji au kumuona ndugu yako?’ akaulizwa Mlinzi
akimuangalia huyo mzee kama anamkagua chini juu...
‘Ni vyema
nikajua kilichotokea,...na nini sababu iliyofanya ndugu yangu kudondoka na
kupoteza fahamu...nani ataniambia kama sio hao watu aliokuwa nao kipindi
anadondoka, na kwanini adondoke humo ndani asidondokee nje,...mpaka afikie
kupoteze fahamu, nakaa naye haijawahi kutokea hivyo...’akasema
‘Ndugu yako
anaonekana ni mgonjwa,...hata ukimuangalia hivi kwa macho anaonekana ni
mgonjwa, sasa labda tukuulieze wewe ndugu yako ana matatizo gani...’akasema
mlinzi
‘Nani
kakuambia ndugu yangu ni mgonjwa,...hata kama ni mgonjwa, haijatokea kudondoka
na kupoteza fahamu nikiwa naye, na sio kwa vile unamuona ni mwembaba ndio useme
ni mgonjwa, watu wengine wanakuwa hivyo kutokana na nakama za maisha tu....’akasema
‘Hahaha,
nakama za maisha eeh, kumbe....’akasea
‘Kumbe
nini....?’ akauliza kaka mtu
‘Kumbe ,
alikuja hapa kuomba, au.na njaa zake..nyie watu nyie, mnatafuta sababu, au....?’ akawa kama anauliza
‘Ni nani
kasema kuwa ndugu yangu alikuja hapa
kuomba....’akasema mzee akionyesha kukasirishwa na kauli hiyo
‘Wewe si
umesema kakonda kwa maisha magumu,....si umesema wewe mwenyewe...’akasema
mlinzi
‘Nimekuambia
alikuja kuomba...’akasema kaka mtu
‘Sasa
tunabishana bure , mimi nimesema ndugi yako anaonekana anaumwa, wewe umekataa,
ukasema kakonda kwa nakama za maisha,...sasa sikiliza ....hayo nakumegea tu,
ila mengi utaambiwa ukifika huko...unanielewa mzee,....yeye alifika hapa, akawa
anaulizia wenyeji, tukampeleka ndani, yaliyotokea huko sisi hatujui....sasa
kama na wewe umekuja na nakama za maisha, hapa sio sehemu ya kutoa misaada....’akasema
mlinzi kwa dharau
‘Sijakuelewa una
maana gani...’akasema mzee
‘Umenielewa
sana, ila unatafuta sabau kama ndugi yako...’akasema
‘Sasa
sikiliza mimi siwezi kuondoka hapa, mpaka niwaone hao waliokuwepo wakati ndugu
yangu anapoteza fahamu, yule kupoteza kwake fahamu ni lazima kuwe na jambo,,
...huenda waligombana, akasukumwa, au kuna kitu kilimfanya apate mshituko,...ndio
nataka kulifahamu hilo, na wewe umesema hujui, ..’akasema
‘Mzee
tuelewane....’akasema
‘Kwanza
umeanza na kashifa zako naomba zikome..umenielewa wewe mlinzi.’akasema
akinyosha kidole.
‘Sio kashfa
mzee, umesema mwenyewe, shidaa ndio imemfanya akonde kihivyo, sasa kama ni
shida ndio uivalie kibwebwe, kugonga majumba ya watu, tuambizane ukweli au,nimekosea
kukuambia ukweli ...ukweli unauma sio....’akasema akitabasamu kwa dharau
‘Ukweli gani
huo,...?’ akauliza mzee sasa akionyesha kukasirika kiukweli
‘Yaishe
mzee....ile ujumbe umefika ....’akasema mlinzi
‘Unajua wewe sasa
umevuka mpaka, nimekuvumilia sana,....sasa nilitoka kuondoka, sasa siondoki, mpaka
nionane na hao mabosi zako,,..’akasema
‘Kama wataka
kupoteza muda wako kusubiria haya
endelea, lakini usisimame hapo..nenda
kulee...ila hapa hakuna sehemu ya kutoa
misaada...’akasema mlinzi
‘Umenichefua
kabisa, hata hivyo siwezi kurudi kijijini bila kuwa na taarifa kamili,
nitawaambiaje ndugu na jamaa, na pili wewe mtu wewe..ni lazima niwaambie mabosi
wako jinsi gani usivyo na adabu, kuzarau watu, hivi wewe unajiona umefika sana
kwa kazi hii ya ulinzi, kuwalinda wenzako wakiwa wamelala...unajiona una kazi
eeh..’akasema kama anauliza
‘Sikiliza
mzee,..wewe kwanza nenda hospitali, unasikia mzee, huko utapata taarifa, kama
zitakuwa sio kamilifu hapo sasa ukija,..utaweza kuwauliza wenyewe, au ndio kama
unataka kushitaki utafanya hivyo, kama wanaweza kuongea na wewe, au kuwasaidia
shida zenu......’akasema mlinzi akitikisa kichwa kwa kujiamini na dharau
Kaka mtu
akafikiria halafu, akageuka kama kuondoka, akawa kama kakumbuka jambo, akauliza
‘Kwanza hivi watu
gani wanaoishi humu wafrika au wazungu?’ akauliza akiwa karudi eneo lile ambalo
mlinzi hataki huyo mzee asimame
‘Mzee, mbona
unarudi nyuma tena...nimeshakuambia, nenda hospitalini, hawa wenye nyumba wawe
wazungu au waafrika hawatoi misaada, ....wewe unachotaka ni nini....ndugu yako
au wenye nyumba, hata wakiwa wazungu wanakuhusu nini?’ akauliza huyu mlinzi
akiwa anachezea rungu lake
‘Nina hitaji
niongee nao,si nimeshakuambia, ....’akasema
‘Hapo mzee sasa
unataka mengine...mzee, sisi kama walinzi tumetimiza wajibu wetu,zaidi ya hapo,
hatuna la kusema..ondoka eneo hili....’akasema huyu mlinzi akionyesha rungu
kama onyo
‘Hivi wewe
unafahamu historia ya hii nyumba ...?’ akauliza akipuuza lile onyo, akawa
anaichunguza hiyo nyumba
‘Hilo
halituhusu...’akasema
‘Inaweza kuwa
ndio sababu ya huyo ndugu yangu kupoteza fahamu,.....nahisi kuna jambo
lilitokea,... na kutokana na hilo itabidi niende nikatoe taarifa polisi wafanye
uchunguzi..’akasema akiendelea kuchunguza
‘Sasa hayo ni
juu yako mzee, kama alichofanyiwa ndugu yako shukurani zake ndio hizo, endelea
..ila nikupe angalizo, kuwa hawa sio watu wa kuogopa polisi, hawa ni wazungu,
wanajua sheria, ni wasomi, ..wanajua wanachokifanya...’akasema mlinzi
‘Kumbe ni
wazungu.....’akasema kwa kushangaa
‘Ndio....’akasema
mlinzi
‘Hata kama ni
wazungu, wasomi, lakini hawawezi kutumia ujanja ujanja wa elimu yao,kudhulumu
wengine, ...waje nchini kwetu wachukue
jasho la mtu kirahisi tu....hili tatizo lazima lifike kwenye vyombo vya sheria,
kama kweli serikali inawanajali raia zake, itafanya jambo, maana huu sasa ni
ukoloni....’akasema sasa akigeuka kutaka kuondoka
Yule mlinzi akiwa
kasimama katikati ya mlango, akasita kuingia ndani, akageuka kumuangalia huyo
mzee, akaingiwa na shauku fulani, akatoka pale mlangoni na kurudishia ule
mlango vizuri,
Akatembea
kuelekea pale aliokuwa yule mzee, ambaye alikuwa kasimama, lakini akionyesha
dalili za kuondoka,...., akamsogelea huyo mzee, na mzee alipogundua huyo mlinzi
yupo nyuma yake akageuka akionyesha wasiwasi, alihisi labda huyo mlinzi kaamua
kumjia kwa shari, akiwa kakunja uso akamuangalia huyo mlinzi
‘Samahani
kidogo mzee, unajua tena unaweza ukasikia jambo, ukaona ni muhimu
kulifuatilia...’akasema na mzee akabakia kimia
‘Hebu mzee niambie
kuna nini kinachoendelea maana huyo unayesema ni ndugu yako wakati alipofika
aliongelea kuhusu hii nyumba, lakini sikumuelewa,....unajua tena kazi zetu,
wanakuja watu wengi, inakuwa wakati mwingine ni usumbufu....’akasema na mzee
akabakia kimia
‘Sasa naona
ajabu hata wewe umeongelea kuhusu hii nyumba, kwani. mzee..hii nyumba
ilikuwaje,....unafahamu nini kuhusu hii nyumba?’ akauliza huyo mlinzi
‘Wewe si
umesema hayakuhusu kwanini unaulizia mambo yasiyokuhusu...?’ sasa mzee akasema hivyo,
akiwa kamuangalia huyo mlinzi
‘Aaah, mzee,
mimi nataka kujua tu, maana nimedadisi watu wanajua eneo hili, wanasema kweli
nyumba hii ilijengwa awali na mtu mwingine, nani sijui,...lakini wengine
wanasema huyo mtu wa awali, alisafiri kwenda kutafuta maisha ulaya, ...nasikia amekufa kwa huu ugonjwa wa kisasa...’akasema
akicheka kwa dharau.
‘Nashangaa
nyie mnakuja na ndoto za ajabu nyumba nyumba, mwenyewe ni marehemu tena kafa
kwa ...huu ugonjwa...lakini baada ya kuuza hili eneo na nyumba,...pesa nahisi
alizitumia kujibia lakini haikuwezekana....mungu kampenda, huo ndio
ukweli...’akasema akishusha sauti
‘Ondoa uchuro
wako hapa...ni nani kakudanganya hilo..’akasema kaka mtu kwa hasira na huyo
mlinzi akawa kama kashtuka kusikia kauli hiyo kutoka kwa huyo mzee
‘Nimesikia
hivyo, na ni taarifa za ukweli mzee, kama mlikuja kutapeli, hiyo mtaumbuka...,
kwani aliyeniambia, ni mtu wa uhakika, ...watu wa usalama wa taifa,...hawawezi
kudanganya, mimi namfahamu jamaa yangu anayemfahamu huyo jamaa.. sasa nyie
jidanganyeni na utapeli wenu, mtaenda kunyea debe, na uzee huo,....’akasema
akionyesha kuzarau
‘Unasikia,
huyo aliyekuambia na wewe nyote hamna akili,...’akasema huyo mzee na mlinzi
akacheka na kusema
‘Hahaha,
mzee, mimi nakusadia, ...unaniambia mimi sina akili,...nyie watu wa ajabu
kweli, mataka kutaeli hata visivyotapelika, hivi mnajiamini vipi.....’akasema
kama anauliza
‘Unajua kwa
kauli yenu hiyo, ni vyema kweli niende polisi, ili ukweli ujulikane, ,...na
kama ningeonana na hao wanaishi humu, ningelijua ni nini kinachoendelea,watu
wanavuisha uwongo, na wewe chunga mdomo wako.....’akasema mzee akimkazia mlinzi
macho
‘Hawa watu
wanarudi saa ngapi...?’ akauliza
‘Mzee, hawa
watu wamekwenda kazini, huwezi kuonana nao kwa hivi sasa....mimi nimekusaidia
kwa hilo, sasa kama unataka kujiabisha haya endelea...’akasema
‘Watarudi tu,
mimi nitaonana nao, nataka nisikie ukweli kutoka kwao, huenda hata hawajui
lolote, wameuziwa tu,.....’akasema mzee
‘Mzee kabla,
hapa kulikuwa na kibada kibovu tu, halafu hawa wakaja kununua eneo kukiwemo
hicho kibanda kibovu...wakakibomoa hicho kibanda, ndio wakajenga hili hekalu, ..’akasema
huyo mlinzi .
‘Kibanda
kibovu!, wewe waulize waliokuwepo hapa kabla, watakuambia ukweli kama kweli kilikuwa
kibanda kibovu....wewe wa kuja tu, hujui lolote...’akasema mzee
‘Sasa mzee,
huo ndio ukweli,...najua kwa utapeli wenu utasema sasa hata huyo jamaa
aliyekuwa na hicho kibanda ni ndugu yenu, ...hahaha, nyie watu bwana, huyo
alikufa kwa ngoma, yeye, alifika uzunguni badala ya kusoma akakalia uhuni,
hahaha, unajua wengi wakifika ulaya wanachofanya ni umalaya...’akatulia na mzee
akawa katulia akimuangalia huyo mlinzi.
‘Halafu mzee nikuulize
kitu, maana huyo aliyekuja hapa na kudondoka, ana matatizo gani, au na yeye
ndio ugonjwa nini...anavyoonekana eeh, mmmh, yule naye anao tu, lakini kwanini
hajaenda ushauri nasaha , inasaidia, wanaumwa siku hizi wanakuwa a hali nzuri
tu, wakifuata ushauri, ...’akasema na mzee akawa kimia tu
‘Halafu mtu
anaumwa, anataka kutapeli nyumba,..hivi anataka afe na nyumba, badala ya
kutulia, anakuja kudai nyumba yake, hahaha, wizi mwingine bwana, ....mzee,.
wewe rudi kijijni ukafuge,....mnafikiri mtaonewa huruma mahakamani, ....acheni
tabia hiyo mbaya.....’akasema
‘Unajua wewe
mlinzi nimekuchoka kwa dharau zako,...mimi siogopi kuwa wewe ni mlinzi,
..mlinzi gani hata silaha huna...mimi nimepitia mgambo, nimepambana na
simba...’akasema sasa akionyesha kukasirika
‘Mzee, sina
lengo la shari, nilitaka kukushauri...maana mnatutia aibu, siku hizi hapa
jijini kumejaa watu matapeli, watu wanauza nyumba za watu wenyewe wakiwa ndani,
pia watu wanaumwa wanataka visababu tu, njaa hii itatuponza kweli...’akasema
‘Kwahiyo mimi
ni tapeli,...unaendelea kunitusi,....umesema ndugu yangu ana ngoma,....tuna
shida.., wewe askari uchwara nahisi wewe
hunitambui nilivyo eeh....’akasema mzee na huyo mlinzi akaona isije kuwa shari
akageuka kutaka kundoka, na hapo akawa kalikoroga, akasikia bega likishikwa, na
wakati anageuka, akakutana na ngumi nzito, iliyompeleka aridhini.
‘Hiii itakufundisha
adabu.....’akasema mzee
Mlinzi hakutarajia
hilo kabisa, alijikuta yupo chini, na kichwa kikawa kimegonga kwenye mawe
yaliyokuwa yamepangwa hapo...
‘Aaaah, wewe
mzee....’akasema huyo mlinzi akishika kichwa...
Na kabla
hajaamuka kupambana na mzee mara magari
mawili yaliyokuwa yameongozana yakawa yanakuja, ilionekana kuwa ndio mabosi wa
hiyo nyumba, maana mlinzi badata ya kupambana na mzee, akakimbilia ndani,
kwenda kufungua geti, na mzee akawa anatetemeka kwa hasira,..
‘Na bado
ngoja nionane na hawa watu.....’mzee akasema akiangalia hayo magari yakiwa yamesimama
getini, kutaka kuingia, yeye kwa haraka akalifuata lile gari la mbele
akasogelea kwenye kiyoo na kugonga maana huwezi kuona ndani....
***********
Mlinzi ambaye
kwa muda huo alishafika kwa ndani akiwa kashikilia kichwa kikivuja damu, huku
mkono mmoja ukifungua mlango ili magari yapite, moyoni akiwa kajawa na hasira,...alisukuma
mlango, na alitaka afanye hiyo kazi haraka atoke nje akapambane na huyo mzee,...
‘Huyu mzee
nitamuonyeaha kuwa mimi ni nani, ngoja...aaah, damu....kichwa, hata ...’akawa
analalamika
Lakini jao
mlango wa geti ulikuwa wazi, alishangaa kuona hayo magari hayapiti,....hakutaka
bosi wake amuone alivyoumia, kwani maswali yatakuwa mengi, lakini kwa hali hiyo
alitakiwa kutimiza wajibu wake kuona kwanini magar hayaingii,
Ikaabidi asogea
kuangalia kuna tatizo gani, ...akamuona yule mzee kasimama pembeni ya
gari,.....akigonga dirisha la gari!
‘Huyu mzee
sasa , ngoja nimuonyeshe kuwa mimi nipo kazini...hawezi kunifanya hivi....’akasema,
sasa akitoka kwenda kupambana na mzee, akiwa tayari na kirungu juu, akimuendea
mzee nia amgonge hicho kirungu huyo mzee kichwani, atoke damu kama alivyotokwa
yeye
Lakini
alichelewa,...
Mlango wa
gari ukafunguliwa, na aliyetoka ni bosi wake mwenye nyumba akiwa kaiva kwa
hasira......Bosi wake aligeuka kumuangalia mlinzi akitaka kuanza kumlaumu kwanini anamruhusu huyo mzee kuzuia gari, akamuangalia mzee, halafu akamgeukia mlinzi,
'Kwanini ..' lakini alichokiona kilimfanya abakia mdomo wazi....
Tuishie hapa kwa leo....
WAZO LA LEO: Kauli za kuongea na watu zinaweza
kutafsiriwa vibaya kutokana na jinsi mtoaji ulivyozitamka, kuna watu wengine
kauli zao ni za kejeli , kuzarau, hata pasipostahiki. Wengine hufanya hivyo kwa
vile ni mabosi, matajiri, au watoto wa watu, au hata mfanyakazi tu...
Tujifunze
jinsi gani ya kuongea na wenzetu, kutegemeana na mtu au mazingira, ili kukwepa
uhasama au sintofahamu zisizo na msingi, kauli nzuri yaweza kujenga mvuto wa
heri, na kuleta maelewano mazuri tu, lakini kauli mbaya zenye zarau, zaweza
kuvuruga amani na hata kujenga chuki...tukumbuke, hekima ni bora sana kuliko
hata mali.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment