Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Tuesday, October 20, 2015

RADHI YA WAZAZI-47



Hatari....!

Kichaa kaona silaha, tena silaha kali.Panga, na moja ya jambo ambalo mzee huyo alikuwa akijaribu kulifanya, ni kuhakikisha kunakuwa hakuna silaha karibu, siku hiyo ikawa kasahau kuliondoa hilo panga, ambalo jamaa alizoea kutembea nalo, na akibadilika anaanza kucharanga watu...

‘Panga hilo ni moja ya vitu vyake alivyokuja navyo toka ulaya, alipewa zawadi alipokwenda ukweni kwa wanapotoka mama mtemi..’alisema mzee,

‘Kwahiyo alikuwa akilipenda sana hilo panga,....sasa baada ya kuharibikiwa likawa ni silaha yake, anatembea nalo, yule anayemsemesha, anamkata nalo, watu wengi waliumizwa sana na hilo panga, ...

Mzee alihakkisha hilo panga analificha mbali kabisa, sehemu ambapo huyo jamaa hawezi kuliona...

‘Sijui ni kwanini,...nililitoa hili panga wakati wanafanya usafi, nikawa na nia ya kulitoa humu ndani kabisa,....sasa mlipokuja nyie mkanisahaulisha....’akasema.

‘Sasa mzee kabla hatujaendelea naona ulifiche, uliondoe hapo au...?’ akasema mwenzangu

‘Sawa nitalitoa, kuna jamaa kasema anataka kulinunua, ndiye namsubiri, kama hatalichukua basi nitakwenda kuliweka sehemu nyingine, hivi sasa kalala, hawezi kufanya lolote...’yalikuwa maongezi ya awali,  na katika kuongea wakajikuta wamesahau kabisa kuhusu hilo panga.

Sasa ndio hapo kaliona....

Panga likaonekana, ....Jamaa akaliona hilo panga!

Wote macho yalitutoka pima kwa uwoga, tukajua sasa ni zamu yetu kucharangwa mapanga,..akilini kila mmoja alikuwa na wazo moja tu, ....kujiokoa,....

Kukimbia...nafsi yangu ikaniambia

Mimi nilishaanza kujiinua, japo sio kwa kusimama kabisa, lakini zile hisia za kufanya hivyo, tayari zilishajijenda mwilini, mwili ulishajiandaa....kukimbia nikawa nimeshajiweka tayari, kama wanavyofanya wanariadha wanavyojiweka tayari kwa kuanza kukimbia....

‘Kwenye mstari wako,...kaa tayari...’ iliyobakia ni sauti ya `goooo’ au filimbi, hapo haikutakiwa kusubiria hiyo `gooo’

Na wakati hayo yakiendelea kichwani mwangu, kumbe  hata mwenzangu alikuwa kafanya hivyo hivyo, alkuja kuniambia hivyo,

Mimi kwa kujifanya siogoi, nikasogeza mkono kumshika mwenzangu kama kumpa matumaini, lakini nilishangaa mkono wangu ukisukumwa pembeni, ..hakuna aliyemuangalia mwenzake.

Tukimbie ....hizo ni nafsi zetu japo hazikutoa tamko

*************

‘Hatari...’

Hata kwa mzee mwenyewe...

Hata kwa mzee mwenyewe ilionekana hivyo, kwani yeye alishapewa dhamana ya kuhakikisha huyo jamaa haumizi watu, na alishawathibitishia hilo, na mara kwa mara ikitokea jamaa kachanganyikiwa watu hukimbia kuja kumpa taarifa na yeye kwa haraka huenda kumuwahi!

Hii sasa ni hatari.....’ alisema mzee akiangalia upande kulipokuweo kabati
Ilikuwa neno la mzee, na kauli hiyo, ilitufanya sasa tuone kumbe kutaka kukimbia kwetu ni halali...nikainua mguu na mwenzangu akawa keshaanza kuvuta hatua, ni ile hali ya mtu kutaka kukimbia ukiwa bado umekaa...

‘Kwahiyo...’nikauliza na.....

Niliona kitu cha ajabu....

Yule mzee kuona vile, akasimama kwa haraka, akasogea kwenye kabati,, akatoa kitu kama kichupa kidogo, akamimina kitu mkononi, na kwa haraka akamuendea jamaa ambaye kwa muda huo, alikuwa keshalikamata panga, akiwa kalishikilia barabara mkononi, kama vile hataki limtoke,...

Yess....here is my weapon....sasa mtaniambia....’akasema kwa sauti

Ni wakati sasa anageuka, mzee, akarusha kitu kama unga usoni kwa huyo jamaa, na ule unga ilimuingia barabara huyu jamaa usoni, tuliona akihangaika kujifuta na kupepesa macho....

‘Shiiit.....’akasema

Yule jamaa ule unga, ulimkuta kama kushitukiza,.....alishitukia kitu kinamwagiwa usoni, na wakati anataka kujifuta na macho yakimuwasha,.. na kabla hajaamua kufanya alichokuwa amepanga kukifanya mara akaanza kuyumba, mara mbili na ya tatu akadondoka chini,

Na haikuchukua muda  mara akanza kukoroma...

Ikawa ndio salama yetu

‘Oh, mzee hii ilikuwa ni balaa,....’nikasema

‘Hatari....’akasema akiwa kalishikilia lile panga mkononi..

‘Sasa mzee lifiche hilo panga mbali kabisa...’alikuwa rafiki yangu tuliyeongezana naye

Tuendelee na kisa chetu

*************

‘Haya ndio maisha niliyo nayo kwasasa, akiwa hapa nyumbani nakuwa na ahueni maana naweza kumdhibiti kihivyo, hanipi shida...., nina silaha nyingi za kumuweza, na zote ni dawa za kienyeji...’akasema huyo mzee

‘Dawa za kienyeji, umetengeneza mwenyewe...kwanini asipelekwe hospitalini ?’ akauliza mwenzangu.

‘Huyu jamaa kweli alitakiwa kuwekwa hospitali maalumu ya watu kama yeye, wenye matatizo ya akili, lakini mimi nikaenda kumtoa,ili niwe naye karibu, .....’akasema mzee

‘Kwanini sasa mzee, huoni hii sasa ni hatari, akishika hilo panga anaweza kuuumiza hata kuua..?’ tukauliza

‘Unajua kama umefuatilia kisa hiki vyema huna haja ya kuniuliza hilo swali....kwanini nikaamua kumchukua niwe naye karibu...’akasema na akawa kama anawaza jambo kwa makini....

‘Mimi nilimchukua huyu mgonjwa nikijua nitaweza kumdhibiti,...lakini pia nilitaka kujua asili ya tatizo huenda nikalimaliza mimi mwenyewe maana ninazo dawa za matatizo ya akili, ila unatakiwa uwe karibu na mgonjwa, umfahamu muda tatizo linapoanza....na je ni la kimaumbile au kuna sababu nyingine...’akasema

‘Kwahiyo kumbe ni mgonjwa wako, yupo kwenye uchunguzi na uangalizi wako, ...’tukasema

‘Wakati nataka kumchukua kule hospitalini, walinikatalia kabisa, nikawaambia mimi namfahamu sana huyu mgonjwa, na nafahamu aina ya tiba yake, kwa muda huo nilijua ni tatizo dogo tu, nitakuja kulimaliza,....mmh, hata,...sivyo kama nilivyofikiria....’akasema

‘Sasa kwanini hujamrudisha, maana kwa hali kama hii mzee mimi naona utakuja kukatwa mapanga....’tukasema

‘Mimi hilo siliogopi sana, hasa nikiwa naye haa karibu, na dawa zangu zikiwepo, ninachoogoa ni wakati yupo mitaani....nimekuwa nikimfuatilia kila anapokwenda, lakini sasa nimechoka,...watu wanaomfahamu wakiona kachanganyikiwa wanakuja haraka kuniambia....’akasema

‘Mimi wakati namchukua hospitalini walitaka niwahakikishie kuwa kweli nitaweza kumdhibiti, akianza vurugu utafanyaje...’akasema

‘Basi mimi nikawaonyesha majaribio mbele yao, kipindi hicho alishachachamaa kuwa anataka kwenda nyumbani kwake, hashikiki,...nikamtuliza kwa dawa zangu, na kweli kila mara, hali ya jamaa ikibadilika, na kuanza kuleta matatizo,  huwa namtuliza kihivyo, ....’akasema

‘Unajua hata Profesa alikuwa na vipaji vya madawa ya magonjwa mbali mbali, lakini kwa tatizo kama hilo alinyosha mkono, hakuweza kabisa kumsaidia huyu mtu...’akaendelea kusema

‘Profesa??’ nikauliza na mzee akatabasamu na kutikisa kichwa halafu akasema

‘Unajua nimemchunguza sana,..nimeona..sizani kama huu ugonjwa wake una dawa...’akasema huyo mzee

‘Kwahiyo katika uchunguzi wako na kukaa naye umeshafahamu huyu mtu ana ugonjwa gani...?’ nikamuuliza

‘Hahaha..vijana sikilizeni, msije mkajidanganya kwa vyovyote iwavyo, ..’akatulia

‘Mhh,katika maandiko, tunaambiwa, kwanza muabudu mungu wako na pili waheshimu wazazi wako, au sio, ina maana baada ya mungu wa pili ni nani ni mzazi wako, au sio..’akasema

‘Ndio mzee....’tukasema kwa pamoja na rafiki yangu

‘Swali niwaulize, ni nani kasema hivyo....?’akatulia

‘Kusema vipi?’ akauliza mwenzangu

‘Muabudu mungu wako halafu watii wazazi wako wawili....’akasema

‘Ni mwenyezimungu mwenyewe...’nikasema

‘Umeonaeeh....sasa kama mwenyewe aliyetuumba  baada ya kusema tumuabudu yeye, akaja kusema tuwatii , tuwaheshimu wazazi wawili, inakuwaje mtoto, ....wewe uliyezaliwa na wazazi wawili, unakuja kumuhini, mzazi wako, ....’akasema

‘Lakini mzee....’nikataka kusema

‘Hakuna lakini, hakuna sababu,...kwa vyovyote iwavyo, mzazi ni mzazi tu, hutakiwi kumkana, ...kwa vyovyote vile labda huyo mzazi atake wewe usimtii aliyeweka hiyo amri ya kuwa baada ya yeye wanaofuatia ni wazazi wawili..kama atakuambia usimuabudu mungu, usifaye ibada, basi huyo naye ana lake jambo....una haki ya kutokumtii...maana atakupeleka kubaya....’akasema

‘Sasa mzee, maana naona kama hujamaliza kisa chetu hutajaona hiyo sehemu, kwa vipi huyu jamaa aliwakana wazazi wake, ina maana huyu ndiye yule kijana...au?’ nikauliza na mwenzangu ambaye alikuwa akimuangalia yule jamaa akiwa kalala chini akikoroma, akauliza
‘Ina maana tatizo la huyu jamaa, kama tulivyoona kwenye simulizi za nyuma basi linatokana na laana....?’ akauliza na mzee akatabasamu na kusema

‘Sio laana, hiyo sio laana....huyo hajalaaniwa.....’akasema mzee akitikisa kichwa kukataa

‘Sasa tatizo ni nini...kalogwa, au ilikuwaje?’ mwenzangu akauliza

‘Hahaha mimi naona ni vyema tuendee na kisa chetu...’akasema

********

‘Hebu turudi nyuma kidogo...;’ akaanza mzee kuendelea na kisa chetu

  Profesa alipofika pale ilipokuwa nyumba yake..., nia ni kuonana na huyo mumiliki mpya wa hiyo nyumba....’akasema mzee akiendelea na simulizi

‘Unajua kitu kilikuwa chako kikachukuliwa na kitu chenyewe kikiwa ni nyumba, kitu ambacho hakiondosheki, kila ukipita unakiona,..na ukiangalia mazingira ya kuchukuliwa kwake ni kama kunyang’anywa tu, inauma kweli....kwa wengine ni rahisi kusahau, lakini sio watu kama Profesa!

Profesa alikuwa na hamu sana ya kuonana na hao wanaosadikiwa kuwa ni wamiliki halali wa hiyo nyumba, ....yeye wakati anatoka huko ulaya, alijua mumiliki halali atakuwa huko ulaya, akiitumia nyumba hiyo kama kitega uchumi tu labda kwa kukodisha, au kama alikuwa Mtanzania, basi atakuwa kaamua kurejea nchini,...sasa ni nani!

‘Nyumba hiyo siku hizi wanaishi wenyewe...’aliambiwa na jamaa mmoja

Ni siku alipofika mara ya kwanza, na kauli hiyo ilimfanya ajiulize sana, ni akina nani hao,..wamekuja lini, kwahiyo ikamjia hamasa ya kutaka kuwafahamu hao watu kwanza.

‘Huyu mumilikini nani..’alijiuliza sana swali hilo, na kwa vile alikuwa hajakata tamaa, japo kisheria ndivyo ilivyo,ya kuwa nyumba hiyo sio nyumba yake tena, maana alishakubali nyumba iuzwe ili madeni ya watu yawezwe kulipwa, ..tena mbele ya mwanasheria wake.

‘Na hata kama waliuza, pesa yote isingeliishia kwenye hayo madeni, ...hebu bro, fikiria ile nyumba yangu, ingeuzwa shilingi ngapi, eti pesa yote hiyo, iliishia kwenye kulipa madeni, sikupata hata senti moja...’akasema kwa uchungu

‘Wao walichofaya kwa roho mbaya zao, walinibambikia madeni mengine yasiyokuwa yangu, na wakati ule sikuwa na uwezo wa kuyakataa,...ningekataaje wakati nilikuwa kwenye wakati mgumu, na wao walijua nitafia huko...’akasema

‘Sasa bro, nipo nje nataka kulifuatilia hili swala, hatua kwa hatua....’akamwambia kaka yake wakati wanasimuliana

‘Unapoteza muda wako bure, kama uliwahi kuweka sahihi yako, tena mbele ya mwanasheria wako mwenyewe, wewe ulitegemea nini,..hao ndugu yangu umeshaliwa, ....’kaka yake alimwambia

‘Sio kirahisi hivyo, bro, unajua haki nyingine ukinyamaza wajanja, wenye roho mbaya wanazifisidi, mimi sikubali kirahisi, nitadai hadi naingizwa kaburini...wao si wanajua nimeshakufa, sasa mzuka wa Profesa utawaandama,...Wewe subiria utaona vumbi langu....’akasema

‘Haya bwana, lakini usije kuniletea matatizo, haya niliyo nayo ni manzito,....yananishinda, ...’akasema kaka mtu

‘Wewe wala usijali,...mimi nitapambana na huyo aliyeinunua.....’akasema

‘Mama mtemi au nani?’ akaulizwa

‘Huyo aliyenunua hiyo nyumba, si anajifanya ana pesa, sasa atajuta kwanini aliinunua hiyo nyumba....’akasema

‘Utafanya nini wewe wakati umejiishia,....?’ kaka yake alimuliza kwa dharau

‘Wewe subiria tu, sitajali yeye ni nani,  nitapambana naye...kwa udi na uvumba..., nyumba hiyo nitaigeuza jinamizi, kila atakayeichukua ashindwe kuishia, labda awe mwendawazimu....!’akasema

‘Samani mzee, nikurudishe nyuma kidogo, ulisema kuonana na hao wanaosaidikiwa una maana gani....?’ akauliza mwenzangu

‘Maana Profesa wakati anafika hapo hakuwa na uhakika, wa kikamilifu kuwa wanaoishi hapo ndio wamiliki halali wa hiyi nyumba,  yeye alijua watu wanaongea tu,kama ilivyo watu wengine kuongea jambo bila ya uhakika,..

Yeye kwa vile anafahamu ukweli halisi, aliwasikiliza tu , lakini moyoni alikuwa akifahami undani wa hiyo nyumba, na hakutaka kuwaelezea kuwa yeye ndiye aliyeiuza hiyo nyumba kwa kulipia madeni,

‘Profesa alikuwa anafahamu kuwa wamiliki halali anaishi ulaya,kutokana na maelezo aliyokuwa kayapata kutoka kwa wakili wake...’akasema mzee

‘Walionunua walikuwa ni Watanzania, su sio, kwahiyo...huenda walikuwa wamerejea...au sio..?’ akasema jamaa yangu

‘Mhhh....huenda, ngoja tuone....’akaguna mzee

*********

‘Kwani kuna tatizo gani....’ Hii ndio sauti iliyomvunja kabisa nguvu profesa, ni sauti anayoifahamu sana, ni sauti ambayo hata akiwa usingizini angeliweza ni nani kaitamka..
Japokuwa alishamuona huyo mwanadada wa kizungu, na jaokuwa hadi anaondoka huko, alikuwa hajawa na uhakika kama wawili hao walishakubaliwa kuoana,....

‘Ni kiindi kilipita, na ukumbuke kipindi kingi, wakati kijana wao ana urafiki na huyo mwanadada, ndicho kipindi walikuwa hawaivani, na hakuwa anafahamu maendelea yao, alikuwa akisikia kwa watu tu.

Kwahiyo aliomuona huyo mwanadada wa kizungu, ndio kwa akili ya haraka ingeliweza kusema watakuwa na kijana wake, lakini yeye akili yake haikumtuma hivyo, alijua huyo mdada alikuwa kaja kwa matembezi tu,...

Huenda huyo mwanadada alifika kwenye likizo, akaja kwa wamiliki wa nyumba hiyo nyumba labda wanafahamiana, na kwa vile wanafahamiana hakuona ubaya kuja kuishi nao mpaka likizo yake iishe, huenda walikodisha, huenda....

Sasa ilipotokea hiyo sauti mlangoni, ikawa kama kitu kimemgonga kichwani, kimechuma kisu kwenye moyo wake, na hao akili haikutaka kuendelea na hizo huenda, ikajikuta ikiishiwa nguvu, na ....akahisi kichwa kikiuma, akahisi mwili ukiisha nguvu na mara giza likatanda usoni akazama kwenye giza.,,,

*************

Who is this man...., a ghost!’ ni sauti aliyoisikia kama ndoto, kabla ya kuzama kabisa kwenye giza, hadi alipozindukana na kujikuta kalala kwenye kitanda, na akili ilipotulia zaidi na pua kuakisi harufu, akajua kumbe yupo hospitalini.

‘Nimefikaje hapa?’ akajiuliza na mara akahisi watu wakiwa karibu yake

‘Kazindukana...’sauti ikasema

‘Ndio...’sauti nyingine ikasema

‘Tunaweza kuongea naye..?’ sauti nyingine ikauliza

‘Kwahivi sasa haiwezekani,..ngojeni apumzike, huyu mtu ana shinikizo la damu,, na hali hiyo imemjia baada ya kupata au kuona kitu cha kumshtua...’akasema docta

‘Lakini sizani kama kaona kitu kama hicho, maana mimi ananifahamu, kama ndio yeye, na mume wangu anamfahamu sana..kama huyu mtu ndiye huyo tunayemfahamu sis...’sauti ya kike ikasema

‘Kama nyie mnasema mlipomuona mlishituka sana, huenda hata yeye ilikuwa hivyo hivyo..’sauti ikasema ambayo profesa alikuja kufahamu kuwa sauti hiyo ilikuwa ni ya dakitari

‘Unajua docta kama huyu mtu ndio yeye ambaye tunamfahamu sisi, ....basi atakuwa kafufuka, maana huyo mtu tuliambiwa alishafariki,...kwa hali aliyotoka nayo huko, ilikuwa sio ya kuishi tena...’akasema

‘Kwanini, kwani alikuwa akiumwa nini...?’ sauti ikauliza

‘Magonjwa ambayo asingeliweza kupona...’sauti ikasema

‘Na alishafikia kipindi hajiwezi...’sauti nyingine ikaendeleza

‘Labda alipofika huku alipata matibabu muafaka, ndio maana hali yake ikarejea vyema, kuumwa sio kufa...’sauti ikasema

‘Docta, unazungumzia ulaya,...unafahamu kabisa huko ulaya matibabu yake nii ya uhakika, na huko ndipo walisema uhai wake hautazidi hata mwezi, ...na sio mwezi tu, waliomleta huku walisema siku walipomfikisha hapa nchini, alikuwa hajiwezi kutokana na maradhi aliyokuwa nayo, na alipofikishwa hoaitalini, alishafikia hatua ya kukata roho...’sauti ikasema.

‘Kwahiyo hawakuwa na uhakika kuwa alikufa...alikata roho,....?’ sauti ikauliza

‘Kwa hali aliyokuwa nayo docta, ....asingeliweza kuishi, na wanasema walipiga simu huku kuwa na uhakika wakaambiwa keshafariki....’sauti ikasema

‘Ila kiukweli mpaka sasa hatuna uhakika kuwa mtu mwenyewe ndio huyu, huenda wanafanana tu...’sauti nyingine ikasema

‘Kwa jinsi ninavyomfahamu huyo mtu, ....labda kama alikuwa na pacha wake, ndio huyu huyu....’sauti ikasema

‘Ndio yeye...una uhakika mume wangu..?’sauti nyingine ikasema

‘Ndio maana nasema labda kama alikuwa na pacha wake....maana kila kitu ni yule yule....’sauti ikasema

‘Hapa ingeliwezekana , . kama ungelikuwa na mahusiano mazuri na jamaa zake ingelifaa 
uwapigie simu, ili wajue kama jamaa yao yupo hapa....’ilikuwa sauti ya kike

‘Hili tulilolifanya linatosha, kama hawana shukurani shauri lao, hivi nani angjitolea kiasi hiki cha pesa, kwa watu ambao hawamuhusu, gharama yote hii tuliyolipa....docta kama hakuna zaidi sisi tunaweza kuondoka,...’sauti ya kiume ikasema

‘Sawa, ni uamuzi wenu tu, kwa vile mumeshalipia kila kitu, na hakuna zaidi ya hapa, gharama za kitanda mumeshalipia, labda kama atazidiwa tena....’akasema docta

‘Basi utanipigia simu, kadi yangu hii hapa..’sauti ya kiume ikasema

‘Mume wangu,lakini  kama ni yule jamaa yako, haifai kuondoka mapema hivi, ni bora tukasubiria kidogo, ili tuwe na uhakika na kwanini alikuja nyumbani....’sauti ya kike

‘Ya nini kusubiria, huenda alikuja hapo kwa shari,hawa watu sio wazuri, unajua niliwauliza walinzi,wakati tunamtoa huyu mgonjwa nje,wanasema huyu mtu alipofika aliulizia mumiliki wa nyumba, na kuna kauli alitoa kuwa..nyumba ilikuwa ni yake.....sasa vitu kama hivyo vinanipa mashaka,....’sauti ikasema

‘Nyumba yake kwa vipi,...basi ni tapeli, ....’akasema mke mtu

‘Kwani nyumba mnayoishi ilikuwa sio yenu awali?’ sauti ikauliza

‘Docta hawa watu ni matepeli,....achana naye,....hata kama ilikuwa sio yetu awali, lakini tulinunua kihalali...na kama .huyu mtu ilikuwa ni yake, kwanini aliuza, alitarajia nini, ....mimi nimeshaanza kumuhisi vibaya, simtaki kabisa akanyage tena pale nyumbani..tumemsaidia tu kiubinadamu,..’sauti ikasema

Na wakati wanaendelea kuongea docta yeye akaondoka, na maongezi yao yakawa yanaleta sauti za kutokukubaliana, na mara ......

‘Haya jamani hapa ni hospitalini kama mna maongezi zaidi mkaongelee nje sio humu ndani..’sauti nyingine ikasema

‘Samahani nesi, sisi tunaondoka...tumeshaongea na docta, kama kuna zaidi tutawasiliana kwenye simu....’wakasema na mara kukawa kimia

Profesa alipoona kupo kimia ndipo akajiinua ....japo kichwa kilikuwa kizito, lakini aliweza kuinuka, akajiinua kitandani na kukaa, ...alitulia kwa muda akijipima kama you bara bara, wakati huo mpira wa maji aliowekewa ulikuwa umeshatolewa,....

Akaangaza huku na kule , akaona hakuna watu zaidi ya mgonjwa mwingine ambaye alikuwa kalala,...akaangalia pembeni ya kitanda, akaona ule mkoba wake wa dawa, kumbe waliamua kuuleta na huo mkoba wake na  kuuweka hapo..

‘Afadhali wamenirudishia dawa zangu, wangelijua kuwa dawa hizi sina thamani kubwa wasingeziitelekeza hapa, lakini baado kama , kama ni yeye, hahaha, labda mimi sio 
Profesa...’akasema akiupekua  huo mkoba wake, na alipoona kila kitu kipo sawa akageuka kushoto na kulia, akaona hakuna mtu akasogelea mlango, akaufungua, na alipoona nje hakuna dalili ya mtu anayemtizama akaanza kutembea kuelekea mlango wa geti la kutokea...

‘Wewe unakwenda wapi....’alisikia sauti nyumba yake, lakini hakugeuka!

WAZO LA LEO:Ubinadamu na utu wema ni, kusaidiana bila kuangalia huyu ni nani, kama umeona mtu anastahiki kusaidiwa na wewe una uwezo wa kufanya hivyo, toa msaada huo kwa moyo mmoja maana hicho utoacho ndicho chako, hiyo ni moja ya akiba yako siku ya malipo. ...

Wengi wetu wenye mamlaka au uwezo, hutoa msaada kwa ria, kwa kujionyesha, au kwa kutarajia kupata badala, ...na wengine hawatoi mpaka wajitangaze kwa watu, hii inaonyesha kuwa nia yao ni kujionyesha, kuwa wanacho,kuwa wamesaidia...je huoni kuwa kwa yule unayemsaidia inaweza kumuumiza moyo, kuwa yeye hana, yeye ni wa kusaidiwa tu...moyoni atajisikia vibaya, Tukumbuke kutoa, kusaidia, kwenye shida, ni moyo,na sio utajiri ,...
Ni mimi: emu-three

No comments :