Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Monday, October 5, 2015

RADHI YA WAZAZI-46




What the hell,... Who is this man..?’ Mwanadada wa kizungu aliyekuwa kashikilia gilasi ya maji ilidondoka mkononi, akawa katoa macho ya uwoga, akiwa haamini anachokiona mbele yake....

Profesa akiwa kaduwaa baada ya kumuona huyo mwanadada wa kizungu vyema usoni, akiwa haamini kuwa ni kweli kwa aliyemuona, maana sura za wazungu nyingine ni kama zinafanana kama hujawazoea vyema, lakini kwa profesa aliyeishi huko, anawafahamu vyema, lakini pia kwa akili za kibinadamu kama hujawekea jambo maanani kichwani, unaweza usiwe makini nalo...

Profesa hakutarajia kabisa kuwa mwenye nyumba hiyo anaweza kuwa ni mtu anayemfahamu, hakutarajia kabisa na haikuwa kichwani mwake, ndio maana alipomuona huyo mwanadada mwanzoni, japo kuna kitu kama hisia ilimjia akihisi ni kama vile aliwahi kuiona hiyo sura mahali,...lakini akili haikukubali kwa haraka,....sasa kamuona kwa usawa wake, wameangaliana, mshituko ...

Profesa alitulia, akipumua taratibu akiogopa kupandisha shinikizo la damu japo kwa hatua hiyo tayari athari zilishajitokeza....ukiwa na shinikizo la damu kitu kidogo tu kinaleta kimuhe muhe kwenye mzunguko wa damu...

Na kabla hajatulia vyema, maana huenda,...huyo mwanadada alialikwa tu na wenye nyumba, au huenda alikuja likizo, akaja kukaa hapo kwa wenye nyumba kwa vile wanafahamiana au kwa vile ...akiwa a hizo huenda nyingi, akijipa matumaini,....mara akasikia sauti, ikisema;;

‘Kwani kuna tatizo gani....’

Ni sauti hii ndiyo iliyomvunja nguvu, ni sauti hii iliyomfanya hata zile juhudi zake za kujipa moyo zikashindwa kuhimili,....akahisi kichwa kikiuma, akahisi mwili ukiisha nguvu na mara giza likatanda usoni akazama kwenye giza....

Tuendelee na kisa chetu

***********

‘Ina maana mpaka unafika hapo hukuwa umesikia au kufahamu wamiliki wa hiyo nyumba, iliyokuwa nyumba yako ni akina nani....?’ nikamuuliza kabla hajaendelea.

‘Kiukweli sikuwa na ufahamu huo, hata kaka yangu alikuwa hajui hilo japokuwa alikuwa akifika huku mjini mara kwa mara,...na alikuwa akikutana na watu waliokuwa wakipita kariu na hiyo nyumba,... lakini kwa vile hakuna aliyefikiria hilo,.....hakuna aliyejali

‘Profesa alikuwa mgonjwa kwa muda mrefu, na maswala ya nyumba hayakuwa na maana, maana ugonjwa huo wengi walitarajia kuwa ni wa kumuondoa profesa duniani, hauana dawa.....’akaendelea kusema huyo mzee

‘Kwahiyo hakuna aliyekuwa akijali maswala ya nyumba, nyumba ya nini, ...nyumba ingekuja kuulizwa baadaye watu wakitafuta urithi......’akasema.

‘Lakini mpaka hapo ulikuwa hujawa na uhakika kuwa hao uliowakuta ndio wamiliki au huenda walikodisha, ...?’ akaulizwa

‘Nyie subirini niendee msiwe na kiherehere...na mkumbuke tunamuongelea Profesa...sio mimi, ...mkumbue sana....’akasema akijinyoha kidogo,...

Na wakati mzee anajinyosha, mara yule jamaa aliyekuwa kalala akasimama, ....yule jamaa tuliyemkuta barabarani, akiwa kachanganyikiwa,....

Yule jamaa aliposimama, aligeuka huku na kule kama vile anatafuta kitu,...sisi tulimuangalia mzee kama ataweza kumsaidia huyo jamaa labda ana njaa...lakini mzee alikaa kimia tu, akiwa na yeye anamuangalia

Baadaye huyo jamaa akatulia, akageuza kichwa taratibu hadi pale walipokaa hao wageni, akawaangalia kwa makini halafu akasema;

‘Unajua dunia niwaambie kitu....’akasogea karibu na walipokaa hao watu

‘Hii dunia hii....’akawa anaonyesha kama kuzungusha duara

‘Hii dunia ni mviringo sio...huku mwanzo unakwenda huku mwisho... ni kama nyumba tu, huku ukuta na huku ukuta ni mfano, tunachukulia hivyo, si tunapenda kila kitu kwa mfani ili tuelewe...

‘Wewe na mimi  kama mwanadamu unatoka ukuta huu kwenda upande mwingine wa nyumba, hujui kabisa kuwa upande huo unaokwenda una mwisho,... utafika sehemu utagota, hakuna kuendelea na mbaya zaidi huwezi kurudi ulipotoka, yaani kila unapokwenda nyuma kunazibwa. .....’akatabasamu

‘Nyie watu, mnamjua mungu...?’ akauliza na kutulia, na huyo mzee ndiye aliyetusaidia hakujibu swali ila alisema;

‘Hawa ni wageni, msomi, unatakiwa uwasabahi. Kwanza, ukawafahamu ni akina nani, hawa ni wageni wako....’akaambiwa

‘Wageni...haaaa, nani asiye  mgeni.....’akashika kidevu kama anashangaa au kutafakari

‘Kila mtu ni mgeni katika hii dunia..na hakuna aliye mwenyeji katika hii dunia, ..sisi sote ni wageni na wasafiri,tulipotoka hatupajui, au nani anayejua katoka wapi,..?’ akasema na kuuliza

‘Kwa kujipa tumaini, tutasema tumetoka ndani ya tumbo la mama...sasa na huko kwenye tumbo la mama ulifikaje, utasema ni kutokana na makutano ya mbegu ya mume na yai la mama, ...tunajipa matumaini hayo....’akawa kama anatafakari kama kutuacha tuelewe anachokiongea

‘Sasa niwaulize,....na hizo mbegu na yai zilitoka wapi......utafika sehemu utajua kuwa hata ulipotoka hupajui.....’akatulia,

‘Kweli si kweli....?’ akawa natuangalia akitarajia labda tumjibu, lakini sisi tulikaa kimia

‘Kwahiyo basi sote hatujui tumetoka wapi,  huo ndio ukweli....

‘ukweli ni kuwa sisi tumejikuta tupo duniani, hahahaha,

‘Tupo duniani bwana, ....hapa kila mtu anajifanya mjanja, anajiona kafika, ...wengine wanamiliki majumba, wanajenga magorofa makubwa,...wanaendesha magari ya kifahari.....wanatawala, wanajiona wao ni .....hahaha

‘Ni maraisii watarajiwa, si mnawaoa wakimwaga sera, mimi nikichaguliwa, nitakuwa....nitafanya...wewe....unajua kesho ilivyo wewe...hakuna hata mmoja anayesema, mimi mungu akijalia...hakuna,..kwanini,...kiburi....

‘Unajua niwaambie kitu..., jana nilifika ofisi fulai..., eti naambiwa kumuona bosi mpaka niwe na miadi naye, niandike kwenye dafutari, ili nipangiwe siku ya kumuona...huyu naye kawa adimu, hajui...hajui kabisa kuwa yeye ni kama mimi tu...

‘Huyo bosi,....hajuii kabisa siku itafika...sio mimi wala yeye, ataondoka tu....anajiona yeye ni tofauti..anadharau wenzake, anatuona tunanuka, ananiona mimi ni punguani.....hajijui tu, kuwa yeye ndio kapungukiwa na ufahamu, huyo angelijua, angeliwanyenyekea wanadamu wenzake...

‘Kwahiyo, hakuna anayejua wapi alipotoka, ...na hapa tulipo sote ni wageni, na tungelijua,....nawaambia hili, tungelijua, tungelikuwa na ufahamu,angalai kidogo tu ....hahaha, tusingehangaika saana,tungelilambana miguuu kutafuta fadhila ....lakini wapii,,.....hahahah...unaniona mimi, eti watu wananiita kichaa, ....’akageuka kumuangalia huyo mzee

‘Eti mzee, mimi ni kichaa....?’ akauliza halafu akawa anajikuna kichwa kama kinawasha na yule mzee akasema

‘Wewe sio kichaa tu, bali wewe ni kichaa msomi....’akasema huyo mzee

‘Msomi eeh,...msomi...mimi ni msomi eeh...tena kichaa, kichaa ni nini....kichaa! .....’akatulia akiwaza

‘Kichaa eeh, punguani, hahaha, unajua mzee sisi sote ni vichaa na punguani,....nikuambie kwanini...angalia tunavyoangaika na dunia,...matendo yetu,...yapime kama sisi sisi sote sio vichaa, punguani.....’akatulia

‘Hivi niwaulize, haya yote ya dunia tunayohangaikia mwisho wake ni nini, umesoma, umeata kazi, ...utajiri, mwisho wake ni nini, utaishia wapi,...utakwenda wapi....?’ akatuangalia kwa makini kama anahitajia jibu kutoka kwetu...

‘Hebu nambieni, utakwenda wapi, hivi mtu mwenye akili atahangaika wee, akijua mwisho wa siku, vyote alivyovihangaika hatavifaidi,....una kazi nzuri una nyumba nzuri,....lakini utakwenda navyo...utaviacha, hivi wewe una akili...?’ akawa kama anauliza

‘Halafu unaniita mimi kichaa, kichaa ni nyie...mama sasa nakula , nalala, popote nakula ...popote nalala...nina shida gani, sihangaiki tena.....halafu unaniita kichaa....hahaha...’akacheka wee hadi anataka kuanguka.

‘Mimi nawachukia sana hao wanajoiita mabosi,....wanajifanya wamefika, eti wanaongea lugha ya wageni, bosi, unawadharau wenzako bosi, ...hata mtu akija kwako, unajisikia, I am a bos, I am a director, ...whatever ...na wakati mwingine wengine wanaona hata kinyaa kujiwa na wageni kama mimi,...hahaha, hahahaha.....’akatembea hatua mbili mbele kama wanavyofanya mwalimu darasani

‘Sasa umepata kazi una maisha mazuri, ....utataka nini tena,...eeh, utaoa, au utaoelewa,...au sio, ndio maisha hayo, lazima ukamilike,..baadaye nini tena...utazaa watoto, au sio..baadaye nini tena,...utakuwa mtu mzima, au sio..utakuja kuitwa baba, halafu ...hahahah, unaitwa mzee kama wewe, ...wanakuita mzee.au sio......ni lazima,  kama umejaliwa, ....hahahaha, usiogope, mimi na wewe, ni lazima tufikia huko....kuitwa nani....wazee...

‘Wapendeni wazee wenu...msije kuwa kama mimi...’hapa akatulia akiwa kama anatafakari kitu

‘Ukishafikia uzee, na wengine hawafikii huko, unakwenda wapi,...nawauliza nyie watu, unakwenda wapi...tusiogoe kusema maana ni lazima, .....’akatulia kama anawaza jambo

‘Kumbuka nilipoanza nilisema dunia ni nini, ni kama nyumba, sasa sisi tutafika mwisho wa nyumba,....huko kuna nini, kuna ukuta hujui nyuma ya ukuta ulipotoka kupoje, kumeshaziba wewe hujui tu, na huku nyuma huwezi kurudi tena,... na mbele umefika mwisho wa ukuta, hujui pa kwenda, hapo sasa unamkuta yule aliyetumwa.....hahahahaha wanaogoa hao....’akacheka huku anaruka ruka.

‘Unamfahamu huyo,utakayemkuta hapo, mwisho wa ukuta  yeye muda wote you anakusubiria,...anajua lazima utamfikia...mimi simtaji, maana hata mimi namuogopa....kweli namuogoa ndio maana nikifika barabarani naangalia kushoto na kulia...’akasema na kutulia

‘Watu wanaogopa...hahahaha, msiogope, maana huyo ni lazima ukutane naye, uwe kijana au mzee, kama safari yako imefika, utamkuta..yupo, anakusubiria, hana wasiwasi, anajua ipo siku utafika tu, utafika kwenye anga zake, mwisho wa ukuta,, na hapo hapotezi muda,...hahahahahaha...’hapo alicheka sana, mpaka akaanguka chini akatulia muda mrefu kweli,

Kwa muda alitulia,sisi tulijua kalala,....na tulitaka mzee aendelee na story yake,kumbe...mara akatikisika kama anataka kuamuka, halafu akarudi kukaa kimia...

Yule mzee akatikisa kichwa, akasema;

‘Ndio hivyo,....akianza kuongea hapo, ni bora mumsikilize tu, ole wako umjibu, ole wake ubishane naye...dawa ni kukaa kimia, maana akiongea sauti za watu zinakuwa kama zinamkera,...na usipomsikiliza ukamdharau na kuondoka ...unakuwa ni adui wake..hugeuka kuwa mbogo,....’akasema mzee

‘Sasa mzee kwa hali hii mnaishije naye....?’ nikamuuliza

‘Hivyo hivyo, leo naona kimecharuka, kuna kipindi anakuwa mtu safi kabisa, lakini hali ikibadilika,....mmh,n hapo ndio kaanza na bora tuwe kimia tumsikilize hadi hapo atakapomaliza ...’akasema huyo mzee

‘Tusubiria, ataamuka muda sio mrefu, ....ataongea wee, atafikia kutukana, na hata kupiga wakati mwingine....., kwahiyo tunaomfahamu akianza kuongea hivyo, tunamsikiliza wee, hatusemi neno maka achoke,.....’akasema huyo mzee

Na ghafla huyu jamaa akasimama kwa haraka, kama vile kapewa amri, akasimama na kuangalia mbele kwa muda , halafu akasema;

‘Tuliishia wapi vile....kwanza niliwaambia dunia  ni nini,...?’ akauliza na kabla hatujasema kitu akasema

‘Dunia ni duara, lakini mimi nimeitolea mfano, kuwa dunia tuione kama nyumba,..au sio, sisi ni wageni tumefika kwenye hiyo nyumba tukaingia ndani, ....ni wageni tu....tulipotoka hatupajui, na muda wa kuishi kwenye hiyo nyumba hatujui, tumekaribishwa tu,.na nani hatujui...lakini ni lazima tuondoke, .tutaondoka tu..., tupende tusipende....mimi na wewe na yule, yoyote hata awe nani atandoka tu, utabakia hao kwani kwako, ...kwani wenzako hawataki kuja kukaa hapo, utasema umewahi hahaha, hujawahi, utaondoka tu....’akatulia

‘Sasa ndugu zanguni, swali ni hili,....kama tunajua kuwa sisi ni wasafiri, ...akumbuka ule wimbo mmoja, unasemaje mzee....wewe wa siku nyingi bwana, unaujua, unaimbaje vile...?’ akawa kama anamuuliza huyo mzee, na mzee akawa kimia tu..

‘Hawa wazee bwana......’akawa kama anafikiria halafu akaanza kuimba;

‘Mimi ni msafiri bado nipo njiani, sijui lini nitafikaaaeeh...ninajiuliza wapi ninapokwenda ,najua bado ni mbali......hahaha,....’ akarudia tena kuimba hivyo, halafu akasema

‘Wewe, mimi, yule na wao, sote ni nani.....wasafiri...na kilamtu anahisi, kuwa tuendao bado ni mbali, lakini hujui, hatujui...unahisi na unajipa moyo tu...bado bado...hivi kweli bado, jana yule kaondoka, leo huyu..kesho naweza kuwa mimi.....hahaha, halafu mnaniita kichaa, kichaa ni nyie....

‘Hebu naambieni,  mtoto anazaliwa leo anakufa...si mnajua kufa ni uzee, ni kuumwa, hebu niulize mtoto, hajaumwa, hajazeeka, kazaliwa, kakaa siku , mwezi, kaondoka,.... kijana anakufa, alijua ni badooo...mtu mnzima anakufa, alijua bado, tunajipa moyo kuwa mzee ndiye wa kufa , eti mzee, kweli si kweli....sijui lini nitafikaeee,...’akatulia alipoimba maneno hayo ya mwisho

‘Jiulize huko unapokwenda unakwenda wapi....maana mwisho wa yote haya ni kaburi..hakuna anayelipinga hilo,...ufanye ufanyalo, uringe uringavyo...utape utapapo...udhulumu, uwe mtenda haki, lakini mwisho wa yote ni kifoooo....’akatulia

‘Nani hatakufa? Eeh, nani hatakufa?, ..hakuna, jana, juzi, tumezika, au sio, unafikiri wao walikuwa hawapendi kuishi...walitarajia kuishi....kuishi hadi kufikia ndoto yao..lakini wapi....nawasikitikia hao mabosi waliopo maofisini, kila siku kuwahadaa wafanyakazi wao,.wadhulumaji wakubwa hao.....eti ukienda mpaka upitie getini, uwe na miadi ya kumuona bosi,..wewe bosi wewe,...’akawa ananyosha kidole

‘Eti bosi, huna lolote wewe...., wewe ni maiti mtarajiwa tu...hahahha....tutaona, kama kweli wewe ni bosi,...kuwa wewe utaishi milele....’hapo akatulia

‘Mimi nilikuwa bosi...nimeishi ulaya,....si sawa mzee...?’ akageuka kumuangalia mzee

‘Mimi nimesomea ulaya, nikafanyakazi ulaya, nilipata kazi ulaya,muulizeni huyo mzee...mimi ni msomi,....’akatulia

‘Nina kila sababu ya kujiita msomi,... maana hapa kwenu, ukijua kiiingereza kama mimi ..sio huko ulaya, hapana, ....ni hapa kweny, huku mnamuoa ni msomi, ni yule anayejua kiingereza, kama hujui kiingereza basi wewe sio msomi, kweli si kweli?.....

‘Hata kama wewe fundi, uajua saana, au uwe nani ...uwe nani, kama kiingereza hakipandi, hujawa msomi, ....mimi hapa najua kiingereza kweli kweli,....najua hesabu kweli kweli, ....najua najua komputa hakuna anayenishinda,....sasa nipo wapi....’hapo akatulia,...

‘Sasa nipo wapi wajamani......sasa nipo wapi, kipo wapi...mmh, nipo wapi jamini, sijijui, sijui..nisaidieni, niambieni nipo wapi.....’akaanza kulia, na hata kufuta machozi...
Alikuwa analia kiukweli,..hadi machozi yanamtoka, na sisi hatukujua kabisa tufanye nini, tulitajia mzee atafanya jambo, lakini mzee alikuwa kajiinamia, na sis tukaona bora tukae kimia...

‘Sasa nipo wapi....nipo wapi, kipo wapi.....yote, hayo yapo wapi....’akachuchumaa na kuendelea kulia, halafu akainuka na kumuendea mzee, akamuangalia huku akiendelea kulia

‘Mzee, wewe ...unajua eeh,...nyumba hii hapa...si unaitaka,...eeh, nzuri eeh, sasa niambie kitu kimoja, nisaidie kuniambia,...mimi nipo wapi....halafu ...eeh, nyumba yote hii yako...dunia hii yako...si mnataka kuishi milele.....eeh, subutu,....nani ataishi milele, lakini mnisaidie kitu...mimi ...nipo wapi....’akasema akimuangalia mzee

Mzee akawa kainama chini tu, katulia,...jamaa kuona hivyo akaanza kumsuta suta mzee akimshika mebagani...

‘Mzee, mzee, nauliza mimi.....sasa nipo wapi, ....nipo wapi?’ akamshika mzee mabegani akitulia kumsukuma sukuma, akawa sasa kamuinamia na mzee akatikisa kichwa kama kukataa, hakusema neno huku, kajiinamia, na yule jamaa alipoona hivyo akatugeukia sisi na kutuangalia, akasema

‘Mzee hajui..lakini nyie najua mnafahamu,...si nawaoana tu, mwajifanya mwajua kila kitu au sio, wajanja wa mjini....wajua dili...au sio, sasa mtaniambia mimi nipo wapi...’akawa anatuangalia kwa macho makali.

‘Jamani nipo wapi...mimi nipo wapi...?’ akawa anatusogelea

‘Hamjui.....eeh...’ akashika kichwa na huku analia

‘Jamani nipo wapi,nimepotea, au nipo kati kati ya msitu, kuna majoka, kuna kila aina ya wanyama,au...mbona sijijui...jamani nipo wapi....hakuna anayejua,.....baba, ...’hapoa aktulia kama kakumbuka kitu

Yes, father, where is my dady.....labda baba anajua,....’akasema na sasa akageuka kumuangalia yule mzee

‘Mzee labda baba anajua eeh, ndio...baba ,....anajua, sasa baba yupo wapi....baba, jamani baba ...baba yupo wapi anisaidie kuniambia nipo wapi, mzee baba yupo wapi...’akawa anamuangalia huyo mzee na mzee akawa kimia tu

‘Mzee ....kweli nimekumbuka, mama, where is my momy.... yupo wapi, mama,...mama, hivi kweli mama, mama yangu ni nani, yupoje,... mzee mama yupo wapi....mama,....my momy, usiniache,...don’t leave me....’akageuka huku na kule kama anatafuta kitu

‘Mama upo wapi,...najua mama atajua mimi nipo wapi ....mama, mzee mama.. yupo wapi,, mzee ...mzee,...mama, mama yangu yupo wapi....hapana, yupo yupo tu, mzee mama you wapi..?’ akauliza akimuangalia huyo mzee..

Mzee alitikisa kichwa akionyesha masikitiko, lakini hakusema neno...

‘Ina maana hakuna anayejua,eeh,...hakuna...hakuna....shiiiiiit....’akawa sasa anafoka, akaanza kuangalia huku na kule kama anatafuta kitu,

‘Mimi nauliza mumekaa kimia,...hahahaha, mwaniona mimi nimechanganyikiwa, mimi ni kichaa au sio, punguani....sasa mtaniambia ....’akageuka huku na kule, kama anaendelea kutafuta kitu

‘Wajinga wakubwa nyie, wapuuzi, ....’akawa sasa anatoa matusi makubwa makubwa.....halafu 
akatulia na akaangalia juu akatulia, halafu akasema;

‘Hakuna eeh, ....haiwezekani,...hakuna anayejua kuwa mimi nipo wapi....niliwaambia toka awali, dunia ni kama nyumba au sio....mumeoanaeeh...lakini mbona mimi .....oh....’akatikisa kichwa

‘Mimi nipo wapi, nyie si mnajifanya mumefika..mnajua wapi mlipo,...mabosi,.... sasa na mimi niambieni nipo wapi.....nyie wapuuzi, nawauliza tena mimi nipo wapi, wewe....’akaninyoshea kidole mimi, nikajikuta nashtuka, maana alinishitukizia...

‘Wewe, niambie mimi nipo wapi, ...’mimi nikawa kimia, akaniangalia kwa muda kama anasubiria jibu, halafu akamgeukia mwenzangu naye akamuuliza swali kama hilo

‘Na wewe...niambieni mimi nipo wapi....’ na mwenzangu naye akawa kimia, halafu sasa akawa kakasirika kabisa

‘Mnaninyamazia, mnaniona mimi mjinga au sio...ngoja, nahisi hamnielewi, nawauliza halafu mnakaa kimia....’akasema na kugeuka akiangalia huku na kule kama anatafuta kitu

‘Mwenzangu akanibonyeza na akawa  akaninong’oneza akisema

‘Hapa sasa hakuna usalama, tukimbie....’akaniambia na mimi nikageuka kumuangalia yule mzee,na yule mzee alionekana kuwa na wasiwasi, ...nahisi hata yeye alishahisi kuwa kinachofuata sasa ni hatari, lakini akawa anaogopa kutuambia, na wakati huo jamaa akawa anajikuna kuna kichwa

‘Mzee....tukimbie...?’ mwenzangu akauliza na huyo jamaa akawa anahangaika akijikuna kichwa utafikiri kuna kitu kinamghasi, na mzee akatuonyesha ishara ya kunyamaza.

‘Mkimbie,...hahaha, mkimbie....hatoki mtu hapa,...kwanza kitu gani hicho mnaniingizia kichwani....’akasema na akawa kama anazuia huku na huku ili mtu asipite

‘Ni nani anasema mkimbie..hatoki mtu hapa.mpaka mniambia mimi nipo wapi....’akasema, mimi nilitamani kumwambia you duniani...lakini nikakumbuka kuwa huyo mzee alisema ukiongea sauti zinamkera...

‘Hata baba...yupo wapi,...,au mama,...hawa watu wapo wapi, na wao hamtaki kuniambia wapo wapi....?’ akatuagalia kila mmoja kwa hatua

‘Kwanza mimi siwajui,...hahaha wakafie mbali.huko, who the hell are they......lakini nyie mnaojifanya mnajua ,....nyie, nyie..mnajiona mumefika, mumefika eeh hahaha, mnajidanganya,...kama mumefika, basi niambienii mimi nipo wapi ...?’ akatukodolea macho, na sisi tukawa kimia

You.....mtaniambia,...mimii nipo wai,  la sivyo, ...eeh, ....kitaeleweka....’akawa anageuka huku na kule kutafuta kitu, akaangaza na ghafla akatuliza kichwa alikuwa kaona kitu...
Mimi nikatupa macho kuona hicho alichokiona, na macho yaliotua kwenye kona ya nyumba, nikahisi damuu ikinienda mbio,...mungu wangu,  lilikuwa ni panga lipo kwenye kona ya nyumba,...

Jamaa akaliona na macho yake yakaonekana ya kimeta meta na dalili ya ukatili ikaonekana....

Na Wenzangu wakaliona lile panga.. na mzee naye akaliona nilimuona akishtuka kama kutaka kusimama, ..., na mwenzangu naye alionekana kama kaona kitu cha kutisha, kwani macho yalikuwa yamemtoka pima kwa uwoga,, .........hatari...!

Hatari.... kila mmoja hapo akawa anawaza lake, kwa jicho moja nikaangalia usawa wa mlangoni,....nikijua hao hakuna kuulizana tena,  najua hata mwenzangu alikuwa na wazo hilo hilo....

‘Eheee,...sasa mtaniambia ....mimi nipo wapi,...who the hell are you anyway, who the hell  are you...’akasema

‘After all, mumefuata nini hapa nyumbani kwangu... mna msaada gani kwangu.....sina baba, sina mama, sina ndugu....who the hell.are they...ni nani wao kwanza, ..siwajui, ...siwajui...who the hell, ....kwanza mimi nani,.... hakuna anayejua, nipo wapi, hakuna anayejua...hahaha,.....’akawa sasa analikaribia lile panga

‘Yes, ...yes, ...hii kitu itamaliza shida....mzee umekuwa ukiificha,hili, leo nimeliata,  leo, leo... nimelipata....’hapo akaanza kujikuna kichwa, mfulilizo....huku anainama kulichukua hilo panga...
Hatari....

NB: Naishia hapa, maana inatisha....

WAZO LA LEO: Chuma uchumacho, ringa uringavyo, fanya ufanyacho, lakini siku itafika, uliyempenda, utamuacha, au atakuacha, ulichochuma utakiacha, ubosi, utajiri, majumba ya kifahari, watoto, utaviacha,....ni nini utakwenda nacho kaburini.....sanda, kabari la kifahari....??, kila mmoja ajiulize kwa wakati wake..’haya yote ya dunia nini...hata maandiko yanasema .ni ya kupita tu au sio,? Au ni uupuuzi mtupu tu, au sio??
Ndugu zanguni, tupendane, tusaidianeni.....tusichukiane, eti kwasababu ya siasa, eti kwasababu ya mali, eti kwasababu ya ubosi, uraisi, ubunge nk.....maana haya yote hayana maana kwetu, mwisho utafika vyote hivyo tutaviacha,...walikuwepo, wakawa na sasa hawapo, na wewe utakuwepo, utakuja kuondoka na kusahaulika,..muhimu ni kujiuliza huko unaokwenda, utakwenda na nini,.

Ni wazi kabisa, huko, kinachohitajika ni MATENDO YAKO MEMA,... Sasa kama ni matendo mema, mbona maisha yako yote yamejaa matendo mabaya, uovu, ufisadi...
Ni mimi: emu-three

No comments :