Bro, ndugu
yako nilikuwa marehemu, yaani pale mpaka unachukuliwa kupelekwa hospitali ya
nje ujue wewe ni wa kufa, au huo ugonjwa wako ni mkubwa sana, ujue unapopelekwa
kwenye hilo gereza , ni kwamba umepelekwa hapo ili ukafe, hawasemi hivyo, ila
inajulikana hivyo!
Kwahiyo ukiumwa
hawakuhangaikiii sana, sana sana watakupiga sindani za kuwasha uhangaike mpaka huo
ugonjwa ukimbie,, la sivyo, utapoteza fahamu, ikiamuaka upo hapo hapo..!
‘Sasa
ikawaje kwako mpaka wewe ukapelekwa hospitalini ya nje..?’ akauliza kaka mtu
‘Siku zangu
zilikuwa hazijafika bro, kwani hali ilikuwa mbaya, mimi mwenyewe nilimuona
malaika mtoa roho akinijia,...nilishaiaga dunia, naona ilipangwa nisife hara
ili nipate muda wa kutubu dhambi zangu...’akasema
‘Sasa
umetubu hizo dhambi zako, wewe uwadhulumu watu haki yao, uwasumbue, uwabie
mpaka kufikia watu kufa, halafu useme utatubu, unaweza kutubu kweli dhambi ya
mtu, uliyemdhulumu, kama hujaweza kumrejeshea haki yake,...au unajidanganya tu?’
akaulizwa
‘Ohh,
bro...nimetubu sana, na kama ni adhabu hiyo niliyoipata imelipia hizo
dhambi,sijawahi kumfanyia mtu ubaya kiasi hicho,..kama nimeweza kuwalipa watu
madeni yao,...mimi naona nimeimiza hayo, japokuwa sikuwa na jinsi, ...
'Bro kama nyumba
imeuzwa , wakasema wanalipia madeni ya hao watu, sasa kama hawakulipia hayo
madeni wakajali matumbo yao, hilo sasa, ni juu yao, mungu anajua ..’akasema
‘Ina maana kweli nyumba imekwenda, lile jumba la kisasa limeuzwa...iliuzwa na pesa wakachukua,..kweli wewe huna maana, unaona ilivyo, ubinafsi wenu umewaponza mungetushirikisha tukajua jinsi ya kuwasaidia, japo hatuna pesa....'akasema kaka mtu
'Lakini mbona sielewi, wao wapo
ulaya na nyumba ipo huku,waliwezaje kuyafanya hayo?’ akaulizwa
‘Nyumba Imekwenda bro, imeniuma kweli,....,
vinginevyo wangenitafuna nyama yangu...na hilo kwao ni rahisi unajua kuna
madalali wa kimataifa, wanawasaliana, na kwa vile hilo liliwekwa kisheria
zaidi, halikuwa na matatizo....’akasema
‘Lakini hata
kama imeuzwa, wewe kama wewe ilikusaidia nini, maana hukutolewa hapo kwenye gereza la kifo,
au...., au ilikuwaje....na hivi kijana wetu ilikuwaje, maana sioni ukimtaja
taja tena...?’akauliza kaka mtu.
‘Ngoja
nikusimulia ilivyokuwa....’akasema
Tuendelee na
kisa chetu...
*********
Siku ya kesi nyingine ilipotajwa mimi
nilichukuliwa nikitokea hospitalini,..kama nilivyosema kuwa hali yangu ilikuwa
mbaya sana, nilichukuliwa nikiwa sijitambui,walikuwa wamebeba kama maiti,na
kilichofanya wafanye hivyo labda, nikuwa mimi sikustahili kufungwa hapo baada
ya kubainika kuwa mimi sijau...sasa sijui walipangaje kuwa nikipona nitarudi hukoo
au la...
Niliombea
nisipone haraka...na hata hivyo kwa hali niliyokuwa nayo haikuwa ya kupona
haraka...ila mfungwa ni mfungwa tu,....
Na siku ya
kesi, nilipoambiwa nahitajika kwenda mahakamani, nilijilegeza kweli, lakini
ilikuwa haisaidii kitu, kwani ilibidi nifike mahakamani, labda kesi iahirishwe
tena, kitu ambacho sikupenda kifanyike kwani ilishaahirishwa mara nyingi..
Nilivyokuwa
nimejilegeza nilijuwa kuwa huenda hakimu atanionea huruma kwa hali niliyokuwa
nayo, hata bila kujilegeza, bado nilikuwa na hali mbaya, niilisha nilikonda,
hadi sura ikawa kama sio yangu na kila mmoja aliyeniona akajua huyu anao...
Hutaamini
watu waliponiona baada ya huruma wakasema na bado wewe ulijifanya mjanja,
kuwabughudhi watu na maisha yao,...umeua.....kwani mama mtemi alikuwa kaongoza
kupakazia ubaya kwa kile mtu, propaganda potofu dhidi yangu zilishawafikia watu
wegu...
********
Siku nipo
hospitalini, nikaambiwa wakili wangu amekuja anataka kuonana na mimi,
nilishangaa kusikia hivyo maana muda sasa nimekuwa sionani na huyu mtu kama
ilivyokuwa awali, kama kawaida ya wakili na mteja wake...nimekuwa nikionana
naye ikitajwa siku ya kusikiliza kesi yetu na tunakutana mahakamani tu.
Kuna siku
ilipotajwa kesi na kupigwa kalenda nilitaka kuongea naye, lakini wakili huyo
akasema ana haraka, hawezi kuongea nami, ..na ikiwahivyo, kesi inatajwa, na
waendesha mashitaka wanatoa udhuru fulani, kesi inaahirishwa.
Wakili huyo alijitahidi kulalamika kwa kusema kuwa
waendesha mashitaka wanapoteza muda,hawana ushahidi zaidi juu ya mteja wake
anateseka kifungoni bila kujulikana kosa lake pia anaumwa, lakini kesi
inaahirishwa na kusogezwa mbele...
Ndio siku hiyo nikiwa hospitalini chini ya
ulinzi nikaambiwa wakili anataka kuongea na mimi, na ningesema nini hapo,
nikatulia tu,na wakili akaja akanisalimia, sikumuitikia, alipoona hiyo hali, yeye
akasema;
‘Najua jinsi
gani unavyojisikia,lakini mimi nimejaribu kadri ya uwezo wangu lakini waendesha
mashitaka ndio wamekuwa ni kikwazo,na nisingeliweza kumlazimisha hakimu...lakini
leo nimekuja na suluhisho ...’akaanza kusema na kuniangalia kama nitasema
lolote, lakini sikusemakitu nilikaa kimia.
Wakili
akaendelea kutabasamu akiniangalia akitaka na mimi nifanye hivyo, lakini
sikutaka hata kumuangalia, ni wakili wangu lakini nilishamchukia nilishamuona
wote lengo lao ni moja, ...akatikisa kichwa kama kukubali, kwa niaba yangu,
akasema;
‘Ni kutokana
na hii hali yako imebidi nimuendee hakimu mwenyewe niongee naye kuwa unateseka
bila sababu yoyote, haikuwa kazi rahisi hasa kesi inapokuwa mahakamani, wengi
hawakubali kuongea na mawakili au washitakiwa kwani itaonekana kama kuna kiti
kinachoendelea,...’akatulia
‘Nilitumia
njia ya kisheria, niliandika mombi ambayo nakala ilipitia kwa wakili muendesha
mashitaka, na hapo hakimu akaona kuna jambo muhimu, na hakuwa na kipingamizi
tena, ukumbuke tangia hapo nilishalalamika, na hakimu akawaita waendesha
mashitaka wakaongea,na aliwakemea na
kuwaambia kesi ikitajwa tena hakuna kuahirishwa ...’akatulia
‘Pamoja na
kumuona ,nilikuwa nimejiandaa kwa mapendekezo muhimu sana...ya kuweza
kukusaidia,na nilijua hayoyatakubaliwa tu....’akatulia
‘Sikutaka
kukimbilia swala la wewekubadilishwa gereza, maana hilo nililipigania mpaka nikakata
tamaa,na nilivyosikia walifanya hivyo wakubwa wa huko kwa vile
uliwadanganya,...’akatulia, akitarajia kuwa hapo nitaongea kitu, lakini
nilikuwa vile vile kama mtu aliyepooza viungo.
‘Kiukweli
mapendekezo ambayo tulikuja kuyaona mimi na mama mtemi, na kijana wako ambayo
ndiyo niliyapeleka mbele ya hakimu, niliona yana msingi ,kwa ajili ya
kukusaidia wewe, kwani tumeona kwa hali uliyo nayo ukirudishwa huko gerezani utaenda kufa tu
kwahiyo tukaona tuyapeleke mapendekezo hayo,na mimi japo sikuwa nimeongea na wewe ikabidi niyawakilishe
tu kwa niaba yako..’akasema
‘Nimeyapitisha
kwa niaba yako kwasababu ya hali yako ya kiafya ...’akasema akitoa makaratasi
kwenye makabrasha yake,...mimi nilikuwa nimejiegemeza ukutani kwenye
kitanda,nikiwa sina hamu tena ya maisha...’akasema
‘Sijui wewe
unasemaje...’akasema sasa akiwa ameshayatoa hayo makaratasi yanayoelezea hayo
mapendekezo waliyopeleka kwa hakimu, akawa ananionyesha ili niyasome, lakini
sikugeuka wala kujigeuza nilikaa vile vile, na alipoona hivyo, akayafungua
mweyewe na akawa kama ananisomea...
‘Ni hivi
kesi ya mauaji dhidi yako haipo, japo ni lazima hilo lipitishwe mahakamani...’akatulia
‘Kuonolewa
kwa kesi hii ni wao waendesha mashitaka baada ya kuwabana kwa ushahidi ikabidi
sasa wakiondoe hicho kipengele cha kuwa wewe ni mshukiwa wa mauajii namba
moja...’akatulia
‘Kukabakia
hoja ya kuwa wewe ni msababishi, na mshirika wa kulitenda hilo kosa, kama
ulivyoona mahakamani hili nililipigania hadi kipengele hicho kikawa hakina
nguvu, lakini bado, hakijatolewa na waendesha mashitaka, ...’akatulia
‘Lakini kesi
ikitajwa tena nina ushahidi wa kuweza kuwashinda, hoja hiyo kifupi haina nguvu,
kwani huwezi kuwa ni sababu,...kama ni msababishaji ni huyo aliyebuni hiyo
kazi...lakini siwezi kusema hivyo, nina ushahidi mwingine nitautoa mahakamani,
...’akatulia
‘Waendesha
mashitaka baada ya kuoana sasa wataumbuka, kwani wamemkatama mtu asiyestahiki,
waakaanza kuhangaika kumtafuta muuaji halisii ni nani...hapo wakajikuta kwenye
mtego zaidi, maana walikuja kumpata mtu ambaye ilikuwa vigumu kwao
kuamini...’akatulia
‘Sasa hilo
likawa ni mtego kwao, kama wanakushinikiza wewe kwa alama za vidole, kama
wanakushinikiza wewe kwa kuonekana kwenye kanda za video, basin a wao wamkamate
mtu wao....’’akasema nilitamani kumuuliza ni nai huy mtu wao, lakini sikutaka
kuongea kabisa
‘Basi kwako
ikawa ni mwiba, na yawezekana mtu wao ndiye muuaji, nitahakikisha haki
inatendeka, wao wanajifanya watawala bora sasa nataka niuone huo utawala wao
bora ni upi, lakini kwa sasa siwezi kushinikiza,...’akasema
‘Ushahidi
upo, japo walificha, alama za vidole zimeoenaka pia kwenye bastola, walificha hilo
mwanzoni sasa imebidi waliweke wazi, japokuwa bado ni siri kutokana na
makubaliano ili ombi letu lipite...’akatulia
‘Mshukuru
sana mama mtemi, kwani mama mtemi alipolipata hilo,..maana hutaamini ilikuwa ni siri, lakini ikafika hadi kwa mama mtemi, sijui ilifikaje,....wao wakafikiria kuwa labda ni mimi
nimemwambia, lakini sio mimi, mama mtemi alilipata hilo kwa kutumia mitandao
yake, unamfahamu tena yule mama ... na alipolipata tu, akawaendea...'akatlia akitabasamu
'Yeye alikwenda moja kwa moja kwa mkuu wa kituo mwenyewe...alifanya makosa kutokuniona mimi kwanza nikamshauri njia sahihi, lakini hata hivyo ilisaidia...’akasema sasa akiwa
kakunja uso kama anawaza jambo.
‘Baadaye, alipomalizana kuongea na mama mtemi, wanajua wenyewe walichoongea, mkuu huyo akawaita watendaji wake, akiwa kahamaki kweli...
''Ni nani kalifikisha hilo jambo kwa mama mtemi..'' akauliza na watendaji wake,
wakabakia kushangaa,kwani hata wao hawakujua ni nani kafanya hivyo....mkuu akawa
anahaha huku na kule, wakawa hawana jinsi...’akatulia.
Wakati wakili huyo akiongea kichwani kwa profesa alikuwa akiwaza...huyu Mkuu, huyu mkuu ana husikanaje na hayo mauaji..profesa
akawa anawaza bila kupata majibu,akilini akahisi kuna kitu mkuu kinamgusa kwenye
hiyo kesi, ni kitu gani, akashindwa kukitambua, na hakutaka kuuliza, hakutaka kuongea kabisa siku hiyo...
‘Hapo, kikao
cha dharura kikaitishwa mkuu akawaita muendesha mashitaka, na mpelelezi, wakatafuta njia ya kufanya na ili wafanikiwe
ni lazima wakubaliane na mimi kuwa hilo shitaka dhidi yako, la muaji ni lazima
liondolwe dhidi yako...’akatulia
‘Unajua...eeh, katika
maisha haya ya sheria, hasa ukipewa dhamana, ukijaribu tu kupindisha sheria
kumsaidia mtu wako, ukumbuke kuwa kuna mtu mwingine ana kosa kama hilo hilo, ...’akatulia
''Sasa hapo... ili na wao wasiwe hatiani..kwahiyo hicho kipengele cha kusababisha mauaji
kikawa hakina nguvu,ilikuwa imebakia umauzi wa hakimu tu...na wakikileta
mahakamani, wataumbuka.’akasema
‘Najua
hawatafanya hivyo...’akasema
‘Sasa
ikabakia kosa la biashara ya mlungula, nimejitahidi kila mbinu kwa uzoefu
wangu, haikusaidia kitu maana sasa jamii,imekuja juu, watu wa haki za binadamu
wamechachamaa, na wale wote uliowafanyia hivyo,wamekubali kutoa ushahidi...’akatulia
‘Mama mtemi
yupo kote kote, na umjuavyo zaidi analalia kule kwenye masilahi yake, kwahiyo
kwa vile kwako aliona kuna masilahi ilibidi akusaidie, lakini hata hivyo upande
mwingine yeye ni kiongozi wa kupigania haki za wahanga wa biashara ya mlungula
huko nako ana masilahi ya uongozi na kuna misaada saada wanapata....
'Kwahiyo, ilipofikia kwenye kipengele cha biashara ya mlungula, akawa hana msaada kwako,....kwa vile ulishatatua lile swala kwa kupitia nyumba, ...na unajua mlishasigishana naye kwenye mambo hayo, kwahiyo, kwenye hicho kipengele akawa yeye ni adui yako, anashinikiza
uadhibiwe vikali...’akasema.
‘Kwahiyo
hapo nikawa sina ujanja,...hata hivyo sikukubali, kwani mimi ni wakili wako ni
lazima nipambane, ..sikujali kuwa mama mtemi ni adui wangu kwa hilo, yeye
keshajipanga kutoa ushahidi dhidi yako...mama mtemi ni kigeu geu,...huyu mama achana naye kabisa, kwake masilahi
mbele....’akatulia
‘Kwa
kipengele hicho, mama mtemi na wanajamii wapo kitu kimoja kuhakikisha wote
wanaofanya biashara ya mlungula, wanaadhibiwa ili biashara hiyo ikome kabisa, watu hawapendi mauchafu yao yawekwe hadharani, hawapendi, hizi sheria nyingine unajua tena, ...hapo
nitafanya nini, iliyobakia ikawa kusubiria hukumu tu..’akatulia
'Nakuelezea haya ili uelewe, naelezea kinamna yako wewe usiyejua sheria ufahamu ninavyokupigania, usione nakupotezea muda, .....'akasema akiangalia saa yake.
‘Nikaongea
na dakitari kuona kama nitapata msaada wowote kutoka kwake, na yeye akasema
yupo tayari kuthibitisha kuwa afya yako haistahiki kurejeshwa gereza hilo,...
'Lakini mambo ya magereza wewe upelekwe wapi, hayamuhusu, yeye kama yeye atathibitisha hali yako tu, nikaona bado
sijakusaidia, kutokana na kesi yenyewe, kiukweli....wewe hukustahiki kupelekwa huko.....’akatulia
‘Kwahiyo sasa
ikabakia jinsi gani ya kufanya, .....nikaona nionane na hawa watu, niongee nao....nisikie kauli yao..,....unaona
hapo, inabidi nikae na maadui zangu, na hapo sikumuhitajia mama mtemi tena, maana
angekutosa,..hilo nililipanga peke yangu.....’akatulia
‘Usinione
kuwa kimia, nilikuwa nakuhangaikia kweli ndugu yangu....'akasema akimkagua Profesa kwa macho, hakuamini kuwa huyu mtu yupo sawa, lakini akaendelea kuongea
'Kiukweli kutokana na kesi yako nimehangaika sana, maana hata marafiki, wale
mashahidi wote niliowategemea sasa wakanigeuka, ndio hapo nikajua jinsi mama
mtemi anavyoheshimika....ikafika sehemu hakuna ujanja, lakini mimi ni mpiganaji
wa mahakamani nina uzoefu wa miaka mingi,nikikuambia hapo hakuna ujanja,kweli
hakuna ujanja...’akatulia
‘Wazo la
kutumia silaha ya afya yako nikaona inaweza kufaa.....japokuwa kisheria bado
ingekuwa ni tatizo...’akatulia.
‘Nikawasiliana nao, kuwa naomba tuongee kuhusu hii kesi
''Tuongee nini, tutaongea mahakamani, .....'wakasema, na walikataa, kata kata, nikaona sasa hapo nifanyeje, ....unacheza na mimi, nikawatishia
kuwa nitawaumbua....walijua namaanisha nini kusema hivyo,...
'Kwanini wasikubali,.. wakaja kukubali kuwa tukutane tuongee kwenye maswala ya kufanikisha eeh kesi, ...hapo walikuwa waangalifu,,,unajue tena sheria, japokuwa hawakufahamu nimekuja na ombi gani...’akatabasamu.
Profesa
akilini alikuwa akijaribu kuwaza hawa watu wana kitu gani ambacho kinafunga
waendesha mashitaka mpaka wakubaliane naye, profesa aliamua kukaa kimia, profesa alihisi
kuwa hicho kitu ni cha siri kati ya mawakili hao, na alishamfahamu profesa kuwa
sio mtu wa kuaminika kwenye mambo yanayoitwa siri.
‘Wakakubali nikutane nao bila mtu mwingine
yoyote...’
‘Nikawaambia,..nina
ombi,....waliposikia hivyo wakaangaliana na kuniuliza ombi gani...’akatulia
‘Niliwaambia
kuwa wewe unaumwa sana..na ni kweli hilo hata wao wamekiri,kwani vyeti vya dakitari vinaonyesha,wakaniuliza sasa
kuumwa kwako kuna nini, maana wewe kweli ni mkosaji hukumu ya makosa yako
inajulikana japokuwa hakimi hajatamka,...
‘Ilibidi niongezee mengine kuwa wewe sio wa
kupona, japokuwa kuumwa sio lazima
ufe,nikawaomba kuwa wewe sio raia wa nchi hii, na ukifa hapa serikali itaingia
gharama kubwa za kukubeba,kwahiyo ombI langu kwao ikawa wewe urejeshwe nchini
kwako....’akasema
‘Mwanzoni
walipinga sana..lakini nikawakumbusha kuwa kwa hilo nipo na mama mtemi na
wanamfahamua alivyo walikaa pembeni badaye wakaja kukubaliana na ombi
hilo....’akasema
‘Wakasema
inabidi wakaongea na hakimu kabla ya siku ya kesi, ila hawana uhakika kama
anaweza kukubaliana na hilo....’akasema
‘Hapo nikawa
nimeutua mzigo, maana ni wao sasa wakatafute njia za kumshawishi hakimu, mimi
hapo simuizi kichwa tena, na walijua wasipofanya hivyo kuna mambo yao mengi
yataibuka...’akatulia
‘Najua hakimu
hatakuwa na kipingamizi kikubwa sana,kwani ushahidi wa vyeti vya dakitari
upo...., na unakumbuka aliwahi kufika kukuona, ilibidi yeye mwenyewe kufika siku kesi yako
ilipoahirishwa...wewe ulikuwa huna fahamu,....’akasema,na mimi nilishangaa
kwani sikumbuki kumuona huyo hakimu
‘Hakimu
alikuja ukiwa una hali mbaya, alikuona na aliondoka akisubiria kusikia umeshafariki, alishangaa
kusikia wewe bado upo hai, ...kweli wewe una roho ya paka....’akasema
kiutani,na moyoni nikasema kumbe hawa watu walijua nitakufa ili mambo yao
yafanikiwe.
Moyoni
nilipanga nikitoka, nikiwa na afya nitapigania haki yangu, hasa nyumba yangu,
lakini nikajiuliza ya nini ,na mimi ni mtu wa kufa tu, kama dakitari
keshathibitisha kuwa maradhi niliyo nayo ni swala la muda tu, anachofanya ni
kunipa dawa za kurefusha maisha tu ,..imebakia nini....lakini cha ajabu waliona
bado ninadunda tu...’akasema akijiangalia.
Basi,wakili
akaendelea kusema;
‘Kwahiyo
ombi la kuwa wewe urejeshwe nyumbani kwenu, nikaona lina nguvu nikaenda kuongea
na mama mtemi, sasa nikijiamini, yeye alilifikiria sana na akaja kukubali akaongea
na kijana wako,....kijana wako hata yeye akaoa ni bora maana atakuja kusumbuka
ukifa , yeye ataonekana ni mtu wa karibu kwako kwahiyo msiba utakuwa ni wake.
‘Kwahiyo
nimewaachia wao hiyo kazi ya kukutana na hakimu kabla kesi haijatajwa
tena,...’akatulia
‘Sasa
nakusikiliza wewe unasemaje..’akasema
Mimi sikuwa na la kuongea, kiukweli moyoni
nililkuwa kama nimekufa, sikuwa na hamu hata ya kuongea, ..akasema;
‘Sasa
kisheria inahitajika wewe uweke sahihi yako kuwa umekubaliana na hayo, kuwa
yametoka moyoni mwako, upo tayari kurudi kwenu,...hapa nimetayarisha maombi
hayo, unatakiwa uweke sahihi yako...’akasema akinionyesha hiyo karatasi, mimi
nilimuangalia tu
‘Bila sahihi
yako itakuwa haina uzito, ..na inatakiwa ionekane uliomba siku nyuma
kabla...ndio maana tarehe imeandikwa ya nyuma....’akasema, na mara akahisi
mabadiliko kwa profesa alianza kama kutingishwa hivi.....alipoona hivyo
Akaiweka peni
karibu ya mkono wa profesa akitaka kumsaidia, lakini profesa alikuwa akitikiswa,
...akatulia kidogo, halafu akaanza tena, hapo wakili akaona hali sio shwari, akatoa, kidau cha rangi, akaweka kwenye kidole cha profesa halafu kwa kushinikiza akaweza kuweka alama ya kidole kwenye hizo karatasi, ....
'Hii inafaa, lakini ingelitakiwa sahihi yako,...ooh, profesa upo sawa kweli, ' akasema huku akimkagua Profesa, kwani ilionekana kabisa hayupo sawa, wakili alipoona hivyo akasema;
‘Sasa mimi
natoka kidogo, naona hali yako haipo shwari, dakitari kaniambia, hali hiyo
inatokea inakuja na kuondoka, nikiiona nisiogope, ila hapana, hapa imezidi inabidi nikamuite tu, huyo dakitari aje tuone atakusaidia vipi, sahihi yako ni muhimu sana, isipoatikana wanaweza kuweka pingamizi wale watu...’akasema na haraka akaondoka.
Profesa
akiwa peke yake, kiukweli hali ilikuwa sio shwari, alionekana kweli anaumwa, na ni moyoni kweli alihitajia kuondoka kurudi kwao, akawa anatamani akafie kwao....akaona ajitahidi tu,akainua mkono na kuchukua ile peni kutaka kuweka sahihi yake lakini mkono ukawa mnzito, akawaka anatikiswa mwili mnzima, akajitahidi na hata kalamu ilipofika kwenye karatasi, akajikuta akikoroga tu...
Profesa hali ikawa ni mbaya, akawa hajiwezi kweli, wakati huo wakili ameshaondoka,
kumuita dakitari, akahisi pumzi ikiwa nzito, nguvu zilikuwa
zimemuishia kabisa, jasho likawa linamtoka, akawa anatikiswa kweli kweli, na
haikuchukua muda akapoteza fahamu...
WAZO LA LEO: Sheria hukata mbele na nyuma, huwezi
ukafumba macho ukiona jambo limetokea sehemu inayokugusa.. ukijaribu tu kupindisha sheria kumsaidia mtu
wako, ukumbuke kuwa kuna mtu mwingine ana kosa kama hilo hilo naye utasemaje!
Kwahiyo ewe mtendaji mwenye dhamana, ewe kiongozi,... timiza wajibu wako kwa
kusimamia haki na uadilifu...
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment