Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeFriday, September 18, 2015

RADHI YA WAZAZI-42


Bro, hutaamini kesi ilianza kupigwa dana dana, kila siku inaahirishwa kwa kisa hiki na kile, mimi nasota huko gerezani, nateseka,...niliumizwa, niliteseka, 
nikanyanyasika, nikazalilika,..sijawahi maishani mwangu, na ilifikia muda sasa nikasema nikipa sumu najiua...’akasema mdogomtu

‘Lakini si ulisema alipofika mama mtemi alisema kuwa keshaweka mambo sawa na wakili wako akasema kesi iliyobakia ni ya kawaida tu, sasa tatizo lilikuwa wapi, au ndio ulikuwa unalipa dhambi za watu...?’ akauliza kaka mtu.

‘Kwaweli hata mimi sikuelewaa...kuna muda nilikuwa naitwa mahakamani kesi inatajwa, inatolewa sababu fulani kuwa shahidi muhimu hayupo, mara kuna uchunguzi haujakamilika,...ikawa ndio hivyo,nikitaka kuongea na wakili wangu, ananiambia atakuja gerezani, ikawa ni kupigana chenga,....walichokitaka wao wamekipata wanahitajia nini tena...’akasema mdogomtu

‘Hali yangu ya kiafya ikawa mbaya sana, nikawa naumwa, na hata wakati mwingine kupoteza fahamu, na kuna muda waliona kuwa mimi ni mtu wa kufa tu, kwani nilikuwa nimebadilika na kuwa na sura ya mfu...walipoona hali yangu ni ,mbaya sana, ndio nikapelekwa kulazwa hospitali ya uraiani,huku nikiwa chini ya ulinzi...’akasema mdogo mtu

‘Siku zikaenda,siku zikapita,..karibu mwaka kukamilika..simuoni mama mtemi, hata wakili nilikuwa nakutana naye mahakamani, ....’akasema mdogo mtu

‘Je kijana wetu...?’ akaulizwa

‘Huyo ndiye hata hakutaka kusikia nikitajwa mvele yake... eti nimemchafulia jina lake...’akasema

Tuendelee na kisa chetu..

******

‘Ndugu hakimu, tunasikitika kuwa kesi hii imechukua muda mrefu sana....’akaanza kuelezea muendesha mashitaka walipofika kwa hakimu

‘Kutokana na mambo yaliyojitokeza tumeona tuje mbele yako kwa mapendekezo ambayo tunaona yatawezesha kuimaliza hii kesi,na hili tatizo katika jamii zetu..’akasema muendesha mashitaka.

‘Kwani kuna tatizo gani, hebu niambieni...hili hatuwezi kulivumilia kesi kuchukua karibu mwaka sasa, kuna tatizo gani?’ akauliza hakimu na muendesha mashitaka akiwa na mpelelezi,akasema...

‘Ndugu muheshimiwa hakimu, kesi hii imetuchanganya sana,...na kilichotuachanganya zaidi ni kuhusu mambo yaliyokuja kujitokeza baadaye, tumegundua matukio mawili ya kamera za nje, zikionyesha watu wawili wengine tofauti...’akasema

‘Na watu hao hawakuwepo kabisa kwenye mashitaka yetu, lakini kutokana na ushahidi tuliouata tumegundua kuwa ni wahusika,....’akasema

‘Walionekana wakitokea ndani wakikimbia kama alivyoonekana mshitakiwa wa awali kwa upande mwingine wa nyuma, ...lakini tofauti na mshitakiwa wao hawakuwa na silaha, lakini kwa uchunguzi wa ndani kama alama za vidole, ilionyesha dhahiri walikuwa ndani ya chumba alipokuwepo marehemu..’akasema mpelelezi

‘Tumefuatilia hilo na uchunguzi huu mpaya umetupa uhakika kuwa watu hao wanaweza kuhusika na mauaji hayo, kwa hivi sasa mmojawapo  tunaye, na kakiri kuwa alikuwepo kweli kwenye chumba alipokuwepo marehemu, na kwanza aliongea naye akaondoka, na aliporudi mara ya pili akakuta mwili wa marehemu ya kuwa alishauwawa ....’akasema

‘Na yupo mwingine huyo yeye alikimbia nchi, kwa hivi sasa hayupo hapa nchini, aliwahi kukimbia mapema... yeye tuna imani anaweza kuwa muhusika mkuu....’akasema

‘Ni nani huyo....?’ akaulizwa

‘Huyu alikuwa mmoja wa walinzi wa kujitegemea, amekuwa akikodiwa kufanya kazi hizo za ulinzi na watu tofauti na mara ya mwisho alikuwa akimlinda dada mmoja aliyekuwa muhudumu wa hoteli,dada huyu alikuja kurubuniwa na mshitakiwa wetu na wakafanya mipango ya mlungula ambayo ndiyo iliyosababisha hadi marehemu kuuwawa...’akasema mpelelezi

‘Yeye na huyu binti waliwahi kutoroka nchini, na kiasi kikubwa cha pesa, na tulivyofuatilia tumegundua pesa hiyo ndiyo hiyo ya mlungula....’akasema mpelelezi

‘Tumekuwa tukiahirisha hii kesi mara kwa mara ili kuwapata hawa watu tukiwa tunawafuatilia ili kujua wapi walipo, lakini cha ajabu, hawakuwahi kufika huko nchini kwao ambapo tulifikiria ndipo walipokimbilia..., na hii imetupa mashaka kuwa, yawezekana hawa watu walibadili safari wakiwa njiani tofauti na nyaraka zao zilivyoonyesha kuwa walikuwa wakirudi nchini mwao ...’akasema

‘Inawezekanaje hao watu watoweke kihivyo, ....maana siku hizi kuna utaalamu wa kufuatilia nyendo za mtu kwa njia ya mitandao, wanapotoka hapa hadi huko wanapokwenda, imekuwaje hawa watu wasipatikane kwa harakai...?’ akauliza hakimu.

‘Hawa watu walitoroka na pesa nyingi sana,...kwahiyo walipofika sehemu ya kubadili ndege, hawakufanya hivyo, wakitumia pesa zao, waliingia kwenye nchi ya jirani, na wakatumia usafiri wa kawaida, au meli kwenda nchi nyingine,lakini bado tunawafuatilia,watapatikana tu muheshimiwa hakimu...’akasema mpelelezi.

‘Sasa kuhusu huyu mshitakiwa na wenzake mumefikia wapi?’ wakaulizwa

‘Kuna wahanga wengi wa kuthibitisha kuwa wahalifu hawa wamekuwa wakifanya hiyo biashara ya mlungula...,na sasa wahanga hao wamekuwa tayari kuelezea ilivyo kuwa....’akasema mpelelezi.

‘Wapo tayari kusimamishwa mahakamani....?’ akauliza hakimu

‘Hapana muheshimiwa hakimu,ndio maana tumekuwa tukiahirisha hii kesi mara kwa mara ili kuona jinsi gani ya kulimaliza hili tatizo bila ya wahanga hao kupata madhara kutokana na mitego waliyotegewa....’akasema muendesha mashitaka.

‘Mara nyingi wahanga wa biashara hii huogopa kujitokeza, kutokana na kashifa iliyopandikizwa,kwani huwa kweli wamefanya hiyo kashifa na ikijulikana wanaogopa kukosa ajira, kuvunjika kwa ndoa zao,au kuadhirika kwenye jamii...’akasema muendesha mashitaka.

‘Na kutokana na kesi hii wengi wametegewa kwenye matendo yanaoweza kuvunja ndoa zao,...walinaswa wakiwa wamekiuka sheria za ndoa zao,na waliambiwa kama wasipotoa pesa taarifa itafikishwa kwa wake zao, au waume zao,  na wake zao , au waume zao, wanaweza kuvunja ndoa... na ndoa hizo zina masilahi kwao’akasema muendesha mashitaka.

‘Na kama tulivyokuambia awali tunajaribu kuangalia, jinsi gani ya kufanya ili tusije kuingilia mambo binafsi, kwahiyo tumekuwa makini kuliweka hili  hadharani,kutokana na maombi ya hao wahanga ambao wamekubalia kushirikiana na polisi,ndio maana tumekuwa tukiahirisha ahirisha hizi kesi,na kwa vile umetuita, tunaona ni wakati muafaka wakuliweka hili wazi mbele yako muheshimiwa hakimu...’akasema muendesha mashitaka.

‘Je kwa kufanya hivyo hamuoni kuwa mnahalalisha makosa yao ya kuvunja amri na sheria za ndoa zao, na mnataka mahakama iwatete kwa hilo...?’ akasema muheshimiwa hakimu.

‘Muheshimiwa hakimu tumeliona hilo,...lakini sisi tumeona kuwa , hayo yabakie kati ya wanandoa wenyewe, tusikiuke ahdi tuliyoiweka kuwa wakijitolea kusema ukweli, sisi tutajitahidi kuficha siri zao... kwani tukiwafikisha mahakamani kila kitu kitajulikaa na hapo tutakuwa tumeshiriki kuvunja ndoa za watu...’akasema

‘Kwahiyo kwa usaidizi wako tunaomba iwe hivyo, kuwa japo watu hao wamekiuka sheria za ndoa zao, makosa hayo yawe kati ya wanandoa , sisi tuweze kuikomesha hii biashara ya mlungula bila kuleta athari nyingine za kijamii...’akasema muendesha mashitaka.

‘Kwahiyo mumefanyaje ili hao wahanga wawe tayari kutoa taarifa na hizo kashifa zao zisiweze kuvunja ndoa zao, ...mjue yote hayo yakifika mahakamani yatawekwa kwenye kumbukumbu, na ili hii kesi iishe hatuna jinsi inabidi muwasimamishe mahakamani,...’akasema hakimu

‘Ndio maana tumekuja kwako kuomba msaada, kama unavyojua, wengi wanakuwa wagumu kushirikiana na polisi, sisi tukaona haina haja,...tukatumia mbinu za kuwafuatilia hawa watu bila ya hata wao wenyewe kujifahamu, tukawafahamu ni nani,tukakutana nao na baadaye ikabidi wakubali, na wakasema wapo tayari kutoa ushahidi kama ushahidi huo hautaweza kuwekwa wazi na kuathiri ndoa zao...’akasema mpelelezi

 ‘Mbinu kubwa ilikuwa kupitia kwenye benki zetu, huko tuna watu wetu ambao waliweza kutupa taarifa za akaunti zenye uwalakini, na kila kiasi kikubwa kilivyotolewa isivyo kawaida ya mteja huyo, tulipata taarifa, na kuanza kufuatilia ni kwanini pesa hiyo ikatolewa....na hili limetusaidia sana.....’akasema mpelelezi

‘Kwa kufanya hivyo mnakiuka sheria za usiri wa mteja, huyo mteja ana haki ya kuwashitaki...mnalifahamu hilo...?’akasema hakimu

‘Ilibidi iwe hivyo, ili kuwabaini hawa watu, ...lakini kiukweli tulikuja kugundua mambo mengi yaliyojificha, yanayotendeka kwenye jamii,na watu wanaumia lakini wanashindwa kushitaki, wanaogopa kushirikiana na polisi....na ni bahati mbaya tu hatukuweza kuzuia haya mauaji, ...’akasema

‘Ina maana mlihisi kuwa kunaweza kutokea hayo mauaji...?’ akaulizwa

‘Hapana hatukulitarajia hilo kabisa, mara nyingi biashara hizi zimekuwa zikifanyika, na mauaji ni nadra, na ikitokea inakuwa labda mtu kujiua mwenyewe, anapoona kadhalilishwa, au atadhalilishwa....’akasema huyo mpelelezi

‘Turudi kwa hawa washitakiwa, kuna huyu mshitakiwa mkuu, je mligunduaje kuwa huyu mshitakiwa ni kiongozi wa biashara hiyo au anatumiwa, au mnataka sasa aweje,maana bado hajahukumiwa...?’ akaulizwa

‘Tulimchunguza sana huyu mshitakiwa, tukawa tunafuatilia nyendo zake,na sasa wengi waliowahi kufanyiwa hii hujuma wameelezea wazi alivyokuwa akifanya, tumehakiki sauti aliyokuwa akitumia sehemu mbali mbali, tumegundua kuwa ndio yeye, hatuna shaka na hilo...’akasema mpelelezi

‘Mhh....kwahiyo mliweka watu mpaka kwenye vyombo vya mawasiliano,...?’ akauliza hakimu

‘Ilibidi tufanye hivyo muheshimiwa hakimu ,ili kukomesha kabisa hii biashara yenye kuumiza jamii...’akasema mpelelezi

‘Na badaye tulikuja kugundua kuwa huyu mtu alikuwa na mshirika mwenza, kama tulivyosema kulikuwa na watu wanaisaidia polisi, na mmojawapo ni aliyekuwa mshirika wa mshitakiwa....mara kwa mara watu wanaondesha biashara hzii hizi walikuwa wakienda kwa huyu jamaa anayejulikana kama mtaalamu,tukajiuliza ni kwanini...’akasema mpelelezi

‘Mtaalamu ni nani..?’ akaulizwa

‘Ni huyu mumiliki wa kampuni ya mitandao, ndiye mbunifu wa biashara hizi za mitandao,na yeye ,ndiye alishirikiana na mshitakiwa kukamilisha hiyo biashara haramu iliyosababisha kifo cha huyo marehemu...’akasema

‘Huyo mtalaamu yupo wapi...?’ akaulizwa

‘Huyo Mtaalamu kwasasa bado anaisaidia polisi, tumeamua kumtumia na kazi aliyopewa ikikamulika na yeye atafikishwa  mbele ya mahakamani yako tukufu kujibu mashitaka yanayomkabili...’akasema muendesha mashitaka wakiwa na mpelelezi

‘Kwahiyo mnataka kusema nini...?’ akauliza hakimu

‘Tunachotaka kusema ni kuwa tumegundua kuwa  mshitakiwa tuliyenaye kwa hivi sasa anapunguziwa mashitaka yake, ....na tuna maombi mengine dhidi yake, kwani hata yeye kakubali kutoa ushirikiano kwa makubaliano kama mahakama yako itakubaliana na hilo...’akasema muendesha mashitaka

‘Kwanini mnasema mnataka kumpungizia mashitaka, ....kwasababu kutokana na ushahidi mlioutoa hapa mahakamani mtu huyo kasababisha hayo mauaji yatokee, akishirikiana na wenzake,  au....?’ akauliza hakimu

‘Ndio muheshimiwa hakimu, sisi tulimshitakia kama muuaji,.... kitu ambacho tumegundua kuwa sio kweli, yeye hastahiki kushitakiwa kama muuaji kwa vile muuaji tumeshamfahamu, japo hajafikishwa mahakamani, tunamtafuta wapi alipojificha,....’akasema

‘Baada ya uchunguzi wa kina tumegundua kuwa mshitakiwa alifika eneo la tukio wakati mauaji hayo yalishafanyika...vielelezo hivyo tunavyo...’akasema muendesha mashitaka.

‘Kwahiyo mnataka mshitakiwa ashitakiwe kwa kosa gani...?’ akauliza hakimu

‘Mshitakiwa anashitakiwa kwa kosa la kuendesha biashara ya mlungula, na kutokana na biashara hiyo akawa mmoja wa waliosababisha kifo cha marehemu,lakini sio aliyemuua marehemu...’akasema muendesha mashitaka

‘Mnasema huyo ni msababishi lakini sio muuaji, mnawezaje kuweka ushahidi wenu mbele ya mahakama,kutofautisha hilo ...?’ akauliza hakimu

‘Ndio muheshimiwa hakimu tutaliweka hilo bayana mbele ya mahakama yako tukufu, kwani huyu mshitakiwa yeye alitumika, akachochea hiyo biashara ili kupatikana hiyo pesa ya mlungula, na pesa ikawa inagombewa na watu wengi,...lakini yeye sio aliyemuua marehemu...’akasema

‘Pesa ikagombewa na watu wengi...!’ hakimu akasema kwa mshangao na muendesha mashitaka akasema;

‘Ndio muheshimiwa hakimu, kuna watu wengi walikuja kufahamu kuwa kuna pesa kama hiyo imetolewa na mhanga wa mlungula, ukiacha watayarishajii wenyewe, na watu hao wakaona ni pesa ambayo ipo nje, ni rahisi kuipata...’akasema muendesha mashitaka

‘Kama ujuavyo watu ambao hupenda pesi bila hata kuzitolea jasho,...walifuatilia na kugundua kuwa  pesa hiyo ni nyingi, wakaanza kufuatilia kuona wapi itapelekwa,...tutakuja kuelezea hilo hatua kwa hatua ilivyofanyika, kwenye ushahidi wetu,..’akasema muendesha mashitaka

‘Katika kufuatilia huko, ndipo kukatokea kunyang’anyana,...ndipo muuaji akalitenda hilo kosa, ....’akasema

‘kwahiyo kwa usemi wako, muuaji hakukususia...?’akaulizwa

‘Kukusudia yawezekana, ...tukimpata huyu mshitakiwa mwingine tutakiwa tumelithibitisha hilo, ...’akasemapata mpelelezi

‘Kwahiyo kumbe bado hamjawa na uhakika...?’ akauliza hakimu.

‘Uhakika upo muheshimiwa hakimu, ila tutakuwa na maelezoo yaliyojitoshelea tukimpata huyo mshitakiwa mwingine..’akasema muendesha mashitaka

‘Kwa mantiki hiyo, huyu mshitakiwa tuliye naye mpaka sasa ambaye mashitaka yake inaendelea ndiye msababishi wa haya yote,...lakini sio muuaji, na muuaji hajapatikana ?’ akauliza

‘Ndio muheshimiwa hakimu...’akasema muendesha mashitaka

‘Na mahakama haiwezi kuthibitisha hilo, mpaka mulete ushahidi na huyo mshitakiwa, mpaka sasa huyu mshitakiwa ndiye anatambulika kama mshukiwa, ni lini mtamfikisha  au mtawafikisha hao washukiwa wengine mahakamani ...?’ akauliza na muendesha mashitaka akageuka kumuangalia mpelelezi.

‘Mumetumia muda mwingi kwenye hii kesi, hatuwezi kuendelea na kesi kama hamjakamilika, na hatuwezi kuendelea kumshikilia huyo mshitakiwa kwa shitaka hilo, kama hamjakamilisha ushahidi wenu, ...hii sasa inakaribia miezii mingapi,mnafanya utani na kazi zenu...?’ akasema hakimu kwa sauti ya ukali.

‘Ndio muheshimiwa hakimuni kweli kesi hii imachukua muda kinyume na tulibvyotarajia, ni kutokana na kuingiliwa na ... ‘akakatiza kuongea na hakimu akauliza

‘Ni nani yupo juu ya sheria, niambieni, kama kuna kikwazo wekeni wazi, hakuna aliye juu ya sheria...’akasema hakimu

‘Ndio muheshimiwa hakimu, ndio maana tunaiomba mahakama yako tukufu itusaidie...’akasema muendesha mashitaka

‘Mahakama iwasaidie kuhusu nini...?’ akauliza hakimu akionyesha mshangao

‘Kuhusu ombi la hawa mashahidi , hawa wahanga wa mlungula,... kutokana na ombi lao kuwa hawataki wajulikane,  na sisi tutahakikisha huyu mshitakwia mwingine anakamatwa,ili kumpata muuaji halisi...’akasema muendesha mashitaka

‘Sasa kati ya hao wawili ,...mnasema mmoja hamjamkamata  na mwingine mnaye tayari ambaye kakubali kushirikiana nanyi, mumeshagundua  ni nani hasa mmuaji ...?’ akaulizwa hakimu,na muendesha mashitaka akageuka kumuangalia mpelelezi.

‘Japo bado kuna utata, ..lakini tuna imani kuwa tukimpata huyo mshitakiwa mwingine, tutaumaliza huo utata....na kuimaliza hii kesi kabisa’akasema muendesha mashitaka akigeuka kumuangalia mpelelezi , ikionyesha kuwa alihitajia maelezo kutoka kwake kwa swali hilo.

Mpelelezi akionekana kusita kutoa hayo maelezo,kwanza akakohoa kusafisha koo, akitaka kuongea kitu, na ilionekana ni jambo nzito kulitamka, lakini hakuwa na jinsi...

‘Muheshimiwa hakimu ....’akaanza kusema, na  kabla hajaendelea simu ya mpelelezi ikatoa sauti ,...kwa haraka akainua hiyo simu na kuiangalia ,  ulikuwa ni ujumbe wa maneno, mpelelezi akasema tafadhali, akawa anausoma huo ujumbe,halafu akainua kichwa, na kukitikisa  kama kukubali kitu, akasema;

‘Mwishowe tumempata...’akamuangalia muendesha mashitaka halafu akageuka kumuangalia hakimu akasema;

‘Muheshimiwa hakimu, mtu tuliyekuwa tukimtafuta ameshakamatwa akiwa na mwenzake...’ akasema huku akitabasamu.

‘Sasa kazi imekwisha....’akasema muendesha mashitaka na hakimu akauliza

‘Huyu mshitakiwa mwingine naye ni nani?’  hakimu akauliza, huku akimuangalia mpelelezi, na baadaye muendesha mashitaka, muendesha mashitaka akitabasamu akasema....

‘Muheshimiwa hakimu, ngoja mimi nikujibu hilo swali ...naye ni miongoni mwa walioomba....lakini ...’akaanza kusema

NB: Tunaishia hapa kwa leo,....naona sasa tunafikia kwenye hitimisho, kama kuna mawazo, nyongeza, tunakaribisha, pia unaweza kuwasiliana nami kwa barua pepe, miram3.com@gmail.com . Huku tukiwa tunajiandaa kwa kisa kingine, tuombeane heri, tuweze kushinda mitihani hii ya maisha.


WAZO LA LEO: Kuna tabia ya kulindana, mtu kafanya kosa, kwa vile ni mtoto wa fulani, mtoto wa mkuu, au muheshimiwa fulani, basi yeye analindwa,kesi yake itapigwa danadana...hii pia inaenda zaidi kwenye sehemu za kazi, wanaopata kipaumbele ni watoto wa waheshimiwa au wakuu fulani, kama unabisha nenda sehemu za kazi, kwa namna hii tunajenga matabaka, wenye nacho na wasio kuwa nacho. Je lini hawa wasio kuwa nacho watapata watu wa kuwalinda, kuwatetea, kuwapa kipaumbele, ....
Ni mimi: emu-three

No comments :