Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Monday, September 14, 2015

RADHI YA WAZAZI-41



  Wakati hayo yakiendelea huko kwa wenye dhamana,..... huku gerezani, alipo profesa nako mambo yalikuwa yamebadilika, ..

Mambo yalimuendea vibaya profesa kwani kinyume na alivyotarajia, na walivyokubaliana, profesa alijikuta akihamishwa gereza na kupelekwa gereza ambalo ni baya kuliko yote kwenye nchi hiyo, na wengi wanaopelekwa huko ni wale walioshindikana.

‘Siku hiyo bro, nilifanywa kushitukiziwa......’akasema mdogo mtu

‘Kwanini uhamishiwe huko na wakati kesi yako ilikuwa bado,na hujahukumiwa?’ akauliza kaka mtu

‘Bro, ujue hata kufungwa kwangu, hata kushitakiwa kwenyewe, yote ni mambo ya fitina tu,  hiyo kesi ni mambo ya kukomoana tu..watu waliataka kujionyesha kuwa wao zaidi, na hawagusiki,....’akasema mdogo mtu

‘Kukomoana wakati wewe kweli ulikuwa unajishughulisha na biashara hiyo ya milungula....au wewe ulitaka ufanye makosa usishitakiwe?’ akaulizwa na kaka mtu

‘Biashara hiyo sikuwa nimefanya peke yangu, wangapi wanafanya mambo hayo na hawajakamatwa, kwanini mimi nikawa ndio mhanga, nilikuja kugundua kuwa pamoja na ya kuwa nilikuwa na makosa lakini kulikuwa na uenevu, wakubwa na familia zao huwa wanalindwa, kuna namna ya kulindana ....’akasema mdogo mtu

‘Mimi sijui.....’akasema kakamtu

‘Ndio hivyo, dunia hii wanyonge ndio wanataabika, wanyonge ndio wanabeba mateso yote ya dunia, watu wanaiba mabilioni, unasikia kabisa wamefisidi, unasikia wamesababisha hasara,  unasikia wamegushi, wamefanya hiki na kile na gharama yake ni mapesa mengi hawa hawafungwi, hawa hawaoenekani wezi,wezi ni hawa wanaoiba kuku,....wanaoiba pesa ndogo ndogo.....’akasema

‘Mimi siyajui hayo...’akasema

‘Nikuambie ukweli, hata sheria zikiwekwa zinawalenga wanyonge tu...kwanini wanyonge wawaghasi wenye nacho, kwanini, hawa wasio nacho, hawaachi kuwauliza wenye nacho wamepataje, wasitoe mauchafu yao yakaonekana...mimi nilikuwa nimewalenga wao....’akasema mdogo mtu

‘Hahaha, unajua mimi hata sikuelewi, uliwalenga wao, au ulikuwa unatafuta masilahi,...lakini tuyaache hayo, unasema ulihamishwa gerezani, ikawaje, vii hujaonana na wakili wako, ili kuandikishana mkataba wa kuuza nyumba, ilikuwaje?’ akauliza kakamtu

‘Ndio hivyo, asubuhi na mapema tunaamuka gari likafika na mara nikaitwa jina langu, nikaambiwa nahamishwa gereza....

Tuendelee na kisa chetu....

‘Kwanini,mbona kesi yangu bado..?’ nikauliza

‘Wewe hukustahiki kuwekwa hapa, hapa wanawekwa watu wa kesi za kawadia, kesi yako ni ya mauaji, ....’akaambiwa

‘Lakini mimi sijaua ...mumesikia hata huko mahakamani, aliyeua hajakamatwa, mimi walinishuku tu, na siwezi kuhukumkiwa kabla mahakama haijaamua hivyo,...’nikajitetea

‘Hayo waulize wahusika sisi tunatimiza wajibu wetu...’akasema huyo mkuu wa msafara, hacheki, ....

‘Mimi siwezi kuondoka hapa mpaka nionane na wakili wangu, nina haki yangu kisheria,....’akasema profesa

‘Mimi hayo sijui,  sisi tunafuta amri kutoka kwa wakubwa zetu,  ingia ndani ya gari tunaondoka sasa hivi, usitupotezee muda....’akasema huyo askari magereza.

‘Mimi siwezi kuondoka hapa mpaka wakili wangu afike...’nikagoma, na wao wakaangaliana, na bila kusita, wakanijia kama vile walikuwa wanajua nitafanya hivyo, walishajua mimi nina kiburi, bro mimi sina nguvu za misuli lakini kwakiburi cha mdomoni, huniwezi....

Lakini mbele ya hao wababe, nilisalimu amri...

‘Mhh , sasa ikawaje..?’ akauliza kaka mtu


*********

‘Profesa aligoma kabisa kuingia kwenye gari, ikabidi watumie nguvu, na kumgonga na virungu vyao kwenye magoti, na hatimaye profesa akasalimu amri, na kuingizwa kwenye hilo gari la wafungwa kama gunia...

‘Unaleta ubishi, ....sasa dawa ya ubishi wako ndio hiyo...’wakasema wakati huo profesa alikuwa akigugumia maumivu

Profesa alifikishwa kwenye hilo gereza ambalo sifa zake zimeenea nchi nzima, na alipofika hapo, akajikuta anakaribishwa kama mtu fulani aliyekuwa akisubiriwa kwa hamu, kama mwanamziki mashuhuri,au mtu fulani aliyekuwa akiongelewa na sasa keshafika...

Akaingizwa ndani na taratibu za kuandikishwa zikafuatwa, na hatimaye, akapelekwa kwenye chumba chake...na kama kawaida vyumba hivyo huchangiwa watu wawili  wawili, mmoja juu na mmoja chini.

‘Nilipofika kwenye hicho chumba mwenzangu ambaye alikuwa yupo humo, hakuwepo, ilikuwa muda wa ambao wengi walikuwa kwenye shughuli mbali mbali, na sikuambiwa kitanda changu ni cha juu au chini.

Nikabakia nimesimama kwa muda,nilishajua gerezani kulivyo, kuna ubabe, na sikutaka kuanza kukosana na huyo aliyekuwa humo, lakini nilikuwa nimechoka, miguu ilikuwa inauma, mwili hauna nguvu, nilihitajia kulala.

Nikakaa kwenye kitanda cha hapo chini, na kwasababu ya kuchoka, na maumivu usingizi ukawa umenichukua,....nilishituka nainuliwa juu kwa juu na kubamizwa chini

‘Wewe ni mdudu gani unalalia kitanda changu..’sauti kama ya chura ilinguruma.

‘Samahani sikujua, ...’nikasema nikiwa sakafuni.

‘Hukujua eeh, sasa utajua...’akasema huku akinisindilia mateke, na kunikanyaga kama mtu anayeua nyoka kwa mguu.

Ilipiata dakika mbili, nikiendelea kupata hicho kipigo,mpaka alipokuja kiranja wa humo ndani na kuuliza

‘Kuna nini kinaendelea humu ndani...’akasema na huyu jamaa akamalizia kunikanyaga kichwani nikahisi vinyota, na kabla sijaa sawa, akamalizia na kunipiga teke la mbavuni, nilihisi mbavu zimeachia.

‘Damu, zikawa zinanitoa puani, mdomoni...’akasema profesa, na ikabidi sasa yule kiranja atoe ishara kwa askari wa gereza liyekuwepo humo, wakafika na kunikuta nipo sakafuni sijitambua

Hilo jamaa lilipoulizwa likasema nimekuja na kulala sehemu yake, na mimi nikaulizwa nikasema mimi ni mgeni sijui ,sikujua kutanda changu ni kipi,

‘Karibu gereza la kifo, hiyo ni chai chakula bado...’akasema huyo kiranja wa hapo, huku akanikagua, naona alijua kweli nimeumizwa, akaamrisha nibebwe na kupelekwa chumba cha huduma ya kwanza, mmoja wa akaniinua kama gunia akaniweka begeni kama vile mtu anaweka gunia begani na kuzidi kuniumiza mbavu, hakujali ninavyolalamika,alinibeba hadi chumba cha huduma ya kwanza na huko, nikapigwa sindano...nikaanza kuhisi mwili ukiuma uma...kuwashwa utafikiri upupu,..

Ile hali ya kuwashwa, ilinifanya nihangaike, ...niliachwa hapo kwa muda, kwakweli, dawa hiyo ilizidi hata hayo maumivu niliyokuwa nayo ya kupigwa, niliwashwa, unajua kuwashwa, ni zaidi ya upupu,nilihangaika, mpaka nalia kama mtoto walipofika walinikuta nalia kwa maumivu nahangaika, siwezi hata kukaa., wakaanza kunicheka ninavyohangaika...

‘Sasa umepona, kama hujapona tukuongezee nyingine....’akasema huyo dakitari, akiwa na askari wa hapo na kiranja wa wafungwa, nikajikuta nikisema

‘Nimepona afande....nisaidieni, nisaidieni...’ akasema profesa na wale maaskari na kiranja wa wafungwa wakawa wanacheka, hadi kushika mbavu...na yule docta akanisogelea na kunipiga sindan nyingine, na haikuchukua muda ile hali ikaisha, na akasema;

‘Haya kama umepona, haya kimbia...’ akasema, na mimi kwa haraka nikaanza  kukimbia kuelekea huko kwenye chumba changu.

Yaani yale mateso ya kuwashwa,  ilibidi nikimbie sana, hadi chumba nilichopangiwa,...milango ile ukifika kwenye chumba chako, kama unatakiwa kuingia, kinajifungua chenyewe, nikaingia, na nilimkuta yule jamaa kalala, anakoroma utafikiri simba, nikapanda kwenye kitanda cha juu, nikiogopa kumuamusha na kusubiri kitakachofuata baadaye.

*******

Usiku ni kama kumekucha, mengi yaliyotokea usiku huo yalikuwa mabaya kiasi kwamba siwezi kusimulia, ...kumbe ikifika usiku wanafanyaje milango hufunguliwa na viranja,...nikajikuta naamushwa, nikatolewa juu ya kitanda hadi sakafuni,..

Lile jamaa jirani wangu, akawa anatizama ninavyozalilishwa,.. niliomba roho tu itoke, na hadi asubuhi kunapambazuka, sikuamini kuwa bado nipo hai, ...niliteseka, nilinyanyasika, nilizalilishwa, hadi saa tisa hivi...

 Ilipofika saa tisa hivi, kukatanda ukimia fulani, kila mtu akarudi sehemu yake, kumbe wenyewe wanafahmu kuwa muda huo ni muda wa ukaguzi, nilihisi ukimia, na  hapo ndio usingizi unataka kunichukua, kengele ikalia, na kengele ikilia ole wako uchelewe, ole wako wako uchelewe kutoka, kwani milango inafunguliwa kwa umeme kwa muda huo ukichelewa unafungiwa ndani na ukikutwa upo ndani na hao viranja, mateso utakayoyapata hutaweza kuyasahau.

Tulitoka nje ya milango yetu, ikaja kukaguliwa halafu mnaongozana kwenye uwanja ambapo hapo mnapangiwa kazi zinaitwa za kupasha viungo moto.., kazi hizo zikiisha kwa saa mbili hivi, sasa mnasimamishwa uwanjani kama kuna wakupelekwa mahakamani, wanachukuliwa, kama kuna wagonjwa ....
Mara nikasikia

‘Profesa una wageni wako...’niliposikia hivyo nikapumua, nikajua hatimaye huenda wakili wangu amekuja na huenda nitajua ni ni wamekifanya na nini mustakabali wangu,

Nilipofika chumba cha wageni nilimkuta wakili na kijana wetu, nilishangaa, maana zaidi aliyekuwa akija alikuwa ni mama mtemi,.... leo yupo kijana wetu, kiukweli nilikuwa kwenye hali mbaya sana, nilikuwa nachechemea, lakini nilijikaza, nisije kuonekana hali niliyo kuwa nayo, nilitamani kulia ili kijana anione ni kama vile kijana ukimuona mzazi, japo sasa mimi ndiye mzazi, machozi yalinitoka...japo nilijaribu kujizuia...

‘Pole sana profesa, najua upo kwenye mateso makubwa, lakini  mambo yalifanyika kwa haraka sana , hata kuhamishwa kwako mimi sikuambiwa,....’akaanza kusema huku akitoa makaratasi kwenye mkoba wake

‘Hutaamini kijana wetu hakunisalimia kabisa aliniangalia kama kinyaa, kama mtu ambaye anamuabisha, ...nilichoka, na wakili akasema;

‘Nimekuja na kijana wako ili awe ni shahidi ,pamoja na mengine mengi yeye aliwahi kuishi kwenye nyumba yako hiyo ambayo itachukuliwa kama dhamana, kwahiyo yeye atakuwakilisha wewe kama mdhamini wako,...’akasema

‘Mama mtemi anaongea na wakuu wa gereza kuona jinsi gani atakavyoweza kusaidiwa, japokuwa gereza hili , haliingiliwi, ukifika huku, hakuna sheria hakuna mtu anayoweza kuingilia....’akasema

‘Sasa kwanza nimuulize kijana wako kama yupo tayari na hili zoezi maana ni zoezi muhimu sana, kila kitu keshakisoma na tathimi ya gharama ya nyumba imeshajulikana na tumeshaongea na watu huko kwenu wamelithibitisha hilo,...’akasema na hata wakiongea akili yangu haikuwepo hapo, nilihisi kichwa kikinguruma sauti za ajabi ajabu..

‘Na madalali tayari wameshapatikana,...lakini tukaona haina haja, kuna watu wapo huku wanaotoka nchini kwako, wapo tayari kuinunua hiyo nyumba yako,imekuwa ni rahisi kwetu, tukaona tuwachukue hao hao...’akasema

‘Muhimu ni kujua kuwa pesa itakayopatikana italipa madeni ya watu, kwani madeni uliyo nayo ni mengi sana, hata sikutegemea..., mama mtemi anayo nakala ya orodha ya madeni, hata mimi ninayo hapa...’ akasema akitoa hiyo nakala na akawa anaikagua...

‘Na zaidi ya hapo tutaona jinsi gani tutakavyoweza kuimaliza hii kesi haraka iwezekanavyo...’akasema

‘Kijana wako ameshirikiana nasi na tumeshapata wateja wazuri tu, na nyumba itanunuliwa kwa pesa nzuri tu, na hilo la madeni ya watu utakuwa hunalo tena..utabakiwa kupambana na maamuzi ya hakimu tu...’akasema

‘Sasa kijana sijui una lolote la kusema kwa mzee wako huyo...’akasema akimgeukia huyo kijana wetu, na kijana wetu akaniangalia na kusema;

‘Mimi sina la kusema muhimu ni kuwa madeni ya watu yatalipika, maana sitaweza kuvumilia hilo, na mimi siwezi kujiingiza kwenye hayo madeni ambayo hayanihusu,...’akasema

‘Na waliponiambia niwe mdhamini,nimekubali tu, kushiirikiana na hilo, ili tu kuhakikisha hakuna kinachobaki kama madeni, ...na mengine hayanihusu, hayo umejitakia mwenyewe acha sheria ichukue mkondowake, na hayo yanategemea mahakama itakavyoamua....’akasema

‘Kwahiyo upo tayari kumsimamia mzee wako, na kuhakikisha kuwa nyumba itawakilishwa kwa mnunuaji...?’ akaulizwa

‘Nipo tayari,..mimi sina tatizo kwa hilo, ili kusiwe na kunyosheana kidole kuwa mimi nilikuwa naishi na mtu mwizi, muuaji,...sipendi...’akasema

‘Profesa huu hapa ni mkataba, unaweza kuupitia, kijana wako ameshasoma na kuona kila kitu kipo tayari, iliyobakia ni wewe tu kuweka sahihi yako na nakala moja tutampatia mnunuaji., nyingine nitabakia nayo mimi na nyingine kijana wako kama mdhamini wako..’akasema

‘Ni nani mnunuaji?’ akauliza sasa profesa alipoona hana jinsi

‘Mnunuaji anafahamiana na kijana wako, hilo halina shida, huyo mnunuzi hakuweza kuja huku, unajua wengi hawapendi kuja sehemu hizi ....’akasema, na profesa akaupitia ule mkataba na kuona gharama gani iliandikwa kama thamani ya hiyo nyumba.

Kiukweli..., ilikuwa ni pesa nzuri tu, hata profesa hakutegemea kuwa nyumba yake itauzwa kwa kiasi chote hicho

‘Sasa hii hapa ni orodha ya madeni ya watu...’akaambiwa na kuipokea hiyo karatasi, alishangaa kuona ile pesa yote inaishia kwenye madeni ya watu, na yeye habakiwi na kitu

‘Haiwezekani..kwanini mumefanya hivi,ina maana gani kunifanyia hivi....’akasema

‘Kwanini ...wewe ulitakaje,..kwani hayo madeni huyatambui, je unafikiri yangelipwaje bila kufanya hivyo?’ akaulizwa.

‘Mimi sina madeni kiasi hicho chote, hayo madeni mengine yametokea wapi....’akasema huku akijaribu kuyapitia hayo madeni yaliyoorodheshwa hapo, na mwisho akaona gharama za kuwalipa watu mbali mbali ili kuhakikisha kesi inakwenda vyema

‘Hizi gharama nyingine hapa analipwa nani...?’ akauliza profesa

‘Hayo ya kuwalipia watu ili kuhakikisha kesi inakwenda vyema, sio hongo, ipo kisheria,...kwahiyo isikutie shaka, utakuja kuona mwenyewe huko mbele, sasa hivi huoni tunaimaliza kesi ya mauaji, ndio kazi zake hizo,....’akaambiwa.

Profesa akapewa peni ili aweke sahihi yake, na wakati anasita mara akamuona mama mtemi akija, na nyuma yake yupo yule jamaa aliyekuwa naye chumba kimoja, na wengine aliwakumbuka ni miongoni mwa wale waliokuwa wakimtesa usiku, wakawa wanaongea na mama mtemi..., halafu wale wafungwa wakaondoka,na mama mtemi akawa anakuja pale walipokuwa wamekaa

‘Ameshaweka sahihi maana sina muda tena hapa...’akasema mama mtemi

‘Ndio anaweka sahihi yake...’akasema wakili

‘Nimeshaongea na mkuu wa kituo, na nimeongea na wakuu wa humu na watemi wa humu kuwa sasa ukitoka hapa kama umekubaliana na wazo hilo wasikusumbue, unajua wengi nawafahamu fahamu hasa wale wa zamani....’akasema

Profesa akawa kashikilia ule mkataba, akageuka kumuangalia kijana wake,kijana wake alikuwa katizama chini, hamuangalii usoni, akageuka kumuangalia mama mtemi, mama mtemi akawa anatabasamu kinafiki tu

Akilini profesa akawa anajaribu kuwaza ina maana hii saini hapa ndio itanimaliza kimaisha sitakuwa na nyumba tena, nyumba ambayo inanifanya nionekane mtu nikirudi nyumbani, nyumba niliyoihangaikia maisha yote....akasita


Na wakati huo huo kichwani akawa anahisi kelele, na milio ya ajabu, akahisi kama kuchanganyikiwa, akajua kama anazidi kukaa jela mwaka tu, atakuwa kichaa, alipohisi hivyo, akaishusha peni  kwenye sehemu ya kuweka sahihi,....
Ni mimi: emu-three

No comments :