Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeThursday, September 10, 2015

RADHI YA WAZAZI-40 ‘Kwanini hukuniambia mapema kuwa kijana wangu alikuwepo kwenye hilo jengo....?’ akauliza mkuu walipokutana tena kwenye kikao cha muda.

‘Niliacha hilo, kwa vile sikuona umuhimu naye..ni kijana wako na unamuamini au sio,....nilijua lifika hapo kwa mambo yake tu...’akasema mpelelezi

‘Ndio ni kweli namuamini sana, ndio maana nikashangaa kwanini alifika kwenye hiyo hoteli....,hiyo hoteli nilishamwambia siimanini, lakini ndio ujana, sasa ndio tatizo limetokea, sasa mimi nimeatoka huko kwenye kikao na wakuu, wanasisitizia kesi hii imalizike mapema kuwe na amani kwenye eneo letu, .....mimi naelekea nyumbani, nitaongea na kijana wangu,nijue alifika hapo hotelini kufuata nini,huyo niachieni mimi....’akasema mkuu

‘Sawa mkuu...lakini.’akasema mpelelezi.

‘Lakini nini kwani kuna kitu mumegundua dhidi yake....?’ akauliza mkuu akimuangalia mpelelezi ,halafu muendesha mashitaka

‘Mhh...’mpelelezi akasita, akimgeukia muendesha mashitaka

‘Kwahiyo...unaposema tukuachie wewe, utaongea naye, ina maana kazi zetu tusifanya hapo sikuelewi mkuu?’ akauliza muendesha mashitaka akimuangalia huyo mkuu.

‘Aaah jamani..., nieleweni, nyie endeleeni na kazi yenu kama kawaida, kwani nimewazuia?...hapana sijawazuia, ila huyo kijana nitaongea naye kwanza ili nijue undani wake, kama alifika hapo kwa jambo gani , siunajua mzazi lazima wajibike kwanza au, ....?’akasema mkuu

‘Sawa mkuu,...lakini kuna mambo tumeyagundua ambayo yanahusiana na huyo kijana....’akasema mpelelezi akimuangalia muendesha mashitaka

‘Mambo gani, kuhusu nini....kafanya nini...?’ akauliza akionyesha uso wa kama kukasirika

Tuendelee na kisa chetu

******

‘Mkuu, mbinu zinaweza kutumika,...kama nilivyosema awali, lolote laweza kufanyika ili kuficha ukweli, yanaweza kufanyika mambo mengi kwa wakati mmoja, wakahusishwa watu wengi kwa mambo tofauti, ili tu ukweli usijulikane...’akasema muendesha mashitaka

‘Ndio maana tulianzia kukuonyesha sababu za matukio yote hayo...’akasema mpelelezi .

‘Lakini kama nilivyowaelewa,na kutoka na kesi inavyokwenda  ina maana kuwa mshitakiwa tuliye naye anaondoka kwenye kosa la mauaji, au...?’ akauliza mkuu

‘Bado hatujalithibitisha hilo, muhimu kwasasa ilikuwa kumtafuta huyu mtu mwingine ambaye tumeshagundua kuwa alikuwepo kabla ya mshitakiwa,..na tukimpata itakuwa rahisi sasa kutafuta ni nani aliyefyatua hiyo risasi, iliyomuua marehemu....’akasema muendesha mashitaka.

‘Mshitakiwa, tumemshikilia kwasababu za alama za vidole kwenye bastola, na pia ni kwa vile alionekana akikimbia akiwa kashikilia bastola, na huu ushahidi ni kutokana na kamera za mitaani....au sio?’ akauliza mkuu kama vile anataka kujenag hoja

‘Ndio na pia alionekana akiingia kuelekea eneo hilo kabla ya tukio....na kaandikisha jina kwenye daftari la wageni,....’ akasema mpelelezi.

‘Aliandika jina lake sahihi...?’ akauliza mkuu

‘Ndio, na hili linatufanya tuanze kumuhisi vinginevyo, maana kama alikuwa na nia mbaya, angeliandika jina tofauti....’akasema mpelelezi.

‘Mhh....lakini kuandika jina tofauti yaweza kuwa na mambo mengi, wengine wanaandika wakiwa na malengo yao, kuficha ukweli, kuwa walifika hapo, hasa wanaume uchwara....sio lazima iwe sababu ya kufanya mauaji, au...?’ akauliza mkuu

‘Ndio mkuu....ndio maana tukawalenga wale ambao tunahisi wanahusiana na tatizo hilo,  ndio maana tulianzia mbali kuelekezea sababu...’akasema mpelelezi

‘Na ndio maana mkamkamata huyo mshitakiwa au sio,kutokana na sababu hizo au sio.., huyo na mwenzake mtaalamu mliwaweka kwenye kushukiwa, mkampata huyu jamaa, mtalaamu hamjamuona na makosa bado....au sio?’ akauliza mkuu

‘Ndio mkuu...’akasema mpelelezi

‘Japo tumempata, lakini bado tunahisi sio yeye aliyefyatua risasi iliyomuua marehemu,...’akasema

‘Lakini ni kwa vile tu yeye kapata mtu wa kumtetea, au sio..lakini pia ni kutokana na jeraha kichwani, kuwa kuna mtu alimpiga kichwani au sio,...?’ akauliza

‘Ndio mkuu...’akasema mpelelezi

‘Sasa hii inaashiria kuwa huenda kulikuwa na mtu mwingine aliyefanya hivyo, na ndiye tunahisi anaweza kuwa ndiye muuaji,au sio, ...’akasema mkuu

‘Ndio mkuu...’akasema mpelelezi

‘Na huyu mtu alikuwa kajificha huko juu, mapema sana...na alipita hapo mapokezi kwa jina bandia,...au sio, ...?’ akauliza

‘Sasa kama sio huyu mshitakiwa, ni nani mwingine, wewe unahisi ni nani mwingine anaweza kuwa ndiye muuaji, ni mtaalamu,...eeh, ni huyu jamaa wao wa kamera, au... kwani kutokana na maelezo yako huyu mtaalamu si walikuwa kundi moja,...kwanini yeye hatujamkamata ...?’ akauliza mkuu

‘Hatuna vigezo vya kumkamata Mtaalamu, kwa vile yeye hajafika eneo la tukio hilo kabisa, kuna ushahidi wa kutosha kuwa siku hiyo yeye alikuwa ofisini kwake....’akasema mpelelezi.

‘Basi kuna mtu mwingine alikuwepo hapo kabla, na atakuwa anaufahamu huo mpango wote na mimi nina wasiwasi na huyu anayeshughulika kamera za hapo kwenye jengo...mlimchunguza nyendo zake, ...?’akasema mkuu na kuuliza

‘Ndio tumechunguza nyendo zake,  ana ushahidi kuwa siku hiyo hakufika hapo kwenye hilo jengo,na tumefuatilia na kuona kuwa ni kweli....’akasema muendesha mashitaka.
Muendesha mashitaka akawa anafungua makabrasha yake akitikisa kichwa kama kukubaliana na maelezo ya mpelelezi....halafu akasema.

‘Mkuu kuna kazi ulitoa , ulimwambia mpelelezi atafute huyu mtu ambaye hakuandika jina lake sahihi,naona tusikie kagundua nini...’akasema mpelelezi

‘Ehe, tuambie , umegundua  ni nani...?’ akaulizwa mpelelezi

‘Mwanzoni, tulijua wapo wawili, maana huyu huyu mtu mmoja aliandikisha mara ya kwanza akatoka, na akaja mara ya pili, akitumia jina bandia ...maana ilibidi tuanzie mbali sana kuona kama tunaweza kugundua kitu....’akasema mpelelezi

‘Kwanini kupoteza muda kuanzia mbali, sisi tulihitajia katika hao watano, ni nani hakuandika jina lake sahihi, haya tuambie uligundua ni nani...?’ akauliza mkuu

‘Kama tungeangalia kwa wale watano tu tusingeligundua kitu,...lakini kwa kufanya hivyo, ndio tukamgundua ni nani...’akasema mpelelezi

‘Sasa huenda ambao hawajaandika majina yao watakuwa ni wengi, hivi kweli wanaweza kutusaidia kwenye hii kesi....ok, tuambie ni nani, tusipoteze muda...?’ akauliza mkuu akimuangalia muendesha mashitaka

‘Yawezekana, ikasaidia, maana yeye ni mpelelezi anajua ni nini anachokifanya....’ akasema muendesha mashitaka akiwa keshafungua makabrasha yake tayari kuanza kuandika..

‘Usianze kundika kwanza....nataka tusikie halafu tuone kipi ni kipi cha kuandika, tusije kujichanganya...’akasema mkuu na muendesha mashitaka akatabsamu huku akiwa kashikilia peni yake kama anataka kundika.

‘Ok, ni nani huyo mwingine...?’ akauliza muendesha mashitaka na mkuu akatikisa kichwa kama kulikubali hilo swali.

‘Nilipowauliza hawa wahudumu, au walinzi walikuwepo, iliwawia shida sana kutambua, na ndio nikawaambia hebu kwanza tuangalia nyuma huenda inaweza kuwasaidia ...’akasema mpelelezi

‘Ehe, ikawaje, maana hata mimi moyo wangu unanipa hamasa kuwa huyo mtu anaweza kuwa muhusika ...kwa namna moja au nyingine kwanini hakuandika jina, angalia alivyofanya marehemu, aliandika jina bandia kwasababu alijua anafanya makosa....unaona eeh...’akasema mkuu akimuangalia muendesha mashitaka.

Tuliporudi nyuma tukiangalia ni nani na nani, wengi waliandika majina yao, na wengi wanatambulikana, na kama hatambulikani, tulitafuta mawasilianoa na kugundua ni nani...tulijaribu kuweka muda maalumu, vinginevyo ingechukua mud asana....’akasema mpelelezi.

‘Ndio tukafika kwa huyu mtu, kabla ya muda ule ya watu watano,  mimi nilipoangalia mwandiko tu, nikagundua kuwa unafanana na wale watu watano,nikamuuliza mlinzi ,na malinzi akasema huyo aliyeandika hivyo  ni nani.....’akasema

‘Akasema ni nani...?’ akauliza

‘Mlinzi hakupenda kusema moja kwa moja, nikambana kuwa asipomsema yeye atahusika kwenye kosa la mauaji, na yeye akamtetea kuwa huyo mtu hawezi kuhusika, ila aliandikahivyo kwasababu maalumu...’akasema

‘Inaruhusiwa...?’ akauliza mkuu

‘Hairuhisiwi, ni ushikaji tu, ni kwa vile huyo mlinzi anaelewana na huyo mtu, basi akakubali iwe hivyo tu, ni kosa..hata yeye alikubali hivyo, ila alifanya hivyo, kwa heshima fulani, na kwa kumuamini huyo mtu....’akasema

‘Huo ni upuuzi,..huyu hajui kazi yake...’akasema mkuu

‘Ndio hivyo,..mimi nilipoona huo muandiko haraka nikashuka hadi wale watu watano..ooh,nikagundua kuwa ni yule yule....’akasema

‘Na hapo mlinzi alisema nini...?’ akauliza

‘Kwa muda huo aliyekuwa akishughulikia kuandikisha alikuwa sio yeye, yeye alikwenda mlangoni kukagua watu, na huyu aliyefika baadaye anasema alizongwa sana na watu,kwahiyo hakuwa makini kuangalia ni nani aliandika jina sio lake...’akasema

‘Hilo linakubalika kweli,....?’ akauliza mkuu akimuangalia muendesha mashitaka na muendesha mashitaka akawa anatabasamu tu..

‘Kwa vile nilisha mgundua ni nani kutoka kwa  huyo mlinzi wa kwanza, kazi yangu ikawa ni rahisi tu, kujua ni kwanini alifanya hivyo....’akasema mpelelezi.

‘Na cha ajabu huyu ndiye pia aliyevuruga utaratibu wa saa, yeye ndiye aliweka saa ambayo sio sahihi, na kuleta mvuruganyo, ...hili hawakuligundua walinzi kwa muda huo,kwa dhana ile ya kumuamini, na kumuheshimu kuwa hawezi kufanya kitu kama hicho...’akasema

‘Ni nani huyo,...?’ akauliza mkuu,sasa akionyesha kuwa na mashaka.

‘Mkuu ni Kijana wako,ndio yeye ambaye hakuandika jina sahihi mkuu....’akasema mpelelezi,na kumfanya mkuu atulie kimia kwa muda, na baadaye akatupa jicho kuangalia kama muendesha mashitaka anaandika kitu.

‘Lakini sio yeye miongoni mwa yale majina matano...tulioyahisi kuwa yana matatizo, au sio?’ akauliza mkuu huku akijikuna kichwa kwa kidole

‘Kama nilivyosema mkuu, kama tusingelianzia mbali, tusingeligundua hilo,..ni huyo huyo...kijana wako mkuu...’akasema mpelelezi.

‘Sio kwamba namtetea, nataka tuwe na uhakika , nimemuhoji na nina uhakika alifika hapo na mambo yake ya ujana...na hilo la kuandika jina sio lake sikuwa na haja ya kumuuliza kwani sikuwa na shaka,sikutarajia kuwa anaweza kufanya hivyo...’akasema mkuu

‘Hata walinzi walisema hivyo,...’akasema mpelelezi, na muendesha mashitaka akawa anaandika, hakuwa ametii ile amri kuwa asindike kwanza

‘Lakini kwa maelezo yake alifika hapo kibiashara zaidi na mambo ya ujana, ...nimemuhoji, nikarizika naye, hana baya alilofanya, labda huko kukiuka taratibu za kuandikisha jina sio lake...’akasema mkuu

‘Ndio mkuu, lakini maelezo tuliyopata hapo yanatuweka kwenye sehemu ya kuamini kuwa kijana wako anaweza kuwa anajua kitu kutokana na tukio hilo,....’akasema muendesha mashitaka

‘Kwa vipi....?’ akauliza mkuu akigeuka kumuangalia muendesha mashitaka

‘Tumeongea na kijana rafiki mwenzake, ili kuona kama walikuwa na mipango ya pamoja lakini mwenzake alisema yeye alitumwa na mama mtemi, kumsubiria mshitakiwa, akitoka amkabili waongee naye...’akasema

‘Kuhusu nini...?’ akauliza mkuu

‘Kuhusu kama alifuata pesa, na kama ni pesa,...mama mtemi anamdai pesa nyingi marehemu , kwahiyoo akizipata tu, mama mtemi atamfuata ili aweze kulipwa deni lake.....’akasema mpelelezi

‘Kwanini amtumie huyo kijana...?’ akaulizwa

‘Kijana anampenda binti wa huyo mama, na yupo tayari kufanya lolote ili kumrizisha huyo mama.. kwa ajili ya binti yake...’akasema muendesha mashitaka

‘Lakini kijana huyo hakusema lolote kuhusu kijana wangu kuwa anaahamu kuwa alikuwa na jambo lolote, zaidi ya kuja hapo kwa ujana wake,...au huyu kijana wamshitakiwa kuna lolote aliongea ...?’ akauliza mkuu

Muendesha mashitaka akakohoa kuashiria kuwa anataka kuongea, na wote wakamgeukia na muendesha mashitaka akasema,;

‘Siku tulisema tuangalie waliondika majina ya bandia ,na pili tuangalie wenye utaalamu wa mitambo ya komputa....kijana wako ana hayo  yote mawili, kutokana na uchunguzi wa mpelelezi na mimi niliamua tufuatane ili niweze kuwa na uhakika kamili

‘Japokuwa sikuwepo muda wote,....niliondoka na kumuacha mpelelezi akiendelea, lakini kijana anaonekana ana makosa......’akasema

‘Kwa vipi?’ akauliza

‘Kama alivyosema mpelelezi,...yeye ndiye aliyeandika jina bandia,....ulitoa amri tumtafute ni nani,.... yeye ndiye aliyeandika saa isiyo sahihi, ....swali hapo ni kwanini afanye hivyo,...najua kwa vile alikuwa na sababu zake, anaweza kujitetea vyovyote,..’akasema muendesha mashitaka.

‘Na unakumbuka, tulikuwa tunamtafuta mtu aliyekuwepo hapo, ambaye ni mtaalamu wa mitamboya kamera,....kijana wako ni mtaalamu wa mitambo ya kamera...’akasema muendesha mashitaka,hapo mkuu akanywea, akakunja uso kama anawaza jambo fulani.

‘Ok, .....Lakini haiwezi ikawa ni sababu ya msingi ya kumshuku yeye, au sio, ukitizama sababu zenu mlizokwisha kuzitaja huko nyuma...simtetezi, mnielewe hivyo,..’  akasema mkuu

‘Ndio mkuu, na sisi tulichofanya ni kutelekeza yale uliyoagiza, na katika kufanya hayo ndio tukaligundua hilo.....’akasema mpelelezi

‘Kiukweli mlivyofanya ni sahihi kabisa, siwalaumu,...ila , ninachotaka mimi ni ili tuwe na ushahidi..mimi nimeongea naye,...nilikaa naye nikaanza kumuhoji, nikiwa naongea sio kama baba, kama mtu wa usalama anayetimiza wajibu wake, ...amekiri kufanya makosa....’akasema

‘Makosa gani mkuu,....?’ akauliza mpelelezi

‘Hayo ya kuandika jina lisilo lake....’akasema mkuu

‘Hilo tu....’akasema muendesha mashitaka

‘Mengine ni utoto hayana maana na wala hayahusiani na kesi yetu....’akasema mkuu, lakini ni vyema mukaongea naye tu, siwazuii, mnaweza kufanya kazi yenu, ila nina uhakika na maelezo yake, hana zaidi kuhusiana nah ii kesi...’akasema mkuu.

‘Hebu mpelelezi aeleze zaidi aliyoyagundua kabla na mimi ijayaelezea ya kwangu...’akasema  muendesha mashitaka

‘Kijana wa mshitakiwa alipofika alikutana na kijana wako, wakasalamiana, na baadaye kijana wako aliaga kuwa anatoka kuna kitu anafuatilia,..’akasema mpelelezi

‘Alisema ni kitu gani, kupitia kwa kijana wa mhitakiwa...?’ akauliza muendesha mashitaka

‘Alisema ana dili anafuatilia, ....kijana wa mshitakiwa anasema hakuwa na zaidi ya kuongea naye kwani yeye alifika hapo na mambo yake...basi kijana wa mkuu, akapandisha kuelekea juu,.. ‘akasema mpelelezi

‘Na nilipowahoji walinzi, huko juu ilikuwa  ni mara ya pili kwenda kwa siku hiyo, alipanda mara ya kwanza akakaa kidogo huko juu , baadaye akarudi na aliporudi ndio akaja kukutana na huyo kijana wa mshitakiwa,...’akasema mpelelezi

‘Ok, endelea...’akasema muendesha mashitaka, alitaka kuuliza kitu lakini akaona haina haja kuuliza kwa muda huo.

‘Na hii mara ya pili ndio akamwambia kijana wa mshitakiwa kuwa kuna kitu anafuatilia huko juu, alimwambia kuna dili,...ni dili gani, au huko juu alimfuata nani, tutasema ndio huo ujana, labda alikuwa na miadi ya binti au sio, huyo binti ni nani,...’akasema muendesha mashitaka

‘Lakini mimi kwa kauli yake alianiambia kuwa, kuna msichana muhudumu wa humo, mara nyingi huyo msichana anafanyia sehemu ya juu ya hilo jengo,...na kwa kuhakiki, niliwapigia simu hao utawala, sikutaka kuongea na huyo binti, na wao wakaniambia ni kweli msichana huyo yupo...’akasema mkuu

‘Ndio msichana huyo yupo, lakini hana urafiki wa akribu na huyo kijana wako, ...tuliongea na huyo msichana akasema ni kweli alimuona huyo kijana akipita akampungia mkono, lakini hawakukaa kuongea, yeye alikuwa na kazi nyingi hakuwa na muda wa kukaa kuongea na mtu...’akasema mpelelezi

‘Ndio hivyo, kijana kaniambia alitaka siku hiyo aongee naye, lakini akamkuta huyo binti ana kazi nyingi, kwahiyo akazuga,..kama alivyosema na kurudi kuondoka zake,...’akasema mkuu

‘Ok, sasa kitu kingine tumechunguza alama za vidole zilizopatikana humo ndani, hatukuweza kupata alama ya mtu mwingine....’akasema mpelelezi

‘Ndani wapi...?’ akauliza mkuu

‘Chumba cha mitambo hiyo ya kamera la hilo jengo, tulitaka kuona kama tunaweza kuona ni nani mwingine aliweza kuingia humo..’akasema mpelelezi

‘Sasa tukaona tuangalize zaidi, tukawa tunatafuta kila mahali kama tunaweza kupata alama za mikono, zilizoachwa, alama mpya kuacha za watendaji wa humo, na kwenye kitasa cha mlango,  tukagundua kitu...kwenye mlango wa kuingilia, tulipata alama ya dole gumba jipya ...’akasema muendesha mashitaka

‘La nani...?’ akauliza mkuu kwa shauku

‘La kijana wako mkuu, unajua watu hujitahidi sana kuwa waangalifu, lakini kuna kosa dogo, hutokea....’akasema muendesha mashitaka

‘Ndio aliniambia kuwa alipofika hapo alitaka kuongea na mtaalamu wa hapo, kuna mambo waliongea kuhusu kazi zao,...hawa wataalamu huwa wanashirikiana sana na alifika hapo kumsalimia na kuongea mawili matatu, ...nahisi hapo ndio aligusa mlango, na kuona umefungwa...’akasema mkuu

‘Kwa dole gumba tu!? Kwanini isiwe kiganja cha mkono, kama alinyonga kitasa kufungua...?’ akauliza muendesha mashitaka.

‘Yawezekana....si unagusa hivi kujaribu kitasa...kwanini unauliza hivyo, ...kuna shaka yoyote dhidi yake....?’ akauliza mkuu

‘Na kwenye chumba alichokuwa marehemu tulitambua alama hiyo hiyo ya dole gumba...’akasema mpelelezi na mkuu, akatoa macho ya kushangaa.

What!..’akasema hivyo tu

‘Na,kwenye mlango na mezani ndani ya hicho chumba alichokuwa marehemu... nahisi soksi aliyokuwa amevaa au kitambaa alichokuwa akitumia kuzuia mikono yake haikuweza kusitiri dole gumba....’akasema mpelelezi na mkuu akaduwaa

‘Una uhakika....?’ akauliza mkuu na muendesha mashitaka akatoa makabrasha yake na kuonyesha hiyo alama ya dole gumba na wapi ilipatikana..

‘Nimethibitisha hilo mkuu, na kiukweli kijana wako anatambua jambo,...na huenda anahusika kwa namna moja au nyingine...au walikutana na marehemu wakaongea, kama waajuana, au .....lolote jingine!’akasema muendesha mashitaka, na mkuu akakunja uso akigeuka kumuangalia mpelelezi. Mpelelezi akawa anamuangalia muendesha mashitaka.

‘Huenda alikuwa akimtafuta huyo jamaa wa kamera, akaingia hadi huko, huenda alikutana na marehemu wanajuana wakawa wanaongea, kama ingekuwa hivyo, akakuelezea hivyo, tungerizika, .... lakini tulikuja kugundua kitu kingine zaidi..’akasema muendesha mashitaka

‘Mpelelezi alipogundua hilo akanipigia simu, nikafika na tukachunguza sasa kwapamoja kujirizisha,...kiukweli ugunduzi huu sasa ulitutia mashaka mpaka tufikie kuamini kuwa huyu kijana anahusika kwa namna moja au nyingine.....’akasema muendesha mashitaka

‘Kitu gani...?’ akauliza mkuu sasa akitoa sauti kavu

‘Mkuu.., unakumbuka kwenye ile silaha,... tulikuwa tumegundua alama ya dole gumba, tukawa hatujagundua ni alama ya nani, ....’akasema kama anauliza.

‘Unataka kusema nini..!?, Kuwa hiyo alama ya dole gumba ni ya kijana wangu, haiwezekani? ...yule kijana hawezi....namfahamu sana....hapo kuna makosa, lazima kuna makosa ....’ akasema mkuu sasa akigeuza kichwa huku na kule.

‘Alama ya dole gumba hilo ni ya kijana wako mkuu...hilo tumethibitisha na pia imeonekana kwenye ule mfuko tuliokuta umetupwa kwenye ngazi za kupandia...’akasema mpelelezi

‘Kwenye mfuko ambao tunasadiki ndio ulikuwa na pesa....’akasema muendesha mashitaka

‘Unasema......oooh, ....yawezekana wakati anapita aliuona hu mfuko akaugusa, lakini mna uhakika kwenye hiyo bastola....kuna alama yake?’mkuu akashika kichwa akionyesha hasira

‘Kwenye hiyo bastola, ...kuna alama ya dole gumba ya kijana wako mkuu....’akasema mpelelezi

‘Inanipa shida kuamini, nimeongea naye, na hakuonyesha wasiwasi wowote, maana namfahamu akiwa na makosa anakuwa na wasiwasi, na mimi kama mzazi ningelitambua hilo,..sina uhakika kama anaweza kuhusika,...kuna kitu kinaendelea kwenye hii kesi...!’ akasema mkuu sasa akishindwa kuzuia hisia zake.

‘Ni kweli mkuu, hata sisi tunahisi kuna kitu...kwani kila tunavyozidi kuchunguza mengi zaidi yanaanza kujitokeza, hata wale tusiowategemea wanahusika....’akasema mpelelezi

‘Nani mwingine zaidi.....?’ akauliza mkuu

‘Kiukweli mkuu, hatukutegemea kukuta alama za kijana wako kwenye hiyo bastola iliyotumika kumuua marehemu! Na hili linatupa fundisho kuwa kwenye kosa usimwamini kila mtu,...’akasema mpelelezi

‘Lakini kwa kijana wangu,...aaa hata sijui, nitamueleza nini mama yae anielewe, lakini ngoja , niongee naye, nahisi kuna kitu...’akawa anatikisa kichwa kuonyesha uchungu fulani.

‘Mkuu hakukuambia hilo ulivyomuhoji, kuwa anahusika, kuwa alifanya lolote, tunashindwa kujua, hiyo bastola ilifikaje mkononi mwake,je ndio yeye aliua, au kulitokea nini zaidi....?’ akauliza mpelelezi, na kabla mkuu hajajibu,muendesha mashitaka akasema

‘Na kwahiyo tulikuwa tunaomba tuongee na huyo kijana,ili tuweze kumuhoji vizuri sisi wenyewe bila ya wewe kuwepo, tutaweza kugundua mengi, kuliko wewe ukiwepo....’akasema muendesha mashitaka.

‘Kiukweli, niliongea naye, namjulia, ni kijana wangu, najua wapi akiongea vipi ananificha kitu, lakini safari hii ilikuwa tofauti, anajiamini,...kiukweli, hata, nahisi kuna kitu, kuna makosa, ....aah,....’Na mara simu ya mkuu ikaita, na mkuu akaiangalia na kusema;

‘Tena ndio huyu hapa ananipigia, ....ngoja niongee naye...’akasema akisimama kuondoka hapo mezani ,kuashiria kuwa hakutaka wenzake wasikie anaongea nini na kijana wake, na wawili hawa wakaangalia bila kusema kitu.


WAZO LA LEO: Unapopewa dhamana ya kutenda kazi fulani kwa mujibu wa sheria, timiza wajibu wako bila kujali ni nani unayemkabili, timiza wajibu wako kwa misingi na sheria na kanuni zinazokulinda, usiangalie kuwa unayekabiliana naye ni bosi wako, au fulani, hata kama ni bosi wako kakiuka sheria, au jamaa zake, usione hofu kutimiza kumkabili ukisimamia kwenye haki. Haki na ukweli ndio utakaokulinda..


Ni mimi: emu-three

No comments :