Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeMonday, August 31, 2015

RADHI YA WAZAZI-36

                                
‘Bro,... sitakuelezea ilivyokuwa kwa mashidi wengine ambao waliitwa kuonyesha kuwa Profesa ndiye muuji, ....mimi sasa nitaenda moja kwa moja kwa muhusika wetu...’akaendelea kusimulia mdogo mtu.

‘Muhusika wetu?’ akauliza kaka mtu

‘Siunajua kesi kama hiyo, wanaanzia mbali, ...na wanawaita watu mbali mbali, waliitwa walinzi na wahudumu wa jengo hilo, maaskari waliokuja badaye, dakitari...na ujue jengo hilo ni kubwa na lina shughuli mbali mbali, kwahiyo walitafuta kila mtu aliyeniona,...

Kwa ushahidi uliotolea, kila mtu aliamini kuwa profesa ndiye aliyefanya hayo mauaji, ...

‘Bro, nilikiona kitanzi hicho....na moyoni nikawa naomba angalau aje shahidi ambaye atatoa ushahidi wa kuniokoa, , ....maana wote waliopita walikuwa wakinikandamiza mimi , japokuwa wakili mtetezi alijitahidi sana kunitetea, lakini ilionekana wazi mimi ni muuaji...’akasema mdogo mtu akiendelea kumsimulia kaka yake.

‘Nikuulize kwanza mdogo wangu je kweli wewe uliua..?’ kaka mtu akauliza swali na mdogo mtu akatabasamu, na kusema...

‘Bro....tuendelee na kisa chetu,....utaona mwenyewe.....’akasema

‘Sasa ilikuwaje kwa kijana wetu hakuitwa tena kutoa ushahidi..?’ akaulizwa

‘Aliitwa, ndio maana nasema tutakwenda moja kwa moja kwa muhusika wetu, kuliko nikianza kuelezea kila alichoongea shahidi, mashahidi walikuwa ni wengi, na waliongea mengi sana....’akasema

‘Nimekuelewa, ....endelea....’akasema kaka mtu

‘Wengi, ....walitarajia,...labda,  kijana wetu , kwa vile nilimlea mimi angeonyesha utu wa kunitetea, angalau kidogo, ikionekana kuwa mimi nakabaliwa na kosa la mauaji, ...kiubinadamu angelitakiwa kuonyesha angalau huruma fulani.

‘Lakini kama uliua, ni nani angekuhurumia,...usimlaumu bure.....’akasema kaka mtu, nay eye hakujali kauli hiyo akaendelea kuongea

‘Na hata mimi moyoni niliomba hivyo,.....aonyeshe moyo wa huruma, angalau aonyeshe msaada fulani,.... japokuwa alikuwa upande wa mashahidi wa wanaoshitaki....

Na wakati nawaza hayo mara nikasikia.....

‘Tunamuita tena shahidi wetu, kijana yule aliyewahi kuishi na mshitakiwa, .....’nikasikia akiitwa kijana wetu, nikiwa nimezama kwenye dimbwi la mawazo....

Tuendelee na kisa chetu........

*************

Kijana wetu alikuja na safari hii hakuonekana na zile mbwe mbwe zake za awali za kunata na madharau, safari hii alionekana mtaratibu na adabu kidogo...

Alifuata taratibu zote za mahakamani, na  akaanza kuhojiwa na muendesha mashitaka kama ilivyo ada..., na hakutaka hata kunitupia jicho, kwani pale nilipo nilikuwa namuangalia kwa jicho la kutia huruma.

‘Wakati unaishi wewe na huyo mlezi wako, uliwahi kumuona mlezi wako huyo, akiwa na bastola...?’ akaulizwa swali, swali lililonifanya nihisi kitu kama kichoma ndani ya moyo. 

Ukumbuke nilishawaambia watu wa usalama walionihoji kuwa mimi sijui kutumia silaha, hasa bastola.

‘Ndio, ...niliwahi kumuona akiwa nayo,....’akasema shahidi moyoni nikasema sasa nimekwisha.

‘Alikuambia bastola ni ya nini.....? akaulizwa, nilitamani shahidi aniangalia ili nimuonyesha ishara ya kuwa asiseme lolote.

‘Alisema bastola hiyo ni ya kikazi, na wakati mwingine huazima kutoka kwa jamaa zake,.....anasema wakati mwingine bastola hiyo anaitumia kuwatishia wale wanaokataa kutoa pesa yake, .....’akasema na watu wakaguna.

‘Kwahiyo aliwahi kukuambia kuwa anaweza kuitumia hiyo silaha...?’ akaulizwa

‘Ndio alisema anaweza kuitumia, na mimi nilimuomba anifundishe, akawa ananionyeshea kuwa ukitaka kufyatua risasi unavuta hiki unalenga hivi....akanionyeshea lakini hakuwahi kunionyesha kwa vitendo.....’akasema

‘Ukisema kwa vitendo una maana gani...?’ akaulizwa

‘Yaani kuifyatua hiyo bastola na kutoa risasi.....’akasema

‘Aliwahi kukuonyesha risasi zake,...?’ akaulizwa

‘Ndio alinionyesha hata jinsi ya kuziingiza hizo risasi kwenye hiyo bastola...’akasema

‘Kwahiyo yeye, alikuambia bastola ya kikazi anapewa na wahusika, au wakati mwingine anaazima, je akiazima huwa anaazima kwa nani...?’ akaulizwa

‘Alisema huwa anaazima kutoka kwa marafiki zake, anaojuana nao, hasa wale anaofanya nao kazi, ...’akasema

‘Anaofanya nao kazi ni akina nani  hao, ....!? Alikuambia kazi gani?’ akaulizwa

‘Aliniambia yeye wakati mwingine anafanyakazi ya ulinzi na watu wengine....kwahiyo anapewa silaha kwa ajili ya kufanikisha ulinzi huo,  na wakati mwingine anakuwa hana kazi, lakini inatokea anahitaji silaha na hayupo kazini, basi hapo huwa anaazima kutoka kwa marafiki zake, ambao kwa muda huo, wanakuwa na silaha....’akasema

‘Hakukuambia ni kwanini ahitajie silaha wakati hayupo kazini, au kwanini alihitajia hiyo silaha?’ akaulizwa

‘Ni wakati akikusanya pesa zake kwa watu anaowadai, huwa anasema ni muhimu kwenda na silaha.....’akasema

‘Ina maana huwa anakusanya pesa nyingi sana mpaka ahitajie silaha,..? Ni pesa zake kutokana na biashara ya madawa au kutokana na nini...?’ akaulizwa

‘Aliniambia kuwa yeye huwa na wateja wake, anaowadai kwa shughuli mbali mbali, kama vile walichukua madawa kwake na shughuli mbali mbali, lakini mimi nilijua tu ni hao anaowadai kwa mlungula, japokuwa hakuweza kuniambia hivyo moja kwa moja...’akasema na watu wakacheka.

‘Alikuambia hivyo...au wewe mwenyewe ulifikiria hivyo?’ akaulizwa

‘Alitumia kauli ya wadeni wake anaowawajibisha kwa uchafu wao, sasa I nani kama sio hao....’akasema, na muendesha mashitaka akasimama na kwenda sehemu yenye vidhibiti vya ushahidi akachukua bastola.

‘Hebu angalia hii silaha,ni silaha gani hii..?’ akaulizwa, shahidi akaiangalia na kusema.

‘Ni bastola.....’akasema

‘Uliwahi kuiona kabla...?’ akaulizwa

‘Ndio, ila sina uhakika kama ndio yenyewe..., lakini zote zinafanana hivyo, aliwahi kunionyesha kama hiyo lakini sina uhakika kuwa kweli ndio hiyo.....’akasema

‘Kwahiyo uliposikia kuwa mlezi wako huyo wa hadaa kaua hukuona ni bahati mbaya, kwa jinsi alivyokuambia, na ulivyoona kuwa alikuwa na silaha kaam hiyo, na angeliweza kuazima kwa marafiki zake, na angeliweza kuitumia, kama mtu angelikataa kumlipa pesa yake...?’ akaulizwa japo swali liliwekewa pingamizi, lakini baadaye ilitakiwa lijibiwe, shahidi akasema

‘Kwakweli mimi sikuona ni ajabu maana aliwahi kuniambia yeye mbele ya pesa yake, haogopi kuivuta hiyo trigger, hasiti kuua,..kama mtu anamdai pesa yake akakataa, atamtishia akileta ubishi, phaaah...’akasema akionyeshea kwa mkono ishara ya bastola.

‘Inatosha kwa hivi sasa, muheshimiwa hakimu kama wakili mtetezi ana maswali kwa shahidi aendelee....

Hakimu akawauliza watetezi kama wana maswali ya kumuuliza huyo shahidi, na wakili mtetezi akasimama, na kumsogelea huyo shahidi;

‘Unakumbuka kuna siku mlezi wako aliitwa shuleni, ukiwa umekosea, ulipokuwa na makundi ya vijana wa mitaani,....’akawa anaelezewa

‘Umeanza yale yale ya utotoni,...’akalalamika shahidi

‘Unakumbuka  siku mlipokamatwa hadi kufikishwa polisi, unakumbuka mlionekana na kitu gani...?’ akaulizwa na huyo shahidi akashituka, na kusema;

‘Muheshimiwa... nilishakuambia kuwa kipindi kile ulikuwa ni utoto...sikuwa na akili za kuelewa kitu, na hayo hayana maana kwangu kwasasa,wewe nai mwanasheria, unajua umri kama ule hauna maana yoyote kisheria....’akasema shahidi

‘Usinifundihe sheria, najua ni kwanini nakuuliza hivyo, wewe jibu swali je siku mlipokamatwa mlikutwa na vitu gani......’akaulizwa

‘Na ...na sigara, si sijui na kitu gani.....’akatulia

‘Kila kitu kipo kwenye maandishi hapa unatakiwa kujibu ukweli mtupu, sema ulikutwa na vitu gani...?’ akaulizwa

‘Bangi, sigara na na ba-ba-stola....lakini ilikuwa ni bastola bandia....’akasema na watu wakacheka

‘Ina maana polisi hawajui kuwa ni bastola bandia,waliandika uwongo, au? Ujue mahakamani,  au uniambie kama walichokiandika kwenye hizo nyaraka zao ilikuwa ni uwongo, walikusingizia...?’akauliza

‘Lakini nimekuambia kipindi kile nilikuwa sijatulia,..kwahiyo sikuwa na akili za kutambua kuwa ni bastola halisi au ni bastola bandia...na siku zilivyokwenda nikaja kujitambua, nikaachana na tabia hiyo, nikawa nasoma,hata walimu walikuja kunishangaa nilivyokuja kubadilika...’akasema

‘Najua kuwa ulikuja kubadilika, baada ya juhudi kubwa za mlezi wako huyo, ila swali langu ni hili,..je kwa umri huo, unaouita wa utoto, ulikuwa huweze kutambua bastola halisi na bandia au sio?’ akaulizwa

‘Ndi-o...’akajibu kwa kusita

‘Je ulijuaje kuwa bastola aliyokuwa nayo mshitakiwa ilikuwa bastola  halisi na sio bandia...au walikuambia hao waliokufundisha kusema hivyo?’ akaulizwa

‘Yeye mwenyewe mshitakiwa ndiye aliniambia kuwa hiyo bastola ni bastola halisi ni hatari, ndio maana hakutaka mimi mwenyewe niishike...’akasema

‘Hebu utkumbushe tena, ni nani aliyekusaidia wewe kubadilia, na kutulia kwenye masomo yako,... mpaka ukawa mtoto mwema, na ukaweza kufuatilia masomo yako, ukaacha utundu, na mambo ya kuiga, kama hayo ya kuvuta bangi, kujiunga na makundi ya kihuni,..na hata akili  za masomo zikaongezeka, ...?’ akaulizwa na akawa kainama chini.

‘Unatakiwa ukinijubu uniangalie, kwanini sasa unainama chini, hujiamini tena,  haya, sema ukweli wako,na ni vyema ukasema ukweli ukumbuke umeapa kuwa hapa utasema ukweli ,ukweli mtupu, ...?’ akaulizwa na hapo akageuka kumuangalia mshitakiwa

‘Ni yeye...mbona nilishajibu hilo swali kabla, ni kweli sio kwamba muda wote alikuwa mtu mbaya,....kuna siku kama hajalewa, anakuwa akinielekeza mambo mema, niishi vipi, nisome, na vitu kama hivyo...’akasema sasa akamwangalia mshitakiwa.

‘Wakati unafanya utundu, ukiwa na makundi mabaya, hamukuwa mnafundishana jinsi ya kuitumia silaha, bastola,....mpaka ikafikia mmoja wenu akajeruhiwa....?’ akaulizwa na akashituka

‘Hayo ni mambo ya kitoto,...ndio mmoja aliumia, ....ndio maana hata tukaja kukamatwa na polisi, ni mambo mengi ya utoto, mengine siyakumbuki...hata wewe  mambo kama hayo uliwahi kupitia...’akasema

‘Tulipitia lakini sio ya kihuni, hadi kuwa na bastola za moto....’akasema wakili halafu akauliza swali

‘Wewe uliwahi kuwashinda wenzako kwa shabaha, umesahau...?’ akaulizwa na hapo akatabasamu, na kusema;

‘Ndio, lakini yalikuwa mambo ya  utoto, ni mambo ya kupita tu, ya kuiga, na kiukweli nilipojifahamu nikawa sitaki tena mambo hayo....’akasema

‘Kwahiyo kumbe ulikuwa unafahamu kutumia bastola,... sio kweli kwamba wewe ulifundishwa na mshitakiwa, na huenda hata kwa mlezi wako huyo, hukuwahi kumuona na bastola,..labda alikuwa na bastola bandia tu, ila umeambiwa useme hivyo, kwa vile unataka mshitakiwa aonekane ana hatia,au sio....?’ akaulizwa na akakaa kimia

‘Seme ukweli hutalaumiwa na yoyote ukiongea ukweli, ni kweli ulifundishwa kusema hivyo au sio,?...’akasema wakili

‘Sijaambiwa nisema hivyo, muulizeni mwenyewe mshitakiwa kama hakuwahi kunionyesha bastola...’akasema kwa sauti ya ukali.

‘Lakini alikuambia ni ya kikazi au sio,....na yeye aliwahi kufanya kazi za ulinzi...au sio...., na aliruhusiwa kuwa na bastola, au sio?’ akaulizwa

‘Ndio aliniambia hivyo...’akasema

‘Ila hayo mengine kuwa angeliweza kuitumia, kwa wadai wake, uliambiwa useme hivyo au sio...?, ‘ akaulizwa na kukaa kimia

‘Mimi sio mtoto mdogo wa kuambiwa nisema hivi au vile, mimi ni msomi naweza kujua ni kiti gani niseme..’akasema kwa sauti ya ukali

‘Sasa kwanini nikikuuliza swali unakaa kimia...?’ akaumuuliza

‘Maswali yako yanakera,..ni ya kujirudia rudia kunitega,...’akasema

‘Lakini ni kweli kuwa kuna mambo umefundishwa kusema, ndio maana unakaa kimia, ukitafakari au sio, hebu tuambie ni nani alikufundisha hivyo, ..?’ akauliza na wakili muendesha mashitaka akaingilia kati kuwa wakili mtetezi anamlazimisha shahidi kuongea anachotaka yeye, na hayo anayoyauliza hayana msingi na kesi yenyewe..

‘Sina zaidi kwa shahidi huyo, ...’akasema wakili na shahidi akaambiwa na muendesha mashitaka kuwa ushahidi wake umekamilika akihitajika tena anaweza kuitwa...

Shahidi huyo alitoka pale sasa akiwa kainama chini hakutaka hata kuwaangalia watu, akatembea hadi mlango wa kutokea halafu akageuza kichwa kuangalia kule alipokaa mshitakiwa, akatikisa kichwa... na kuondoka kuelekea chumba cha mashahidi.

‘Shahidi mwingine....’hakimu akasema akiangalia saa yake.

 ‘Siku hiyo bro, kila mmoja alijua mimi siwezi kukwepa kitanzi, na hadi siku hiyo, sio kwamba kesi iliendeshwa kwa siki moja, ilikuwa inaendelea kwa siku kadhaa, lakini walitaka iishe haraka, ili kama walivyodai, eneo lao liwe na amani, na siku walikuwa wamebakiwa mashahidi wachache  tu

‘Na kwa ujumla hao waliokuwa wamebakia, ilikuwa ni kama kuhitimisha tu,....kwakweli hadi hapo nikajikuta sasa nikijua mimi ni wa kifungo cha maisha kama sio kunyongwa,  nilitamani kulia, ...kidume mie....’akasema

‘Kwanini utamani kulia, na wakati wewe mwenyewe ndiye ulijitakia kwa uroho wako,....?’ akamuuliza kaka yake

‘Bro sio uroho,  ni kutafuta maisha,...’akasema

‘Haya bro, ngoja nipumzike, tukija kukutana nitakusimulia ili uone ushahidi uliofuta kwa jinsi ulivyokuja kubadili mambo,..’akasema

‘Na kijana wetu hakuitwa tena,...?’ akauliza kaka mtu

‘Utakuja kuona huko mbele, uone mwanao alivyo na roho mbaya,....sijui karithi kutoka wapi...’akasema kwa sauti ya hasira

‘Hahaha...umeona eeh,...na umesahau kuwa yeye ndiye aliyekuwa akikulisha kwa miaka sijui mingapi, ukawa unatumia pesa ya wafadhili kwa mgongo wake,vya bure hulemeza, na ukivikosa unaweza kulalamika kama vile ni halali yako....’akasema kaka mtu

‘Sasa huyo wakili mtetezi alikuwa akimlipa nani, ....maana ulisema huna pesa, au ndio hizo pesa ulizochukua za mlungula....?’ akaulizwa

‘Bro,...utakuja kuuona, na  hutaamini ukija kuwasikia mashahidi hawa waliokuja kuitwa baadaye , na hasa pale walipokuwa wakihojiwa na wakili mtetezi....’akasema

‘Haya endelea...’

‘Tutaendelea lakini sio leo nimechoka,acha nipumzike, si unajua mimi ni mgonjwa...’akasema msimuliaji

NB: Tutaendelea sehemu ijayo


WAZO LA LEO: Katika maswala la mlinganyo,...kutafuta haki,  yenye kuamua mambo ya pande mbili, ili kupata ukweli, na kutoa maamuzi yenye busara, ni vyema, ukawa huegemei upande wowote, hata kama mmojawapo ni rafiki yako, mwenzetu, au hata kama ni upande wako, au hata kama ni ndugu yako, kwa nia njema, unachotakiwa ni kusikiliza sehemu zote mbili bila kujali upande wowote.  Halafu ndio utoe maamuzi kwa uadilifu.
Ni mimi: emu-three

No comments :