‘DNA, sio ushahidi sahihi.....?’
akauliza wakili mtetezi, akimuangalia wakili muendesha mashitaka aliyekuwa
akiikagua ile karatasi, na wakili muendesha mashitaka akasema.
‘Kila kitu chawezekana mbele ya
wanadamu .....’
‘Lakini sio kwa vipimo kama hivyo,
hiyo ni DNA, na imesainiwa na dakitari bingwa anayefahamika,.. ‘akasema
‘Kama unaitoa kama ushahidi fuata
utaratibu,.... lakini kwa hivi sasa siwezi kuikubalia karatasi kama hii kuwa ni
ushahidi...haina vigezo stahiki....’akasema muendesha mashitaka huku akiwa
kaishikilia ile karatasi, akawa anatembea kuelekea sehemu yake ya kukaa, na
wakili mtetezi akasema
‘Sijaikabidhi hiyo nyaraka kama
ushahidi muheshimiwa ....’akasema wakili mtetezi na muendesha mashitaka akawa
bado kaishikilia ile karatasi akiikagua,
wakati huo wakili mtetezi alikuwa kamkarabia, na kunyosha mkono kutaka kuichukua
ile karatasi,
Hakimu alipoona ile hali akasema;
‘Taratibu zifuatwe mawakili....kama
ni ushahidi ukabidhiwe kiutaratibu, sitaki kuwafundisha kazi najua mnaelewa ni
nini kifanyike kwa taratibu za kimahakama.....’
‘Muheshimiwa hakimu natambua kabisa
bado muda wangu wa kutoa ushahidi , niliitoa tu kumuweka sawa huyu shahidi ili atambue
kuwa hapa ni mahakamani, na anachotakiwa ni kusema ukweli, na ajue kuwa hapa
kuna mawakili wanasheria, wanaotambua kazi yao vyema....’akasema wakili huyo
akimuangalia huyo shahidi na huyo shahidi akawa kainama chini.
‘Wakili mtetezi endelea na maswali
yako kwa shahidi...’akasema hakimu
Wakati huo wakili mtetezi alikuwa keshaichukua
ile karatasi akawa nayo mkononi, huku akimsogelea shahidi, na shahidi alikuwa kainama chini, kama anawaza jambo,....
Tuendelee na
kisa chetu....
**************
‘Upo tayari
tuendelee na maswali yangu....’wakili mtetezi akauliza huku akimwangalia
shahidi na tabasamu mdomoni, na shahidi akainua kichwa kumuangalia wakili huyo
akasema;
‘Nipo tayari
muheshimiwa...’ na alipotamka maneno hayo wakili mtetezi akasema
‘Good, safi kabisa,..Sasa unaanza
kuelewa, na kuheshimu mahakama, hapa hatutaki kiburi na dharau, kijana anaanza
kuelewa..’akasema wakili mtetezi akimgeukia wakili muendesha mashitaka na
wakili muendesha mashitaka alikuwa akibonyeza bonyeza simu yake yaonekana
alikuwa akiwasiliana na mtu kwa njia ya ujumbe wa maneno.
‘Kama
mlivyoona shahidi huyo alikuwa akidanganya, na inasikitisha kuwa amefikia
hatua hata anawakana wazazi wake, hii ni
hatari kabisa....’akasema wakili mtetezi.
‘Kwanini
unawakana wazazi wako shahidi....’akasema wakili akimuangalia huyo shahidi
usoni.
‘Mimi
sijawakana wazazi wangu,...ila ninachosema muheshimiwa ni kuwa hao watu sio
wazazi wangu ....hao watu ni waongo, mimi nawafahamu, nimeishi na
huyomshitakwia nyumba moja namfahamu tabia yake, nimekutana na haowatu
wanaoitwa ni wazazi wangu, nimewaona, ....sio wazazi wangu, kwahiyo mimi sipo
tayari kuwakubali hata kwa siku moja...’akasema shahidi huyo.
‘Kwasababu
gani huwezi kuwakubali na wakati ushahidi nimeshakuonyesha, hukubaliana na
hivyo vipimo,...?’ akaulizwa
‘Siwezi
kukubaliana navyo, kwasababu sio kweli,,...kama ungekuwa ni ushaidi sahihi ungeliutoa
kama ushahidi, lakini kwa vile unatambua sio sahihi ndio maana unanionyesha kwa
hivi, na hata, hao wazazi wangu kabisa kabisa, siwezi kuwakubali kwa vyovyote
vile...’akasema
‘Je kama ushahidi
huo upo kwenye ushahidi wangu, na vipimo hivyo
ni vya kweli, bado utaendelea kuwakana hao wazazi kuwa sio wazazi wako...?’
akaulizwa
‘Nimeshakuambia
hao sio wazazi wangu, nina uhakika huo
ushahidi sio halali...na kamwe sitaweza kuwakubali watu kama hao, hilo
nakuhakikishia, watafute mtoto mwingine sio mimi, ....’akasema akitikisa
kichwa.
‘Nakuuliza
tena hata kama kipimo hicho ni sahihi...hutaweza kuwakubali hao wazazi kuwa ni
wazazi wako, na kwasababu gani...?’ akauliza na wakili muendesha mashitaka
akaingilia kati akasema hayo maswali hayana msingii na hayana uhusiano na kesi.
‘Yana
uhusiano na kesi, kwasababu ya kupima uhakika wa majibu ya shahidi, na tunataka
kuhakikisha kuwa mshitakiwa ni baba mdogo wa huyu shahidi, kitu ambacho huyu
shahidi ana kipiga, na ni vyema tukaisaidia jamii, huyu ni mtoto ana wazazi wake,
iakuwaje asiwakubali, .....’akasema wakili mtetezi.
‘Wakili
endelea na maswali mengine, hilo limeeleweka.....’akasema hakimu baada ya kutulia
akiwaza jambo. Na wakili mtetezi akamwangalia wakili muendesha mashitaka,halafu
akamgeukia shahidi, akatabasamu,.
Shahidi
alikuwa kakunja uso ,kuonyesha kakasirika, na kama isingelikuwa ni mahakama,
huenda, angeliondoka, zake, ..akamuangalia wakili mtetezi, safari kwa macho
yasiyo yakujiamini,na wakili akauliza swali jingine.
‘Wewe
unasema kuwa mlezi wako, uliyekuwa ukiishi naye alikuwa akifanya biashara ya
mlungula, sawa si sawa.....?’ akaulizwa
‘Nilishaelezea
hilo,....muheshimiwa,....ndio alikuwa akifanya biashara ya mlungula...muheshimiwa..’akasema
‘Kipindi
hicho ulikuwa mdogo, ulijuaje kuwa alikuwa akifanya biashara ya mlungula...?’
akaulizwa
‘Kipindi
hicho, sikuwa makini na hilo, japokuwa nilijua kuwa anafanya vitendo hivyo,
lakini jinsi nilivyozidi kukua, nimekuja kugundua na kutambua vyema kuwa
alikuwa akifanya biashara ya mlungula....’akasema
‘Kwahiyo kwa
kipindi hicho hukuwa unafahamu hivyo,umekuja kufahamu sasa hivi ulipoongea na
wakili muendesha mashitaka?’ akaulizwa
‘Nilijua
hivyo kipindi hicho nilishakuwa mkubwa wa kutambua,...., ila sikuwa makini,...nilijua
hivyo, hata kabla ya kuongea na wakili muendesha mashitaka....muheshimiwa’akasema
‘Kama ni
hivyo, ...kuwa ulikuwa unajua kuwa baba yako mdogo alikuwa anaendesha biashara
ya mlungula,...ina maana na wewe ulikuwa muhusika wa biashara hizo za mlungula
au sio...?’ akaulizwa.
‘Kwa vipi niwe
muhusika,...,maana mimi nilikuwa mdogo tu, na ...sikuwa nafuatilia mambo yake,
mimi nilikuwa nasoma, nay eye alikuwa na kazi zake, na mimi sikuwa na muda
wakufuatilia ni nini anachokifanya, ila nilikuwa naona,nasikia anavyoongea na
simu, naona matendo yake...’akasema kwa hamaki
‘Kwa vile
ulikuwa hufuatilii mambo yake, ...hukuwa na uhakika kama kweli alikuwa akifanya
biashara hizo au la....umejua hivyo baada ya kuongea na muendesha mashitaka au
sio...?’
‘Nimeshakuambia,...muheshimiwa, nilikuwa naona, na pia nasikia,akiwasiliana
na watu,..’akasema kwa hamaki.
‘Kwahiyo
shughuli hizo zakuwasiliana na watu, akifuatilia milungula alikuwa akizifanyia
humo ndani, unasikia, unaona akiongea na
wagusika, au sio....?’ akaulizwa
Shahidi akakaa
kimia...
‘Huna
uhakika na hilo, ....au nikuulize tena swali langu...?’ akaulizwa
‘Mara nyingi
mawasiliana ya biashara hizo hakuwa akizifanyia ndani, alishaniambia kuwa vitu
kama hivyo, huwa anatakiwa kuchukua tahadhari, kwahiyo mara nyingi alikuwa
haongelei hapo ndani....’akasema.
‘Kwahiyo
humo ndani alikuwa akiwasiliana kuhusu mambo mengine ya kikazi na mambo yake
binafsi..?’ akaulizwa
‘Ndio....muheshimiwa’akasema
kwa sauti ndogo
‘Kwahiyo
huna uhakika kuwa hata huko nje alikuwa akiwasiliana kuhusu biashara hiyo ya
mlungula, huenda ni mambo hay ohayo ya kikazi, au sio....?’ akauliza na shahidi
akakaa kimia, halafu akasema;
‘Ndio sina
uhakika....lakini ...alishaniambia kuwa akiwa anafanya mambo hayo anachukua
tahadhari,..huenda huko alikuwa akifanya hivyo...’akasema
‘Huenda ,
ina maana huna uhaika.....’akasema na kabla shahidi huyo hajajibu wakili
akauliza swali jingine.
‘Katika
nyumba mliyokuwa mkiishi wewe ulikuwa na chumba chako au mlikuwa mnachangia
chumba kimoja na baba yako mdogo....?’ akaulizwa
‘Nilikuwa na
chumba changu,....na yeye alikuwa na
chumba chake muheshimiwa, na halafu kwanini unamuita baba yangu mdogo? ’akasema
na kuuliza
‘Kwani mdogo
wa baba huwa anatwaje...?’ akaulizwa
‘Lakini huyo
sio mdogo wa baba yangu, na hata wafadhili wanafahamu hilo, hata sheria za hapa
zinafahau hivyo, ndio maana nilitafutia wafadhili, hilo lipo wazi, usitake
kulazimiha,...hao sio wazazi wangu nielewe hivyo, na haitakuwa hivyo kamwe...’akasema
‘Swali langu
jingine ni hili je huyo baba yako mdogo,...ulisema alikuwa akija na
wanawake,..humo ndani mnapoishi au sio?’ akaulizwa
‘Ndio....huyo
`m-shi-ta-ki-wa’ alikuwa akija na wanawake wengine...muheshimiwa.’akasema
akimuangalia wakili huyo kwa makini.
‘Na akija na
wanawake hao, wewe unakuwa chumbani
kwako, na yeye anaingia chumbani kwako, .....au sio...?’akaambiwa
‘Hapana
alikuwa akiingia chumbani kwake,kwanini aingie chumbani kwangu...?.’akasema na
kuuliza
‘Na wewe
wakati huo upo wapi, wakati anaingia na hao wanawake?’ akaulizwa
‘Chumbani
kwangu,..nasoma...au nimelala....’akasema
‘Sasa
uliwaonaje wakifanya huo uchafu,maana kwa kauli yako ya mwanzo ulisema alikuwa
akija na wanawake na kufanya uchafu wao mbele yako,..au sikukusikia vyema? ‘akauliza
na kabla hajajibu wakili akauliza
‘Au usema
ukweli,.... wewe ulikuwa na tabia ya kwenda kuwachungulia chumbani kwao...’watu
wakacheka
‘Mimi siwezi
kufanya hivyo,...sikuwahi kwenda kuwachungulia, mimi sia tabia hizo chafu,...
mimi nilikuwa nasoma chumbani kwangu, sikuwahi hata siku moja kufanya mambo
kama hayo.....’akasema kwa hamaki na alipotambua kuwa kaongea kwa hamaki
akasema;
‘Muheshimiwa...’.
‘Kwahiyo
hiyo kauli uliyosema mwanzoni kuwa alikuwa kifanya uchafu mbele yako, ulikuwa
umejitungia, wewe mwenyewe, au uliambiwa useme hivyo,....?’akaambiwa na kabla
hajasema neno akaulizwa swali jingine.
‘Hebu
nikuulize swali, ni nani wanavaa hereni, na kusuka nywele, kwa kawaida ni nani
wanafanya hivyo...?’ akaulizwa na akaonyesha uso wa kutahayari, na kugeuka kwa
muendesha mashitaka ili amtetee kwa swali hilo.
‘Swali hilo
linahusiana nini na kesi hii......’akasema akionyesha mikono ya kutahayari, na
huku akiendelea kumuangalia muendesha mashitaka.
‘Hiyo sio
kazi yako, kazi yako ni kujibu swali ninalokuuliza...’akaambiwa
‘Ni
wanawake.....’akasema na alipogundua hilo swali ni la mtego, akasema
‘Hata
wanaume , wasanii, wacheza mziki, ...wanafanya hivyo...’akasema
‘Kwanini wewe
umetoboa masikio, unasuka nywele, eeeh, kwani wewe ni msanii, mwanamziki au....kwanini
unawaiga wanawake, hujiamini ?’
akaulizwa,na akajishika masikio, na kusema
‘Ni uamuzi
wangu binafsi,..sizani kama inakuhusu...na ni mitindo tu’akasema
‘Je mzazi
wako alifurahia hicho kitendo...?’ akaulizwa
‘Kitendo
gani....?’ akauliza
‘Cha wewe
kutoba masikio na kusuka nywele....?’ akaambiwa
‘Hapana
hakupenda, ...alinikemea...alinikataza....’akasema
‘Wewe
ulipokemewa ulisema nini...?’ akaulizwa
‘Nilimwambia
...ni usasa zaidi, wengi wanafanya hivyo, ...sioni ubaya wake, ...akaniambia
inaleta picha mbaya hasa ....,na akasema hao anaowaita wazazi wangu hawatapenda
wakiniona hivyo,na kipindi hicho nilikuwa sijakutaa na hao anaowaita wazazi
wangu...’akasema
‘Wewe
unavuta sigara, ...?’ akaulizwa
‘Mwanzoni
nilijaribu nikaacha,siunajua tena utoto, ujana, muheshimiwa....’akasema
‘Kwanini
uliacha...?’ akaulizwa
‘Niliona
haina maana yoyote kwangu...nilikuja kujitambua...’akasema
‘Hukuacha
baada ya kukatazwa na mlezi wako...?’ akaulizwa
‘Ndio....alinkataza...’akasema
‘Uliwahi
kuvuta bhangi...?’ akaulizwa na hapo akakaa kimia bila kujibu hilo swali.
‘Kwanini
hutaki kujibu hilo swali....?’ akaulizwa
‘Kwasababu
ni mambo ya utotoni, ujanani, wengi hupitia, na baadaye huacha, ni kama kuuliza
kama niliwahi kula mchanga, au...kuchezea uchafu nikiwa mdogo....hayo wengi
wanayapitia na baadaye huachana nayo..’akasema
‘Huachana
nayo wakipata mtu wa kuyakemea hayo mambo au sio...?’ akaulizwa
‘Ndio....’akajibu
huku akibenua mdomo kama anaona kero, na alipojitambua akasema
‘Ndio
muheshimiwa, wakipata mtu wa kuwakemea, na wengie huacha wenyewe
wakijitambua...’akasema
‘Kuna
kipindi wewe ulibobea kwenye mziki, ukawa unapigisha mziki nyumbani, na ukawa
husomi,....unakumbuka...?’ akaulizwa
‘Ndio lakini
ni kipindi nikiwa mdogo, sielewi kitu, nilipokuwa mkubwa nikabadilika....’akasema
‘Ni nani
alikukataza kufanya hivyo....?’ akaulizwa
‘Kufanya
nini....?’ akaulizwa
‘Kuvuta
bhangi, kupiga mziki,....ili usome ....?’ akaulizwa
‘Ni
yeye....’akasema
‘Ni yeye
nani...?’ akaulizwa
‘Mshitakiwa...’akasema
akionyesha kidole pale alipokaa mshitakiwa
‘Je kipindi
unavuta sigara, ukajaribu hata bhangi, ukawa unapigisha miziki , ukawa hata
kusoma hupendi ilikuwa kipindi gani, ukiwa shuleni bweni au uliporudi nyumbani
kukaa na baba yako mdogo...?’ akaulizwa
‘Ni kipindi
nikiwa bweni, nilikuwa natoroka shule, kwenda nje, na wenzangu, walikuwa
wakinihadaa tu, lakini niliporudi kukaa na .....huyo mshitakiwa nikaanza
kubadilika,nilishajitambua,....’akasema
‘Ulibadilika
kwa vile alikuonya, akawa anakuelekeza lipi jema na lipi baya, akawa
anakukataza kuvuta sigara, kupiga miziki,....ili usome ,ili uwe na elimu ambay
o sasa unayo....kweli si kweli....?’ akaulizwa
‘Lakini pia
na mimi niliona havina faida kwangu, ....ndio nikaacha...’akasema
‘Je kama
ungeliendelea kukaa bweni, ungebadilika, sema kwa ukweli wako...?’ akaulizwa
‘Ningebadilika
ndio....wengi wanabadilika, ni swala la uamuzi...na umri unachangia....’akasema
‘Je baba
yako huyo mdogo hakuchangia kubadilika kwako,hakukukataza kuvuta bangi, kuvuta
sigara, kucheza mziko, hakukuelekeza kusoma, akawa anakuasa uwe mtoto
mwema...?’ akaulizwa
‘Alinikataza
ndio...sijakataa hilo...ila pia na mimi mwenyewe nilihajitambua nikaona hayo
hayana umuhimu ,muheshimiwa..’akasema
‘Halafu
unasema ni mlezi mbaya, unasahahu yote hayo, kuwa aliwahi kukuanya,
kukuelekeza,...hebu jiulize kama angeacha ukawa unapiga mziki, husomi,
....ukawa unavuta bangi, ungefika hapo ulipo...yote hayo umeyasahau....sina
zaidi muheshimiwa, ....’akasema mtetezi na muendesha mashitaka akasema
******
‘Tunaingia
sehemu ya pili, shahidi unaweza kuondoka, tutakuita tena kwenye sehemu ya pili,
...’akasema muendesha mashitaka na shahidi akawa anatoka sehemu ile ya kutolea
ushahidi akiwa kainama chini,tofauti na alivyoingia kwa mbwembwe...
‘Unajua
ukweli huwa unauma wazazi wengi hawapendi kuambiwa hawajui kulea,au kazi
wanaofanya ya kuingiza pesa sio halali, hata kama kweli wamekosea, au kazi
wanayofanya sio sahihi, ...sio halali watasema kwani, kwani wewe unakula
nini....’akaongea na watu wakacheka.
‘Wapo,
tunawaona...’akazidi kusisitizia
‘Kijana
usijali upo sahihi kabisa, umezungumza ukweli wako...’akasema na wakati huo
huyo shahidi alikuwa anatembea kumpita huyo wakili muendesha mashitaka.
‘Sasa tunaingia
kipengele muhimu sana, kipengele cha kuonyesha jinsi mshitakiwa alivyotenda
kosa la kumiga risasi marehemu na
kusababisha kifo chake.....’akasema
NB: Naona
tuishie hapa....
WAZO LA LEO: Mtoto
umleavyo ndivyo akuavyo, na watoto wengi huiga matendo yetu wazazi , au matendo
ya walezi wao, au hao wanaishi karibu nao..., matendo huigwa haraka
sana,....sasa ni jukumu letu wazazi, hasa wale wanaokuwa nje ya kazi kwa muda
mwingi, na kazi ya kulea watoto ikawa mikononi mwa wafanyakazi wan je,
tujitahidi kuwaelekeza hao wafanyakazi tabia ambazo zitakuwa kiyoo kwa watoto
wetu,vinginevyo, tutakuja kujilaumu wakati tumeshachelewa
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment