Hakimu akawaruhusu upande wa utetezi
wamuulize huyo shahidi maswali, na wakili mtetezi akasimama, kwanza akawa kama
anawaza jambo, alishika mkoba wake kama anataka kutoa kitu, halafu akasita,
akatulia pale pale kwa muda, kama anawaza jambo....
Halafu kwa mwendo wa taratibu akamsogelea
mshitakiwa kama anataka kumuambia kitu, lakini hakufanya hivyo, akageuka
kuelekea alipo shahidi.Akitembea mwendo ule ule wa taratibu.....
Alipofika kwa shahidi, alimuangalia
usoni akiwa kama anamchunguza akamuangalia huyo shahidi moja kwa moja usoni...,
na shahidi naye akawa anamuangalia huyo wakili bila kuangalia pembeni au chini....
Shahidi naye alijitahidi kumuangalia
wakili, huenda alishaambiwa ujanja wa mawakili kuwa asimuogope wakili pale
anapomuangalia usoni au pale anapotoa maswali ya vitisho, kwahiyo shahidi huyu
akajitahidi nay eye kumuangalia wakili huyo usoni.
Wakawa wanaangaliana
Baadaye wakili alisema....
‘Wewe shahidi ni muongo, ....’
Tuendelee na
kisa chetu...
********
Baadaye
wakili huyu akasogea nyuma, lakini bado akiwa anamuangalia huyo shahidi,....na
mdomoni akawa anatabasamu,kama vile kagundua kitu.
Wakili huyu akageuka upande wa watazamaji, watu waliofika hapo
mahakamani, walikuwa ni wengi, na kwa sauti kama ya kunong’oana akasema...
‘Shahidi
huyu ni muongo....’akasema na watu
wakaguna na minong’ono ikatanda,....hakimu akapiga rungu lake na kusema kuwe na
utaratibu halafu akasema;
‘Wakili
mtetezi unapoteza muda,....’akasema na wakili akamgeukia hakimu, akainama kama
vile anataka kuondoka au kusema hana swali,lakini kwa haraka akamgeukia shahidi
na kusema;
‘Wewe ni
muongo,....unaidanganya mahakama,....hilo kosa....’akasema na shihidi akabakia
kimia, lakini hakuacha kumuangalia huyo wakili , lakini usoni kwake alikuwa
keshakunja alama za kuashiria kuwa kakasirika.
‘Baba yako
na mama yako ni nani.....?’ wakili akamuuliza akiwa kamkazia macho,lakini
mdomoni akiwa anatabasamu,
Shahidi
hakujibu kwanza, alimgeukia wakili wake,
na wakili wake akamuashiria ajibu hilo swali.
‘Siwajui....’akasema
huyo shahid kwa sauti yenye kuonyesha kukerwa na hata sauti ilikuwa ya
kukasirika.
‘Kwahiyo
wewe ulizaliwaje, kama huna baba au mama...?’ akaulizwa swali tena na wakili
huyo, huku wakili huyo akitabasamu.
‘Nimesema
siwajui,... hata kama wapo sijawahi kuwaona...’akasema akionyesha dharau.
‘Unaona
ulivyo muongo,..dharau, ndio tabia yako sio, je hujawahi kuwaona baba na mama
yako..waliokuzaa...?’ wakili akauliza sasa nay eye akionyesha ukali katika sauti yake, na wakili muendesha mashitaka akatoa pingamizi
kuwa wakili huyo kuwa wakili huyo anamlazimisha shahidi kuongea kitu ambacho
keshajibu, na hakimu akamuonya wakili huyo.
‘Wewe
unasema wapo, lakini kama hawapo hujawahi kuwaona....au sio...?’ akaulizwa
‘Nilishajibu
...sijawahi kuwaona.....’akasema
‘Ila
wapo...?’ akaulizwa
‘Sijui....’akasema
‘Sasa kama
hujui, nikuwa alitokea msamaria mwema akahangaika kukutafutia wazazi wako,
baada ya yeye kukuokota ukiwa maporini, ukitaka kuliwa na wanyama....’akatulia
‘Huyo
msamaria akahangaika kuwatafuta wazazi wako, huku akihangaika kutafuta jinsi
gani utasoma,...yeye akafanya uchunguzi , na katika kukukagua akagundua kuna
kufanana fanana fulani na ndugu yake..., siunajua damu ya mtu
haipotei....’akasema wakili.
‘Mimi sio
damu yake kabisa....kakudanganya tu...’akasema shahidi
‘Huyo
msamaria mwema, akahisi wewe ni damu yao...’akaendelea kusema huyo wakili bila
kujali maneno ya huyo shahidi
‘Wewe wasema
....’akasema shahidi
‘Sijakuambia
unijibue,.....’hatimaye wakili akasema kumuashiria huyo shahidi aimuingilie,
wakati anaongea
‘Unatunga
uwongo, nashindwa kuvumilia huo uwongo wako....’akasema sahahidi.
‘Sasa kama
huyo msamaria mwema, kaja kugundua kuwa
kumbe wazazi wako pia ni ndugu zake, je kufanya hivyo ndio kafanya makosa...au
kwa vile tu umeona kuwa watu hao ni masikini, wanaishi kijijini, hawana kitu...?’ akaulizwa
‘Ndio
kafanya makosa,.....kwasababu sio kweli,...na sijawakataa kwasababu ni
masikini, mimi sijui kama ni masikini, ila hayo unayatunga wewe mwenyewe kutoka
kichwani mwako...’akasema shahidi
‘Una uhakika
gani kuwa sio kweli, kuwa natunga kutoka kichwani kwangu....kuwa hao uliowaoana
sio wazazi wako?’ akaulizwa na hapo muendesha mashitaka akataka kuingilia
lakini akaonekana kusita, akatulia.
‘Akina nani
nani hao.....?’ akauliza kwa sauti ya hasira
‘Hao uliowahi
kutambulishwa kwako kuwa ni wazazi wako , baba na mama yako, wewe ukawakana....’akaambiwa
‘Niliwakana
kwasababu kweli sio wazazi wangu,...nilishawashitukia, nikajua kuwa ni mbinu tu zao, za kutaka kupata pesa kupitia
mgongo wangu,....’akasema
‘Swali...je
una ushahidi gani kuwa hao sio wazazi wako, ...wakati wewe unafanana na baba
yako...?’ akaulizwa
‘Nafanana na
yule mzee, unanichekesha kweli,....Kwanza nikuambie ukweli, mimi sura yangu haifanani
kabisa na huyo mtu, hujawahi kumuona kama ungemuona ungekubaliana na mimi....yeye
ni mweuzi tiii, na mimi ni maji ya kunde, si unaniona nilivyo...’akasema na
watu wakacheka,
‘Na pili tabia
na mienendo zetu hazioani kabisa, kama angekuwa ni baba yangu, angalau
kungelikuwa na kijitabia fulani kinachofanana na mimi,..lakini hakuna kitu kama
hicho kabisa, huyo jamaa anamihasira utafikiri nini....’akasema
‘Na tatu...unawaona
walivyo, matendo yao, hasa huyo mshitakiwa, tapeli, mwizi, ...anapenda pesa,na
anaonekana kabisa anaweza kufanya lolote ili tu apate pesa bila kujali sheria...na
zaidi ya hayo, hakuna ushahidi kisheria kuwa watu hao nina uhusiano nao
kabisa....’akasema.
‘Hakuna
ushahidi kisheria kuwa watu hao wana uhusiano na wewe, wewev unajua ushahidi
gani wa kisheria wa kukuonyesha kuwa wewe una mahusiano na hao watu.....?’
akauliza na wakili akaingilia kati hilo swali.
‘Hilo swali
limetokana na majibu yake...’akajitetea wakili mtetezi, na hakimu akasema
lijibiwe
‘Hiyo ni
kazi yako wewe, mwanasheria, unaniuliza mimi.....’akasema
‘Ndio
nimekuuliza wewe, ni ushaidi gani ambao unautambua, wa kisheria, wa kukuonyesha
kuwa wewe una mahusiano na hao ....?’ akaulizwa
‘Kuna vyeti
vya kuzaliwa, kuna...kitu chochote cha kuonyesha kuwa mimi nina damu, au
...hata labda kurithiwa,ni lazima kuwe na nyaraka za kisheria, unafahamu
unanidhihaki tu,....kama angelitaka niwe mwanae angetafuta hata hicho cheti cha
kunirithi,.hana, najua hana ....’akasema
‘Una uhakika
na hilo....?’ akauliza wakili huyo akimuangalia kwa makini.
‘Ndio nina
uhakika, wewe si wakili wao nionyeshe huo ushahidi kama unao, kama sio unatafuta
pesa tu kwa kuwatetea wahalifu hao....’akasema na wakili akatabasamu.
‘Je
nikikuonyesha ushahidi kuwa hao ulio onyeshwa kule kijijini ni wazazi wako halali
utasemaje....?’ akaulizwa na wakili ,na shahidi huyo akacheka kwa dharau na
kusema
‘Hakuna kitu
kama hicho,..labda huo ushahidi uwe wa
kugushi, wa kitapeli, maana huyu mtu chochote anaweza kufanya, hata kusingizia
kuwa yeye ana udugu na raisi ili apate pesa za familia ya raisi yeye anaweza
kusema hivyo.....’akasema na watu wakacheka, na walipotulia alipoona wakili
mtetezi naye katulia akaendelea kusema
‘Mimi
...siwezi kuwa na wazazi kama hao,....kabisa kabisa nakataa kwa nguvu zangu
zote, hakuna na hakutaweza kuwepo na ushahidi wowote zaidi ya maneno ya uwongo,
kuonyesha kuwa mimi ni mtoto wa hao watu, hao watu ni waongo,
matapeli....’akasema,na huyo wakili akamgeukia na kusema;
‘Wewe shahidi ni muongo, umefundishwa kuongea hivyo,
hadi kufikia kuukana ukweli wa asili yako,unafikia hatua ya kuwakana hata
wazazi waliokuzaa, unamkana mama yako mzazi, unajua jinsi gani mama yako
alivyokuhangaikia, ukiwa tumboni, akakuzaa kwa shida, unafahamu mama yako ...’akasema
na wakili muendesha mashitaka akaingilia na kusema wakili analazimisha shahidi
aseme uwongo, na shahidi akasema kwa hasira
‘Huyu wakili
ni muongo, mimi ninachosema mbele ya mahakama hii ni ukweli mtupu,na sijawahi
kuukana uasili wangu, nilichokikana hapa ni tabia chafu za hao watu,,...utapeli, wizi, ....nk mimi
sina tabia chafu, kama asili yetu ni tabia chafu basi mimi sitakubali kuwa na
asili hiyo,..na hao watu sio wazazi wangu.’akasema na watu wakamshangilia.
Wakili
mtetezi kwanza akatabasamu, halafu
akasogea kwenye makabrasha yake, akatoa karatasi, ilikuwa kuu-kuu, akaiangalia
kwa makini kama anasoma kitu, akatulia kama anawaza jambo, halafu akageuka
kumuangalia shahidi akasema;
‘Wewe
ulisema kuwa hakuna ushahidi wowote wa kuonyesha kuwa wewe huna mahusiano
yoyote na familia hiyo....siku hizi hakuna ujanja bwana, huwezi kumkana mzazi
wako....’akasema na shahidi akawa anaonyesha uso wa kujua ni kitu gani,
akageuka kumuangalia wakili wake, na wakili muendesha mashitaka naye akawa
anaangalia ni kitu kashika huyo wakili mtetezi.
‘Huu hapa ni
ushahidi unaoonyesha kuwa wewe ni mtoto wa damu wa kaka wa huyu mshitakiwa ...’akasema
akiwa kashikilia ile karatasi, sasa akiwa kamsogelea shahidi.
‘Wewe si
umesoma, hebu angalia hapa kumeandikwa nini....?’ akawa anaonyeshwa hiyo
karatasi,
‘Its
fake..najua lazima atatafuta nyaraka za uwogo....’akasema
‘It’s a
fake....wewe ni msomi, kitu kama hiki kinaweza kufojiwa, wewe ulizaliwa huko
anapotokea huyu mshitakiwa,na mshitakiwa ni baba yako mdogo, ushahidi huu hapa.....’akasema
akimkabidhi huyo kijana karatasi hiyo, na wakili muendesha mashitaka akainuka
pale alipokuwa amekaa na kwenda hadi pale aliposimama shahidi, akaichukua ile
karatasi,....
‘Huu sio
ushahidi sa-hi-hi.....!?’akasema kwa kuuliza muendesha mashitaka na
akayamalizia hayo maneno ya mwisho kwa taratibu.
‘Umeitoa hii
kama ushahidi....?’ akauliza wakili muendesha mashitaka, na wakili mtetezi
akasema;
‘Sijaitoa
hiyo na kuikabidhi kama ushahidi , kwani natambua fika, muda wangu wa kufanya hivyo bado, ila nimeitoa
ili kumuweka sawa huyu shahidi wako kuwa asiendelee kuongopa,....’akasema
‘Hiyo sio
kazi yako kuoana kuwa anaogopa...ni kazi ya muheshimiwa hakimu...’akasema
wakili muendesha mashitaka.
‘Najua,...lakini
shahidi wako alitaka kuuona huo ushahidi, ili akili yake itambua kuwa hapa sio
sehemu ya kuongopa, anatakiwa kila anachokiongea ajue kuwa ni sahihi, hapa yupo
mbele ya mahakama, kaapa,...na zaidi ni msomi...sio kwamba kuwa haelewi
anachokiongea, hata kama kafundishwa aongee hivyo,....
'Kwanini wewe shahidi ukubali
kurubuiwa, uje kuwakana wazazi wako mbele ya mahakama, mbele ya mungu utakuja
kusema nini,.....sio vizuri....’akasema huyo wakili, wakati huo, wakili muendesha
mashitaka akawa bado anaendelea kuichunguza ile karatasi
‘It’s a fake...sio ushahidi sahihi huo,
anawadanganya...mimi siwezi hata siku moja kukubali huo ushahidi hadi kufa.....never..’akasema huyo shahidi
akumuashiria wakili muendesha mashitaka kwa kidole, na kiganja cha mkono, na wakili
mtetezi akasema;
‘DNA, sio
ushahidi sahihi.....?’ akauliza wakili mtetezi, akimuangalia wakili muendesha
mashitaka na wakili muendesha mashitaka akasema
‘Kila kitu
chawezekana mbele ya wanadamu .....’akasema na akawa anatembea kuelekea sehemu
yake ya kukaa huku akiwa bado kashikilia ile karatasi, na wakili mtetezi
akasema
‘Sijaikabidhi
hiyo nyaraka kama ushahidi muheshimiwa na hakimu akasema;
‘Taratibu
zifuatwe mawakili...., wakili mtetezi endelea na maswali yako kwa shahidi...’akasema
hakimu, na wakili mtetezi akageuka kumuangalia shahidi, na shahidi sasa alikuwa
kainama chini, kama anawaza jambo,....
NB: Mahakama
inaendelea, tuishie hapa kwa leo kwa swali, kwa tafakari,...kauli za ‘sitakubali
kamwe ,au hata nikifia asije, au
sitakwenda hata nikifa,..au ....kauli za viapizo ambazo sio rahisi
kutimizwa, zina maana gani kutamka midomoni kwetu,.....haya tuone kama kijana
ataweza kutimiza ahadi yake hiyo kuwa hatakubali kuwa ni wazazi wake kamwe,....
WAZO LA LEO: Tujifunze kujijengea tabia njema,
kwa kauli na vitendo. Kusema ukweli ni
moja ya tabia njema, tusiogope kusema ukweli hata kama ukweli huo, utaumiza
watu, hata kama ukweli huo utakuumiza hata wewe mwenyewe, ukweli ni silaha, na
ukweli ni ngao, ukiwa mkweli,utashinda wakati wote, kwani ukweli ni uaminifu
kwako kwa jamii na mbele ya mwenyezimungu muumba.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment