Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeTuesday, August 25, 2015

RADHI YA WAZAZI-33


Kesi ilianza, profesa akasimamishwa kama mshitakiwa mkuu,wa mauaji , mvunjifu wa amani kwa jamii, na muendesha biashara ya milungula,(blackmailer)....

Kesi hiyo ilkuwa kesi iliyowavuta watu wengi, hutaamini hata wakubwa walifika, na hata wengine kutuma wawakilishi wao...

‘Mhh, naona hii kesi ina jambo...’mmoja wa waandishi wa habari akawa anadodosa

‘Hii sio kesi ya mauaji tu, nahisi kuna zaidi ya hilo, marehemu hakuwa maarufu kuwavuta watu wengi kiasi hiki,  na weni ni watu wakubwa na mashuhuri, Unahisi kuna jambo gani....’akamuuliza mtu mmoja.

‘Mhh, mauaji.....wakati ni hawa watu wamekuja na njaa zao kwenye nchi yetu wanatuleta matatizo,...hawa watu inabidi wafukuzwe kabisa....’akasema jamaa mmoja, na wengine wakawa wanamuunga mkono.

‘Lakini huwezi kumuhukumu mtu mpaka ijulikane kuwa kweli ana kosa, je huyu mtu ana kosa gani, na kwanini wakubwa wavutike na hii kesi...?’ akauliza

‘Kuna masilahi binafsi na hii kesi na wahusika watakuwa wanahusika na masilahi yao, ...’akasema mtu mmoja lakini alipoulizwa zaidi hakusema akaonekana akihangaika kutaka kuingia ndani ya mahakama....

‘Nahitajika ndani , nimechelewa....’akasema

Hayo yakiendelea huko nje, ndani ya mahakama, kesi ilikuwa ikiendelea....

*********

Taratibu mbali mbali za kimahakama zilifuatwa na waendesha mashitaka, walianza kazi ya kuitambulisha kesi, na kuielezea hiyo kesi ilivyo..kwa ilikuwa sio siku ya kwanza, kwani kesi hiyo ilishatambulishwa na siku hiyo ilikuwa siku ya kuanza kesi yenyewe, basi ikaanza kazi ya kuwaita mashahidi.

Muendesha mashitaka akaanza kuijenga hiyo kesi, ....na kila shahidi aliyeitwa, akawa anaongozwa na muendesha mashitaka halafu utetezi inamuhoji huyo shahidi.
Wakili wa mshitakiwa akijitahidi kukabiliana na mashitaka hayo kwa nguvu zote, na kinyume na walivyofikiria kuwa wataweza kumfunga mshitakiwa  hata ikibidi kifungo cha maisha lakini ikawa kinyume chake,  kwani wakili wa utetezi, alifanya kazi yake barabara, ...

Kuna baadhi ya hoja zilizoingia kwenye malumban makali, ....

*********

‘Unasema mshitakiwa alifika kuchukua mzigo alioelekezwa na watu wake, na mzigo huo angeupata kwa marahemu,....nashangaa hao watu hawatajwi, ....sawa lakini unasema alipofika kwa marehemu ili kuuchukua huo mzigo, wakakosana na mshitakiwa akatoa bastola,   akamuonyesha marehemu.....’akaanza mtetezi.

‘Huyu mshitakiwa alipita sehemu ya mapokezi, na sehemu ya mapokezi wanakaguliwa, kutokana na taratibu za hilo jengo zilivyo, sasa nawauliza,huyu mshitakiwa aliipitaje hapo na hiyo bastola...?’akauliza mtetezi kumuhoji shahidi aliyesimamishwa.

‘Huyu mshitakiwa ana historia za uhalifu, asingeshindwa kutumia ujanja kuihifadhi hiyo bastola sehemu yoyote humo ndani, na wakati anapita muda huo, ili kuficha uhalifu wake asitambulikane ‘ akasema

‘Huyu mshitakiwa wakati anapita alikaguliwa na walinzi au sio, kawa ilivyo kawaida, alionekana na silaha?’ akaulizwa huyo shahidi

‘Kwa muda huo hakuonekana na silaha....’akaambiwa

‘Ndio nauliza hiyo silaha ilipatikana wapi , kama sio kulikuwa na mtu mwingine ambaye alifanya huo uhalifu, na kumbambikia mshitakiwa....’akasema muendesha mashitaka.

‘Kutokana na melezo ya walinzi wa hapo kwenye hilo jengo, ni kuwa silaha haziruhusiwi kwenye hilo jengo, mtu haruhisiwi kuingia na silaha, kweli si kweli,...sasa msshitakiwa alipitaje bila kuonekana na hiyo silaha...ndilo swali langu...’akauliza

‘Waulize hao walinzi....’akasema huyo shahidi na watu wakacheka.

‘Hii ni kuonyesha kuwa kulikuwa na mhalifu mwingine alikuwepo hapo kabla, akafanya huo uhalifu, na kwa vile polisi mumeshindwa kumpata huyo mhalifu mumeamua kumbambikiwa huyu mshitakiwa,......’akasema

‘Hayo ni maoni yako toa ushahidi kuonyesha kuwa kulikuwa na mtu mwingine....’akaambiwa

‘Hiyo sio kazi yangu, kazi yangu ni kumtetea huyu mtu mnayemuonea,...’akasema mtetezi

‘Sina swali jingine, ...’akasema wakili mtetezi.

********

Kati ya mashahidi waliowavutia watu waliokuwepo hapo mahakamani, ni mmoja aliyetambulikana kama kijana wa mshitakiwa, japokuwa yeye baadaye alikana kuwa yeye sio kijana wa mshitakiwa....

‘Huyu ni kijana aliyelelewa na mshitakiwa, kijana huyu alitolewa porini akiwa anatangatanga...kuna vielelezo vingi tu vya kuonyesha hilo tukio,....’muendesha mashitaka akawa anatoa maelezo

‘Kijana huyu aliishi na mshitakiwa toka akiwa mtoto, kwahiyo anamfahamu vyema mshitakiwa,...kwahiyo yote anayoyaelezea, anayafahamu , sio uzushi, yeye anamfahamu mshitakiwa tabia yake na kazi yake, ...na pia ana muheshimu kama mtu aliyemsaidia hadi kufikia hapo alipo....’akaendelea kuelezea

‘Mbona wewe ndio unatoa maelezo.....’wakaanza kulalamika watu wa utetezi

‘Nataka muone ukweli ulivyo, kuwa hata kijana wake alishaona uhalifu wake, ndio maana tunamuita kama shahidi......’ilielezewa.

‘Muheshimiwa hakimu, muendesha mashitaka anageuza mahakama yako uwanja wa siasa, .....tunahitajia ushahidi au shahidi sio maneno yake....’akalalamika mtetezi

‘Namuita shahidi yangu, ni kijana aliyelelewa na mshitakiwa mwenyewe ......’akasema muendesha mashitaka.

Huyo aliyetambulikana kama ‘kijana wake’  alipita na kusimama mbele ya sehemu ya mashahidi, baada ya taratibu zote kufuatwa muendesha mashitaka akawa anamuongoza kwenye kutoa maelezo yake.

Kijana , akielezea kazi za huyo mlezi wake,....akaelezea kuwa mwanzoni mshitakiwa alikuwa muuza madawa ya kienyeji, na humo akawa anachanganya na madawa yasiyotakiwa, yapo kama madawa ya kulevya...

‘Ulijuaje kuwa yapo kama madawa ya kulevya.....?’ akaulizwa

‘Niliambiwa na mwenyewe mshitakiwa na pia mshitakiwa aliwahi kushitakiwa kwa kosa hilo la kuuza madawa ambayo yapo katika kundi la madawa ya kulevya....’akasema

‘Kwahiyo upo ushahidi wa kimahakama kuwa mshitakiwa aliwahi kupatikana na kosa hilo....’akasema muendesha mashitaka

Katika kuelekezea tabia ya mshitakiwa, shahidi alisema mshitakiwa ni mtu mwenye tamaa alipenda sana pesa, na hata pesa zake za matumizi amazo zilikuwa zinapitia kwa mshitakiwa alikuwa akizitumia mshitakiwa badala ya kupewa yeye, yeye akawa anasoma kwa shida, na wakati mwingine ilibidi awe anaomba msaada kwa wasamaria wema....maelezo hayo yaliwashangaza sana  watu...

‘Lakini huyu ni mzazi, mlezi wako, ..kwanini akufanyie hivyo, au wewe ulikuwa humuheshimu, .....’akaambiwa

‘Mlezi, au mzazi anaangaliwa kwa utendaji wake kwa mtoto aliyekabidhiwa....lakini huyu 
mshitakiwa hakuwa na ubinadamu na mimi yeye alinitumia tu, ili apate pesa kwa masilahi yake,...’akasema

‘Je pesa hizo zilikuwa zikitolewa na nani?’ akaulizwa

‘Na wafadhili waliojitolea kunisaidia....’akasema

‘Kwa tabia hiyo wewe ulimuonaje huyo mlezi wako...?’ akaulizwa

‘Kwakweli japokuwa nilimuheshimu sana, kama mlezi, nikawa namuita dad wangu ....lakini baadaye niliona sio mtu anayestahiki kuitwa mlezi au mzazi wangu , hafai kuitwa mzazi kabisa labda ni kwa vile hajui uchungu wa mtoto...’kauli hiyo ikawafanya watu wacheke.

‘Hebu tuambie ni mambo gani uliyoyaona mpaka uone kuwa mshitakiwa hafai kuitwa mzazi au mlezi wako...?’ akaulizwa

‘Kama ni mlezi kwanini alikuwa akinidanganya, je mzazi anatakiwa kuwafundisha watoto uwongo, kuwadanganya, kuwaibia haki yao....’akasema

‘Yeye alikuwa anachukua pesa zangu kwa wafadhili,...anatumia hanisaidii sana kama ilivyotakiwa, alitumia mgongo wangu kujinufaisha yeye mwenyewe...., anawadanganya wafadhili, kuwa kuna hiki na hiki, kila akitaka pesa lakini hakinunui, ...mzazi gani hana uchungu na mwanae, anachoangalia ni tumbo lake,starehe zake.....’akasema.

‘Je ulionaje kuwa alikuwa akitumia pesa zako kwa starehe zake....?’ akaulizwa

‘Alikuwa mlevi sana, akawa anabadili wanawake, kila siku anakuja na mwanamke mpya, na wanastarehe mbele yangu....’akasema na watu wakawa wanacheka.

‘Kwahiyo wewe uliwezaje kuvumilia hiyo, kuwa unaishi na mzazi mwenye tabia chafu, kama ulivyosema na zaidi uligundua kuwa ni mhalifu...?’ akaulizwa

‘Mwanzoni niliogopa kuchukua hatua yoyote maana nilikuwa mdogo asiyeweza kufanya lolote..na kiukweli nilikuwa namuheshimu kama alivyotoa kwenye vyombo vya habari kuwa aliniokota, nilimuona kama mtu mwenye huruma kanitoa kwenye hatari, na kunisaidia,....kwahiyo sikuweza kumchukulia hatua yoyote, nilimuoa kama mlezi wangu...’akasema

‘Kwahiyo hiyo habari kuwa alikuokota porini uliichukuliaje....?’ akaulizwa

‘Nilipokuwa mkubwa na kuweza kuchanganua mambo, nimekuja kugundua kuwa habarii hiyo sio ya kweli,....’akasema

‘Kwanini sio ya kweli maana hadi wafadhili waliamini hiyo habari,....?’ akaulizwa

‘Mimi nimeishi na huyu mtu, kutokana na tabia yake, anaweza kutunga uwongo wowote ili tu apate pesa, ni mwerevu sana wa kutunga uwongo uonakane ni ukweli, ...kwahiyo nilipochanganua niliona kabisa hiyo habari kaitunga tu, mimi siamini kuwa kweli aliniokota porini....’akasema

‘Sasa kwanini hukumshitakia .....?’ akaulizwa

‘Kama nilivyosema mwanzoni nilikuwa mdogo, nilikuwa naogopa, na sikujua nianzie wapi, lakini kwa jinsi nilivyozidi kukua, .... na kusoma zaidi, nikagudua kuwa huyu mtu hafai kabisa kuwa ni mlezi...’akasema

‘Na kiukweli kwa muda ule nilikuwa sina mtu wa kunisaidia kimawazo, au kunieleleza, ....baadaye akili ikanijia kuwa naishi na mtu asiyefaa kuwa mzazi, na pale nilipopata kazi tu, na kuona kuwa na naweza kusimama peke yangu, ndio nikachukua hatua,...’akasema

‘Ulichukua hatua gani....?’ akaulizwa

‘Kwanza nikaachana naye, niliona nikiishi naye na mimi nitaonekana nina tabia kama yake, ya uhalifu, na...pili nikawa natafuta njia za kumfikisha mahakamani kama raia mwema...., maana sikupenda tabia yake hiyo chafu anayowafanyia raia wema.....’akasema

‘Kwanini umshitakie baba yako, mlezi wako....?’ akaulizwa

‘Muheshimiwa hakimu, huyo sio baba yangu,na wala sio mlezi wangu...sio damu yangu kabisa..., siwezi kuwa na baba au mlezi kama huyo,yeye  alitumia ulezi kuninyonya tu,..huyo ni tapeli, mimi nawaambia ukweli maana niliishi naye....’akasema na watu wakacheka.

‘Kwahiyo wewe una uhakika kuwa mshitakiwa hana uhusiano na wewe.....?’ akaulizwa tena

‘Kiukweli, hawezi kuwa na mahusiano na mimi, yeye na ndugu zake....’akasema

‘Ndugu zake ni akina nani....?’ akaulizwa

‘Yeye ana ndugu zake huko kwao, na alinipeleka kwa ndugu zake ili kuhalalisha uwongo wake, ...huko wapi sijui,na kunitambulisha kwa mzee mmoja mwenye sura mbaya eti ni baba yangu, lakini kiukweli, huyu sio baba yangu,walinitumia njia hiyo ili waweze kuhalalisha utapeli wao..., ili wapate pesa hizo kwa wafadhili..’akasema

‘Unasema alikupeleka huko kijijini kwao, ili kukutambulisha kwa watu na akasema hao ni ndugu zake,...na mmojawapo alikuwa ni  kaka yake mshitakiwa , na huyo kaka yake ukaambiwa ni baba yako,  kwanini wafanye hivyo...?.’akasema

‘Ndio alinipeleka huko nchini kwake, akanitambulisha kwa kaka yake, walifanya hivyo, baada ya kuongea, kuna siku tukiwa huku alikuwa akipigiana simu na huyo kaka yake kuwa ana mipango ya kuingiza pesa, na akirudi huko atamuambia ni mipango gani...’akasema

‘Wewe kwanini unahisi kuwa huyo uliyetambulishwa kuwa ni baba yako, sio baba yako kiukweli....?’ akaulizwa

‘Hebu jamani, niwaulize..., kama si uwongo, mimi ni mtoto wa ndugu yake, kwanini akaja kudai huku kuwa aliniokota maporini, mimi si mtoto wa kaka yake eeh? usahihi ulikuwa upi, labda aniambia walipanga yeye na kaka yake wafanye hivyo....’akasema

‘Usahihi ulitakiwa uwe vipi?’ akaulizwa

‘Kama aliniokota kama anavyodai,... alitakiwa kunikabidhi kwa kaka yake..., si eti jamani, mtu kaokota mtoto cha kwanza kufanya ni nini, ni kutangaza kwa watu, kuwa umeokota mtoto, mtoto ni wa nani,.....haya tufanye hata kaka yake hawajuani vyema, sasa huyo kaka yake ambaye anadai ni baba yangu alikuwa wapi mpaka nipotee maporini, hakuwahi kutangaza au kuuliza kuwa kapotelewa na mtoto,...jamani huyu mtu anatufanya sisi wajinga hatuwezi kufikiri....’ akasema

‘Je wewe hukuwahi kumuuliza swali hilo wakati mnaishi naye....?’ akaulizwa

‘Swali gani, maana mimi nilikuwa namkera sana kwa kumuuliza maswali mengi tu, kutaka kujua ukweli, muulizeni mwenyewe hapo, nilikuwa namkera kwa maswali mapaka anakasirika, na kuamua kwenda kuninywea, .....’akasema na watu wakacheka.

‘Hebu toa mifano michache ya maswali uliyokuwa ukimuuliza,.....’akaambiwa

‘Niliwahi kumuuliza swali mara nyingi la uasili wangu, kwani mwanzoni kiukweli nilijua yeye ni baba yangu, akaja kuniambia yeye sio baba yangu, nikataka kujua kwanini yeye sio baba yangu, ndio akaja kuniambia kuwa aliniokota tu maporini...’akasema

‘Baadaye akaja kuniambia kuwa eti amewagundua wazazi wangu ni akina nani, lakini iwe siri yangu maana akisema hatutapata tena misaada, mimi kama mtoto nilikubaliana naye, lakini moyoni sikufurahia kudanganya ...

‘Sasa ndio akaja na uwongo uliopitiliza kuwa eti kagundua kuwa baba aliyenizaa ni kaka yake, na bahati mbaya kaka yake na mkewe waliachana, na mimi nikawa nalelewa na mama, eti mimi yawezekana nilimtoroka mama nikapotea maporini...hiyo ndio hadithi yake aliniyotungia...’akasema na watu wakacheka.

‘Hukuamini alipokuelezea hivyo?’ akaulizwa

‘Hata ungelikuwa wewe, je ungeamini uwongo kama huo...., kama ni hivyo, kwanini asinirudishe kwa huyo mama yangu, si unajua mama walivyo wakipoteza watoto wao wanavyoteseka, angenipeleka huko kwa mama yangu, au kumwambia kaka yake kuwa kaniokota, yeye kafanya nini,....?’ akawa kama anauliza

‘Je waliwahi kukuonyesha huyo mama wanayedai ni mama yako...?’ akaulizwa

‘Ndio, ....kipindi cha mwisho, nilipokuwa huko, aliwahi kunilipeleka kwa mama mmoja  hivi, wakadai huyo ni mama yangu, mama mwenyewe anaonekana kachanganyikiwa....’akasema

‘Kwa vipi...?’ akaulizwa

‘Aliponiona alibakia hivi.....kunitolea macho,...kunikodolea macho, akawa kama anataka kunimeza, au kutaka kunifanya kitu kibaya, ...nikakimbia...’akasema

‘Unahisi kwanini walisema huyo ndiye mama yako?’ akaulizwa

‘Mimi nahisi walimtafuta mama mwenye shida, wakamuhonga pesa, ili ajifanye yeye ni mama yangu, ..mimi siwezi kuwa na wazazi kama hao, hebu niangalieni mimi, na hao wazazi hatuendani kabisa...’akasema na watu wakacheka

‘Kwani hao wazazi wapoje, hawafanani na wewe....?’ akaulizwa

‘Hawafanani na mimi kabisa, kabisa....huyu mtu ni tapeli,...rejeeni historia yake na
mambo ambayo amekuwa akiyafanya, anauza dawa zisizo na utaalamu,kachukua majani na magome ya miti, ... anawahadaa watu kuwa zinatibu,...hana utaalamu wowote, hebu muulizeni kaenda wapi shule ya madawa, ..eti anajiita profesa...’akasema na watu wakacheka

‘Na zaidi akashindwa kutumia akili ya kujenga hoja ya uwongo wake, angalau akatafuta watu wanaofanana-fanana na mimi....ananitafutia watu wenye sura mbaya...’akasema na watu wakacheka.

‘Wewe unahisi ulizaliwa wapi....?’ akaulizwa

‘Mimi nahisi,..... naweza nikawa nimezaliwa huko huko, au hata huku, siwezi kujua maana yeye ndiye anajua aliniibia wapi, ...yawezekana alikwenda hospitali akaniiba na kuniweka msituni na kunipiga picha ili ionekane hivyo....’akasema na watu wakacheka.

‘Jamani hili sio la kucheka,...., wanadamu ndio tumefikia hapo, watu wanaweza kufanya chochote, ili tu wapate pesa,...bila kujali ni halali au ni haramu, bila kujali utu wa wenzake, ....hivi hamjasikia katika sehemu za Afrika kuna watu wanakata wanadamu wenzao viongo vyao vya mwili wakidai eti watapata utajiri kwa kutumia viungo hivyo...., hamjasikia hizo taarifa, basi huyu mshitakiwa anatokea huko, ....’akasema na watu wakaguna na wengine kufikia kuzomea.

‘Tufuate utaratibu hatutaki kelele mahakamani...’akasema hakimu akigonga kirungu chake.

‘Samahani muheshimiwa hakimu, sikuwa na nia ya kuwafanya watu wapige kelele, lakini ni muhimu wakalielewa hilo, kuwa mbele ya mali, mbele ya pesa, mbele ya  utajiri, cheo ,madaraka, watu hawajali tena ubinadamu, ....kwahiyo yote haya yanawezekana kwa wanadamu wenye tamaa kama huyu mshitakiwa,....’akasema muendesha mashitaka.

Wakili mtetezi akasema muendesha mashitaka anachofanya ni kutoa maoni yake, hayo maelezo hayana msingi wowote na kesi iliyopo mbele ya hakimu, na hakimu akasema muendesha mashitaka aendelee, lakini amtumie shahidi kutoa maelezo,  sio yeye kutoa maelezo yake binafasi.

‘Sawa muheshimiwa hakimu.....’akasema muendesha mahitaka.

‘Je shahidi, ... kwanini unafanya hivyo, kwanini unajitolea huyu mtu aliyekuwa mlezi wako afungwe?, kwani wewe huna upendo kwa mlezi wake.., angalau kwa kumshukuru kwa wema aliokutendea....?’ akaulizwa

‘Mimi sio kwamba namchukia mlezi huyu, kweli kuna mengi alinisaidia,....lakini mimi kama raia mwema natimiza wajibu wangu, nimesoma, nina elimu, nafahamu sheria na haki za binadamu,... na natambua haki za raia, ..natambua utu wa binadamu,...sasa elimu yangu itakuwa na fadia gani, kama nitaona mabaya, ...nitaoa udhalimu, wizi, unatendeka halafu nikae kimia....’akasema

‘Kiukweli mimi niligundua anachofanya huyu mtu sio haki, hajali utu wa wengine, anafikia kuwazalilisha watu wengine kwa kuchukua siri zao za ndani, mambo ya chumbani ya siri, anayatumia kama biashara,  huu sio utu,...hata kama mtu kakosea,njia njema ni kumuendea na kumuelezea, kumshawishi,..kwa hekima ,na sio alivyokuwa akifanya huyu mtu....’akasema

‘Uliwahi kuziona hiz siri za chumbani, eeh, japokuwa ulikuwa mtoto huruhisiwi, lakini labda kwa bahati mbaya, au yeye mwenyewe alwiahi kukuonyesha ...?’ akaulizwa

‘Alikuwa anafanya sana siri, akija na video zake anajifungia chumbani, hakupeda nizione,  lakini kuna siku niliingia chumbani kwake, nilikuwa natafua kitu, akiwa nje, nikaona moja ya kanda ya video, nikaona nione ndani kua nini, nikaweka kwenye komputa aliyokuwa nayo, mamama....sio nzuri, mwenye niliziba macho, na muda huo huo akawa kaingia

‘Akakukuta ukiwa unaangalia, akasemaje...?’ akauliza

‘Unafanya nini wewe,...akaniambia hivyo, nikamuuliza kwaninii anachukua video chafu kama hizo, wakati hata shuleni tumeambiwa hazitakiwi, akasema hizo zitamuingizia pesa....’akasema  na watu wakecheka

‘Zitamuingizia pesa,! Kwa vipi, hukumuuliza swali kama hilo?’ akauliza na mtetezi 
akaweka pingamizi, na muendesha mashitaka akauliza kwa namna nyingine, na shahidi akasema.

‘Alipokufuma ukiziangalia, ...je aliwahi kukuambia kazipataje, kazinunua au zimetoka wapi....?’ akaulizwa

‘Alisema hajazinunua, ....nikamuuliza zimetoka wapi, akasema, yeye ni mpelelezi huru, wa kuwaadhibu watu hasa wanaojifanya ni viongozi au waume wanaojifanya ni waume safi lakini kwa siri ni wachafu..akaniambia anachofanya yeye ni kutafuta uchafu wao kama huo, na kuwaadhibu,...’akasema

‘Kuwaadhibu! Kwa kuchukua picha kama hizo anawaadhibu, alikuwambia kwa vipi?’ akaulizwa

‘Ndio nilimuuliza kwa vipi, akaniambia, akizipata kama hizo anawasiliana na hao watu, na kuwaambia kagundua huo uchafu wao kama ni waume za watu, na kama kiiongozi, huenda kakiuka maadili ya kazi, anamwambia hivyo hivyo, ....kuwa kagundua madhambi yake....’akasema

‘Halafu.akishayagundua, anakuja nayo nyumbani anayaweka tu...’akasema muendesha mashitaka.

‘Hayaweki tu, ....akishawasiliana nao, anawatishia kuwa wasipompa pesa anataka kiasi fulani, basi atayaanika madhambi ya hadharani, au atampelekea mke wa huyo mume....ni mtu wa ajabu kweli!’akasema na watu wakacheka

‘Uliwahi kumsikia akifanya hivyo, au alikuelezea kuwa anafanya hivyo....?’ akaulizwa

‘Alinielezea tu, anasema akiwasiliana na hao watu hawezi kuwasiliana nao nyumbani, anatafuta simu za mitaani, .....’akasema

‘Sasa ukasikia hivyo, ukaona hivyo...wewe ukiwa kijana mdogo muda huo, ulilichukuliaje hilo,....licha ya kuwa wewe ulikuwa ni mdogo...siulikuwa mdogo wakati umezifuma hizo kanda za video, au...?’ akaulizwa

‘Nilikuwa mdogo ndio, lakini nilishakuwa na akili,....mkubwa ,nimeshabalehe...Kiukweli, mtu kama mimi sikupenda hiyo hali, shuleni tumefundishwa maadili mema, kuwa matendo kama hayo, mapicha machafu kama hayo, hayafai, sasa mzazi, mlezi, anayaleta nyumbani na anasema ndiyo yanayompatia pesa.... niliumia sana...’akasema kwa sauti ya uchungu.

‘Kwahiyo ukawa unaishije na mtu kama huyo...?’ akaulizwa

‘Kiukweli sikupenda kuishi na mtu mwenye tabia chafu kama hizo, na hata wenzangu walianza kuninyoshea vidole kuwa baba yangu ana biashara haramu, anauza madawa haramu...’akasema

‘Waligundueja au wewe uliwaambia...?’ akaulizwa

‘Hata mimi sijui ...waligunduaje,...labda ni kutokana na ile kesi aliyowahi kushitakiwa kuwa unauza madawa ..’akasema

‘Kwahiyo shuleni, au katika hali ya kawaida ulijisikije,...?’ akaulizwa

‘Nilijisikia vibaya sana, nikawa sina raha, ...lakini nilimtetea mlezi wangu huyo, na hata kupigana na wengine, waliponitania...ikafika sasa moyo ukaanza kuniambia kuwa huyu  mtu anaweza kuwa kweli sio baba wa kweli, yawezekana ananitumia tu.....’akatulia.

‘Kwa uoni wako ulivyomuona alifaa kuwa mlezi wako,au mzazi wako?’ akaulizwa

‘Kwa uoni wangu japokuwa nilikuwa mdogo, niliona kabisa huyo hafai kuwa mzazi wangu, au mzazi wa yoyote yule,....’akasema.

‘Ulishawahi kumuambia hivyo, kuwa yeye hafai kuwa mlezi wako au wa yoyote yule?’ akaulizwa

‘Ndio..., kuna siku nilimuambia hadi tukafikia kugombana kwa hilo, nikamwambia kuwa yeye hastahiki kuwa mlezi wangu au dad wangu...’akasema

‘Akafanyaje, alichukua hatua gani kwako....?’ akaulizwa

‘Alienda akalewa...huwa akikasirika analewa, akija ni vurugu, basi siku hiyo alipokuja akaanza kunisema, akasema....ooh, ....wewe ulikuwa hujui eeh,...wewe ni mtoto wa kuokotwa tu, ..., usiye na baba wala mama....mimi nimejitolea kuwa mlezi wako, halafu huniheshimu...unasema sifai, unafikiri unakula nini,..kama ni uchafu kama ni madhambi, lakini.....ndio unakula....’

‘Hebi nikuulize kwanza,  wewe si ulikuwa unaishi kwa asilimia shuleni, bwenini au....?’ akaulizwa

‘Mwanzoni ilikuwa hivyo,  nilikuwa nakaa shuleni, lakini baadaye aliamua nikae naye....’ akasema

‘Kwanini...?’ akaulizwa

‘Ni ili aweze kupata pesa nyingi kutoka kwa wafadhili, mwanzoni sikujua lengo lake hilo, akaja kuniambia hivyo,...sikukataa, nikakubali tu, nikijua yeye ni dad wangu...’akasema

‘Ukilinganisha maisha ya kuishi naye nay a bwenini, ni yepi bora?’ akaulizwa

‘Kiukweli kwa hali kama hiyo, niliona aheri ningelikaa huko huko bwenini,...na alivyonisema hivyo, kuwa mimi ni mtoto wa kuokotwa,...niliumia sana...ilimuambia mimi narudi kukaa bwenini..’akatulia

‘Akasemaje, ...?’ akaulizwa, na wakili mtetezi akasema maswali anayouliza muendesha mashitaka hayana msingi na hiyo kesi, ni kupoteza muda.

‘Ndugu muheshimiwa hakimu, msingi wa maswali haya ni kujua tabia ya huyu mtu, ili mahakama yak tukufu ione ubaya wa huyu mtu kwa jamii, ...jinsi gani watu kama hawa wanavyoharibu kizazi cha taifa,.....na ni moja ya mashitaka yake...’akasema muendesha mashitaka na hakimu akasema aendelee

‘Lakini usipoteze muda wa maswali yenye kujirudia rudia...shahidi endelea kujibu swali uliloulizwa’akasema hakimu

‘Siku ya kesho yake aliniomba msamaha, huwa anafanya hivyo na mipombe yake ikimuishia kichwani anakuomba msamaha, na kusema aliongea tu kwa vile alikuwa kakerwa na kauli zangu, na alikuwa kalewa kuondoa mawazo, ...’akasema

‘Kwa maoni yako, kabla hatujamalizana na sehemu hiyo unaweza kusema nini kuwaambia wazazi kama hao....’akaambiwa, na wakili mtetezi akasema wakili huyo anauliza maswali ya kuhitimisha,na hakimu akasema anaruhusu asikia kauli ya ya huyo kijana...

‘Kama mimi, ninachoweza kuwaambia watu kama hawa wanaojifanya ni walezi, au wazazi kwa njia ya udanganyifu, wasifaye hivyo, kwani wanawaharibu watoto, wanawajengea watoto ,vijana tabia mbaya....’akasema

‘Ndio maana kwa moyo wangu wote nikaapa siku nikipata nafasi, nitajitahidi kuisaidia serikali kuwafichua watu kama hawa, kupambana na hawa wahalifu....na nasema hata nikirudi huko ninakoambiwa nimetokea, ndio ...sitakataa kurudi maaa huenda, ndio nyumbani kweli, lakini kama raia mwema,nitasaidia kuwapinga wazazi wenye tabia kama hizi, kuwa hawafai kwenye jamii,...’akasema

‘Kwani wewe hukubali kuwa umetokea huko alipotokea mshitakiwa...?’ akaulizwa

‘Nakubali mimi huenda nimetoka huko maana hata ngozi yangu ni ya huko, lakini sitakubali kupewa wazazi kama hao, waongo...wahalifu matapeli...na hata wakisema vipi kuwa wao ni wazazi wangu, sitakubali kamwe,...hao sio wazazi wangu kabisa....’akasema. na watu wakashangilia.

‘Maana kiukweli wazazi kama hao, kwa tabia kama hiyo, lolote wanaweza kufanya hata kuua....’akasema na watu wakacheka.

‘Wazazi kama hao, wanaweza hata kuua, kwanini unasema hivyo....’akasema muendesha mashitaka na wakili mtetezi akapinga hilo swali,
Muendesha mashitaka akamgeukia hakimu na kusema

‘Ahsante wakili mtetezi umenisaidia kunikumbusha kuwa swali hilo litakuja kwenye sehemu ya pili ya shitaka la muaji..., ndugu muheshimiwa hakimu nimemalizana na shahidi huyu kwa sehemu hiyo, nitaendelea naye kwenye kipengere kingine...’akasema na kugeuka kurudi sehemu yake.

Hakimu akawaruhusu upande wa utetezi wamuulize huyo shahidi, na wakili mtetezi akasimama kwanza akawa kama anawaza jambo, akatulia pale pale kwa muda, ....

Halafu kwa taratibu akatembea kumsogelea huyo shahidi huku akamuangalia moja kwa moja usoni..., na shahidi naye akawa anamuangalia huyo wakili bila kuangalia pembeni au chini,  wakawa wanaangaliana, na hata wakili huyo alipomkaribia huyo shahidi hakuacha kumuangalia hivyo hivyo.

Dakika moja ikapita wakiwa hivyo... mpaka watu wakacheka....

‘Wakili mtetezi, huna maswali ya kumuuliza shahidi huyo,...kama huna maswali tuingie sehemu nyingine...’akasema hakimu. Na wakili mtetezi akiendelea kumtizama huyo shahidi machoni moja kwa moja halafu akasema;

‘Huyu shahidi  ni muongo, wewe ni muongo, unaiongopea mahakama, unajua hilo  kosa kubwa, kuongopea mahakama....’akaanza kusema wakili mtetezi,na shahidi akataka kujitetea, lakini wakili muendesha mashitaka akamuashiria atulie....

NB, Tuone mapambano ya wanasheria wakiwa mahakamani, ....na ndio tutafichua siri kubwa ya mauaji yaliyotokea je ni kweli profesa ndiye aliyefaya hayo mauaji au kuna mtu mwingine...

WAZO LA LEO:  Uharibifu mwingi, uchafu mwingi, dhuluma....nk, unaenea duniani kwasababu watu wameshindwa kupambana nao, kuambizana ukweli, kukosoana, kukatazana,...watu wanamuona mtu ni mkosaji, muharibifu, mfisadi, mdhulamaji, lakini hawataki kumsema, kumkemea,kumwambia au ....kumuelimisha, au kumchukulia hatua, eti kwasababu ni mtu mkubwa, eti ni mwenzetu, eti ni ndugu yetu,...
Na matokea yake mambo hayo yanatapakaa yanaonekana ni kawaida tu, baraka inatoweka,...uchafu, na ubaya unazidi, unaenea,....

Jamani, tusipoamrishana kutenda mema, na tukakatazana kutenda maovu, dunia yetu itakuwa hivyo, vurugu, dhuluma, ufisadi,watu wataishi kiujanja ujanja, ...na amani itakuwa ni kitendawili.

ANGALIZO: Kampeni ndio hizo zimeanza, tuwapime wagombea wetu kwa kuwahoji mambo yenye tija, tuuone uadilifu wao,...kwasasa ni kauli zao tu, matendo yao tulishayaona, kwani tuliishi nao, wakafanya waliyoyafanya wakiwa watendaji, .....je kwa kauli zao wataweza kutuhakikishia hilo...kutuhakikishia uadilifu wao mbele ya mungu,  ili maandiko yawekwe, kumbukumbu ziwepo, ,...Ni mimi: emu-three

No comments :