Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeMonday, August 3, 2015

RADHI YA WAZAZI-27‘Bro, siku ninasomewa mashitaka yangu sikuamini...., ‘ akaendelea kuhadhia jamaa akimuhadithia kaka yake,

‘Mashitaka gani....?’ akauliza kaka mtu

‘Ya kuua.....’akasema

‘Ina maana uliua...?’ kaka mtu akauliza kwa mshangao.

‘Si...nilikuambia niliwahi kufungwa kwa kesi ya mauaji,....’akasema

‘Sawa, uliniambia ulikuwa na kesi , ukafungwa, ...sasa ninachokuuliza je ni kweli uliwahi kuua, na ulimuaa nani....ndio swali langu?’

Wewe tuendelee na simulizi la maisha yangu ya Ulaya, na kijana wetu, utakuja kufahamu yaliyonikuta, sio mchezo kaka, usinione nipo hivi,....nusu mfu , ukafikiria ni madawa ya kulevya, sio kweli....sio kweli....sikiliza kisa uelewe mwenyewe

‘Na kijana naye .....hakuwahi kujiingiza kwenye hayo maisha mabaya....mimi sitakuelewa kwa hilo....?’ akauliza

‘Kijana wako sio mtu....sijui kachukua damu na tabia ya nani.....alichonifanyia huko ulaya,sitaki hata kukutana naye tena, hanijui, hanitambui, .....’akasema

‘Kwaini,.....ilikuwaje akabadilika hivyo, hata wewe asikutambue, wewe dad wake,....hahaha, hebu endelea na kisa chako,maana yote umeyataka wewe,nataka kujua maisha yake yalikuwaje, na je atarudi lini huku nyumbani....’akasema

Tuendelee na kisa chetu

********

Bro, siku nafikishwa mahakamani kusomewa shitaka la kuua, nilibakia kama mtu zezeta, mtu aliyechanganyikiwa, sikuamini.....’ akaanza kuongea akimuangalia kaka yake , kaka yake akitaka kuongea lakini hakumpa nafasi akaendelea kuongea

‘Nilishitakiwa kwa kosa la kuua,.....kosa la kuwa kiongozi wa biashara ya mlungula,....kosa la kuendesha biashara ya mdawa haramu, kosa.....,yakatajwa makosa mengi na mwisho, kosa la kuishi kwenye nchi hiyo kinyume cha sheria...’akatulia

‘Bro....ukitajiwa kesi ya mauji hata kama hujaua, unakuwa unakioa kitanzi shingoni mwako....unajua siku yoyote utanyongwa, utafungwa kifungo cha maisha, au...ukikoswa koswa,kifungo cha miaka mingi jela.....,’ akaendelea kusimulia

‘Kwahiyo mimi nikasimamishwa mbele ya hakimu, kwa mara nyingine, na safari hii, ukipatikana ushahidi wa kumrizisha hakimu, basi....,mimi ni mtu wa kunyongwa, .....’akatulia akishika shavu

‘Bro,na ujanja wangu wote, nililia....hahaha,  unaamini hilo bro, ilifikia muda nilitoa machozi na sio mara moja, kwa kesi hiyo...nilijuta, nikaomba, na kumkumbuka mama......’akatulia

‘Mambo yakikufika shingoni, hata kama ulikuwaje, utamkumbuka mama yako....hahaha, unajua bro, nimeishi ulaya siku zote napambana na maisha ya shida, ...lakini sikuwahi kuwakumbuka wazazi wangu, .....maana ukiwakumbuka na maisha niliyokuwa naishi, utaogopa, ...ni maisha yasiyofaa, sasa wazazi hapo utawakumbukaje....’akatulia

‘Bro, lakini  siku nasubiria, siku nasubiria.....kuwa napelekwa jela ,....kwanza ile nasubiria kupelekwa gereza baya kuliko yote huko....nilimkumbuka mama, nikalia,....’akatulia

‘Profesa Mti dawa,...., unahaki ya kutafuta wakili,...na kesi yako itasikilizwa tarehe.....’yaliyokuwa yakiongelewa siku hiyo skuweza kuyasikia kabisa, ni neno moja moja,....nilisikia tu pale nilipoamurishwa nisimame, ili kurudishwa rumande....

‘Simama, twende huku....’ 

Nikasimama nikipepesuka,...mwili hauna nguvu, njaa, ...na mawazo, unajua ilikuwa siku ya tatu, siwezi hata kula, chakula hakimezeki....maana nlikamatwa ijumaa usiku, jumamosi, ...ilikuwa siku ya kuhojiwa, ...nilihojiwa siku nzima, mapaka akili ikawa hafanyi kazi,na jumapili, nikawa nimelala tu,...lakini usingizi upo wapi, mawazo tu

‘Na Jumatatu, ndio nikafikishwa mahakamani,....kwahiyo sikuwa na nguvu kabisa, na pale nilipoambiwa, twende huku,...nilikuwa nakokotwa tu... na ghafla kitu kikatanda usoni, nikajikuta nikizama kwenye giza,....nilipozindukana nilijikuta nipo kitandani, hospitali na pingu mkononi.....

‘Lakini hujasema ilikuwaje,....uliuaje, au ilitokeaje mpaka ushitakiwe kwa mauaji,..uliua kweli, au...?’ akauliza kaka mtu.

********

'Bro, ....sikumbuki ku-ua....' akasema mdogo mtu

'Sasa ilikuwaje....?' akaulizwa

'Bro wewe endelea kusikiliza utanielewa tu....'akasema

 Basi profesa alizindukana, kutoka kwenye kupotewa na fahamu na alijkuta yupo kitandani na pingu mkononi....askari wakimlinda asije kutoroka.

Profesa alishaonekana ni mtu hatari, ni kiongozi wa kundi hatari, lililokuwa likitafutwa na polisi kwa muda mrefu, kwa biashara ya mlungula, huko wanaita blackmail.

'Bro,niliandikwa kwenye magazeti yote kuwa hatimaye yule mtu hatari wa biashara ya mlungula, amekamatwa, na nimekamatwa nikiwa nimeua mtu mwingine...usikie magazeti yalivyo wachohezi, eti, nikiwa nimeua mtu mwingine....’akatulia.

‘Niliua lini bro, hivi mimi naweza kuua mtu,...na tena waliandika kuwa huyo aliyeuwawa ni wa pili, lakini ili kunogesha biashara yao ya magezeti,ili nionekane mtu mbaya,.....wakaandika hivyo, na ukisoma ndani huoni hayo mauaji mengine nilivyoyafanya na mimi, na inasemekana...’akatulia.

‘Basi nilipofikishwa hospitalini, unajua hakuna dawa zaidi, ilikuwa driu ya maji ya glucose,sijui kama kuna zaidi, ikanirejesha kwenye uhai, nikawa mtu tena,..ilikuwa na njaa, na zaidi ni mawazo...siwezi kusema nilipigwa, niliwahi kuzabwa vibao viwili vitatu, wakati nahojiwa siku ile ya jumamosi lakini havikuniathiri...

‘Unajua wenzetu wapo makini sana na watuhumiwa, kuna haki za kumlinda mshitakiwa, wanakuwa makini sana, wasije kulaumiwa kwa hilo, kwahiyo sikuteswa, sikushinikizwakwa vitisho, wao wana mbinu zao nyingine,  za kisomi,na utajikuta unasema tu....’akatulia.

Basi nikiwa pale hospitalini, nikiombea kama yawezekana niendelee kukaa hapo, lakini huna ujanja, ....siku ya pili nikaambiwa hali yangu ipo shwari naweza kurudishwa rumande...hapo moyo pwaaah, unajaribu kuzuia ubongo, iwe ni ndoto, iwe sio kweli....

‘Basi bro.., nikatolewa hapo hospitalini hadi rumande, nilipokuwa nimeshikiliwa,na huko nikaambiwa siku inayofuata nitapelekwa gerezani, kwani hapo hawakai watu wauwaji kama mimi....

‘Endelea na kisa chako...’kaka mtu kwanza alitaka kuuliza swali, lakini akaona atavuruga utaratibu wa mdogo wake,

******

‘Nimeua...mimi sijaua....’nikasema kwa mara ya kwanza baada ay kutoka hospitalini na kufikishwa rumande na sasa naambiwa kuwa nahitajika kupelekwa gerezani, na gereza lenyewe nililotajiwa, ni gereza baya sana.....

‘Wengi  walio-ua huwa wanasema hivyo hivyo...kwahiyo kwako mimi sioni ajabu.’akasema askari mmoja wa hapo ani askari mdogo,tu, lakini naye alikuwa na na kazi ya kunihoji ili kuweka kumbukumbu zao, na yeye anasema alikuwepo kwenye harakati za kunikamata na kwa muda huo, alifika kuweka mambo yake sawa, kabla sijaondolewa hapo.

‘Afande mimi sijaua,....mungu ndiye shahidi,....nilifika nikakuta huyo mtu ameshauliwa, nimeeleza na kuelezea tena, sijui mnataka niseme nini,....huo ndio ukweli ulivyo....’nikasema kujitetea.

‘Hayo tutayaona mbele ya hakimu, ila nilitaka tushirikiane vizuri, tusipoteze muda, ukiri kosa, na nione jinsi gani ya kukusaidia, sasa huko mbele utakutana na wanaohusika mimi nitafika kama mtoa ushahidi tu....’akasema huyo ofisa usalama, na pemeni yake alikuwepo mkuu wa kituo hicho.

‘Mnaona hali yangu ilivyo,naumwa,....sasamimi nawaomba munisaidie nisipelekwe gerezani, huko kwa afya yangu wataniua hao watu wa huko,...mimi sijaua, hizo ni mbinu zimefanywa ili nikauliwe huko.....huo ndio ukweli,mtafuteni muaji halisi, ....mtampata tu, lakini sio mimi...mnapoteza kwa mtu asiye na hatia...’akasema profesa

‘Kama ulijua usingejiingiza kwenye tabia hiyo chafu, watu kama nyie hata mimi siwapendi,..japokuwa haki za binadamu zipo lakini nyie watu hamstahili kukaa na jamii....wewe ni kiongozi wa mlungula, na nakumbuka sio mara ya kwanza kushitakiwa kwa makosa kama hayo...’akasema mkuu wa hicho kituo

‘Yote ni makosa ya kusingiziwa, wewe mwenyewe si ulioana kwenye kesi iliyopita, mbona baadaye nilikuja kuachiwa, walipofanya uchunguzi nikaonekana sina hatia ni uonevu tu, sisi waafrika mnatuonea sana,ni kwanini mnatuchukia...?’ akauliza profesa

‘Hamna cha Uafrika hapo, hakuna cha ukabila hapa, kinachotafutwa ni haki, ...huwezi kufanya kosa ukajivika uhali yako, wengi wanatumia uhali zao,ukabila udini, kufichia makosa yao, wanafikiria wakijivika kilemba hich hawatapatikana kirahisi....’akasema ofisa mpelelezi

‘Hebu fikiria ni hali gani mnayomsababishia mtu mliyemuingiza kwenye hiyo biashara...., unajua watu wengine hufikia hata kutaka kujiua, ....’akasema mkuu huyo.

‘Sio kutaka, wengine wanajiua kweli....na kosa ni la hawa watu, wanachofanya ni kutoa vitisho baada ya kutengeneza uchafu wao, mambo ambayo hayakutakiwa kuonekana kwa jamii, mnatishia kuyatangaza, mnadai pesa,kama mtu hana pesa mnafikii atafanyaje....anaona ni bora afe tu kuliko kuadhirika.....’akasema huyo mpelelezi.

‘Lakini mimi sijawahi kufanya hivyo, ....mimi nimekuwa raia mwema, ...mengine wanaisingizia tu afande....’akasema profesa

‘Ushahidi tunao,...nimefika hapa kukuona tu, kuhakikisha kuwa kila kitu kipo kama inavyotakiwa, na kesho nitakuja kuhakikisha umefika gerezani, ...’akasema

‘Ina maana hamtaki kunisaidia ,mimi naumwa, kwanini mnampeleka mgonjwa gerezani, hiyo sio haki, zingatieni haki za binadamu.....’akasema

‘Leo wewe unaona una haki, je hao raia uliokuwa ukiwasumbua hawana haki,...wana haki ya kuishi kwa usalama, lakini nyie watu wacheche mnakuja kuwasumbua, mumeharibu amani ya eneo letu, kwa tamaa zenu za utajiri wa haraka haraka na sasa mnafikia kuua, yule jamaa  wa watu ana kosa gani....’akasema

‘Afande, nimeshakuambia mimi sijaua..mimi sio muuaji,nieleweni jamani.’akasema

‘Mhh, najua utakana sana, hakuna muuaji anayekubali kosa...lakini ushahdi wote umeshapatikana kuwa wewe umeua...’akasema

‘Ushahidi gani huo, najua utatengenezwa tu, kwani hilo ni gumu, ....’akasema profesa

‘Bastola uliyotumia kumuua huyo jamaa, ina alama zako za mikononi....mashahidi wanaokujua kwa tabia zako chafu wameshapatikana, na jinsi ulivyopanga huo mchezo mchafu imeshajulikana, kila kitu kipo wazi,.....sasa utabisha nini....’akasema

‘Kwa hali hiyo,nahitaji wakili afande, naona nikiongea na nyie hamtanisaidia kitu, nimeshawaambia ukweli wote humuamini,...najua bila wakili mtamfunga mtu asiye na hatia nyie watu mna chuki sana na ngozi nyeusi....nawajua sana nyie watu..., ’akasema profesa akijua akisema hivyo itasaidia.

‘Wakili utampata hiyo ni haki yako, kama unahitajia wakili wa kujitegemea ni pesa yako, kama unahitajia wakili wa serikali atakuja mtaongea naye....sasa ni wakati wako kujipanga, najua unazo pesa nyingi sana kwa tabia hiyo chafu....’akasema mkuu wa hicho kituo akimuangalia askari mpelelezi aliyekuwa akiandika kumbukumbu zake.

‘Nimechukua pesa gani  mnanizulia bure, mim sikujua kuna pesa, sikujua kuwa huo mzigo ni pesa, kama ni pesa basi mumeziona nyie,....’akasema

‘Unajua kabisa kuwa mzigo huo ni pesa, unajua kabisa kwasababu wewe ni kiongozi uliyekuwa ukiongozo hilo kundi la mlungula, na unajua kabisa pesa hizo zipo wapi....’akaambiwa

‘Sijui niwaambie nini ili muweze kunielewa, mimi ni kama tarishi tu, kuwa ...nikachukue mzigo sehemu fulani, kama nilivyowaelezea awali, mara nyingi huwa nachukua ile sehemu ya hotelini hapo kunajulikana, lakini safari hii nilielekezwa kwenye hilo jengo, kwenye hiyo hoteli,....na niliambiwa ni mzigo,sio pesa,...’akatulia

‘Uliambiwa utakutaje huo mzigo....?’ akaulizwa

‘Niliambiwa nikifika hapo nitakutana na mtu na huyo mtu atanikabidhi huo mzigo...’akasema

‘Sasa mkisema ni pesa, mimi siwaelewi,...na nilipofika hapo, ndio nikamkuta huyo mtu kalala sakafuni, ....’akasema

‘Je huo mzigo uliukuta...’akaulizwa

‘Nimewaambia sikuweza hata kuhangaika na huo mzigo..., nilimuona huyo jamaa akiwa kalala sakafuni akitokwa na damu , kwenye dimbwi la damu,na hali kama hiyo hata kama mzigo ungekuwepo nisingeliweza kuuchukua.....’akasema

‘Ukafanya nini sasa ....?’ akaulizwa

‘Nikataharuki, nikatoka mbio, nikiwa na lengo la kutafuta kibanda cha simu ili niwapigie simu polisi, ndio natoka kwenye hicho chumba, nikapigwa na kitu kisogoni, nikapoteza fahamu....’akasema

‘Hukumuona aliyekupiga hicho kitu kichwani.....?’ akaulizwa

‘Sikumuona kabisa...’akasema

‘Ikawaje...?’ akaulizwa

‘Nilipoteza fahamu, nilipoamuka,...nikawa najaribu kukumbuka,....kwa vile nilizimia, na sikuelewa, na kichwa kikawa kinaniuma sana, nikaanza kutanga tanga, huku najaribu kukumbuka, na kutanga tanga huko, nikajikuta nipo nje, nikasikia mlio wa king’ora cha polisi, nikahisi kuogopa nikakimbia....’akasema

‘Ukakimbilia wapi?’ akaulizwa

‘Sehemu ya jirani tu, nikatafuta sehemu nikalala kidogo, kichwa kilikuwa kinaniuma sana, nikatafuta dawa ya maumivi,nikameza.....’akasema

‘Dawa ulizipatia wapi...?’ akaulizwa

‘Nilinunua dukani,.....’akasema

‘Nilipomeza nikatulia, nikitafakari la kufanya,....na hapo ndio nikajaribu kukumbuka jinsi ilivyotokea, nikaona sasa ni bora niwafahamishe polisi, na wakati natoka ndio nikakamatwa...’akasema

‘Wewe unasema ulitumwa kuchukua mzigo ni na nani hao waliokutuma....?’ akaulizwa

‘Nimeshakuambia kuwa hao watu siwajui tuliwasiliana nao kwenye simu tu,....’akasema na mpelelezi akatikisa kichwa kuonyesha kupoteza muda wake. Na mkuu wa hicho kituo akauliza

‘Sasa ukichukua huo mzigo unaupeleka wapi...kama waliokutuma huwajui na unaowapelekea huwajui?’ akaulizwa

‘Waliniambia nikikabidhiwa huo mzigo niwaambie tayari, halafu wao watanielekeza wapi sehemu ya kuupeleka huo mzigo,...’akasema

‘Watu waliokutuma huo mzigo huwafahamu,....wakakuambia ukiupata wanakueleza wapi pa kuupeleka, wewe unawaamini vipi, je yakiwa ni madawa ya kulevya, ....?’ akaulizwa

‘Ukiwa katika hali yangu, huna uhakika wa ajira kazi yoyote unaweza kuifanya, ili mradi mwisho wa siku unapata ujira wako....’akasema

‘Kazi yoyote unaweza kuifanya, au sio....?’ akaulizwa

‘Ndio, ilimradi naiweza, na ni sahihi .....na kazi zenyewe ni hizo za kutumwa mizigo, mara nyingi ndio kazi zangu, kutumwa, kufanya usafi,..na vitu kama hivyo, kazi zisizo na taabu au ubaya wowote....’akasema

‘Unapochukua mzigo kama huo, mara nyingi huko unapopeleka, unakutana na mtu mwenyewe, au unafikisha wapi....?’ akaulizwa

‘Nilishawaambia mimi nafuata maelekezo ya anayenituma, niufikishe kwa mtu, au niufikishe mahali fulani,....’akasema

‘Kwa mzigo huo uliambiwaje,....?’ akaulizwa

‘Niliambiwa nikifika hapo nitamkuta huyo mtu, atanipa huo mzigo nikishaupewa, nitapewa maagizo mengine.....’akasema

‘Na gharama zako utalipwaje,maana sizani kama unaifanya hiyo kazi bure tu.....’akaulizwa na huyo mkuu

‘Wananielekeza wapi pa kuchukua gharama zangu, gharama sio tatizo, napata ushuru wangu, bila wasiwasi, sijawahi kudhulumiwa.....’akasema

‘Kwahiyo hiyo ndio kazi yako ya kutumwa, kupeleka mizigo,...na kulipwa ushuru...,naje unawasilianaje na hao wanaokupa hiyo mizigo au hao unaowapelekea hiyo mizigo...?’ akaulizwa

‘Nimeshawaambia ,mimi nawasiliana na hao wanaonituma tu, kila kitu wananielekeza wao, sijui jingine lolote,...’akasema

‘Na kwa kazi hiyo, nilipigiwa simu kuwa niende hapo nitakuatana na huyo mtu, atanipa huo mzigo, ...siwajui ni akina nani,mimi niliwaamini najua nikiufikisha nitalipwa pesa yangu, wakati mwingine unaweza kuwafahamu, lakini kama hawa wa sasa hivi, sikuweza kuwafahamu kabisa...’akasema

‘Hayo maelezo yako hayana ukweli na hayaingii akilini...kabisa,hakuna kazi kama hiyo wewe uelekezwe kwa simu, na watu usiowafahamu, ...hata hivyo kila kazi ya kipato, inakibali, je kazi yako hiyo umepatia wapi hicho kibali..?’ akaulizwa

‘Kazi hiyo haina kibali, maana ni kazi ya muda , sio kwamba, ndiyo kazi naishi nayo hiyo tu,inatokea tu,....kwa mtu kuniamini kuwa naweza kuuchukua huo mzigo na kuufikisha sehemu husika..’akasema

‘Unafikiri ni kwanini hao watu hawafanyi hiyo kazi peke yao, mpaka wakutume wewe....?’ akaulizwa

‘Mimi sijui.....’akasema

‘Umeshawahi kutumwa mara ngapi kwa kazi kama hiyo...?’ akaulizwa

‘Mhh,sikumbuki, ...yawezekana mara tano,au zaidi..sikumbuki, ni kwa vile naaminika na watu....’akasema

‘Kabla ya kazi hiyo unakumbuka ulitumwa lini kuchukua mzigo kama huo kuupeleka sehemu fulani, ukalipwa....?’ akaulizwa

‘Mhh....hata sikumbuki, ni muda kidogo,unajua kazi kama hizo ni za muda tu,..inatokea tu, sasa sikumbuki ..sikumbuki,.....’akatulia

‘Nikuambia kitu, maelezo yako hayana ukweli, na unaposema hukumbuki, inaonyesha kuwa wewe ni muongo...’akaambiwa

‘Sasa mnataka nisemeje...niambieni mnavyotaka nyie...’akasema

‘Unajua,wewe utakumbuka tu, ukifika gerezani,huko utasema kila kitu, maana huko kuna watu wakorofi, wauwaji, walioshindikana,watu ambao huwezi kuamini kuwa walizaliwa na wazazi,hawana utu....’akaambiwa

‘Yaani mnataka nipelekwe huko kwa vile sijawaambia mnayotaka nyie, au...?’ akauliza

‘Wewe umekamatwa kwa kosa la kuua,...wewe jamii inakutambua kama mkorofi, jamii imekuchoka, hilo gereza linakufaa wewe,....’akaambiwa

‘Ina maana napelekwa kwa gereza la ....’akashindwa hata kumalizia mara akasikia kuwa ana mgeni na haraka akasimama akiwa na mawazo huenda akawa ni mtaalamuu au mtu yoyote anayemfahamu kaja kujaribu kumwekea dhamana.

‘Nasikia una mgeni wako huko, sisi tumemalizana na wewe, nitakutana nawe huko gerezani kuhakikisha umefikishwa huko, na zaidi ya hapo ni kuwa ujiandae, umtafute wakili wako, la sivyo, useme tukutafutie wakili wa serikali....’akaambiwa

‘Mimi kwa hivi sasa nawaomba, ....msinipeleke huko gerezani, na ...’akasema

‘Kuna mgeni wake huyu mtu afande, ...’huyo aliyetumwa akasisitiza

‘Sawa ...tumemalizana naye,....’wakasema na kuondoka, na profesa akabakia na askari mlinzi, ambaye atampeleka kwa huyo mgeni.

Alitembea pamoja na huyo askari mlinzi hadi sehemu ya wanapokuwa wageni, akaambiwa asubiri,..haikupita muda akaambiwa;

‘Yaonekana mgeni wako bado anaongea na mkuu, subiri kidogo

‘Nimeambiwa nina mgeni yupo huku ananisubiri, halafu tena, mnasema nisubiri kwanza huyo mgeni ni nani....’akajitetea

‘Mgeni wako anaongea na mkuu wa mkuu wa kituo....’akaambiwa

‘Kwahiyo nifanyeje, maana nimechoka kuongea na watu, kama ni askari, mwambieni nimechoka, sitaki kuulizwa maswali tena...’akasema

‘Huwezi kutupangia kazi,kwanza ujue umecheleweshwa kupelekwa gerezani, wenzako mliofungwa nao siku hiyo wote wameshapelekwa gerezani, sema wewe umesubirishwa  hapa kwa vile ulikuwa unaumwa....’akaambiwa

‘Sasa ni nani huyo mgeni wangu......?’ akauliza

‘Ni mimi....’sauti iliyomshitua, na kumfanya atetemeke mwili mnzima, na muda huo ulikuwa muda wake wa mwisho wa kuonana na mtu wa kumsaidia....,aliombea na kutarajia mgeni atakaye kuja awe mtu wa msaada, lakini sauti aliyoisikia, ilimuashiria kuwa sasa yupo matatani, sasa hana msaada tena, na...kesho asubuhi na mapema ni safari ya kwenda gerezani

Akaogopa hata kugeuka, akabakia akiwa amesimama, akiwazia mengi, akiwazia, jinsi gani atakavyopokelewa na wabaya wake, watu ambao alishawahi kukosana nao, watu ambao aliwahi hata yeye mwenyewe kuwarubuni, na hata kutoa ushahidi ili watu hao wafungwe kwa ajili ya kuingiza pesa, kwake kupata pesa ilikuwa jambo lolote,....sasa atakwenda kukutana nao huko gerezani...

‘Ipo siku na wewe utafungwa, na nipo tayari kusubiria hadi siku hiyo, ili tukatane huko gerezani, na ukija utakuwa hawara yangu.....’akakumbuka siku alipokwenda kutoa ushahidi wa jamaa mmoja aliyeshitakiwa kwa madawa ya kulevya, na yeye akathibitisha kuwa kweli aliwahi kumuoana akiuza madawa hayo.

Huko jela kuna watu wangu, ....ukifika huko ujue ndio mwisho wako....’akakumbuka hiyo sauti kutoka kwa mama mtemi.

Na leo yupo rumande anasubiria kupelekwa huko, huko kwenye gereza lililoshindikana, gereza ambalo waliwahi kufika huko wakaweza kumaliza kifungo, wakitoka, utawaonea huruma, kwani ni lazima watatoka na tatizo fulani mwilini na wengine hawamalizi mwezi, wanapoteza maisha.....

‘Gereza hilo,...liliwahi kufungwa kwa vituko vyake,....kipindi hicho lilitambulikana kama  gereza la kifo, wale wanaojulikana kuwa ni wauwaji, ...wakorofi wa jamii, ambao wanatakiwa kufia huko ndio wanapelekwa huko...kuna visa vibaya hata havielezeki,....’aliwahi kuambiwa siku moja

‘Mtu ukipangiwa kwenda huko ni bora ujiue tu....’akaambiwa

‘Hata kama hujahukumiwa unaweza kupelekwa huko?’ akauliza

‘Hata kama hujahukumiwa!, kama kesi yako ni mauji, na wewe waonekana mkorof wa jamii, ...unapelekwa ukisubiria kesi yako huko,....na hasa kama una jambo hutaki kulisema, ...na usiposema litaleta madhara,......wanakutupia huko, ukionja joto yake utasema kila kitu....’akaambiwa

‘Mhh...’siku hiyo aliogopa kabisa kwenda jela....

 Leo hii anaambiwa kesho anapelekwa huko, na ili asipelekwe huko, labda kungelitokea wakili akaongea na wakuu wa hapo au wa huko, huenda wangelimtetea,...huenda angelipelekwa gereza jingine, akisubiria kesi yake,....

‘Lakini mimi sijaua, kwanini hawanielewi,.....’alijikuta akisema peke yake.

‘Mimi sikubali kwenda huko, ni bora nijue....’akasema kwa sauti, akiwa anasubiria huyo mgeni wake, aliombea huyo mgeni awe mtu atakayeweza kumsaidia, awe ni jamaa yake, na jamaa yake ni nani, labda kijana wake, labda mtaalamu, ....labda

Sasa sauti anayoisikia sasa,.....aliombea vinginevyo, ....akajua sasa kaisha, sasa alichokuwa akiambiwa ndio hicho anakwenda kupambaa nacho, na njia peke yake sasa ni kujiua tu....

‘Huyo hapo ndiye mgeni wako,....’akaambiwa na mlinzi, na akabakia akiwa ameduwaa

‘Mnapewa nusu saa tu ya kuongea maana muda umekwisha wa kuonana na wageni...’akaambiwa,

‘Na hata ruhusa hiyo ilipotolewa, profesa hakutamani kugeuka kuonana na huyo mgeni wake, akabakia amesimama, akiwa kampa mgongo huyo mgeni wake, alikuwa hatamani kugeuka kuonana na huyo mgeni wake...

NB: Tuishie hapa kwa leo


WAZO LA LEO: Kujua maumivu, au ubaya wa jambo, ni mpaka likupate na wewe, ukiambiwa tu, au ukiona mwenzako, anahangaika ,au analalamika, utaona ni jambo la kawaida tu, na utaweza kumpa ushauri mwenzako kuwa avumilia ndio maisha, au utalichukulia ni la kawaida tu, lakini siku likikukuta, ..hapo ndio unaweza kusimulia, kwani...aisifuye mvua imemnyeshea.
Ni mimi: emu-three

No comments :