‘Jana
nilikutana na kijana wako..., mmh sikuwa nafahamu kuwa wewe ulikuja na kijana huyo kutoka huko kwenu, unajua
tena nafahamu jambo pale ninapolifanyia kazi, kama halina umuhimu kwa kazi
zangu sina muda wa kulifuatilia, ....’akasema akitegemea kuulizwa swali,lakini
swali halikutoka, na kwahiyo akaendelea kuongea.
‘Na kama
unavyofahamu kazi zetu, kitu kidogo kinaweza kukuvuta kutaka kujua zaidi...ili
kupata ushahidi halisi kwa jambo unalolifanyia kazi.....naikizingatiwa kuwa
niliwahi kufanya kazi fulani kabla kumuhusu huyo kijana...’akaanza kuongea na
hapo moyo wa profesa ukaanza kudunda.
‘Ni kazi
gani...’ alitamani kuuliza hivyo, lakini akajizuia kufunua mdomo wake, na kusubiria
huenda jibu litatokea.
‘Unajua
maisha yalivyo,....mh huwezi kujua jinsi gani mwenzako anavyohangaika, unaweza
kumuona katulia, ukaona karizika,ukasema
mhh yule hana shida,...lakini kuna mwingine hawezi kutulia, shida zake zote
zitajulikana, kiukweli watu tunatofautiana kwenye kuonyesha ubinafsi wetu....’akatulia
‘Mbona
kachanganya mada, ana maana gani huyu mtu...’akawa anajiuliza huku akichunga
kufungua mdomo wake.
‘Sasa mimi
nina shida..kwa mfano ,mimi nina shida...unaelewa hapo, natolea kwa mfano..nina
shida, ...lakini huwezi kunisaidia mpaka ujue ni shida gani,hata kama una uwezo
au sio.....na ....’akageuka kumuangalia Profesa,na profesa alikuwa kimia, kwa
muda huo alikuwa akimuwazia kijana wake, ...
Ni muda sasa
hawajawasiliana,na hata kaka yake akipiga simu kuulizia, hajui hata atamuambia
nini, japokuwa kaka yake alikuwa kakata kauli tena ya kuwasiliaa naye baada ya
wao kuondoka bila kuaga,...na hata yeye hakuwa anataka kumpigia simu, ni kama
mahusiano ya udugu uliokuwepo awali yalikuwa yamefutika,....kisa ni huyo
kijana.
Pia akakumbuka
kuwa tangia wahasimiane na huyo kijana, japo alijitahidi kujipeleka kwake,
lakini ilifikia mahali akaona haina haja tena, kwani hakuwahi kukaribishwa, ...
Ikawa sasa hakuna
kukutana, au hata kupigiana simu, na hata ikitokea wakutane njiani, ikitokea ni
kusalimiana kwa mikono, hay, hay. Ili tu ionekane kuwa hakuna uhasama dhidi
yao, na hata ile dad, dad, ikawa
haipo tena.
Na baadaye
ndio akasikia kuwa kijana wake huyo kajiunga na mama mtemi kutafuta ushahidi wa
kumuweka yeye ndani, ...kusikia hivyo, akajua kuwa kijana sasa anamchukia,...na
keshapandikizwa chuki , na kwa vile kijana anamfahamu sana...kweli anaweza
kutumika kumuangamiza..
Moyoni akajijutia
mwenyewe kwa kumfanya huyo kijana awe rafiki na binti wa huyo mama,....mwanzoni
alijua huenda kwa kufanya hivyo, atajenga udugu, ataweza kupata mengi kwa huyo
mama kwa kupitia wawili hao kumbe imakuwa kinyume chake,....imekuwa kama
kajipalilia ubaya zaidi
Sasa alivyoanza
kuongea huyu mpelelezi kuhusu huyo kijana, akajua ni yale yale ya mama mtemi,
lakini alipoanza kuongea kuhusu jamaa kutoka India, akajua ehe,huenda mpelelezi
kaajiriwa na huyo jamaa, lakini kwa jinsi anavyochanganya mambo, huwezi kujua
msimamo wa huyu mtu.
Profesa
alishamsoma huyu mtu kuwa lengo lake ni kumchanganya,,...unahitajika kuwa
makini kwa huyu jamaa, kwani wakati
mwingine anataka kukuchimba kupata taarifa fulani...
‘Kama
unavyonijua mimi, nilikuwa askari wa serikali, ...baadaye nikatoka huko, kwasababu
zangu binafsi,...nikaona nijiajiri, na kiukweli, japokuwa ni ngumu kujiajiri
kwa kazi kama hizi, maana unajiweka mtu kati,..., lakini nimeweza kujiendeleza...’akatulia
‘Usionine
hivi profesa,...mimi huko kwetu ,... unajua hata mimi natoka afrika japo wazazi
wangu ni mchanganyiko...ndio maana nipo half
cast, nusu ni mwafrika,....huko kwetu ninapotoka nina miradi yangu,
nikirudi nyumbani naweza kujivunia...ndio maana nataka kukushauri..uwe kama
mimi....najuahata wewe umewekeza au sio....’akasema
‘Lakini kama
ujuavyo maisha ya hapa,...yanahitaji gharama nyingi sana...watu hawaelewi hasa
huko nyumbani, ....huko kwetu hakuna tofauti sana na huko kwenu,...kwahiyo
tabia ni zile zile...hawajui kuwa kile unachopata kinaishia kwenye ...malipo
mengi tu, hapa huna ujanja wa kukwepakodi,...si unaona ilivyo, nyie wakati
mwingi mnatafutwa kwa kukwepa kodi,mimi siwezi kukwepa, hata sekunde moja,...’akatulia
‘Mimi
nawafahamu sana nyie, kwa jinsi gani mnavyokwepa kodi, katika kazi zangu hizi nimeliona
hilo, lakini huko tupaache, siwezi kuwashitaki kwa hilo...’akatulia na profesa
akajua ni katika namna ya kumtisha.
‘Lakini sasa
ni kuhusu huyu kijana wako...’akatulia, na hapo profesa akajua kuna bomu
linakuja
‘Huyu kijana
wako kamchumbia binti wa mama mtemi,...hahaha....’akasema na kucheka, na hapo
profesa akapumua
‘Unajua
niliposikia mara ya kwanza, sikuamini....’akatulia na profesa alitaka kumuuliza
kwanini, lakini hakutaka kufungua mdomo wake, akatulia tuli
‘Sio kwamba huyo
kijana ...hamfai huyo binti, ...hapana ila yule binti alivyo tu, sizani kama
wataendana..., si unamfahamu yule binti alivyo...najua wewe uliishi pale
ukamuona huyo binti alivyo, wengi wanajiuliza...mbona kitabia hafanani na
wazazi wake au sio,...kuna siri kubwa sana...lakini hayo hayatuhusu....’akatulia
‘Na hapo
ndio watu kama nyie mnatumbukiza mikono yenu kuwachunguza, ila ...nakukanya
tena na tena usije kujaribu kitu kama hicho tena pale kwa huyo mama,...kwani
hata hivyo, sijui kama utaweza kumalizana na huyo mama, umeshaweka sumu na sumu
hiyo inakurudia mwenyewe, nakupa hilo kama angalizo, yule mama anakuchukia....’akatulia
‘Hayo
tuyaache, ....mimi nazungumzia huyu kijana .....mmh,huyu binti, huyu binti ni
kila kitu kwa huyo mama,...kwa wazazi wake, na ukitaka ukosane na huyo mama ujaribu
kuingilia mambo ya binti yake, kiujumla wanampenda sana binti yao, nawaheshimu
kwa hilo, sijui kwanini hawaki kupata mtoto mwingine, ni siri yao, na mimi
sipendi kuingilia siri za watu kama hawajanihusisha,ndio kawaida yangu...’akatulia
Profesa
alitaka kubishana naye kuhusu hilo, lakini akagundua jamaa kaongea hivyo
kumtega, ili aongee, ili aweze kutegwa kimaswali, akafunga mdomo wake, japokuwa
aliona kupotezewa muda kwa mambo yasiyoungana...na profesa alijua kuwa jamaa
alifanya hivyo kwa malengo fulani, .....
‘Siku kijana
wako alipogundulikana kuwa ana mahusiano na binti wa huyo mama, nikaitwa....’hapo
akageuka kumtupia jicho profesa, akitarajia swali, lakini profesa akawa makini.
‘Unajua tena
yule mama ni mtu kanizoea sana, akitaka kujua jambo ananitafuta, na mimi
namsaidia na wakati mwingine bure tu, ...sasa kunipa kazi kama hiyo....mhh,
niliona kama kunipotezea muda wangu...maana hiyo sio kesi ya kunipa
mimi...lakini sikumkatalia, nikijua ni kazi ya siku moja nampa taarifa
yake....’akaegemea usukani
‘Mhh...hutaamini,
..kitu nilikiona kidogo, kikanifanya nisafiri hadi Tanzania kwa mara ya
kwanza....’akasema hapo profesa akashituka, na akataka kusema neno lakini akaona
atulie kwanza.
‘Wanasema
tembea ujue mambo,...ukikaa sehemu moja tu, unakuwa huelewi, dunia hii ina
mambo, unaweza ukamkuta mtu barabarani anaongea peke yake, ukasema ni kichaa,
kachanganyikiwa, lakini....we acha tu....’akatulia
‘Sasa
nisikupotezee muda wako, najua hili utalipokea kwa mikono miwili, maana
kiukweli nimeshakusoma, nimeshakufahamu, na wapi unapotokea...na mengi kuhusu
wewe nimeshayafahamu tu,....’akakuna kichwa kama kinamuwasha
‘Kwako wewe
kukujua,... sihitaji kabisa hata kwenda kwa mtaalamu, maana na yeye anajifanya
mjanja,...unajua ka-utalamu kake ka mitandao, watu wanamuona kama mganga wa
kienyeji wa kupiga ramli, wakiwa na shida,...hata shida ndogo tu, wanapoteza
pesa zao kwenda kwake, basi anavimba kichwa,..eti wanakwenda kwake kutaka kujua
hili na lile....mmh, kweli wajinga ndio waliwao....
‘Sasa ubaya
wa binadamu, watu wanakuamini,watu wanakuona msaada kwao,lakini inafikia mahali
unatakabari, unajiona wewe ni zaidi....wewe ni
mtaalamu....unawasaliti....’akatulia
‘Na baya
zaidi, kaona kuna njia nyingine ya kupata kipato kwa kubuni kazi ...basi
ingelikuwa ni kazi halali basi, ...yeye kaamua kubuni kazi za ....hata
ujambazi, huyu mtu ni mbaya sana,...atawaingiza wengi jela,...mimi sijui,
lakini huko anapokwenda ni kubaya sana, tena sana...’akatulia
‘Najua ni
rafiki yako, najua unaweza kwenda kumuambia haya, lakini mimi simuogopi,
anajifanya eti anajua mambo yangu mengi, eti nina ubaya umejificha, mimi
nilimuambia aupeleke huo ubaya mahakamani tukapambane huko kisheria, mbona
haupeleki,...’akatulia
‘Yule jamaa
anaishi kihivyo,.. yeye anachotishia ni kuniharibia jina langu, nionekane
sifai, eti ninyang’anywe leseni yangu, nimemwambia ajaribu, kama
hataumbuka,...hawezi , hata siku moja hawezi...’akatulia
‘Kwahiyo na
wewe nakuona mpo naye sambamba, nakuambia kama rafiki yangu, uwe makini na huyo
jamaa , haaminiki...., uwe makini sana....ukiataka kunisikiliza haya, ukiona
labda mimi nakupekenyua its up to you..,
..ila ipo siku utayakumbuka haya ninayokuambia...’akasema
‘Ni hayo tu,
au kuna jingine...’akauliza profesa akitaka kutoka nje ya gari
‘Ni kuhusu
kijana wako...’akasema mpelelezi akiwa hamuangalii profesa, kama vile anajua
akitaja kuhusu kijana wake jamaa atataulia.
‘Ana
nini..,?’ akauliza profesa akimkazia macho mpelelezi japo moyoni alikuwa na
wasiwasi.
‘Kanipa kazi,
...’ akasema sasa akimtupia macho profesa akionyesha uso wa kutahayari kama
vile hakutaka kuliongelea hilo,....
‘Unajua kazi
nyingine ni siri...lakini wewe ni rafiki yangu, nikaona nikudokezee hilo, na unajua
mimi sitaki wewe uje kuishia jela,....’akatulia
‘Kijana
wangu kakupa kazi ya kunichunguza mimi...usitake nikuamini....hilo halipo!’ akasema
kwa kuonyesha uso wa mshangao, akilini alijua kuwa inawezekana kweli kafanya
hivyo, lakini hakutaka huyo jamaa amuone anamuamini.
‘Sijakuambia
hivyo....kwanini anipe kazi ya kukuchunguza wewe,....hapana sivyo
ninavyomaanisha, kwani wewe una kosa
lolote dhidi yake...au?’ akasema kwa kuuliza.
‘Tatizo lako
hueleweki, najua hapa kuna kitu unanitafuta, na huna uhakika nacho, unachofanya
ni kinichimba, kunichezea akili, unajua unanipotezea muda wangu, nimekusikiliza
wee, sijaona lolote la maana, sasa nakuambia muda wangu wa kukusikiliza umekwisha,
mimi naondoka, kama una jingine nitafute kwa muda wako....’akasema sasa
akifungua mlango wa gari.
‘Kijana wako
alikukana, akasema wewe sio baba yake halali,....’akasema
‘Kwani ni
uwongo....’akasema profesa
‘Kijana wako
anasema wewe ulitumia mbinu, na kujifanya wewe ni mlezi wake, ili tu upate pesa
kwa kutumia mgongo wake...’ akasema
‘Ina maana
hao wafadhili ni wajinga, ....kawaulize kama mimi niliongea uwongo,....’akasema
‘Na zaidi ya
hayo, kijana wako amekiri kuwa wewe unajishughulisha na biashara ya
mlungula,....ana ushahidi kwa hilo,.....na yupo tayari kuutoa mahakamani
ikibidi..hata ukifungwa yeye hana cha kujutia kwa vile anajua ni kweli, hata
yeye haimfurahishi kusikia ana mtu kama wewe unayejifanya ni mlezi wake, kumbe
ni hadaa za kujinufaisha tu.....’akasema
‘Ndio hilo,
au kuna jingine....’akasema profesa sasa akiwa keshafungua mlango akijivuta
kutoka nje,
‘Akasema wewe
unauza madawa ya kulevya, na pia una madawa ukichanganya na pombe humfanya mtu
asijielewe, afanye mambo kinyume na matakwa yake,na akizindukana,...unakuwa
umeshamfanyia mambo ambayo hayafai, unamfanya kama zezeta, na kujituma kufanya
kile unachotaka, na hapo unatumia huo uchafu alioufanya kwa mbinu zako kuja kum-blackmail.huyo
mtu ili kupata pesa....’akasema
‘Mhh,
hahaha, na wewe ukaamini hayo, ...au ndio kazi aliyokutuma, na sasa unataka
kuhakiki kuwa ni kweli au si kweli...?’ akauliza
‘Niliposafiri
kwenda Tanzania,....kabla sijayajua hayo, nilifanya utafiti, kuchunguza kutaka
kujua uhalali wa dawa zako,....profesa unajua wewe ni mtaalamu sana, ....unajua
ungetulia ukaweka mambo yako sawa, ungejipatia jina kwa dawa zako....’akasema
‘Dawa
zangu....?’ akauliza
‘Ndio dawa
zako za tiba mbadala...na...hizo unazotumia kwa kuleweshea na kupumbaza
watu..’akasema na profesa hapo akabakia kimia
‘Dawa zako
zina nguvu sana...ila wewe unazitumia
vibaya....na hiyo ni kutokana na tamaa yako...’akasema
‘Zile dawa
zingesaidia katika upasuaji....unaona eeh, na..hata katika mambo ya usalama,
kwa wahalifu,....hayo ni mambo halali, kiukweli ungefaidika sana kwa hizo dawa......mimi
kwa vile nimepitia polisi,naweza kukusaidia, unachotakiwa ni kuniambia ukweli
na tuone jinsi gani ya kusaidiana, ili ufike mbali...’akasema
‘Sihitaji
msaada wa mtu yoyote, maana hayo unayoongea usifikiri sikuyafanyia kazi, nimehangaika
kiguu na njia kutaka dawa zangu zitambulikane, zipate haki miliki, lakini
....usinikumbushe mbali...na nimechoka,...nia yangu ni kutafuta njia nyingine
ya kupata pesa, walinifunga wakidai nauza madawa ya kulevya, achana na mimi
kabisa...’akasema
‘Wewe
hujasema ukweli kuhusu madawa yako, ....walijua wewe unachanganya a madawa ya
kulevya,....ilitakiwa upate mtu wa uhakika wa kukusaidia...mimi naweza kuifanya
hiyo kazi, tukishirikiana...’akasema
‘Nikuambie ukweli mimi sihitaji
tena kujisumbua kwa mambo ya madawa,....mipango yangu ni kutafuta njia nyingine ya kupata pesa,
basi.....’akasema profesa.
‘Njia gani
nyingine profesa,....umekata tamaa mapema, unasikia, wewe hukupata mtu sahihi
wa kukusaidia, sio kila mtu ni mwema, wengine wanapenda kutumia wenzao kwa
hadaa, na jingine ni wewe mwenyewe tu...wewe kinachokupoza ni kuwa unataka
upate pesa nyingi kwa haraka, ...ndio maana hufanikiwi....sikiliza ,mimi
ninaweza kukusaidia,...’akasema
‘Kunisaidia
wewe...kunisaidia mimi, ....?....niambie kwa vipi.....?’ akauliza
‘Eheee, sasa
unaanza kunielewa, ...muhimu kwanza nifahamu kama upo tayari, na ukinisikiliza
ukanielezea hatua uliyofikia, tunaweza kufika mahali,...najua awali tatizo
ilikuwa ni pesa ya kuanzia,....sasa najua pesa za mtaji sio tatizo....hilo
tutalipanga...’akasema
‘Mhh,
tutapatia wapi mtaji, wakati...wewe mwenyewe hapo unatafuta pesa, mtaji ni
pesa, na pesa ndio hizo ngumu,...usinipotezee muda wangu...’akasema
‘Pesa ya
mtaji itapatikana,...ni wewe tu,..’akasema
‘Kwa
vipi...?’ akauliza
‘Kwanza
niambie ukweli....unajua ,mimi ni askari, nilikuwa askari, sasa mimi ni mtu
binafsi,na naweza kusikia jambo, nikalipima kwanza, nikamshauri mteja, kuwa
hilo ni tatizo, achana nalo, au endelea nalo...’akasema
‘Unajua
tofauti yangu na askari hao wengine ndio hiyo,....sifanyi kumfunga mtu, nafanya
kutoa ushauri,....unaona, sasa ugumu wa hizi kazi unatokana a kupata ukweli
sahihi,....jinsi gani mtu atakavyofunguka, au kuficha jambo...sasa wewe
ukiniambia ukweli, itakuwa ni vyema zaidi...’akasema
‘Ukweli,
ukweli, ukweli kuhusu nini....?’ akauliza profesa akipaza sauti.
‘Profesa,
mimi mpaka nakuja kwako, ujue nimeshafanya kazi ya kutosha najua ni jambo gani
unalolifanya hadi sasa...najua kuwa mpo kwenye dili ya pesa nyingi, na ujue
pesa nyingi ni hatari....najua yote hayo, ila ....napenda wewe uwe mkweli ili
tusaidiane....’akasema
‘Kwahiyo
shida yako ni pesa, na kwa vile umesikia tetesi kuwa nipo kwenye dili ya pesa
nyingi unataka na wewe uzipate, au sio...kama ni hivyo umedanganyika...hakuna
kitu kama hicho...ni nani huyo kakudanganya?’ akawa kama anauliza
‘Sikiliza
profesa, mimi nimeshakuambia kuwa sipendi kuja kuwaumiza watu kwa kufichua siri
zako ambazo nina uhakika zitawafunga, huwa napenda kuwa muwazi, ili na wao ...watu
hao waliojiingiza kwenye ubaya wajijue, na wajirudi, waone kosa lao,...unajua
wengine wanaona wanachofanya ni sahihi ,, kwa vile tu wanapata pesa,...lakini
mtu kama huyo unaweza kumsaidia akabadilika, na kuwa raia mwema,...unaona
hilo...’akasema
‘Kwahiyo wewe
umeona kuwa mimi ni raia mbaya, unataka niachane na hizo hisia zako kuwa mimi
nafanya biashara haramu, kuwa natumia madawa kuwapumbaza watu waishiwe
kujitambua ....na kutenda yasiyo faa...ndivyo unavyonibambikizia makosa au
sio..sasa sikiliza, wewe kama una ushaidi peleka huo ushahidi mahamani
tutakutana huko.....’akafungua mlango.
‘Sio mimi wa
kufanya hivyo, mimi hiyo sio kazi yangu, nielewe hapo, kama ningekuwa nafanya
hivyo, kesi ya mama mtemi si ungelishakamatwa na kushitakiwa...’ akasema
‘Kuna watu
wengi wanakutafuta tu, wana visasi na wewe kwa uliyowafanyia, wanatafuta sababu, na ushahidi,....na mimi nikitaka naweza kuwasaidia,....lakini wewe ni rafiki yangu, au sio, ...’akasema
‘Rafiki yangu!...wewe,...?! Na nikuulize ni akina
nani hao...?’ akauliza
‘Wapo wengi tu , na sasa kaongezeka, yule raia kutoka India...na yeye hajakutambua tu kuwa wewe upo nyuma ya hayo mambo, lakini yupo mbioni, atakutambua tu...unaona hali ilivyo, ni kwamba kwa vyovyote unanihitajia mimi,
ndio nikaona nije tuongee,.....sasa uamuzi ni wako, kama unakaidi, sawa, mimi
nitafanya kazi yangu, lakini usije kunilaumu...’akasema
‘Una maana huyo
raia kutoka India, ndiye kakupa kazi ya kunichunguza..?’ akauliza kwa mshangao,
sasa akiwa kashusha mguu mmoja nje...na kabla hajajibiwa, mara simu yake
ikaita, na alipotizama aliona ni tajiri wake...
‘Kesho
nataka kuonana na wewe....’akaambiwa
‘Kesho.....mmmh
tutawasiliana nipo sehemu mbaya....’akasema
‘Ni muhimu,
sana..nataka tuongee, kama unaweza kunisaidia....’akaambiwa kwenye simu
‘Kuhusu
nini.....?’ akauliza
‘Ukija
nyumbani tutaongea,...kuja asubuhi, halafu tutakwenda benki, kazi moja
utafanya,.....mengine nitakujulisha ukifika, ....usikose....’akaambiwa na simu
ikakatika.
Profesa
akili ikampaa, ina maana jamaa anataka kumkabidhi yeye hizo pesa, azipeleke
mahali ambapo alishapangiwa huyo mtu kuzifikisha, na hapo hapo yeye ndiye
anatakiwa kuzichukua ili wakutane na mtaalamu, kugawana.....,alipowaza hivyo,
kwa haraka akafungua mlango wa gari kushusha miguu yote nje kutaka kuondoka.
‘Jamaa
aliniambia wewe na mimi tutashirikiana kuupeleka mzigo mahali, ili kumnasa
mbaya wake...’akaambiwa na mpelelezi, na wakati huo profesa alikuwa keshatoka
nje ya gari, tayari kufunga mlango wa gari, lakini kwa kauli hiyo akasita....
NB: Ni nini
kitaendelea
WAZO LA LEO: Nafsi ina nguvu sana, nafsi ina
tabia ya kukutuma hata kule kusipofaa, na ikashawishi akili kukubali jambo,
ambalo kiukweli halifai, ni kwa vile kuna masilahi tu,...na ili kufanikiwa hilo
nafsi italipamba hilo jambo, na ikatuma akili ikajenga hoja za kujirizisha. Ni
kazi kubwa kupambana na nafsi, ukiwa hua msimamo, lakini kama una msimamo, na
tabia yako ikawa kwenye kutenda yaliyo haki, na ukweli, ni rahisi sana
kuishinda nafsi. Tujitahidi kuwa wakweli na kutenda yaliyo haki.IJUMAA KAREEM.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment